Lizaboni
JF-Expert Member
- Feb 21, 2013
- 33,894
- 20,375
Weekend hii niliwasili Dar es Salaam kwa shughuli zangu za kibiashara. Nikaamua kutumia nafasi hiyo kutembelea Daraja la Mwalimu Nyerere ili kuona jinsi mfumo wa malipo unavyofanya kazi. Kwa hakika nimeshuhudia mfumo unaenda vema na kwa muda nilioenda, hakukuwa na foleni kutoka Kurasini kwenda Kigamboni badala yake kulikuwa na kafoleni kadogo kutoka Kigamboni kwenda Kurasini.
Hata hivyo, pamoja na uzuri wote huo, kuna jambo kubwa sana nimeliona ambalo ama limefanywa kwa makusudi ama kwa bahati mbaya. Wakati Rais anafungua daraja lile baada ya ujenzi kukamilika, alituambia kuwa litaitwa Daraja la Mwalimu Nyerere. Hii ni kwa lengo la kumuenzi mwasisi huyo wa taifa letu ambaye aliweka azma ya kujenga daraja hilo ila alishindwa kufanya hivyo kutokana na kukosa fedha.
Pamoja na kwamba imepita muda sasa tangu daraja hilo lifunguliwe, TRA na NSSF hawajui kuwa daraja hilo linaitwa Mwalimu Nyerere Bridge. Wao mpaka sasa wanalitambua kwa jina la Kigamboni Bridge. Imenisikitisha na imenihuzunisha na sijui nini hatua za kuwachukulia watu wanaopuuza agizo na tamko la Rais kwa makusudi. Risiti wanazotoa zinaonesha kuwa daraja hilo ni la Kigamboni na si la Mwalimu Nyerere. Kuna ugumu gani wa kubadilisha jina?
Aidha, kilichonishangaza zaidi ni kwamba hakuna bango lolote linalotambulisha wapi daraja lilipo hasa kwa sisi wageni tunaokuja kushangaa kwa mara ya kwanza. Kwa maoni yangu, kwa vile daraja hilo ni kitega uchumi, ni vema wakaweka Bango kubwa pale kwenye taa za UHASIBU yaani zinapokutana barabara za Kilwa na Mandela. Bango hilo pia lioneshe mwelekeo wa daraja lilipo. Bango kama hilo pia linaweza kuwekwa pale Ubungo na TAZARA hali itakayorahisisha kwa wageni kwenda moja kwa moja darajani bila ya kuuliza. Kwenye mabango hayo, waoneshe pia umbali wa daraja lilipo kutoka katika kila bango. Kwa nchi za wenzetu ndivyo wanavyotumia.
Otherwise, nachukua fursa hii kuipongeza serikali yangu ya CCM kwa kushirikiana na NSSF kwa kujenga daraja kubwa na zuri ambalo hakika ni urithi wa taifa letu.