Nyuma yako (Riwaya ya S. Mollel)

*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 26*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

“Hata nami ningependa kwenda huko kabla ya kukoma kwa maisha yangu!” Vio akasema kwa furaha. Wakakumbatiana tena na tena. Walikuwa na furaha sana, waliona sasa wameshaukwaa.

Lakini pasipo kujua, Jack Pyong alikuwa amesimama mahali akiwatazama, moyo wake ukiwa unavuja damu.

“Vio,” Jack akaita kwa kunong’ona. “Nimekukosea nini?” akauliza kana kwamba Vio yu pembeni yake kisha akajikongoja taratibu kulifuata gari.

ENDELEA

Alipolifikia hakufanya kitu bali akaendelea kutazama mpaka pale aliposhtukiwa. Vio alibumbuwaa kumwona Jack, na kwa kiasi fulani akahofu, lakini kwa upande wa Gotham kwake ilikuwa kinyume, ni kama vile alikuwa anatarajia ujio wa Jack kwani hakuwa anahofu wala kuhenya, alimtazama Jack kisha akampuuza.

“Vio,” Jack akaita na kuuliza, “nimekukosea nini wewe?”

Mashavu yake yakafunikwa na machozi, alikuwa anang’ata meno kwa uchungu. Kidogo Vio akabanwa na haya.

Lakini kadiri muda ulivyokuwa unaenda, Jack akawa anapatwa na hasira. Akajikuta akitaka kumdaka Vio na kumwadhibu kadiri awezavyo lakini Gotham akammudu mwanaume huyo na kumkandika makonde kadhaa kabla ya kumwacha hapo akiwa anavuja damu na hajielewi.

Uso wa Jack ulikuwa unavuja damu, jicho lake moja limevimba na tumbo lake linauma haswa kwa kukandikwa ngumi! Lakini Jack hakuwa anaumizwa sana na hayo majeraha bali kutendwa kwake na Vio.

Huko kulimuuma kusipokuwa na mithili. Alihisi moyo wake unasinyaa kwanguvu kumimina damu.

“Kwanini Vio?”

Alijikunyata akiwa gizani.

**

Saa mbili asubuhi …

“Nyanyuka twende!” alisema bwana Charles Smith akimtazama Miss Danielle, bwana huyo aliyekuwa amevalia suti nyeusi iliyobana mwili wake mwembamba.

Alikuwa ni mwanasheria wa Danielle. Punde alikuwa ametoka kuongea na inspekta James Peak na kaufikiana kulipeleka shauri hilo mahakamani, mahali ambapo mteja wake atapata haki yake.

Basi Danielle akanyanyuka na kuongozana na bwana Charles mpaka kwenye gari na kutimka toka kituoni. Mwanamke huyo alikuwa amejikunyata akiwa amemezwa na mawazo.

“Usijali, miss,” Charles akamtoa hofu. “Ni kesi ndogo sana isiyo na ushahidi. Tutakapoenda mahakamani haitachukua muda kuimaliza na kuifutilia mbali!”

Na zaidi bwana huyo akapendekeza waweke fidia ya juu kwa serikali kwa kumpotezea muda mteja wake na pia kumchafulia taswira yake mbele ya jamii.

“Unaonaje?” akauliza bwana Charles akitabasamu.

“Ni sawa,” akajibu Danielle kisha akanyamaza asiongeze jambo, basi safari yao ikawa kimya kwa muda.

Bwana Charles hakujua nini ambacho kinamtatiza Danielle kichwani. Alimwona mwanamke huyo akiwa ametulia kupita kiasi na kwakuwa hakutaka kumtibua akaamua naye kuufunga mdomo wake.

Walipotembea kwa muda fulani Danielle akamuuliza bwana Charles kuhusu ile fidia aliyokuwa ameisema awali, anadhani itakuwa ni kiasi gani? Hapo bwana huyu akapata kujua angalu kile ambacho kilikuwa kinakatiza kwenye ubongo wa huyu mwanamke.

Alitabasamu akimwangalia.

“Inaweza ikawa pesa kubwa sana, inategemea na wewe utakuwa unahitaji kiasi gani.”

Danielle akafikiria kidogo, ni kama vile alipata wazo jema, alifyatua miguu yake aliyokuwa ameikunyata akamwangalia bwana Charles na kumuuliza,

“Una uhakika tunaweza kushinda hii kesi?”

Bwana Charles akatikisa kichwa. “Sijaona ugumu wake, miss. Nimeshahangaika na kesi kubwa na ngumu kuliko hii … huko kote nikatoka salama!”

Kauli hiyo ikapandikiza mmea ndani ya moyo wa Danielle.

Kuna kitu alifikiria na kwa namna moja kikaukimbiza moyo wake.

**

Saa moja jioni …

“Unaweza ukapumzika sasa,” alisema Marshall akiwa anamfunika Jack shuka.

Jack alikuwa na macho mekundu ila la kulia likiwa jekundu zaidi. Uso wake ulikuwa umevilia damu na kuzibwa na bandeji baadhi ya sehemu. Alikuwa amechoka lakini pia ameumizwa. Majeraha ya mwili waweza kuyatia dawa, vipi ya mapenzi?

Marshall alikuwa anafahamu kile ambacho Jack alikuwa anapitia. Alikuwa anafahamu namna gani ambavyo mwanaume huyo alikuwa akimpenda Vio, kwa moyo wake wote, ilikuwa ni ngumu kuukubali ukweli kwamba mwanamke huyo alikuwa akimdanganya.

Ukweli ulikuwa mchungu kuukubali kuumeza.

“Jack, yapasa uache jambo hili lipite sasa,” alisema Marshall aliyekuwa ameketi pembeni ya Jack. Alikuwa akimtazama rafikiye kwa imani.

“Kuendelea kulibeba hili hakutaleta lolote jema zaidi ya maumivu. Sawa, Jack?”

Jack alikuwa akitazama kingo ya kitanda kwa fikira. Macho yake yalikuwa yanadondosha machozi. Machozi na damu.

Alimtazama Marshall kisha akamuuliza, “Ulikuwa unayafahamu haya, Tony, sio?”

Marshall akashusha pumzi ndefu puani. “Jack, si muda mzuri wa kuongelea haya.”

“Ulikuwa unafahamu, sio?” Jack akakazia swali lake. Alikuwa anamtazama Marshall kwa macho yake mekundu.

“Kwanini haukuniambia muda wote huo, Tony?”

“Jack, sikutaka kukuumiza.”

“Mbona sasa naumia?”

“Samahani, Jack. Nilitaka nilimalize jambo hili kwa mikono yangu, ni kwamba nimekawia.”

“Tony, siku zote ulikuwa unajua Vio ananizunguka lakini ukanyamaza. Umeniumiza.”

“Najua, Jack. Nisamehe sana.”

Jack akarudisha macho yake kwenye kingo ya kitanda akiendelea kuwaza.

“Kumbe ndo’ mana alikuwa anataka uondoke karibu na mimi. Ndo’ maana alikuwa hataki kuja kukuona. Kwanini sikuyajua yote haya mapema? Kwanini nilikuwa mpofu kiasi hiki?”

Marshall akamsihi Jack aachane na fikra hizo kwani zitazidi kumuumiza, lakini kidogo kwa Jack swala hilo likawa gumu, alishindwa kunyamaza, moyo ulikuwa unamuuma sana.

Mwishowe akamwomba Marshall akamletee kinywaji kikali ili apate kunywa kujipumbaza, mwanzoni Jack akawa mgumu kutimiza agizo hilo lakini alipokuja kuona kwamba pengine litakuwa ni tiba ya muda kwa Jack, akaamua kwenda zake kumfuatia.

Baada ya dakika kadhaa akawa amerejea akiwa amebebelea chupa kubwa ya vodka, akammiminia Jack glasi kadhaa na haikuchukua muda Jack akajikuta akielemewa na kichwa, akalala.

Marshall akamfunika vema shuka kisha akamtakia usiku mwema. Akiwa hapo pembeni ya Jack, akafikiria kumhusu Vio, akafikiria kuhusu Gotham.

Aliona watu hao wanastahili kuadhibiwa. Haiwezekani waishi maisha kwa furaha tele ingali wamemuumiza rafiki yake, tena pasipo huruma!

Kila ngumi iliyomgusa Jack, itarudi mara tatu yake. Aliapa kwenye hilo.


**

“Mbona umekawia sana?” Katie alimuuliza Marshall punde baada ya mwanaume huyo kuingia ndani. Ulikuwa ni usiku wa saa tano sasa.

“Kulikuwa kuna mambo kadhaa ambayo nisingeweza kuyaacha,” Marshall akamwambia Katie na kisha akambusu mwanamke huyo kwenye lips zake.

“Vipi lakini? Unaendelea vema?”

Katie akatabasamu.

“Nipo sawa maana upo hapa!”

Wakakumbatiana kisha Marshall akambeba mwanamke huyo juu juu mpaka kochini alipomlaza.

“Nilikukumbuka kweli,” akasema Katie. “Nilijihisi mpweke sana, siku nyingine usiwe unaniacha kwa muda hivyo Marshall.”

“Basi nimeshafika, kuna tatizo?”

Wakatazama kwa mapenzi na kupeana mabusu. Wakafurahia haswa muda wao.

Lakini wakiwa hawana hili wala lile, hawakuwa wanajua kwamba hawapo wenyewe. Nje ya kuta kulikuwa kumepaki magari manne, na bwana James Peak akiwa na maajenti wengine wa FBI pamoja na polisi walikuwa wapo maeneo ya karibu wakitazama kila kinachoendelea. Walikuwa wameshazigira eneo zima wakisubiria amri tu.

Katika hali ya kushtua, bunduki ikalia kwanguvu na risasi ikafyatuka kumfuata Marshall! Kufumba na kufumbua, risasi iyo ikatoboa kochi pembeni kidogo ya bega la mwanaume huyo.

“Amka Katie! Kimbia!” Marshall akafoka akimnyanyua Katie, mambo yalikuwa yamekwisha haribika, lakini wasifike mbali, risasi zikarushwa kwa fujo sana na tatu zikazama ndani ya mwili wa Katie!

**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 27*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Katika hali ya kushtua, bunduki ikalia kwanguvu na risasi ikafyatuka kumfuata Marshall! Kufumba na kufumbua, risasi iyo ikatoboa kochi pembeni kidogo ya bega la mwanaume huyo.

“Amka Katie! Kimbia!” Marshall akafoka akimnyanyua Katie, mambo yalikuwa yamekwisha haribika, lakini wasifike mbali, risasi zikarushwa kwa fujo sana na tatu zikazama ndani ya mwili wa Katie!

ENDELEA

Mwanamke huyo akadondoka chini akilalama kwa maumivu, upesi Marshall akamnyanyua mwanamke huyo na kujificha naye nyuma ya ukuta wa korido. Katie alikuwa anakufa.

Marshall akamsihi sana Katie abaki naye, alimwomba asimwache kwani bado anmhitaji, hawezi kuishi bila yeye.


Katie akiwa anatiririsha machozi, akamtazama Marshall na kumshika shavu kwa mkono wake dhaifu. Mgongo wake ulikuwa unachuruza damu. Shingo yake ilikuwa imejeruhiwa pia, bila shaka uti wake wa mgongo ulikuwa umedhurika.

Mwanamke huyo akatabasamu akiwa anabubujikwa. Ilikuwa ni namna ya ajabu. Uso wake ulimpasha moyo wa Marshall.

Alimtazama Marshall kwa kama sekunde mbili alafu akamwambia, “Nafurahi kufia mikononi mwako. Nakupenda sana, Marshall.”

“Tafadhali, Katie!” Marshall akasema kwa kutetemeka. Mikono yake ilikuwa inayumba na sauti yake inatikisika. Macho yake yalikuwa yanabubujikwa na machozi mdomo wake akishindwa kuutuliza, ulikuwa unatetemeka kwa kupindapinda. Alijitahidi kubana meno yake lakini bado haikuwa inasaidia.

Moyo wake ulikuwa unavunjika. Moyo wake ulikuwa unavuja damu. Hakuwahi kuhisi hisia kama hizo hapo nyuma. Hakuwahi kuhisi namna ile tangu kuzaliwa kwake, hisia za hasira, uchungu na mfadhaiko kwa pamoja!

“Naenda, Marshall,” akasema Katie kwa sauti ya chini. “Pambana vita vyako vema, tutakutana.”

Maneno hayo yakamuumiza sana Marshall, alitamani kupiga yowe kali, ukunga wa maumivu. Kifua chake kilikuwa kinawaka moto. Ni kama vile alikuwa anataka kulipuka!

Haikupita dakika, Katie akazima. Marshall akamwita Katie kana kwamba mama aliyempoteza mwanaye kwenye shimo kubwa, kumwita kwa kilio cha uchungu.

Rudi Katie. Nisamehe. Samahani Katie! Alilia sana. Muda mwingine sauti yake haikuwa inasikika sababu ya milio ya bunduki.

Aliinamishia kichwa chake kwenye kifua cha Katie. Kifua kilikuwa kimya kisicho na mapigo. Kilikuwa tayari ni kifua cha mfu.

**

“Acha kufyatua risasi!” alifoka bwana James akinyoosha mkono wake juu. Kwa wakati huohuo alikuwa akiongea na chombo cha mawasiliano kuwapasha na wale wengine ambao wapo upande mwingine mwa jengo. Basi milio yote ya bunduki ikakoma!

“Nani aliwaambia mrushe risasi?” Bwana James akafoka kuuliza. Alimtazama mmoja wa ajenti wa FBI aliyekuwa kando yake upande wa kushoto, alikuwa ni wa kwanza kabisa kutupa risasi, akamfuata na kumkwida nguo yake, “Afisa nani alikwambia utupe risasi?”

Ajenti huyo wa FBI akatoa mkono wa bwana James kwenye nguo yake. Alimtazama bwana James kwa kiburi, akamwambia, “sipo chini ya order yako, sawa?”

Bwana James akang’ata meno yake kumwambia kwa msisitizo, “Upo kwenye order yangu, hapa tupo kumkamata mtu ninayemshughulikia na kesi yangu, si kama mtu aliyetoroka gerezani bali kama mtuhumiwa wa mauaji!”

Kitu ambacho bwana James Peak, mpelelezi, hakuwa anakijua ni kwamba ajenti huyo wa FBI alikuwa ni mtu mwenye mabwana wawili. Si tu FBI bali pia na bwana Ian Livermore.

Alikuwapo kwenye misheni hii kummaliza Marshall na si vinginevyo. Kama Marshall akiwahi kushikwa na mikono ya dola, pengine atapewa uhuru wa kuongea, pengine atasema ambayo hayatakiwi kusemwa!

Halikuwa jambo jema kabisa hilo.

Basi baada ya bwana James Peak kutoa agizo la risasi kukoma, kukawa tulivu haswa. Akauliza kwenye kifaa chake cha mawasiliano kama kuna yeyote anayemwona Marshall kwenye ‘sight’, bado kukawa kimya.

Hakuna aliyekuwa anamwona Marshall.

Kidogo tu kabla ya mawasiliano hayo kukoma, taa zote za makazi ya Marshall zikazima na kukawa kiza totoro! Sio tu kumwona Marshall, sasa kukawa kutokuona chochote ndani ya nyumba ya Marshall.

“Anataka kufanya nini?” James akauliza kwa sauti ya chini akiwa anatazama makazi ya Marshall, alihisi kuna kitu kinaendelea japo bado hakifahamu, na ni wazi kitu hicho si kizuri kwake.

Basi upesi akaamuru taa zimulike makazi hayo na watu wote wawe ‘attention’ muda wote. Baada ya hapo akatoa agizo la watu kadhaa kuzama ndani ya makazi ya Marshall kutazama kinachoendelea ndani.

Taa bado zilikuwa zinamulika lakini si kote. Hawakuwa wamejiandaa na tukio kama hilo, taa zilikuwa si kubwa hivyo ilikuwa inawalazimu kuhamishia huku na kule kumulika.

Watu watano wakaingia ndani wakiwa wamebebelea bunduki. Taratibu taratibu walisonga kwa uangalifu, bado mwanga ulikuwa hafifu hivyo wakawa wanategemea kurunzi ndogo ambazo zipo kwenye silaha zao.

Walimulika wakiwa wanazama ndani ya mlango. Walipozama wakaendelea kumulika wasione kitu.

“Vipi?” sauti ikauliza kwenye vyombo vyao vya mawasiliano. “Mmeona kitu?”

“Hapana, bado hatujaona kitu!” mmoja wao akajibu.

“Hamna dalili ya mtu humo?” sauti ya bwana James ikauliza tena. Kabla ya yule kiongozi wa wale watano waliongia ndani hajajibu, wakasikia sauti ya mtu akiwa anateta kwa mbali, basi akanong’oneza akiwa amekodoa macho,

“Ngoja!”

Kisha wakaanza kusonga kufuata kule waliposikia sauti. Ni kweli kulikuwa na sauti hiyo na si kwamba masikio yao yalikuwa na matatizo.

“Kuna sauti ya mtu!” sauti ikasikika kwenye sikio la bwana James.

Akiwa amebonyezea kidole kwenye kifaa hicho cha usikivu, bwana huyo akauliza,

“Ya jinsia gani?”

“Ya kiume,” akajibiwa.

“Ipo upande gani mwa nyumba?” James akauliza tena, mara hii kidogo kukawa na ukimya, akarudia tena na mara akajibiwa ni upande wa magharibi mwa geti.

“Mmeshafika? Mmeona kitu?” James akauliza tena, alikuwa na mchecheto wa kutaka kufahamu, moyo wake ulikuwa unapiga kwa mbali, angetulia pale tu angesikia kama Marshall ameonekana na ametiwa nguvuni.

“Vipi mmefika?” akarudia kuuliza. “Mmeona kitu huko?” sauti yake ilikuwa kubwa tofauti na ya hapo awali lakini bado hakukuwa na majibu.

Kidogo sauti ikasikika,

“Tume--”

Kabla haijamalizika, milio ya bunduki ikaita kwanguvu na kwa wingi! Milio hiyo haikukoma ndani ya muda mfupi, bwana James Peak alikuwa mtulivu sana kuskiza lakini ndani ya muda akawa amepoteza uvumilivu, akaamrisha watu zaidi waende ndani.

Milio ya risasi ikaendelea kulia, na ndani ya muda mfupi, watu waliopo nyuma ya jengo wakatoa taarifa kumwona mtu, isichukue muda bwana James akazama naye ndani kwani risasi zilikuwa zinaendelea kuvuma.

Alipozama humo, baada ya muda, akabaini hakukuwa na mtu bali tu bunduki kadhaa zilikuwa zimefungwa na kamba na kuachwa zinatema risasi. Wale watu watano wa mwanzoni wote walikuwa wameuawa, wapo chini wakivuja damu.

“Mkuu, ametoroka!” alisema mtu aliyekuwa nyuma ya jengo, hapo ndiyo bwana James akatambua kuwa mchezo ule wa bunduki kutupwa ulikuwa umepangwa kwa ajili ya kuwapotezea muda na ‘attention’.

Alipoenda kutazama huko nyuma akamkuta ni mtu mmoja tu ndiye ambaye alikuwa anajiweza, naye alikuwa amelala chini akiwa anavuja damu. Ni kwamba mwanaume huyo alijivuta kufuata kifaa cha mawasiliano na kukibandua toka kwenye mwili mfu wa mkuu wake kisha ndipo akamtaarifu bwana James.

“Ametoroka,” alisema jamaa huyo kwa kukoroma, macho yake yalikuwa yamelegea kinywa chake kikiwa wazi. “Ametoroka na mtu mgongoni,” alimalizia jamaa huyo na kisha akapoteza fahamu.


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 28*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Alipoenda kutazama huko nyuma akamkuta ni mtu mmoja tu ndiye ambaye alikuwa anajiweza, naye alikuwa amelala chini akiwa anavuja damu. Ni kwamba mwanaume huyo alijivuta kufuata kifaa cha mawasiliano na kukibandua toka kwenye mwili mfu wa mkuu wake kisha ndipo akamtaarifu bwana James.

“Ametoroka,” alisema jamaa huyo kwa kukoroma, macho yake yalikuwa yamelegea kinywa chake kikiwa wazi. “Ametoroka na mtu mgongoni,” alimalizia jamaa huyo na kisha akapoteza fahamu.

ENDELEA

Bwana James akawa amekanganyikiwa, mambo haya hayakuwa yanamwingia kichwani kabisa, ni kivipi Marshall akatoroka kwenye umati kama ule? Tena wenye silaha na watu wafanisi?

Kidogo akawa amejifunza ni mtu wa aina gani anasumbuka naye, Marshall hakuwa mtu wa kawaida, siku hiyo alijifunza funzo hilo muhimi kabisa.

Akashusha pumzi ndefu kabla hajawataarifu watu wa huduma kwa wagonjwa ambao walifika muda si mrefu na kuanza kuwaokota watu lakini pia kuwapatia huduma. Na kwa muda huohuo vyombo vya habari vikiwa vimejazana kukusanya mawili matatu hapo.

Bwana James hakutaka kuongea jambo, akajiweka mbali na vyombo vya habari akijaribu kutafakari mambo yalivyotokea, japokuwa agizo lilitoka kwa hospitali zote na sehemu za huduma juu ya kutoa taarifa endapo wakipata majeruhi wa risasi, bado bwana James hakuwa anaona kama inatosha.

Bado aliona anatakiwa kutafuta njia mbadala za kumpata Marshall, lakini sasa atampataje? Aliona kichwa chake kinapasuka. Njia mbadala ya kumpata mwanaume huyo ilikuwa ni kwa kupitia Katie, sehemu dhaifu ya mwanaume huyo, sasa wameshaitifua.

Kwa upande wa Jack na Danielle kulikuwa ni ‘complicated’ sana, njia hizo zilikuwa ngumu na si za moja kwa moja, mosi Jack haijulikani yupo wapi na kwa upande wa Danielle napo kesi itaenda kunguruma mahakamani tena ikiwa haina hata ushahidi!

Alizamia sana kwenye fikira, ghafla akashtushwa na mtu aliyegonga kioo chake kumtaka akishushe, alipotazama akamtambua mwanaume huyo ni ajenti wa FBI kwa kupitia mavazi yake, akashusha kioo na kumtazama mwanaume huyo kwa maulizo.

Mwanaume huyo akatoa kitambulisho kumwonyesha bwana James kisha akampatia mkono kwa salamu.

“Pole sana kwa kilichotukia,” alisema mwanaume huyo akiegemea mlango. Kwa jina alikuwa ni William Bogeyman.

“Unaweza kuniambia kipi kilitukia tafadhali?” akauliza bwana huyo akiwa anamtazama bwana James.

“Hamna maelezo makubwa, afisa,” akaeleza James kwa uso wa kusonona, “ni kwamba mhalifu ametu ‘outsmart’. Mipango yake ilikuwa bora zaidi ya kwetu.”

Bwana William Bogeyman akatabasamu kwa mbali, “Unajua nini bwana James, pengine haukuwa unajua Marshall ni mtu wa aina gani. Ni afisa wa zamani wa CIA, tena akiwa mmoja wa watu wakupewa kazi kubwa na kuzitekeleza kwa ufanisi mkubwa. Ana rekodi ‘udisputed’ kwenye misheni zake zote. Hajawahi kupoteza hata moja.

Hata moja.

Anajua kila mbinu za kiintelijensia. Anajua michezo yote ya silaha na amefundishwa namna gani ya kutumia akili yake mara tatu zaidi ya kwako. Ni mtaalamu wa mapigano ya silaha na pia pasipo silaha.

Nathubutu kusema ni adui mkubwa kuliko gaidi mwingine yeyote toka kwenye mataifa adui ya Marekani kwani yeye anafahamu vizuri serikali, milango na kila baraza la Marekani kama kiganja cha mkono wake wa kuume.

Kwahiyo unapokuwa unasumbuka naye, beba tahadhari hiyo!”

Bwana William akamalizia akimtazama bwana Marshall kwa macho ya kumpa pole.

“Nashukuru, afisa,” akaitikia James kisha akabonyeza mlango kupandisha kioo.

Mara bwana William akakizuia kioo kwa mkono na kumwambia, “Unaonaje kesi hii ukaikabidhi? Nadhani kuna haja ya kuipeleka mbele zaidi ya hapa.”

Bwana James akatikisa kichwa, “hapana, sijashindwa kiasi hicho afisa. Kila mtu atende na nafasi yake. Sijaona haja ya kunyanyua mikono hivi sasa.”

Baada ya James kusema hayo akaendelea kupandisha kioo chake na sasa kikafunga kabisa. Bwana William akamtazama kwa kama sekunde tatu alafu akaondoka zake, basi punde waandishi wa habari wakamjia bwana James, ni kama vile waliagizwa, wakiwa wamebebelea vinasa sauti na kamera kana kwamba wameona fumanizi.

Bwana James kuona vivyo akaamua awashe gari lake na kutimka.

**

“Kwahiyo?” akauliza Ian Livermore. Alikuwa amesimama kandokando ya meza yake akiwa ameshika kiuno. Uso wake ulikuwa umemezwa na fikira lakini pia sononeko.

“Nilijitahidi kumlenga laki--”

“Lakini nini mbwa wewe?” bwana Ian akafokea simu. “Hivi kinachowashinda kumaliza kazi tukakaa kwa amani ni kitu gani? Mbona mnakuwa wajinga kiasi hiki?”

Bwana Ian alifoka na kufoka mate yakiruka. Alikuwa ameghafirika kweli. Alikuwa ameketi akiwa anangoja habari njema lakini mwisho wa siku ikawa upuuzi. Siku yake nzima ilikuwa imeharibika ingawa ni asubuhi.

“Mkuu, haikuwa kazi rahisi. Tulimzingira lakini akatoka katika namna ya ajabu!”

“Kwanini na wewe hukumpata katika namna ya ajabu?”

“Mkuu … mkuu, hai--”

“Hai nini? Nisikuone mpaka uwe umempata huyo mtu. La sivyo ishia hukohuko!” aliposema hayo akakata simu na kuibamizia mezani, akashusha pumzi ndefu na kuketi.

Mambo yalikuwa yanazidi kuwa magumu.

Kidogo mlango ukagongwa na bwana William Bogeyman akaingia na kumsalimu, mwanaume huyo alikuwa amevalia suti pasipo tai, akamhabarisha bwana Ian kuhusu namna alivyokutana na bwana James na kujaribu kumshawishi akabidhi kesi pasipo mafanikio.

“Sikujua kama ni kichwa ngumu, hakuridhia japo nilimshawishi.”

Bwana Ian akakuna kidevu chake kwa fikira kisha akamwambia bwana William kuwa ni namna gani mambo yatakuwa magumu endapo bwana James ataendelea kuifuatilia kesi hiyo.

Kama mwanaume huyo akiwa wa kwanza kumpata Marshall akiwa hai basi mambo yatakwenda kombo zaidi kwani pasipo ugumu mwanaume huyo anaweza akaeleza kila kitu anachokijua, jambo ambalo ni hasi kabisa kwenye mipango yao.

Ni lazima, kwa namna yoyote ile, wampate ama wamuume Marshall kabla haijawa vinginevyo!

“Sasa vipi kumhusu yule bwana?” akauliza William. “Hatokubali kuiachia kesi kwa wepesi?”

“Willy!” Ian akafoka kuita. “Upo hapa kwasababu una uwezo, kwasababu akili yako ina akili, sasa unaponiuliza maswali hayo unanifanya nianze kukutilia mashaka. Ina maana unazidiwa akili na mpelelezi? A common inspector?”

“Hapana, si --”

“Ni nini basi? Kweli upo hapa kunambia mpelelezi amekushinda?”

William akawa kimya, kinywa kilikuwa kizito. Basi bwana Ian akaendelea kuongea sana na sana, mwishowe akamtimua bwana William atokomee mpaka atakapokamilisha kazi yake. Hata kumwona kabisa.

**

Saa tatu asubuhi …

Jack alikuwa ameketi kwenye sebule ndogo akiwa anatazama runinga huku mkono wake wa kuume ukiwa umeshikilia chupa kubwa ya vodka.

Macho yake yalikuwa mekundu yanayorembua. Uso wake ulikuwa hoi na mchovu, ni kama vile mtu ambaye hajalala kwa juma zima. Alikuwa si mtu mwenye nguvu. Kifua chake kilikuwa wazi akiwa amevalia bukta pekee.

“... maeneo yote ya karibu yamefanyiwa upembuzi lakini hakuna matunda. Mtuhumiwa ametoroka na mpaka sasa haijajulikana yup wapi. Ilikuwa ni ajabu na kweli. Ilikuwa ni kama mchezo wa kuigiza kwenye maisha halisi …” aliongea mfikisha habari wa kike ndani ya kideo. Mwanamke mwenye nywele ndefu nyeusi akiwa ameshikilia kipaza sauti rangi ya samawati.

Mwanahabari huyo alikuwa amesimama mbele ya nyumba iliyokuwa inamhifadhi Katie na Marshall kabla ya kuvamiwa na maafisa usalama.

Basi Jack akatikisa kichwa chake na kunywa fundo moja la vodka na kusema,

“Upo wapi Marshall?”

Kisha akatazama chini kama mtu anayetafuta jambo.

“Sikuwahi kuwaza kama yatafikia hapa,” akasema na punde chozi likamchuruza.


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --29*

*Simulizi za series*

*NAKUJA KWA AJILI YAKO*

ILIPOISHIA

Mwanahabari huyo alikuwa amesimama mbele ya nyumba iliyokuwa inamhifadhi Katie na Marshall kabla ya kuvamiwa na maafisa usalama.

Basi Jack akatikisa kichwa chake na kunywa fundo moja la vodka na kusema,

“Upo wapi Marshall?”

Kisha akatazama chini kama mtu anayetafuta jambo.

“Sikuwahi kuwaza kama yatafikia hapa,” akasema na punde chozi likamchuruza.

ENDELEA

Zilipita siku sita pasipo Marshall kubainika yu wapi. Polisi, maajenti wa usalama na hata maadui walimtafuta kila kona pasipo mafanikio, haikuwa imebainika yu wapi wala anafanya nini huko. Swala hilo kwa kiasi fulani likawapa matumbo joto maadui zake kwani hawakuwa wana uhakika na kile kifuatacho, jambo hilo si zuri kwenye uono wao.

Basi bwana James Peak akiwa ameketi ofisini mwake, akawa mjawa wa mawazo sana. Kila mara angewapigia simu washirika wake na kuwauliza kama wamepata kitu lakini majibu yakiwa yaleyale, hamna jambo.

Alijaribu kila awazalo, akafika kila alipopashuku lakini bado ngoma ikawa ngumu. Kuna muda aliwaza kunyanyua mikono juu kwa kesi hii lakini akipiga moyo konde, labda kesho itakuwa bora zaidi basi akapambana.

“Vipi?” aliuliza kwenye simu. “Umeambulia kitu?”

“Ndio, mkuu,” sauti ikasema ndani ya simu, basi upesi bwana James Peak akajikusanya na kwenda huko ambapo aliyempigia yuwapo. Alikuwa ni mjawa wa shauku. Ndani ya nusu saa akawa amewasili na kukutana na mabwana wawili ambao walikuwa wameegesha vyombo vyao kando ya barabara.

“Morris!” bwana James akaita akiwa anafunga mlango wa gari lake, bwana huyo alikuwa anatembea kwa kurusha miguu upesi.

“Vipi? Nini mmepata?” James akauliza akiwa anakaribia wanaume hao wawili. Punde akawasili na kuwasalimu kwa kuwapatia mkono.

“Mkuu kuna kitu hapa cha kuona!” alisema bwana Morris kisha akajiveka glovu nyeupe na kumwonyesha bwana James kipande cha nguo. “Nadhani utakuwa unakitambua hiki.”

Bwana James alipotazama kipande hicho akabaini moja kwa moja kilikuwa ni nguo ya mwanamke aliyekuwa na Marshall wakati walipovamia nyumba hiyo, yaani Katie.

Kipande hicho cha nguo kilikuwa na mabaki ya damu.

“Hamna kingine?” akauliza bwana James.

“Hamna mkuu!” akajibu Morris akitikisa kichwa. “Tumesaka sana maeneo ya karibu pasipo mafanikio lakini tunaamini bwana yule atakuwa alikatiza hapa akiwa na usafiri kutokana na alama za matairi.

“Atakuwa ameenda wapi?” akajiuliza bwana James akiwa ameshika kiuno anakodolea barabara. Hakuwa ametosheka na basi akawataka watumishi wake waendelee na kusaka mahali hapo kama kuna kingine.

Baada ya msako usio na manufaa, wakaondoka bwana James akirudi ofisini kwake. Aliagiza kitambaa kile kifanyiwe upembuzi wa vinasaba kisha aletewe majibu, na pia akafanya kutoa taarifa za mazingatio kwenye ule uelekeo ambao Marshall alikuwa ameelekea.

Baada ya kufanya vivyo akapumzika.

**

Mlango ulifunguliwa na bwana James akazama ndani alipojiketia sebuleni na kunyoosha miguu.

Alikuwa mchovu aliyechoshwa na kazi. Aliwasha taa ndani ya makazi yake kisha akafanya namna ya kwenda kupooza mwili wake bafuni. Alipokoga akajirejesha sebuleni ambapo aliketi na kuwasha runinga.

Si kwamba alikuwa anatazana runinga hiyo bali ilikuwa inampa tu ‘kampani’, ingali akiwa anakula basi sauti ilikuwa inaruruma nyuma yake.

Alikula akijaribu kuwaza mambo kadhaa. Mara kwa mara alikuwa anashika simu yake na kutazama kama kuna jambo kisha akaendelea kula.

Ni punde akiwa anaendelea kula ndipo akasikia sauti iliyomgusa toka kwenye runinga. Sauti hiyo ilikuwa inaripoti kuonekana kwa Marshall maeneo fulani ya jiji la Philadelphia. Bwana James akiwa ameacha kula, akatazama na kuskiza kwa umakini.

“Mtuhumiwa huyo alionekana akiwa amebebelea mkoba mweusi na mwenye mwendo wa upesi akiwa anatazama chini. Ni pale gari lilimkosa kumgonga ndipo akanyanyua uso na kuangaza, alikuwa amevalia kofia nyekundu na suti traki rangi ya kijivu.”

Habari ilipoenda mbele zaidi akasikika pia muuzaji wa ‘mall’ akisema kuwa amemhudumia mtuhumiwa huyo lakini hakumjali sana mpaka pale ambapo mteja mmoja alimshtua kwa maulizo.

Mwisho kabisa moja wa washuhudiaji akasema ni gari aina gani aliyoonekana nayo bwana Marshall kutimkia.

Basi upesi bwana James akawapasha habari wenzake juu ya yale yote ambayo ameyaona na pia akatoa maagizo kadhaa juu ya wale washuhudiaji kwa mrengo wa kuhojiwa.

“Upembuzi uanze mara moja, Chevy Sonic nyeusi, mwanaume aliyevalia kofia nyekundu na traki ya kijivu - narudia, mwanaume aliyevalia kofia nyekundu na traki ya kijivu!” alisisitiza bwana James akisema modeli ya gari aliloonekana nalo Marshall lakini pia mavazi.

Akamaliza kula na kwenda ndani kujipumzisha. Bwana huyu anaishi mwenyewe kwenye makazi yake japo ni makubwa. Amekuwa akifungua geti na kujifungia kwa miaka miwili sasa baada ya kuachana na mke wake ambaye alikabidhiwa watoto kwasababu ya baba kuonekana kutingwa na kazi kupita kiasi, hana muda na familia.

Lakini kabla hajajilaza akagundua kuna karatasi juu ya meza yake ya chumbani. Wakati anaingia kwa mara ya kwanza chumbani humo hakuiona, ni sababu hakutia umakini wake huko. Karatasi hiyo ilikuwa pembeni kidogo mwa taa ndogo yenye mtindo wa uyoga.

Basi akaichukua na kuitazama, ulikuwa ni ujumbe, ujumbe wenye maneno machache - nakuja kwa ajili yako.

Bwana James akatazama dirishani na kisha mlangoni. Alianza kujihisi hayupo salama. Ni nani amemtumia ujumbe huo na amepitia wapi mpaka kumfikishia mezani, tena chumbani?

Ujumbe huo ulimfanya akatazame kitasa cha mlango wake wa chumbani, aliuacha mlango huo ukiwa umefungwa kama anakumbuka vema. Akatazama pia na mlango wa mbele na nyuma ya makazi yake lakini hakubaini kuvunjwa.

Sasa ujumbe huu ulikuwa umefikishwaje?

Alijikuta akipoteza amani kabisa. Ni Marshall? Kichwa chake kikagonga. Alikaa na kusimama, alisimama na kuketi akiwa na maulizo. Ni namna gani ilivyowezekana?

Alikubali ya kwamba yeyote yule ambaye atakuwa ameleta ujumbe huo atakuwa ni mkufunzi aidha kwenye wizi ama intelijensia. Ni mtu anayejua kuumba vyuma na pini kutengua vitasa hata vile vya kisasa. Ni mtu ambaye anamfuatilia.

Na huyo si mwingine bali Marshall!

Akanyanyua simu yake apige, lakini kabla simu haijaita, akasikia - tas! Kisha nyumba ikazima taa na kuzamia kwenye kiza totoro! Ni mwanga wa simu tu ndiyo ambao ukabaki kung’aza chumba.

Bwana James akatazama huku na kule akielekea simu yake kupata mwanga. Alijawa na hofu. Macho yalimtoka na kasi yake ya kuhema ikaongezeka.

Upesi akaendea kabati lake na kufungua atoe bunduki, ajabu hakuzikuta., badala yake akakuta ujumbe kwenye kuta ya kabati ukiwa unasema - hakuna silaha itakayokuweka salama dhidi yangu.

Basi akahisi kuchanganyikiwa, sasa akawa anatetemeka kwa woga. Mwanga wa simu ulitikisikatikisika sababu ya mkono wake kuyumba.

Hakuwa na silaha ndani kabisa, zingine zilikuwapo kwenye usafiri ambao ulikuwapo nje kwenye uwanja wa maegesho. Shida ni kufika huko.

Basi akangoja akisimamisha masikio. Hakusikia kitu. Baada ya kama robo saa, akafungua mlango wa chumba chake afuate ‘Main switch’ kutazama. Ilikuwa wazi switch hiyo ilikuwa imezimwa ndiyo maana ikatoa mlio ule.

Alisonga kwa tahadhari. Alipofungua switch kutazama akaona mshale wa ‘on’ ukiwa chini, main switch ilikuwa imezimwa. Na ndani ya kiboksi hicho cha switch kulikuwapo na kifaa kidogo maalumu cha kujifyatua, kifaa hicho ndicho kilifyatua switch na kuzima umeme.

Bwana James akawasha umeme na kuangaza, hakukuwa na mtu. Alikuwa mwenyewe kabisa nyumba nzima.

Huo ulikuwa ni UJUMBE tu.


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 30*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Alisonga kwa tahadhari. Alipofungua switch kutazama akaona mshale wa ‘on’ ukiwa chini, main switch ilikuwa imezimwa. Na ndani ya kiboksi hicho cha switch kulikuwapo na kifaa kidogo maalumu cha kujifyatua, kifaa hicho ndicho kilifyatua switch na kuzima umeme.

Bwana James akawasha umeme na kuangaza, hakukuwa na mtu. Alikuwa mwenyewe kabisa nyumba nzima.

Huo ulikuwa ni UJUMBE tu.

ENDELEA

Kesho yake alipokuwa kazini alimezwa sana na fikira. Hakuwa na furaha wala amani kabisa, alijihisi yupo uchi kabisa kwa Marshall na hilo halikuwa na mjadala, mosi mwanaume huyo amefika nyumbani kwake na pili amefanikiwa kuingia mpaka kwenye chumba alalacho na kuacha ujumbe.

Tatu na mwisho, ameweza mpaka kutegea kifaa ndani humo, vipi kama kingekuwa bomu?

Aliwaza kwanini Marshall hakumuibukia siku hiyo na badala yake kuwambia anamjia? Atamjia lini? Na kwa njia gani?

Alizamia kwenye fikra mpaka pale alipokuja kushtushwa na mmoja wa washirika wake akiwa amemletea majibu ya vinasaba ya kile kipande cha nguo cha jana. Majibu hayo yalithibitisha kuwa kipande kile cha nguo kilikuwa ni cha Katie.

Basi bwana James akaagiza pia picha ya mwanamke huyo iwekwe mtandaoni na pia kwenye makaratasi kumtafuta popote alipo. Endapo kuna mtu atamuona popote pale, atoe taarifa.

Japo watu hawa waliamini Katie anaweza akawa amekufa, bado walitoa nafasi ya kukosolewa mawazo yao hayo.

Yule mshirika akabeba maagizo ya mkuu wake vema, lakini haikuwa kitu cha kujificha, alimwona mkuu wake akiwa mtu mwenye kutingwa.

“Kuna lolote mkuu mbali na hili?” akauliza.

Baada ya James kutulia kwa kama dakika moja, akashusha pumzi ndefu puani alafu akamwambia mshirika wake, Morris kwa jina, yale ambayo yametokea jana yake. Habarizo zikamshtua Morris.

“Ni kweli unayoyasema?”

“Kweli na hakika,” akasema James akifungua droo yake. Punde akatoa ule ujumbe ambao aliukuta mezani na kumkabidhi Morris, ujumbe huo ulikuwa umehifadhiwa ndani ya kikaratasi kidogo cha nailoni.

Basi Morris akatumbua macho kuusoma ujumbe, na alipomaliza akamtazama bwana James kwa macho kodo, akamuuliza, “Sasa tunafanyaje?”

“Nenda maabara kikaangaliwe vinasaba vilivyomo humo!” James akaagiza, bwana Morris akanyanyuka na kutimiza agizo hilo upesi. Baada ya muda mchache akaja na majibu, hakukuwa na kitu isipokuwa vinasaba vya bwana James mwenyewe sababu ya kushika karatasi hiyo jana yake usiku.

“Hawajaona kingine?” James akatahamaki. Morris akatikisa kichwa kukanusha. Hakukuwa na cha ziada.

“Kweli si mjinga,” akasema bwana James kwa mafikirio. Ni wazi aliyeweka ujumbe huo alikuwa amevalia glovu kuficha alamaze za vidole. Kama basi yu mwangalifu kiasi hicho, kwanini mwanaume huyo, yaani Marshall, alitupa kipande kile cha nguo ya Katie?

“Mkuu,” akaita Morris na kusema, “pengine bwana huyu hutumia njia za kupumbaza.”

“Unamaanisha nini?” akauliza James akimtazama Morris apate kung’amua umbo.

“Inawezekana,” Morris akadokeza na kuendeleza, “inawezekana bwana huyu akawa amefanya jambo lile kwa kusudi kabisa ya kupoteza mwelekeo wetu.”

“Kivipi?” bwana James akawahi kuuliza kabla Morris hajakata kauli.

“Si unaona wote tuliamini huenda bwana yule akawa katika jiji la Philadelphia?” akamalizia Morris na kwa namna moja bwana James akaelewa nadharia yake.

“Bwana huyo anaweza akawa popote pale,” alisema Morris, “na zaidi anaweza akawa yupo karibu kabisa na sisi.”

Baada ya Morris kusema hayo hakukaa sana akaenda zake akimwacha James Peak mpweke.

“Kama mtu huyu aliweza kutoroka kwenye gereza lenye ulinzi mkali, atashindwa kuingia na kutoka ndani kwangu?”

Aliwaza.

Alisahau baada ya masaa kadhaa alikuwa na siku ndefu mahakamani.

**

“Niambie ni nini umefanya?” aliuliza bwana Ian Livermore. Bwana huyo alikuwa yupo ofisini kwake akiwa ameanika miguu mezani. Kama kawaida alikuwa amevalia suti nadhifu na viatu halisi.

“Mkuu, usijali, hili swala lipo mikononi mwangu,” sauti ilisemea simuni.

“Nimekuuliza, umefanya nini William, sijataka soga zako!” alifoka Ian, basi mtu yule ndani ya simu akamweleza kinagaubaga kile alichokifanya. Ni namna gani ambavyo amepandikiza ugumu kwenye kesi ya bwana James Peak kwa ajili ya kumshinikiza mpelelezi huyo aachie kesi.

“Nina uhakika,” sauti ilisema simuni, “baada ya tukio hili atakuwa na maulizo sana kichwani na moja kwa moja atamhisi Marshall, hapo sasa ndipo wakati wetu wa kummaliza kabisa kwa mpango wa pili.”

“William,” Ian akaita kisha kuuliza, “ukishamaliza kupanga ya huyo mtu, unakuja lini kupanga ya kumpata mtu ambaye ndiye lengo letu?”

“Usijali, mkuu, naamini katika mipango hii jamaa huyo ataibuka,” akaeleza William.

“Una uhakika gani?”

“Ninaamini hilo, mkuu. Haitachukua muda kabla ya Marshall kuanza kuja kwenye njia ya bwana James. Hatoweza kuacha roho ya Katie iende pasipo kudai.”

Bwana Ian Livermore akashusha pumzi ndefu alafu akasema, “Omba mpango huo utimie, la sivyo…” akakata simu na kubamizia mezani kama ilivyo ada.

**

Charles Smith alitabasamu akimtazama Danielle. Mwanamke huyo alikuwa amesimama kizimbani akiwa anatetea hoja yake ya kutokuhusika na mawasiliano na mtuhumiwa wa mauaji lakini pia mtoro wa gereza, bwana Marshall.

Bwana Charles, mwanasheria wa Danielle, hakuwa na hofu usoni mwake. Alikuwa ameshatimiza jukumu lake la kumtetea mteja wake kwa kila njia awezayo na kwa hoja alizotoa, ni bayana aliona wingu la neema likiegemea kwao.

Alimchakaza vibaya mwanasheria wa serikali na kumfanya ajione mtupu mbele ya hadhira. Hakukuwa na shahidi bali madhanio yasiyo na vielelezo.

Basi baada ya hakimu kupata mapumziko mafupi ya uchambuzi, sasa alikuwa tayari amezama ndani ya chumba kutoa hukumu. Bwana Charles alimtikisia kichwa Miss Danielle na kumwonyesha ishara ya ngumi kwani kidogo mwanamke huyo alionyesha mashaka usoni mwake.

Mara kadhaa alikuwa anamtazama bwana James Peak na kukutana naye macho kwa macho. Moyo wake haukuwa kwenye mapigo ya kawaida.

Utulivu ukameza mahakama na sasa hakimu akashika hatamu kutoa hitimisho. Kheri Miss Danielle akakutwa hana hatia na kwa neno la mahakama ikaamriwa mwanamke huyo asafishwe na pia alipwe fidia kwa usumbufu na kuharibiwa taswira yake kwenye jamii!

Danielle akafurahi sana. Akamkumbatia bwana Charles na kumbusu kama shukrani lakini kwa upande wa bwana James ukawa ni majonzi. Bwana huyo alikuwa ameinamisha kichwa chake chini akiwa amekubali kuhadhirika lakini pia akiwa anajihisi mkosefu sana kwa kuitia hasara serikali.

Alinyanyuka akakusanya vitu vyake na kuondoka kwa kasi. Miss Danielle akamtazama mwanaume huyo akitokomea kama kimbunga. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kutabasamu na kutabasamu.

Lakini mwanamke huyo ingali akiwa hapo mahakamani alipata kumwona mwanaume ambaye alimtilia mashaka. Mwanaume huyo alikuwa amekaa kwenye viti vya nyuma akiwa amevalia miwani na ‘earphone’ nyeupe masikioni. Alikuwa ana nywele ndefu na kwa kipindi chote kesi ilipokuwa inaendelea hakupata kunyanyua uso wake.

Miss Danielle alimtazama bwana Charles na kumwambia amngoje kwani kuna mtu anataka kuongea naye. Aliporudisha uso wake kuangaza, hakumwona mtu huyo tena.

Alikuwa amepotea machoni.

**
 

Similar Discussions

10 Reactions
Reply
Back
Top Bottom