popie
JF-Expert Member
- May 28, 2016
- 801
- 575
Good job
*NYUMA YAKO – 12*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Mikono yao ya kulia niliiona ikiwa imezama kotini. Bila shaka kushikilia bunduki.
Hapa ikanilazimu nifanye maamuzi ya upesi kuokoa roho yangu.
ENDELEA
Ni upesi nikanyanyuka nikiwa nimebebelea ile ndoo ya taka, nikawatupia! Wakiwa wamedaka na kudondoka nayo chini, nikawawahi nisiwape muda wa kujiandaa. Mmoja nikampoka bunduki na kisha nikamdaka na kumwekea tundu la bunduki kichwani nikimwamuru mwingine aweke silaha yake chini.
“Fanya upesi kabla sijammwaga mwenzio ubongo!”
Huyu niliyekuwa nimemdaka alikuwa ni yule mwanaume niliyekuwa naye kwenye basi. Mwenzake, mwanaume mrefu mwenye mwili mpana, akan’tazama kwa mashaka kama mtu ajiulizaye nini cha kufanya.
“Nimesema weka silaha chini!” Nikamwamuru. “sitasema tena sasa hivi, utaokota maiti ya mwenzako!”
Basi akainama na kuweka silaha yake chini akiwa anan’tazama kwa kukodoa.
“Ninyi ni wakina nani?” nikauliza. “Kwanini mnanifuata?”
Kimya. Hamna aliyenijibu. Nikarudia tena kuwauliza mara hii nikikaza sauti zaidi, lakini haikuleta tofauti! Hakuna aliyenijibu.
“Sina muda wa kupoteza na ninyi! Kama hamtanipa majibu ya maswali yangu basi nitawamaliza maana haitakuwa hasara kwangu.”
Nilipomaliza tu hiyo kauli, bwana yule niliyekuwa nimemkaba, akawahi kuudaka mkono wangu wenye silaha, akajigeuza upesi akitaka kufanya shambulio kwa ngumi ila kwa upesi nikamkwepa, na nilipoona yule mwenzake ametwaa bunduki aliyoiweka chini, nikafanya jitihada za haraka za kumdaka mwanaume yule mwenye mustachi na kisha nikajikinga naye.
Hapo mwenzake akapata kigugumizi cha kufyatua bunduki, nikamtupia risasi mbili na kumlaza chini hajiwezi. Kisha mwanaume yule niliyemkaba nikamziraisha na kumweka begani. Ikanipasa niondoke mapema eneo hilo kwani milio ya bunduki ingewafanya vyombo vya usalama kujongea hapo muda si mrefu.
**
Saa moja usiku …
Baada ya kutoka kuoga, nilijifuta maji na kisha kumjongea mateka wangu ambaye nilikuwa nimemfungia kitini. Alikuwa bado hajarudi fahamuni hivyo nikamwagia maji na kumtaka ajibu maswali yangu kama salama ya roho yake.
Lakini mwanaume huyo hakuogopa kabisa. Akiwa anan’tazama usoni, akaniambia hatajibu swali langu hata moja. Na nikitaka nimuue pasipo kujichosha. Hapo ikabidi nitafute namna ya kumfanya aongee.
Nikamnyanyua na kumpeleka bafuni. Nikamvika mfuko wa kitambaa kichwa kizima na kuanza kumwagia maji usoni mwake kumnyima pumzi. Akahangaika sana. Lakini kila nilipouvua mfuko huo na kumuuliza, bado hakuwa tayari!
Nikamtesa sana mpaka mwishowe akawa amepoteza nguvu kabisa. Macho yalilegea na mdomo akaacha wazi akitapika maji, ila bado hakuwa amenipa majibu ya maswali yangu. Bado alikuwa na roho ngumu!
Basi nikaona nimpe mapumziko alafu tutaendelea tena muda utakaporuhusu, kwa muda huo nikawasiliana na Daniele na kumwambia yaliyotukia. Naye akaniambia hatua aliyofikia pamoja na timu yake. Siku hiyo alikuwa ameonana na Makamu wa Raisi na pia mke wa Raisi. Wote alifanikiwa kuwafanyia mahojiano lakini hakuna kikubwa alichoking’amua, zaidi mke wa Raisi alikuwa anaumwa na anatazamia kwenda kwao, Australia, kwa ajili ya mapumziko.
Na zaidi ya yote, alipata taarifa kuwa O’Neil, yule bwana aliyetupatia kiasi kidogo cha taarifa, amekutwa akiwa amekufa huko Massachusetts! Mwili wake umekutwa ukiwa mtupu na ishara ya kupitia mateso.
Habari hiyo ikanishtua kwa namna yake. Nani atakuwa amemuua O’Neil? Na je kifo chake kitakuwa na mahusiano na taarifa zile alizotupatia?
Nikamtaka Daniele afuatilie kwa undani juu ya kifo hicho kwani kitakuwa nacho kina mlango wa kutupeleka tunapopahitaji. Basi hata nilipokata simu, nikaendelea kuwaza juu ya kifo cha O’neil. Si bure mzee yule hakuwa anataka kujihusisha na haya mambo!
Lakini kifo hiko kikanipa maswali sana juu ya wauaji. Je pia watakuwa wanajua kuhusu mimi na taarifa zile za bwana O’neil?
Mara mlango ukagongwa na kuniamsha toka kwenye lindi la mawazo. Nikanyanyuka toka kitandani na kwenda mlangoni kumkuta mhudumu. Mwanamke mrembo mwenye mashavu mekundu. Aliniambia kuhusu chakula, kipo tayari kwenye hall, lakini kabla hajaenda, bwana yule niliyekuwa nimemfungia bafuni, akaanza kupiga kelele akigugumia!
Mhudumu akan’tazama kwa hofu, nami kumpoza nikamwambia huyo ni mwenzangu yu hoi anaumwa. Lakini ni wazi maneno hayo hayakumkosha mhudumu, akaenda zake akiwa na sura ya mashaka, na hata mwendo wake ukiwa wa kasi!
Muda kidogo, kama dakika mbili, mlango ukagongwa kwanguvu. Kabla sijauendea nikauliza, “Nani?” sauti ya kiume ikanijibu, “Staff!”
Taratibu nikasonga na kuchungulia nje kwa kupitia tundu mlangoni. Huko nikaona majibaba mawili wakiwa wamevalia sare za hoteli. Walikuwa ni walinzi. Hapa nikapata kujua kuwa mhudumu yule alienda kutoa taarifa juu ya sauti ile alosikia chumbani mwangu.
Nikaufungua mlango, na pasipo kuonyesha lolote usoni mwangu, nikawauliza, “naweza kuwasaidia?”
“Tumekuja kufanya ukaguzi chumbani mwako!” mmoja akajibu akinitazama machoni.
“Mtakaguaje chumba cha mteja?” nikawauliza nikiwakunjia ndita.
“Ndugu, ni jukumu letu kuhakikisha kuna usalama ndani ya hoteli. Kama unaona ni shida, basi tuwaite polisi watekeleze hilo!” akasema yule bwana aliyejielezea hapo awali. Kidogo nikafikiria na kuona ni kheri nikawaruhusu watu hao waingie ndani na kufanya ukaguzi kuliko ujio wa polisi hapo.
Basi, kama watu wanaofahamu kinachoendelea, wakanyookea bafuni, huko wakamkuta bwana yule niliyemfungia. Wakamfungua kamba toka kwenye kiti na kumweka huru. Kisha mimi wakaniweka chini ya ulinzi wakinituhumu kama mtekaji!
“Upo sawa?” Mmoja akamuuliza yule bwana waliyemwacha huru. Naye kwa uchovu akawajibu, “nipo sawa, nashukuru.”
Wakamuuliza kwanini mimi nilimfungia kule bafuni, naye akatoa maelezo ya wongo kuwa nilitaka kumuua kisa nikitaka pesa toka kwake, basi walinzi wakapiga simu polisi kutoa taarifa juu yangu.
“Huyo anawaongopea,” nikapaza sauti. “ni yeye ndiye anataka kuniua. Yeye pamoja na mwenziwe!”
Lakini nani aniamini? Mazingira yalikuwa yananisaliti na kuninyooshea kidole kuwa mimi ni muuaji. Basi tukiwa hapo, ndani ya muda mfupi tu, yule jamaa, jambazi, kwa upesi akawadhibiti walinzi wa hoteli na kuwaweka chini ya ulinzi. Alitumia bunduki niliyompokonya. Bunduki hiyo nilikuwa nimeiweka kwenye droo ya kitanda.
Alipofanikisha hilo, akaninyooshea tundu la risasi na kuniamuru niseme kile kilichonileta Ujerumani. Tena niseme upesi kabla hajanimaliza aende zake.
Nikamwambia huku nikinyoosha mkono juu, “mimi ni mtalii tu! Sitambui kwanini wanifuatilia namna hii!”
“Usinifanye mimi ni mjinga! Natambua kinachoendelea na kama uki—” hakumalizia, nikawa nimemtupia stuli iliyokuwa imesimama kando yangu. Stuli hiyo kwakuwa niliitupa kwanguvu, ikafyeka miguu yake na kumwangusha chini! Kabla hajaamka, walinzi wakamuwahi kumpokonya silaha, ila ajabu akafurukuta kwanguvu na kumtupa mlinzi mmoja kando kwa kumkandika teke zito. Na huyo mwingine akamchapa kiwiko na kisha ngumi nzito, akalala kando amezirai.
Kabla hajateka tena bunduki, nikajitupa na kuunyoosha mguu wangu kuisogezea mbali kwa teke, alafu nikaunyanyua kutaka kumkandika kifuani. Akakwepa. Akajirushia mgongo kunifuata. Akatupa ngumi yake, nikaiyeya, ya pili nikaidaka na kuiviringita! Akajizungusha na kutupa kiwiko, nacho nikakisogezea pembeni na alafu kumdaka shingo yake na kumkaba kwanguvu zangu zote.
Akatapatapa akituma viwiko vyake. Havikunipata. Ila kimoja kilitifua mbavu yangu na kunipa maumivu makali. Nikavumilia na kuendelea kumkaba. Akatupa tena kingine, hakikunipata, cha tatu kikanitifua tena. Hapo nikashindwa kuvumilia!
Bwana huyu akajichomoa toka kwenye mikono yangu na kisha akaniadhibu kwa ngumi ya shavu la kulia. Mdomo ukalowana damu. Lakini sikumruhusu achukue bunduki. Alipotaka kufanya hivyo, nikamuwahi kumvuta. Akatupa teke, nalo nikamdaka na kumvuta kwanguvu, alafu nikamrukia mgongoni na kumkaba tena. Mara hii mikono yake niliikandamizia na magoti yangu, hakuweza kufurukuta!
Akapoteza kabisa nguvu. Macho yakaanza kuelekea juu. Nikalegeza mikono yangu na kumuuliza ametumwa na nani. Kwa mbali nikamsikia akisema, “Rodolfo!” kisha akazirai!
***