Nyakati hizi ngumu twahitaji uongozi, si utawala

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,005
Nyakati hizi ngumu twahitaji uongozi, si utawala

Johnson Mbwambo Novemba 19, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

NDUGU zangu, nyakati tunazopitia hivi sasa ni ngumu, tunahitaji uongozi na si utawala. Si siri kwamba Taifa linapitia kipindi kigumu mno kinachohitaji si tu hekima, ujasiri na uvumilivu wa watawala wetu; bali pia Watanzania wote kwa ujumla.

Kwa mtazamo wangu, ukiondoa kipindi kile cha vita kati yetu na nduli Iddi Amin na miaka michache iliyofuatia baada ya vita hiyo, hakuna kipindi kingine chochote ambacho Taifa limepitia majaribu makubwa kama hiki cha sasa.

Rais wetu, Jakaya Kikwete ameingia madarakani katika kipindi ambapo nchi imekumbwa na kashfa kubwa za wizi wa pesa za umma za EPA na Meremeta, kwa kiwango ambacho hakijapata kuonekana katika historia ya nchi yetu.

Tunapaswa kumwonea huruma Kikwete kwa sababu yeye ameingia Ikulu na kurithi tu tatizo hilo; kwani wakati mapesa hayo ya EPA au ya Meremeta yakichotwa, yeye hakuwa Rais wetu.

Ni bahati mbaya sana kwamba aliyekuwa Rais wakati mapesa hayo yakichotwa (mwaka 2000 na 2005), Benjamin Mkapa, sasa yuko pembeni akila pensheni yake na kumwacha mwenzake (Kikwete) akihangaika kupambana na dhoruba za skandali hizo alizomwachia. Lakini yeye (Kikwete) ndiye Rais wa sasa; hivyo anabeba yote; kama ambavyo Obama atakavyobeba matatizo yote yaliyoachwa na Bush.

Ni bahati mbaya vilevile kwamba baadhi ya maswahiba na watu wa karibu waliomsaidia Kikwete katika kampeni iliyomwingiza Ikulu mwaka 2005, wamo katika orodha ya mafisadi waliochota fedha hizo, na inasemekana sehemu ya fedha hizo zilitumbukizwa katika kampeni iliyompa yeye ushindi.

Kutokana na mwamko wa baadhi ya vyombo vya habari, NGOs na vyama vya siasa, na pia kutokana na kuimarika kwa teknolojia ya mawasiliano na upashanaji habari, sasa Watanzania wengi, mijini na vijijini, wanaujua ukweli kuhusu EPA. Na wanataka haki itendeke kwa wahusika wote kufikishwa mahakamani.

Rais, baada ya tafakuri jadidi, ameridhia baadhi wapelekwe mahakamani, lakini kilio cha wananchi ni kuona vigogo wote wa wizi wa pesa hizo wanafikishwa mahakamani na si wateule wachache ambao ni vijidagaa.

Yeye amesema ameliachia suala zima Idara ya Mashitaka (DPP); kwani ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba. Haifahamiki kama DPP naye atafanya tafakuri jadidi na hatimaye kuwafikisha pia mahakamani vigogo wote ambao bado hawajafikishwa.

Asipofanya hivyo, EPA bado itaendelea kumzonga Rais Kikwete; kwani kama nilivyosema mwanzo, wananchi wanataka haki itendeke kwa wote.

Aidha, kesi hizo zitakapoanza kusikilizwa haifahamiki itakuaje iwapo mmoja wa watuhumiwa atataka Rais aliyekuwa madarakani kipindi wizi huo ukitokea; Benjamin Mkapa, aitwe mahakamani kutoa ushahidi; au endapo mtuhumiwa mmoja ataamua ‘kumwaga yote hadharani”. Vyovyote vile, haya ni mazingira magumu kwa Rais na chama chake cha CCM.

Ni mazingira ambayo yangemkosesha raha mtu yeyote ambaye angekuwa amevaa viatu vya Kikwete wakati huu. Lakini kama vile skandali hiyo ya mafisadi haitoshi kumnyima raha, yapo pia matatizo mengine kibao yanayoiandama Serikali yake ikiwemo migomo ya walimu, migomo ya vyuo vikuu, madai ya wastaafu wa EAC, nikitaja machache. Na hata ndani ya chama chake CCM, mambo si shwari.

Kama vile pia hayo nayo, katika ujumla wake, hayatoshi kumnyima usingizi; limekuja tatizo jingine la kidunia ambalo halikutarajiwa kabisa – tatizo la anguko la uchumi wa dunia ambalo asili yake ni kusambaratika kwa mfumo wa kifedha wa Marekani.

Athari kwa Tanzania kutokana na tatizo hilo, kama mwenyewe Rais Kikwete alivyoeleza kwenye hotuba yake kwa Taifa, Oktoba 31, ni kupungua nchini kwa mapato yanayotokana na utalii, ni kupungua kwa mauzo yetu ya nje, ni kupungua kwa mikopo ya kibiashara, na kupungua kwa uwekezaji kutoka nje.

Lakini zaidi ya yote ni kupungua kwa misaada tuliyokuwa tukiitegemea sana kutoka kwa wahisani wa nje – Marekani , Uingereza na nchi kadhaa za Ulaya. Vilevile ni kupungua au kutoweka kabisa kwa mikopo tuliyokuwa tukipata kutoka vyombo vya fedha vya kimataifa kama WB na IMF.

Na hili la kupungua kwa misaada kutoka kwa ‘wajomba wa Ughaibuni’ halina mjadala. Kama Serikali yenyewe ya Marekani sasa ina deni linalofikia dola trilioni 10, itafikiriaje kuendelea kuzisaidia nchi masikini kama yetu? Vivyo hivyo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na hata nchi za Scandinavia.

Na kama athari za anguko hilo la uchumi kwa nchi yetu ni hizo ambazo Rais alizitaja katika hotuba yake ya Oktoba 31, maana yake ni kwamba kutakuwa na nakisi kubwa mno katika bajeti ya Serikali yetu; kwani mapato yetu ya pesa za kigeni yatapungua na hata makusanyo ya ndani ya kodi nayo yatapungua.

Katika mazingira hayo ya nakisi kubwa katika bajeti, zitapatikana wapi pesa si tu za kuwalipa wote wanaodai malimbikizo yao au nyongeza zao za mishahara (walimu, madaktari n.k), lakini hata za kuendesha shughuli za kimsingi za Serikali kama vile ulipaji mishahara na utoaji huduma za jamii?

Kwa sababu ya nakisi hiyo, na kwa sababu sasa Watanzania wameamka na wanajua jinsi ya kushinikiza kudai haki zao, tutashuhudia ongezeko la maandamano na migomo katika kipindi ambacho athari za anguko la uchumi wa dunia zitakapotugusa kweli kweli hivi karibuni.

Serikali yetu itatakiwa kulipa hiki na kile wakati pesa hakuna. Hakika, hayo ni mambo yatakayomwongezea Rais Kikwete ugumu wa kutawala na kumkosesha raha. Anaweza hata kulaani ni kwa nini anguko hili la uchumi wa dunia ambalo ni la kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 70, limekuja wakati yeye ni Rais! Atajiuliza ni kwa nini halikungoja amalize kipindi chake cha utawala?!

Lakini, kama nilivyosema mwanzo, ili sote tuweze kukivuka kipindi hiki kigumu katika historia ya Taifa letu, inahitajika uongozi na si utawala. Unahitajika uongozi wenye hekima, busara na uvumilivu si tu kwa Rais Kikwete; lakini pia kwa Watanzania wote.

Sote tunajua kwamba, kwa hulka yetu binadamu, matatizo yakizidi yanajenga gadhabu, na matunda ya gadhabu ni maamuzi yasiyo na hekima au busara ndani yake.

Kipindi kama hiki cha kwetu cha matatizo makubwa kilipata kujenga gadhabu kwa watawala kwingineko duniani, na gadhabu hizo zikabadilisha marais waliokuwa wapole na waadilifu kuwa madikteta!

Huwa inakuwa hivi: Serikali ikiishiwa majibu ya matatizo ya wananchi, watatoka court jesters (walamba miguu ya watawala) na kumshauri Rais huyo mwadilifu na mpole kwamba tatizo si EPA, wala si kukithiri kwa ufisadi; bali ni baadhi ya vyombo vya habari, na kwamba hatua sahihi ni kuwanyamazisha kwa kuvifungia vyombo hivyo na kuwakamata wahariri na waandishi.

Rais mwenye gadhabu iliyotokana na kuzongwa na matatizo ya nchi, na aliyeishiwa na uvumilivu, atawasikiliza court jesters hao na kuridhia hatua hiyo isiyo ya busara waliyoipendekeza, hatua ambayo inaweza kuiingiza nchi kwenye udikteta!

Mathalan, kama hapa kwetu nchini tatizo kubwa linalomkosesha raha Rais litakuwa ni EPA, watatokea court jesters walio karibu na watuhumiwa hao na kumwambia Rais kuwa wanaochochea tatizo hilo ni magazeti kadhaa. Na watamshauri kuyafungia magazeti hayo, na hata kuwakamata waandishi; huku wakidai kuwa magazeti hayo ni ya uchochezi na hivyo yanahatarisha ‘usalama wa taifa’; wakati tatizo ni EPA, si magazeti.

Yaani watajaribu kutunyamazisha akina sisi wa vyombo vya habari wakitumia kisingizio cha ‘usalama wa taifa’. Kisingizio hicho huwa kinatumiwa kote Dunia ya Tatu na watawala wanaoishiwa njia za kutatua matatizo ya wananchi wao.

Na iwapo itatokea Rais kuwasikiliza court jesters hao na kufanya hivyo watakavyomshauri; yaani kufungia magazeti na kukamata waandishi, basi, tutakuwa hatuko mbali sana kuufikia udikteta.


Ndugu zangu, kuliko wakati mwingine wowote, nchi yetu inapitia kipindi kigumu mno hivi sasa. Tumwombe Mungu amjazie Rais wetu Kikwete na Watanzania wote hekima, ujasiri na uvumilivu tuweze kuvuka salama kipindi hiki kigumu tunachokipitia katika historia ya Taifa letu; ili hilo lisitokee na kuiingiza nchi yetu katika udikteta.

Email: mbwambojohnson@yahoo.com
 
Back
Top Bottom