ombwe la uongozi Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu

ngoshwe

JF-Expert Member
Mar 31, 2009
4,131
931
Kupitia magazeti ya jana tarehe 28 Septemba, 2011 Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ilijibu makala hii ya Deusdedit Jovin ambayo kimsingi ina mantiki kubwa. Bodi imonyesha kumbeza na kumtuhumu mwandishi huyu kuwa ni Mbinafsi, asie na uzalendo, asiefanya utafiti kabal ya kuandika nk. Lakini kwa undani, Bodi imeshindwa kujibu hoja za msingi zilizotolewa na mwandishi ikiwemo vigezo vinavyotumika kukokotoa mikpo na msingi halisi wa kukadiria mikopo kwa walengwa.

Kwa hivi sasa Bodi inatoa mikopo kwa kuzingatia taarifa za kwenye makaratasi tu (Paper work) na mbaya zaidi inasema inaangalia pia "background" za gharama ambazo mwambaji amekuwa akitumia katika shule za awali..hizi eti ndo zinapima kiwango cha utajiri au umaskini wa mwombaji??. Hivi inawezekana kweli mtu akaishi katika mfumo huo huo wa maisha bila kuteteleka? Ni wangapi wanakuwa na maisha mazuri mwanzoni na baadae kuporomoka na kuwa maskini wa kutupwa??
Ikiwa watanzania wote ni maskini kwa mujibu wa takwimu, na ikiwa fedha zinazotumika kutoa mikpo ni kodin za watanzania wote bila kujali umaskini au utajiri alionao kila mmoja wetu, kwa nini pasiwe na "uniform approach" katika kutoa uamuzi wa wanaostaili kupata mikopo??..kwa mfano katika nchi nyingine, utaratibu ni kupitia benki za kawaida ila Serikali ndio inatoa udhamini tu.

Katika majibu yake, Bodi inasema imeshindwa kuwahudumia waombaji wote wa mwaka 2011/2012 kutokana na ufinyu wa Bajeti, lakini cha kushangaza, Bodi haikuwahi kutangaza kabla ya Tuhuma zailizoandikwa katika Gazeti la Raia Mwema, ni kiasi gani imepewa kwa mwaka huu wa Bajeti kwa ajili ya mikopo na kiasi gani ingehitaji. Bodi INA USIRI MKUBWA, imekuwa ikiibuka na kujibu hoja tu pale inapotuhumiwa, lakini katika hali ya kawaida haijui kuwa inapaswa kuwapa wadau taarifa za nini kinaendelea. Kwa mfano, imezungumzia kuwa utartaibu mzima wa ukokotoaji unapaswa kutanghazwa na Waziri anayehusika katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Sheria inayoanzisha Chombo hicho, lakini haijabainisha ni Gazeti lipi (Government Notice Number - GN) ambalo wamewahi kutoa tokea chombo hicho kuanzishwa. Achilia Gazeti hilo la Serikali ambalo linaweza kuwa ni taratibu ndefu na lisiwafikie wengi, Bodi haijawahi hata kutoa katika magazeti ya kawaida mfumo huo wa ukokotoaji wala majina ya walioidhionihsiwa, kukataliwa au lah...pengine inadhani watanzania wote wanaweza kuingia kwenye tovuti yao na kusoma habari zao, lakini haijui kuwa sio maeneo yote ya nchi hii yanafikiwa na huduma ya intaneti...(nao wanaishi dunia ya kusadikika)!!. Ikumbukwe Bodi hii ni ile iel iliyowahi kuwajia juu vijana wa UVCCM kwakiwatuhumu kuwa ni "Wazushi" ( Rejea: https://www.jamiiforums.com/habari-...881-bodi-ya-mikopo-vijana-ccm-ni-wazushi.html...). Lakini katika majibu waliyotoa kwa mwandishi Jovin wa Raia Mwema, wanarejea tena kwa kumtuhumu kuwa naye ni mchochezi, hana takwimu na hajui analoandika... Bodi imesahau kuwa, Mwandishi kama huyu Mzalendo aliyepaswa kuelimishwa ili atumike kuelimisha watanzania wengine kuhusu Bodi hiyo, na asiandike haya ambayo wao wanaona ni "Uwongo na Uchonganishi".

Walitarajia mwandishi aandike nini kama wao wameficha taarifa muhimu za yale wanayofanya??


imekuwa na usiri Mkubwa katika utendaji wake mpaka ituhumiwe ndipo ijibu hoja
.


Ni dhahiri kuna ombwe la uongozi Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
Deusdedit Jovin

  • ‘Madudu' iliyoyafanya safari hii makubwa
  • Waathirika wa ‘madudu' hayo wawasilisha andiko Ikulu

AKIWA amelala kitandani muda mfupi kabla mauti hayajamfika, mpagani wa Kiingereza, Bertrand Russel, alikutwa na bintiye akisoma misahafu. Akiwa amepigwa na butwaa kubwa, binti huyo alimtaka babaye aseme iwapo ‘ameokoka' katika sekunde za mwisho wa uhai wake.
"Hapana sijaokoka", baba yake alijibu. "Pamoja na ubaunsa wa mwili wa kitu ambacho baadhi ya waumini hukiita Mungu", Russel aliendelea; "ninachofanya mimi siku zote hadi sasa ni kutafuta na kuanika hadharani ombwe la uongozi wa taasisi za ulimwengu, ombwe ambalo kwa maoni yangu, linalotokana na ufidodido wa fikra za Mungu huyo."
Kazi aliyokuwa akiifanya mpagani Bertrand Russel wakati wa uhai wake inafanana sana na kazi inayopaswa kufanywa na raia mmoja mmoja, watafiti, waandishi, wanaharakati, wanazuoni, asasi za kiraia, na vyama vya upinzani katika kila dola inayojulikana kama Jamhuri ya Kidemokrasia, Tanzania ikiwa ni dola mojawapo.
Kazi yetu, ikiwa katika sura ya "upagani wa kisiasa", na sio "upagani wa kidini" kama ilivyokuwa kwa Bertrand Russel, ni kutafuta na kuanika hadharani ombwe la uongozi wa taasisi za serikali, ombwe linalotokana na ufidodido wa fikra za baadhi ya viongozi wa serikali hiyo.
Katika makala hii ninatekeleza jukumu hili kwa kuchunguza mfano mmojawapo kwa kutumia ushahidi unaohusiana na utendaji kazi mbovu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini.
Asilimia 40 ya wanafunzi elimu ya juu wamenyimwa mikopo
Mjadala wetu unaanzia kwenye mikopo hewa kwa baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu. Hivi karibuni bodi hiyo ilitoa orodha ya wanafunzi wa elimu ya juu waliopatiwa mikopo kwa kipindi cha mwaka 2011/12. Pia Bodi hiyo imetoa orodha ya waombaji ambao hawakupewa mkopo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo, Lubambula Machunda, wanafunzi 23,340 watakaojiunga na vyuo vikuu nchini kwa mwaka wa masomo wa 2011/12 wamepatiwa mikopo. Wanafunzi hawa ni sehemu ya wanafunzi 37,924 waliopata udahili vyuoni.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo, alisema kuwa wanafunzi 1,995 wamekosa mikopo kutokana na makosa yanayohusiana na ujazaji wa fomu. Sababu hizo zimetajwa na Kaimu Mkurugenzi huyo kama ifuatavyo: Wanafunzi 138 majina yao ya kuomba mikopo yalitofautiana na majina ya waliodahiliwa; wanafunzi 823 walibainika kuwa wanaendelea kunufaika kwa mikopo; wanafunzi 213 maombi yao hayakushughulikiwa kutokana na kubainika kuwa na matatizo; na wanafunzi 821 hawakusaini na kukubaliana na masharti ya mikopo.
Pia Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo alisema kuwa kwa mwaka huu, wanafunzi 23,340 waliopewa mikopo ni wachache kulinganisha na mwaka jana ambao walikuwa 25,000. Alisema kuwa sababu zilizochangia kushuka kwa idadi ya waliopata mikopo ni kuwepo kwa waombaji wengi zaidi kuliko uwezo wa bodi kipesa.
Kwa maneno haya, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo anakiri kwamba bodi yake imethubutu, ikagonga mwamba na sasa inachapa makitaimu kama sio kuserereka kwa kurudi nyuma! Jambo hili ni kinyume kabisa na kauli mbiu ya "tumethubutu, tumeweza na sasa tunasonga mbele" anayotamba nayo Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa.
Kitendawili katika utoaji mikopo mwaka huu
Maelezo ya Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo yanazua maswali mengi kuliko majibu kuhusu kilichofanywa na Bodi ya Mikopo mwaka huu. Kwa mfano, kuna ushahidi wa kuaminika unaopingana na maelezo ya Kaimu Mkurugenzi huyo. Tuone mifano michache ya ushahidi uliokusanywa na mwandishi wa makala hii.
Mnamo Septemba 7, 2011, baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu waliamua kwenda makao makuu ya Bodi ya Mikopo yaliyoko Msasani, jijini Dar es Salaam, ili kujua kwa nini hawakupewa mkopo wakati wanaamini wanazo sifa za kisheria za kupewa mkopo. Nilikuwa miongoni mwao kwa kuwa nami nilikuwa nafuatilia jambo hilo hilo kwa niaba ya mdogo wangu aliyechaguliwa kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha SAUT.
Wakati tunaendelea kusubiri mabosi wa Bodi ya Mikopo ili tuzungumze nao, nilifanya kazi ya kupeleleza matatizo ya vijana niliowakuta makao makuu ya bodi. Niligundua kwamba, baadhi ya waombaji walijaza fomu zao na kuziwasilisha katika bodi, lakini majina yao hayaonekani katika orodha ya wale waliopata wala ile ya waliokosa mikopo. Niligundua pia kwamba, baadhi ya waombaji ni yatima, lakini wamenyimwa mkopo; na niligundua kwamba, baadhi ya waombaji ni wanafunzi kutoka familia makini kabisa lakini hawakupewa mkopo.
Pia niligundua kwamba, baadhi ya waombaji wamechaguliwa kusoma kozi za kipaumbele lakini hawakupewa mkopo. Niligundua vilevile kwamba, baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa kusoma kozi ambazo sio za kipaumbele wamepewa mkopo.
Kama vile hiyo haitoshi, niligundua kwamba waombaji waliopewa mkopo wametajiwa kiwango cha mkopo tu bila kuonyesha ni gredi gani ya mkopo wamepata; na niligundua kwamba, baadhi ya waombaji walikuwa wamebeba nakala za fomu walizozijaza hapo awali, zikiwa zimejazwa vema na kuwasilishwa kwenye bodi baada ya kuzisaini na kufanya malipo yote.
Miongoni mwa vijana hawa, kulikuwa na yatima mmoja kutoka Mbeya anayeitwa Enea Nicola Mahenge. Amechaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dodoma. Alikuwa na barua kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kwa ajili ya kumtambulisha kwenye Bodi ya Mikopo ili asaidiwe.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba AB.120/304/01/33 imeandikwa Septemba 5, 2011 na kusainiwa na ndugu I.S. Rimoy, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya.
Pia alikuwepo kijana mwingine anayeitwa Yasin Said kutoka Kyela. Amechaguliwa kusoma Chuo Kikuu cha Muhimbili kozi ya udaktari. Hii ni kozi ya kipaumbele, lakini hakupewa mkopo. Vile vile alikuwepo binti mmoja anayesoma Chuo Kikuu cha Makumira (kitivo cha sheria) anayeitwa Josephine Mutabirwa.
Namba yake ya usajili ni TU/M/LLB/09/986. Mwaka wa kwanza hakupewa mkopo kwa sababu namba yake ya usajili iligongana na namba ya mwenzake ambaye amepata mkopo. Chuo kimekosoa jambo hilo na kuiandikia bodi kupitia barua ya Agosti 03, 2011. Mpaka juzi hakuwa amepatiwa mkopo na hakuwa anajua hatima yake. Na orodha ya kasoro hizi ni ndefu.
Mifano hii michache inatosha kuonyesha kitendawili kinachohitaji kuteguliwa hapa. Tunajua kuwa Bodi ya Mikopo imekusanya taarifa za waombaji kwa njia ya mtandao. Hivyo, taarifa zote zimejikusanya katika kompyuta kubwa iliyoko wanakojua wao. Kwa kimombo kompyuta ya aina hii huitwa server na zile kompyuta ndogo tulizokuwa tunatumia katika migahawa ya intaneti kwa ajili ya kuomba mikopo zinaitwa clients.
Maafisa kadhaa wa bodi hiyo wamesikika wakisema kuwa kompyuta za bodi zinayo programu kwa ajili ya kukokotoa gredi za mikopo kwa kuzingatia taarifa zilizoingizwa na wanafunzi. Programu ya aina hiyo hutengenezwa na wanadamu kwa kutafsiri fomula fulani fulani katika lugha inayozungumzwa na kompyuta. Katika makala hii fomula inayotuhusu ni ile ya kukokotoa gredi ya mkopo.
Kwa mfano, mwaka jana, nchini Kenya walikuwa wanatumia fomula inayoonekana katika picha hapo juu. Katika fomula hiyo ya Kenya, utaona kwamba Bodi ya Mikopo ya Kenya inatumia kipato cha familia (family income) kama msingi wa kukokotoa gredi ya mkopo kwa mwombaji anayetoka katika familia husika.
Kwa ajili ya kubaini kipato cha familia, Bodi ya Mikopo Kenya inakusanya taarifa zifuatazo : elimu ya wazazi, ajira ya wazazi, idadi ya watoto wa mwombaji wanaosoma, idadi ya watoto wa mzazi wa mwombaji wanaosoma, idadi ya ndugu wa mwombaji, kiwango cha gharama za elimu zinazotumika kuwaelimisha ndugu wa mwombaji, matumizi ya familia kwa mwezi, aina ya sekondari iliyohudhuriwa na mwombaji, aina ya familia anakotoma mwombaji (mzazi mmoja/hana wazazi wote/hapana), na pasi ya mwombaji katika elimu ya sekondari.
Taarifa hizi zikitumiwa na kompyuta ambayo imepewa fomula sahihi, hakuna yatima atakayekosa mkopo, hakuna mwanafunzi wa kozi ya kipaumbele atakosa mkopo, na hakuna mwanafunzi wa familia maskini atakosa mkopo.
Na kwa kweli, hata bila kusubiri bodi ya mikopo imwambie mtu amepata mkopo kiasi gani, mwanafunzi mwenyewe atatumia taarifa alizozijaza kubaini gredi yake ya mkopo.
Kwa kuangalia taarifa ambazo waombaji wa mikopo hapa Tanzania wanatakiwa kuzitoa, ni wazi kwamba hatuna tofauti kubwa na Wakenya. Tofauti pekee na Wakenya ni kwamba fomula ya kukokotoa gredi hapa kwetu Tanzania imefanywa siri ya Bodi ya Mikopo! Nafikiri hata Rais Kikwete haifahamu! Lazima tuendelee kuhoji chanzo cha usiri unaozunguka fomula hiyo.
Usiri wa fomula ya kukokotoa gredi wa nini?

Tayari tunafahamu kwamba baadhi ya wanafunzi walinyimwa mikopo huku wakiwa na sifa za kisheria za kupata mkopo. Tumethibitisha kuwa walijaza taarifa zote kikamilifu na kuziingiza kwenye kompyuta ya Bodi ya Mikopo. Kwa hiyo, wakati wa kukokotoa gredi za mikopo ya wanafunzi hawa, huenda jambo mojawapo kati ya mambo yafuatayo lilitokea.
Ama maafisa wa bodi walitumia kompyuta iliyolishwa fomula mbovu au maafisa wa bodi walifanya kazi ya kukokotoa gredi za mikopo kwa kutumia utaratibu wa kubahatisha kwa msaada wa karatasi na kalamu, na hivyo kuzalisha makosa mengi madogo madogo. Au maafisa wa bodi walitumia kompyuta iliyolishwa fomula sahihi, lakini kwa baadhi ya wanafunzi tu!
Hiki ndicho kitendawili kinachohitaji kuteguliwa. Na jawabu lolote litakalotolewa kwa kitendawili hiki ni ushahidi tosha kwamba katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuna ombwe la uongozi unaotokana na ufidodido wa fikra za baadhi ya watendaji wake.
Utafiti kutegua kitendawili hiki
Tukiwa na kitendawili hiki kichwani, na baada ya kusubiri sana, hatimaye, tulifanikiwa kuzungumza na msemaji mmoja wa bodi kuhusu matatizo ya waombaji waliokosa mkopo. Baada ya kuzunguka sana, msemaji huyo aliamua kusema mambo ambayo ukiyatazama vizuri yanatoa mwanga kuhusu kilichotokea.

Kati ya mengine, alitueleza mambo yafuatayo: Kwamba, bodi haikutumia kompyuta kupima uwezo wa kiuchumi (means testing) kwa kila familia ya mwanafunzi aliyeomba, na kwamba kilichofanywa na bodi ni kutumia kompyuta kupima uwezo wa kiuchumi kwa baadhi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya vipaumbele, zoezi ambalo lilimaliza pesa yote iliyokuwepo. Na kwa sababu hizo, kuna wanafunzi ambao huenda walikuwa na sifa za kupata mikopo lakini hawakupata. Kwa hiyo, akatuelekeza tuache kumtaka aangalie fomu tulizokuwa tumebeba ili atueleze ni kitu gani katika fomu hizo kimesababisha mkopo kukosekana.
Baada ya majibu haya, tulimwomba msemaji huyo atupatie fomula inayopaswa kutumiwa na bodi katika kukokotoa gredi za mikopo kwa wanafunzi wote. Hakutupa fomula hiyo kwa maelezo kwamba yeye sio mtaalamu wa kompyuta. Badala yake akatwambia tumwone Afisa Mikopo aliyemtaja kwa jina moja la Laizer.
Tulikwenda chumba namba 15 ambako tuliambiwa ndio ofisi ya Bwana Laiser lakini hakuwepo. Hatimaye tulimwomba atuitie Mkurugenzi wa Bodi ili ajibu maswali yetu, lakini hakukubaliana nasi.
Kwa sababu ya usumbufu huu, na kwa kuzingatia kwamba katika kikao cha Bunge lililopita Waziri wa Elimu aliahidi kuwa matatizo haya hayatakuwepo, tuliamua kuandika "petisheni ya rufaa" (petition of appeal) kwa Rais dhidi ya maamuzi mabovu yaliyofanywa na uongozi wa Bodi ya Mikopo.
Tulikubaliana kwamba, rufaa hii ipelekwe Ikulu na Waziri wa Elimu na Mafunzo apewe nakala tu. Hatukutaka kukata rufaa kwa waziri kwa kuwa naye tayari tulimtuhumu kufanya uzembe.
Wanafunzi waliokuwepo makao makuu ya Bodi ya Mikopo, Septemba 7, 2011, walisaini petisheni ya rufaa hiyo na kukubaliana kumtuma mwandishi wa makala hii akaiwasilishe Ikulu.
Mwandishi huyu aliikabidhi petisheni ya rufaa hiyo katika mapokezi ya Ikulu saa 10.15 siku hiyo hiyo. Nakala ya petisheni ya rufaa hiyo aliikabidhi kwa Katibu Muhtasi wa Waziri wa Elimu na Mafunzo saa 10.25 siku hiyo hiyo.

Hitimisho na maana ya hitimisho hilo Kwa kuzingatia maelezo yote hapo juu, ni hitimisho la mwandishi wa makala hii kwamba Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini inafanya kazi kwa kubahatisha.
Ni bodi ambayo inaikwamisha serikali katika azima yake ya kufikia malengo ya taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ni bodi inayokwamisha utekelezaji wa Sera ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999. Na kubwa zaidi, ni bodi inayoigombanisha serikali na watu wake pasipo sababu za msingi.
Kwa maneno mepesi, kuna ombwe la uongozi ndani ya bodi hiyo.
Mapendekezo kwa Rais Kikwete
Hivyo, basi, kwa lengo la kuhakikisha kwamba Sera ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuelekea 2015, na Dira ya Taifa Kuelekea Mwaka 2025 vinatekelezeka, ni maoni yangu kwamba ofisi ya Rais lazima ichukue hatua za makusudi kutekeleza mapendekezo ya vijana wa elimu ya juu waliomwandikia petisheni ya rufaa mnamo Septemba 7, 2011. Kwa ajili ya msisitizo, nayarudia mapendekezo ya wanafunzi hao:
Mosi, wanapendekeza kwamba Bodi ya Mikopo iweke bayana fomula inayopaswa kutumika katika zoezi la kukokotoa gredi za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu;
Pili, napendekeza kwamba Bodi ya Mikopo ikubali kwamba ilikosea na hivyo kupitia upya maombi ya wanafunzi wote walioomba mikopo katika mwaka 2011/12 ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Propaganda zinazofanywa kupitia vyombo vya habari sio tiba ya tatizo.
Tatu, wanapendekeza kwamba, kuhusu wanafunzi 1,995 waliokosa mikopo kutokana na kile wanachokiita makosa yanayohusiana na ujazaji wa fomu, Bodi ya Mikopo iweke bayana nani amenyimwa kwa sababu ipi; na kisha kueleza hatima ya wanafunzi hawa katika suala zima la mikopo. Kosa la kiuandishi haliwezi kufuta milele haki ya mwanafunzi kupata mkopo.
Nne, wanapendekeza kwamba, Rais ayaagize mabenki yaweke utaratibu wa kuwakopesha wanafunzi wote waliopata udahili katika taasisi za elimu ya juu, ambapo serikali atakuwa ndiye mdhamini. Jambo hili laweza kufanyika kwa kumdhamini mwanafunzi mmoja mmoja au kwa Bodi ya Mikopo kuchukua hatua ya kukopa pesa toka taasisi za fedha ili iweze kuzitumia katika kutimiza majukumu yake ipasavyo;
Tano, wanapendekeza kwamba, Bodi ya Mikopo ihakikishe kwamba zoezi la kuomba mikopo linakuwa ni endelevu, na sio la msimu kama ilivyo sasa hivi. Kwa mfano, sasa tayari wamefunga mfumo wa kuomba mikopo uliokuwa umewekwa katika mtandao wake. Lakini bado kuna vyuo bado vinafanya udahili. Matangazo tunayasikia redioni na kuyaona magazetini.
Na sita, wanapendekeza kwamba, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo awajibishwe kwa manufaa ya umma kwa kufanya madudu yote kama tulivyoyaeleza hapo juu halafu akalidanganya taifa.
Kwa ujumla, wanachotaka wanafunzi wa elimu ya juu niliokutana nao pale makao makuu ya Bodi ya Mikopo ni kuona kwamba kigezo pekee cha mwanafunzi wa elimu ya juu kupatiwa mkopo ni ushahidi wa udahiri.

Hofu yangu ni kwamba Rais Kikwete anaweza kupuuzia mapendekezo haya, lakini akiyapuuzia atakuwa ametupa sababu ya kujenga imani kwamba hata Ikulu kuna ombwe la uongozi.



Raia Mwema
 
Magazet yap mkuu,ningependa nifuatilie nione pumba zao jins walivyojibu hoja hiyo.
 
Hii bodi ya mikopo iliyo chini ya ukurugenzi wa nyatega na akina lubambula machunda haijawahi kukidhi haja ya kuwepo kwake tangu ilipoanzishwa.

Hawajui namna ya kufanya means testing na wala hawana formula maalum ya kukokotoa mahesabu kwa ajili ya waombaji.

Wamegeuka kupiga propaganda kupitia vyombo vya habari badala ya kutumia muda wao vizuri kujifunza namna ya kuboresha utendaji wao.

 
Magazet yap mkuu,ningependa nifuatilie nione pumba zao jins walivyojibu hoja hiyo.
Ni pampoja na Gazeti la Majira Mkuu la tarehe 29/09/2011. Imetolewa Kama taarifa kwa UMMA
 
Ni pampoja na Gazeti la Mwananchi Mkuu la tarehe 29/09/2011
Aksante ngoja nikalicheck!
Hawa jamaa taarifa zao sio sahihi kuna jamaa zangu weng tu majina hayaonekani kotekote,waliopata hawamo waliokosa hawamo wala sehemu yoyote ile majina hayaonekani.
Je,tuseme bodi haijapata maombi yao?.EMS nayo ilichelewesha barua?.Au hata online applications zilichelewa!
Wa release majina yote ya waliomba mikopo waoneshe makosa yaliyofanywa ili wayatambue na wasiyarudie au wapewe nafasi ya kufanya marekebisho!
Imagine waliokosa kwa mjibu wao ni 13,382 nimejumlisha wale wenye matatizo mbalimbali kwa mjibu wao- Name differene,Contract problems,Not eligible, not need etc.
Sasa fanya 13382*30000= 401,460,000/- hizo pesa zote wamegawana!
Bado wale wasioonekana kotekote idad yao haijajulikana.Ni Wizi mtupu!

 
Vile vile VITISHO wanavyovitoa kupitia Vyombo vya Habari juu ya watakaoandamana kudai haki zao za msingi ninaviita ni Ulimbukeni. Vitisho havitufikishi popote.
 
Back
Top Bottom