PAC Report

Binti Maria

Senior Member
Jun 26, 2007
158
33
Hii nayo wabunge wakigangamala kuna uwezekano mkubwa mtu mwingine akakimbia ofisi. Welcome to the land of kashfa!

_________________________________________________________________________________________________
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
0clip_image002.gif

BUNGE LA TANZANIA
________________

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)
_______________

TAARIFA YA MWAKA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU
ZA SERIKALI KUHUSU HESABU ZILIZOKAGULIWA ZA SERIKALI KUU NA MASHIRIKA YA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA ULIOISHIA JUNI 30, 2013
_______________________

(Imeandaliwa kwa kuzingatia Kanuni ya120 na kuwasilishwa Bungeni kwa
mujibu wa Kanuni ya 114 (15) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007)



Imetayarishwa na:
IDARA YA KAMATI ZA BUNGE
OFISI YA BUNGE
S.L.P 941
DODOMA 28 JANUARI 2015





YALIYOMO
SEHEMU YA KWANZA
1.0Utangulizi1
1.1Maelezo ya awali 1
1.2Majukumu ya kikanuni ya Kamati 2
1.3Miongozo iliyotumika katika utekelezaji wa shughuli za Kamati 3
SEHEMU YA PILI
2.0Uchambuzi wa Taarifa za Ukaguzi Maalum na Taarifa za Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013
5
2.1Taarifa ya awali kuhusu ukaguzi maalum wa misamaha ya kodi5
2.2Matokeo ya ukaguzi maalum wa fedha za ushuru wa mauzo nje ya nchi na ruzuku ya serikali kwa zao la korosho katika mkoa wa mtwara katika kipindi cha 2006/07 hadi 2010/1110
2.3Ukaguzi maalum wa ujenzi wa jengo la kumbi za watu mashuhuri katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa julius nyerere dar es salaam (jnia) katika kipindi cha 2006 hadi 201216
2.4Ukaguzi maalum wa kuthibitisha iwapo kulikuwa na tija katika matumizi ya shilingi bilioni 9 na milioni 600 katika vikao mbalimbali vya mabaraza ya wafanyakazi, manunuzi na matangazo katika mamlaka ya bandari tanzania (TPA) kwa mwaka wa fedha 2011/201221
2.5Taarifa maalum kuhusu matokeo ya ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na hatma ya hisa za Serikali katika benki hiyo25
2.6Taarifa maalum ya Kamati kuhusu Hali ya kifedha na kiutendaji ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)32
2.7Taarifa maalum kuhusu Deni la Sh. 1,875,896,246,224.48 ambalo Serikali inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii35
2.8Taarifa maalum kuhusu Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL)36
2.9Hoja za Ukaguzi kuhusu dosari katika umiliki wa Nyumba za Mashirika ya Umma38
2.10Taarifa maalum kuhusu gharama halisi zinazotumika katika kutangaza Hotuba za bajeti kwenye magazeti baada ya kusomwa bungeni40
2.11Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Tathmini ya zoezi la Ubinafsishaji41
SEHEMU YA TATU
4.0Mapendekezo ya Kamati42
SEHEMU YA NNE
5.0Hitimisho53



SEHEMU YA KWANZA
________________

1.0 UTANGULIZI
1.1 Miongozo ya Uwasilishwaji wa Taarifa
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kukushukuru kwa kunipa fursa ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu, pamoja na mambo mengine, maoni na mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) juu ya Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma. Maoni na Mapendekezo yanatokana na uchambuzi wa kina wa Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) juu ya Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013, Taarifa za Kaguzi Maalum mbalimbali zilizofanywa na CAG na Taarifa ya Msajili wa Hazina (The Treasury Notes) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2012 pamoja na Ziara za ukaguzi wa ufanisi katika baadhi ya miradi inayotekelezwa na Serikali Kuu pamoja na Mashirika ya Umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inaanza kufanya kazi zake baada ya Kupokea Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kama inavyoeleweka aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ndugu. Ludovick Utouh amestaafu Utumishi wa Umma hivi karibuni. Kamati inampongeza kwa dhati kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya ya kuimarisha usimamizi na uwajibikaji wa fedha za Umma, ni ukweli ulio wazi kuwa Ndugu Utouh ameandika historia kubwa katika dhana nzima ya usimamizi wa fedha za Umma katika Nchi, hii kwa Niaba ya Kamati, tunampongeza na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu na yenye baraka kwa kazi iliyotukuka kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Kamati inampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kumteua Profesa Mussa Assad kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Kamati inamaamini kuwa Profesa Mussa Assad akiwa ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya fedha atafanya kazi zake kwa weledi na uadilifu mkubwa. Tangu ateuliwe, Kamati imepata ushirikiano mkubwa wa Profesa Assad na Ofisi nzima ya Taifa ya Ukaguzi, Kamati itaendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya usimamizi imara wa fedha za Umma katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya pekee, Kamati inapenda kumpongeza Ndugu Lawrence Mafuru ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuwa Msajili wa Hazina nafasi ambayo tangu mwaka 2009 imekuwa ikikaimiwa na watendaji mbalimbali wa Serikali, hali ambayo ilikwamisha ufanisi wa Ofisi hiyo muhimu kwa Taifa. Ni imani ya Kamati kuwa Ndugu Lawrence Mafuru atatumia uzoefu wake alioupata kwenye sekta binafsi kuchochea fursa za mabadiliko ya kimaendeleo katika Mashirika ya umma na uwekezaji wa umma (Public Investment).
1.2 Majukumu ya kikanuni ya Kamati
Mheshimiwa Spika, Kamati hii kwa kuzingatia Nyongeza ya Nane chini ya Kanuni ya 115 (2) fasili Ndogo ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, ina majukumu ya kikanuni yafuatayo;
a) Kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara za Serikali na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali;
b) Kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyokwishatolewa na Kamati yenye lengo la kuondoa matatizo hayo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara za Serikali na Mashirika ya Umma; na
c) Kutoa mapendekezo na ushauri kwa Wizara za Serikali na Mashirika ya Umma kuhusu matumizi mazuri ya fedha za umma.
d) Kutathmini ufanisi wa Mashirika ya Umma;
e) Kufuatilia utekelezwaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma.
1.3 Miongozo iliyotumika katika utekelezaji wa shughuli za Kamati
Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza majukumu yake, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma imetumia nyenzo zifuatazo:-
a) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake;
b) Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2007 na maboresho yaliyofanyika kwenye Nyongeza ya Nane;
c) Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa za Fedha za Serikali Kuu kwa Mwaka ulioishia Tarehe 30 Juni, 2012;
d) Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa za Fedha za Mashirika ya Umma kwa Mwaka ulioishia Tarehe 30 Juni, 2012;
e) Taarifa za Kaguzi Maalum mbalimbali zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali;
f) Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2004, Sheria ya Fedha za Umma ya Mwaka 2001 na Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008;
g) Taarifa za Mhasibu Mkuu wa Serikali kuhusu mapato na matumizi ya kila Fungu pamoja na Taarifa ya Mhakiki Mali wa Serikali kuhusu usimamizi wa mali za Serikali;
h) Taarifa za Msajili wa Hazina kama Mwenye hisa Mkuu katika Mashirika yote ambapo Serikali imewekeza;
i) Taarifa za Hesabu zilizokaguliwa za kila Fungu na Shirika kwa Mwaka wa Fedha unaojadiliwa ikiambatanishwa na majibu ya hoja za Ukaguzi kutoka katika Manejimenti ya kila Fungu na Shirika husika;
j) Taarifa za kitafiti kutoka maeneo mbalimbali juu ya mambo yanayogusa majukumu ya Kamati na;
k) Ziara za Ukaguzi wa Ufanisi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Kuu pamoja na mashirika ya Umma.
1.4 Mheshimiwa Spika, Taarifa hii ina Sehemu Nne yaani, Sehemu ya Kwanza ni utangulizi, Sehemu ya Pili ni Uchambuzi wa Taarifa za Ukaguzi Maalum mbalimbali na Taarifa za Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013, Sehemu ya Tatu ni Maoni na Mapendekezo ya Kamati, Sehemu ya Nne ni Hitimisho.















SEHEMU YA PILI
______________

2.0 UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA KAGUZI MAALUM MBALIMBALI NA TAARIFA ZA HESABU ZILIZOKAGULIWA ZA SERIKALI KUU NA MASHIRKA YA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA JUNI 30, 2013
2.1 TAARIFA YA AWALI KUHUSU UKAGUZI MAALUM WA MISAMAHA YA KODI;
2.1.1 Mheshimiwa Spika, Misamaha ya kodi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ilikuwa ni asilimia tatu (3%) ya Pato la Taifa (GDP). Kwa miaka mitatu ya nyuma 2010/2011 hadi 2012/2013 misamaha ya kodi ilikuwa na wastani wa asilimia 3.33 ya Pato la Taifa. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2011/2012 mapato yaliyopotea (lost revenue) kutokana na misamaha ya kodi yalikuwa asilimia 4.3 ya pato la Taifa kiasi ambacho ndio cha kiwango cha juu kabisa katika miaka 5 iliyopita. Aidha, kwa nchi ya Kenya misamaha ya kodi ni asilimia 1 ya pato la Taifa. Hadi kufikia Juni 30, 2013 misamaha ya kodi iliyokuwa imetolewa ilikuwa na thamani ya Sh. 1.5 trilioni. Hata hivyo, kufikia mwezi Juni 2014, misamaha hii iliongezeka kwa takribani asilimia 22.6 mpaka kufikia Sh. 1.8 trilioni.
2.1.2 Mheshimiwa Spika, Ukubwa wa mapato yanayopotea kutokana na misamaha ya kodi mwaka hadi mwaka uliipa mashaka Kamati kama Sheria zinazosimamia utoaji na matumizi ya misamaha ya kodi zinafuatwa, kiwango cha mapato tunayoacha au kusamehe ni sahihi na malengo yaliyokusudiwa yanatimia. Kwa lengo la kuthibitisha hayo na kuishauri Serikali juu ya namna bora ya kusimamia matumizi ya misamaha ya kodi kwa manufaa ya nchi, Kamati ilikubaliana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuanza utaratibu wa kufanya Ukaguzi Maalum wa Misamaha ya Kodi kila mwaka kuanzia mwaka wa fedha wa 2012/2013.
2.1.3 Mheshimiwa Spika, Katika kikao chake cha tarehe 2/4/2013 Kamati pia iliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ianishe Sheria zote zinazosababisha uvujaji wa mapato ya Serikali kutokana na misamaha ya kodi na kupeleka mapendekezo Serikalini ili Bunge liweze kufanyia marekebisho. Aidha, Mamlaka ya Mapato bado haijakamilisha mchakato wa marekebisho ya Sheria husika.
2.1.4 Mheshimiwa Spika, Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alianza kufanya Ukaguzi maalum wa Misamaha ya Kodi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013 mnamo mwezi Februari, 2014 na kuwasilisha kwenye Kamati Ripoti ya Matokeo ya Awali ya Ukaguzi huo tarehe 23 Januari, 2015 kupitia barua Na. FA.249/309/01/55. Kwa mujibu wa Ripoti hiyo, ukaguzi huo unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni ulihusisha misamaha ya kodi iliyotolewa kwa Makampuni ya Madini, Taasisi za Kijeshi, Maduka yanayouza bidhaa zilizosamehewa kodi katika viwanja vya ndege (Aiport Duty Free Shops), Wawekezaji wenye Vyeti vya kupatiwa motisha kutoka TIC, Wawekezaji kwenye EPZ (Export Processing Zones), Misheni za kidiplomasia na Umoja wa Mataifa, Watumishi wa Serikali, Mashirika ya Dini na Mashirika ya hisani ya Jamii.
2.1.5 Mheshimiwa Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, katika Ripoti ya awali aliyoiwasilisha kwa Kamati amebaini yafuatayo;
a) Ukiukwaji wa maelekezo ya Serikali uliosababisha hasara ya Sh. 22,325,178,728 kufuatia kuhamishwa kwa mafuta yenye msamaha wa kodi kutoka kwa Makampuni ya Madini kwenda kwa Wakandarasi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti hiyo, M/S Geita Gold Mines na Resolute Tanzania Limited walihamisha mafuta yaliyosamehewa kodi yenye thamani ya Sh.22,325,178,728 kwenda kwa Wakandarasi mbalimbali (M/S Geita Gold Mines - Sh. 22,305,069,488 na Resolute Tanzania Limited - Sh. 20,109,240). Uhamishaji huo ulikuwa ni kinyume na Tangazo la Serikali Na. 480 la tarehe 25 Oktoba 2002 lililoelekeza kusitisha msamaha wa kodi pale ambapo mafuta yaliyosamehewa kodi yatatumika kwa matumizi tofauti na yaliyokusudiwa au yatahamishiwa, kuuzwa au kupewa mtu mwingine ambaye hana haki ya kupewa msamaha huo.
b) Matumizi ya misamaha ya kodi kwa malengo tofauti na yaliyokusudiwa na kusababisha upotevu wa mapato ya Sh. 392,701,602.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 na 2012/2013 Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd ya Arusha iliyokuwa na cheti (Na.030863) cha kupatiwa motisha kutoka TIC iliagiza magari 28 na kusamehewa kodi yenye thamani ya Sh. 465,235,220.10. Ukaguzi maalum umebaini kuwa Kampuni hiyo inamiliki magari mawili tu ambapo moja lina namba za usajili T 721 AFM lililonunuliwa tarehe 10/01/2005 na na lingine lina namba za usajili T 461 AUU lililonunuliwa tarehe 30/04/2008 . Aidha, magari hayo si kati ya yale magari 28 yaliyoingizwa nchini kwa msamaha wa kodi.
Mheshimiwa Spika, Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato (Arusha) ilikiri kuwa baadhi ya magari hayo yalisajiliwa na TRA na yanatumiwa na watu binafsi ambao hawakuwa na haki ya kupewa msamaha wa kodi. Pamoja na TRA kufanikiwa kuwakamata wamiliki wa magari 5 kati ya 28 na kurejesha kodi iliyosamehewa kimakosa ya Sh. 72,533,618, Kamati ilishangazwa na kitendo cha TRA kutositisha usajili wa magari hayo ilhali ikijua kabisa wamiliki hao wapya hawastahili kupewa msamaha wa kodi. Kamati inashawishika kuamini kuwa baadhi ya Maafisa wa TRA walikula njama na wamiliki hao wapya wa magari kwa maslahi binafsi katika kusajili magari hayo au kuna udhaifu mkubwa katika mifumo ya udhibiti matumizi mabaya ya misamaha ya kodi.
c) Misamaha ya kodi iliyotolewa kwa Kampuni isiyostahili yenye thamani ya Sh.53,399,565.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited ilipewa msamaha wa kodi kwa ajili ya mradi wa ujenzi na upanuzi wa hoteli kadhaa katika kiwanja No. 2531 kilichopo katika kijiji cha Changarawe wilayani Karatu, Arusha. Ukaguzi Maalum umebaini kuwa Kampuni hiyo iliagiza magari 3 kwa kutumia msamaha huo wa kodi na magari hayo yalipata msamaha wa kodi wenye thamani ya Sh.72,641,972.80 (BMW X5 - Sh.39,145,405.60; Toyota Land Cruiser Prado - Sh.14,254,160.40; na Hyundai Santa -Sh.19,242,406.80).
Mheshimiwa Spika, Wakaguzi walipoenda kukagua mradi huo, hawakukuta gari hata moja ingawa Menejimenti ya Kampuni iliweza kuthibitisha ununuzi wa gari moja tu (Hyundai Santa mpya) na hawakuwa na taarifa ya ununuzi wa hayo magari mengine. Kwa maana hiyo, Serikali ilipoteza mapato ya Sh.53,399,569 kwa kusamehe kodi ya uagizaji wa BMW X5 na Toyota Land Cruiser Prado kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, mapungufu ya aina hii yanaashiria kuwepo dalili za nyaraka kugushiwa katika kuwezesha msamaha wa kodi kutolewa kwa mtu au Kampuni isiyostahili.
d) Utoaji wa misamaha ya kodi isiyo na ukomo kwa ajili utekelezaji wa miradi ya ukarabati na upanuzi wa makampuni mbalimbali ulioikosesha Serikali mapato ya Sh. 63,213,537,216.70 katika mwaka wa ukaguzi.
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi umebaini kuwa misamaha ya kodi iliyotolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa uwekezaji uliokwishafanyika imeongezeka kutoka Sh. 34,205,432,788.50 kwa mwaka 2011/2012 hadi Sh. 63,213,537,216.70 kwa mwaka 2012/2013 ambalo ni ongezeko la asilimia 84.81. Kukosekana kwa ukomo wa muda, kiasi na aina ya vifaa vinavyopewa msamaha wa kodi kumetengeneza mianya kwa baadhi ya wawekezaji kufaidika na misamaha ya kodi isiyo na ukomo kwa kuwa ukarabati na upanuzi endelevu wa miradi ya makampuni. Kamati inaona si sahihi kuendelea kutoa misamaha ya kodi kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miradi ambayo ilifaidika na misamaha hiyo wakati inaanzishwa na kuiendelea kuikosesha Serikali mapato kwa muda mrefu.
e) Misamaha ya kodi ya Sh. 13,081,104,878 iliyotolewa kwa kuzingatia maombi yasiyo na nyaraka za kutosha.
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi umebani uwepo wa misamaha ya kodi ya Sh.13,081,104,878 iliyotolewa kwa wawekezaji mbalimbali bila kuwepo kwa nyaraka zinazohitajika. Nyaraka zilizokosekana ni pamoja na kibali za msamaha wa kodi kutoka Hazina, kibali kutoka Wizara mama, Taarifa ya matumizi yanayoendelea ya misamaha ya kodi kibali cha ujenzi, Taarifa za ukaguzi wa kushitukiza. Hii ni kinyume na taratibu za uandaaji na usimamizi wa matumizi ya misamaha ya kodi ambazo zinaitaka Mamlaka ya Mapato kuhakikisha maombi yote ya misamaha ya kodi hayashughulikiwa mpaka zinapowasilisha nyaraka zinazohitaji kisheria.
f) Kufungwa kwa duka la bidhaa zilizosamehewa kodi bila kuwasilisha TRA Hesabu za matumizi ya misamaha ya kodi kulikoisababishia Serikali hasara ya Sh.3, 824,547,526.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya M/s Conti- Africa Ltd katika miaka ya 2011/2012 na 2012/2013 ilipewa msamaha wa kodi wenye thamani ya Sh.3, 824,547,526 kwa ajili ya bidhaa zitakazouzwa kwenye duka la Jeshi huko Arusha. Hata hivyo, Wakaguzi walipoenda Arusha hawakulikuta duka hilo na Menejimenti ya TRA (Arusha) iliwathibitishia Wakaguzi kuwa Kampuni hiyo ilifunga biashara hiyo muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, Kamati haikufurahishwa na kitendo cha Kampuni hiyo kufunga biashara bila kuwasilisha TRA hesabu za misamaha ya kodi na TRA kutofuatilia kama msamaha wa kodi uliotolewa unatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Ni wazi kwamba, TRA kutofanya ufuatiliaji kunatoa fursa ka bidhaa zilizosamehewa kodi kupelekwa kwenye maduka yasiyo ya kijeshi na kuikosesha mapato Serikali.


2.2 MATOKEO YA UKAGUZI MAALUM WA FEDHA ZA USHURU WA MAUZO NJE YA NCHI NA RUZUKU YA SERIKALI KWA ZAO LA KOROSHO KATIKA MKOA WA MTWARA KATIKA KIPINDI CHA 2006/07 HADI 2010/11
Mheshimiwa Spika, iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara mnamo mwezi Mei 2011 ziliomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalum kwa lengo la kuthibitisha yafuatayo:-
a) Ni sababu gani fedha za ruzuku, pamoja na ushuru wa korosho ghafi hazipelekwi kwenye Halmashauri zinazolima zao hilo ili Halmashauri hizo ziweze kupanga matumizi ya fedha hizo kama ilivyo kwa fedha zingine za Halmashauri hizo.
b) Kwa kiwango gani Wakurugenzi wa Halmashauri wanaruhusiwa katika kuidhinisha malipo ya fedha za ruzuku pamoja na ushuru wa mauzo ya korosho ghafi.
c) Ni kwa kiwango gani maafisa wa ngazi za Mkoa na Bodi ya Korosho wamezingatia taratibu za udhibiti wa fedha za ruzuku na ushuru wa mauzo ya korosho ghafi ili zitumike kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa.
d) Ni kwa idhini ya nani Halmashauri ziliruhusiwa kutumia fedha zaidi ya magao wake.
2.2.1 Mheshimiwa Spika, katika kuthibitisha sababu za ruzuku pamoja na ushuru wa korosho ghafi kutopelekwa kwenye Halmashauri zinazolima zao hilo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amebaini kuwa Sheria Na.21 ya 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 iliyokuwa ikielekeza kuwa fedha za makusanyo ya ushuru wa usafirishaji korosho ghafi nje ya nchi kupelekwa Halmashauri zinazolima korosho ilifutwa na Bunge na kutungwa Sheria mpya Na.18 ya mwaka 2009. Aidha, Sheria Na.18 ya mwaka 2009 ilifanyiwa marekebisho na Sheria ya fedha ya mwaka 2010 kwa kuingizwa kifungu Na.17A kinachotoza ‘Export Levy’ na kuelekeza asilimia 65 (65%) ya ‘Export Levy’ hiyo ipelekwe kwenye Mfuko wa kuendeleza zao la Korosho na asilimia 35 (35%) ibakie Hazina kwenye Mfuko mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo maboresho ya Sheria yaliyofanywa na Bunge yanaelekeza fedha hizo kufikia walengwa kupitia Mfuko wa kuendeleza zao la Korosho na sio kupitia Halmashauri zenye wakulima wa zao la korosho.
2.2.2 Mheshimiwa Spika, kimsingi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amethibitisha ushiriki wa Watendaji Wakuu wa Halmashauri katika kuidhinisha malipo ya fedha za ruzuku na ushuru wa korosho ghafi ingawa ukaguzi wake ulibaini mapungufu yafuatayo;
a) Hasara ya Shs.223,815,000 inayotokana na malipo kwa pembejeo ambazo hazikupokelewa
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi umebaini kuwa Kampuni za Mukpar Tanzania Ltd na Equatorial Africa Ltd zililipwa na Bodi ya Korosho Shs.223,815,000 zaidi ya fedha ambazo walipaswa kulipwa kama utaratibu wa ulipaji wa asilimia 50 ungefuatwa katika msimu wa 2009/10. Kimsingi utaratibu huu unaelekeza kuwa Bodi ya Korosho humlipa Mzabuni asilimia 50 ya bei ya pembejeo baada ya kupata nyaraka zinazothibitisha kuwa Vyama vya Msingi vimelipa asilimia 50 ya bei ya pembejeo.
Mheshimiwa Spika, ukaguzi umebaini utaratibu huo haukufuatwa na kilichofanyika ni Mfuko wa Pembejeo wa Wilaya ya Masasi kupita Katibu wa Mfuko huo (Afisa Kilimo wa Wialaya ya Masasi) kutoa vibali vya kugushi vya malipo kwa Bodi ya Korosho kwa kigezo kuwa Mfuko umepokea pembejeo zote kutoka kwa Mukpar Tanzania Ltd na Vyama vya msingi vimeshalipa asilimia 50 ya bei ya pembejeo. Hivyo, kusababisha Bodi ya Korosho kuilipa kimakosa Mukpar Shs. 292,375,000 pamoja na usafiri Shs.2,880,000 (lita 24000*Shs120).
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipomuhoji Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho alithibitisha kutopokelewa kwa pembejeo hizo mpaka sasa na hakuna juhudu zozote zilizofanyika kuokoa fedha hizo. Aidha, mpaka sasa si Mukpar (T) Ltd wala Afisa Kilimo wa Wilaya ambaye amechukuliwa hatua za kinidhamu au za kisheria.
b) Malipo ya pembejeo pasipo viambatanisho Shs. 184,564,500
Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Pembejeo wa Wilaya ya Tandahimba (MPEWATA) unadaiwa kiasi cha Shs. 184,564,500 na makampuni ya Bytrade Tanzania (Shs. 154,564,500) na Mega Generics Limited (Shs. 30,000,000). Kampuni hizo zililipwa kiasi cha Shs. 262,132,500 (asilimia 50 ya Shs. 524,265,000) na Bodi ya Korosho kinyume cha utaratibu unaoelekeza Bodi kulipa asilimia 50 ya bei ya pembejeo baada ya kupata nyaraka zinazothibitisha kuwa Vyama vya Msingi vimelipa asilimia 50 ya bei ya pembejeo. Malipo ya Shs. 262,132,500 yalifanywa bila uthibitisho wa malipo ya Vyama vya Msingi kufanyika, hadi wakati wa Kamati inahoji Menejimenti ya Bodi ya Korosho pembejeo zenye thamani ya Sh.154, 564,500 zilizolipiwa ruzuku zilikuwa hazijapelekwa kwa wakulima na hazijulikani zilipo na hakuna hatua za kisheria wala za kinidhamu zilizochukuliwa kwa waliohusika.
2.2.3 Mheshimiwa Spika, katika kukagua hali ya udhibiti wa fedha za ruzuku na ushuru wa mauzo ya korosho ghafi ili zitumike kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa, Ukaguzi umebaini yafuatayo:-
a) Matumizi ya fedha za ruzuku na ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi kuendeshea shughuli za ofisi Shs. 1,075,046,004
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi umebaini kuwa kiasi cha Shs.1,075,046,004 kilitumiwa na Bodi ya Korosho kulipia matumizi mbalimbali ya Ofisi ikiwemo mishahara, gharama za matengenezo, bili za umeme n.k. ikiwa ni kinyume na maelekezo ya sheria inayotaka fedha hizo zitumike kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho. Fedha hizo ni nje ya fedha za usimamizi. Aidha, Kamati ilipoihoji Menejimenti ya Bodi ya Korosho ilishindwa kuthibitisha kuwa fedha hizo ni mgao wao na haikuweza kuwasilisha kibali cha kutumia fedha hizo.
Jedwali 1: Mchanganuo wa fedha zilizotumika kulipia madai mbalimbali ya Ofisi
MwakaJumla ya MatumiziFedha za UsimamiziZiada ya fedha iliyotumika
2006/07
2007/08
2008/09
2009/10
2010/11
382,676,430
115,496,912
365,365,153
315,845,456
285,662,053
50,000,000
100,000,000
80,000,000
80,000,000
80,000,000
332,676,430
15,496,912
285,365,153
235,845,456
205,662,053
1,465,046,004390,000,0001,075,046,004

b) Kukosekana kwa uthibitisho wa matumizi ya marejesho ya mikopo ya Ruzuku Shs. 345,958,266 katika Bodi ya Korosho
Mheshimiwa Spika, Katika msimu wa mwaka 2006/2007, kiasi cha Shs.345, 958,266 kilirejeshwa Bodi ya Korosho kutoka Halmashauri za Wilaya mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha Mfuko (Revolving Fund). Aidha, mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo haukupatikana wakati wa ukaguzi maalum. Hata, Kamati ilipohoji Menejimenti ya Bodi ya Korosho haikuweza kuthibitisha matumizi ya fedha hizo.



Jedwali 2: Marejesho ya Mikopo ya ruzuku kwa Wilaya za Mtwara
HalmashauriDeni (Mgao) ShsMarejesho Shs.Bakaa Shs.
Mtwara (M)55,275,38025,372,94029,902,440
Mtwara (V)139,89149040,433,73699,457,754
Tandahimba380,125,059162,151,590217,973,469
Newala183,807,909100,000,00083,807,909
Masasi349,620,95018,000,000331,620,950
JUMLA1,108,788345,958,266762,762,522

c) Deni la Pembejeo Shs.762,762,522
Mheshimiwa Spika, Halmashauri za Manispaa ya Mtwara, Wilaya ya Mtwara, Tandahimba, Newala na Masasi zilipelekewa pembejeo zenye thamani ya Sh.1,108,720,788 ambapo fedha hizo zilitakiwa kurudishwa Bodi ya Korosho kwa ajili ya kuanzisha Mfuko Endelevu wa Pembejeo (Revolving Fund). Halmashauri zilizotajwa hapo juu zilikiri kupokea pembejeo hizo na kuzikopesha kwa Vyama vya Msingi/wadau mbalimbali wa zao la Korosho. Ukaguzi ulibaini kuwa Halmashauri zote za Wilaya zimegoma kurejesha fedha hizo Bodi ya Korosho kwa maelezo kwamba ni fedha halali za Halmashauri hizo kwa mujibu wa sheria Na.9 ya mwaka 1982.
Mheshimiwa Spika, mpaka ukaguzi huu maalum unakamilika, kiasi cha Shs.762,762,522 kilikuwa hakijakusanywa kutoka kwa Vyama vya Msingi/wadau mbalimbali waliokopeshwa pembejeo kama jedwali hapa chini linavyoonyesha:




Jedwali 3: Marejesho ya Mikopo ya Pembejeo kwa Halmashauri za Mtwara
HALMASHAURIDENI (MGAO)MAREJESHO BAKAA
MTWARA (M)55,275,38025,372,94029,902,440
MTWARA (V)139,891,49040,433,73699,457,754
TANDAHIMBA380,125,059162,151,590217,973,469
NEWALA183,807,909100,000,00083,807,909
MASASI349,620,95018,000,000331,620,950
JUMLA1,108,720,788345,958,266762,762,522

d) Ruzuku kulipia Pembejeo ambazo hazikuombwa na wakulima
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2011/2012, Wakulima wa Halmashauri ya Newala walipeleka mahitaji yao ya pembejeo (dawa aina ya Sulphur ya unga) kwa ajili ya zao la korosho. Badala yake, Halmashauri ilipelekewa pembejeo aina ya Falcon (Sulphur ya maji) ambayo ndiyo ilikuwa kwenye ruzuku na hivyo kusababisha migogoro na wakulima ambao waligoma kutumia pembejeo aina ya Falcon na hivyo kulazimika kujinunulia pembejeo aina ya Sulphur kutoka kampuni ya Abbasi Tanzania LTD ambayo haikuwa kwenye mfumo wa ruzuku.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, Ukaguzi maalum umebaini kuwa dawa zote zinafanya kazi moja na kuwa Sulphur ya unga ina madhara kwenye udongo. Hivyo, ni wazi kuwa elimu ya kutosha haitolewi kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya baadhi ya pembejeo na hivyo kufanya wakulima waone wanahujumiwa kwa kutopelekewa aina za pembejeo walizoomba. Hata hivyo, Kamati haikuweza kupata taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa kuthibitisha kutofaa kwa matumizi ya dawa aina ya sulphur ya unga.

e) Kutozingatiwa kwa mapendekezo ya wakulima
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi huu maalum umebaini kuwa Bodi ya Korosho imekuwa haizingatii maelekezo ya wakulima na hivyo kuamua kuwapelekea pembejeo wanazoona wao zinafaa. Hali hii imekuwa ikisababisha migogoro isiyokuwa ya lazima baina ya wakulima na Bodi ya Korosho kupitia Vyama vyao vya Msingi.
f) Kukosekana kwa Taarifa na nyaraka mbalimbali
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Korosho ilitoa maelekezo kwa wadau wa zao la korosho katika ngazi mbalimbali kuhusu namna ya kutunza na kuandaa taarifa ya matumizi ya fedha za pembejeo ikionyesha orodha ya wakulima walionufaika na pembejeo za ruzuku. Pamoja na kuwepo kwa maelekezo hayo, Halmashauri za Wilaya ya Tandahimba, Nanyumbu, Masasi, Mtwara (M) na Mtwara (V) hazijawahi kuandaa Taarifa hizo na hakuna barua yoyote kutoka Bodi ya Korosho ya kuwataka wadau wa zao la korosho kuandaa na kuwasilisha taarifa hizo. Hali hii inaleta wasiwasi kama Bodi ya Korosho inafanya kazi ya usimamizi kama inavyotakiwa ili kuhakikisha wakulima wananufaika na pembejeo za ruzuku.
2.3 UKAGUZI MAALUM WA UJENZI WA JENGO LA KUMBI ZA WATU MASHUHURI KATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE DAR ES SALAAM (JNIA) KATIKA KIPINDI CHA 2006 HADI 2012
Mheshimiwa Spika, Baada ya uchambuzi wa kina wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Ukaguzi Maalum wa Ujenzi wa jengo la kumbi za watu mashuhuri katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, ilibainika kuwa mnamo mwaka 2007, Serikali ya Tanzania kupitia iliyokuwa Wizara ya Miundombinu waliingia mkataba na Kampuni ya China Songangol International Limited (CSIL) ili kufanikisha Miradi kumi na moja ya uwekezaji na uendelezaji katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusainiwa kwa [1]makubaliano (MOU) baina ya wadau hao wawili (Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na China Sonangol International Limited, CSIL) ilikubaliwa kwamba awamu ya kwanza ya mradi ihusishe miradi mitatu ambayo ni pamoja na Ujenzi wa Jengo la wageni wa kitaifa, makubaliano ambayo yalisainiwa tarehe 28 Februari, 2007. Baada ya Ukaguzi maalum, maeneo yafuatayo yaligundulika kuwa na dosari kutokana na ujenzi wa jengo hilo;
2.3.1 Ujenzi kuanza kufanyika bila kupata kibali cha Baraza la Mawaziri
Mheshimiwa Spika, Katika kupitia Hati za makubaliano baina ya Wizara ya Miundombinu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Kampuni ya CSIL, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alibaini kuwa Wizara ya Miundombinu iliandaa rasimu ya Waraka na kuuwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri kuomba kibali cha Serikali kuendelea na utekelezaji wa ujenzi wa jengo la wageni wa kitaifa (State Recepetion Building) kwa njia ya ubia kwa kushirikiana na CSIL.

Mheshimiwa Spika, katika ukaguzi maalum uliofanyika, ilibainika kuwa kulikuwa na mapungufu katika Waraka husika kwani haukuwa umesainiwa na Waziri wa Miundombinu, haukuwa na tarehe ikionyesha uliandaliwa lini na pia haukuwa na namba ya kuonyesha ni waraka namba ngapi na zaidi hapakuwepo na uthibitisho iwapo Waheshimiwa Mawaziri waliridhia kwa hatua zaidi za kumshauri Mheshimiwa Rais ili kuagiza ujenzi wa jengo hilo.

Mheshimiwa Spika, Kamati itahitaji kupata maelezo ya kina ya Serikali iwapo mchakato wa kuruhusu ujenzi wa jengo hilo ulipitia taratibu zote za kupata idhini ya Baraza la Mawaziri ikizingatiwa kuwa Kampuni ya CSIL baadaye ilishindwa kutekeleza majukumu yake ya kimkataba ikiwamo uendelezaji wa eneo la Terminal three katika Uwanja wa JNIA.
2.3.2 Mkanganyiko kuhusu mchango wa Serikali katika ujenzi wa jengo hilo.
Mheshimiwa Spika, Dosari kubwa nyingine iliyobainika na CAG kuhusu ujenzi wa Jengo la watu mashuhuri katika Uwanja wa JNIA ni kuhusu kiasi cha gharama ambacho Serikali ilichangia katika ujenzi husika. Mkanganyiko wa gharama za Serikali katika ujenzi huo ulitokana na taarifa za awali kuonyesha kuwa Serikali ilichangia kiasi cha Dola za Kimarekani milioni mbili (sawa na Shilingi bilioni tatu za kitanzania).
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum baada ya kupitia na kuchambua nyaraka mbalimbali za mikataba na manunuzi ilithibitisha kuwa gharama za mchango wa Serikali katika Jengo la kumbi za watu Mashuhuri kwa kazi zilizofanyika ulikuwa ni Shilingi 869,485,164 na sio bilioni tatu (3,000,000,000). Hivyo basi, ni muhimu Serikali ikalifahamisha bunge lako tukufu utata wa gharama hizo ulitokana na jambo gani.
2.3.3 Mapungufu kuhusu gharama halisi za ujenzi wa jengo la watu Mashuhuri katika JNIA
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi uliofanyika bado unadhihirisha kwamba gharama halisi za Ujenzi wa Jengo la watu Mashuhuri katika Uwanja wa Julius Nyerere zina mkanganyiko. Katika Ukaguzi wao, Wakaguzi walishindwa kupata nyaraka wala vielelezo vyovyote vilivyomo kwenye majalada ya Ofisi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na yale ya Kiwanja cha JNIA ikiwamo Mkataba kwa ajli ya kuonyesha gharama halisi za ujenzi wa jengo hilo. Kilichopatakina kwa wakaguzi ni “Offer of Grant for VIP Lounge” yenye thamani ya RMB 27,980,000 ambazo ni sawa na Sh.5, 335,359,318.

Mheshimiwa Spika, tafsiri ya kukosekana mikataba hapo juu inaashiria kwamba Mkandarasi (M/s Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd) pamoja na Mfadhili (M/s China International Fund Limited) hawakukabidhi nyaraka za ujenzi Serikalini na hivyo kushindwa kufahamu gharama halisi iliyolipwa na Mfadhili huyo.

Mheshimiwa Spika, ili kupata thamani halisi ya ujenzi wa Jengo hilo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa barua ya tarehe 3/04/2014 yenye kumb. Na. AB/235/280/08 aliiagiza Wizara ya Uchukuzi iwasiliane na Mthamini Mkuu wa Majengo ya Serikali ili kufanya tathmini ya gharama halisi za ujenzi wa Jengo hilo. Kwa mujibu wa Taarifa ya Mthamini Mkuu wa Majengo ya Serikali, hadi kufikia Mwezi Mei, 2014 gharama za Ujenzi wa Jengo hilo ilikuwa ni sawa na Sh.3,072,000,000 na mchango wa Serikali kwa shughuli zisizohusu ujenzi wa Jengo ulikuwa jumla ya Sh.869,485,164 tu.

Mheshimiwa Spika, Katika mikutano mbalimbali ya Bunge lako tukufu mwaka 2011 na 2012, Serikali ilitoa tamko kuwa Jengo la Watu Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam lilijengwa kwa jumla ya Shilingi 12 bilioni, tofauti ya Shilingi bilioni 9 kutoka gharama iliyoainishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali.

2.3.4 Kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi kulikofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA)

Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum ulibaini kuwa manunuzi ya jumla ya Sh.916, 917,145 yaliofanywa na TAA yalifanywa kinyume na kifungu namba 45 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act) Na. 21 ya mwaka 2004. Kifungu husika kinaitaka Mamlaka ya Ununuzi kuainisha manunuzi yote yanayotarajiwa kufanywa katika mwaka husika katika Mpango wa Manunuzi wa mwaka (Annual Procurement Plan).

Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum ulithibitisha kuwa manunuzi ya jumla ya Sh.916, 917,145 hayakuwamo kwenye mpango wa manunuzi wa mwaka katika miaka iliyohusisha Ukaguzi maalum 2009 hadi 2011. Athari ya jambo kama hilo kufanyika ni kuwa manunuzi hayo yalifanywa pasipo kuwepo kwenye bajeti wala Mpango wa Manunuzi na vilevile kutokupata idhini ya Bodi ya Zabuni au ya Ushauri ya Wizara. Kwa namna nyingine, uamuzi huo usiokuwa wa kisheria ulisababisha kutotekelezwa kwa shughuli zingine za TAA zilizokuwepo kwenye mpango ili kutoa nafasi kwa manunuzi haya yasiyokuwepo kwenye mpango kufanyika.

2.3.5 Malipo yaliofanywa bila kuwepo na ushindani wa bei

Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum umebainisha kuwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania ilifanya Malipo ya kiasi cha Sh.283,803,729 kwa watoa huduma mbalimbali bila kufanya ushindani wa bei ambao ungesaidia kupata bei nafuu ya huduma na vifaa ili kuokoa fedha za Umma kama inavyoelekezwa na Kanuni ya manunuzi ya Umma Na. 68 (4-5) ya mwaka 2005.

Mheshimiwa Spika, Athari inayotokana na maamuzi ya kutoshindanisha bei ili kupata huduma au vifaa ni kukosekana kwa uthibitisho wa thamani ya fedha katika manunuzi hayo. Hivyo, kutoshindanisha bei wakati wa manunuzi ya huduma na vifaa kulisababisha TAA kuwa na matumizi yasiokuwa na gharama nafuu kwa kipindi chote cha ujenzi wa jengo hilo.

2.3.6 Malipo yaliofanyika bila kufuata taratibu za Manunuzi

Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum ulipitia nyaraka mbalimbali ili kubaini iwapo mchakato wa manunuzi wakati wa ujenzi wa Jengo la watu mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ulifuata utaratibu. Katika Ukaguzi huu, ilibainika kuwa manunuzi yanayofikia kiasi cha Sh.737, 240,842 yaliyofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Dar es Salaam hayakufuta mchakato wa manunuzi.

Mheshimiwa Spika, kukiukwa kwa Sheria ya Manunuzi kunatoa taswira kuwa Watumishi wasiokuwa waaminifu walitumia mwanya huo kununua vifaa na huduma zilizo juu ya kiwango cha malipo ya kawaida kwa manufaa yao binafsi. Aidha, kukiukwa kwa Sheria hiyo kulisababisha uwepo wa matumizi mabaya ya fedha za TAA.

2.3.7 Mali, Vifaa na Samani kutothaminishwa na kuwekewa alama za utambuzi
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum umebaini kuwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) haina uthibitisho wowote wa hati za kupokelea mali, vifaa na samani husika (Delivery notes) unaonyesha kupokelewa kutoka kwa Mfadhili (China Sonangol International Limited, CSIL).
Mheshimiwa Spika, Kutokana na dosari zilizojitokeza kuhusiana na makabidhiano ya jengo na mali zilizopo, ni dhahiri kuwa kumekuwepo na mifumo dhaifu iliyosababisha kutokuwepo kwa makabidhiano rasmi ya Jengo hilo kutoka kwa Mfadhili. Uwezekano wa mali kuibwa, kuhamishwa, kuuzwa, kupotea au kubadilishwa ni mkubwa na zaidi mali hizo zitashindwa kujumuishwa katika Hesabu za mwaka za Mamlaka kinyume na utaratibu wa kimataifa wa Taarifa za Hesabu ( IFRS).
2.4 UKAGUZI MAALUM WA KUTHIBITISHA IWAPO KULIKUWA NA TIJA KATIKA MATUMIZI YA SHILINGI BILIONI 9 NA MILIONI 600 KATIKA VIKAO MBALIMBALI VYA MABARAZA YA WAFANYAKAZI, MANUNUZI NA MATANGAZO KATIKA MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA (TPA) KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012
Mheshimiwa Spika, Ukaguzi maalum wa matumizi ya zaidi ya Sh. 9,600,000,000 yaliokuwa yamefanywa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) uliombwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) baada ya kuchambua na kujadili Taarifa ya Hesabu za Mamlaka kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 212.
Mheshimiwa Spika, baada ya kujadili kwa kina Taarifa husika, Kamati ilimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya Ukaguzi maalum wa matumizi hayo ili kuona iwapo yalikuwa sahihi na kama TPA na Taifa lilipata tija kwa matumizi husika. Aidha, Ukaguzi maalum ulibaini mambo yafuatayo;
2.4.1 Matumizi ya Shilingi 684,705, 237 yalitumika bila kuwa na uhusiano na Vikao vya Wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika, baada ya Ukaguzi maalum na baada ya CAG kupokea majibu ya hoja za ukaguzi kutoka kwa Bodi ya TPA, ilibainika kuwa kuna matumizi ya Sh.684, 705,237 yaliofanyika lakini hayakuwa na uhusiano wowote na vikao vya wafanyakazi kama ilivyokuwa imetaarifiwa na Menejimenti ya TPA.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya fedha hizo kwa kazi isiyokusudiwa yanadhidhirisha uwepo wa mianya kwa watumishi wasiokuwa waaminifu kujipatia fedha za Umma bila ya kuzingatia Sheria na Miongozo ya matumizi ya fedha. Hadi tunapowasilisha Taarifa hii, Mamlaka ya Bandari Tanzania haijatoa uthibitisho wa namna fedha hizo zilivyotumika.
2.4.2 Kutopatikana kwa nyaraka za matumizi ya Sh. 384,199,742.40 zinazodaiwa kutumika kwa matangazo
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia Ukaguzi maalum na mahojiano na Kamati, ilibainika kuwa TPA wamekuwa wakifanya matangazo mbalimbali kwa njia ya redio, televisheni, magazeti na vipeperushi. Hata hivyo, katika uhakiki wa matumizi husika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi ya jumla ya Sh. 384,199,742.40 ambazo TPA walidai kuwa zilitumika kwa matangazo.
Mheshimiwa Spika, kutopatikana kwa uthibitisho wa nyaraka za matumizi ya fedha hizi ni kiashiria kingine cha udhaifu katika usimamizi wa fedha za Umma uliopo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Aidha, jambo hili pia ni kiashiria cha matumizi mabaya ya fedha za Umma na ubadhirifu.
2.4.3 Malipo ya viwango vipya vya Fedha za kujikimu TZS 62,825,725.97 (Perdiem) bila kupata kibali cha Msajili wa Hazina
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, na kwa kuzingatia maelekezo ya Ofisi hiyo yenye jukumu la kusimamia utendaji wa Mashirika ya Umma, Mashirika yote ya Umma yana wajibu wa kupata kibali cha Msajili wa Hazina kabla ya kuanza kulipa viwango vipya vya mishahara na posho za kujikimu.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya Ukaguzi maalum yamebainisha kuwa Bodi ya TPA iliidhinisha na kuanza kulipa Malipo na viwango vipya vya posho ya safari ya kujikimu kwa watumishi wake bila ya kupata kibali cha Msajili wa Hazina jambo ambalo ni kinyume na Sheria. Kwa mwaka husika wa Ukaguzi, Jumla ya Sh. 62,825,725.97 zililipwa kwa Watumishi wa TPA kinyume na utaratibu na matakwa ya Sheria.
Jedwali 4: Viwango vya Posho za kujikimu kwa Watumishi wa TPA (Ndani ya Nchi)
Ngazi ya MshaharaKiwango cha Posho (Kabla ya Mabadiliko)Kiwango cha Posho (Baada ya Mabadiliko)
TPSS 4270,000500,000
TPSS 3270,000400,000
TPSS 1-2217,000320,000
TPGS 7-8164,000215,000
TPGS 3-6118,000156,000
TPOS 494,000125,000
TPGS 1-294,000125,000
TPOS 1-394,000125,000

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiwa imepewa Jukumu la kikanuni la kusimamia matumizi ya fedha za Umma, katika Kikao chake cha tarehe 15 Januari, 2015 ilipokutana na Bodi na Menejimenti ya TPA iliagiza fedha hizo zote zilizolipwa kwa wahusika kinyume na utaratibu na kabla ya kibali cha Msajili wa Hazina (kilichotoka Januari, 2015) zirejeshwe mara moja. Ni imani ya Kamati kuwa hii itakuwa njia bora ya kudhibiti Bodi na Menejimenti za Mashirika ya Umma zinazokiuka miongozo ya Msajili wa Hazina katika masuala ya viwango vya mishahara na posho za kujikimu.
2.4.4 Manunuzi ya dharula yenye thamani ya Tshs. 6,355,500,000, Dola za Kimarekani 810,000 na Euro 13,915
Mheshimiwa Spika,[2]kifungu 42 (a) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2005 G.N No.97 kinawataka Maafisa masuhuli katika Taasisi za Umma kuhakikisha kuwa wanafanya maoteo ya manunuzi ya dharula yanayoweza kutokea katika mwaka husika wa fedha katika Taasisi zao na kisha kuainisha njia za ununuzi zitakazotumiwa ili kuhakikisha kuwa tija inapatikana katika manunuzi husika.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilishtushwa na manunuzi yenye thamani kubwa ya zaidi ya Shilingi Bilioni 8 za kitanzania kufanywa kwa njia ya dharula katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA). Kufuatia hoja hii ya Ukaguzi na kwa kuzingatia [3]kifungu 42(1) (c) ya GN No. 97 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPA) ya mwaka 2004, Mamlaka ya Bandari ilitakiwa kupata kibali cha Mlipaji Mkuu wa Serikali (Paymaster General) ili kuhalalisha udharula wa manunuzi yaliofanyika.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 6 Machi, 2013 kupitia barua yenye kumbukumbu Na.PPRA/AE/106/C/20 Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma ilimwandikia Mlipaji Mkuu wa Serikali ikimshauri kuwa ni vema manunuzi haya ya dharula yaliofanywa na TPA yakafanyiwa Ukaguzi maalum kutokana na utata uliopo. Ni kwa msingi huo hadi leo hii, Mlipaji Mkuu wa Serikali hajatoa kibali cha kuruhusu idhini ya uhalali wa manunuzi husika.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la manunuzi ya dharula na tena yenye thamani kubwa kama ilivyotajwa hapo juu, ni dhahiri kuwa fedha za Umma zimetumika vibaya kwa baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu kutengeneza udharula usiokuwepo ili wajipatie fedha kwa njia ya udanganyifu. Ukaguzi maalum umebainisha kuwa mambo yanayoitwa ya [4]dharula yaliohusisha manunuzi hayo ni ya muda mrefu na ya kihistoria ikiwa ni pamoja na msongamano wa mizigo bandarini, ufanisi mdogo wa Kampuni ya TITCS na pia kutumia fedha kwa dharula wakati manunuzi husika yalipangwa katika mpango wa mwaka wa manunuzi wa Shirika.
Mheshimiwa Spika, mapungufu katika uzingatiaji wa Sheria ya manunuzi kwa mujibu wa matokeo ya Ukaguzi maalum yamejitokeza pia katika maeneo ya ujenzi wa (a) gati namba 2 na 3 katika Bandari ya Dar es Salaam (b) Ujenzi wa magati katika [5]Bandari za mwambao wa ziwa Tanganyika ambapo imebainika kuwa Mkandarasi aliyepewa kazi hana uwezo wa kutosha na hivyo takribani Sh.5, 517,986,016 zipo hatarini kupotea iwapo hatua za haraka na za makusudi hazitachukuliwa na Serikali.
2.5 TAARIFA MAALUM KUHUSU MATOKEO YA UBINAFSISHAJI WA BENKI YA TAIFA YA BIASHARA (NBC) NA HATMA YA HISA ZA SERIKALI KATIKA BENKI HIYO
Mheshimiwa Spika, Kamati ina jukumu la kuangalia na kufuatilia uwekezaji unaofanywa na Serikali katika Mashirika mbalimbali ya Umma na Taasisi za kibiashara. Kamati hufanya kazi hii kwa karibu na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya kujadili Taarifa ya Msajili wa Hazina (The Treasury Statement) kila mwaka inayobainisha kwa kina Uwekezaji wa Serikali, Dhamana za Serikali, Mikopo ya Serikali na pia Mapato yatokanayo na Uwekezaji husika.

Mheshimiwa Spika, katika Taarifa ya Msajili wa Hazina kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2013 pamoja na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa husika, Kamati imebaini kuwa kuna uwezekano wa Serikali kupoteza hisa inazomiliki katika NBC iwapo jitihada za haraka hazitachukuliwa. Uchambuzi ufuatao wa Kamati kwa kuzingatia Taarifa nilizozieleza hapo awali unabainisha dosari za mchakato mzima wa kuuzwa kwa NBC na hatma ya uwekezaji wa hisa za Serikali.

2.5.1 Mchakato wa kuuzwa NBC

Mheshimiwa Spika, Baada ya kukamilika kwa marekebisho ya NBC kama ilivyoelekezwa na Baraza la Mawaziri kwa kuundwa kwa NMB Bank Ltd, NBC (1997) Ltd na NBC Holding Corporation, Serikali iliamuru mchakato wa mauzo ya hisa asilimia 70 ya hisa za NBC (1997) Ltd na NMB Ltd kwa Mwekezaji mahiri uanze. Mnamo mwaka 1998 NBC (1997) Ltd iliwekwa chini ya uangalizi wa iliyokuwa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma (Public Corporations Act) ya mwaka 1992. Matangazo ya awamu ya kwanza ya kukaribisha zabuni za ununuzi wa hisa asilimia 70 za NBC yalianza kutolewa kuanzia tarehe 1 Agosti mpaka 30 Novemba, 1998. Matangazo hayo yalitolewa kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi. Hadi kufikia tarehe ya mwisho ya wasilisho la zabuni 30 Novemba, 1998, Taasisi nne ziliwasilisha zabuni zao. Taasisi zililikuwa zifuatazo:
a) Stanbic (T) Limited;
b) The Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA);
c) First Adili Bancorp/Tanzanian Consortium; na
d) Barclays Bank Plc (UK).

Mheshimiwa Spika, Tarehe 5 Disemba, 1998, Timu ya Wataalam wa Serikali (Divestiture Technical Team) kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali ilifanya tathmini ya zabuni (Evaluation of technical bids). Kimsingi, katika tathmini hiyo, zabuni ya Barclays Bank Plc iliweza kupata alama za juu kwa wasilisho la kiufundi (technical bid), ingawa kwa upande wa wasilisho la kifedha (financial bid) lilikuwa na mapungufu mbalimbali ambayo yaliwasilishwa kwenye Kikao cha Makamishina wa PSRC (PSRC Commission) kwa taarifa na hatua zaidi. Makamishina wa PSRC baada ya kupitia Taarifa ya zabuni hiyo walielekeza zabuni hiyo itangazwe upya. Awamu ya pili ya zabuni ya ununuzi wa hisa asilimia 70 za NBC ilikuwa kwa njia ya barua za mwaliko wa wasilisho la zabuni kwa wazabuni 60 waliogawanyika katika makundi matatu. Makundi hayo ni:

a) Wazabuni 8 waliowasilisha zabuni zao kwenye zabuni ya awali ya Novemba, 1998;
b) Wazabuni 8 ambao walinunua “Information Memorandum/Bid Document” lakini hawakuwasilisha zabuni zao kwenye zabuni ya awali ya Novemba, 1998; na
c) Wazabuni 48 Wawekezaji mahiri ambao hapo awali waliandikiwa barua ya mwaliko na Mhe. Waziri wa Fedha kupitia barua yake ya tarehe 30 Oktoba, 1998.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 29 Januari, 1999 ilikuwa ni tarehe ya mwisho ya kuwasilisha zabuni hii kulingana na barua ya mwaliko iliyotajwa hapo juu. Hadi tarehe ya mwisho (29 Januari, 1999) ya wasilisho la zabuni, ni Taasisi nne tu ndizo zilizowasilisha zabuni zao. Taasisi hizo ni:
a) Stanbic (T) Limited;
b) ABSA Group of South Africa;
c) First Adili Bancorp/Tanzanian Consortium; na
d) Barclays Bank Plc (UK).

2.5.2 Kuuzwa kwa NBC kwa ABSA GROUP
Mheshimiwa Spika, ABSA Group Limited walishinda zabuni ya ununuzi wa asilimia 70 ya hisa za NBC kwa bei ya shilingi za Kitanzania billioni 15.0 ambazo zilikuwa ni sawa na Dola za Marekani millioni 21.834 kulingana na “exchange rate” ya tarehe ambayo makubaliano yalifikiwa, yaani tarehe 31 Machi 1999. Mazungumzo baina ya Serikali na ABSA juu ubinafsishaji wa NBC Ltd ikiwemo matakwa ya kisheria ya Benki Kuu juu ya hali ya kifedha/dhamana ya benki, mahitaji ya uwekezaji na bei ya mauzo yalifanyika kuanzia mwezi Februari, 1999. Pande husika zilikubaliana kwamba Serikali itoe dhamana za shilingi za Kitanzania billioni 28.7 wakati wa kufunga mauzo (yaani tarehe 31-3-2000) pamoja na guarantee ya kulipa any shortfall ili kufikisha mtaji wa Shillingi za Kitanzania billioni 7.8.

Mheshimiwa Spika, Serikali na ABSA walikubaliana kwamba Serikali italipa sehemu ya fedha za hiyo shortfall baada ya kukamilika kwa ukaguzi wa mahesabu ya kufunga mauzo. Baada ya ukaguzi kufanyika, dhamana zilizotakiwa kuongezwa ndani ya benki ili kufikia mtaji wa shilingi za Kitanzania billioni 7.8 zilikuwa ni Shilingi za Kitanzania billioni 6.094. ABSA Group walisaini mkataba wa awali wa mauzo tarehe 22 Julai, 1999 na kulipa Dola za Marekani 2,183,400 ambazo ni sawa na asilimia kumi (10%) ya bei ya manunuzi. Kwa mujibu wa makubaliano kiasi hicho kiliwekwa kwenye akaunti maalum (ESCROW ACCOUNT) ya ABSA Group iliyofunguliwa katika benki ya Standard Chartered hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ABSA Group Limited walisaini mkataba wa mauzo tarehe 14 Disemba, 1999 na kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo ndani ya mkataba huo, ABSA Group walilipa shillingi za Kitanzani billioni 12 kati ya shilingi billioni 15 (sawa na Dola za Marekani 14,999,630.86 kulingana na exchange rate ya Machi 31, 2000. Malipo hayo yalifanywa kwa njia ya bankers cheque iliyowasilishwa kwa Mwenyekiti wa NBC Ltd mnamo mwezi Machi 2000 wakati wa makabidhiano ya hisa. Cheque hiyo ilikuwa cleared na fedha kuingia kwenye account ya NBC iliyopo Chasemanhattan Bank USA mnamo tarehe 4 April 2000. Kiasi hicho cha Shilingi bilioni 12.0 kililipwa moja kwa moja NBC Ltd ili kujazia mtaji wa Benki na hivyo kuiwezesha NBC kukidhi masharti ya Benki Kuu ya Tanzania ya kupata leseni. Kwa mujibu wa Mkataba wa mauzo, ABSA Group walitakiwa kulipa shillingi za Kitanzania billioni 3 iliyobakia katika awamu tatu; shillingi bilioni 1.0 ilitakiwa kulipwa Machi 2004; shillingi billioni 1.0 ilitakiwa kulipwa Machi 2005 na shillingi billioni 1.0 ilitakiwa kulipwa Machi 2006. Kiasi chote cha shilingi bilioni 3.0 kililipwa Wizara ya Fedha kulingana na makubaliano.

2.5.3 Jukumu la Kuongeza Mtaji katika NBC
Mheshimiwa Spika, Serikali inamiliki asilimia thelathini (30%) ya hisa katika Benki ya NBC Limited. Tatizo la mtaji wa NBC Limited, lilianza kujitokeza kuanzia mwaka wa fedha 2010, hali ambayo ilipelekea NBC kupewa notisi na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kupewa taarifa kuwa, ifikapo tarehe 30 Juni, 2012 iwe imeongeza mtaji wake ili kutokiuka Sheria inayoihitaji benki hiyo kuwa na uwiano wa mtaji usiopungua kiwango cha asilimia 12 (Capital Adequacy Ratio). Serikali ilikubaliana na wanahisa wengine yaani ABSA GROUP na International Finance Corporation kuiomba Benki Kuu ya Tanzania kutoa ruhusa kwa NBC Limited kuendesha shughuli zake katika hali hiyo ya upungufu wa mtaji hadi tarehe 30 Septemba, 2012 ili kutoa nafasi kwa wanahisa kutafuta utatuzi wa namna ya kuongeza Mtaji wa Benki hiyo.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa ruhusa ya nyongeza ya muda wenye vipindi vya miezi mitatu hadi tarehe 31 Disemba, 2012 na kwa mara ya mwisho iliongeza muda wa ruhusa hiyo hadi tarehe 31 Machi, 2013. Katika ruhusa ya mwisho, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kuruhusu Mwanahisa atakayeshindwa kutoa mtaji katika benki awe tayari kupunguziwa umiliki wa hisa zake“diluted” ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa kuongeza mtaji ifikapo tarehe 31 Machi, 2013.
Mheshimiwa Spika, Katika Kikao cha Wanahisa kilichofanyika tarehe 25 Machi 2013; Wanahisa, kwa kauli moja, walikubaliana kuongeza Mtaji wa Benki NBC 1999 Ltd kwa kulipia hisa za ziada 570,000 kwa bei ya shilingi 131,766.00 kwa kila hisa. Ikiwa ni sawa na mtaji uliotakiwa kuongezwa katika NBC ili kufikia kiwango kinachotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania cha Shilingi za Kitanzania bilioni 75,049,620,000. Serikali ilitakiwa kutoa shilingi za Kitanzania bilioni 22.5 ikiwa ni asilimia 30 sawa na kiwango cha hisa inazomiliki.
Mheshimiwa Spika, Sababu zilizochangia kushuka kwa mtaji wa benki ya NBC 1999 Ltd na kuathiri ufanisi wake ni pamoja na utekelezaji na usimamiaji usio thabiti wa Utoaji wa Mikopo kwenye biashara ya Usafirishaji ambao uliigharimu benki kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 55 kutokana na wateja kutolipa mikopo hiyo. Mtaji wa benki ulipungua kutokana na utekelezaji wa Sera ya Benki Mama (ABSA) inayohusu utambuzi wa faida, ya “Group Retail Impairment Policy” ambayo ilichangia kupunguza faida ya benki NBC 1999 Ltd kwa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 30.
Mheshimiwa Spika, Benki ilipata hasara kutokana na makosa ya kiuhasibu kwa kutumia mfumo (accounting system) uliosababisha kutambua mapato hewa kwa kupitia “interest suspense account” ndani ya utunzaji wa hesabu za benki. Hali hii iliongeza hasara ya shilingi za Kitanzania bilioni 36.8 baada ya mapato hayo hewa kuondolewa.Gharama kubwa katika kukarabati na kuboresha mtandao wa mawasiliano (IT Replatforming) kulisababisha benki NBC 1999 Ltd kuingia gharama ya shilingi za Kitanzania bilioni 26 ambazo zilirekodiwa kihasibu kama ``intangible assets’’ ambazo Benki Kuu ya Tanzania haizitambui katika kukokotoa mtaji halisi wa benki[6] (TIER 1 CAPITAL RATIO).
Mheshimiwa Spika, Baada ya Wanahisa kukaa kikao cha tarehe 25 Machi 2013 walikubaliana kuongeza mtaji kwa kununua hisa za ziada kabla ya tarehe 31 Machi 2013; IFC (ambao wanamiliki asilimia 15 ya hisa katika NBC) pamoja na ABSA (wanaomiliki asilimia 55 ya hisa katika NBC) waliahidi kulipia hisa zao za ziada ifikapo tarehe 28 Machi 2013. Kwa kuwa Serikali kwa wakati huo haikuwa imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 22.5 katika Bajeti yake kwa ajili ya kuongeza mtaji katika NBC; Serikali ilikubaliana na Barclays/ABSA kuwa ABSA wailipie Serikali kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 22.5 katika benki ya NBC 1999 Limited kama mkopo kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Wakaguzi waliomba makubaliano hayo yaani “Memorundum of Understanding (MoU)” ya Serikali kukopeshwa kiasi hicho cha fedha na “call option agreement” lakini hayakuweza kupatikana kutoka kwa Msajiri wa Hazina. Hata hivyo Serikali itaendelea kumiliki asilimia 30 ya hisa katika NBC kabla ya tarehe 31 Machi 2015 kama itaweza kurudisha mkopo wa Barclays/ABSA (kwa maana nyingine kutekeleza ununuzi wa haki zake ambazo zilinunuliwa na Barclays/ABSA kwa kiingereza “to exercise her call option”). Serikali inalazimika kutekeleza ahadi hii kabla ya tarehe 31 Machi 2015 vinginevyo hisa za Serikali katika NBC zitapunguzwa (diluted).
Mheshimiwa Spika, Pia, wakaguzi walifanya kikao na maafisa kutoka kwa Msajili wa Hazina, Benki Kuu ya Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kujua ni lini Serikali italipa kiasi hicho lakini waliambiwa kuwa barua ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali bado inapitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
2.6 TAARIFA MAALUM YA KAMATI KUHUSU HALI YA KIFEDHA NA KIUTENDAJI YA KAMPUNI YA SIMU TANZANIA (TTCL)
2.6.1 Mheshimiwa Spika, tarehe 21 Januari 2015, Kamati ilifanya kikao cha mashauriano kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Msajili wa Hazina, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Menejiment ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL). Lengo la kikao hicho likiwa ni kutafuta namna bora ya kuikwamua TTCL kutoka katika hali mbaya ya kifedha na kiutendaji ili iweze kuhimili ushindani uliopo katika sekta ya mawasiliano nchini.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuelezea hali ya TTCL naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kuwa TTCL ilianzishwa kwa Sheria ya Kampuni ya Simu Tanzania Na. 20 ya mwaka 1993 na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni Na. 212, tarehe 31 Desemba 1993 baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania mwaka 1993. Hadi hivi sasa Hisa za TTCL zinamilikiwa na Serikali na Bharti Airtel Tanzania B.V kwa uwiano wa asilimia 65 na asilimia 35 sawia na hivi sasa kuna mazungumzo kati ya Serikali na Bharti Airtel juu ya Serikali kununua hisa asilimia 35 za Bharti Airtel ili imiliki asilimia 100 za TTCL.
2.6.2 Hali ya TTCL
a) Mapato na matumizi ya Kampuni kwa mwaka 2013
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa, TTCL ilipata hasara ya Sh. 20.883 bilioni kwa mwaka 2012 na hasara ya Sh. 16.258 bilioni kwa mwaka 2013.
Jedwali 5: Mapato na matumizi ya TTCL
2013
Sh.
2012
Sh.
2013/2012
Variance
2013/2012
Variance
Revenue93.613bn92.443bn1.170bn1%
Direct Costs(29.064bn)(37.917bn)(8.853bn)-23%
Gross Profit64.549bn54.526bn10.023bn18%
Operating Costs – Cash related(79.180bn)(73.686bn)5.494bn7%
Profit/(Loss) After Tax(16.258)(20.883bn)4.625bn22%

b) Majumuisho ya Hasara (Accummulated Losses)
Mheshimiwa Spika, kutokana na TTCL kupata hasara kwa muda mrefu, takribani kwa miaka 10, Kampuni sasa imekuwa na jumuisho kubwa la hasara ambayo kwa mwaka 2013 imefikia jumla la Sh. 334.48 bilioni. Ukubwa wa hasara hii umeiondolea TTCL mvuto wa kukopeshwa na Taasisi za Fedha hata zile zenye nia ya kuikopesha.
c) Hali ya kifedha
Mheshimiwa Spika, ukosefu wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa TTCL kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi wa TTCL kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Aidha, tangu TTCL ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango wa kutafuta mkopo kutoka mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na masharti ya kupata udhamini wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa fedha za kutosha kuendesha Kampuni kumesababisha TTCL kushindwa kuboresha au kukarabati miundombinu inayoendelea kuchakaa. Hivi sasa karibu asilimia 50 ya miundombinu ya TTCL ni michakavu (obsolete) na inahitaji kubadilishwa na mitambo ya kisasa.
d) Mizania Hasi (Deficit Shareholders Equity)
Mheshimiwa Spika, wingi wa hasara ikijumuishwa na uhaba wa uwekezaji umepelekea TTCL kuwa na mtaji hasi wa wanahisa (Negative shareholders Equity) ambapo mpaka kufikia mwaka 2013 TTCL imekuwa na mtaji hasi wa jumla ya Sh.87.896 bilioni. Hii ikitafsiriwa kitaalamu inamaanisha kuwa TTCL ni Kampuni muflisi.
Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2005 Serikali iliipa TTCL mkopo wa jumla ya Dola za Marekani milioni 28 kwa ajili ya kulipa wafanyakazi waliostaafishwa, deni hilo halijalipwa mpaka sasa na limefikiwa jumla ya Sh. 76.6 bilioni pamoja na riba. Aidha, ukiacha deni hili TTCL inadaiwa na TCRA jumla ya Sh. 25 bilioni hivyo kufanya jumla ya deni kuwa Sh. 101.6 bilioni.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kuna umuhimu wa Serikali kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye Sekta ya Mawasiliano ikizingatiwa kuwa Kampuni hiyo ndiyo inayoendesha Mkongo wa Taifa, ina wafanyakazi ( 1549) wanaotegemea ajira katika Kampuni hiyo na inatoa huduma ya internet kwa makampuni mengine ya simu nchini.


2.7 TAARIFA MAALUM KUHUSU DENI LA SH. 1,875,896,246,224.48 AMBALO SERIKALI INADAIWA NA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
2.7.1 Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Oktoba, 2014, Kamati ilifanya kikao cha mashauriano kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gavana wa Benki Kuu, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Msajili wa Hazina na Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
2.7.2 Mheshimiwa Spika, Dhumuni la kikao hicho lilikuwa kujadili na kutafuta ufumbuzi juu ya hoja ya ukaguzi iliyoibuliwa kwenye Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusiana na ukaguzi kwa Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma zinazoishia tarehe 30 Juni 2013. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo na ukaguzi uliofanyika baadaye, mpaka kufikia tarehe 30 Septemba 2014 Serikali ilikuwa inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii jumla ya Sh.1, 875,896,246,224.48. Aidha, ilifahamika kuwa deni hilo halijumuishi deni la Serikali kwa PSPF la Sh. 7,066,530,000,000.00 ambalo lilianza mwaka 1999 baada ya PSPF kulipa mafao ya Wanachama ambao kisheria walistahili kulipwa lakini walikuwa hawachangii kwenye Mfuko huo.
2.7.3 Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kulipwa kwanza kwa deni la Sh.1, 875,896,224.48 ili mifuko ya Hifadhi ya Jamii iweze kujiendesha bila matatizo, makubaliano yafuatayo yalifikiwa katika kikao hicho:-
a) Serikali kulipa kwanza asilimia 50 ya deni hilo kwa kutoa Hati fungani (Special Government Bond) ifikapo tarehe 14 Novemba, 2014 endapo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii itasamehe kiasi cha tozo kilichojumuishwa katika deni hilo kinachotokana na malimbikizo ya madeni kwa miradi na mikopo ya Serikali.
b) Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujadiliana na Bodi za Wadhamini kuhusu kuridhiwa kwa ombi la Serikali la kusamehewa na Mifuko hiyo kiasi cha tozo kilichojumuishwa kwenye deni hilo ili iweze kulipa sehemu ya deni hilo kwa utaratibu ulioelezwa hapo juu.
2.7.4 Mheshimiwa Spika, Bodi za Wadhamini wa Mifuko hiyo ziliridhia kusamehe tozo hizo endapo Serikali ingetoa Hati Fungani hiyo tarehe 14 Novemba, 2014. Lakini cha kusikitisha Serikali haikutimiza ahadi yake na mpaka Kamati inawasilisha taarifa yake makubaliano hayo hayajatekelezwa na Mifuko imeendelea kuwa katika hali mbaya ya kifedha. Kamati inapendekeza kuwa Serikali itekeleze makubaliano hayo mara moja na bila kuchelewa na ukopaji holela wa Serikali kwa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii nchini ukome mara moja.
2.8 TAARIFA MAALUM KUHUSU KAMPUNI YA NDEGE YA TANZANIA (ATCL)
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ilianzishwa mwezi Novemba 2002 baada ya Serikali kubinafsisha lililokuwa Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania Corporation, ATC); katika Shirika hilo, Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) lilinunua hisa asilimia 49 ndani ya ATC. Hata hivyo ubia kati ya ATCL na SAA ulikabiliwa na matatizo ya kiuendeshaji na kulazimika kusitishwa mwezi Agosti 2006 na ATCL kurejeshwa tena Serikalini kwa asilimia 100.
2.8.1 Hali halisi ya ATCL kwa sasa
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Msajili wa Hazina kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013 na kwa kuzingatia Taarifa ya Wizara ya Uchukuzi, imebainika kuwa ATCL kwa sasa ina Ndege moja tu aina ya Dash 8 – Q 300, Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House lililoko mtaa wa Ohio, Dar es Salaam huku ikiwa na madeni makubwa kama itakavyofafanuliwa hapo baadae.
2.8.2 ATCL imefikaje hapo ilipo kifedha na kuwa na Madeni makubwa?
Mheshimiwa Spika, baada ya kuvunjika kwa mkataba wa ubia baina ya SAA ana ATC, mnamo mwezi Machi 2008, Wizara ya Miundombinu kwa wakati huo iliingia katika makubaliano na Kampuni ya China Sonangol kuwa Kampuni hiyo ya China ingeleta ndege mpya 7 kwa ATCL ikiwamo Ndege 5 aina ya Airbus ambazo zingewasili mwaka 2012 na 2013.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Msajili wa Hazina na Uongozi wa Wizara ya Uchukuzi, Wakati ATCL ikisubiri ndege hizo mpya, Kampuni ya China Sonangol iliitambulisha Kampuni ya Wallis Trading Inc kwa ATCL na kisha Kampuni hizi mbili (Wallis Trading Inc na ATCL) zikaingia mkataba wa Ukodishaji ndege aina ya Airbus 320 kwa kipindi cha miaka 6 kwa Malipo ya USD 370,000 kila mwezi.
Mheshimiwa Spika, huu ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho wa ATCL, kwani baada ya Ndege hiyo kuwasili ilifanya kazi kwa muda wa miezi sita tu na baadae ilifungiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya usafiri wa anga. Ndege hiyo ilipelekwa kwa matengenezo makubwa mwezi Julai, 2009 nchini Ufaransa na haijawahi kurudi hadi leo wakati ambapo Serikali kama mdhamini wa ATCL anadaiwa fedha nyingi na Kampuni ya Wallis.
Mheshimiwa Spika, kutokana na deni la ATCL kwa Wallis linalofikia USD 42,459,316.12 hadi tarehe 31 Oktoba, 2011 na kufuatia majadiliano mbalimbali baina ya Serikali na Kampuni hiyo, Serikali imekwishalipa jumla ya USD 26,115,428.75 hadi sasa wakati bakaa inayodaiwa ni USD 23,996,327.82.
Mheshimiwa Spika, Kamati inasikitishwa sana na upotevu huu wa fedha za Umma ambao umetokana na mkataba mbovu ulioingiwa na watumishi wa Umma wasiokuwa waaminifu na uchungu na Taifa lao. Mabilioni ya fedha yanaoendelea kulipwa kwa Kampuni ya Wallis kwa huduma ya ndege iliyofanya kazi hapa nchini kwa miezi sita tu na kisha ndege hiyo kupelekwa Ufaransa kwa matengenezo ni fedheha kubwa kwa wazalendo wa Taifa letu. Aidha, Taarifa zinasema ndege hiyo ikiwa Ufaransa ilipakwa rangi na kukodishwa kwa Shirika la ndege la nchi ya Guinea wakati Serikali yetu ikiendelea kulipia tozo ya ukodishaji wa ndege husika.
Mheshimiwa Spika, ni wakati sasa kwa Serikali kuamua kwa dhati kushughulikia suala la ATCL kwa mapana yake ikiwa ni pamoja na kuangalia uhalali wa kulipa deni la Wallis (ambalo lipo chini ya dhamana ya Serikali, hivyo ni fedha za Umma) ambaye kimsingi naye alikiuka makubaliano ya Mkataba kwa kukodisha ndege iliyokuwa imekodishwa tayari kwa ATCL. Aidha, ni muhimu wahusika wa uingiaji wa mkataba husika wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke.
2.9 HOJA ZA UKAGUZI KUHUSU DOSARI KATIKA UMILIKI WA NYUMBA ZA MASHIRIKA
2.9.1 Bodi ya Sukari Tanzania
Mheshimiwa Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tangu mwaka 2012 amekuwa akitoa hoja kuhusu nyumba ya Bodi ya Sukari inayokaliwa sasa na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika.
Mheshimiwa Spika, Nyumba ya Bodi ya Sukari iliyopo kwenye Kiwanja Na. 482 Bray Road Masaki, Dar es Salaam ambayo anakaa Mhe. Stephen Wassira (Mb) haijarudishwa kwenye umiliki wa Bodi tangu February 12, 2008 kiongozi huyo alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Uratibu na Mahusiano. Juhudi za Bodi za kumuomba kiongozi huyo kurudisha nyumba hiyo na baadaye kuwasiliana na Katibu Mkuu Kiongozi kwa barua iliyoandikwa Disemba 2011 na kujibiwa Mwezi huo huo kwa ahadi kuwa nyumba hiyo ingerudishwa kwa Bodi ya Sukari hazikufanikiwa. Hivyo, mpaka Kamati inawasilisha Taarifa yake nyumba hiyo bado haijarudishwa.

Mheshimiwa Spika, Kufuatia kutorudishwa kwa nyumba hiyo mpaka sasa, Kamati iliielekeza Bodi ya Sukari kumuandikia barua Waziri husika ili arudishe nyumba hiyo na Msajili wa Hazina kuhakikisha umiliki wa nyumba hiyo unabaki kwa Bodi ya Sukari. Hata hivyo, Kamati ilipata taarifa kutoka kwa Msajili wa Hazina kuwa kwa sasa Serikali ipo katika mchakato wa kuhamisha umiliki wa nyumba hiyo kutoka Bodi ya Sukari kwenda Wakala wa Majengo (TBA), kitendo ambacho kinafanyika bila kuihusisha Bodi ya Sukari wala Msajili wa Hazina kinadhihirisha uwepo wa mipango ya baadhi ya watumishi ndani ya Serikali kwa makusudi au kwa kushinikizwa wanataka kuhakikisha nyumba hiyo inabaki katika umiliki wa mtu binafsi.
2.9.2 Bodi ya Korosho Tanzania
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa National Agricultural Products Board (NAPB) au Cashewnut Authority of Tanzania (CATA) na kuundwa Bodi ya Korosho, hatua kadhaa zilichukuliwa za kubadilisha majina yaliyokuwepo kwenye hati miliki za viwanja na nyumba kutoka majina ya NAPB au CATA kuwa Bodi ya Korosho.
Mheshimiwa Spika, Kamati imepata taarifa kutoka kwa CAG kuwa Bodi ya Korosho ilinyang’anywa umiliki wa Nyumba iliyopo kwenye Kiwanja Na. 37 maeneo ya Ursino, Upanga Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, Kiwanja hiko ambacho kilitakiwa kuhamishiwa kwenye umiliki wa Bodi ya Korosho, hapo awali tarehe 23 Januari 1967 kilisajiliwa kwa jina la National Agricultural Products Board kwa Hati Na. 9425. Miliki hiyo ilirejeshwa Ofisi ya Ardhi Kinondoni mnamo tarehe 13 Aprili, 2011. Ofisi hiyo iliandaa Hati nyingine kwa jina la Mohamed Said Hamad wa S.L.P 90164 Dar es Salaam. Hati husika ziliwasilishwa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi na kusainiwa tarehe 15 Aprili 2011 na baadaye kuwasilishwa Ofisi ya Msajili wa Hati na kusajiliwa kwa Hati Na. 98733.
Mheshimiwa Spika, Jambo la kushangaza tarehe 22 Juni, 2011 Ofisi ya Msajili wa Hati ilipokea nyaraka za uhamisho wa miliki hiyo kwenda kwa Ndugu Silvestry Francis Koka wa S.L.P 9014 Dar es Salaam. Baada ya uhamisho huo kufanyika, Mamlaka ya Korosho iliwasilisha nyaraka za zuio (caveat) mnamo tarehe 4 Mei 2012. Lengo likiwa ni kuzuia muamala wowote kuhusu miliki hiyo usifanyike. Aidha, Bodi ya Korosho Tanzania ilitoa taarifa kwa Ofisi ya Mkurugenzi Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili ifanye uchunguzi wa kina na kuwapata waliohusika kuhamisha na hatimaye kuuza kiwanja cha Bodi ya Korosho bila ridhaa ya mamlaka husika. Hivyo, kwa kuwa muamala uliofanyika una mazingira ya udanganyifu (fraud), Kamati inapenda kusisitiza uchunguzi wa DCI ukamilike haraka iwezekanavyo ili wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
2.10 TAARIFA MAALUM KUHUSU GHARAMA HALISI ZINAZOTUMIKA KATIKA KUTANGAZA BAJETI KWENYE MAGAZETI BAADA YA KUSOMWA BUNGENI
Mheshimiwa Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amebaini kuwa fedha jumla ya Sh.2,545,517,366.79 zilitumika kwa kipindi cha miaka miwili kama gharama za machapisho ya hotuba za bajeti za Wizara 21 na Taasisi 5 kama ilivyoainishwa katika Jedwali hapa chini. Aidha, kati ya matumizi hayo, kiasi cha Sh.184,239,208 kilikuwa bado kulipwa hadi wakati wa ukaguzi huu na kilihusu machapisho ya hotuba za bajeti kwa vipindi vya 2011/2012 na 2012/2013.
Jedwali 6: Fedha zilizotumika kwa kipindi cha miaka miwili
Mwaka wa FedhaIdadi ya WizaraIdadi ya TaasisiKiasi kilicholipwa (Sh)Kiasi bado kulipwa (Sh)Jumla ya matumizi (Sh)
2011/20121921,097,433,579.9234,175,248.001,131,608,827.92
2012/20131841,263,844,578.80150,063,960.071,413,908,538.87
Jumla2152,361,278,158.72184,239,208.072,545,517,366.79

Mheshimiwa Spika, kudhihirisha matumizi makubwa ya fedha zinazotumiwa na Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika kutangaza bajeti zao, Kamati ilibaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini peke yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ilitumia jumla ya Sh. 211,547,952 kwa ajili ya kutangaza Hotuba ya Bajeti ya Wizara kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Mathalani mojawapo ya chombo cha habari kiitwacho Jambo Concepts Tanzania kililipwa jumla ya Sh. 49.01 milioni ndani ya siku moja kwa ajili ya kutangaza Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo siku ya tarehe 13 Juni 2013. Jambo la kujiuliza ni msingi upi Wizara iliutumia katika kulipia Kiasi kikubwa cha fedha kwa chombo cha habari kimoja kwa Tangazo la siku moja wakati kwa vyombo vingine vya habari vililipwa wastani wa Sh. 9 hadi 11 milioni kwa huduma ya aina hiyo.
Mheshimiwa Spika, huu ni ushahidi wa wazi kuwa kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma yenye taswira za upendeleo kwa baadhi ya Taasisi za Umma kutumia mwanya wa kutangaza Hotuba za Bajeti za Wizara kwa malengo yasiyo bayana na ni viashiria vya matumizi mabaya ya madaraka na kukosekana udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma.
2.11 TAARIFA YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KUHUSU TATHMINI YA ZOEZI LA UBINAFSISHAJI
Mheshimiwa Spika, Mnamo mwaka 2012, iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilipendekeza kwa Bunge lako Tukufu na kisha kuridhiwa kama azimio la Bunge kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ifanye tathmini kuhusu zoezi zima la ubinafsishaji wa yaliokuwa Mashirika ya Umma ili kuangalia maeneo yapi zoezi husika lilifanikiwa na wapi halikufanikiwa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Ofisi ya CAG imefanya zoezi hilo kwa Mashirika kumi yaliobinafsishwa na wamewasilisha taarifa hiyo mbele ya Kamati. Kamati ipo katika hatua za awali za kushughulikia Taarifa hiyo ambayo pia nitaiwasilisha Ofisini kwako kwa maelekezo zaidi.



SEHEMU YA TATU
______________

3.0 MAPENDEKEZO YA KAMATI
3.1 Uwepo wa mapungufu mengi katika matumizi ya misamaha ya kodi katika mwaka wa fedha wa 2012/2013;
KWA KUWA, Misamaha ya kodi imeendelea kuongezeka kila mwaka na Taarifa ya awali ya ukaguzi wa misamaha hiyo uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeonyesha mapungufu makubwa katika matumizi ya misamaha hiyo kama ilivyoanishwa kwenye Sehemu ya pili ya Taarifa hii,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza yafuatayo;
a) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanzisha Kitengo cha kusimamia misamaha ya kodi ambacho kitakuwa na jukumu la kufuatilia matumizi ya misamaha ya kodi na kuwasiliana na Mamlaka zingine zenye jukumu la kutoa misamaha ya kodi.
b) Mamlaka ya Mapato ianzishe utaratibu wa kuzikagua (Inspection and Monitoring Visits) mara kwa mara Kampuni zilizopewa misamaha ya kodi kwa lengo la kuhakikisha Kampuni hizo zinatekeleza matakwa ya Sheria na kuepusha hasara inayotokana na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi. Aidha, TRA ihakikishe inaokoa kodi yenye thamani ya Sh.22,325,178,728 iliyopotea kutokana kukosekana kwa udhibiti na usimamizi mzuri wa matumizi wa misamaha ya kodi kwa kuitaka kampuni ya Geita Goldmines kulipa fedha hiyo pamoja na adhabu kali.
c) Mamlaka ya Mapato iongeze udhibiti wa misamaha ya kodi inayotolewa kwa waagizaji wa magari ikiwa ni pamoja na kuhakikisha gari lililosamehewa kodi linasajiliwa kwa jina la muagizaji (importer). Aidha, TRA ihakikishe Kampuni ya Kiliwarrior Expeditions Ltd na Kampuni ya Kilemakyaro Mountain Lodge Limited zinarudisha haraka iwezekanavyo mapato yaliyopotea ya Sh. 392,701,602 na Sh.53,399,565 sawia kutokana na udangajifu uliofanyika katika uigizaji wa magari na Kampuni hizo zifutiwe mara moja msamaha wa kodi wa kuingiza magari nchini
d) Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato ihakikishe inafanya uchunguzi na makampuni yanayodaiwa kodi kutokana na kutumia vibaya misamaha ya kodi yarudishe fedha hiyo na Maafisa wa Mamlaka ya mapato walioshiriki katika udanganyifu huo wachukuliwe hatua za kinidhamu na za kisheria.
e) Mamlaka ya Mapato ihakikishe maduka ya bidhaa zilizosamehewa kodi na makampuni yenye misamaha ya kodi yanawasilisha hesabu zake zinazohusu misamaha ya kodi kabla ya kufunga biashara. Aidha, TRA ifanye uchunguzi kuhusiana na matumizi ya msamaha wa kodi uliotolewa kwa M/s Conti- Africa Ltd kabla na baada ya kufunga biashara yake na kuhakikisha mapato yaliyopotea ya Sh.3,824,547,526 yanarudishwa na Kampuni hiyo.
f) Mamlaka ya Mapato ihakikishe Makampuni yaliyosamehewa kodi yanawasilisha Taarifa za Matumizi ya misamaha ya kodi kabla ya kupewa msamaha mwingine wa kodi.
g) Mamlaka ya Mapato ihakikishe maombi yote ya misamaha ya kodi hayashughulikiwi mpaka ziwasilishwe nyaraka sahihi zinazohitajika kisheria.
h) Menejimenti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ianzishe mchakato wa kurekebisha Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kuondoa misamaha ya kodi kwa ukarabati au upanuzi wa miradi ya Makampuni yaliofaidika na misamaha hapo awali wakati wa uanzishwaji wake.



3.2 Mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi maalum wa wa fedha za ushuru wa mauzo nje ya nchi na ruzuku ya Serikali kwa zao la korosho katika Mkoa wa Mtwara katika kipindi cha 2006/07 hadi 2010/11
3.2.1 KWA KUWA, Taarifa ya Ukaguzi maalum wa fedha za ushuru wa mauzo nje ya nchi na ruzuku ya Serikali kwa zao la korosho katika Mkoa wa Mtwara katika kipindi cha 2006/07 hadi 2010/11 imeonyesha kuwepo kwa mapungufu makubwa katika matumizi ya fedha hizo kama ilivyoanishwa kwenye Sehemu ya pili ya Taarifa hii,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza yafuatayo,
a) Fedha za ruzuku na ushuru wa mauzo ya korosho nje ya nchi Shs. 1,075,046,004 zilizotumika kulipia gharama za kuendesha ofisi kinyume na makusudio ya Sheria inayotaka fedha hizo zitumike kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho. Kwa mantiki hiyo Bodi ya Korosho inapaswa kuzirejesha fedha hizo kwenye akaunti ya pembejeo na zitumike kama Sheria inayoelekeza.
b) Bodi ya Korosho itoe mchanganuo kuonesha marejesho ya mikopo iliyotolewa 2006/2007 ipatayo Shs. 345,958,266 yalivyotumika.
a) Bodi ya Korosho kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ihakikishe inapeleka TAKUKURU maelezo kuhusu udanganyifu uliopelekea Kampuni ya Mukpar Tanzania Ltd kulipwa kimakosa Shs.223,815,000 ili uchunguzi uweze kufanyika. Aidha, Maafisa wa Bodi ya Korosho na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi watakaothibitika kushiriki kwenye udanganyifu huo wachukuliwe hatua za kinidhamu na za kisheria.
b) Uagizaji wa pembejeo za korosho na hasa madawa ufanywe kwa mfumo wa uagizaji wa pamoja (Bulk Procurement) kwa zabuni itakayoendeshwa na Bodi ya korosho na wasambazaji wakubwa, wa kati na wadogo wanunue kutokana na zabuni hiyo na kusambaza kwa wakulima. Hii itaondoa ukiritimba wa uagizaji wa madawa na kushusha bei ambayo mkulima ananunua madawa na kuondoa kwa kiasi kikubwa rushwa iliyokithiri katika biashara ya madawa ya korosho.
c) Bodi ya Korosho kama msimamzi na mlipaji wa fedha ihakikishe malipo yanafanyika baada ya Halmashauri husika kuthibitisha kutoa kibali na pia kupokea pembejeo ili kuepuka pembejeo zilizokwishalipiwa kutoletwa na wauzaji wa pembejeo hizo.
d) Bodi ya Korosho pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo(ARI) ziendelee kushirikiana na Maafisa Kilimo kutoa elimu kwa wakulima mara kwa mara kuhusiana na matumizi ya madawa/pembejeo ili kuepuka migogoro ya wakulima kukataa kutumia pembejeo zilizolipiwa ruzuku.
e) Bodi ya Korosho izingatie mapendekezo ya wakulima wakati wa kufanya mchakato wa kuagiza pembejeo ili kukidhi matakwa ya wakulima.
f) Bodi ya Korosho na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ziendelee kufanya ukaguzi wa madawa mapema kabla hayajasambazwa kwa wakulima ili kuepuka usambazaji wa madawa yaliyokwisha muda wake wa matumizi.
g) Halmashauri zihakikishe zinatunza kumbukumbu za malipo ya fedha za ruzuku na ushuru wa korosho ghafi ili kuwezesha uhakiki wa fedha hizo wakati wowote inapotakiwa.
h) Halmashauri zifanye juhudi kuhakikisha kuwa fedha zote zinazohusu pembejeo zilizokopeshwa kwa wadau/Vyama vya Msingi katika msimu wa mwaka 2006/07, zinakusanywa na kupelekwa katika Mfuko wa Pembejeo wa Wilaya kama ilivyoamriwa na kikao cha RCC cha tarehe 26 Mei 2010 ili kuendelea kuwanufaisha wakulima wengine.
i) Bodi ya Korosho izingatie mgawanyo wa fedha na matumizi ya kila Halmashauri, ili kila Halmashauri itumie kulingana na kiwango ilichotengewa.
j) Bodi ya Korosho isihamishe fedha za Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine bila kupata idhini ya Halmashaui yenye fedha husika.
3.2.2 KWA KUWA, Uzalishaji wa Korosho umeongezeka na kufikia takribani tani 200,000 kwa mwaka katika msimu uliokwisha na kwamba Tanzania inapoteza fedha za kigeni kwa wastani wa dola za kimarekani 110 milioni kwa mwaka katika kipindi cha miaka 5 iliyopita kutokana na kuendelea kuuza korosho ghafi nje ya nchi (The African Cashew Alliance Report 2014),
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza kuwa sehemu ya ushuru wa korosho (Export levy) unaopelekwa Hazina utumike kujenga Viwanda vya kubangua Korosho vya ngazi ya kati na ngazi ya chini ( vijijini) mpaka hapo nchi itakapoweza kubangua korosho yote nchini. Aidha, Viwanda vitakavyojengwa viendeshwe kwa ubia kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Ushirika wa Wakulima.
3.3 Utata juu ya gharama halisi za Ujenzi wa Jengo la kumbi za Watu Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere
KWA KUWA, Taarifa ya Ukaguzi maalum wa Ujenzi wa Jengo la kumbi za watu mashuhuri katika Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere imeonyesha kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za Umma na ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Manunuzi kama ilivyoanishwa kwenye Sehemu ya pili ya Taarifa hii,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza Serikali kupitia vyombo vyake vya dola ikiwepo TAKUKURU kufanya uchunguzi wa jinai kwa walioshiriki kuipotezea Serikali zaidi ya Shilingi bilioni 9 na Wahusika wachukuliwe hatua za kisheria haraka iwezekenavyo.
3.4 Mapungufu yaliyojitokeza katika Ukaguzi Maalum wa Matumizi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
KWA KUWA, Taarifa ya Ukaguzi maalum wa matumizi mbalimbali ya fedha za Mamlaka ya Bandari Tanzania imeonyesha kuwepo na ukiukwaji mkubwa wa Sheria za Fedha, Sheria ya Manunuzi, usimamizi mbovu wa miradi ya Mamlaka, udhibiti mdogo katika matumizi ya fedha za Mamlaka na ubadhirifu katika malipo yanayofanywa kwa Wafanyakazi,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza yafuatayo:-
a) Mamlaka ya Bandari Tanzania iongeze udhibiti katika matumizi yanayofanyika kwa ajili ya vikao vya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama zisizo za lazima na idadi ya vikao visivyo vya lazima. Aidha, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aendele kufuatilia kwa umakini matumizi yanayofanyika katika eneo hili kila mwaka.
b) Mamlaka ya Bandari Tanzania ihakikishe inaboresha mfumo wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu ili kudhibiti suala la ukosefu wa kumbukumbu na nyaraka. Aidha, Mamlaka ya Bandari iwasilishe kwa Wakaguzi nyaraka zinazothibitisha matumizi ya jumla ya Sh. 384,199,742.40 zinazodaiwa kutumika kwa matangazo tu.
c) Mamlaka ya Bandari Tanzania izingatie matakwa ya Sheria zinazosimamia fedha kabla ya kuanza kufanya malipo ya aina mbalimbali hususan kwa wafanyakazi wake.
d) Serikali ichukue hatua za haraka na za makusudi kuokoa jumla ya Sh.5,517,986,016 ambazo ni gharama ya ujenzi wa magati katika mwambao wa Ziwa Tanganyika ambapo imebainika kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania imempa kazi ya ujenzi wa magati hayo Mkandarasi asiye na uwezo wa kifedha na sifa za kufanya ujenzi huo.
3.5 Mapendekezo mahsusi kuhusu ya kuikwamua Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na hatma ya Hisa za Serikali katika Benki hiyo
KWA KUWA, Serikali inaelekea kupoteza umiliki wa asilimia 25 za hisa katika NBC kama itashindwa kulipa Shilingi bilioni 22.5 kwa Barclays/ABSA kabla ya tarehe 15 Machi 2015,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza yafuatayo:-
a) Gavana wa Benki Kuu, Msajili wa Hazina na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wafanye mapitio ya mchakato wa ubinafsishaji wa Benki ya NBC na mikataba yote (Technical Assistance Agreement, Shareholding agreements, uwiano wa uongozi ndani ya NBC) iliyoingiwa hapo awali ili kuona kama kuna tija ya vifungu na makubaliano waliyomo katika mikataba hiyo kwa sasa ili waweze kuishauri Serikali hatua za kuchukua kuikwamua NBC na kulinda hisa za Serikali katika Benki hiyo.
b) Baada ya Tathmini hiyo Serikali ihakikishe inalipa Shilingi bilioni 22.5 kwa Barclays/ABSA kabla ya tarehe 15 Machi 2015 ili kunusuru hisa zake kuchuliwa;
c) Serikali baada ya kulipia hisa zake ifikiriye kuziuza kwa wananchi kama ilivyoainishwa kwenye mkataba kuwa baada ya kubinafsisha NBC hisa za Serikali zitauzwa kwa wananchi.
d) Serikali kupitia NBC ihakikishe inawachukulia hatua za kisheria haraka iwezekanavyo Wafanyabiashara wote waliohusika na uchukuaji wa mikopo ya usafirishaji iliyopelekea NBC kupata hasara kubwa.


3.6 Mapendekezo ya Hatua mahsusi za kuikwamua Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)
KWA KUWA, kuna umuhimu wa kuikwamua Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye sekta ya mawasiliano,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza hatua zifuatazo zichukuliwe haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuikwamua TTCL:-
a) Serikali kununua hisa asilimia 35 zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika TTCL kwa gharama ndogo ikizingatiwa Bharti Airtel haikutimiza kikamilifu masharti ya mkataba wa mauziano ya hisa hizo hapo awali kwani tangu inunue hisa hizo haijafanya uwekezaji katika Kampuni ya TTCL.
b) TTCL isamehewe deni la Serikali Sh. 76.6 bilioni na deni la TCRA Sh. 25 bilioni ambayo jumla yake ni Sh. 101.6 bilioni na fedha hizo zipelekwe kuongeza mtaji ili Kampuni itoke kwenye kuwa na mtaji hasi wa Sh. 87.896 bilioni na kuwa na mtaji chanya wa sh. 13.704 bilioni. Likifanyika hili basi Kampuni hiyo itaweza kukopesheka.
c) Serikali ikamilishe taratibu zake za kuimilikisha TTCL Mkongo wa Taifa ili izidi kuuendeleza kwa ufanisi na kuongeza mapato ya TTCL.
d) Kutokana na TTCL kuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi (1549) isiyoweza kuwalipa kuna umuhimu wa kufanya Marekebisho ya Muundo wa Kampuni. Aidha, zinahitajika Sh. 32 bilioni kwa ajili ya kugharamia urekebishaji wa muundo wa Kampuni ili uendane na mahitaji ya utoaji wa huduma mbalimbali.
e) Serikali itakapokamilisha umiliki wake kwa asilimia 100 iwekeze mtaji zaidi baada ya kufanya tathmini ya mahitaji ya Kampuni. Hatua hii ihusishe kuwezesha Watanzania kumiliki kampuni hii kupitia soko la Hisa la Dar es Salaam.

3.7 Mapendekezo ya kuinusuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii isishindwe kutoa huduma kwa Wanachama wake na Wastaafu kutokana na Serikali kushindwa kuilipa Deni la Jumla ya Sh.1, 875,896,246,224.48.
KWA KUWA, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inakabiliwa kupungukiwa uwezo wa Fedha za kujiendesha kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh. 1,875,896,246,224.48 kama ilivyoainishwa kwenye Sehemu ya Pili ya Taarifa hii,
NA KWA KUWA, Kamati imefanya kila linalowezekana kuwezesha deni hilo lilipwe kwa manufaa ya wanachama wa Mifuko hiyo na Wastaafu,
HIVYO BASI, Kamati inaliomba Bunge lako Tukufu kuazimia Serikali ilipe deni hilo haraka iwezekanavyo ile kuinusuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika changamoto ya kushindwa kulipa mafao ya Wastaafu na kutoa huduma nyingine.
3.8 Mapendekezo kuhusu deni la USD 23,996,327.82 ambalo ATCL inadaiwa na Wallis Trading Inc.
KWA KUWA, Serikali haikunufaika na mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus kutoka kwa Kampuni ya Wallis baada ya ndege hiyo kugundulika ni mbovu ndani ya miezi sita na kupelekwa kutengenezwa kwa muda mrefu,
NA KWA KUWA, Serikali inaendelea kulipa tozo ya ukodishaji wa ndege hiyo ambayo haifanyika kazi,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza yafuatayo;
a) Serikali kuangalia uhalali wa kulipa deni la Wallis ambaye kimsingi naye alikiuka makubaliano ya Mkataba kwa kukodisha ndege iliyokuwa imekodishwa tayari kwa ATCL.
b) Serikali ihakikishe inawafikisha kwenye vyombo vya Sheria ili haki itendeke kwa wahusika wa uingiaji wa mkataba huo unaoendelea kuipa hasara Serikali kwani hadi sasa hakuna kesi iliyopelekwa mahakamani mahususi kwa waliongia mkataba husika.

3.9 Mapendekezo kuhusu umiliki wa nyumba za Mashirika ya Umma
3.9.1 Bodi ya Sukari Tanzania
KWA KUWA, Nyumba iliyopo Kiwanja Na. 482 Bray Road Masaki, Dar es Salaam ni chanzo cha mapato ya Bodi ya Sukari na Uhamishaji wa umiliki wa nyumba hiyo kwenda TBA haukushirikisha Bodi husika,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza kwamba utwaaji wowote wa nyumba za Shirika lazima ufuate taratibu za kisheria ikiwemo maamuzi ya Bodi husika. Bunge liitake Serikali kufuata taratibu za kuichukua nyumba ya Bodi ya Sukari (iwapo ni kwa masalahi mapana ya Taifa) kuipeleka Wakala wa Nyumba ( TBA). Hatua hii pia ihusishe Bodi ya Sukari kulipwa thamani ya nyumba hiyo ili kukomesha mtindo wa Serikali kujichukulia nyumba za Mashirika ya Umma bila kufuata taratibu na kuzimilikisha kwa watu au Viongozi binafsi kama ilivyokwishatokea miaka ya nyuma.
3.9.2 Bodi ya Korosho Tanzania
KWA KUWA, Uuzaji wa Nyumba iliyopo kwenye Kiwanja Na. 37 maeneo ya Ursino, Kinondoni, Dar es Salaam una mazingira ya udanganyifu (Utapeli) wa kughushi nyaraka na matumizi mabaya ya madaraka ambayo ni makosa ya jinai,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza Jeshi la Polisi likamilishe uchunguzi na kuwafikisha mahakamani waliohusika na uuzaji wa nyumba ya Bodi ya Korosho na Msajili wa Hazina ahakikishe Bodi ya Korosho inapata hati miliki ya nyumba zake zote bila kuchelewa.
3.10 Mapendekezo Kuhusu Gharama za Matumizi ya Wizara na Taasisi zake kutangaza Hotuba za Bajeti
KWA KUWA, imebainika kuwa Wizara na Taasisi nyingi za Serikali zinatumia gharama kubwa kwa matangazo ya Hotuba za bajeti, NA KWA KUWA matangazo hayo hayalingani na tija ya gharama zilizotumika,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, atoe kipaumbele maalum cha Ukaguzi kukagua matumizi husika na pia Maafisa masuhuli waagizwe kupunguza matumizi hayo yasiokuwa ya lazima kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.





















SEHEMU YA NNE
______________
4.0 Hitimisho
4.1 Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati imeeleza kwa kina namna Kamati ilivyotekeleza majukumu yake ya msingi na mafanikio iliyopata katika utekelezaji wa majukumu yake. Pamoja na kuainisha mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika Hesabu za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013 na kutoa mapendekezo ya namna ya kuondoa mapungufu hayo kwa maendeleo ya Taifa.
4.2 Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa uongozi wako makini ambao umeniwezesha mimi kuwasilisha Taarifa hii hapa Bungeni na kuiwezesha Kamati yangu kutekeleza majukumu yake bila vikwazo kwa kutoa maelekezo na miongozo thabiti pale Kamati ilipohitaji msaada wako.
4.3 Mheshimiwa Spika, ninapenda kuwashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi kwa jinsi tulivyoshirikiana katika kuweka mikakati mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge na Kamati zake.
4.4 Mheshimiwa Spika, nawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa kutekeleza majukumu ya Kamati hii kwa moyo na uadilifu mkubwa. Aidha nawapongeza kwa kushiriki kikamilifu katika kuboresha mijadala, maoni na mapendekezo ya Kamati na kunipa heshima ya kuiwasilisha Taarifa hii mbele ya Bunge lako tukufu. Mheshimiwa Spika, naomba kuwatambua Wajumbe hao kama ifuatavyo,
1) Mhe. Zitto Zuberi Kabwe, Mb - Mwenyekiti
2) Mhe. Deo Haule Filikunjombe, Mb - M/Mwenyekiti
3) Mhe. Asha Mshimba Jecha, Mb - Mjumbe
4) Mhe. Dkt. Hadji H. Mponda, Mb - Mjumbe
5) Mhe. Hezekiah N. Chibulunje, Mb - Mjumbe
6) Mhe. Gaudence C. Kayombo, Mb - Mjumbe
7) Mhe. Abdul Jabir Marombwa, Mb - Mjumbe
8) Mhe. Zaynab Matitu Vullu, Mb - Mjumbe
9) Mhe. Lucy Fidelis Owenya, Mb - Mjumbe
10) Mhe. Ester Nicholas Matiko, Mb - Mjumbe
11) Mhe. Deusiderius John Mipata, Mb - Mjumbe
12) Mhe. Ali Keissy Mohamed, Mb - Mjumbe
13) Mhe. Zainabu Rashid Kawawa, Mb - Mjumbe
14) Mhe. Kheri Ali Khamis, Mb - Mjumbe
15) Mhe. Faida Mohamed Bakar, Mb - Mjumbe
16) Mhe. Ismail Aden Rage, Mb - Mjumbe
17) Mhe. Modestus Dickson Kilufi, Mb - Mjumbe
18) Mhe. Kombo Khamis Kombo, Mb - Mjumbe
19) Mhe. Catherine V. Magige, Mb - Mjumbe
20) Mhe. Lolesia J. Bukwimba, Mb - Mjumbe
21) Mhe. Amina M. Mwidau, Mb - Mjumbe

4.5 Mheshimiwa Spika, Napenda kumshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas D. Kashililah kwa ushauri wake kwa Kamati kwa kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu ya Kamati. Shukrani kwa Idara ya Kamati za Bunge kwa kuratibu shughuli za Kamati chini ya Makatibu wa Kamati ya PAC Ndugu. Mathew N. Kileo na Ndugu. Erick S. Maseke, pamoja na Waandishi wa Taarifa Rasmi za Bunge.
4.6 Mheshimiwa Spika,katika kutekeleza kazi zake, Kamati ilikuwa ikishirikiana na Wataalam kutoka Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali na Kamishna wa bajeti. Nawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kuhakikisha Kamati hii inatekeleza majukumu yake vema.
4.7 Mheshimiwa Spika, Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Naomba kutoa Hoja.

Mhe. Zitto Z. Kabwe, Mb.
MWENYEKITI
KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI (PAC)
28 Januari, 2015


[1] Makubaliano ya awali yaliosainiwa tarehe 13 Machi, 2007

[2] Kanuni ya 42(a) ya Kanuni za Ukaguzi wa Umma za Mwaka 2005

[3] Regulation 42(1) (c) of GN 97 of the PPA , 2004

[4] Ukurasa wa 37 wa Kitabu cha Hoja za Ukaguzi Maalum uliofanywa na CAG kuhusu TPA

[5] Kipili, Kagunga, Lagosa and Sibwesa Jetties

[6] TIER 1 CAPITAL RATIO
Means the ratio of (a) Tier 1 capital, comprised of common stock and retained earnings, less goodwill or any other intangible assets to (b) risk weighted assets and off-balance sheet exposures as defined in terms of the BASLE PAPER
View attachment 222684
 
mkuu hii serekali ya ccm imejaa madudu mengi ya ufisadi ndo maana dawa yao ni kuipiga chini "serekale" nzima hapo October!
 
Back
Top Bottom