Ombwe la uongozi, inahitajika kafara au hekima? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ombwe la uongozi, inahitajika kafara au hekima?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Ntemi Kazwile, Feb 3, 2011.

 1. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #1
  Feb 3, 2011
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135


  [​IMG]
  Msomaji Raia​
  Februari 2, 2011[​IMG]
  WIKI iliyopita nilihoji kama tamko la Ridhiwani Kikwete lililenga kuziba ombwe la uongozi wa taifa letu. Nimepokea maoni mengi yanayokubaliana nami kuwa ni kweli ombwe lipo na kama kawaida ya ombwe, huwa linakaribisha yeyote kujifanya ni kiongozi anayejaribu kuliziba. Hata mimi “Msomaji Raia”, si ajabu nikawa katika kundi la kuziba ombwe hilo. Kwa hiyo, kimsingi niliyoyasema wakati huo, halikuwa tusi kwa Ridhiwani Kikwete bali ni hali halisi. Ngoma imekosa mwenyewe, kila mmoja anaingia uwanjani kucheza.
  Tangu awamu hii ya Rais Kikwete iingie madarakani, imepata mapingo mengi na orodha ni ndefu. Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, tetemeko likipita mara moja huacha nyufa na kuonyesha udhaifu wa nyumba ulipo. Lakini tetemeko likirudi mara kadhaa, kuna hatari nyumba hiyo kuanguka hata kama zamani ilidhaniwa kuwa ni imara.
  Mapigo yanayoendelea kuipiga serikali ya Kikwete, hata kama hatupendi, yanaendelea kudhoofisha uwezo wa serikali kufanya kazi kama serikali moja yenye agenda inayoeleweka. Hata Waziri Steven Wassira amenukuliwa akiwaambia wapiga kura wake wa Bunda kuwa wamwache Rais Kikwete afanye kazi yake bila kulazimika kutoa maelezo yake na msimamo wake kuhusu suala la Dowans. Ukiona wananchi wa Bunda wanamwandama Waziri wa Serikali kwa maswali mazito, ujue hilo ni tetemeko na likiendelea linaweza kuleta madhara makubwa.
  Kati ya mapigo yote, hili la Dowans ambalo ni mtoto halisi wa Richmond, ni pigo la nguvu kwa serikali. Pigo hili limekisambaratisha chama ndani ya miaka mitatu. Nakubaliana na kada maarufu wa chama hicho aitwaye Hussein Bashe ambaye amenukuliwa pia akisema kuwa kwa miaka mitatu, serikali imeshindwa kufanya kazi ya maana bali kujadili Dowans na Richmond wakati nchi imebaki gizani.
  Haya ni maneno mazito kusemwa na kada wa CCM, lakini kwa kuwa yamesemwa, inadhihirisha jinsi gani suala hili linavyozidi kuweka nyufa za hatari katika mshikamano wa chama na serikali yake. Linaloonekana wazi ni kuwa Jemadari wa Chama, Rais Kikwete amepigwa na ‘dubwasha’ hili linaloitwa Dowans akakimbilia ukimya. Maaskari wake na wasaidizi wake wametawanyika na kila askari ameamua kufa kupambana kivyake. Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba hajulikani yuko wapi, Kada maarufu Abdulrahman Kinana anaugulia ofisini kwake, John Chiligati alijaribu akaungua mikono na sasa ameapa hatalizungumzia suala hili tena wakati yeye ndiye mwenezi wa Chama.
  Kiserikali, Waziri Mkuu muungwana wetu Pinda anaelekea kuchafuliwa sana na pigo hili la dowans. Amejitahidi sana kulibeba kwa uangalifu lakini damu za wahanga wa pigo hili zinaanza kuchafua mavazi yake. Katika hali kama tuliyo nayo kwa sasa, huwezi kutetea suala la Dowans ukabaki mwadilifu na heshima yako mbele ya jamii. Mzee Pinda, Wassira na wengine kama hao, wanaolazimika kujificha nyuma ya utawala wa sheria ili kuharalisha ulipaji wa faini ya dowans, wanafanya jambo la hatari kwa dhamira zao na uadilifu wao. Na kwa kuwa wao wenyewe hawawezi kusema hadharani misimamo yao halisi wakawa salama, nalazimika kuwasemea maana nawafahamu, kuwa waachane na suala la ulipaji wa dowans na kwa kuwa sasa ombwe linatawala, hawatalaumiwa maana hawakujiteua. Hii ndiyo hekima inayowasaidia watawala wakati wa shida inayomgusa mkuu wa nchi.
  Liko kundi linalohoji ni nani katufikisha hapa tulipo na mapigo yote haya? Kundi hili linataka watu hao wajulikane na wachukuliwe hatua kali ili kuiokoa serikali hii na mambo mabaya kama ya Tunisia na Misri. Kundi hili lilianza kutetea msimamo huu mapema sana na hata katika vikao vya NEC na CC vilisimama kidete kutetea msimamo huu. Katika vikao vya Butiama, nusura Mwenyekiti ashindwe kuongoza kikao kile kwa sababu kundi hili la kutoa kafara watuhumiwa lilikuwa na hoja ya nguvu sana. Hivi sasa Jakaya anajuta ni kwa nini hakukubaliana nalo wakati ule maana msimamo huu ulifaa wakati ule kuliko sasa. Kafara kama ingetolewa wakati ule ingetibu baadhi ya magonjwa na hasa hili la Dowans maana lilikuwa bado dogo sana. Ninalotaka kusema hapa ni kuwa, katika orodha ya waliotufikisha hapa ni pamoja na Mwenyekiti wetu asiyefanya maamuzi kwa wakati.
  Watetezi wa Jakaya wanasema, Jakaya alirithi ufisadi huu wote huu kutoka kwa mtangulizi wake. Wanakwenda mbali na kuorodhesha mapigo yote yanayoipiga hii serikali na kudai yalikuwepo wakati Jakaya anaingia madarakani. Msaidizi mmoja wa Jakaya ametueleza hata kwa kutaja majina ya watu kuwa Richmond, EPA, Mahakama ya Kadhi, Rada, na mengine yalianza kabla Jakaya hajaingia madarakani na kuwa watu hao ndio walaumiwe siyo Jakaya. Msaidizi huyu aliye Ikulu anasema, uvumilivu umefikia kikomo na sasa Jakaya yuko tayari awatoe kafara waliotufikisha hapa lakini asilaumiwe endapo hata mtangulizi wake na wapambe wake wataguswa. Tumemweleza kuwa aache kutisha watu wazima, afanye hiyo kafara kuliko kuendelea kuteketeza kuku na mbuzi kwa ushirikina usio na faida. Kama atachelewa kama alivyochelewa Butiama, yanaweza kumkuta kama ya Hosni Mubaraka aliyelazimika kuvunja baraza la mawaziri lakini bado waandamanaji wakaendelela kuingia mabarabarani.
  Liko kundi linalohoji na kudadisi namna ya kutoka hapa tulipokwama? Kwa sasa kile kipindi cha Mzee Makwaia wa Kuhenga cha Channel Ten kiitwacho “Je Tutafika?” hakina tija kwa sababu inafahamika kuwa kwa mwendo huu hatufiki. Kinachotakiwa sasa ni kuhoji, Je tutokeje hapa?
  Kafara niliyoijadili hapo juu kwa hakika haiwezi kutukwamua hapa tulipo. Unapokuwa na baba mwenye nyumba asiyeamua wakati nyumba iko kwenye matatizo makubwa, yeye binafsi anakuwa ni tatizo.
  Wazoefu wa mambo ya utawala wanasema ni afadhali kushughulikia matatizo ya nyumba kuliko kushughulikia matatizo ya mwenye nyumba. Hekima ya hali ya juu inatakiwa katika kufanya uamuzi bila kuchelewa kwa sasa. Hasira ya wananchi inayotokana na ukali wa maisha inazidi kupanda na tumeona wenyewe yaliyotokea Babati wiki iliyopita.
  Wakati kafara inaweza kutuliza hasira hizi, lakini ni kwa muda mfupi maana kafara hiyo haibadilishi ugumu wa maisha unaowakabili watanzania wengi wa vijijini. Lakini pia hekima ya kutotumia kafara haiwezi kuiunganisha serikali iliyochanganyikiwa ili iwe ni serikali inayoonekana inatawala na kujali maslahi ya wananchi. Kumbe basi kinachotakiwa ni kutumia hekima na kafara kwa pamoja. Nachelea kusema, muda unaonekana kutokuwa upande wa serikali na majuto yanaweza kuwa mjukuu.  Source:Ombwe la uongozi, inahitajika kafara au hekima?
   
 2. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #2
  Feb 3, 2011
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Wakimkamata Mwanakijiji basi huyu mwandishi ni noma zaidi, kila ninaposoma makala zake napata imani zaidi kuwa huyu si mtu wa kawaida bali mtu mwenye mirija mirefu ya habari, nadhani ni mtu wa UWT!

  Tunashukuru kuna wazalendo UWT ambao wanatusaidia kuijua serikali yetu vizuri... Long live Msomaji wa Raia
   
 3. Babu Lao

  Babu Lao JF-Expert Member

  #3
  Feb 3, 2011
  Joined: Nov 2, 2010
  Messages: 2,056
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  Kwa upembuzi yakinifu ulotoa hapo juu, mimi naona ombwe la uongozi linahitaji hekima tena ilopita hizi za kawaida sababu nanukuu''Unapokuwa na baba mwenye nyumba asiyeamua wakati nyumba iko kwenye matatizo makubwa, yeye binafsi anakuwa ni tatizo'' na ''Wazoefu wa mambo ya utawala wanasema ni afadhali kushughulikia matatizo ya nyumba kuliko kushughulikia matatizo ya mwenye nyumba''. Bila shaka hapa tunahitaji hekima kubwa... Asante kwa uchambuzi na mwenye masikio na asikilize na mwenye macho na kujua kusoma asome mwenyewe!!!
   
 4. Ntemi Kazwile

  Ntemi Kazwile JF-Expert Member

  #4
  Feb 4, 2011
  Joined: May 14, 2010
  Messages: 2,145
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 135
  Kweli tupu Babu,

  Iliyonitoa kamasi ni hii hapa

  "Tumemweleza kuwa aache kutisha watu wazima, afanye hiyo kafara kuliko kuendelea kuteketeza kuku na mbuzi kwa ushirikina usio na faida"
  Swali je ina maana kuna kuku na mbuzi wanateketezwa kwa kafara na mkulu??
   
Loading...