09 Dec, 2019: Maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika. Wafungwa 5,533 wapata msamaha wa Rais. Mbowe ataka maridhiano ya Kitaifa

Return Of Undertaker

JF-Expert Member
Jun 12, 2012
4,572
26,867
Habari wadau! Tukutane hapa kujua yanayojiri leo mwanza kwenye mahadhimisho ya miaka ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika:

Update: Majeshi mbalimbali ya gwaride yanaingia uwanjani.
Updates: Waziri mkuu na rais wa Zanzibar wanaingia uwanjani pamoja na makamu wa rais

Leo nawaona wanajeshi toka China wakiwa jukwaa kuu.




09:15 Rais Magufuli ndio anaingia uwanjani

“Nilitembelea Magereza nikashuhudia kuna mlundikano wa wafungwa, mpaka leo kuna Wafungwa 17,547 na Mahabusu 18,256, hii ni idadi kubwa, kwa hao wafungwa kuna baadhi wamefungwa makosa madogo, sijui kaiba kuku, kujibizana na mpenzi wake.

“Leo natangaza kuwasamehe wafungwa 5,533, ni mara ya kwanza kwa msamaha mkubwa kama huu kutokea, najua watu watashangaa lakini nimetumia siku hii ya Uhuru kusamehe, sifurahi kuongoza nchi yenye watu wengi Magerezani.

“Msamaha huu utawahusisha wafungwa waliofungwa kati ya kipindi cha siku moja hadi mwaka mmoja, na wale Wafungwa waliofungwa Miaka mingi kama 30, 20, 10 au mitano na wamebakiza muda mfupi kumaliza. Aliyewasamehe ni Mungu.” Rais Magufuli.

"Wakati tunapata Uhuru tulikuwa na Chuo Kikuu kimoja lakini kwa sasa tumefikia Vyuo Vikuu 48, lakini pia hata idadi ya watu wakati tunapata Uhuru tulikuwa Milioni 9 lakini sasa tuko zaidi ya Mil. 55." - Rais @Magufuli.

Mbowe, aomba maridhiano, demokrasia, uhuru na upendo.

WATUHUMIWA 256 WA UHUJUMI UCHUMI WALIOOMBA MSAMAHA WAACHIWA

Lakini pia napenda kuipongeza ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali - DPP wakishirikiana na mahakama kwa kufuta kesi na kuachia mahabusu zaidi ya 345…lakini pia imefuta kesi za waliokuwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi 256,” – Rais Magufuli


#Miaka58YaUhuru

========

MIAKA 58 YA UHURU: Historia yaandikwa

HISTORIA ya aina yake imeandikwa katika sherehe za miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 57 ya Jamhuri, zilizofanyika kwa mara ya kwanza katika Kanda ya Ziwa, na mkoani Mwanza.

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana, uwanja huo na maeneo ya jirani vikiwamo Viwanja vya Furahisha, kuliandikwa historia kutokana na kufana kwa sherehe hizo, zilizohanikizwa na burudani mbalimbali za kwaya, muziki wa kizazi kipya, wa jadi (Sungusungu), gwaride, halaiki na maonesho ya ndege vita.

Historia hiyo inatokana na ukweli kwamba katika sherehe za jana, mambo ya msingi ya kitaifa yalipewa kipaumbele cha pekee na Rais John Magufuli na viongozi wengine wa kitaifa.

Mbali ya Rais Magufuli, sherehe hizo zilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hasssan, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, maspika Job Ndugai (Bunge la Tanzania), Zubeir Ali Maulid (Baraza la Wawakilishi Zanzibar).

Pia walikuwapo majaji wakuu, Profesa Hamis Juma (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na Othman Makungu (Zanzibar) pamoja na marais wastaafu Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu wastaafu Mizengo Pinda, John Malecela, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Lakini pia walikuwapo viongozi wa vyama vya upinzani akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuhudhuria sherehe za kitaifa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani 2015.

Mbowe alifuatana na viongozi wake mbalimbali wakiwamo wabunge John Mnyika (Kibamba), John Heche (Tarime Vijijini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na aliyekuwa Mbunge wa Ilemela, Ezekiel Wenje na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu. Viongozi wengine wa upinzani walikuwa ni John Cheyo (UDP), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), John Shibuda (ADA-TADEA), Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFFP), Said Soud Said na Hamad Rashid Mohammed (ADC).

Mambo yaliyofanya sherehe hizo kuwa za kihistoria ni pamoja na uamuzi wa Rais Magufuli, kuwasamehe wafungwa 5,533, idadi ambayo ni kubwa na haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii.

Wafungwa hao waliosamehewa ni wale walioko magerezani kwa kufungwa kuanzia siku moja hadi mwaka mmoja, waliofungwa miaka mingi kuanzia miaka mitano hadi 30 waliobakiza mwaka mmoja kumaliza vifungo vyao. Rais Magufuli alisema ametoa msamaha huo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45(1)(a-b) na Sheria ya Magereza Kifungu cha 49 Sura ya 58.

Uamuzi huo wa kihistoria wa Rais kusamehe idadi kubwa ya wafungwa, pia unatokana ziara yake ya hivi karibuni kwenye Gereza Kuu la Butimba mkoani Mwanza ambako alishuhudia msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu, lakini pia hali hiyo iko katika magereza yote nchini. Alisema kwa mujibu wa takwimu alizo nazo, kuna jumla ya wafungwa 17,547 na mahabusu 18,256 nchini, hivyo kufanya jumla yao wote kuwa 35,803.

“Pia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Waziri wa Katiba na Sheria wamefanya kazi kubwa na kuwasamehe mahabusu 345 na waliokuwa wanakabiliwa kesi mbalimbali na 256 wa kesi za uhujumu uchumi, kwa hiyo watu 601 wameachiwa huru,” alieleza Rais Magufuli.

Aliwataka wanufaika wa msamaha huo, kujutia makosa yao na wasirudie makosa au kusiwepo na mtu mwingine yeyote, kufanya makosa akidhani atapa msamaha.

Idadi ya waliosamehewa kila mkoa
Aliitaja mikoa na idadi ya wafungwa na mahabusu waliosamehewa kwenye mabano kuwa ni Kagera (713), Dodoma (385), Morogoro (365), Mara (260), Mbeya (259), Kigoma (252), Tanga (245), Geita (230), Rukwa (214), Arusha (208) na Manyara 207.

Mikoa mingine ni Tabora (207), Mwanza (190), Ruvuma (181), Singida (139), Simiyu (136), Lindi (299), Pwani (128), Iringa (110), Songwe (96), Katavi (74), Shinyanga (74) na Njombe 70.

Alisema wanufaika wa msamaha huo, wataanza kutoka magerezani leo. Rais alimkabidhi Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike orodha ya wafungwa wote watakaonufaika na msamaha huo.
Alimkabidhi orodha hiyo papo hapo mbele ya umati. Viongozi watoa kauli Jambo jingine la kihistoria kwenye sherehe hizo jana ni uamuzi wa Rais Magufuli kuwapa nafasi ya kuzungumza viongozi mbalimbali, wakiwamo wastaafu na viongozi wastaafu.

Sherehe za Uhuru zilizoeleka kuwa ni za gwaride tu na shughuli nyingine chache bila ya kuwapo kwa hotuba, lakini katika miaka ya karibu, kiongozi wa nchi amekuwa akitumia kutoa hotuba, lakini jana akaenda mbali zaidi na kuwapa nafasi wastaafu, wapinzani na viongozi wengine kusalimia wananchi.

Miongoni mwa walioongumza ni marais wastaafu Mkapa na Mwinyi, lakini pia Rais wa Zanzibar, Dk Shein, mawaziri wakuu wastaafu Pinda, Lowassa, Malecela na Sumaye, pamoja na viongozi kadhaa wa upinzani.

Viongozi hao kwa sehemu kubwa walisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, umoja, mshikamano na kufanya kazi ili taifa liondokane na utegemezi.

“Mimi nawahimiza Watanzania wote tuendelee kudumisha umoja, amani na tufanye kazi kwa bidii,” alisema Mkapa aliyewasalimu wananchi kwa salamu yake iliyokuwa maarufu wakati wa utawala wake, akisema “Mambo.”

Kwa upande wake, Mzee Mwinyi aliyekuwa maarufu kwa jina la “Ruksa” wakati wa utawala wake kati ya mwaka 1985 hadi 1995, alianza kwa kuonesha umahiri wake katika lugha ya Kiswahili, akionesha utofauti wa matumizi ya maneno ya “Nawapongezeni na “Nawapongeza.”

Lakini ujumbe wake, ulikuwa ni kukubali kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais Magufuli, akimpongeza. Aliwataka Watanzania kumwombea dua Rais ili jicho la wabaya lisimdhuru, lakini pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutunza amani, umoja na usalama wa nchi.

Naye Lowassa ambaye mwaka 2015 alipambana na Dk Magufuli kuwania urais akiwa na Chadema kabla ya kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni, aliwataka Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli kwani mtindo wake wa uongozi, utaletea taifa maendeleo makubwa katika kipindi chake cha miaka 10.

Sumaye ambaye kama Lowassa alikimbilia Chadema mwaka 2015, kabla ya kujitoa wiki iliyopita, akidai kufanyiwa ‘figisu’ katika kuwania Uenyekiti wa Kanda ya Pwani na ule wa Taifa wa Chadema, alisema kama taifa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ya kupata uhuru wa kiuchumi ili kuondokana na utegemezi.
Cheyo wa UDP na Profesa Lipumba wote walipongeza kazi kubwa, inayofanywa na Rais Magufuli, na kuwataka kuendelea kuwaunga mkono.

Hamad Rashid ambaye ni Waziri wa Afya katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alizungumzia suala la kulinda amani na Muungano wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia viongozi hao wa vyama vya upinzani, wakiongozwa na Mbowe, walitaka sherehe hizo zisaidie kuwepo na maridhiano ya kisiasa na utengamano wa kisiasa na kuimarisha demokrasia.

“Miaka 58 ya Uhuru ni uthibitisho kwamba kuna haja ya kuwepo kwa maridhiano, mshikamano na upendo kati yetu, siku ya leo ifungue milango ya kupendana, maridhiano yatakayotusaidia katika kujenga taifa letu,” alisema Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro.

Mbowe alisema Rais Magufuli ana nafasi ya pekee ya kujenga maridhiano na utengamano nchini.

Sherehe Kanda ya Ziwa

Katika kuvunja mazoea, serikali iliamua sherehe hizo kufanyika Kanda ya Ziwa katika Mkoa wa Mwanza. Hiyo ni historia kubwa iliyobebwa na sherehe za miaka 58 ya Uhuru, kwani mara nyingi sherehe hizo hufanyika Dar es Salaam na Dodoma. Rais Magufuli aliwasifu wananchi wa Kanda ya Ziwa, kwa kujitokeza kwa wingi ndani na nje ya Uwanja wa CCM Kirumba katika sherehe hizo. Alisema haijapata kutokea.

“Ikumbukwe kuwa hatukufanya sherehe hizi kwa miaka miwili, mwaka 2015 na mwaka 2018 na badala yake fedha zake zilifanya kazi za maendeleo,” alisema Rais Magufuli.

“Hivyo hivyo ndio sababu tukaamua tufanye sherehe hizi mkoani Mwanza tofauti na ilivyozoeleka, hii ni kwa sababu ya kubadili mazoea.”

Alisema sherehe hizo huambatana na fursa mbalimbali, kuchochea maendeleo ya mkoa huo. Jambo jingine la kihistoria lililopamba sherehe hizo jana ni kundi la wananchi wa kabila la Wasukuma 1,200 walioingia uwanjani, wakiwa wamevalia mavazi ya asili.

Wasukuma hao ni walinzi wa jadi maarufu Sungusungu. Wakiwa uwanjani hapo walicheza na kuimba na kuzunguka uwanja, hali iliyonogesha zaidi sherehe hizo.

Watanzania wapongezwa
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewapongeza Watanzania kwa maendeleo waliyoyapata katika miaka 58. Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi nzuri, inayofanywa na Watanzania wenyewe. Katika hilo, aliwataka Watanzania wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili matunda ya kuwa huru kisiasa, yatoe mbegu bora ya kuwa huru kiuchumi.

Aliyataja baadhi ya mambo makubwa ya kimaendeleo, yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 58 ya Uhuru ni ujenzi wa kilometa 12, 679.55 za barabara za lami kutoka kilometa 360 za lami wakati nchi inapata Uhuru, kilometa zingine zaidi ya 2,400 zinajengwa na zingine 7,087 zipo katika hatua mbalimbali za kuanza kujengwa.

Kuhusu sekta ya afya, alisema vituo vya kutolea huduma ya afya, alisema vimeongezeka kutoka 1,095 wakati tunapata Uhuru hadi kufikia 7,293 kwa sasa, lakini pia wataalam katika sekta mbalimbali nao wameongezeka.

Nafasi ya Tanzania kimataifa
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, katika kusherehekea miaka 58 ya uhuru, Tanzania inajivunia kwa mchango ilioutoa kimataifa ikiwemo ukombozi wa Bara la Afrika, kutafuta amani na kujenga mtangamano, kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Pia alisema katika miaka 58 ya Uhuru, Tanzania imekuwa na mahusiano mazuri na mataifa mbalimbali duniani.

Chanzo: Habari leo
 
Dhana ya wewe ukisusa wengine wala huku maisha yakiendelea kama kawaida imeanza kuwaingia baadhi ya wanasiasa!

Ni sawa na mtoto ambaye kama hujamtimizia baadhi ya maombi yake hususa kula chakula ulichompikia akitegemea utambembeleza lakini ukimpuuza baadaye anaanza tena kukuomba chakula akidai ana njaa!

Niwapongeze wale wanasiasa ambao wamefanya self assessment na kugundua kuwa kususa kwao kwenye sherehe za kitaifa hakuna impact yoyote ya kisiasa kwa taifa na kwa sababu hiyo wameamua kubadili msimamo!
 
Ving'ora vinapita mtaani kwetu nyasaka hapa Sasa sijui ndo wanawahi kabla mvua kunyesha na Kama kawa kumejaa wingu na Giza ngoja nisogeze kiangalia mbali labda Kuna chochote
 
Habari wadau! Tukutane hapa kujua yanayojiri leo mwanza kwenye mahadhimisho ya miaka ya miaka 58 ya uhuru wa Tanganyika
Tena safari hii na sisi washabiki wa chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema, tutashiriki kikamilifu kwenye maadhimisho hayo, tena tukiwa tumevaa date za chama chetu cha Chadema

In Magufuli's voice "Maendeleo hayana chama"
 
Tabia za ovyo wewe na familia yako unahisi kila familia iko hivyo. Wengine mtoto akisusa mzazi huwezi kula. Mitabia yenu ya kikatili ya sukumana land msilete humu.
Wewe umejuaje kama hiyo tabia yako ambayo mtoto akisusa na wewe mzazi wake huwezi kula sio tabia ya hovyo?

Nani amekuambia mimi ni msukuma lakini pia unaonekana unachuki na wasukuma na una fikra za kibaguzi.

Kwa hiyo unataka kuniambia na kuwaaminisha wasomaji kuwa wasukuma wana tabia za hovyo!
 
Kuna baadhi ya wanasiasa wamesema hawawezi kuhudhuria kwenye sherehe ya kumbukumbu ya uhuru wa Tanganyika kwa sababu hakuna uhuru.

Tusije kushangaaa kuona wanasiasa waliosema hawawezi kuhudhuria wanakuwa mstari wa mbele katika kuelezea na kukosoa yatakayojiri kwenye sherehe hizo katika uwanja wa Kirumba, Mwanza.

Hawa wanasiasa lazima waelewe kuwa hata kuangalia tukio la kumbukumbu ya uhuru kwenye luninga (Tv) haina tofauti na mtu ambaye amehudhuria sherehe hizo. Kama hawataki kuhudhuria kwenye sherehe hizo kwa sababu hazina maana kwa sasa basi wasiangalie hata yanayojiri kwa kutumia luninga (Tv) ili kuutendea haki msimamo wao.

Kutokuangalia yanayojiri kwa njia ya luninga (Tv) watakuwa wamelitendea haki tangazo lao la kutokuhudhuria kwenye sherehe hizo.

Nchi hii kuna baadhi ya watu utawasikia wakisema, ''Mimi huwa siangalii kituo fulani cha luninga'' lakini cha kushangaza huwa wa kwanza kuelezea tukio linalotokea kwenye kituo hicho cha luninga!
 
Tunasheherekea Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa mkoloni mweupe; lakini ipo siku tutasheherekea Uhuru wa Tanzania kutoka kwa mkoloni mweusi ambae ni Mhe Magufuli! ... Povu ruksa!!
Una maanisha 2020 Tanzania itapata uhuru?
Kwa njia ipi? Sina povu lakini Akili imejiuliza imekosa majibu.
 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anaongoza Maelfu ya Watanzania kusherekea Miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Katika historia Tanzania Bara wakati huo ikiitwa Tanganyika ilipata Uhuru wake Disemba 09, 1961.

 
13 Reactions
Reply
Back
Top Bottom