“Operesheni Mauaji” 1976 vs "Operesheni Tokomeza" 2013

EMT

Platinum Member
Jan 13, 2010
14,483
15,303
Wakati taifa likipita katika kupindi kigumu cha kupima uadilifu wa viongozi, wengine wakijiuzulu huku wengine wakendelea kulalamika, hebu tujikumbushe kwa kifupi yaliyotokea Shinyanga mwaka 1976 halafu linganisha na yalitokea mwaka 2013 (zaidi ya miaka 40 baadae).

Mnano Januari 24, 1976, Serikali iliitisha kikao mjini Shinyanga chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati ule, Rashid Mfaume Kawawa, kuzungumzia na kutafuta suluhisho juu ya wimbi la mauaji ya kulipiza visasi, lililozuka katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Waliohudhuria kikao hicho, ni pamoja na aliyekuwa Waziri, Ofisi ya Rais (Usalama wa Taifa), Siyovelwa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi na maofisa wa Polisi Waandamizi pamoja na Watendaji Wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa kutoka Dar es Salaam na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa hiyo miwili.

Katika kikao hicho, ilikubaliwa ianzishwe ‘Operesheni Mauaji' kuwakamata wote walioshukiwa kujihusisha na mauaji ya watu wasio na hatia, kwa ajili ya kuhojiwa ili kupata watuhumiwa halisi kwa njia zinazokubalika kwa kuzingatia sheria, kinyume chake, mahojiano hayo yaligeuka mateso ya binadamu na mauaji ya kutisha.

Mkoani Shinyanga, mahojiano ya kikatili na kuteswa yalifanyika wilayani Maswa, kijiji cha Ng'wanang'holo ambapo mkoani Mwanza, watuhumiwa walifungwa kwenye Gereza la Butimba na kuchukuliwa kila siku kupelekwa Kigoto kwa mahojiano, ambako Mazegenuka na Ng'wana Ng'hoboko walikumbana na mauti kwa njia ya kuteswa kwa kipigo.

Akizungumza na Mtanzania mwaka 2007, Mzee Nhalilo Ikerenga Mkigila, mmoja wa walioteswa katika operesheni hiyo na ambaye amelemaa mkono na makovu mengi mwilini kutokana na mateso akiwa gerezani, alisema kuwa mwaka 1974 Serikali ilieendesha operesheni ya kukamata watu waliotuhumiwa kuwa ni wachawi na ndipo alikumbwa na huo mkasa kijijini kwake Manonga Wilayani Maswa hata kuwekwa mahabusu katika gereza la Nhumbu- Shinyanga sehemu anasema kuwa alikuwa akipata mateso ya kinyama hata kumsababishia athari za kiafya na hata watu wengine 6 walikamatwa katika mkumbo huo kufa baada ya muda mfupi.

"Tulikuwa tunachapwa kwa viboko, tunapakwa maji ya pilipili kwenye njia ya haja kubwa, kwenye sehemu zilizochubuka baada ya kuchapwa, wanawake walikuwa wakibakwa kwenye sehemu zao za siri, machoni na hata kuna kipindi ilinisababishia upofu," alisema.

Alisema kuwa wanaume na wanawake katika gereza hilo walikuwa wanavuliwa uchi na kuwekwa sehemu moja huku mateso haya ya kinyama yakiendelea, anasimulia jinsi ambavyo walipokuwa wanaamishwa katika gereza la Mwanholo mkuu wa gereza la kwanza aliwasomea dua akisema: "Ndugu zangu kutoka Shinyanga naomba Mungu awasaidie mrudi salama, mtakwenda Mwanholo mtakayoyaona huko naomba Mungu awasaidie mrudi salama," alisema mkuu wa gereza la Nhumbu.

Operesheni hii iliendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa (Area Commissioner) kwa kipindi hicho Michael Mabawa ambaye alikuwa akituma polisi kukamata watu waliohisiwa na jamii kuwa ni wachawi. Operesheni hiyo iligubikwa na uongo mwingi hata madaktari waliohusika kufanya uchunguzi wa majeruhi, licha ya kuwa watu hao waliteswa, kukosa hewa na kuwa na njaa, waliandika kuwa vifo hivyo vilikuwa vya kawaida.

Januari 22, 1977, Mawaziri wawili, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Usalama wa Taifa), Peter Siyovelwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi (baadaye Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili), walijiuzulu kwa kuwajibika kwa mauaji ya raia wawili, yaliyofanywa na polisi mkoani Mwanza kwa njia ya mateso bila wao kujua. Kwenye barua yake ya kujiuzulu, Mwinyi aliandika: "Kisiasa nakiri kuwa nahusika, siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi."

Mwinyi aliendelea kukiri kwamba: "…vyombo vinavyohusika na utekelezaji, polisi ikiwemo, vilivuka mipaka ya wajibu wao na vikajipa madaraka ya kuogelea katika vitendo viovu vya kishenzi, kinyama na kikatili hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa kushukiwa tu kwamba wanahusika wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu." Mwinyi alisema: "Kwa hiyo, Mwalimu, nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hili, naomba unikubalie kujiuzulu."

Licha ya mawaziri hao wawili pamoja na wakuu wa mikoa ya Mwanza, Peter Kisumo, na Marco Mabawa wa mkoa wa Shinyanga ajiuzulu kwa kuwajibika. Mkuu wa Wialya ya Maswa, Michael Mabawa nae alistaafishwa kwa manufaa ya umma. Hata hivyo, aliyekuwa kinara wa maelekezo yaliyosababisha hatua kuchukuliwa, Waziri Mkuu Rashid Kawawa alipoteza tuu wadhifa wake kwa muda.

Maofisa wawili wa ngazi za juu serikalini; Ofisa Usalama Mkoa wa Mwanza, Godfrey James Ihuya na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Isaias Kassim Mkwawa, walishitakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka saba baada ya kupatikana na hatia kwa kosa la kuuaa bila kukusudia. Maofisa Usalama wa Taifa wengine wawili, Andrew Ibrahimu Mayalla na James Mulokozi; nao walipata kifungo hicho kwa kusababisha kifo cha Masaga Mahulu Mazegenuka wa mjini Mwanza, na Ng'wana Ng'hoboko, kutoka wilaya ya Magu wakati wakiwahoji kwa njia ya mateso na utwezaji eneo la Kigoto mjini Mwanza, ambako walipelekwa na kuhojiwa, wote wakituhumiwa kushiriki katika wimbi la mauaji ya watu waliodhaniwa wachawi na majambazi katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza mwaka huo. Kwa Mkoa wa Mwanza pekee, watu 374 walikamatwa na kuhojiwa; na kwa mkoa wa Shinyanga, watu 390 walikamatwa katika operesheni hiyo iliyopewa jina la "Operesheni Mauaji."

Hukumu hiyo, iliyotolewa mjini Mwanza na aliyekuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu nchini, Nassoro Mzavas, ilielezewa kuwa ya kihistoria kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kwa wale waliokabidhiwa jukumu la kulinda sheria, amani na utulivu, kuhukumiwa kwa vitendo vya ukatili na kinyama; na kwa wale waliokabidhiwa madaraka ya kusimamia vyombo vya Serikali, kuwajibika kwa kujiuzulu nyadhifa zao kwa kuficha nyuso zao. Hizo zilikuwa enzi za utawala bora nchini, kitu kinachoelekea kutoweka leo.

"Operesheni Mauaji" ilisimamishwa na mauaji kuanza tena kiasi kwamba kufikia mwishoni mwa miaka 1980s, hali ilikuwa mbaya sana. Mwaka 1988, serikali aliamua kuunda Tume a Mongela kufanya uchunguzi. Tume hiyo iliripoti kuwa kati ya mwaka 1970 hadi 1984, watu 3693 (wanaume 1407 na wanawake 2286) waliuawa Tanzania nzima kwa kuhisiwa kuwa ni wachawi . Kati ya hao, vifo 2347 (63.5%) vilitokea Mwanza, Shinyanga na Tabora. Tokea kipindi hicho, mauaji bado yamekuwa yakiendelea, kiasi cha kufikia hata kuuawa kwa alibino kwa sababu za kichawi.

Baada ya miaka zaidi ya 40 tunaambiwa kuwa serikali imerudia unyama ule ule kwenye operesheni yake ya "Operesheni Tokomeza" dhidi ya majangili Serikali inatuhumiwa kwa kufanya;

  1. Mheshimiwa Spika, badhi ya wananchi wakiwemo viongozi, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na Watumishi wa Serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi Kamati ilipozuru maeneo hayo. Mfano; Vijana watatu wa Kijiji cha Osteti, Kata ya Chapakazi, Wilayani Kiteto, walituhumiwa kujihusisha na biashara ya Meno ya Tembo. Vijana hao ni Nyafuka Ng'onja, Ng'onja Kipana na Mswaya Karani.
  2. Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao. Mfano; ndugu Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanae wa kiume (11) akishuhudia. Pia alidai kulazimishwa kuchora picha ya Chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake. Vilevile, Bi. Neema Moses wa Babati alidai kuvuliwa nguo na kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa chupa sehemu zake za siri.
  3. Aidha, baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa. Mfano; katika Kata ya Iputi, Wilaya ya Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na Askari wawili (2) wa Operesheni Tokomeza Ujangili mida ya usiku. Vilevile, mama mmoja mkazi wa Kata ya Matongo Wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu (3) wa Operesheni Tokomeza Ujangili huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki.
  4. Watuhumiwa waliokamatwa walifanyiwa upekuzi bila kuhusisha viongozi wa Serikali za maeneo husika na kutokuwepo kwa mashahidi na hati za upekuzi. Mfano; Ndg. Abdallah Pata na Bi. Flora Mwarabu wa Kata ya Iputi Wilayani Ulanga na Ndg. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati, walipekuliwa bila kufuata utaratibu.
  5. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa waliopelekwa katika kambi za mahojiano walidai kutwezwa kwa adhabu zinazokiuka haki za binadamu. Mfano; Diwani wa Kata ya Sakasaka wilaya ya Meatu Ndg. Peter Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama kuning'inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti. Mheshimiwa Spika, kutokana naukatili uliopitiliza, baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti).
  6. Mheshimiwa Spika, ilidaiwa kuwa wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili, baadhi ya watuhumiwa walipoteza mifugo, mali na fedha zao. Mfano; katika Wilaya ya Ulanga Kata ya Iputimwananchimmoja alidai kuporwa sanduku la VICOBA lenye shilingi laki saba na nusu (750,000/=) pamoja na simu ya mkononi na Askari wa Operesheni Tokomeza waliovamia nyumbani kwake. Vilevile Ndugu Musa Masanja wa Sakasaka Wilaya ya Meatu, alidai kuporwa shilingi laki tatu 300,000/= pamoja na simu 2 za mkononi na Askari Askari wa Operesheni. Mheshimiwa Spika,Pia ilidaiwa kuwa mifugo ya watuhumiwa ilikamatwa na kuingizwa ndani ya maeneo ya hifadhina kufa kwa kupigwa risasi au kukosa maji na malisho kutokana na kuzuiliwa kwa muda mrefu.
  7. Baadhi ya mifugo ilitozwa faini bila stakabadhi au stakabadhi kuonesha viwango vidogo ikilinganishwa na fedha halisi iliyolipwa. Mfano:Ndugu Sosoma Shimula mwenye Ng'ombe 1700 Wilayani Kasulu alidai kwamba alitakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni thelathini (30,000,000/=, alipowasihi alipunguziwa hadi Milioni kumi na mbili (12,000,000/=) hata hivyo aliweza kulipa Milioni kumi (10,000,000/=). Alionesha Kamati stakabadhi inayoonesha kuwa amelipa faini ya shilingi milioni moja tu (1,000,000/=). Stakabadhi hiyo ilijazwa sehemu ya tarakimu, lakini hakuna kilichoandikwa katika sehemu ya kiasi cha fedha kwa maneno. (Tazama Kiambatisho Na. 4)
  8. Mheshimiwa Spika, baadhi ya watuhumiwa walidai kupigwa na kuumizwa na askari wa Operesheni na wengine kupata ulemavu wa kudumu. Mfano; katika Wilaya ya Itilima,Kijiji cha Mbogo NdgSita Rumala alidai kupigwa na kuvunjwa mkono alionesha wajumbe mkono uliokuwa umefungwa bandeji ngumu (P.O.P). Aidha, Diwani Peter Samwel Ndekija wa Kata ya Sakasaka, Wilaya ya Meatu, alidai kupigwa na kuumizwa vibaya mgongoni na alionesha kwa wajumbe wa Kamati makovu aliyoyapata. Vilevile,ilielezwa kuwa Ndugu Munanka Machumbe (24) ambaye ni bubu alipigwa risasi 3zilizomjeruhi mapajani na kuharibu sehemu za siri wakati akijaribu kuwahoji Askari wa Operesheni kwa ishara sababu za kumtesa baba yake. Aidha, katika tuko lingine Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ali Mohamed (70) aishiye kijiji cha Iputi, alidai kurushwa kichura na kutandikwabakora na Askari wa Operesheni Tokomeza.Pia,Ndg. Nyasongo Magoro Serengeti waKata ya Majimoto wilaya ya Mulele alidhalilishwa mbele ya wananchi wake. (Tazama Kiambatisho Na. 5)
  9. Mheshimiwa Spika,wakati wa Operesheni, mifugo mingi ilikuwa hifadhinilakini hata ile iliyokuwa nje ya hifadhi iliingizwa na askari wa hifadhi na wafugaji kutakiwa walipe faini ya shilingi Milioni tatu (3,000,000/=) hadi Sita (6,000,000/=) kwa idadi ya ng'ombe 30 hadi ng'ombe 100 na aliyeshindwa kulipa faini mifugo yake iliuawa au kupigwa mnada na mfugaji kufilisiwa. Walioshindwa kulipa faini mifugo ilipigwa mnada na wafugaji hawakuruhusiwa kununua wala kukaribia eneo la mnada, na katika mnada mifugo iliuzwa kwa bei ya chini kuliko faini iliyotozwa Mfano; shilingi elfu sitini (60,000/ kwa kila ng'ombe.
  10. Ilidaiwa kwamba, baadhi ya watuhumiwa walidai kubambikwa makosa ambayo hawahusiki nayo kama vile kumiliki silaha kinyume na sheria, kukutwa na bangi au nyara za Serikalimfano; Bw. Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati alidai kubambikiwa kesi ya kumiliki bunduki kukutwa na mkia wa twiga kinyume cha sheria. Mheshimiwa Spika, pia Bibi Zuhura Ali wa Kilombero alidai kuteswa huku akilazimishwa kutoa silaha ambayo hakuwa nayo. Aidha, Bw. Melkzedeck Abraham Sarakikya wa Itigi alidai kuteswa akilazimishwa atoe silaha.
  11. Mheshimiwa Spika, baadhi ya wananchiwalidai kuwa ndugu zao waliteswa kikatili kwa muda mrefuna bila kupatiwa huduma za lazima kama chakula, maji na matibabu (siku 1 -2) hadi mauti yalipowafika. Kwa mfanoNdg. Kipara Issa wa Wilaya ya Kaliua na ndugu Emiliana Gasper Maro wa Gallapo, Wilaya ya Babati. Aidha, wananchi hao walidaikuwa mahojiano kwa watuhumiwa yaliambatana na mateso makali kwa muda mrefu kiasi cha kusababisha vifo. (Tazama Kiambatisho Na. 6). Vilevile, watuhumiwa wengine waliodaiwa kupoteza maisha wakati wa Operesheni Tokomeza ni Ndg. Wegesa Kirigiti wa Kijiji cha Remagwe na Ndg. Peter Masea wa Kijiji cha Mrito (Tarime), Ndg. Mohamed Buto (Masasi) na Gervas Nzoya (Kasulu).
  12. Mheshimiwa Spika, pamoja na uthibitisho wa picha zilizotolewa na wananchi kuhusu kuteswa hadi kufa kwa Bi Emiliana Gasper Maro, Serikali kupitia Mkurugenzi wa Wanyamapori ilitoa Taarifa kwa Umma ikipinga Taarifa iliyorushwa na kituo cha luninga cha ITV tarehe 19 Oktoba 2013 kuhusu mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Askari wa kupambana na ujangili. Taarifa hiyo ya Serikali inapinga kuwa Askari wa Operesheni Tokomeza hawauski na kifo cha mtajwa. Taarifa hiyo imeonekana kukosa umakini kutokana na kujichanganya juu ya watu inaowazungumzia. Taarifa hiyo inazungumzia majina mawili tofauti (Evelyn Gasper na Mariana Gaspar Mallo wa eneo la Olongadiola) wakati muathirika halisi ni Bi. Emilliana Gasper Maro wa Kijiji cha Orngadida, Gallapo. (Tazama kiambatisho Na.7)
  13. Mheshimiwa Spika, kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanyama ilidaiwa kwamba ng'ombe walipigwa risasi, na ndama walikufa kwa kukosa maziwa kutokana na mama zao kukamatwa na kuzuiwa kwenye mazizi yaliyopo maeneo ya hifadhi kwa muda mrefu. (Tazama Kiambatisho Na. Rushwa kwenye Mapori ya Akiba).
  14. Mheshimiwa Spika,Wananchi walidai kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa watumishi wanaosimamia mapori ya akiba ya Maswa, Kigosi Moyowosi, Burigi, Kimisi na Mkungunero kwa kutaja majina ya baadhi ya watumishi wanaowatuhumu. Mfano; Ndg. Kileo mtumishiwa pori la Maswa, alidaiwa kuwa na tabia ya kutoza wananchi faini bila stakabadhi au kutoa stakabadhi kinyume na faini iliyotolewa au kutoa stakabadhi bandia. Aidha, katika pori la Kigosi-moyowosi, watumishi wafuatao walidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa; Ndg. Msocha, Alfred, Kobelo na Odhiambo. Aidha, ilidaiwa kuwa katika mapori ya Kigosi Moyowosi na Kimisi zaidi ya wafugaji 100 wenye ng'ombe wanaokadiriwa kuwa 50,000 wanalipia kuchungia ng'ombe wao kwenye mapori hayo ya hifadhi tangu mwaka 2000 kwa malipo maalum na hata Operesheni Tokomeza haikuwagusa.
  15. Aidha, ilidaiwa kuwaNdg. Msocha (Meneja wa Pori la Akiba la Kigosi Muyowosi), alituhumiwa na baadhi ya wananchi kuwa amekuwa akiwakodisha wafugaji hao kwa vipindi vya miezi mitatu, na wafugaji huruhusiwa kulipa tena muda unapoisha. Aidha, Mfugaji ambaye hulipa kiasi kidogo hulazimishwa kulipa huku akipigwa namifugo yake kuuawa kwa kupigwa risasi. Ilielezwa kuwa, Wafugaji na Askari Wanyamapori huwasiliana kwa simu ilil kutekeleza makubaliano ya malipo kwa malisho yao. Nambaza simu zinazodaiwa kuwa za Askari Wanyamapori zimeorodheshwa. (Tazama Kiambatisho Na. 9)
 
Haya hayatofautiani sana na yale yaliyotokea Mtwara, Tena nakumbuka baada
ya ajali iliyoua wanajeshi kadhaa muheshimiwa nchimbi aliahidi kuwa damu yao
haitaenda bure.....

Lakini kwa kuwa Mtwara HAWASTAHILI CHOCHOTE mambo yamepita salama bila
kuundwa kamati na kama imeundwa basi haijafanya kazi yake kama ilivyotokea
huko kwa Wenzetu. Watu wameuwawa, watu wameteswa watu wamepata ulemavu
watu wamebakwa kuna tofauti gani?
 
isikiie kwenye mitandao tu lakini pindi ikitokea ndugu yako amepata ukilema kwa sababu ya mtu ambaye anatembelea V8 HAAAA SIJUI ITAKUWAJE?
 
Haya hayatofautiani sana na yale yaliyotokea Mtwara, Tena nakumbuka baada
ya ajali iliyoua wanajeshi kadhaa muheshimiwa nchimbi aliahidi kuwa damu yao
haitaenda bure.....

Lakini kwa kuwa Mtwara HAWASTAHILI CHOCHOTE mambo yamepita salama bila
kuundwa kamati na kama imeundwa basi haijafanya kazi yake kama ilivyotokea
huko kwa Wenzetu. Watu wameuwawa, watu wameteswa watu wamepata ulemavu
watu wamebakwa kuna tofauti gani?
MIMI NATAKA MUONE UCHUNGU WALIOUPATA WAPEMBA 2001.KUPITIA WATANGANYIKA, MALIPO HAPA HAPA DUNIANI
 
3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom