Nyuma yako (Riwaya ya S. Mollel)

*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 03*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Mara nikajikuta nikipiga magoti na huku kichwa kikinizunguka kana kwamba pia. Sikuweza kusimama japo nilijitahidi. Macho ni kama yalijawa na ukungu, hayakuwa yanaona vema. Nilihii misuli yangu inasinyaa kudhoofika.

Kwa mbali nilisikia kishindo cha mtu kikinijongea na kukomea mbele yangu kisha sauti ya mtu ikininong’oneza, “Umekwisha, Marshall.”

Baada ya hapo nikadondoka na kupoteza fahamu kabisa. Nilikuwa kizani nisielewe chochote kile!

ENDELEA

Sikuwa najua nini kiliendelea mpaka pale nilipokuja kuamka majira fulani nikiwa nipo ndani ya chumba chenye ukubwa wa wastani kikimulikwa na taa. Nilikuwa juu ya kitanda chembamba kigumu chenye kulialia. Mbali na hivyo ndani ya chumba kulikuwamo na viti vitatu vilivyojaladiwa na saruji sakafuni. Viti hivyo vhyote vilikuwa vinatazamana na kitanda nilichokuwa nimelala.

Nikajaribu kuamka na kuketi. Kichwa kilikuwa kinaniuma na macho yangu bado hayakuwa na uwezo wake kamili. Yalikuwa yanarembua yakiwa yanaona kiza.

Nilipotulia hapo kwa kama dakika mbili, nikaendelea kuangazaangaza ndani ya chumba hicho. Nikabaini kuna kamera moja ambayo ipo juu kabisa ya kona ikin’tazama. Nilipojaribu kusogea, kamera hiyo ikasonga pia.

Nikiwa naitazama, nayo ikan’tazama. Nikatazama mlango wa chumba hicho, ulikuwa ni wa chuma usio na cha kufungulia kwa ndani. Nikajaribu kusimama niuendee. Niliposimama nikajihisi mdhaifu sana.

Nilijaribu kupiga hatua na namna ambavyo nilikuwa sioni vizuri, nikashindwa kutengemaa. Nikaketi kitandani na ndani ya muda mfupi nikasikia mlio wa ‘beep’ na mara mlango ukafunguka, wakaingia wanaume watatu. Mmoja nilimwona akiwa amebakia nje.

Miongoni mwa watu hao walioingia, alikuwa ni bwana yule Rodney Rufus. Niliweza kumkubuka upesi ila wale aliokuwa anaongozana nao, yaani wawili aliozama nao ndani, sikuweza kuwatambua. Mmoja alikuwa amebebelea bunduki ya kisasa kabisa yenye asili ya kirusi, Saritch 308, mwingine akibebelea ‘briefcase’.

Kwa wakati huo sikuwa naijua ile bunduki ni ya aina gani kwani sikuwa na kumbukumbu za aina hiyo.

Bwana Rodney akajongea karibu yangu na kuketi kwenye kiti cha katikati ya vile vingine, wale wanaume wengine wakisimama na silaha zao. Bwana huyo akan’tazama na kuniuliza,

“Unaendeleaje?”

Sikumjibu. Swali lake lilikuwa ni utani kwangu. Ni wao ndiyo walionchoma sindano, watashindwaje kujua najisikiaje? Nikamtazama na kumuuliza, “Mnataka nini kwangu?”

Akatabasamu.

“Mbona una haraka sana, bwana Marshall?” akauliza akikumbatisha mikono yake mapajani. “Marshall, hakuna chochote tunachotaka kutoka kwako bali ukweli na kukiri kwako tu. Kwanini ulijaribu kumuua Raisi? Ulikuwa unamtumikia nani?”

Nikamtazama bwana huyo na kumkazia macho, “Bwana Rodney,” nikamwita na kusema, “Nikuambie mara ngapi kuwa sijui chochote unachokiongea? Sina haja ya kumuua Raisi, ya nini nifanye hivyo? Kwa faida gani?”

“Ni nini ulikuwa unafanya nchini Ujerumani mbali na kazi uliyotumwa?” akauliza bwana Rodney. Nikiwa namtazama pasipo kupepesa, nikamwambia hakuna chochote ninachokumbuka isipokuwa niliachiwa na wabwana walioniteka na kufuta kumbukumbu zangu kichwani, hivyo siwezi kuafiki jambo ambalo sina uhakika nalo.

“Bwana Rodney, kwanini usingefanya jitihada za kuwatafuta wale walionikamata na kuwafanyia mahojiano? Huoni ingekuwa kheri kwako na kwangu pia?”

Niliposema hayo, bwana Rodney akachukua briefcase toka kwa yule mwanaume aliyekuwa amelibebelea alafu akafungua na kutoa karatasi kama nne hivi, akanikabidhi.

Nilipozitazama karatasi hiyo nikaona picha za ile klabu ambayo nalikuwa nafanya kazi papo kama mlinzi. Bwana Rodney akauliza, “Unapafahamu hapo, si ndio?”

“Ndio, napafahamu,” nikamjibu.

“Wanafanya biashara gani?” akaniuliza tena akiwa anan’tazama kwa umakini.

“Wanaendesha klabu ya usiku,” nikajibu na kukomea hapo.

“Na kipi kingine?” akauliza Rodney na punde akatoa karatasi zingine na kunikabidhi. Mara hii nilipotazama nikaona picha zangu nikiwa kwenye ile ‘trip’ pamoja na meneja. Picha hizo zilionyesha namna nilivyokuwa nangozana na meneja kuzama jengoni.

“Na huko ulienda kufanya makubaliano gani?” Rodney akauliza. Asiningoje nijibu, aakafunga briefcase lake na kuniambia kuwa wanajua kila kitu ambacho nilikuwa nafanya nchini Ujerumani. Namna gani ambavyo nalikuwa nafanya biashara ya madawa na hata kuua watu.

Kama haitoshi kwa vielelezo zaidi, akaniambia wana rekodi zangu zote za simu, kwa njia ya mwito na ujumbe kuwa nilishiriki kupanga kumpoteza na kumuua Raisi.

Alimionyesha simu akiwa anasema hayo.

“Kwahiyo kuanzia sasa, wewe na meneja wako wote mpo chini ya ulinzi mkali. Lakini pia na wale wote uliokuwa unashirikiana nao ulipokuwa nchini Ujerumani. Sikia Marshall, hauwezi kutoka kwenye hili. Ni bora ukaonyesha ushirikiano wako kama majuto kwa ulichokifanya kwa taifa kubwa duniani.”

Aliposema hayo akan’tazama kwa kama sekunde tatu pasipo kunena kitu. Nami nilinyamaza maana sikuwa namwelewa wala kuona kama anataka kunielewa.

Aliniuliza, “Upo tayari kuyamaliza haya?”

Nikamjibu siko tayari kumaliza kitu ambacho sijakianzisha, basi akatabasamu na kusema dawa yanu ipo jikoni. Akatia mkono wake wa kuume mfukoni kisha ule wa kushoto ukamgusa yule mwanaume mbeba briefcase huku akiuendea zake mlango.

Mara nikamwona mwanaume yule mwenye briefcase akitoa sindano ndani ya briefcase na kuitazama. Sindano hiyo ilikuwa na kimiminika rangi ya karoti iliyokoza. Akaweka briefcase chini na kujiandaa kunichoma.

“Hey hey!” nikawahasa, “ngojeni tafadhali! Ngojeni!”

Hawakunijali, nikamwona yule mwanaume mwenye sindano akinijongea zaidi. Nikajaribu kupambana lakini nikaiishia kuchapwa teke zito lililonilaza kitandani. Sikuwa najiweza kabisa.

Basi bwana yule akan’toboa mkono wangu wa kuume na kunizamishia kimiminika ndani ya sindano. Sikuwa naelewa kitu kile kilikuwa ni dawa ama sumu. Nilijihisi baridi la ajabu mpaka nikitetemeka.

Kwa mbali niliwasikia watu wale wakiondoka na kufunga mlango. Baada ya muda mwili wangu ukarudi kwenye joto la kawaida lakini bado nikijihisi si mzima. Basi nikajikunyata na punde nikazamia gizani.

Sifahamu nilikuja kuamka baada ya masaa mangapi. Nilikuwa nahisi njaa sana.

Nilipoketi kitandani nikabaini kuna sinia ya chakula mbele kidogo ya kitanda. Kwa pupa nikawahi sinia hilo na kufakamia. Sikuwa na uhakika nilikaa siku ngapi pasipo kula. Ile njaa haikuwa ya siku moja.

Hata majira yenyewe nilikuwa siyafahamu. Taa zilikuwa zinawaka tu. Hamna hata dirisha la kukufanya uone ya huko nje.

Nikala na nilipomaliza ndipo hata nikahema na kugundua kulikuwa na chupa ya maji pia kando na mguu wa kitanda. Nikanywa maji na kujilaza kitandani. Hapo ndipo nikawaza kile chakula kitakuwa kililetwa muda gani maana hakikuwa na joto lolote lile. Kilikuwa cha baridi sana, kama si njaa zangu basi nisingehangaika nacho.

Kama baada ya masaa matatu, wanaume wawili wakaja ndani ya chumba changu na kunidunga sindano tena. Ratiba hiyo ikaendelea kwa kama juma moja mfululizo.

Lakini kadiri muda ulivyokuwa unaenda, nikabaini najiwa na nguvu na pia kumbukumbu zangu zaanza kujiunda upya kichwani.

Kuna muda nilikuwa naota mambo niliyowahi kuyafanya kazini. Baadhi ya maeneo na pia watu. Nilijihisi ajabu mwanzoni lakini nikaja kuona kawaida hata nikapatwa na hamu sana ya kujifahamu.

Siku moja punde tu baada ya kuamka, nikaona bahasha ya kaki juu ya kiti. Niliijongea bahasha hiyo na kufungua nijue kilichomo ndani.

Nilipochana na kutazama nikaona picha za mtu mwenye kuvalia miwani. Kwa namna ambayo siifahamu, nikajikuta nasema, “Jack … Jack Pyong!”

Nalikuwa nimemkumbuka rafiki yangu! Nikahisi furaha sana lakini haikudumu kwa muda. Nilijiuliza ni nini kitakuwa kimemtokea kama mimi nipo mule ndani chini ya watu?

Je atakuwa salama?


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 04*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Nilipochana na kutazama nikaona picha za mtu mwenye kuvalia miwani. Kwa namna ambayo siifahamu, nikajikuta nasema, “Jack … Jack Pyong!”

Nalikuwa nimemkumbuka rafiki yangu! Nikahisi furaha sana lakini haikudumu kwa muda. Nilijiuliza ni nini kitakuwa kimemtokea kama mimi nipo mule ndani chini ya watu?

Je atakuwa salama?

ENDELEA

Lakini nikajikuta pia nikiwaza kwanini watu wale waliamua kun’letea picha ya Jack Pyong? Lengo lao lilikuwa ni nini haswa? Kama haitoshi siku iliyofuata wakaniwekea na picha ya nyumba yangu pamoja pia na picha kadhaa nilizokuwapo kazini.

Kadiri nilivyotazama hizo picha kumbukumbu zangu zikawa zinanijia taratibu. Nikaanza kupata afya ya kichwa na hatimaye nilipokuja kuona picha ya kisiwa nilichoenda mwanzoni wakati napambana kumtafuta Raisi, pia na za Miss Danielle James, kumbukumbu zangu zikanikaa sawia kwa kiasi kikubwa.

Nadhani ndilo lilikuwa lengo la wale watu kuniletea picha hizo. Wanikumbushe yale yote niliyoyapitia. Lakini bado kwenye kumbukumbu zangu hakukuwa na mahali ambapo nilikumbuka nikimteketeza Raisi? Mbona nashutumiwa kwa hilo?

Nikawaza nisipate majibu.

Nikiwa katika hali nzuri sasa hata ya kimwili mbali tu na kiakili na kumbukumbu, picha ya mwisho kuletewa ikawa ya Henessy na Britney. Nilitazama picha hizo na kukumbuka kila tone ya jambo. Nikajikuta nikijawa na hamu kubwa ya kujua wapi alipo Henessy.

Nilipanga bwana Rodney atakapokuja anieleze kuhusu jambo hilo.

Siku inayofuata, bwana Rodney akafika ndani ya chumba changu nilimofungiwa na kama kawaida akiwa ameongozana na watu wawili waliobebelea silaha. Aliketi na kuanza kuniuliza maswali juu ya hali yangu.

Alipomaliza kuhusu hayo akasema, “Vipi umekumbuka uliyoyatenda?”

Nikamwambia nimekumbuka kila lililo jema ambalo nimeshiriki kwa moyo wangu wote, nguvu na akili zote lakini hakuna mahali ambapo naliona kuwa nimehusika kumpoteza Raisi.

Niliposema hivyo, akakuna kideu chake kikavu akin’tazama. “Bwana Marshall, nadhani haujakumbuka vema. Itabidi tuendelee na dozi!”

Nikatahamaki, “Unataka nikumbukeje kitu ambacho sijakifanya?” nikiuliza hilo nilitoa macho kumkazia. “Sijashiriki kufanya lolote lile baya juu ya Raisi. Sawa?”

Hakusema jambo kwa sekunde mbili. Akafyatua nne yake ya miguu na kuuliza, “Miongoni mwa picha nilizokupatia, kuna wapendwa wako, sio?” kabla sijajibu akaendeleza maneno, “sidhani kama utakuwa radhi kuwapoteza. Lakini naona kwa ukaidi wako huko ndipo unaelekea.”

Nikamuuliza, “Una maanisha nini?”

“Namaanisha kwamba ukumbuke. Kumbuka wewe mpumbavu!” alisema sentensi yake ya pili kwa sauti ya juu. Nikamtazama nikiwa najiuliza kichwani. Kuna kitu kilisumbua ubongo wangu.

“Bwana Rodney, kitambulisho changu cha kazi huwa natembea nacho muda wote. Nilikipoteza wakati natekwa na wale watu waliofuta kumbukumbu yangu. Unaweza kuniambia ulikipatia wapi?”

Akatabasamu pasipo kunipatia neno.

“Ulikuwa unajua kama nina tatizo la kupoteza kumbukumbu zangu, si ndio?” nikamtazama naye akan’tazama. Akatikisa kichwa na kusema, “Ndugu, sijaja hapa uniulize maswali bali ujibu maswali yangu.”

Lakini sikujali sana kauli yake. Nalikuwa namtazama nikijaribu kukumbuka mambo kichwani. Ajabu kila nilipojitahidi kukumbuka kama nilishawahi kumwona bwana yule machoni, yaani Bwana Rodney, akili yangu haikukubali kabisa. Alikuwa ni mgeni kwenye mboni zangu.

Inawezekanaje nisimjue mtu huyo kama atakuwa ametokea makao makuu ya CIA. Kuna mtu nisiyemfahamu mule? Ndiyo huenda kuna watu wengi ila mpaka mtu kukabidhiwa majukumu kama yale, si haba. Atakuwa ni mtu mwenye nyadhifa. Mbona sasa ni mgeni kwangu?

“Bwana Rodney, sidhani kama wewe ni afisa CIA. Unafanya kazi USSS?” Akatabasamu tena. Kabla hajatia neno, nikaongeza, “Lakini ninyi USSS mlizuiwa kuhusika na hili kwasababu za kiuwajibikaji.”

“Mimi sio USSS!” Akafoka. Alikuwa anan’tazama kwa macho ya kutisha lakini nisijali sana. Kuna vitu vingi vilikuwa vinaendelea kichwani mwangu. Nilikuwa nahangaika sana kuunganisha matukio yalete maana.

“Unamjua Ian Livermore?” nikamuuliza kumhusu yule ajenti wa USSS ambaye alilaghai kufia kwenye ajali ya moto wa nyumba yake. “ … ndiye aliyekupa hiyo dawa ya kumbukumbu?” nikaendelea kumjaza maswali. Nilipotelea fikirani. Kwa muda kidogo nilikuwa na ‘enjoy’ namna ambavyo akili yangu iliweza kuyakumbuka yote hayo kwa wepesi.

Namna ambavyo napata uwanja mpana wa kuhoji na kufuatilia. Si bure wale maadui walifanya namna kunifuta uwezo wangu wa kukumbuka. Walikuwa na dhamira kubwa.

“Rodney, mlinifuta kumbukumbu ili mnipandikizie hili unalotaka nilikumbuke?” nikauliza. Hapo bwana Rodney akatoa macho zaidi. “INATOSHA! SITAKI KUSIKIA UPUMBAVU WAKO!” akasimama na kuzamisha mkono wake mfukoni. Sikujua anatafuta nini. Nikiwa namngoja atoe akitoacho, nikajikuta natokwa na swali,

“Yu kwapi Henessy?”

Upesi akachoropoa mkono wake mfukoni na kunitupia picha akisema, “Sasa ni juu yako. Ufanye ninachokuambia ama nimmalize!”

Nilipotazama picha ile nikamwona Katie.

“Hiyo ni picha yake ya jana akiwa anatembea katika jiji la Berlin. Unadhani tusingeweza kumpata tena!” alibweka Bwana Rodney. Nikamtazama na kung’ata meno yangu.

“Mkidiriki kumgusa kwa namna yoyote ile, nitakufanya ujutie kuzaliwa,” nikamweleza nikikunja ndita, ajabu akacheka.

“Kama unampenda huyo malaya wako, basi fanya ninachokuagiza. La sivyo! …” akanionyesha ishara ya kukata shingo akiwa ametoa macho, “Nammaliza!” akasema na kwenda zake akitembea kwa upesi.

Sikumwona tena mpaka baada ya kama siku mbili, ambapo siku hiyo niliyomtia machoni alikuwa akiongozana na mwanamke aliyemfunika kichwa na mfuko mweusi wa kitambaa na mikono yake wamemfunga nyuma ya mgongo. Mwanamke huyo alikuwa amevalia suruali ya kumbana na topu rangi ya kijivu.

Kwa kumtazama tu nikambaini ni Katie!

“Kaa chini!!” aliniamuru mlinzi aliyeongozana na Bwana Rodney. Alipayuka vivyo wakiwa wameninyooshea bunduki. Nami nikatii nikiwa namtazama Katie kwa mashaka.

“Leo utasema ni njano ama nyekundu!” akafoka Rodney. Akamvua Katie kitambaa cheusi kichwani na kusema, “Utafanya kwa njia yetu ama yako!”

Katie alikuwa amefungwa mdomo kwa kamba iliyotanua kingo za mdomowe. Alikuwa amejawa na woga na macho yake yakiwa mekundu yanatiririsha machozi. Alikuwa analia na kitu hicho kiliniumiza sana.

Yule bwana aliyekuwa amemshika Katie, akamsukumia mwanamke huyo kwanguvu kuja kwangu, nikawahi kumdaka, na nilipowatazama nikawaona wakijiendea.

Nikamfungua Katie kamba ya mdomoni na mikononi. Nikamkumbatia kwanguvu na kumuuliza juu ya hali yake. Alikuwa analia sana hawezi hata kuongea akaeleweka.

“Usijali, Katie,” nilimtoa hofu. “Utakuwa sawa, mpenzi. Usijali,” nilisema nikimkumbatia. Alilowaniha bega langu kwa machozi.

“Nilikuambia uwatazame kama wanakufuata,” nikamwambia nikiwa namtoa begani na kumtazama. Nilimwonea huruma kwa anayoyapitia. Lakini pia nikajikuta nikijichukia kwa kujiona sababu ya kumzamisha kwenye dimbwi la matatizo.

Nikamwomba samahani sana lakini nikamwahidi kumaliza kila kitu.

Hatujakaa sana, wale mabwana wakarudi na kumchukua Katie. Bwana Rodney akan’tazama na kuniuliza,

“Amekuambia kila kitu?”

Nikamtazama kwa hasira nisiweze kusema jambo. Akatabasamu na kuniuliza, “Amekuambia kama ana mimba changa?”

Kauli hiyo ikanishtua, Bwana Rodney aliliona hilo, akatabasamu zaidi na kupeleka kichwa chake pembeni. “Sasa ni juu yako. Sawa bwana mdogo?” akasema na kunipa mgongo aende.

Nikajikuta nasema,

“Nitafanya mtakacho!”

Akageuka akionyesha meno yake kwa furaha.

“Sasa umekua,” akasema akipiga makofi. Nikamsisitiza,

“Tafadhali, msimfanye chochote huyo mwanamke.”


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 05*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Nikajikuta nasema,

“Nitafanya mtakacho!”

Akageuka akionyesha meno yake kwa furaha.

“Sasa umekua,” akasema akipiga makofi. Nikamsisitiza,

“Tafadhali, msimfanye chochote huyo mwanamke.”

ENDELEA

Hakusema jambo, akaenda zake. Lakini kabla hajafunga mlango na kupotea kabisa, akan’tazama tena na kutabasamu. Alinifanya nijiulize maswali kichwani mtu yule alikuwa ni nani haswa na ni nini alikuwa anataka kwenye yale yote. Wana malengo gani na kipi haswa watanufaika na mkakati huo?

Basi nikajikuta najiuliza pasi na kikomo. Sikutaka kabisa Katie ahusishwe na hili jambo lakini nilikuwa nimeshakawia. Sikuwa na la kufanya.

Sikuwa na budi bali kungoja kile ambacho wataamua watesi wangu.

Ikiwa kama masaa matatu yamepita, wakaja wanaume wanne waliobebelea silaha na kuniamuru niwafuate. Waliniveka pingu mikononi na kamba ya minyororo miguuni.

Nikaongozana nao mpaka nje, wakanipakiza kwenye ‘karandinga’ lenye rangi ya manjano na kisha safari ikaanza ya kwenda nisipopajua.

Ndani ya basi nilikuwa mwenyewe tu, lakini ulinzi mkubwa. Nilitazama madirishani kukagua mazingira. Kulikuwa ni mchana jua lawaka. Nilipokuwa mule ndani nilidhani ni usiku ama jioni. Nilikuwa nimekosea.

Kwa muda kidogo nikajikuta nikifurahia kutoka ndani ya chumba kile. Ama hakika ni kheri kurogwa kuliko kukoa uhuru. Nilitazama namna ambavyo miti ikipishana na basi kwenda nyuma.

Nilitazama ndege wakipaa na mawingu yakijichanua. Hakika ilikuwa inapendeza. Sina namna ya kushukuru vitu hivyo kwa kunipotezea msongo wa mawazo. Akili yangu ilipumzika.

Tulikatiza uwanda wa milima na miti mirefu na mifupi. Muda mwingine tukiivuka milima ama kuikwepa. Laiti kama nisingalikuwa kifungoni, ilikuwa ni safari ya aina yake.

Niliporudisha macho yangu ndani ya basi, ndipo nikarejea kwenye uhalisia wangu unaouma. Nilikuwa kifungoni. Nilikuwa sina uhuru.

Nikawatazama wale watu wanaoongozana na mimi. Walikuwa wamevalia sare za bluu nyeusi, vichwani wamejibandika kofia ‘kapelo’. mikononi mwao wamebebelea bunduki nzito. Ni kana kwamba wanamsafirisha gaidi.

Sikuwahi kuwaza kama kuna siku nitajikuta kwenye mazingira kama hayo kwa asili ya kazi yangu. Basi jambo hili likanikumbusha mbali sana, sikuwa na uhakika kama ilikuwa ni miaka mitatu ama miwili huko nyuma.

Siku hiyo ilikuwa imetingwa sana na kazi, ambapo sisi maajenti wa CIA kwa kushirikiana na FBI tulikuwa tumelazimika kumsindikiza gaidi mmoja wa ki - Thailand aitwaye Sam Jaa.

Alikuwa ni ‘teenage’ mwenye kujawa na michoro mgongo mzima. Alikuwa amekuja Marekani kama mtalii lakini mwenye adhma ya kufanya tukio moja kubwa la kigaidi.

Akiwa amefika hapa nchini, kwa takribani baada ya juma moja, akaanza kufanya kazi yake kwa weledi. Hakuwa ameingia na chochote kile isipokuwa kitambulisho chake cha kughushi, pasi ya kusafiria, vitabu viwili vya riwaya, pesa ya mahitaji na nguo mbili za kubadili.

Ilikuwa ni ajabu kwa namna Sam alivyokuwa ana ujuzi mkubwa wa kutengeneza silaha kwani alitumia vitu vya kawaida kabisa alivyokuwa anavinunua madukani na mahali pengine, vitu ambavyo haviwezi kumfanya mtu amuwazie kwa ubaya, mathalani mafuta ya taa, viberiti, dawa za mbu, unga wa baruti, betri za magari na kadhalika, napo akivinunua kwa mipango.

Baada ya kukusanya vitu hivyo kwa takribani miezi miwili, akaanza kuvifanyia kazi kwa kuviunda kwa pamoja, kazi ambayo ilimchukua takribani mwezi mwingine kamili.

Kitu ambacho kilimfanya Sam aanze kutazamwa kwa jicho la mazingatio ni pale siku moja alamanusura achome makazi yake kwa moto wakati alipokuwa anafanya moja ya majaribio yake.

Ni kheri aliwahi kuuzima moto kwa kutumia ‘fire extinguisher’ lakini harufu ya moto na taharuki vilikuwa tayari vimeshatapakaa. Mwenye nyumba akamwonya na kumtoza faini ambayo alistaajabu kijana huyo akiitoa kwa cash toka kabatini, lakini mbali na hapo akiwa ameona baadhi ya vitu ambavyo vilimpa mashaka.

Alitoa taarifa kwenye mamlaka na ndipo Sam akaanza kufuatiliwa kwa ukaribu. Ajenti wa FBI wakagundua kijana huyo alikuwa akienda kwenye ‘subway’ na kuzurura humo kwa takribani masaa kisha akitoka.

Alikuwa akifanya vivyo kila baada ya siku tatu. Ilipofuatiliwa akaunti yake ya benki, wakabaini alikuwa akitumiwa kiasi kikubwa sana cha pesa kila juma na mtu ambaye yu nchini Thailand. Na hapo ndipo sisi kama CIA tukaagizwa tukafuatilie hilo.

Ikiwa ni siku ya jumapili, naam nakumbuka hiyo siku, ajenti wa FBI wakaenda kwenye makazi ya Sam ili wapate kumtia nguvuni. Walipofika huko, hawakumkuta, chumba kilikuwa kitupu na ukutani akiwa ameandika kwa ki - Thailand, ‘Mmechelewa kidogo’, akiwa ametumia spray ya rangi.

Basi haraka taarifa zikatoka kuamrisha watu wote watoke kwenye subway kwani kuna dharura. Polisi wakamiminika maeneo hayo na kuwasihi watu wote watoke nje kwasababu za kiusalama. Na taarifa za kuuzuia usafiri huo zikatolewa na watu wakazitii.

Ajenti wa FBI pamoja pia na polisi wakazama kwa wingi ndani ya subway kumsaka bwana Sam. Wataalamu pia wa kufyatua mabomu wakaongoza njia wakikagua ni wapi ambapo Sam atakuwa ameweka milipuko yake kuwamaliza watu.

Walipofanya msako kwa kama lisaa limoja wasipate matunda ndipo ajenti Danielle James akabaini kuwa Sam hakuwapo humo, kwa kutumia kamera zilizokuwa zimetundikwa kwenye eneo husika, tena kwa macho makini sana.

Kumbe Sam alibadili nguo kwa takribani mara nne akiwa maeneo tofauti tofauti ya lile eneo. Ni wazi Sam alikuwa ameshajua kila sehemu ambapo kulikuwapo na kamera hivyo akajifunza namna ya kuzilaghai.

Lakini baada ya hilo kugundulika, ndipo kidogo tu maajenti pamoja pia na maafisa polisi wakabaini hakukuwa na vifaa vyovyote vya milipuko vilivyopandikizwa kama walivyokuwa wanadhani. Sam alikuwa amewachezea akili.

Lakini waliligundua hilo kwa namna ya ajabu kidogo. Afisa mmoja wa polisi alikohoa mpaka kutoa matone ya damu, alipowatarifu wenzake nao punde wakaanza kuhisi mapafu yanawabana wakihema.

Kumbe Sam alikuwa amechafua hali ya hewa kwa kujaza sumu, na ‘target’ yake ikiwa ni wanausalama ambao aliwapata vema pasipo kutoa jasho.

Walimfuata yeye.

Walijipeleka kifoni.

Mara karandinga likasimama na kun’toa mawazoni mwangu. Nilipotazama mbele yangu nikaona jengo moja kubwa lakini lenye kupeperusha bendera ya Marekani. Hapo nikashushwa na kuzamishwa humo ambapo punde nilionana na watu ambao walinilisha maneno mdomoni mwangu na kunipa pia nafasi ya kuonana na Katie.

Nikiwa natiririsha machozi, nikamwambia Katie kwa upole, “Uwe unakuja kun’tembelea gerezani.” kisha asikae sana akachukuliwa na mimi nikazamia kizani.

Ikachukua siku mbili tu, nikawa nimepandishwa kizimbani nikituhumiwa kwa uhaini. Siku hiyo nikaona vyombo vya habari vingi vikiwa hapo kushuhudia.

Kuja kuona ni kipi watakipata kwenye vyombo vyao vya habari kwa ajili ya wateja kesho.

Lakini pia nikamwona bwana Ethan Benjamin, Inspekta general wa CIA, pamoja na maajenti kadhaa. Kidogo nikamwona pia Jack Pyong akiwa ameongozana na Miss Danielle James, ajenti wa FBI niliyekuwa nafanya naye kazi kwenye kesi ya Raisi.

Ulipopita muda kidogo nikamwona pia Kelly. Alikuwa amekuja kwa kukawia. Alitazama saa yake akiketi. Alin’tazama kwa mashaka sana uso wake ukiwa umwenywea. Hata nilipomtazama Jack naye alikuwa akin’tazama katika namna ya kuninyong’onyesha. Sikutaka kumtazama zaidi kwani ningeshindwa kuzuia chozi.

Muda si mwingi, kukaombwa utulivu na kesi ikaanza kusikilizwa. Sikutaka mambo yawe mengi. Akilini mwangu nilikuwa namuwazia Katie na usalama wake, lakini pia na usalama wa mtoto ambaye amembebelea tumboni.

Nilikuwa na mambo mengi kichwani na niliona kama kuwapo pale kulikuwa kunanipotezea muda.

Nilipoulizwa kama nakiri kosa lililonileta pale mahakamani, moja kwa moja nikajibu ndio. Kidogo umati ukashangazwa na hilo, haswa Jack Pyong na wenzake niwajuao.

Basi hakimu pasipo kusita akanihukumu kifo, nami nikainamisha shingo yangu kutazama chini.

Niliona yamekwisha.


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 06*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Nilikuwa na mambo mengi kichwani na niliona kama kuwapo pale kulikuwa kunanipotezea muda.

Nilipoulizwa kama nakiri kosa lililonileta pale mahakamani, moja kwa moja nikajibu ndio. Kidogo umati ukashangazwa na hilo, haswa Jack Pyong na wenzake niwajuao.

Basi hakimu pasipo kusita akanihukumu kifo, nami nikainamisha shingo yangu kutazama chini.

Niliona yamekwisha.

ENDELEA

Baada ya siku tatu, ndani ya gereza, Louisiana State Penitentiary …

Nilikuwa ndani ya chumba changu chakavu nikifikiria baadhi ya mambo kichwani. Sikuwahi kuwaza kama siku moja n’takuwa ndani ya gereza tena kwa kosa kama lile nililohukumiwa. Ilikuwa inaniumiza moyo wangu. Kuna muda nilikuwa nasahau kama nipo kifungoni. Uhalisia ulikuwa unauma mno.

Katika gereza hili, wafungwa wengi walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha, na wengine wakingoja adhabu yao ya kifo ikiwamo mimi. Gereza hili lilikuwa lina uwezo wa kutunza watu takribani 6,300, na kutokana na urefu wa vifungo vya watu ambao walikuwa wanaishi humo iliwalazimu kuweka huduma ya hospitali na matatizo ya akili.

Ni moja ya gereza kubwa mno ndani ya nchi likiwa na vitengo mbalimbali. Kitengo chetu cha watu wanaosubiriwa kuuawa kilikuwa kimejitenga mbali kidogo na vitengo vingine kama vile wafungwa wa kawaida. Na kwa upande wetu utaratibu ulikuwa ni wa tofauti na wenzetu.

Mosi, wafungwa wanaongoja hukumu ya kifo kwa siku hupewa lisaa limoja tu nje ya vyumba vyao. Lisaa hilo ndilo linahusisha kuoga, kufanya mazoezi, kukaguliwa na kuongea na wageni mara moja moja.

Mfungwa huwa amefungwa pingu muda wote, isipokuwa akiwa anaoga, akiwa chumbani mwake au akiwa kwenye uwanja wa mazoezi.

Fikiria upo ndani ya chumba kimoja chenye urefu wa futi nane kwa kumi kwa masaa ishirini na tatu. Humo ukitazamana na kitanda chako chembamba, choo na sinki. Si bure wengine huwa wanachanganyikiwa wakiwa wanangoja hukumu zao za vifo. Huwa na hasira kupita kiasi hata kufanya vurugu kujiumiza.

Ni nini utaogopa kufanya ukiwa unajua unavuta pumzi yako ya mwisho?

Pili, wafungwa wanaongoja hukumu zao za vifo uhesabiwa karibia mara mbili ndani ya lisaa limoja. Mara nyingine yakupasa uamke hata ukiwa usingizini ili uhesabiwe. Ni kawaida mara kadhaa lango kugongwa kwanguvu na kumulikwa machoni ukiamriwa uamke uhesabiwe.

Kama haitoshi, kila kitu kinawekewa mipaka. Tulikuwa tunatakiwa kuoga mara moja tu ndani ya masaa 48. na muda wetu wa kufanya mazoezi ulikuwa ni masaa manne tu kwa juma zima. Eneo la kufanyia mazoezi lilikuwa ni dogo na lenye ulinzi mkali. Muda mwingine mfungwa hukatazwa kufanya mazoezi na mwenziwe kwasababu za kiusalama.

Kuna muda ndani ya vyumba vyetu joto lilikuwa kali mno kuvumilika, karibia hata nyuzi joto tisini. Nilikuwa navuja mno na kupatwa na kiu mara kwa mara. Nilikuwa natamani kupata upepo hata kidogo lakini haikuwa inawezekana. Niliwaza hali ingekuaje endapo majira ya baridi yangefika?

Kuna muda niliona ni bora nikauawa nijue moja kuliko kuendelea kkaa humo. Ilikuwa inashangaza namna ambavyo walinzi wangetutazama kama tupo wazima, sikujua ni ya nini ingali tunaenda kufa, lakini kwa utaratibu haikuwa inatakiwa mfungwa afe kwasababu nyingine yoyote ile, isipokuwa kwa hukumu yake tu.

Baada ya kukaa humo gerezani kwa takribani juma moja, Jack Pyong akaja kun’tembelea gerezani. Tukiwa tumetenganishwa na ukuta wa kioo, nikaongea naye akiniuliza swali la kwanza kabisa kama ni kweli nilifanya kile kitendo ambacho nilikiri mahakamani.

Nikiwa namtazama na huku nimeshikilia simu ninayotumia kuzungumzia, nikamwambia maneno machache, “Unajua uhalisia, Jack.” baada ya hapo nikamwona akidondosha chozi. Alikuwa ananifahamu kiundani. Najua alifahamu kuwa sihusiki na hilo jambo. Hata nilipokuwa nakiri kwangu mahakamani, aliduwaa haswa.

“Najua hilo, Tony,” alisema akishika kioo. Nami nikashika kioo sambamba na mkono wake viganja vyetu vikitazamana.

Japo wote tulikuwa tumeweka viganja hapo, hamna mtu aliyekuwa anauhisi mkono wa mwenzake. Kioo kilikuwa kipana na kigumu. Ni mguso wa kihisia tu ndio ambao tulikuwa tukiupata.

“Kwanini ukafanya hivyo, Tony,” Jack akaniuliza. “Unafanya haya kwa ajili ya nani?” akaongezea.

Nikamtazama pasipo kusema kitu kwa sekunde chache. “Jack,” nikamwita na kumwambia, “Ni habari ndefu.”

“Najua, Tony. Nataka tu kumfahamu aliyehusika. Ni nani?” akauliza kwa mkazo, lakini kabla sijatia neno nikasikia sauti ya kugonga nyuma yangu. Nilipotazama nikamwona askari, alikuwa ananitaka ninyanyuke kwani muda wangu umekwisha.

Alikuwa ananitazama kwa uso mgumu. Macho yake yalikuwa yamepandwa na ndita na mdomo wake akiuvuta.

“Naomba muda kidogo, tafadhali,” nikamwomba.

Hakujali. Alinifuata na kunishika mkono karibia na kwapani akinitaka nisimame. Hakuonyesha kama atanielewa. Ilinibidi nimwage Jack kwa kumpungia kiganja changu kabla hatujaachanishwa kabisa kurudishwa ndani kwenye ngome yangu.

Baada ya hapo siku yangu ikarejea kuwa kawaida kama siku zingine. Siku ngumu na isiyopendeza. Nikiishi kana kwamba nipo jehanamu.

Nikiwa nimejilaza kwenye kitanda changu, ikiwa imepta kama lisaa tangu niwasiliane na Jack Pyon, nikasikia lango likigongwa. Niliporusha macho kutazama nikamwona askari akiwa amesimama hapo akiwa ameshikilia kirungu chake chenye mshikio. Nikadhani amekuja hapo kunihesabu, basi nikasimama na kumsogelea.

Punde nikaona watu wengine watatu ambao niliwatambua kama mafundi. Walikuwa wamevalia sare ‘overall’ rangi ya bluu na buti nyeusi. Wawili walikuwa wamebebelea boksi na mmoja akiwa amebebelea mkebe.

Basi lango likafunguliwa na watu hao wakaingia ndani. Askari akiwa amesimama langoni, mafundi wale wakafanya matengenezo yao kwa muda wa kama lisaa limoja. Walikuwa wamekuja kuunganisha runinga.

Iliwachukua muda kidogo maana nyaya zilizokuwamo ndani ya chumba changu zilikuwa chakavu. Walipomaliza wakajaribisha kuona kama ipo sawa. Waliporidhika wakamtaarifu askari na kisha wakaenda zao.

Wakiwa wanaenda niliwatazama sana watu hao na kwa namna moja nikiwaonea wivu kwa kuwa huru. Wanakuja na kuniacha mule kwenye kiota chenye kutu. Lakini zaidi nikawakagua pasipo haja. Pengine ni kwasababu nilikuwa nimeshazoea mambo hayo, kila kitu nikikitazama kwa umakini.

Walikuwa wamebebelea vitambulisho vyao kwenye mfuko ikiwa mmoja tu ndiye ambaye amekining’iniza shingoni. Walipoongea na askari kidogo basi wakaenda zao wakimwacha askari hapo, askari akafunga lango lile, na kabla hajaondoka akan’tazama kidogo, mtazamo wa kunionya kisha akasema,

“Furahia muda wako!”

Nikampuuzia na kutazama runinga ile iliyokuwa imewekwa mbele yangu. Wamefikiria nini kuniwekea hicho kitu? Nikawaza. Hakukuwa na jambo maalum isipokuwa ni utaratibu wao.

Basi nikaiwasha na kutazama. Ilikuwa inaonyesha. Nikaweka chaneli fulani na kuendelea kuikodolea nikiwa navuta muda wangu. Angalau runinga ile ilinisaidia kunitoa kwenye mawazo ya kila muda.

Nilitazama taarifa ya habari nyakati za usiku kabla ya kulala.

Kesho yake kwenye majira ya mchana, saa nane, nikaja kuitwa nikiambiwa kuna mgeni amekuja kunijulia hali. Nilipoenda kitengoni, nikakutana na Katie. Nilifurahi sana kumwona. Alitabasamu nami nikajikuta nikitabasamu zaidi.

“Unaendeleaje?” aliniuliza kwa sauti yake ya upole. Japo tulikuwa tunatumia simu, nilikuwa naihisi sauti yake kana kwamba ananinong’oneza. Nilitamani sana nimkumbatie na kumwambia kila kitu kitakuwa sawa lakini sikuwa naweza. Hicho kitu kiliniumiza sana.

Niliweka kiganja changu kiooni, naye akakiweka cha kwake akitabasamu kwa mbali, nikamjibu, “Naendelea vizuri,” kisha nikamuuliza, “Vipi wewe mpenzi?”

Naye akanijibu yuko sawa. Baada ya hapo nikataka kujua ni wapi anaishi na kama yu salama huko.

“Nipo South Carolina kwa shangazi yangu,” alinijibu na kisha akanihakikishia kuwa yu salama. “Tangu ulipohukumiwa, sijaonana na wale watu kabisa.”

Niliamini hayo anayonambia maana kazi ya kunimaliza ilikuwa imekwisha. Watu wale hawakuwa wananihitaji tena, nimeshakiri mahakamani na kuhukumiwa kifo. Nadhani walikuwa wamepumzika sasa, ama wakikutana mahali wakinywa na kufurahia ushindi.

Niliongea na Katie kwa kama dakika tatu tu kabla ya kumsikia askari akija kunitoa hapo. Nilimsihi sana aonane na Jack nikimtajia anwani yake, na yeye pia akaniambia atakuwa anakuja kuniona mara kadhaa hapo gerezani.

Siku hiyo nilipoenda chumbani mwangu, sikuwasha runinga kabisa, nikakaa kuwaza sana juu ya Katie na hali aliyomo, alikuwa ananihitaji sana katika muda ule, lakini zaidi nikawazia kumhusu mwanangu endapo Katie atajifungua, masikini hatamwona baba yake. Niliumizwa sana.

Nilishindwa kulala siku hiyo.

Vipi kama kesho ikawa siku yangu ya kuuawa?


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 07*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Siku hiyo nilipoenda chumbani mwangu, sikuwasha runinga kabisa, nikakaa kuwaza sana juu ya Katie na hali aliyomo, alikuwa ananihitaji sana katika muda ule, lakini zaidi nikawazia kumhusu mwanangu endapo Katie atajifungua, masikini hatamwona baba yake. Niliumizwa sana.

Nilishindwa kulala siku hiyo.

Vipi kama kesho ikawa siku yangu ya kuuawa?

ENDELEA

Ili niupate usingizi, ilinibidi nijipe matumaini kuwa Katie atakuwa salama baada ya kuonana na Jack. Nilivuta pumzi ndefu na kujifunika shuka nikijaribu kulala lakini bado mawazo hayakunitoka.

Baada ya kama lisaa limoja baada ya kuamua kuwa Katie atakuwa vema, nikaanza kuuonja usingizi kwa kurembua, lakini napo usikae, nikasikia mtu akigonga mlango na kunisihi ninyanyuke. Alikuwa ni askari amekuja kutuhesabu.

Basi sikuwa na jinsi nikasimama na kumtazama askari huyo. Alinimulika usoni na kuniambia nitanue kinywa, nikatii. Kabla hajaondoka akaniuliza maswali mengine juu ya hali yangu. Aliponiuliza kama nimekula siku hiyo, nikiwa nimechoshwa na maswali yake yasiyokoma, nikalipuka na kumjibu aniache nilale!

Akatanua mdomo, “Ah!” kisha akaniuliza, “Unawezaje kunijibu hivyo wewe marehemu mtarajiwa?” aliniuliza akinimulika usoni, macho yakaniuma japokuwa nimeyafumba. Nikaweka kiganja changu kujiziba na mwanga huku nikikunja ndita.

“Nakuuliza wewe!” akafoka.

“Kuna haja gani ya kuzozana?” nikamuuliza kwa ustaarabu. “Mimi na wewe wote ni marehemu watarajiwa. Wadhani utaishi milele?”

Kauli hiyo ikamshangaza na kumuudhi bwana yule. Nilimsikia akinguruma kwa ubabe na akakandika lango langu la chuma akisema, “Kelele mbuzi wewe!”

Nami nikanyamaza. Nilikuwa naona ananichosha zaidi. Nilitamani kumwondoa pale alipo lakini sikuwa naweza. Alikuwa ni kero kupita kiasi.

“Heri ya mimi, wewe ni marehemu ambaye siku zake zipo wazi na zinahesabika. Hautapita juma hili utakuwa tayari ushakufa. Vipi utataka kifo cha aina gani? Sindano ya sumu? Kiti cha umeme, risasi ama chumba cha gesi?” kisha akacheka kinafki. “Msaliti wa taifa wewe!” akanitusi na kwenda zake.

Angalau akawa ameenda, lakini pia nikajikuta nikiwa nimefahamu hatma yangu; watanimaliza ndani ya juma hilo, basi ndiyo nikakosa usingizi kabisa mpaka jua linapambazuka.

Kesho yake nikaenda kwenye uwanja wa mazoezi na kuketi huko. Si kwamba nilitaka kufanya mazoezi, la hasha, nilikuwa nataka kubadilisha tu mazingira. Kukaa mule ndani kulikuwa kunachosha, na muda mwingine kulikuwa kunatisha.

Nikiwa nimekaa hapo, nikawatazama wenzangu waliokuwa wanaongoja hatma ya maisha yao kama mimi. Walikuwa ni watano kwa idadi. Mmojawao alikuwa mnene kupita wote na sura yake ilikuwa ya kipole kabisa, nilishangazwa ni nini kimemleta mule ndani ya gereza.

Akiwa amevalia miwani ya macho, alikuwa anachuchumaa na kusimama, zoezi alilokuwa analifanya taratibu taratibu. Alikuwa anatweta jasho jingi tofauti kabisa na zoezi alilokuwa analifanya.

Nikiwa namtazama, nikaanza kumhesabia zamu alizokuwa anaenda chini na kurudi juu. Akiwa amefikisha tatu tangu nianze kumpa jicho, akadondoka chini! Wenzake watatu waliokuwa mbali kidogo naye, wakaangua kicheko.

“Mtazame yule kiroba!” mmoja alidhihaki. Hakuna aliyeenda kumsaidia. Basi mimi nikanyanyuka na kupiga hatua kadhaa kumfuata. Nikamnyanyua na kumpa pole. Akaketi kitini na kunitazama kama mtu aliyejawa na woga. Hakusema neno akawa anapambana kutengeneza pumzi yake.

Kwa kumtazama tu nikafahamu hana miaka inayozidi ishirini na tatu. Alikuwa mdogo sana kuwamo eneo kama hilo.

“Naitwa Marshall,” nikajitambulisha nikimpa mkono. Hakuupokea, bado alikuwa anahema kwanza lakini pia akiwa na hofu usoni.

“Usijali, mimi si mtu mbaya,” nikamwambia nikimtazama.

“Usingekuwa mtu mbaya ungekuwa humu?” akaniuliza. Nikatabasamu na kuweka mkono wangu begani mwake. “Sikia, kid. Si kila unayemwona jela ana hatia. Maisha hayako sawa kama unavyoweza kudhani,” nilimwambia kwa sauti ya utaratibu kana kwamba mzazi akimwonya mwanae. Akanitazama na kuniuliza kwanini nipo mule, nikamjibu ni habari ndefu ambayo asingependa sana kuisikia kisha nikanyanyuka na kumwambia awe makini na afya yake.

“Kumbuka bado upo hai,” nikamwambia kisha nikachukua hatua kuondoka. Nilipopiga hatua nne, akapaza sauti yake akisema, “William, naitwa William Jones.”

Nikageuka na kumtazama. “Nashukuru Willy.” alafu nikaenda zangu.

Dakika kadhaa mbele, tukaja kutolewa kwenye uwanja wa mazoezi kurudishwa kwenye vyumba vyetu. Tulikuwa chini ya ulinzi pingu zikibana mikono.

Nilipofika nikaoga na kulala kitandani baada ya kuwasha runinga. Siku hiyo nikiwa natazama habari nikabahatika kumwona Makamu wa Raisi, ambaye kwa muda huo ndiye alikuwa akikaimu nafasi ya Raisi, akiwa anahojiwa na kituo kimoja cha matangazo.

Kusema ukweli kwa muda wote ule ambao sikuwa najifahamu, nimepoteza kumbukumbu zangu, nilikuwa nimepitwa na mengi sana ulimwenguni, haswa Marekani.

Sikuwa nafahamu kuwa Makamu wa Raisi alikuwa ndiye Raisi rasmi sasa baada ya yule wa awali kutoonekana, lakini pia kwa kupitia matangazo hayo nikapata kujua kuwa nchi ya Marekani ilikuwa kwenye mazungumzo na umoja wa nchi kubwa zinazozalisha mafuta duniani kwa minajili ya kibiashara.

Kiongozi huyo alipoulizwa kuhusu swala la kupotea kwa Raisi na namna gani linavyomuathiri, akapambanua kuwa jambo hilo ni jeraha kubwa sana kwake na kwa Marekani nzima, lakini akaenda mbele kwa kusema kuwa anaamini huo ni mchezo mchafu amba umefanywa na maadui wa Marekani kwa kutumia nyenzo waliyoiunda wao wenyewe.

“... adui anapokuwa nje, ni rahisi kupambana naye. Lakini anaposhirikiana na wa ndani, kunatengeneza nyufa. Ni rahisi kwa ukuta kubomoka,” alisema kwa hisia.

“Na vipi, unaona bado kuna matumaini ya kumpata mwenzako huyo wa karibu akiwa hai?” mtangazaji akauliza. Kidogo bwana kiongozi akatikisa kichwa akisema, “ Uwezekano ni mdogo mno, tunamini atakuwa ameuawa. Kama sivyo, basi itakuwa ni ajabu kubwa.”

Kauli hiyo ikagonga sana kichwa changu. SIKUAMINI KABISA KAMA RAISI AMEKUFA. Kama ni maadui zake wamemuua kama inavyoaminika, kwanini mwili wake usionekane? Kwanini ufichwe?

Bado niliamini Raisi yupo hai. Yupo mahali. Na watu wa kwanza kabisa wanaotakiwa kusema juu ya hilo, wakiwa ni wale wakina Ian Livermore. Niliumia sana kuhusishwa na lile jambo. Nikaumia zaidi kwani mwanangu atakuja kuishi akidhani baba yake alikuwa ni adui wa taifa.

Ni siku hiyo ndiyo nikaamua kufanya namna yoyote ilem nitoke humo ndani ya gereza. Nikitoka humo nikawasake wale wote ninaowatuhumu na mmoja baada ya mwingine atasema anachokifahamu.

Hata kama nikifa, basi nife nikiwa nasafisha jina langu.

Basi nikalala nikiapa endapo nitakuwa bado hai ndani ya juma moja tu la ziada, mipango yangu itakamilika bayana. Juma moja litatosha kabisa kwa mimi kutandaza mipango yangu ya kuaminika kabisa ya kutoroka mule ndani.

Ndani ya juma hilo nisome mianya yote. Kila mtu na kila zamu. Kila mlango na kila dirisha liwezekanalo na namna zake.

Lakini sasa nitapaje juma moja hilo moja la ziada? Hapo ndipo paliniumiza kichwa. Askari yule aliniambia halitapita juma hilo kabla ya pumzi yangu kung’olewa, ni nini sasa nifanye? Sikulala nikiwaza.

Kesho yake yalipofika majira ya mchana wa saa nane, nikapata ugeni, alikuwa ni Miss Danielle, ajenti wa FBI niliyekuwa nashirikiana naye kwenye kesi ya kupotea kwa Raisi.

Niliongea naye kwa uchache sana, akiwa amekuja kuhakikisha kama kweli nilichokisema mahakamni ni cha ukweli. Baada ya hapo nikamuuliza ni nini alipata kwenye chunguzi zake, lakini akaniambia hana muda wa kueleza hayo, na kesi hiyo ilikuwa tayari imeshafungwa.

“Kivipi?” nikashangaa. “kesi inafungwaje, ina maana nyote mnaamini Raisi amekufa?”

Danielle akatazama chini akitikisa kichwa. “Hata kama hatuamini, kuna nini cha ziada? Anyway, ilikuwa ni amri toka juu. Nilitakiwa kufunga kesi hiyo.” aliongea kama mtu aliyechoka. Niliona kwenye macho yake hakuwa na furaha juu ya hilo.

“Nikikuambia kitu utasadiki?” nikamuuliza nikimtazama machoni. Kabla hajanijibu, nikamwambia mimi sikuhusika na mauaji wala kupotea kwa Raisi, lakini najua wapi pa kuanzia kuutafuta ukweli.

Akaniuliza, “Utautafutaje ukweli na upo humu ndani, Marshall?”

“Ndio maana nataka kutoka,” nikamjibu na kumwambia, “Tafadhali nisaidie.”

“Nakusaidiaje Marshall?” akatumbua macho.

“Fanya namna univutie muda,” nikamwambia na kusisitizia, “Nahitaji juma moja tu.”

Punde askari akaja kunitoa. Kabla sijanyanyuka, nikamuuliza Danielle, “Promise?”

Hakunijibu. Alinitazama nikinyanyuka kisha akatikisa kichwa chake. Tukaachana.


**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 08*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

“Ndio maana nataka kutoka,” nikamjibu na kumwambia, “Tafadhali nisaidie.”

“Nakusaidiaje Marshall?” akatumbua macho.

“Fanya namna univutie muda,” nikamwambia na kusisitizia, “Nahitaji juma moja tu.”

Punde askari akaja kunitoa. Kabla sijanyanyuka, nikamuuliza Danielle, “Promise?”

Hakunijibu. Alinitazama nikinyanyuka kisha akatikisa kichwa chake. Tukaachana.

ENDELEA

Sikuwa najua ni namna gani nitatoka mule lakini nilikuwa na matumaini. Matumaini hushinda njaa. Nililala na kuwaza na kuwazua kila namna na kila njia lakini kila mahali nikawa napaona pa moto. Hapapitiki kirahisi.

Nikanyanyuka na kusimamia dirisha langu kutazama nje. Dirisha lilikuwa juu kidogo hivyo ilinipasa kuning’inia kwenye nondo. Nilipotazama kwa uchache tu, kabla sijakata hata kiu, mara nikasikia kishindo cha mtu, nilipogeuka kuangaza nikaona mwanga wa kurunzi, basi nikatoka hapo dirishani upesi na kuketi kitandani. Alikuwa ni askari.

Akanimulika na kuniuliza juu ya hali yangu. Nilipomjibu, akaendelea kumulikamulika ndani ya chumba changu kwa muda kidogo kabla hajajiendea zake.

Ndani ya chumba mwanga ulikuwa hafifu na muda mwingine ukizima kabisa haswa nyakati za usiku.

Ilipopita kama dakika tatu tangu askari yule aondoke kwenye lango langu, nikasikia sauti kubwa ya chuma kikigongwa -- kang! Kag! Kang! Sauti hiyo ilinishtua na kunifanya nisimamishe masikio kuskiza. Nilimsikia askari akifoka kwa kuamuru na kidogo akaongea na ‘radio call’ yake aliyoitundika begani kabla ya muda mfupi kusikia lango likifunguliwa.

Nilikuwa nasikia karibu kila kitu kwani askari alikuwa kwenye chumba cha mbele yangu. Na ndani ya chumba hicho alikuwa anakaa yule kijana mnene niliyeongea naye kwa muda mfupi kwenye uwanja wa mazoezi. Hali yake kiafya ilinifanya niwe makini kuskiza nikiwa nina hamu haswa ya kutaka kujua nini kimemkumba kijana yule.

Kidogo nikaona askari wengine wawili wakipita kuelekea huko, na miongoni mwao, kama sijakosea, alikuwapo mtu wa kutoa huduma ya kwanza. Alikuwa ni mwanamke aliyevalia koti refu la bluu. Ilikuwa rahisi kumtofautisha. Pamoja naye alikuwa anaburuza kifaa chenye matairi.

Walipita kwa mwendo mkali sana wakiwa wanateta. Haikuchukua dakika tano, nadhani baada ya kumfanyia huduma ya kwanza na kuona haileti matunda kwa mgonjwa, nikawaona wakiwa wanarejea wakiwa wanasukuma kitoroli kilichombebelea kijana yule.

Nilitazama kwa kukodoa nikitaka kujua kilichomsibu kijana yule lakini sikuambulia kitu isipokuwa kumwona akiwa ametanua mdomo na kuhema kama bata. Punde tu akawa amepotea machoni pangu!

Nikasimama na kuwaza kidogo. Na hapo ndipo nilipoanza kupata tafakuri itakayonisaidia kutoroka kwenye ngome hiyo.

Jua lilipokuja kusimama, nikafanya namna kuonana na kijana yule mgonjwa. Kwa taarifa za askari waliokuwa wanatusimamia nikabaini alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya gereza kwa matibabu zaidi. Bado hali yake haikuwa inaridhisha, na nilipodadisi zaidi nikagundua amekuwa akisumbuliwa na tatizo la msukumo mdogo wa damu mwilini.

Kwa namna yake nikawaza na kukubaliana na akili yangu kwamba, pengine … pengine njia ya hospitali ikawa ni njia sanifu kabisa kwa lengo langu, lakini yanipasa kuweka mwili wangu tayari na mapambano. Njia hiyo haitakuwa rahisi hata kidogo na mimi sikuwa tayari kabisa kupoteza.

Hiyo ilikuwa ni nafasi yangu na ningelifanya lolote kuhakikisha nafanikisha hilo. Kama ikishindikana, basi na nife.

Nikaanza kupiga ‘push-up’ kila nilipoamka na kabla sijalala. Kwa kila siku nilikuwa napiga mitupo 200. Mara kadhaa askari walikuwa wakinikuta nafanya mazoezi ndani ya chumba changu. Na nilipopata wasaa wa kufanya mazoezi kwenye uwanja, nikafanya vivyo vema. Nikaanza kuhisi mwili wangu umeanza kukaa vema.

Nikatafuta wasaa wa kuongea na Willy, yule kijana aliyezidiwa siku mbili zilizopita. Nakumbuka mara ya kwanza kuanza kumpeleleza tulikuwa kwenye uwanja wa mazoezi. Baada ya kumuuliza kuhusu hali yake, nikaanza kumdadisi juu ya mazingira ya hospitali na nilipopata cha kun’tosha, nikiwa nimetumia kama siku mbili za kukutana naye, nikawa nipo huru sasa kuanza kusuka mipango yangu.

Nikabainisha kila jambo, na ikiwa imebakia siku mbili tu itimie juma moja, nikawa nipo tayari kabisa. Siku hiyo nikiwa nimelala kwenye chumba changu, askari akapita usiku akiwa amebebelea kurunzi ambayo hakuwa ameiwasha.

Akasimama langoni mwangu na kuniamuru nisimame. Alikuwa ni yule askari aliyenihabarisha kuwa nina muda mchache kuelekea kwenye kifo changu. Ilikuwa ni kama bahati kukutana naye tena, kwasababu nisizoweza kueleza, nilitaka siku yangu ya tukio awepo kushuhudia.

Aliniamuru nisimame kwa matusi kabisa lakini sikutii. Akatishia endapo akiingia ndani basi atanisambaratisha na kunimaliza kabla ya siku zangu, bado nikawa mkaidi! Wakati huo nilikuwa nimejishika tumbo na mdomo wangu nimeuachama.

Basi baada ya kuona sifanyi jambo, akafungua lango langu akiendelea kulaani. Aliponifikia atake kuniadhibu, akadaka pua yake akisema, “Mmmmh mmh! Harufu ya nini hiyo?”

Alipotazama akabaini kuna kinyesi kitandani mwangu.

“We mbwa, umenyea kitandani! Nitakuua leo!” akanguruma. Akiwa anatumbua macho yaliyokuwa yanang’aa vema. Sikumpa nafasi, nikaanza kutapika haswa, upesi akarukia kando akinilaani haswa kuwa namchafua. Alikuwa amekasirika kweli lakini nilifahamu nilikuwa nimempatia konani.

Hakuwa na ujanja na alilazimika kuamini nipo kwenye hali mbaya hivyo akawaita wenzake na watu wa huduma waje upesi kunitazama. Ndani ya muda mfupi, wakafika na nikachukuliwa kupelekewa hospitali.

“Kuna shida gani na hawa watu?” nilimsikia mtoa huduma akiuliza. Akiwa anasindikizwa na maaskari, tukafika hospitali nikasafishwa na kulazwa kitandani ingali pingu ikiwa imebana mkono wangu.

Baada ya daktari kufanya vipimo vyake akabaini nilikuwa nasumbuliwa na ‘food poisoning’ na nilitakiwa nipatiwe mapumziko na chakula safi kwa muda, pia na dawa kadhaa za kutumia.

Nikiwa nimejilaza kitandani hoi, nikamsikia daktari akisema kuwa nitakuwa hapo kitandani kwa masaa kadhaa tu, kama ni zaidi basi ni siku moja ama mbili.

Kweli hali ilikuwa dhoofu’lihali, sikuwa nina nguvu kama niwavyo katika uzima wangu, lakini nilikuwa nimesababisha mwenyewe hali hiyo. Jana yake nikiwa nakula chakula cha jioni nikakichanganya na maziwa yaliyoharibika ambayo niliwayeka kwenye joto kali nikiyafumbata kwenye foil na kuyatundika dirishani kupigwa na jua kali kwa takribani siku tatu!

Tumbo lilikuwa linaniuma na kuninguruma, pia niliharisha haswa, na kwa kufanya tukio liwe kubwa zaidi nikajikaza kwa kufanyia hilo kitandani. Kadiri nilivyokuwa nangoja askari aje uvumilivu ukawa mgumu zaidi na zaidi lakini sikuwa na namna.

Na nilipanga kufanya vivyo hata kwa nitakapokuwapo kule wodini mpaka pale nitakapopata wasaa wa kuwekwa kwenye mazingira yangu binafsi na daktari.

Ilipopita siku moja, nikaanza kufanya jitihada za kujibana pumzi kushusha mapigo yangu ya moyo. Hiyo ilikuwa ni moja ya mbinu ambayo tulifunzwa mafunzoni ili kuitumia kwenye mazingira ya utekwaji.

Niliweza kufanya hivyo kwa ufanisi mkubwa mpaka kumuaminisha daktari kuwa hali yangu ni mbaya na basi ningehitaji uangalizi maalumu hivyo nikahamishiwa kwenye kitengo cha uangalizi mkubwa ambapo humo sikuwa nimefungwa pingu bali nimefunikwa uso na kinyago cha kuhemea na pia mwili wangu ukiwa umetundikiwa nyaya mbalimbali kifuani na kichwani.

Nilijua fika sitakuwapo humo kwa muda kwahiyo yanipasa nifanye mambo yangu upesi. Nikafumba macho na kutulia kwa takribani nusu saa nikiwa navuta hewa ndefu ndani na kuitoa, kwa kufanya hivyo nikaboresha mapigo yangu ya moyo na mzunguko wa damu mwilini.

Nilitazama kando na kando, nilikuwa mwenyewe. Sauti za mashine zilikuwa zinalia kwa mbali.

Nikachomoa sindano ya dripu mkononi na kuishikilia vema mkononi. Ilikuwa ndiyo silaha ambayo ningeweza kuitumia kwa muda huo. Punde mlango ukafunguliwa, akaingia daktari.

Alirusha macho yake kwenye mashine alafu akanijongea kunitazama. Hapo kifuani mwangu nikasema, “hii ndiyo nafasi,” haraka macho yangu yakatazama shingo yake kubaini ‘point’ dhaifu.


***
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) --- 09*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Nikachomoa sindano ya dripu mkononi na kuishikilia vema mkononi. Ilikuwa ndiyo silaha ambayo ningeweza kuitumia kwa muda huo. Punde mlango ukafunguliwa, akaingia daktari.

Alirusha macho yake kwenye mashine alafu akanijongea kunitazama. Hapo kifuani mwangu nikasema, “hii ndiyo nafasi,” haraka macho yangu yakatazama shingo yake kubaini ‘point’ dhaifu.

ENDELEA

Upesi nikanyanyua mkono wangu na kutoboa upande wa kushoto wa shingo yake, karibia kabisa na shina, kisha nikamdaka akiwa amedhoofu na hajiwezi. Nikamlaza chini kwa utulivu na kisha nikamjulia hali kama hatokuwa na madhara kwangu ndani ya muda mfupi ujao.

Alikuwa amepooza. Macho yake yalikuwa yanafanya kazi lakini mwili wake ukiwa kama wa mtu mfu, hakuwa anajiweza. Ni vema. Nikafunga mlango na kumvua nguo zake nizichukue. Baada ya hapo nikatoka nikiwa nimevalia kinyago cha kufunika pua na mdomo wangu - kinyago ambacho nilikiopoa ndani ya chumba kile cha watu mahututi.

Nikiwa natembea kwa kujikaza nisionyeshe dosari, nikakatiza mbele kabisa ya wodi mbele ya askari kisha nikadaka korido. Nilikuwa natazamatazama kila kona kuhakikisha usalama wangu, lengo langu lilikuwa ni kuhakikisha nakuwa wa kwanza kuiona hatari kabla ya hatari kuniona mimi.

Lakini bado sikuwa vema kiafya. Nilihisi mwangu ukiwa dhaifu usiojiweza katika namna ya uhai. Kuna muda nilikuwa nahisi kupoteza uwezo wangu wa kuona ama viungo vikiwa dhaifu lakini bado sikusimama, nilikazana, huo ulikuwa ni muda wangu na ilinipasa nivune kila jema niwezalo.

Nilipoacha korido kwa kuikata kona, nikasikia sauti nyuma yangu inapaza, hey ngoja! Heey! Nilibaini alikuwa ni askari alikuwa akiniita. Nilihofia sana kwani bado ungali mapema, sikutaka niharibu kazi yangu.

Basi nikakazana kutembea na huku nikifikiria nini nifanye. Ubaya sikuwa naijua hospitali ipasavyo, sikupata fursa hiyo, ni kitu kigumu sana kwa mfungwa kutembelea hospitali kwa kuikagua, hilo lilikuwa bayana.

Nilichokuwa nakifanya ni kutembea kwa makisio tu na kusema vibango vya juu ya milango. Nilikuwa naomba nipate stoo ama chumba chochote ambamo humo nitapata kujificha kwa muda nikijua kinachoendelea lakini pia na kusoma ramani.

Nyuma nikasikia vishindo vya mtu akikimbia. Vilikuwa vinakuja kwa kasi, lakini kabla havijanifikia, vikasimama na nikasikia sauti ya watu wakiteta, hapo nikapata kujua kuwa askari alikuwa amesimama kuongea na mtu ambaye nilipishana naye muda si mrefu.

Nikaongeza kasi zaidi na punde nikazama ndani ya chumba cha maabara. Humo kulikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakiendelea na kazi zao. Walinitazama na wakiwa hawana mashaka nami, wakaendelea na majukumu yao. Nalijua hawakuwa wakinifahamu.

Basi nikasonga kando na kuwaita, walipokuja nikawashughulikia, kwa kama sekunde kadhaa tu, wakawa chini. Kitendo tu cha kumaliza, nikasikia mlango wa maabara unagongwa mara mbili na kisha mlango ukafunguliwa. Alikuwa ni askari!

Alirusha macho huku na kule asione jambo. Nilikuwa nimejibana kwenye moja ya meza kuu zilizokuwa zinapatikana kwenye maabara. Mkono wake wa kuume alikuwa ameuweka kiunoni akiwa ameshikilia kitako cha bunduki.

Nilimwona uso wake ukiwa umejawa na shaka. Bila maulizo, alikuwa akinitafuta. Alikuwa amenigundua ama? Sikuwa najua japo niliamini vivyo, lakini nilikuwa nina uhakika kuwa hajatoa taarifa kwa wenzie. Kama angelikuwa amelifanya hivyo, king’ora kingaliwaka hospitali na humo wangetiririka askari kadhaa.

Akiwa ameuacha mlango wazi akajongea kuzama ndani, bado mkono wake ulikuwa kwenye kitako cha bunduki. Alipopoa macho kukodoa akizidi kupiga hatua kuzama.

“Hellow! Kuna mtu yeyote ndani?” akapaza kuuliza. “Kuna yeote humu!” akapaza zaidi. Alikuwa anzidi kusonga na kusonga.

Kumpoteza uelekeo, nikatupia kifaa cha maabara upande wake wa kushoto, upesi akatazama, aliporejesha uso wake alipokuwa ameuweka awali, akawa amekawia, nilisharuka kumdandia!

Nilidondoka naye chini na kumbamizia kichwa sakafuni, papo hapo akazirai! Nikasimama nikijiuliza nifanyeje.

Upesi nikampekua mfukoni mwake na kumkuta akiwa na kitambulisho, nikakitazama na kuona kuna namna naweza kukilaghai. Nikatazama kwenye meza ya maabara na kubandua ‘bubble gum’ iliyokuwa imebandikwa mbali kidogo na mimi.

Nikasoma baadhi ya kemikali kwenye vyupa alafu nikachagua moja, kwa kutumia usanifu wangu, humo nikaloweka bubble gum niliyoinyofoa mezani na kisha nikachukua kipande cha chupa ya kifaa kile nilichokitupa kumpoteza mwelekeo askari.

Kwa kutumia kipande hicho, nikamnyoa askari yule ndevu zake, mustachi, alafu nikajibandikia mimi kwa kutumia bubble gum ile niliyoiloweka kwenye kemikali, mustachi ukakaa vema.

Nikamvua sare zake na kuzivaa alafu upesi nikamuhifadhi kule ambapo nimewahifadhi wale wataalamu wa maabara. Sasa nikatoka nikiwa ‘askari’ si ‘daktari’ tena. Kofia nilizibia macho na kufanya mustachi tu ndiyo uwe unang’aa kulaghai mwonekano wangu.

Nikiwa nimeweka mkono wa kushoto ndani ya mfuko, nikatembea kwa kujiamini. Ndani ya muda mfupi nikafanya namna ya kupapata mahali pa kuhifadhia miili ya watu waliokufa, hapo nikamkuta askari mmoja na mtaalamu aliyekuwa anafanya kazi ya uhakiki na kurekodi miili.

Lakini kabla sijafanya jambo, king’ora sasa kikaanza kulia kuashiria kuna hatari. Sasa wakawa wameshajua kuna mchezo umefanyika, mfungwa ametoroka!

Wale askari niliowakuta pale, upesi wakatoka katika lile eneo wakimwacha mtaalamu, wao wakakimbilia huko kwenye tukio. Nikasonga kumfuata yule mtaalamu na kumtaka aendelee na kazi yake kwani miili yapaswa kupakiwa na kutoka upesi kwa ajili ya maziko.

“Lakini king’ora kimelia!” akaniambia kwa tahadhari.

“Unadhani sijasikia kama kimelia?” nikamuuliza nikimkazia macho, wakati huo nikaanza kuhisi mwili wangu ukiwa dhaifu zaidi. Nilihisi miguu inataka kunidondosha na macho yanapoteza uono.

Basi yule mtaalamu akaguna kwa kushusha pumzi puani alafu akafanya utaratibu wa kupakia miili ile kwenye gari maalumu kwa ajili ya kupeleka miili nje ya gereza, na mimi nikapanda humo ndani.

Gari likatembea kidogo na kukomea mahali ambapo uhakiki ulikuwa unafanyika tena. Hapo kulikuwa ni kituo chenye askari kama nane, walipanda wawili na kutazama ile miili yote, ilikuwa minne, kisha gari likakaguliwa na mimi, kama askari sasa, nikiulizwa kuhusu mrejesho.

Baada ya kila kitu kuwa sawa, akapanda askari mwingine ndani, sasa tukawa watu wanne mule, mimi, dereva, na wahusika wawili wa uzikaji, kisha gari likaruhusiwa tukaendelea na safari, ila bado atujalifikia lango kuu. Gari lilikuwa linasonga kwa taratibu kabisa, nikitamani hata nilisukume.

Yule askari aliyepanda akanisogelea karibu na kunisalimu, kisha akaketi kando kando na mimi.

Tukasonga. Tulipofika kwenye lango kuu, hatukukaa sana, likafunguliwa tukapita, hapo angalau nikapata ‘pumzi’. Nilianza kuona mpango wangu unakamilika.

Gari likaongeza mwendo na baada ya kama nusu kilometa, nikamwona askari yule aliyekuwa amekaa kando kidogo na mimi akiwa anasinzia. Kichwa chake kilikuwa kinaenda mbele na nyuma, muda mwingine akijitahidi kukaza macho pasipo mafanikio.

Baada ya mwendo mchache zaidi, nikasikia sauti ikitoka kwenye ‘radio call’ ya askari huyo. Sauti hiyo ilivuma kwa muda kidogo lakini askari yule akiwa hana habari, alikuwa anapambana na usingizi. Nilitamani sana niisikie sauti hiyo lakini ilikuwa mbali na mimi. Nilitaka nijue ilikuwa inahusu nini.

Mara punde nikamwona askari huyo akikodoa! Sikujua nini kilimstusha. Upesi akadaka radio call yake na kuwasiliana, alafu punde kidogo akaamuru gari lisimame! Akasimama akiendelea kuwasiliana na radio call yake hiyo.

Kama sekunde nne tu, nikamsikia akipaza sauti,

“Rudisha gari gerezani!”

**
 
*NYUMA YAKO (MSIMU WA PILI) -- 10*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Mara punde nikamwona askari huyo akikodoa! Sikujua nini kilimstusha. Upesi akadaka radio call yake na kuwasiliana, alafu punde kidogo akaamuru gari lisimame! Akasimama akiendelea kuwasiliana na radio call yake hiyo.

Kama sekunde nne tu, nikamsikia akipaza sauti,

“Rudisha gari gerezani!”

ENDELEA

Nikapatwa na mshtuko haswa kusikia kauli hiyo, yani turudi tena kule! Haiwezekani.

Katika namna ya upesi kabisa, nikafanya jitihada za kumkwatua askari huyo miguu, puh! Akadondoka chini na kujigonga kwenye kingo ya kiti, papo hapo alikuwa amepoteza fahamu. Alikuwa anavuja damu akiwa ameachama mdomo wake kama shimo.

Basi upesi nikadaka silaha yake na kuwaweka wote waliokuwemo mule ndani chini ya ulinzi. Wakanyoosha mikono kutii. Nikiwa nimeweka sura ya kazi, nikawaamuru wote washuke chini, wakatii.

Waliposhuka nikadaka usukani na kuendesha gari hilo kwa takribani kilomita moja kabla sijashuka na kudaka gari jingine kwa ajili ya usalama. Wakati huo nilikuwa tayari nimebadili nguo zangu kwa kuvaa nguo fulani ambazo zilikuwamo ndani ya gari.

Baada ya hapo nikapotelea kabisa ndani ndani mpaka pale nilipojihisi kuwa nipo salama. Kwa macho yangu nikashuhudia habari zikitangazwa kwenye runinga na hata kuzisikia redioni juu ya utorokaji wangu gerezani huku donge nono la zawadi likiwa nimetangazwa kwa mtu yeyote yule atakayetoa taarifa juu ya upatikanaji wangu.

Nikahakikisha naficha uso wangu ipasavyo kwa kutumia sweta lenye kofia na kisha nikashika barabara kwenda kwenye anwani ya makazi ya Jack Pyong, huko kulikuwa karibu kupafikia. Ilikuwa ni safari ya masaa yasiyozidi matatu tokea nilipokimbilia.

Nikiwa kwenye gari sasa, nimeegemeza kichwa changu kwenye kioo, nikawa natazama mikono tangu nikijaribu kuwaza kichwani. Nilikuwa nimetingwa haswa, lakini pia hali yangu ya kiafya haikuwa njema. Sikuwa poa kama ninavyojifahamu.

Nilitamani kwenda hospitali lakini sikuwa naweza. Kwenda huko kungekuwa ndiyo njia ya kwanza kabisa kukamatwa, ilinibidi tu nijikaze nikitumaini nitakapofika nyumbani kwa Jack Pyong basi matatizo yangu yatatafutiwa ufumbuzi kwa namna moja.

Sikuwa najua nitakachokikuta huko wala ya mbeleni.


**

“Kila kitu kipo tayari?” aliuliza Jack Pyong akimtazama Violette. Mwanamke huyo aliyekuwa amevalia gauni fupi linalokomea kwenye magoti yake, alikuwa akijikwatua uso wake mbele ya kioo.

“Bado kidogo, mpenzi. Ningoje!” alisema akijipakaa poda.

“Muda wote huo!” Jack akalalama na kisha akatazama saa yake ya mkononi. “Tumeshachelewa, ujue!”

“Namalizia, mpenzi!” akasema Vio na kisha akafumba mdomo wake akiupakaa lipstick. Basi Jack kujiepusha na kukwazika akatoka hapo chumbani na kwenda kuketi sebuleni, alikuwa yu tayari kabisa kwa ajili ya safari, amevalia suti nyeusi na kiatu chake cha ngozi kinang’aa.

Nywele zake zameta na ananukia marashi mazuri. Amekuwa akimngojea Vio kwa takribani lisaa sasa.

Akasonya na kutazama saa yake kwa mara nyingine. Akiwa anaelekea kuboreka kwa kukaa kwenye kiti kwa muda, akanyanyuka na kuendea jokofu apate kutoa kinywaji.

Akatoa chupa ya juisi na kunywa mafundo mawili akiegemea jokofu. Lakini akiwa hapo ndipo akasikia sauti ya kitu ambacho kilimfanya ajongee dirisha kutazama. Ni kama vile kishindo cha mtu. Hakuwa na uhakika.

Alitazama nje pasipo kuona jambo, lakini punde akasikia tena kishindo cha mtu, mara hii alikuwa na uhakika zaidi. Ni kidogo tu ndipo akaona mtu akizama ndani ya eneo lake kwa kuruka ukuta!

Alikuwa ni mtu aliyevalia ngo nyeusi na kuficha uso wake kwa barakoa rangi ya pinki. Mkononi mwake alikuwa amebebelea bunduki!

Jack akamezwa na hofu! Upesi akakimbia kumfuata Vio apate kumtaarifu kuhusu uvamizi. Alipofika, akiwa ametumbua macho na kukunja ndita, akapaza sauti: “Vio jifiche upesi!”

Vio akamtazama kwa mshangao, hakuwa amemaliza.

“Jifiche!” Jack akaropoka. “Kuna majambazi!”

Pupa zikamjaa Violette. Hakuna alilofanya likaeleweka. Alisimama akiwa ametumbua macho na kukung’uta viganja vyake, aliachama mdomo kwa hofu na akatumbua macho kwa woga.

“Jack, kweli? Jack!”

Upesi Jack akamdaka na kumkimbizia kabatini, hakuwa anatosha, upesi tena akamlaza na kumtaka aingie chini ya kitanda.

“Kakaa humo na unyamaze!” Jack akamsihi alafu akatoka kwenda kuifuata silaha yake kabatini. Alitazama kuitafuta lakini hakuiona.

“Shit!” akalaani. “Imeenda wapi?” akajiuliza akiwa anatota jasho. Akainamisha mgongo kutazama chini ya kabati lakini napo hola, hakukuwa na kitu.

“Mungu wangu!”

Mara akasikia mlango ukibamizwa na watu wakizama ndani.

“Nimekwisha leo!” akajikuta akisema ingali akitetemeka vibaya mno, hakujua cha kufanya, alijikuta akisimama na kungoja. Punde majambazi wakawa wamezama ndani na kumfikia, wakamwamuru apige magoti na aseme kile wanachokitaka kama anataka abakiwe na uhai wake.

Mmoja alikuwa amevalia barakoa nyeusi na mwingine akiwa amevalia barakoa nyeusi.

“Hatupo hapa kupoteza muda na wewe!” alisema yule mwenye barakoa ya pinki. Alikuwa ni mwanamke kwa sauti yake. “Tupo hapa utueleza Marshall yupo wapi?”

Swali hilo likamshangaza Jack. Kwa mara ya kwanza alidhani amesikia vibaya ikampasa aulize.

“Umetusikia vema,” akasema yule jambazi wa kike, “Tunataka kujua Marshall yupo wapi? Sema haraka kabla hatujakumiminia risasi kutoboa kichwa chako!”

Basi Jack akasema hafahamu lolote kuhusiana na Marshall. Kitu pekee anachojua ni kwamba mwanaume huyo amekamatwa na anatumikia kifungo chake jela.

“Unatutania, sio?” akafoka jambazi mwenye barakoa nyeusi, yeye alikuwa ni mwanaume. “Unatufanya sisi ni wehu. Marshall ametoroka gerezani, tuambie ameenda wapi? - nakuhesabia mpaka tano!”

Jack akawatazama wale majambazi akiwa ametabasamu,

“Ametoroka kweli? - ametoroka?”

Na nusu akaangua kicheko. “Nilijua tu Marshall hatokufa kizembe namna hiyo!”

Alikuwa kama mtu aliyerukwa na akili. Majambazi walitazamana kwa mshangao kisha yule wa kike akamkita na kitako cha bunduki kichwani, akalalama kwa maumivu!

“We mpumbavu hatupo hapa kwa ajili ya matani! Moja, tueleze alipo, mbili, tatu! Nne…”

“Sijui jamani!” Jack akapaza sauti akijicha kichwa chake kwa mikono. “Nawaapia sijui alipo. Kama ningekuwa najua, ningekuwa wa kwanza kwenda kuonana naye… nisingalikuwapo hapa!”

“Tano!” akasema yule jambazi mwanaume, akataka kubonyeza kitufe cha kutolea risasi lakini ghafla akajizuiza baada ya kusikia sauti ya kike ikisema, “Ngoja! Usimfyatulie risasi tafadhali!”

Vio akatoka uvunguni na kunyoosha mikono yake juu. Macho yake yalikuwa yanatiririsha machozi, akitazama chini.

“Hatujui Marshall alipo. Kama tungelikuwa tunajua tungewaambia.”

Jambazi yule wa kike akamdaka Vio na kumburuza chini, akamnyooshea tundu la bunduki akimtazama Jack. “Kama usiposema, nitamuua huyu malaya itakapofika tatu. Moja! …”

“Sijui!” Jack akalia. “Tafadhali, usimuue!”

“Mbili …” jambazi akaendelea kuhesabu. “Tatu!”

Mara sauti ya bunduki ikavuma, paaah! Naye Jack akapasa sauti kulalama, lakini ajabu akamwona yule jambazi wa kike akidondoka. Hajakaa vema, sauti nyingine ya bunduki ikatwaa hewa na mara yule jambazi wa kiume akadondoka pia.

Wote walikuwa wamelala chini wakiwa wanavuja damu.

Jack alipotazama risasi zimetokea wapi, akamwona Marshall akiwa amesimama mbele kidogo ya mlango. Mlango wa chumba chake ulikuwa unatazama na wa ule sebuleni.

“Marshall!” Jack akajikuta akipaza, ila punde akamwona Marshall akidondoka chini kama mzigo tih!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom