Nyerere Doctrine: Ni jibu kwa mipaka ya kifisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nyerere Doctrine: Ni jibu kwa mipaka ya kifisadi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Sep 9, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Sep 9, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  [h=2][/h]Alhamisi, Septemba 06, 2012 07:53 Na Prince M. Bagenda  [​IMG][​IMG][​IMG]

  *Ni kati ya Malawi na Tanzania
  *Nyerere Doctrine ilibuniwa na Nyerere kabla ya uhuru
  *Ilianza kutumika mwaka 1963
  *Malawi ilijitawala 1964 na kunufaika na hiyo falsafa

  MIGOGORO mingi Afrika na kwingineko ni migogoro ambayo nchi changa zilizopata uhuru wake kutoka kwa wakoloni zilijikuta zimerithi. Baadhi ya migogoro hiyo ni migogoro ya mipaka, uhasama kati ya makabila na mpangilio mzima katika mfumo wa
  utawala wa nchi changa.

  Mwalimu Nyerere ni kiongozi mmojawapo duniani ambaye aliyaona hayo mapema na kulazimika kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya nchi changa ikiwemo Tanzania hususani suala la nchi zilizokuwa makoloni kurithi mikataba ambayo wenye himaya na walioshika makoloni waliingia na kuzihusisha nchi zao ambapo wananchi walikuwa wanatawaliwa bila ridhaa yao.

  Ubunifu wa Nyerere kuhusu nchi changa zifanyeje kuhusiana na mikataba ya kurithi ilizaa falsafa ya kisiasa na kisheria ambayo inajulikana duniani kote kama “Nyerere Doctrine” katika taaluma na somo la sheria ya kimataifa Nyerere Doctrine ilileta mwelekeo mpya ambao kwa hakika ni jinsi watu wa nchi changa wanavyotafsiri sheria za kimataifa katika jitihada zao za kutafuta nafasi zao na kuamirisha uhuru na enzi za mataifa yao.

  Kwa kifupi Mwalimu Nyerere alitafakari na kujiuliza kwa kupata uhuru nini wajibu wa taifa jipya katika dunia ambayo iligawanywa vipande vipande na kuwa himaya za makoloni ya mataifa makubwa? Jibu lake ni kwamba taifa jipya halikuwa na uhuru wa kuingia mikataba. Mikataba yote ambayo mataifa makubwa yaliingia ambayo inayahusu makoloni ilikuwa kwa faida ya waliokuwa wameshika makoloni na kamwe haiwezi kurithiwa bila taifa jipya kujiuliza. Kwa mfano Waingereza na Wajerumani walishika makoloni katika mabara ya Afrika na Asia. Walikaa pamoja na kuwekeana mikataba kama ule wa Heligoland Treaty 1890 na wa Berlin 1890/95.

  Ni hii mikataba iliyogawa mataifa yapi ya Afrika yatawaliwe na Waingereza na yapi yatawaliwe na Wajerumani na mipaka yao iweje. Katika kujigawia makoloni kulitokea vita ambapo watu walioingizwa katika utawala wa mabavu walipinga na kupigania haki yao ya uzawa na pia kulitokea kulazimisha mipaka ya kuchongwa bila kufuata matakwa ya watu. Wakoloni walichofanya ni kile walichoona wao kinawafaa na wasipigane. Lakini kwa kufanya hivyo walikuwa wanapanda mbegu za uhasama kwa mataifa yajayo ambayo yaliibuka baada ya ukoloni.

  Kwa kifupi falsafa ya Mwalimu Nyerere kuhusu mataifa mapya yaridhie vipi mikataba iliyowekwa na wakoloni ilikuwa ni falsafa ya ukombozi ambayo mpaka sasa ni gumzo kwa wanazuoni, wanasiasa na wanahabari duniani kote. Ni mchango thabiti wa mawazo yaliyotukuka ambayo yalitolewa bila mbwembwe na yakakubalika kama mwongozo kwa mataifa mapya yanayoibuka kutokana na kutawaliwa.

  Mawazo ya Mwalimu Nyerere katika kile ambacho kinaitwa Nyerere Doctrine yalimpa nguvu Mzee Nelson Mandela mwishoni mwa miaka ya 1980 na kuanzia miaka 1990 ambapo Makaburu waliona sera zao za kibaguzi zilikuwa sera mufilisi ambazo haziwezi kuwafikisha popote bali kuendelea kuchochea vurugu na ghasia kati na baina ya watu wa mataifa mbalimbali wa Afrika Kusini.

  Wakati akiwa mfungwa Makaburu walimwendea Mandela na kumtaka wajadiliane naye kuhusu namna ya kumaliza matatizo ya Afrika Kusini. Alichowaambia Mandela ni kwamba yeye ni mfungwa na hana uhuru. Hivyo mtu aliyefungwa na asiye na uhuru hawezi kuingia katika majadiliano na wale wenye kumfunga bila sababu na mfungwa bila kuwa na uhuru. Maneno hayo ya Mandela ambayo aliyasema miaka zaidi ya 30 tangu nchi nyingi ikiwemo na Tanzania kupata uhuru ni sawa na yale aliyoyasema Mwalimu Nyerere kuhusiana na mataifa mapya kurithi mikataba ambayo mataifa makubwa yaliingia kati na baina yao katika jitihada za kujenga himaya zao za makoloni na kutawala dunia. Kwamba watu wa mataifa yaliyokuwa makoloni hawakuwa na kauli yoyote kuhusiana na mikataba ambayo iliainisha mipaka ya nchi zao.

  Mwalimu Nyerere akibainisha na kuainisha falsafa ya kisiasa na kisheria kuhusu mataifa mapya kurithi mikataba ipi yanapokuwa huru (Nyerere Doctrine) anasema, “kuhusiana na uhalali wa mikataba ambayo nchi mpya zinarithi, serikali ya Tanganyika iko tayari kuendelea kutumia mikataba hiyo kwa masharti ya mikataba hiyo na kwa msingi kwamba ina faida kwa taifa jipya kwa kipindi cha miaka miwili tangu taifa letu lipate uhuru mpaka mwisho wa mwaka 1963, isipokuwa pale ambapo mikataba itafutwa au kurekebishwa na pande mbili husika.

  Alisema itakapofika mwisho wa mwaka 1963 serikali ya Tanganyika itachukulia kwamba mikataba yoyote ambayo itakuwa haijafanyiwa mapitio na kujadiliwa upya au kurekebishwa basi kwa msingi wa sheria ya kimataifa itakuwa haitakuwa hai na itakuwa imejifuta”.

  Jamhuri ya Tanganyika iliyozaliwa mwaka 1962 mwaka mmoja baada ya uhuru, iliondosha mahusiano ya Tanganyika huru na serikali ya Uingereza. Ikumbukwe kwamba baada ya uhuru Malikia wa Uingereza alikuwa mkuu wa nchi na waziri mkuu alikuwa ni mkuu wa serikali. Kuanzishwa kwa mfumo wa Jamhuri nafasi mbili za mkuu wa serikali na mkuu wa nchi ziliunganishwa. Huo ulikuwa mwanzo wa kukataa mikataba na mipangilio ya kikoloni ambayo haikuwa na faida kwetu.

  Mwaka mmoja baada ya kuanzishwa mfumo wa serikali ya Jamhuri yaani Desemba 31, 1963 ndipo tangazo kuhusu mikataba ipi tunaweza kuirithi na mingine tusiyoweza kuirithi ilianza kutumika.

  Wakati tangazo la mtazamo na msimamo mpya wa serikali kuhusu mikataba ya kikoloni lilianza kutumika, Malawi ilikuwa bado haijapata uhuru wake na Waingereza kama wenye himaya ambao waliingia kwenye mikataba ya Heligoland 1890 na Berlin 1895, bado walikuwa wanaitawala Nyasaland kufikia Desemba 1963. Walikuwa hawajaleta maombi kwa serikali ya Tanganyika kuzungumzia mpaka wa ziwa Nyasa basi mkataba uliosainiwa kati ya Uingereza na Ujerumani ulikuwa batili.

  Mwalimu Nyerere alimtaarifu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati ule kuhusiana na jinsi taifa jipya la Tanganyika litakavyoshugulikia suala la kurithi mikataba iliyowekwa na wakoloni. Ramani ambazo Tanzania ilipeleka Umoja wa Mataifa ilipojiunga na umoja huo tangu mwaka 1961/62, ilikuwa inaonyesha Tanganyika yenye mpaka na Malawi ambao unaonyesha mpaka kupita katikati ya ziwa na siyo kwenye mwalo wa ziwa upande wa Mashariki mwa ziwa Nyasa kama Malawi inavyodai.

  Madai ya Malawi kwamba ziwa lote la Nyasa ni lake hayaungwi mkono na jinsi maziwa katika sehemu hii ya Afrika Mashariki na Kati yalivyo na mipaka yake kati na baina ya nchi. Karibu maziwa yote yakiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Albert na Ziwa Jipe mipaka imetenga sehemu gani ya maji iko upande wa nchi gani, isipokuwa madai ya Malawi ya mipaka ya Ziwa Nyasa ambayo inakuwa kwenye ardhi ya Tanzania.

  Wakati lilipojitokeza tatizo la mpaka kati ya Tanzania na Malawi mwaka 1967, Rais Kamuzi Banda wa Malawi alidai kwamba si ziwa tu ni la Malawi bali hata Wilaya za Kyela, Rungwe, Mbinga na Songea ni sehemu za Malawi. Baada ya kufanya madai hayo na Mwalimu Nyerere kuyasikia basi alitangaza kwamba Kamuzu Banda anadai pia na bandari ya Dar es salaam kwamba ni yake!

  Waingereza katika utawala wao walipendelea nchi ambazo zilikuwa makoloni yao moja kwa moja kama Kenya, Malawi, Zambia na Zimbambwe dhidi ya koloni la Tanganyika ambalo halikuwa koloni kwa maana ya utawala wa moja kwa moja. Tanganyika ilikuwa chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa ikisimamiwa na Uingereza.

  Hivyo masuala mengi kama vile ya mpaka kati yake na Malawi yaliachwa hivi hivi ingawa Waingereza walikuwa wanajua ukweli kwamba walichokuwa wamefanya kimkataba hakina uhalisi na kutakuwepo maswali na hata uchochezi wa kuvurugana kati ya Malawi na Tanzania.

  Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), ulikubali mipaka iliyopo iendelee kuwepo na kuziachia nchi zenye migogoro ya mipaka zenyewe zijadiliane au zitafute suluhisho katika Mahakama za Kimataifa. Katika miaka 50 tangu nchi nyingi za Kiafrika zipate uhuru kumekuwepo na migogoro mingi ya mipaka.

  Nchi kama vile Uganda na Tanzania zilikubaliana kurekebisha mipaka yao kwa hiari yao wenyewe. Kuna nchi kama Nigeria na Cameroon na Libya na Tunisia zilikubaliana kwenda kwenye Mahakama ya Dunia, kwenda kumaliza matatizo yao ya mipaka. Nchi mpya kama Eritrea zimeibuka na zina mipaka yao inayotambuliwa kimataifa ingawa mipaka kati yake na Ethiopia imekuwa chanzo cha mapigano kati ya nchi hizo mbili.

  Vilevile Sudan Kusini ni taifa jipya ambalo mipaka yake na Sudan Kaskazini imesababisha vita kati na baina ya nchi hizo mbili. Kwa Malawi na Tanzania suala la mpaka upite wapi katika ziwa Nyasa ni suala ambalo halipaswi kuleta matatizo. Sheria za kuweka mipaka katika sehemu za majini ziko wazi kwamba ni sehemu za katikati ambapo sehemu moja ya maji inakuwa upande wa nchi moja na sehemu nyingine inakuwa upande wa nchi nyingine.

  Katika miaka ya 60, Malawi ilianza kuchochewa na makaburu waliotaka kuishambulia Tanzania kwa kuwahifadhi waliokuwa wapigania uhuru. Zamu hii mashirika ya kimataifa yanayotaka kupora raslimali za Afrika yanataka kuchochea mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania kutokana kwamba nchi hizi zina raslimali ya madini ya Uraniamu na ziwa Nyasa lina uwezekano mkubwa wa kupatikana mafuta na gesi chini ya ziwa. Tahadhari kubwa inapaswa kuchukuliwa kwa kufichua hujuma ambazo zinataka kufanywa kwa kuingiza mataifa machanga katika vita visivyo na faida.

   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Sep 9, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145

  Nyerere alikuwa ana akili na kuona mbali... kweli Wazungu hawa wanataka NCHI za Africa zigombane ili tuwe OPEN PIT wachukue Mali zetu bure kama

  CONGO-KINSASHA
   
 3. Kiranga

  Kiranga JF-Expert Member

  #3
  Sep 9, 2012
  Joined: Jan 29, 2009
  Messages: 34,607
  Likes Received: 6,185
  Trophy Points: 280
  Mwandishi hajalitendea haki hili suala la OAU kukubali "mipaka iliyopo" wala hajaelezea kwa kirefu contradiction iliyopo kati ya "Nyerere Doctrine" kama ilivyoletwa kwetu na hii habari, kwamba inakataa mikataba ya wakoloni isiyorejewa, na mwongozo wa Nyerere uliopelekea OAU kukubali "mipaka iliyopo" ambao Nyerere aliutoa baada ya kuona matatizo ya mzozo wa mpaka na Malawi.

  Nyerere ni mmoja wa kulaumiwa katika mgogoro huu kwa sababu alilifuga tatizo kwa miaka mingi bila kulipatia ufumbuzi.
   
Loading...