Ombi la Malinzi latupwa

Replica

JF-Expert Member
Aug 28, 2017
1,444
7,803
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imetupilia mbali ombi la utetezi katika kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili aliyekua Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Jamal Malinzi na wenzake.

MALINZI.jpg

JAMAL MALINZI.
Utetezi katika kesi hiyo ulitaka Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), kwenda kutoa maeleza sababu ya kukaa na jalada ofisini kwake kwa siku 37, bila kulifanyia kazi.

Uamuzi huo ulisomwa Ijumaa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya kupitia hoja za pande zote mbili.

Hakimu Mashauri alisema DPP anafanya kazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya hatua za kikazi.

Alisema kesi hiyo itatajwa Ijumaa na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Awali upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga. Walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 28, mwaka huu.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha ambazo ni dola za Marekani 375,418.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Juni 5, mwaka 2016 katika ofisi za TFF zilizopo Ilala, jijini Dar es Salaam, Malinzi na Mwesiga walighushi nyaraka za Kamati Tendaji ya shirikisho hilo kwamba imebadilisha mtia saini wa akaunti zake kutoka Edger Leonard Masoud na kuwa Nsiande Isawafo Mwanga huku wakijua sio kweli.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa Septemba Mosi, mwaka 2016 katika benki ya Stanbic Tanzania Limited tawi la Kati, lililopo Kinondoni, jijini, kwa makusudi Mwesiga aliwasilisha nyaraka za kamati hiyo zilizoghushiwa akionyesha kuwa imebadilisha mtia saini wa akaunti zote za TFF.

AMEIKOPESHA TFF
Katika shtaka la tatu hadi la saba, ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Novemba 6 na Desemba 17, mwaka 2013, Malinzi alighushi risiti akionyesha kuwa ameikopesha TFF jumla ya dola za Marekani 38,832.

Katuga alidai katika shtaka la nane hadi la 10, katika tarehe tofauti kati ya Machi 26 na Machi 13, mwaka 2014, Malinzi alighushi risiti akionyesha kuwa ameikopesha TFF jumla ya Dola za Marekani 85,000.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shtaka la 11 hadi la 13, katika tarehe tofauti kati ya Mei 16 na Julai 11, mwaka 2016, Malinzi alighushi risiti akionyesha kuwa ameikopesha TFF dola za Marekani 28,000.

Swai alidai kuwa katika shtaka la 14 hadi la 16, katika ofisi za shirikisho hilo, tarehe tofauti kati ya Julai 15 na 25, mwaka 2014 alighushi risiti akionyesha kuwa aliikopesha TFF dola za Marekani 19,000.

Ilidaiwa kuwa katika shtaka la 17 hadi la 19, Agosti 17, 19 na Oktoba 11, mwaka 2014, katika ofisi za shirikisho hilo, Rais huyo alighushi risiti akionyesha kuwa aliikopesha TFF dola za Marekani 11,000.

Swai aliendelea kuwasomea kwamba, katika shtaka la 20 hadi 23, kati ya Julai 22, mwaka 2015, Mei 9, Juni 16 na Agosti 2, mwaka 2016 katika ofisi za shirikisho hilo, alighushi risiti akionyesha kuwa aliikopesha TFF dola za Marekani 20,000.

Katika shtaka la 24 na 25, ilidaiwa kuwa kati ya Septemba 19 na 22, mwaka 2016 katika ofisi za shirikisho hilo, Malinzi alighushi risiti akionyesha kuwa aliikopesha TFF dola za Marekani 16,000.

Swai alidai katika shtaka la 26, kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, mwaka 2016, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la kutakatisha dola za Marekani 375,418 huku wakijua ni zao la uhalifu na zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la 27, ilidaiwa kuwa katika terehe tofauti kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, mwaka 2016, Malinzi na Mwesiga katika benki ya Stanbic wote kwa pamoja walijipatia dola za Marekani 375,418 huku wakijua zimepatikana kwa njia ya kughushi.

Katika shtaka la 28, katika terehe tofauti kati ya Septemba Mosi na Oktoba 19, mwaka huu katika ofisi za TFF, aliwasaidia Malinzi na Mwasiga kujipatia dola 375,418 huku akijua fedha hizo ni zao la kughushi nyaraka za kuhamisha fedha.

Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo.
 
Malinzi mwizi sana ila hakuwa anatumia akili hata ndogo tu kwenye kuforge hizo receipts..
 
Back
Top Bottom