Pamba kuing’oa CCM Kanda ya Ziwa

WATANABE

JF-Expert Member
Apr 13, 2011
1,092
466
Pamba kuing’oa CCM Kanda ya Ziwa


Waandishi Wetu

Mwanza
Toleo la 243
13 Jun 2012










243_pamba.jpg



  • Itaongeza pale kilipofika CHADEMA
  • Wakulimwa wachoshwa kukopwa, kutapeliwa
  • Mbunge asema watachagua rais wao




PAMBA ama maarufu huko nyuma kama dhababu nyeupe, itakuwa ni kete muhimu katika siasa za Kanda za Ziwa na Magharibi kuanzia sasa hadi Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Raia Mwema limebaini.
Taarifa zinaonyesha ya kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho tayari kina upinzani wa kutosha katika maeneo ya wakulima wa pamba,hasa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinaweza kudhoofika zaidi kwa kushindwa kusimamia, pamoja na mambo mengine, bei nzuri ya zao hilo wanayoitaka wakulima wake.
Ni hali hiyo ambayo imemfanya mmoja wa makada wa CCM, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalah kusema kuwa wakulima wa pamba na wategemezi wao ni zaidi ya watu milioni 14, idadi ambayo ni kubwa kuliko hata wananchi waliompigia kura Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hivyo wana uwezo wa kumchagua rais wao kama Serikali haitawajali msimu huu.
Mpaka sasa hakuna bei ya kuanzia kununua pamba msimu huu iliyokwisha kutangazwa na uwezekano mkubwa ni kwamba huenda bei hiyo ikawa chini kuliko ya msimu wa mwaka jana.
Mwanzoni mwa mwezi huu wadau wa pamba walikutana hapa kujadili sekta ya pamba na hadi tunakwenda mitamboni, hakuna jibu lililokuwa limepatikana huku taarifa zikisema hata tarehe ya kuanza kwa msimu sasa imesogezwa mbele.
Hadi kufukia jana Jumanne, bei elekezi ya ununuzi msimu huu ilikuwa haijatangazwa ikiwa ni wiki moja tangu Mkutano wa Tisa wa Wadau wa Sekta Ndogo ya Pamba kufanyika jijini hapa ambao kwa kawaida ndiyo humpa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kutangaza bei hiyo na tarehe ya kuanza kwa msimu wa ununuzi.
Akifungua mkutano huo wa wadau wa pamba, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Chritospher Chiza alikwepa kuzungumzia suala la bei hali iliyosababisha Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, kuhoji huku Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba na Mbunge wa Magu, Festus Limbu, akiahidi kuwa hoja hiyo ingezungumzwa wakati wa mada ya Maendeleo ya Sekta ya Pamba ingawa bei dira haikutajwa zaidi ya kugusia bei ya pamba katika soko la dunia ambayo mpaka jana Jumanne ilikuwa senti 82.5 kwa ratili ya pamba nyuzi.
Bei ya kuanzia kununua kwa msimu wa mwaka jana ilikuwa shilingi 1,100 kwa kilo moja ya pamba mbegu wakati huo bei katika soko la dunia ikiwa ni dola ya kimarekani moja na senti mbili.
Habari za uhakika zinasema kuwa Chama cha Wanunuzi wa Pamba (TCA), Bodi ya Pamba na Chama cha Wakulima wa Pamba (TACOGA) vilishindwa kuelewana katika kikao kilichofanyika jijini hapa Juni Mosi mwaka huu ambapo wakulima walitaka bei ya kuanzia iwe shilingi 700 huku wanunuzi wakitaka iwe shilingi 500 hali iliyosabibisha kikao hicho kumalizika bila kufikiwa mwafaka wa bei ya kuanzia.
Katika kikao hicho cha wadau baadhi ya wadau akiwemo Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo, walitaka bei ya kuanzia isiwe chini ya shilingi 1,000.
Kutokana na wadau kuwa wakali huku Waziri mhusika akikosa jibu la moja kwa moja la bei ya kuanzia, Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba aliagiza Bodi hiyo, TCA na TACOGA kukutana juzi Jumatatu kujadili tena bei elekezi, kikao ambacho hakijafanyika.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Bodi ya Pamba ameliambia Raia Mwema ya kuwa msimu wa ununuzi ulikuwa uanze Jumatatu ijayo (Juni 18) lakini kutokana na kutokuwapo kwa bei ya kuanzia umeahirishwa na badala yake siku hiyo ndiyo Bodi, wanunuzi na wakulima watakutana tena kupanga bei ya kuanzia lakini akisisitiza kuwa bei hiyo itatokana na bei katika soko la kimataifa.
“Tulikuwa tukutane juzi (Jumatatu) lakini imeahirishwa mpaka tarehe 18 (Juni, 2012) siku tuliyopanga msimu wa ununuzi kuanza. Lakini tufanyeje ndugu yangu, bila bei ya kuanzia huwezi kufungua msimu wa manunuzi, na haya mambo yanaingiliana na siasa, kwa hiyo mpaka wiki ijayo ndipo tutajua,” alisema ofisa huyo.
Baadhi ya maofisa wa Benki ya Raslimali (TIB) na ile ya CRDB ambao benki zao ni wakopeshaji wakubwa wa wanunuzi wa pamba wamesema kuwa itakuwa vigumu kutoa mkopo msimu huu kama bei katika soko la dunia itaendelea kushuka huku wakulima wakisaidiwa na wanasiasa, wakitaka bei dira iwe juu kwani wanunuzi wengi bado wanadaiwa fedha nyingi.
“Hebu sikiliza, wanunuzi wengi bado wana madeni katika benki zetu kwa misimu iliyopita, sasa sisi tutaangalia msimu huu bei katika soko la kimataifa ikoje. Tukikokotoa tukaona hakuna faida na wakalazimisha bei kubwa ya kununua hatutawakopesha msimu huu. Tuache siasa. Katika hili lazima kuwepo win-win situation.
“Serikali yenyewe inalia haina fedha, hivyo hata kufidia kwa maana ya ku-top- up bei msimu huu ni vigumu kama ilivyofanya kipindi kile (2009/2010,” anasema ofisa mmoja mwandamizi wa benki hizo kwa sharti la kutotajwa.
Kwa mujibu wa Dk. Limbu uzalishaji wa pamba mbegu mwaka huu unatarajia kuongezeka kutoka tani 225,000 za msimu uliopita hadi kufikia kati ya tani 300,000 -350,000 msimu huu.
Mmoja wa wanunuzi wa pamba ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema kuwa kuongezeka kwa uzalishaji na kushuka kwa bei ya pamba katika soko la kimataifa huenda ndiko kunaifanya Serikali iwe na kigugumizi cha kuahidi kuongeza bei kama itashuka kama ilivyofanya katika msimu wa mwaka 2009/2010.
“Mwaka huu tutakuwa watazamaji, maana wakulima wamelima na wengine wametumia gharama kubwa na kuna watu mbegu zao hazikuota katika baadhi ya maeneo. Sasa leo ukawaambie pamba ni shilingi 500, si unatafuta mgogoro? Na huku benki napo unadaiwa halafu watu (wanasiasa) wanalazimisha isiwe chini ya shilingi 1000. Wakati mwaka juzi tulipopata hasara kutokana na kushuka kwa bei, (stimulus package) wakalipwa ambao hawakupata hasara au wengine kuzidishiwa. Wengine tuliambulia patupu sasa mwaka huu utathubutu kama si kutafuta hasira za waananchi, ” alisema mnunuzi huyo.
Uwezekano wa Serikali kutoa nyongeza ya bei kutokana na kudorora kwa bei katika soko la kimataifa unakuwa mdogo zaidi kutokana na ukweli kuwa kati ya fedha za ruzuku ya mbegu na viuwadudu vya za zao la pamba ilizopaswa kutoa msimu uliopita shilingi bilioni 6.9 imetoa shilingi milioni 600 tu, jambo lililozua mjadala mkali miongoni mwa wadau wakidai kuwa Serikali haitoi kipaumbele kwa zao hilo.
Kwa mujibu wa Bodi ya Pamba, upangaji wa bei dira ya kununulia huzingatia vigezo kadhaa, kama gharama za uzalishaji za mkulima, gharama za ununuzi wa pamba na uendeshaji, gharama za uchambuaji wa pamba, kiwango cha ubadilishaji wa fedha, faida ya mchambuaji, bei ya pamba nyuzi katika soko la kimataifa na bei ya mbegu kwa kilo moja.
Makamu mwenyekiti wa TACOGA, Godfrey Mokiri anasema kuwa msimamo wa chama hicho cha wakulima ni bei dira iwe asilimia 75 ya bei iliyopo katika soko la kimataifa.
“Tutakutana tarehe 18 (Juni, 2012) kujadili tena bei ya kuanzia, lakini sisi mapendekezo yetu ni iwe asilimia 75 ya bei iliyopo sasa katika soko la dunia. Tutaangalia hadi siku hiyo bei itakuwaje lakini hili ni la kujadili wadau wote ili kila upande usiumie,” alisema.
Baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa bei ya pamba huenda ikageuzwa ajenda ya kisiasa kwa vyama vya Upinzani kuitumia kujijenga katika ukanda huu ambao una idadi kubwa ya wapiga kura.
Tayari wabunge kutoka mikoa inayolima pamba bila kujali itikadi za vyama vyao wameapa kuikaba koo Serikali katika mkutano huu wa Bunge la Bajeti iwapo itatangaza bei itakayompunja mkulima.
Hayo yakiendelea, kuna kila dalili ya kuwa sekta ya pamba nchini imo hatarini kutoweka kama Serikali haitachukua hatua madhubuti, za makusudi na za haraka kukomesha ufisadi mkubwa ulioivamia sekta hiyo unaowakatisha tamaa wakulima wa zao hilo.
Wakichangia mawazo kwenye Mkutano wa Tisa wa Wadau wa Pamba nchini, mwanzoni mwa mwezi huu hapa, wadau walionyesha masikitiko kuona ufisadi wanaofanyiwa wakulima na makampuni ya ndani na ya nje yanayojishughulisha na zao la pamba, kwa kuwauzia mbegu na pembejeo mbovu pamoja na kuwapunja bei ya zao hilo.
Wajumbe wa mkutano huo wa kila mwaka ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya; maofisa maendeleo, kilimo na mifugo na wabunge kutoka mikoa 13 inayolima pamba nchini, wanunuzi wa pamba, wawakilishi wa wakulima na taasisi za fedha.
Katika maoni yao, wadau walibaini na kuhoji kitendo cha Serikali kumgeuza mkulima kuwa mtaji wa biashara za makampuni yanayoashiria kuwa ya kinyonyaji.
“Hatutaki kuletewa ghiriba za Ki-“Monsanto” za kibeberu (makampuni hodhi ya kimataifa) nyingine ya kuwaangamiza wakulima wetu; Serikali lazima iwalinde dhidi ya utumwa huu wa Kilimo”, alitahadharisha Mbunge Dk. Kigwangala.
Tayari Waziri Chiza amekiri kuwa na taarifa jinsi wakulima walivyoingia hasara kubwa kwa kuuziwa mbegu za pamba za kupanda mbovu na ambazo hazikuweza kuota, kiasi kwamba inakadiriwa zaidi ya asilimia mbili ya wakulima wameathirika na utapeli huo wa wafanyabiashara.
Raia Mwema limezungumza na baadhi ya wadau kwa nyakati mbali mbali juu ya tatizo la mbegu kutokuota.
Nathan Kulujwila, Ofisa Maendeleo Kilimo na Mifugo Mkoa wa Mwanza na Samwel Ogenda Sassi, Ofisa Maendeleo Kilimo na Mifugo Mkoa wa Mara, wamekiri kushuhudia tukio hilo katika Mikoa yao, kama ambavyo alivyokiri Mashaka Igai, mkulima wa Kijiji cha Mariwanda, Wilaya ya Bunda akisema: “Hakuna watu wajinga kama Wakulima. Hawawezi kudai wala kutetea haki zao kwa maandamano wafanyavyo wafanyakazi. Wanaendelea kukamuliwa jasho lao kwa kuuziwa mbegu makapi zisizoota na madawa bandia na Serikali haishtuki kwa sababu hawana meno.”
Malalamiko mengine mbali ya mbegu za viwandani, ni gharama kubwa na hali ya kutokuota kwa mbegu zinazozalishwa na kampuni ya kigeni iitwayo “Quton (T) Limited” iliyosajiliwa hapa nchini kwa ajili ya kuzalisha na kuuza mbegu za kisasa.
Mbali na wakulima, wabunge pia wameonya juu ya hatari ya kufuta matumizi ya mbegu asilia na kutegemea mbegu zenye vinasaba (GMO) zinazozalishwa na kusambazwa na kampuni hiyo kuwa ni ukoloni mpya unaovamia Sekta ya Pamba.
Donald Max, Mbunge wa Nyang’hwale, wilayani Geita alihoji, ni kwa nini Chuo cha Utafiti cha Ukiriguru, chenye kujitosheleza kwa wataalamu, kisipewe kazi hiyo.
“Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika iamke, ivisaidie vyombo vya utafiti vya hapa nchini badala ya kudakia mashirika ya kimataifa yenye lengo la kuangamiza mkulima mdogo”, alitoa wito Max.
Malimi Benjamin, mkulima wa kijiji cha Sapiwi, Wilaya ya Bariadi alieleza shaka kama Serikali ipo kuwasaidia wananchi wake akisema: “Miaka 50 ya uhuru bado tunahitaji wageni katika kilimo, ambao ndio hao hao wanaoamua bei ya mazao yetu. Ukoloni unarudi na sidhani kama Serikali ina chochote cha kujivunia kwa kuturejesha utumwani”.
Kwa nyakati tofauti Dk. Kigwangala na Cheyo, waliitahadharisha Serikali juu ya kukimbilia mbegu zenye vinasaba wakisema kwamba huo ndio mwanzo wa kifo cha mkulima na wakatilia shaka Mkataba wa kuzalisha mbegu kati ya Quton na Serikali.
Raia Mwema imefanikiwa kuona nakala ya mkataba huo na kubaini kuwa ni wa upande mmoja, ukiibana zaidi Serikali kwa maslahi Quton.
Novemba 4, 2009, Quton (T) Ltd, iliingia mkataba na Serikali kupitia Bodi ya Pamba (TCB), Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza Zao la Pamba (CDTF), na Chama cha Wanunuzi wa Pamba (TCA) kwa upande wa pili, wa kuzalisha, kuchakata na kusambaza mbegu za pamba za kupanda kwa wakulima.
Mkataba huo wa miaka saba, unaipa kampuni ya Quton pekee haki isiyohojika ya kuzalisha mbegu za pamba nchini kwa kutumia teknolojia mpya, pamoja na haki ya kuagiza mbegu nyingine kutoka nje na kuzipa TCB na TCA jukumu la kuhakikisha kwamba, mbegu zote zinanunuliwa na wakulima kwa bei zinazoamuliwa na kampuni hiyo.
Raia Mwema limebaini kwa mfano, kwamba, wakati msimu 2011/2012 bei ya mbegu za kawaida kwa wakulima ilikuwa 350/= kwa kilo, bei ya mbegu za Quton ilikuwa 700/= kwa kilo; na kwa msimu 2012/2013, Quton watauza mbegu kwa bei zaidi ya 2,000/= kwa kilo, ikizingatiwa kwamba gharama yao ya kuchakata (process) kilo moja ni dola za Kimarekani 1.20.
Aidha, Mkataba huo hautoi haki kwa TCB, TCA, CDTF na wakulima ya kudai fidia kwa udhaifu wowote wa mbegu hizo na kwa athari zozote watakazopata.
Mkataba huo unawapa Quton, haki isiyohojika, ya kukataa kutumia aina yoyote ya mbegu iliyozalishwa hapa nchini na unaitaka TCB kutoa kwa Quton, haki isiyoingiliwa, ya kuzalisha mbegu kwa miaka saba na kwa TCB kutokutoa haki hiyo kwa mtu au kampuni yoyote bila ridhaa ya Quton.
Mkataba pia unaitaka TCA kuhakikisha kuwa, wanachama wake wananunua mbegu za Quton bila hiari na kuhakikisha pia kwamba hawaingilii mkataba huo.
Kwa wananchi wengi, mkataba huo unaonekana ni wa kuitafutia kipato Quton kwa kuwalazimisha wakulima kulipia bei kubwa mbegu hizo ilizochakatwa, kwa fedha za kigeni kila mwaka, kwa vile zinapandwa kwa mwaka mmoja tu na hazitoi mazao zikipandwa mwaka unaofuata.
Mbali na kuuziwa mbegu zisizoota, wadau wameilalamikia pia Bodi ya Pamba kwa kuruhusu wakulima kuuziwa dawa bandia za kuuwa wadudu kupitia CDTF ambayo ndiyo mwagizaji na mnunuzi wa Pembejeo za Kilimo.
Inakadiriwa kuwa, karibu asilimia 30 ya pamba iliyolimwa msimu 2012/2013 imeathirika kwa kushambuliwa na wadudu licha ya matumizi makubwa ya viuawadudu.
“Madawa waliouziwa wakulima, tena kwa bei kubwa hayaui; yamewatia hasara kubwa na kuwafukarisha”, alilalamika Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Serengeti, William Makunja; huku Konda Kingi wa Zagayu, Bariadi, alilalamika akisema:
“Shamba langu la ekari 10 ni miti tupu; halina matunda, wadudu wanakula kila kitu licha ya kupuliza dawa mara mbili, wadudu hawafi”.
Alisema, mwanzoni waliambiwa na maofisa wa Bodi ya Pamba kuwa, dawa hiyo ilikuwa na uwezo wa kuuwa wadudu saa 48 baada ya kupuliziwa, lakini haikuweza kuuwa. Kisha wakaambiwa wachanganye na chumvi; vivyo hivyo wadudu hawakufa.
Mkulima mwingine, John Nkwande kutoka Shinyanga Vijijini alihoji: “ Tumechoka kudanganywa na Serikali; kila mwaka ni mbegu na pembejeo mbovu; kila mwaka ni bei duni! Lini tutajikomboa, wakati hawa (Serikali na wanunuzi wa pamba) wakishibisha matumbo tu kwa jasho letu? Ningekuwa na uwezo, wote hawa wangeishia rumande.”
Elias Mabuba, mkulima kutoka Musoma Vijijini, alikuwa jasiri vya kutosha kumwonyesha Waziri Chiza, chupa ya dawa ya kuuwa wadudu aina ya 5 Ec aliyouziwa, aina ya Innsectido, iliyokwisha muda tangu 2009, lakini ganda lenye kuonesha muda wa 2009, limebandikwa juu yake ganda jipya lenye nembo ya CDTF kusomeka dawa hiyo ni hai hadi 2013, kuashiria kwamba CDTF wana hoja za kujibu kuhusiana na ufisadi huu.
Dawa zinazolalamikiwa ni pamoja na Bamethrin 2.5 Ec, iliyouzwa na kampuni za Bajuta International (T) Ltd na Bambana General Vitagro Ltd; Agrothrin 25 Ec iliyouzwa na Suba Agro Trading Ltd na Meru Agrotours Company, Innsectido 5 Ec, iliyouzwa na kampuni ya Bytrade (T) Ltd, Zetabestox 10% Ec, iliyouzwa na kampuni ya Equatorial Africa, na Agrothrin 10 Ec iliyouzwa na Muhere Enterprises (T) Ltd.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mfuko wa CDTF, Essau Mwalukasa, jumla ya chupa 4,000,000 zenye thamani ya Sh. 8bn/= ziliagizwa mwaka 2011/2012, ikilinganishwa na chupa 2,000,000 zilizoagizwa mwaka 2010/2011. Baadhi ya wanachama wa TCA na wakulima, licha ya kukerwa na uhafifu wa dawa hizo, wanatilia shaka kiwango kikubwa kinachodaiwa kuagizwa wakisema kama ingekuwa hivyo, upungufu wa dawa usingelalamikiwa na wakulima mwaka huu.
Januari 23, mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, alionya juu ya wakulima kuuziwa viuawadudu bandia akisema: “Si kila mtu anaruhusiwa kuuza madawa, na akaitaka Bodi ya Pamba kuchukua jukumu la kutangaza tenda na matokeo ya nani ameteuliwa na aina ya viuawadudu vitakavyotumika.
Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Pamba, Namba 2 ya 2001, TCB ndiyo yenye mamlaka na jukumu pekee la “kuteua watu wanaofaa kutoa na kusambaza pembejeo na matumizi yake”, wajibu ambao unaonekana imeutelekeza kwa kuachia CDTF isiyotambulika kisheria kwa kazi hiyo.
Raia Mwema limeona Tangazo la Tenda la CDTF la Agosti 15, 2011 ambalo, pamoja na mambo mengine, liliwapa nafasi wauzaji wa pembejeo za kilimo, kuagiza bidhaa walizoona wao zinafaa, na wapeleke maelezo (specifications) ndani ya zabuni zao, kana kwamba CDTF walikuwa hawajui walichohitaji.
Utafiti umeonyesha kuwa, licha ya mkulima wa pamba kupanua kilimo chake pamoja na kuongeza matumizi ya pembejeo kila mwaka, mavuno na kipato chake vimekuwa kikipungua mwaka hadi mwaka na kuwa masikini kuliko mwanzo, hali inayoashiria kuna kasoro kubwa katika usimamizi wa sekta hii huku lawama zikutupwa kwa chama tawala.
Tatizo la viuwawadudu bandia kwa sekta ya pamba limekithiri na kuathiri kwa kiwango kikubwa Kilimo cha pamba.
Kwa mfano, mwaka 2009/2010 wakati kiwango cha viuawadudu kilichosambazwa kiliongezeka kutoka chupa 860,000 mwaka uliotangulia, kufikia chupa 1,226,862, mavuno yalishuka kutoka tani 400,000 (2008/2009) hadi tani 266,000.
Vivyo hivyo, mwaka 2010/2011, ziliposambazwa chupa 4,562,975 za viuawadudu, mavuno yalishuka kwa asilimia 59 ya uzalishaji wa 2008/2009, na asilimia 39 ya uzalishaji wa 2009/2010 kufikia tani 163,000 za pamba.
Kwa mujibu wa wadau, kushuka kwa mavuno licha ya wakulima kupanua kilimo maradufu kunaonyesha mambo mawili: Ama madawa yaliyoagizwa na kusambazwa na CDTF ni mabovu; au sehemu kubwa hayakuwafikia wakulima kwa maana ya kusambaza dawa “hewa”.
Mwaka 2010/2011, Serikali ilitoa ruzuku ya Sh. 8.5 bilioni za pembejeo kwa wakulima; na kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa TCB, Marco Mtunga, mfumo wa utoaji na usambazaji wa pembejeo hizo kwa njia ya Vocha mwaka huo ulihujumiwa kiasi kwamba, sehemu kubwa ya pembejeo hazikuwafikia wakulima, na pia kwamba hata kile kidogo kilichowafikia, ubora wake ulikuwa hafifu.
Alisema kwa sababu hii, mavuno yalishuka na kusababisha wanunuzi wa pamba kushindwa kukidhi mikataba ya nje na kushitakiwa mahakama za nje, na hatimaye kufungiwa kuuza pamba kwenye soko la Kimataifa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga kwa upande wake anaona hujuma anayofanyiwa mkulima wa pamba haivumiliki, na kwamba kwa nchi kama China na Rwanda, wahujumu wa jasho la mtu mdogo hawaachwi kutamba.
Aprili mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Profesa Maghembe, aliunda Tume ya Wataalamu 10 kuchunguza migogoro, uendeshaji na usimamizi wa Tasnia ya Pamba kufuatia malalamiko mengi ya wadau wa Sekta hiyo.
Raia Mwema halijaweza kufahamu kama Tume hiyo imekamilisha Taarifa yake na kuwasilisha kwa Waziri, au la.
Hata hivyo, kuundwa kwa Tume hiyo ni kielelezo kwamba, Serikali imeanza kuguswa na kashfa nyingi zinazoikabili tasnia ya pamba na mapenzi ya kisiasa ya wakukima wa pamba kwa chama tawala.
 
Mimi ni kijana niliyeamua kurudi kijijini wilaya ya Magu na kuamua kuwa mkulima wa kilimo cha pamba kitu ambacho ni nadra sana kufanywa na vijana wa leo, lakini kinachinisikisha na kunifanya nifikirie tene kurudi mjini ili tuendelee kubanana huko ni jinsi serikali yetu inavyoshindwa kutujali sisi wakulima wadogowadogo.
 
Makala ya ukweli sana hii. Huu Ndiyo uandishi unaotakiwa

Kama mbunge nini mchango wako ktk pamba ukiwa bungeni? Ili tuendelee pana 2 njia yaani chama tawala kuondoka madarakani au wananchi kupambana kwa nguvu zao zote.
 
Back
Top Bottom