Ongezeko la Watumiaji wa Mitandao ya Kijamii Tanzania ni fursa kibiashara

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Mitandao ya kijamii imekuwa nyenzo muhimu ya biashara katika karne ya 21 hasa kutokana na urahisi wa kufanya biashara na kuongezeka kwa fursa ukilinganisha na biashara nje ya mitandao. Zaidi ya nusu ya watu bilioni 7.8 duniani wanatumia mtandao wa intaneti, ambapo kwa jicho la kibiashara, hiyo ni fursa kubwa ya kufanya biashara mtandaoni.

Fursa ya kufanya biashara kidigitali inaongezeka kila siku kutokana na ongezeko la watu wanaotumia mtandao wa intaneti. Kati ya mwezi Januari mwaka 2020 na Januari 2021, watumiaji wa intaneti duniani waliongezeka kwa asilimia 7.3%. Mitandao ya kijamii inafungua fursa nyingi zaidi za kibiashara kutokana na urahisi wake wa matumizi. Tanzania ina watumiaji hai milioni 5 wa mitandao ya kijamii, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 mwaka 2021 ukilinganisha na mwaka 2020.

Licha ya kuwepo watumiaji zaidi ya milioni 28 wa intaneti nchini Tanzania, ni asilimia 11.6 tu ya watu wanaofanya manunuzi kupitia mtandao. Zipo sababu nyingi za kuwa na idadi hii ndogo, mojawapo ikiwa kukosa uelewa kuhusu nguvu ya kufanya biashara mtandaoni.

Mtandao wa Facebook ndio mtandao wenye uwezo wa kuwafikia watu wengi zaidi nchini Tanzania, ukifikia hadi watumiaji milioni 4. Huu si mtandao wa kuupuuzia unapoandaa mipango ya biashara mtandaoni. Instagram inafuatia kwa karibu, ikiwa na uwezo wa kuwafikia watu milioni 2.8, huku Twitter ikiweza kuwafikia watu laki mbili.

Mitandao ya kijamii imetengenezwa kwa lengo madhubuti la kuongeza muingiliano baina ya watu. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya mahitaji ya matumizi, mitandao ya kijamii imetoa fursa ya kujiweka kibiashara, mfano kwa kutumia Facebook Business, Instagram Business, WhatsApp Business nk. Matumizi sahihi ya vifaa hivi vya kidigitali yanaweza kusaidia kubadilisha utendaji wako wa kibiashara kwa kukupatia wateja wengi zaidi.

 
Back
Top Bottom