WATU 25 wamekamatwa na polisi wilayani Nzega kwa tuhuma za kunywa pombe asubuhi kinyume na agizo la serikali.
Akizungumza na Nipashe juzi, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nzega, Juma Majura, alisema agizo hilo ni la mkuu wa wilaya hiyo, Jacqueline Liana, la kuwataka wananchi kufanya kazi badala ya kunywa pombe.
Majura alisema msako umehusisha vilabu mbalimbali vya pombe za kienyeji aina ya komoni inayotengenezwa kwa kutumia mahindi, wengi wakiwa vijana wenye uwezo wa kufanya kazi.
Liana alisema msako huo ni endelevu baada ya nguvu kazi ya taifa ambayo ni vijana, kujikita kunywa pombe wakati wengine wakiwa wanafanya kazi za uzalishaji mali na kusababisha umaskini miongoni mwao.
“Sijakataza watu kunywa pombe kama watakavyotafsiri baadhi ya watu, bali nachotaka kila mtu awajibike katika nafasi yake ili kuhakikisha anazalisha na kujishughulisha muda wa kazi tofauti na wanavyofanya starehe ya unywaji pombe toka asubuhi hadi jioni,” alisema.
Aidha, aliwataka wanaofanya biashara hizo kufuata agizo la serikali la kufungua biashara zao ifikapo saa 10 jioni kwa lengo la kuepukana na mgogoro dhidi ya vyombo vya dola.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji Nzega, Hawa Mniga, alisema kwa sasa halmashauri itaanza kutoa masharti na maelekezo kwa wafanyabiashara wa pombe za kienyeji na wale wa baa, ili kufuata maagizo ya serikali.
Aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanafungua biashara zao muda uliopangwa ili kuepuka na mgogoro na polisi.
Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa katika msako huo, walilalamikia tukio hilo kwa madai wameonewa kutokana na kila mtu kuwa na uhuru wa kufanya kwa kutumia rasilimali zake bila kuvunja sheria za nchi.
Hamis Ismail, alisema serikali imewaonea kwa kuwakamata kutokana na muda wao wa kazi kuwa usiku, hivyo kitendo cha kuwakamata ni kuwadhalilisha wananchi.
Chanzo: Nipashe
Kwa upande wangu naona kama vile Kitwanga kaikumbusha serikali kuna walevi wanakunywa pombe muda wa kazi.
Tunakumbushwa #HapaKaziTu