Nyerere Day 2022: Nyumba ya Bi. Mwamtoro bint Chuma Mtaa wa New Street na Kariakoo

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,908
30,249


NYUMBA ALIYOJENGA NA ALIYOISHI MWALIMU MTAA WA IFUNDA MAGOMENI 1958

Tulipomaliza mahojinao yetu nje ya nyumba ya Bi. Mwamtoro bint Chuma nyumba ambayo iko nyuma ya Ofisi Ndogo ya CCM tukaelekea Magomeni Mtaa wa Ifunda kwenye nyumba aliyojenga Mwalimu mwaka wa 1958 na akaishi pale kwa kipindi kifupi akahamia Sea View nyumba ya serikali.

Mwalimu alikuwa sasa anangojea kuongoza serikali ya madaraka mwaka wa 1960 kisha uhuru kamili na kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika.

Hivi sasa nyumba hii ya Magomeni imegeuzwa kuwa kumbukizi ya Mwalimu Nyerere.

Historia yake imehifadhiwa katika nyumba hii pakiwa na picha zake na vitu alivyotumia wakati akiishi hapo.

Tulipokelewa vyema sana na wafanyakazi wote wa nyumba hiyo wakubwa kwa wadogo khasa kwa kuwa Jaffar na amesaidia sana kupitia AZAM TV kuitangaza nyumba hii ya Baba wa Taifa kwa umma.

''Mzee Mohamed nakuomba tufunge kipindi hiki kwa wewe kueleza machache katika katika picha hizi za Baba wa Taifa ziliopo hapa,'' Jaffar aliniambia.

Wakuu wa nyumba hii walikuwa wametuzunguka kusikiliza nikamsikia mmoja anasema nyuma ya mgongo wangu kuwa mimi ninajua mengi sana katika historia ya Mwalimu Nyerere.

Nilicheka kimoyomoyo.
Najua kwa nini alisema hivyo.

Sababu ni kuwa walipokuwa wanatafuta picha za Mwalimu Nyerere niliwapatia picha nyingi na baadhi zipo hapo wamezitundika ukutani kwa kila ajae pale kuziona.

Niliwapatia picha nyingi kutoka Maktaba ya Picha ya Ukoo wa Sykes.

''Naomba nizieleze picha tatu na sabubu ni kuwa mimi ndiyo nilihusika kuziweka hadharani kwa watu wote kuziona na kuzifahamu.''

Hapa nilisimama na kuomba radhi nisieleweke kuwa najipigia zumari langu mwenyewe.

''Picha hizi wamenipa watu mimi nimezifikisha hapa nyumbani kwa Baba wa Taifa ili ziwakumbushe wataokuja hapa historia ya Mwalimu Nyerere na historia ya wale ambao walikuwa na yeye katika siku zile ngumu za kupigania uhuru lakini kwa bahati mbaya wamesahaulika.''

Jicho langu likaenda kwenye picha Ali Msham akiwa na Mwalimu Nyerere, John Rupia, Zuberi Mtemvu na vijana wa Bantu Group, picha iliyopigwa nyumbani kwa Ali Msham Magomeni, Mtaa wa Jaribu mwaka wa 1955.

Nikamweleza Ali Msham alikuwa nani kwa TANU, Mwalimu Nyerere na Mama Maria.

Picha hii wamenipa watoto wa Ali Msham na ni kati ya picha 11 walizoniokabidhi nizitumie nipendavyo kwa manufaa ya umma.

Nikaisogelea picha nyingine ya mwaka huo huo 1955 safari ya kwanza ya Mwalimu Nyerere UNO picha iliyopigwa uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.

Wamesimama watu wengi kwenye picha hii pembeni ya Mwalimu alikuwa Iddi Faiz Mafungo na nikamweleza nani alikuwa Iddi Faiz Mafungo.

''Huyu alikuwa Mweka Hazina wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na Mweka Hazina wa TANU kadi yake ya TANU ni No. 24 na No. 25 ni ya ndigi yake Iddi Tosiri na yeye ndiye alikuwa mkusanyaji wa fedha za safari ya Mwalimu Nyerere UNO.

Iddi Faiz na Iddi Tosiri ndiyo walimtambulisha Nyerere kwa Sheikh Mohamed Ramiyya Bagamoyo''

Picha hii niliipata kwa Jim Bailey, Mzungu kutoka Afrika ya Kusini aliyekuwa mmiliki wa gazeti la Drum.

Kuna baadhi ya wafanyakazi wa Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere ndiyo kwa mara ya kwanza wanaisikia historia ya Iddi Faiz Mafungo.

Nikahitimisha kwa kueleza picha maarufu ya Mwalimu Nyerere akiwa na Baraza la Wazee wa TANU.

Kidole changu kikaenda kwa Said Chamwenyewe nikawaeleza wasikilizaji wangu kuwa Mzee Said Chamwenyewe ndiye aliyeipatia wanachama wake wa kwanza TANU kutoka Rufiji.

Nikamaliza kwa kueleza kuwa picha hiyo nilipewa na Msakala Tambaza, mjukuu wa Mzee Mohamed Tambaza.

Historia ya Baba wa Taifa Mwalimu Kambarage Nyerere inapendeza pale inapoelezwa na historiza za wazalendo wengine waliopigania uhuru na Mwalimu bega kwa bega.

1666063756938.png
1666063794583.png
1666063829051.png
1666063867224.png
1666063897937.png


PICHA

Ali Msham waliosimama wapili.

Hapo ni nyumbani kwake Magomeni yupo na Bantu Group.

Waliokaa kulia Zuberi Mtemvu, Julius Nyerere na John Rupia.

Kuliani kwa Nyerere kavaa kanzu koti na tarbush ni Iddi Faiz Mafungo.

Baraza la Wazee wa TANU.

Jaffar Mponda akiwa na watendaji wa Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere.

Bi. Mwamtoro bint Chuma akipiga kura Uchaguzi Mkuu mwaka wa 1970.
 
Back
Top Bottom