Nyerere analia, Kikwete angalia uamuzi ni wako

Kiranja

JF-Expert Member
May 19, 2007
751
336
Nyerere analia, Kikwete angalia, uamuzi ni wako
Mbaraka Islam
Toleo la 264
19 Oct 2012

KWA kawaida ndoto hutafsiriwa kwa maana nyingi kulingana na hisia, imani na msimamo wa mtu anayewasilisha ama kupokea ujumbe husika, lakini kwa hili naandika nikiamini kwamba kuna ujumbe mzito ndani yake.

Hii ni mara ya pili kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kunijia katika ndoto na mara zote hutokea wakati kuna jambo zito linalohusu hatima ya Tanzania, taifa aliloliasisi kuanzia miaka ya hamsini. Nitaeleza baadaye ili kwa sasa nieleze ya sasa.

Nilishituka katika usingizi na kujisikia mzito kupita kiasi na ghafla nikajikuta niko katika nyumba moja ya kawaida kabisa mahali ambako nikaaminishwa kwamba ndipo makazi halisi ya Baba wa Taifa.

Kwa kuwa kazi yangu ni kutafuta habari, nilihitaji sana maoni ya Baba wa Taifa, mtu ambaye anaujua kwa dhati uchungu wa Tanzania, watu wake na rasilimali zake na mara moja nikamkabili mzee huyo ambaye alikuwa anaonekana kuwa mwenye mawazo mengi na huzuni iliyomfanya kuwa na uso uliochoka.

Nilisita kumuuliza kuhusu kilichokuwa kikinikera kwani alianza kulia aliponiona hali iliyonifanya nami nishindwe kujizuia kububujikwa machozi.

Nilianza kulia naye alinikumbatia na kuniambia, “Nalilia Tanzania yangu, najutia yaliyotokea. Sikujua kwamba niliyemuamini amefanya yale niliyoyapinga kwa nguvu zangu zote.”

Nilipata ujasiri na kutoa kijitabu changu cha kuchukua dondoo za habari ili nianze kunukuu maneno yake. Kwa bahati mbaya nilikuta kijitabu hicho kimejaa, hakina nafasi kubwa ya kuandika.

Nikaokota vipande vya karatasi jirani na tulipokuwa tumekaa na kuanza kuandika maneno hayo. Katika mazungumzo yetu nilijiona mpumbavu kwa kutokuwa na kaseti ndogo ya kurekodi, baada ya kuona mazungumzo yananoga.

Nilitaka kujua undani wa maneno yake, na kwa kweli hakuwa na mengi ya kuzungumza na mahojiano yalikuwa mafupi mno, kiasi cha kunifanya nipate maneno machache kutoka kwake.

Baada ya kusema analilia Tanzania yake, Mwalimu alisema, “Zimwi la ajabu lenye mapembe ya rushwa, kulindana na matumizi mabaya ya madaraka, limeimeza Tanzania yangu. Msikate tamaa, pambaneni. Mwambie Jakaya (Rais Jakaya Kikwete) aangalie.”

Baada ya maneno hayo nilipoteza ujasiri maana nilipoteza mwelekeo na sikuweza kuendelea na mahojiano yale kwa kina. Katika hali ya kawaida, mimi sio mtu wa kushindwa kufanya mahojiano na mtu yeyote, hasa nikipata nafasi lakini kwa Mwalimu nilikwama.

Kabla sijaondoka aliniomba nimsindikize akapumzike kwa kuwa alikuwa amechoka. Nilimshika mkono na kumpeleka hadi chumbani kwake, ambako kulikuwa na vitanda vitatu na kabla hajalala akasema, “Nilimzuia Jakaya mwaka 1995 nikijua mwenzetu amekomaa na ni msafi kumbe amekuja kuniaibisha kabisa.”

Hayo ni maneno machache na pengine kutokana na kuguswa nayo, ndiyo niliyoweza kuyanukuu nilipozinduka huku uso wangu ukiwa umetapakaa machozi.

Nimejiuliza na kuwauliza watu wa karibu nami kuhusiana na ndoto hiyo, lakini nimepata majibu mchanganyiko ndio sababu hasa nimeamua kuwapa nafasi Watanzania wa Mwalimu Nyerere nao wapate maneno hayo. Sio lazima wayaamini, lakini wapate ujumbe.

Mara baada ya Mwalimu kufariki, nilipata kuota ndoto ambayo alinieleza huku akitembea kwamba niwaambie ‘jamaa zangu’ kwamba hajapendezwa kabisa na kuuzwa ama kubinafsishwa kwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), jambo ambalo nakumbuka aliwahi kuliweka wazi wakati wa uhai wake tulipokuwa mjini Arusha.

Siku hiyo ilikuwa ni ziara ndefu ya kuanzia Dar es Salaam, Iringa mjini na hatimaye vijijini na baadaye Arusha, safari ambayo nilibaini ukakamavu wa Mwalimu katika umri wa utu uzima na hiyo ilikuwa miezi michache kabla ya kwenda nchini Uingereza kwa matibabu, safari iliyokuwa ya moja kwa moja. Hakurejea tena akiwa hai. Alipoteza maisha yake akiwa huko baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya damu.

Lakini, hadi sasa sifahamu kinachonisukuma kuwa na hisia kali na Mwalimu Nyerere, kwani kabla hata ya kutangazwa kuugua kwake, nilipata kuwaeleza wakubwa wangu wa kazi wakati ule, Salva Rweyemamu, aliyekuwa Mhariri Mtendaji wangu ambaye tulikubaliana kuwa na subira kabla ya kuandika habari hiyo.

Ilikuwa ni gazeti moja litolewalo kwa wiki kwa lugha ya Kiingereza ndilo lililotusukuma kuanza kuandika habari za ugonjwa wa Mwalimu, kwani liliandika habari ikielezea kwamba Mwalimu amezidiwa na amesafirishwa kwenda nje ya nchi, jambo ambalo halikuwa sahihi wakati huo. Tukaandika ukweli kwamba anaumwa, lakini yupo nchini.

Tuliendelea kufuatilia habari zake hadi siku ambayo alikuwa akiondoka nchini kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Uswisi (Swiss Air), siku ambayo ni waandishi watatu tu ndio walikuwapo uwanja wa ndege, Absalom Kibanda, ambaye sasa ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima na mwanahabari mpiga picha, Emmanuel Herman, ambaye kwa sasa yupo Gazeti la Mwananchi.

Siku hiyo nakumbuka, uwanjani hapo kulikuwa na kundi la waandishi wa habari waliofika kupokea wanamichezo waliofika Dar es Salaam kwa ndege ya Swiss Air iliyomchukua Mwalimu, lakini baada ya kuwapokea wanamichezo waliondoka bila kujua Baba wa Taifa anaondoka kwa mara ya mwisho kwenda Uingereza.

Nakumbuka baada ya makosa kadhaa ya kitaaluma kutokea, nilimwambia Kibanda kwamba Mwalimu hatarudi. Sikuwa na sababu zozote za kusema maneno hayo na hakuna aliyezingatia maneno hayo na ndio maana hata mpiga picha wetu Herman hakupiga picha za kutosha katika tukio hilo. Niliumia sana.

Nakumbuka hata waliomsindikiza hawakuwa watu wazito kwani alikuwapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, John Chiligati na upande wa Polisi, alikuwapo aliyekuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Mkwama, na pia ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje, ambaye alikuwa pale kusimamia itifaki.

Hata aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, alikutana na Mwalimu pale VIP akiwa katika safari zake na hakuwa katika orodha ya waliofika kumsindikiza Mwalimu na mkewe Maria, huku familia ikiwakilishwa na mabinti wawili ambao walionekana wakiipungia mkono ndege iliyomchukua Mwalimu, ikiwa angani.

Hisia hizo zinanipeleka siku ya kifo chake, nilipojikuta nikianguka mara baada ya kuona sura ya Baba wa Taifa pale nyumbani kwake Msasani na haikuishia hapo kwani nilitoka nyumbani kwenda kusindikiza mwili Uwanja wa Ndege kwenda Butiama, lakini nilijikuta ‘nikidandia’ ndege ya Jeshi la Afrika Kusini kwenda Musoma na hatimaye Butiama.

Halikuwa jambo la kawaida, kwani sikuwa na chochote zaidi ya nguo nilizokuwa nimevaa hata niliponyeshewa mvua tukiwa katika msafara wa mwili wa Mwalimu, sikuwa na nguo za kubadili na huko nilimkuta muongoza kwaya katika mazishi ya Mwalimu, Ansbert Ngurumo (mwanahabari mwenzagu), ambaye naye “alizamia” kufika Butiama; hakuwa ameaga ofisini. Tulivutwa na mzimu wa Nyerere.

Hata Benjamin Mkapa, akiwa Rais aliyekuwa madarakani, alisema mbele ya kaburi la Mwalimu kwamba watakaofanya mambo kinyume cha wosia wa Baba wa Taifa, “jinamizi lake litawashukia,” na kwa hakika inaelekea sasa “jinamizi” linaelekea kumshukia yeye.

Hakuna ubishi kwamba mambo mengi ambayo Mwalimu aliyapinga kwa nguvu zake zote hadi anakata roho, Mkapa ameyakiuka ikiwa ni pamoja na sio tu kushindwa kabisa kupambana na rushwa, bali pia yeye binafsi kuhusishwa rushwa na ufisadi.

Mwalimu alipinga kabisa Ikulu kutumika kujinufaisha, lakini mara tu alipoaga dunia, Mkapa alianzisha kampuni akitumia rasilimali za umma, ikiwa ni pamoja na majengo, magari, wataalamu na hata kuamua kushirikiana na waziri wake, Daniel Yona kufanya biashara wote wakiwa madarakani.

Pamoja na kufahamu wazi kwamba Baba wa Taifa alipinga kabisa kuuzwa kwa NBC, Mkapa alijenga uhusiano wenye utata mkubwa na wamiliki wa benki hiyo, uhusiano ambao ulimuwezesha kuendelea kujineemesha yeye na familia yake na kujitanua kwa kujipatia nyumba nyingine jirani na ile aliyokuwa akiishi pale Sea View, Dar es Salaam.

Ni Mkapa huyo huyo ambaye sasa tunaambiwa kwamba kwa baraka zake, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanya ‘madudu’ ya ajabu ambayo kwa hakika ndiyo yaliyofanya Baba wa Taifa, anijie katika ndoto baada ya kubaini kwamba nimekuwa nikiumia sana kwa jinsi Tanzania yetu ilivyotumbukizwa katika “janga la kujitakia”.

Hakuna asiyefahamu kwamba Mkapa alitetewa kwa nguvu zote na Baba wa Taifa, wakati huo akionekana kama mtu pekee msafi katika kundi kubwa la wanasiasa walioomba kuwania urais mwaka 1995, mwalimu huko aliko sasa anajuta, lakini anamwambia Jakaya aangalie.

Mwalimu analia Jakaya angalia, Tanzania na Watanzania kwanza mambo mengine baadaye, tuko nyuma yako ukiamua.

Kuamua kwa Kikwete kutatokana na utashi wake binafsi na sio wa mashabiki wala watu wanaojikomba kwake.

Ni kuamua ndiko kutampa sifa na baraka tele kutoka kwa Mungu Mkuu baada ya kutovaa sura ya aibu kwa watu ambao wanamkwamisha kutekeleza azma yake.

Azma kubwa ya Kikwete ni maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini sasa anaonekana kushindwa na wengi tunaamini kuwa anaweza, isipokuwa anaangushwa na hao wapambe wanaomzunguka.

Wapambe wake ni wengi wakiwamo marafiki zake, wasaidizi wake wa karibu serikalini ambao kila jambo wao wanaona ni hewala, wakati ukweli ni kwamba Watanzania wanateketea na kutomuamini rais wao waliyemchangua kwa kura nyingi.

Ni vyema, sasa Kikwete akaamua kabla muda haujawa mwingi, akawatosa wote wanaomuangusha na kumfanya kukosa thawabu.

Nakumbuka Simba wa Vita, Waziri Mkuu mstaafu, Rashidi Mfaume Kawawa aliwahi kukieleza kikao kimoja cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, kwamba ni vyema mtu anayetoboa jahazi akatoswa mapema, kwani kulelewa na kushangilia huku akiendelea na hujuma zake, mwisho wake ni abiria wote, pamoja na nahodha kuzama na kupoteza maisha.

Kikwete, wakati wa kuwatosa wote wanaokuangusha ni sasa na usijali urafiki, uswahiba au undugu na watu wa aina hiyo na hapo utakuwa umeokoka na kulitendea haki taifa la Watanzania.
Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Kulikoni, Januari, mwaka 2008.
Soma zaidi kuhusu:
Mwalimu Nyerere
Kikwete
Tufuatilie mtandaoni:
Wasiliana na mwandishi
Mbaraka Islam
Maoni ya Wasomaji
kAMA kIKWETE ANA UJASIRI
Permalink Submitted by BODI (not verified) on Sun, 2012-10-21 23:33.

kAMA kIKWETE ANA UJASIRI ATASAMEHEWA AKIWEZA KUANGALIA NA KUTETEA MASLAHI YA WATANZANIA WOTE AMBAO WAMAMELIKWAMUA TAIFA LETU KWA MALI NA HALI. WENGI LICHA YA NYERERE WALIPOTEZA UHAI, KOTE TANZANIA BARA NA VISIWANI. HAWA NI BABU ZETU, BIBIZETU, KAKA ZETU, DADA ZETU, WAJOMBA, SHANGAZI, WATOTO WETU NA VIJUKUU VYETU.
DAMU ZAO, HAZIJAPOTEA BURE KWA KUPEWA CHUMVI NA MKOLONI.
SHIDA NA MATATIZO YA WATANZANIA WOTE NCHINI, WALIOPORWA, WALIOFYEKWA, WALIOPOTEZWA, NA WALIOVIFUNGONONI BILA HILA.WAUZAJI BARABARANI, WAGONJWA, VILEMA, NI AFRICA TU NA WABANTU WANAOJALI VITU KAMA HIVI KWA SABABU YA UBANTU WETU.
TUSIUUZE UBANTU WETU KWA KIGARI, SIMU, PIKIPIKI, SURUALI, AU KIJUMBA. HUWEZI KUUUZA MBANTU KWA MZUNGU NA MAKABURU KWA VITU. nA MKAPA ALIYEJENGA aFRICA YA KUSINI, NI NYERERE ALIYAWASAIDIA WAAFRIKA YA KUSINI WENGI, KIELIMU, HALI, NA MALI.
WEWE UNAKWENDA KUJICHOPEKA PALE NA WALE WALE MAKABURU, MZUNGU MWEUSI KWA JASHO LA nYERERE NA WATANZANIA WOTE BILA AIBU.YOU DONT EVEN HAVE HALF A PERSONALITY AND DIGNITY NYERERE HAD.RUDISHA MALI YA WATANZANIA YOTE.INABIDI UWEKWE NDANI BILA PINGAMIZI. MALI ZAKO ZOTE, NA MKEO NA WATOTO WAKO NA ACCOUNT ZOTE, NI MALI YA WATANZANIA WOTE.
KWA NINI NYERERE ALIE, KWA NINI WATANZANIA WAKUOGOPE, WAZIDIKUKULINDA, WAKULIPE TENA?
kIKWETE, kAMA HUJAHUSIKA, HATA KAMA UMEHUSIKA,KAZA MOYO
FUMBA MACHO JISALIMISHE NA RUDISHA HALI, HADHI, NA USALAMA WA NCHI.
WATANZANIA SI WANYAMA,
WATANZANIA SI WAPUMBAVU,
WATANZANIA, UKIMYA WAO, UTULIVU WAO, UMEFIKIA SEHEMU, ISIYOWEZEKANA.
WOTE WANAKUUNGA MKONO FANYA UJASIRI.

reply

Ni watanzania gani
Permalink Submitted by Kibuga Mwalu (not verified) on Thu, 2012-10-25 12:23.

Ni watanzania gani wanaomuunga mkono Kikwete katika hali ambayo huwezi kuifananisha na amani wala vurugu. Siku ziende aondoke aingie mwizi mwingine!

reply

Nimesoma makala yako ya
Permalink Submitted by Nkwazi Mhango (not verified) on Sat, 2012-10-27 05:58.

Nimesoma makala yako ya kwenye Raia Mwema tangu alhamis nadhani zaidi ya mara tano au sita. Imenigusa hadi nikaingia kwenye makabrasha yangu na kukumbuka ile niliyoiandika mwaka 2006 ambayo naiambatanisha. Kuna kitabu changu kinaitwa SIKIA MWALIMU NYERERE sijapata pa kukichapisha lakini nshakiandika. Hakuna kitu kimenigusa kama ujasiri wa kuwanyoshea kidole Mkapa na Kikwete moja kwa moja. Wengi wanaogopa kuwaambia ukweli. Mie nimetokea kuchukiwa kwa hili ingawa sitakata tamaa maana Tanzania ni yetu sote. Kuna haja ya kuandika sana kuhusiana na walivyomsaliti mwalimu tufafanikiwa hasa ikizingatiwa kuwa hata kama ameishafariki bado ana nguvu kuliko hawa wezi wa sasa. Niliandika kitabu kiitwacho NYUMA YA PAZIA mchapishaji wa Kitabu changu cha SAA YA UKOMBOZI akaogopa kukichapisha kiasi cha kukataa miswada mingine niliyomtumia baada ya kumgusa fisadi mmoja anayefukuzia madaraka kwa sasa kwa kuhonga kila paka panya
 
Watanzania tumesalitiwa vya kutosha!

Inauma sana. Hakuna anayejali.
 
Nyerere ndio aliyepanda mbegu za udini kwa kupendelea dini fulani sasa haya ndio matunda Yake na bado
TUtegemeee mengi kuliko haya YANAKUJA NA ANGEKUWEPO ANGATAMANI NA KUONA UCHAFU ALIOUFANYA
 
Nyerere ndio aliyepanda mbegu za udini kwa kupendelea dini fulani sasa haya ndio matunda Yake na bado
TUtegemeee mengi kuliko haya YANAKUJA NA ANGEKUWEPO ANGATAMANI NA KUONA UCHAFU ALIOUFANYA

Ni kweli Nyerere alipanda mbegu ya udini kwa kupendelea waislam maana alitaifisha shule zilizokuwa zinamilikiwa na taasisi za dini ambapo 80% zilikuwa zinamilikiwa na wakristo na akazifanya kuwa za serikali ili na waislam wengi wasome!
 
Viongozi wetu wana mioyo migumu sana, hata uandikeje, hata uote ndoto kiasi gani kamwe hawajuti kwa wanayowafanyia Watanzania, na kwa vile Watanzania nasi tu watu wa ajabu tunaishia kulalamika tu bila hatua yoyote.
 
nyerere ndo nani? kila kitu nyerere wengi wanaomzungumza huyu marehemu hawakuwepo kipindi chake cha utawala.Ni mtu mbaya na katili sana kuwahi kutawala tz.watu wengi wamepotezwa na kuuliwa,wengine kupoteza mali zao.nahisi kutapika akitajwa huyu marehemu
 
Back
Top Bottom