Nondo za CHADEMA leo bungeni kuitaka serikali iwajibike kutengeneza fursa za maendeleo ya vijana

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,070
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH MBILINYI KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KURIDHIA MKATABA WA VIJANA WA AFRIKA (AFRICAN YOUTH CHARTER) LA MWAKA, 2006
Mheshimiwa Spika,naomba kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu azimio tajwa hapo juu kwa mujibu wa kanuni za Bunge kanuni ya 86(6), toleo la mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika,
kwakuwa hii ni mara yangu ya kwanza kwa mwaka huu wa 2012 naomba kutoa salaam za mwaka mpya kwa waheshimiwa wote waliopata bahati ya kuingia mwaka huu salama na pia kuwapa pole wale wote waliopatwa na maswahibu ambayo yako nje ya uwezo wao. Aidha ni washukuru wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya hasa wale wa Jimbo la Mbeya Mjini kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatika katika kuijenga upya Mbeya yetu. Nawaomba mwaka huu ushirikiano uzidi ili maendeleo yapatikane kwa haraka.

Mheshimiwa Spika,
azimio hili ni muhimu sana hasa wakati huu ambapo vijana wa taifa hili wanakabiliwa na changamoto nyingi sana za maisha katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.

Mheshimiwa Spika,
kwa sababu tupo kwenye mchakato wa maandalizi ya kupata Katiba mpya na bora kwa maslahi ya Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, kidini, kikanda au ubaguzi wa aina yoyote ule ni vizuri sasa kuwe na utaratibu wa kufanya mikataba ya kimataifa kama huu wa leo kuanza kutumika pale tu serikali inapousaini.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu utawezesha serikali kujipanga na kufanya tathmini ya kina juu ya mikataba hii kabla ya kuisaini na pia utasaidia kuondoa utaratibu unaolalamikiwa kila mara kwa serikali kuchelewesha mikataba ya kimataifa ambayo ni muhimu kwa ustawi wa jamii yote. Hii inadhihirika katika mkataba huu ambao umesainiwa Nov. 2008 na leo ni zaidi ya miaka mitatu imeshapita bila mkataba huu kuletwa katika Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayo maoni yafuatayo kuhusu mkataba wa vijana wa Afrika.

i. Haki ya kumiliki mali

Mheshimiwa Spika, haki hii ipo katika ibara ya 9 ya mkataba huu ambapo kila kijana ana haki ya kumiliki au kurithi mali na kuhakikisha kuwa vijana wote wa kike na wa kiume wana haki hiyo kama ilivyoainishwa bila ubaguzi wa aina yoyote ule.

Mheshimiwa Spika, ni rai ya kambi rasmi ya upinzani kuwa serikali inazingatia masharti ya ibara hii kwa sababu ipo tabia ambayo imekuwa ikilalamikiwa sana na vijana ambapo mamlaka za serikali za mitaa wamekuwa na tabia ya kuwanyanyasa sana Wamachinga ikiwa ni pamoja na tuhuma za baadhi ya askari kuwapora au kuharibu bidhaa za vijana wanaojihusisha na biashara ndogondogo, na hata baadhi ya vijana hao kupoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, hali hii inajitokeza sana katika miji mikubwa hapa nchini kama jiji la Mbeya ambapo kulitokea vurugu kubwa kati ya wafanyabiashara wadogo wadogo na mamlaka za serikali. Pia katika Jiji la Dar es Salaa hali kama hii hujitokeza mara kwa mara mathalani pale Manispaa ya Kinondoni ilipobomoa soko la Big Brother usiku wa manane na kusababisha mali nyingi kupotea na mpaka leo vijana wale hawajalipwa fidia kwa uharibifu huo.

Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kuheshimu matakwa ya ibara hii ikiwa ni pamoja na kuboresha na kutenga maeneo rasmi kwa kuwashirikisha kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ambao kimsingi wengi wao ni vijana ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikitokea katika sehemu mbalimbali hapa nchini.

ii.
Maendeleo ya vijana

Mheshimiwa Spika, changamoto za vijana kimaendeleo ni nyingi sana na juhudi za kupunguza na hatimaye kuziondoa zinaonekana kutokuwekewa mkazo na serikali. Hii ni pamoja na kuwepo kwa wimbi kubwa la vijana mijini na vijijini kutokuwa na ajira na kushindwa kujiajiri.

Mheshimiwa Spika,
kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kuja na mpango mkakati wa dharura hapa Bungeni kuhusu tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwa huu sasa si wakati wa porojo za maisha bora kwa kila mtanzania wakati kila kukicha vijana wengi wanashinda vijiweni bila ajira. Hili ni bomu linalosubiri kulipuka kama serikali haitachukua hatua za dharura kuwanusuru vijana na tatizo hili.

Mheshimiwa Spika,
kambi ya upinzani inaitaka serikali kuweka mkazo wa kufufua viwanda vingi ambavyo vilikabidhiwa kwa wanaoitwa wawekezaji ambao wameathiri moja kwa moja uzalishaji wa awali na hivyo kufanya ajira nyingi sana kupotea, mathalani, kiwanda cha zana za kilimo (ZZK) Mbeya,kiwanda cha nguo cha Mbeya (Mbeya Textile mill), kiwanda cha nguo cha urafiki, kiwanda cha mbao cha Mkumbara na viwanda vingi mkoani Tanga ambavyo vimezorota sana kama sio kufa kabisa, na vingine kugeuzwa maghala ya kuhifadhia pombe.

Mheshimiwa Spika,
bila kuwa na mpango mkakati wa kuunusuru uchumi wetu kwa kuongeza uzalishaji katika viwanda, kilimo na sekta zingine ni wazi tatizo la ajira halitapungua na litazidi kuongezeka. Katika mpango mkakati huo ambao tunaitaka serikali kuuleta ni vizuri wazingatie ndani yake ni namna gani ya kuleta mabadiliko ya uchumi yanayoendana na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

iii.
Haki ya kupata taarifa

Mheshimiwa Spika, ibara ya 10 (3)(a) ya mkataba huu unaitaka serikali kuhakikisha vijana wanapata habari kila wakati kuhusu mambo mbalimbali yanayotokea hapa nchini na kimataifa. Hili linahitajika kwa kuvishirikisha kwa karibu vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoitaka serikali kuacha vitisho kwa vyombo vya habari kwenye hotuba yetu mbadala wakati wa Bunge la bajeti mwaka jana kwa wizara hii, kambi rasmi ya upinzani tunarudia tena kuwa ni wazi masharti ya ibara hii hayatatimia kwa sababu pamoja na kueleza sikitiko letu kwa serikali kulipa gazeti la Mwananchi vitisho gazeti la mwananchi, bado Serikali imeenda mbali zaidi kwa kuwakamata wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa makala ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wanatimiza wajibu wao wa kuwapa taarifa wananchi wakiwemo vijana.

Mheshimiwa Spika,
kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kufuta/kufanyia marekebisho sheria zote ambazo sio rafiki kwa vyombo vya habari kama vile sheria ya usalama wa taifa, na pia sheria ya magazeti ambayo imekuwa ikipigiwa kelele siku hadi siku na wadau wa habari.

iv. Masuala ya elimu

Mheshimiwa Spika,
mkataba huu pia unaitaka serikali kuwapa elimu vijana na kuwawezesha kujua haki zao za msingi lakini kubwa zaidi ni kuwapa elimu hiyo katika mazingira ya kidemokrasia ili kupata ujuzi na pia kuwajengea uwezo wa kujiamini katika masuala mbalimbali kama inavyoelezwa katika ibara ya 10(3)(d).
Mheshimiwa Spika, imekuwepo tabia ya serikali kutumia nguvu kubwa na kufanya maamuzi ambayo sio mazuri kujenga mazingira ya kidemokrasia katika taasisi zetu za elimu hususani ya vyuo vikuu.

Mheshimiwa Spika,
hivi sasa mamia ya wanafunzi wa elimu ya juu wapo nyumbani kwa kusimamishwa au kufukuzwa vyuoni kwa sababu ambazo kwa namna moja au nyingine unaendeleza tabia ileile ya serikali kushughulikia matokeo badala ya kiini cha matatizo. Kwa sababu badala ya kutatua matatizo yanayowakumba wanafunzi kama vile kukosa au kucheleweshewa mikopo kutoka bodi ya mikopo na matatizo ya malazi; bado serikali imekuwa ikiwafungulia mashtaka na pia kuwafukuza wanafunzi kwa sababu za kisiasa huku wakisingizia baadhi ya vyama vya siasa kuwa ndio chanzo badala ya kuzingatia uhalali wa madai ya vijana hao wanavyuo.

Mheshimiwa Spika,
kambi rasmi ya upinzani inaitaka wizara ya elimu kuwarudisha wanafunzi wote waliofukuzwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Dodoma, Chuo kikuu cha tiba cha Muhimbili kwa sababu kwa kuwaacha wanafunzi hao mtaani sio suluhisho la matatizo katika taasisi za elimu ya juu nchini lakini pia ni kinyume na mkataba huu ambao unataka mazingira ya kidemkrasia katika kutoa elimu.

Mheshimiwa Spika,
mkataba huu pia unaitaka serikali kutoa elimu bora ambayo itawapa vijana ujuzi baada ya kuipata kama ilivyoainishwa katika ibara ya 13(1). Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuondoa dhana iliyojengeka ya ubaguzi wa kitaasisi katika shule zetu za sekondari na msingi kwa sababu kwa sasa hivi kuna tofauti kubwa sana kati ya shule za sekondari maarufu kama shule za kata na shule za watu binafsi katika ubora na ufaulu.

Jambo hili la tatizo la ubora wa elimu pia lipo katika shule za msingi ambapo ni kawaida kwa maeneo mengi hapa nchini kukuta watoto wetu wanakaa chini kwa kuwa shule zetu hazina madawati. Serikali inatakiwa kuzingatia masharti ya ibara hii kwa kutilia mkazo kutoa elimu bora na sio bora elimu ili kutoa elimu inayokidhi ustawi wa jamii.


Mheshimiwa Spika,
kambi rasmi ya upinzani tunaitaka serikali kutenga rasilimali za kutosha kwenye elimu kama ambavyo inaelekezwa katika ibara ya 13(4)(i) ya mkataba huu na kuhakikisha rasilimali hizo zinasimamiwa vilivyo ili kuweza kukidhi malengo yake na kuondoa ufisadi katika miradi mbalimbali katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika; kwenye Azimio la Serikali kuhusiana na mkataba huu imeelezwa kuwa katika mchakato wa kuridhia mkataba wa vijana wa Afrika, Serikali imebaini kwamba masharti ya ibara 13 (4) (h) hayakubaliki katika mazingira ya Tanzania. Masharti hayo ni yale yanayoruhusu vijana wajawazito au walioolewa kuendelea na masomo na kwamba serikali imeeleza kuwa masharti hayo ni kinyume cha sera za nchi ya Tanzania na mazingira yetu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa maelezo ya ziada kuhusu sababu ambazo serikali imezieleza kwa Umoja wa Afrika (AU) pamoja na bunge kupatiwa nakala ya vielelezo vilivyowasilishwa. Aidha, serikali ieleze iwapo katika kufanya uchambuzi juu ya kifungu husika ilipata maoni ya wadau wa msingi wanaosimamia masuala ya haki za vijana wa kike nchini. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza bungeni kuhusu maandalizi ya mfumo maalum kwa ajili ya kuwawezesha vijana wa kike waliojifungua kuweza kupata haki ya elimu na kulinda haki zao za kijinsia.

v. Ushirikishwaji wa vijana

Mheshimiwa Spika, mkataba huu katika ibara ya 11(2)(a) umeweka mkazo na sharti kwa serikali kuwashirikisha vijana katika shughuli mbalimbali za kila siku hii ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha vijana ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa ajira au elimu kutoa mawazo yao moja kwa moja na hivyo kuwa sehemu ya maamuzi ya mambo mbali yanayowahusu moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa ushiriki wa Vijana Bungeni utakuwa na tija kwa mujibu wa Ibara tajwa kama, Serikali itazingatia kubadili mfumo wa uchaguzi ili kuwa na mfumo wa uwakilishi wa uwiano (proportional representation) na hivyo kupanua wigo wa uwakilishi wa vijana Bungeni na kwenye vyombo vingine vya maamuzi.

vi. Benki ya vijana

Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa kwenye mkataba huu ibara ya 11(2) (g) unaitaka serikali kuwawezesha vijana kifedha na kuwajengea uwezo ni wakati mwafaka sasa kwa serikali kuzingatia maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuanza rasmi mchakato wa kuanzisha benki ya vijana ili kukidhi masharti haya.

Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani tunatoa msisitizo kwa serikali kuwa, benki hiyo ya vijana itakayoanzishwa iwe ya vijana wote kama jina linavyosadifu na ambayo haitawabagua vijana kiitikadi ili kuweza kuwajengea uwezo kifedha na hivyo kuwakwamua kiuchumi.

vii. Sera ya vijana

Mheshimiwa Spika, sera ya sasa ya vijana ya mwaka 2007 ina utofauti mkubwa sana na masharti ya mkataba huu ambao unaridhiwa na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na serikali kukataa masharti ya ibara ya 12 (1)(h) kuhusu Bunge kutunga sera na baadae kuwa na sheria itakayoendana na mkataba huu kuhusu sera ya maendeleo ya vijana. Kambi ya upinzani tunaitaka serikali ifanye mapitio (review) ya Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ili iendane na hali halisi ya vijana na taifa kwa sasa pamoja na masharti ya mkataba wa vijana tunaoridhia. Aidha, serikali ilete bungeni muswada wa sheria kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa wa sera hiyo pamoja na masharti ya mkataba wa vijana Afrika. Bila sheria matamko ya sera na mkataba huu yatabaki kuwa maneno matamu bila matendo ya kubadili maisha ya vijana hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

viii.
Baraza la vijana

Mheshimiwa Spika, umepita muda mrefu sana toka kambi rasmi ya upinzani pamoja na wanaharakati wa masuala ya vijana kuitaka Serikali kuanzisha baraza la vijana ambalo kwa namna moja au nyingine utawapa fursa vijana kuwa pamoja na kuweza kutoa maoni yao kwa pamoja bila kuingiliwa na itikadi za vyama vya siasa. Kwa kuwa ibara ya 12 (i) ya Mkataba huu wa vijana inataka serikali kuanzisha mpango utakaoratibu namna ya kuwaunganisha vijana, ni wakati mwafaka kuanzisha baraza hilo ili kuwapa vijana chombo watakachotumia kujadili mambo yao mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru waheshimiwa wote kwa kunisikiliza, na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.........................................
Joseph O. Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo.
01.02.2012



 
tatizo najua magamba hawatekeleza hayo.hongera mbilinyi.hongera kambi rasm ya upinzani munaona mbali tatizo serikali.
 
Vijana wanaweza,Tz itajengwa upya na vijana,uongozi ni kipaji thx Sugu,kazeni mliopo ndani na mfunge ule mlango wa wazee 2015 ibaki milango miwili tu ya vijana na wanataaluma wa ukweli wenye mapenzi mema na taifa letu
 
Mh! Hakuna hata RIP kwa Regia Mtema?! Ingekua vyema mwanzo wa hotuba,yangesemwa maneno ya kumkumbuka Regia na kumwomba Mwenyenzi Mungu aendelee kumpumzisha kwa amani.

Anyway,hotuba ina mambo mengi ya msingi juu ya vijana. Pia imeonyesha ni kiasi gani serikali hisivyo makini katika kutatua kero za vijana. Haiwezekani mkataba uliosainiwa mwaka 2008 uje leo bungeni kuidhinishwa!
 
CHADEMA Bana! muwe fair, mmeweka hotuba ya kambi rasmi ya upinzani lakini utekelezaji wa hotuba hiyo unatokana na hotuba rasmi ya upande wa serikali iliyowasilishwa na Nchimbi pamoja na hotuba ya mwenyekiti wa kamati. Leteni na hotuba hizo ili tuchangie kwa ufasaha.
 
daaah hivi haya mambo kuna team maanlumu huwa inayaandika eeeh mweeee.
 
CHADEMA Bana! muwe fair, mmeweka hotuba ya kambi rasmi ya upinzani lakini utekelezaji wa hotuba hiyo unatokana na hotuba rasmi ya upande wa serikali iliyowasilishwa na Nchimbi pamoja na hotuba ya mwenyekiti wa kamati. Leteni na hotuba hizo ili tuchangie kwa ufasaha.

Thubutu!!
 
Mh! Hakuna hata RIP kwa Regia Mtema?! Ingekua vyema mwanzo wa hotuba,yangesemwa maneno ya kumkumbuka Regia na kumwomba Mwenyenzi Mungu aendelee kumpumzisha kwa amani.

Anyway,hotuba ina mambo mengi ya msingi juu ya vijana. Pia imeonyesha ni kiasi gani serikali hisivyo makini katika kutatua kero za vijana. Haiwezekani mkataba uliosainiwa mwaka 2008 uje leo bungeni kuidhinishwa!

nzi bhana,rudia kusoma mwanzoni ila kumbuka wabunge waliofariki ni wawili.pamoja
 
daaah hivi haya mambo kuna team maanlumu huwa inayaandika eeeh mweeee.

kwa maana iyo unataka kuniambia mh joseph mbilinyi hawezi kuyaandika ama? Iyo trela watu wa mbeya ndo tunajua who is suggu na ndo maana tukampa kura.
 
Kama wadanganyika wataendelea kupokea sukari,mchele,khanga,vitenge,nyama,pombe and the like kutoka magambani, hotuba nzuri kama hii zitaendelea kuwa "day dreaming" ktk implementation.
 
CHADEMA Bana! muwe fair, mmeweka hotuba ya kambi rasmi ya upinzani lakini utekelezaji wa hotuba hiyo unatokana na hotuba rasmi ya upande wa serikali iliyowasilishwa na Nchimbi pamoja na hotuba ya mwenyekiti wa kamati. Leteni na hotuba hizo ili tuchangie kwa ufasaha.


Si vibaya kama utawasiliana na nchimbi na mwenyekiti wa kamati wakupatie hotuba zao uzilete hapa. Hii ni hotuba ya msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kutoka chadema. Hilo nalo gumu kulielewa?
 
Hotuba nzuri sana, imechambua mkataba pamoja na kuuhusisha na matatizo yanayowakabili vijana.

Bravo Sugu.
 
8 Reactions
Reply
Back
Top Bottom