Ole wake Tanzania tusipoisaidia

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,825
287,849
Ole wake Tanzania tusipoisaidia

Deus Bugaywa
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

HAKUNA wakati muhimu kwa wananchi wa Tanzania kuuishi na kuutumia vyema wosia wa hayati Baba wa Taifa alioliachia taifa hili katika utenzi uliohitimisha kitabu chake cha ‘Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania’.

Tumebakiza muda mchache kabla ya kufika mahali ambako si ushauri huo au kitu kingine chochote kinaweza kuirekebisha hali ya nchi yetu ili istawi.

Tukichelewa leo nchi hii itakuwa imeparaganyika na kusambaratika katika kila uga, kiasi kwamba hakutakuwa na namna yoyote ya kuirekebisha hali hiyo, isipokuwa majuto, kilio na kusaga meno.

Wosia wa baba yetu unasema hivi:

Ole wake Tanzania
Tusipoisaidia!
Niwezalo nimefanya
Kushauri na kuonya

Namlilia Jalia.
Atumulikie njia;
Tanzania ailinde
Waovu wasiivunde.

Nasi tumsaidie,
Yote tusimwachie!
Amina, tena Amina!
Amina, tena Amina!

Tayari waovu wamekwishaanza kuivunda Tanzania yetu, lakini bahati mbaya tumeamua kumwachia Jalia kila kitu, iko haja ya sisi wenye nchi kumsaidia Muumba wetu katika kufanya Tanzania ile tuitakayo.

Kukaa tu na kutazama kila kitu, hata kama tunasali sana bila sisi wenyewe kufanya chochote, si tunajidanganya, lakini pia tunamkosea Muumba, tunafanya dhambi, kwa sababu ni amri yake kwamba tuutiishe ulimwengu.

Hapa ilipofika nchi hii nzuri ya mama Afrika inahitaji kukombolewa kwa vita vikali vya kimapinduzi, tunahitaji mapinduzi ya kikweli ili kuinusuru nchi hii.

Mapambano yamekwishaanza na dalili za mwanzo zimekwishaanza na zinaonyesha ushindi uko upande wa ukweli.

Bado kama wananchi hatujayapokea mapambano hayo kama inavyotakiwa ili kujihakikishia ushindi, tunaonekana ni aina ya watu tunaotaka mabadiliko, lakini tunaogopa kuyafanya yatokee, hili halitatusaidia lazima tukubali kuwa na akili kama za mwendawazimu kidogo ili ukombozi wa kweli upatikane.

Na kazi yetu iliyobaki si kubwa kama tunavyodhani, kwa sababu moja ya kazi kubwa kwenye mapambano kama haya ni kujua nani yuko upande upi.

Tumshukuru Mungu kwamba Watanzania tayari tumeangaziwa na sasa tunafahamu na kuwataja watu hata kwa majina, kwamba nani ni mwenzetu na nani anataka kutufanya watwana wake daima.

Mgawanyiko uliojitokeza dhahiri sasa, hata kwa kina Thomaso, ndani ya CCM na kwenye Bunge letu tukufu, ni ushindi kwa ukweli na ukombozi wa nchi hii kwa sababu tumeweza kujua nani kiongozi wa wananchi na nani kiongozi mchumia tumbo.

Kwamba katika nchi hii sasa hata mtoto wa Darasa la Tano atakwambia nani huwezi kumtenganisha na ufisadi na nani ni mzalendo halisi wa nchi hii. Hii ni dalili nzuri ya kuimarisha mapambano haya.

Tunapochagua viongozi tunaamini wanapaswa kuongozwa na dhamiri zao njema na safi, kutambua kwamba wao ni watumishi wa umma wa Watanzania na kwamba wanapaswa kutumika kwa ajili ya ustawi wa Watanzani hao.

Bahati mbaya ni kwamba wapo baadhi viongozi wetu tuliowapa jukumu hilo wakadhani ni wasaa wa wao wa kujilimbikizia mali kwa gharama ya ujinga, vifo na umaskini wa sisi tuliobaki.

Wana roho za ‘mtakavitu’. Wameitafuna nchi bila huruma, wakafika mahali wakadhani ufisadi kwa mali yetu ni haki yao ya msingi.

Ndiyo maana unaona hawalali, wanakesha kupanga mbinu na mikakati kutaka kujitakasa ili eti jamii iwaone watakatifu, sijui jamii ya aina hivyo, inawezekana hawa watu wameshawaona Watanzania ni watu mbumbumbu kiasi kwamba wanaweza kudanganyika na vitu vidogo, kwamba watuhumiwa wa ufisadi wa mali yao mara wageuke watakatifu…hapana sisi si wajinga wa viwango hivyo.

Ni wakati wa sisi kusimama na kuusimamia ukweli, haiwezekani eti mtu unamwita kiongozi wako - mbunge wako - anasimama ndani ya Bunge anatetea ufisadi, anajifanya kutoa ushauri eti yako matatizo mengi ya wananchi yakiwamo ya maji na barabara, kwa hiyo muda utumukie kujadili hayo badala ya ufisadi.

Hivi inawezekana tuna viongozi na wawakilishi wetu waliokosa upeo kwa kiwango hicho? Kwamba mbunge anashindwa kupata uwiano wa shida za watu wake na ufisadi unaoendelea nchini, eti inawezekana akawa hajui kwamba hiyo barabara au maji anayopigia kelele kila siku ili asikike na wananchi wake havipatikani kwa sababu ya ufisadi huo?

Kama kweli tunao viongozi wa aina hiyo tuna bahati mbaya, lakini wengine wao ni wasomi wa haja, ni wazi hawa wanaamua kujitoa fahamu ili watetee wanachokitetea kwa ajili ya maslahi binafsi.

Hawa ndio tunaopaswa kuanza nao, tuwakatae kwa nguvu zetu zote. Mwaka 2010 ndio kiwe kipimo cha kama Watanzania wameamua kweli kujikomboa au bado wanataka waendelee kuishi na nira ngumu na mzigo mzito wa ufisadi au wameamua kulainisha nira hizo na kuufanya mzigo kuwa mwepesi.

Tunahitaji kweli uendawazimu wa kurekebisha hali ya mambo katika nchi yetu, lakini utakuwa ni uendawazimu kipeo cha pili kama kuna watu wataweza kumchagua mtu awe mbunge wao, ambaye ushahidi uko wazi kwamba yeye anatetea maswahiba kama kwamba wao ndiyo jimbo au chama kama kwamba waliomchagua wataishi kwa chama badala ya mkate na huduma bora za jamii.

Lazima tuupokee na kuukubali ukweli katika sura zake zote kama alivyowahi kunukuliwa mwanafalsafa wa zamani wa Ujerumani, Arthur, kwamba “ukweli wowote hupitia ngazi tatu – kukejeliwa, kupingwa na ikibidi damu kumwagika na kukubalika - kwa kuwa ukweli hujisimamia wenyewe”.

Kwetu ukweli kuhusu ufisadi ulianza kwa kujeliwa, wakati ile ‘list of shame’ inatajwa wapo waliopuuza na kuwakejeli kwa kila hali na hata kuwaita walioitaja waropokaji.

Lakini kadri siku zinavyokwenda, ukweli unazidi kujipambanua na uongo, sasa wamegundua hilo wameanza kuupinga kwa kila mbinu.

Wangine wamekwenda bungeni kupinga kile ambacho wenyewe walikipitisha kwa nguvu na watu wakawapa heshima, hadhi ya bunge ikapanda heshima yake ikarudi.

Kimetokea nini hapa katikati hadi baadhi yao waanze kula matapishi yao kwamba Richmond ilikuwa siasa?

Kilichotokea ni dhahiri: kwanza wanatimiza sheria ya maumbile kwamba mfa maji lazima atapetape, ili andiko litimie kwamba ukweli haukubaliki kirahisi na ili uwe ukweli ni lazima upimwe, upitie misukosuko ili hatimaye ukija kusimama kila mtu asiwe na shaka kwamba huo ndio ukweli halisi.

Ni jukumu letu wenye nchi kuisimamia nchi yetu wenyewe na kuhakikisha hatutazami haya mambo kama raia waalikwa, lazima tujue hakuna Tanzania nyingine mahali popote katika sayari hii.

Maana ya msuguano tunaoushuhudia sasa na kwanini tumefika hapa jibu moja la jumla ni kwamba, hatuna uongozi imara, uongozi wetu sasa ni dhaifu. Yapo mengi yasingekuwa tena ya mjadala hapa kama tungekuwa na viongozi wenye sifa za kuitwa viongozi.

Nchi na chama imemegeka vipande viwili, viongozi wetu sasa wako kwenye ‘dilemma’ hawajui wajiunge na upande upi, ule wa mafisadi au upande wa pili, kwa sababu wamekosa ujasiri na hekima za kiuongozi, ni kama wale aliowasema Mwalimu Nyerere katika utenzi wake mwingine kwenye kitabu nilichonukuu awali;

“Kifo cha maji kushoto
Kulia kifo cha moto
Kila moja ni balaa
Kote huko hatari
Hujui ufanyeje.”

Wakati viongozi wetu wakitafuta cha kufanya nchi inakwenda mrama, wakijataharuki kila kitu kimekwenda kombo, ndiyo maana kama wenye nchi hatupaswi kuwa watazamaji, tuingie kwenye uwanja wa mapambano kila mtu alipo na kwa silaha yake tuiokoe nchi hii na ufisadi.

Ole wetu tusipofanya hivyo, ole wake Tanzania tusipoisadia, itakuwa ole kunapokucha, ole kunapokuchwa, ni ole, tena ole na ole hata milele.

Mungu ibariki Tanzania!

drbugaywa@yahoo.com
0734 449 421
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom