Nukuu kutoka mkutano wa wabunge na asasi za kiraia (AZAKI)

Sophist

Platinum Member
Mar 26, 2009
4,484
3,400
Ndugu,
Tafadhali soma hizo nukuu za waheshimiwa wabunge wa Bunge letu tukufu, halafu wasilisha maoni yako.
wasalaam.


NUKUU KUTOKA MKUTANO WA WABUNGE NA ASASI ZA KIRAIA (AZAKi)

Mahali: Dodoma Hotel, Dodoma, Tanzania

Tarehe: Aprili 23, 2009

Utangulizi
Tangu 2003 Asasi ya The Foundation for Civil Society (FCS) imekuwa ikiongoza jitihada za mashauriano ya kuanzishwa ushirikiano rasmi baina ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na AZAKi. Kilele cha mashauriano ya Juni 2008 baina ya Bunge na AZAKi, kupitia FCS, kiliweka bayana kuwa ni muda muafaka kurasmisha mahusiano baina yao. Kwa kuzingatia hilo, Aprili 23, 2009 FCS iliandaa na kuwezesha mkutano wa mashauriano ya awali juu ya namna Bunge na AZAKi wanaweza kuanzisha na kuendeleza mahusiano rasmi. Mkutano husika ulifanyika kama ilivyopangwa, Dodoma Hotel. Mwenyekiti wa mkutano huo alikuwa Mhe. Jenesta Mhagama, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii. Mkutano ulianza saa 8 mchana. FCS iliandaa rasmu 2 kwa ajili ya majadiliano: Mapendekezo ya AZAKi juu ya Kuimarisha Mahusiano ya na Bunge kwa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge na Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii 23/04/2009, Dodoma; na Waraka wa Makubaliano ya Ushirikiano [Memorandum of Understanding (MoU)] Kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na AZAKi Tanzania.

Mahudhurio
FCS ilialika AZAKi kadhaa kutoka Dar es Salaam na Dodoma kuwakilisha AZAKi nyingine nchini. Jumla ya AZAKi zilizoalikwa haikuzidi 15. Bunge liliwakilishwa na wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Makatibu wa Kamati hizo, Mawaziri na Ma-Naibu Waziri, wafanyakazi wa Bunge, pamoja na Maofisa wa offisi ya Msajili wa NGOs (serikali).

Nukuu
Zifuatazo ni nukuu za washiriki wa mkutano huo, hususan wabunge. Mkurugenzi Mtendaji wa FCS alizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa AZAKi. Maoni/mawazo ya Wabunge yananukuliwa na mwandishi wetu kama ifuatavyo hapo chini:

Mh. Job Ndugai
· Tayari Bunge limetoa fursa kadhaa kwa AZAKi kushirikiana na Bunge, mfano public hearing.
· Bajeti ya serikali ni siri (siyo rahisi na wala haipaswi kufahamika mpaka isomwe Bungeni.
· Hata hivyo, AZAKi zimekuwa zikipotosha hoja mbalimbali za wabunge kwa wananchi – Policy Forum kwa mfano, imekuwa ikipotosha sana wananchi kuhusiana na CDF. Wanapotosha! Wamelipia tangazo TBC1. Tangazo hili limelipiwa kwa muda mrefu na linaendelea kupotosha. Linatangazwa muda mfupi kabla ya taarifa ya habari ya TBC1. Huu ni upotoshaji. Sasa tutashirikianaje na AZAKi ikiwa wanaendelea kutupiga vita namna hii? Huu utakuwa ni ushirikiano wa namna gani?

Mh. Kapuya
· Bajeti, kujadiliwa hadharani! Kwa utaratibu wa serikali zote duniani – haifanyiki hivyo – haiwezekani.
· Majadiliano mengine biana ya AZAKI na Bunge kuhusiana na Bajeti yatahitaji muda mwingine zaidi ya miezi 3. Kujadiliana na kukubaliana nadani ya muda mfupi inaweza kuwa vigumu.

Mh. Lubeleje
· Zamani hakukuwa na public hearing; badaye ilipotokea haja ya kufanya hivyo, “tuliruhusu.”
· Bajeti – kama walivyosema waliotangulia [haiwezekani kujadiliwa hadharani na AZAKi].
· Miswada ina taratibu zake (mlolongo), hii inaweza kuwa ngumu kama miswada itajadiliwa na AZAKi baada ya kujadiliwa na kamati husika.
· Shukrani – kwa kazi zenu, AZAKi, ahsanteni sana.

Mh. Ruth Nkya:
· Uwakilishi unaonekana kuwa ni haba, mikoa mingine haijawakilishwa. Ushiriki ufanyike kupitia kanda zote – kanda 4.
· Makubaliano haya ni ya kisheria/nashauri kuwa wabunge wote sharti washiriki kujadiliana na kukubaliana.
· Bajeti – Bajeti za serikali ziwe wazi, sawa, lakini mbona Bajeti za AZAKi hazijatakiwa kuweka Bajeti zao wazi kwa Serikali? Mabadiliko yanatakiwa kufanyika.
· Bajeti huanzia ngazi ya kijiji, kata, halmashauri za wilaya hadi ngazi ya wizara (taifa). AZAKi waboreshe Bajeti kupitia ngazi za chini, kuishia ngazi ya wilaya.
· AZAKi nyingine zinalalamikiwa na wananchi. Utawala bora dani ya AZAKi uwekwe wazi. Ubainishwe na kutajwa kama eneo la makubaliano haya kati ya Bunge na AZAKi – iwapo yatapitishwa.

Mh. Kwang
· Mapendekezo mengi yanagusa Katiba ya nchi. [Mapendekezo ya makubaliano] ..”kama bunge kupitia kwa AZAKi lifanye mrejesho wa utekelezaji…”, yanahitaji mjadala mpana zaidi ili kuangalia maeneo mahsusi ya kushirikiana.
· Kanuni [za Bunge] zinabainisha utaratibu wa kushiriki kwenye mikutano ya public hearings.
· Miswada ya sheria; baada ya first readings inakuwa public document.
· Kuiweka saini [katika hati ya makubaliano] - sina uhakika kuwa utaratibu huu upo sehemu nyingine duniani.
· Maonesho ya AZAKi yamekuwa yakifanyika hapa Dodoma kwenye viwanja vya Bunge, lakini maonesho hayo ni kwa Wabunge tu? Wadau, wengine je? Maonesho yapanuliwe.

Mh. Mwenyekiti
· Upanuzi wa (maonesho) huende hadi kwa madiwani [ngazi ya halmashauri za wilaya].
· AZAKi kuunga mkono CDF [kama alivyosema Mh. Ndugai] ni muhimu katika mashirikiano yetu. CDF ni mpango mzuri, utafaa kusaidia wananchi kuondokana na umaskini.
· CDF itawaondolea wananchi matatizo

Mh. Mwenyekiti:
· Katika makubaliano yetu ya 2008, ilikuwa kwamba FCS iratibu nakushauri kuhusu CDF; mbona kwenye MoU hakuna?

Mh. John Komba:
· CDF iko wapi? AZAKi zimekuwa zinapinga kwa nguvu sana dhidi ya CDF!
· AZAKi wanamwakilisha nani?
· AZAKi wanapinga harakati za wabunge majimboni!

Mh. Mwenyekiti
· Anachosema Mh John Komba ni kwamba AZAKi zikiunga mkono CDF Wabunge nao wataunga mkono makubaliano haya.

Mh. Msumi:
· AZAKi wako karibu zaidi na wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto. Mahusiano baina ya AZAKi na wizara yaimarishwe kwanza kabla ya kuimarisha mahusiano na Bunge.
· Bunge ni Chombo cha uwakilishi.
· Inakuwaje AZAKi zifanye shughuli wilayani wakati mbunge haina taarifa? Huu ndio uhusiano unaotakiwa kati ya mbunge na AZAKi?
· CDF-wabunge wawezeshwe kutoa “financial support” kwa wananchi wapohitaji misaada wakati wa mikutano ya hadhara au wananchi mmoja mmoja kama ilivyo kwa Ma DC na Ma RC.
· AZAKi wasafishe hali ya hewa kwanza [wakubaliane na wabunge kuhusu CDF] kabla ya Bunge kusaini makubaliano ya mashirikiano na AZAKi.

Mh. Anna Lupembe:
· AZAKI, hawatekelezi, hawana hamara kwa wananchi.
· Rukwa hakuna AZAKi. Hazionekani kuhamasisha wananchi kuhusu watoto yatima, wanaoishi na virusi vya ukimwi (WAVIU), wazee na kadhalika.
· AZAKi wanafanyaje kutatua matatizo ya wananchi?

Mh. Joel Bendera:
· Ushauri: kwa yale yote yaliyozungumzwa na waheshimiwa wabunge, FCS ichukue serious note.
· AZAKI wanaweza kuchukua jukumu la kuwa washauri – lengo ni kuwakomboa wanananchi dhidi ya umaskini.
· Taratibu za kuendesha Bunge, serikali, mahakama zisiingiliwe.
· Tukae tuangalie namna ya kushirikiana kabla ya kufika mbali.

Mh. Bujiku Sakila
· AZAKI zinakaribishwa kwenye jimbo langu – sitarajii kuwa zitanivurugia.
· Tatizo: AZAKi zinahitaji vyanzo vya fedha. Wafadhili wengine hawana nia njema na serikali – wanapenda kuchokonoa. AZAKi wanatakiwa kuwa makini na [hila za] wafadhili wao. Wafadhili wanapenda kupenyeza mambo yao na utamaduni wao kupitia ufadhili.

Mh. Mkuchika:
· AZAKi ziko za aina 2: local na international
· AZAKi za kimataifa hawataki kwenda katika maeneo ya periphery yaani pembezoni.
· Mimi ni chairman wa Newala Development Foundation. FCS imetupatia pesa tumejenga barabara. Tunashukuru.
· Machapisho yanatakiwa kuandaliwa kwa Kiingereza; [Kwa machapisho haya ya FCS] Kiswahili kilistahili kutumika ili kila Mtanzania aweze kusoma na kufahamu yaliyomo.

Mh. (Viti maalum CCM)
· Angalizo: Bajeti ni siri; wafanyabiashara wanaweza kula njma na kupandisha bei iwapo watajua matarajio ya mapendekezo ya bei za bidhaa kadhaa yaliyomo ndani ya bajeti kabla ya bajeti kutangazwa [fiscal policy].

Mh. Misanga
· Kunatakiwa kuwa na vision ya pamoja kama tunataka kushirikiana.
· CDF ni kama point of departure. AZAKi hawaungi mkono CDF kabisa. Angalia yaliyoandikwa ukurasa wa 20 katika chapisho la FCS. [Anasoma na kunukuu baadhi ya maandishi katika ukurasa wa 20; Newsletter 2008 July – September].
· Haya maneno siyo kweli kabisa! Kwamba wananchi wamepoteza imani na wabunge na serikali yao! Hapana hili siyo kweli! FCS inatakiwa kuwa inahariri vizuri machapisho yake.

Vice Chairman:
· Tumekwisha kubaliana kuwa Kiswahili kitumike katika semina na mawasiliano yote kwa umma.
· CDF ni hatua na njia nzuri sana ya kuwakomboa wananchi.
· Katibu wa Bunge atashauriana na Kamati (Maendeleo ya Jamii)

J. Ulanga:
· Lengo la mkutano huu lilikuwa kuanzisha mjadala, siyo maamuzi [kuamua mapendekezo ya kushirikiana] – hili limefanikiwa.
· Mapendekezo yote [ya awali] tayari yanatekelezwa na mapendekezo yote ya wabunge [katika mkutano huu] yatafanyiwa kazi.
· Lengo letu ni kuendelea kushauriana na hatimaye tukubaliane. Ni kwa njia hii tutaweza kufanya kazi pamoja [badala ya kutuhumiana].

Mwenyekiti [Way Forward]
· Tuendeleze lengo la awali na hatimaye kufikia ushirikiano kamili [bsins ya AZAKi na Bunge].
· Hoja imechukuliwana. Kamati ya Maendeleo ya Jamii itaiwasiliana hoja hii katika Ofisi ya Spika na hatimaye kuamua juu ya jambo la kufanya.
· Kamati [Maendeleo ya Jamii] itaandaa utaratibu wa kuwezesha wabunge wote kujadili mapendekezo ya mashirikiano kabla ya kukubali au kukataa ushirikiano rasmi na AZAKi.
· Wakati mwingine makablasha yawe yanawasilishwa mapema kwa waheshimiwa wabunge ili waweze kusoma yaliyomo [nyaraka husika] kabla ya majadiliano kuanza.
· Ahsanteni.
 
Back
Top Bottom