NONDO wala Ushirika wataziacha salama SACCOS?

Mongoiwe

JF-Expert Member
Feb 26, 2008
524
263
Souse:http://www.fredkatulanda.blog.com/

KWA wakulima wa kada mbalimbali kile kipindi cha muda ama wakati ambapo wamekuwa wakikitumia kwa ajili ya kuuza mazao yao baada ya kuyavuna hujulikana kama ‘Msimu’.
Ni katika wakati huu ndugu zetu (Hususani sisi tuliokulia Vijijini) ambao tuliiwaita wakulima huu ndiyo ulikuwa sawa na kipindi cha mwisho wa Mwezi kwao. Kwani ni kipindi hiki ambapo nao walitarajia kupata ‘haki yao ’ ama kifuta jasho tutokana na kumenyeka kwa muda mrefu katika kilimo.
Kwa wakulima wengi kipindi hiki kwao kilikuwa ni kipindi cha kukusanyika katika vyama vyao vya ushirika na kupima mazao yao kwa ajili ya kuuza. Nasema vyma vya ushirika kwa vile hii ndiyo ilikuwa njia ya wakati huo iliyokuwa ikitumika kwao kuuza mazao.
Ni kutokana na umuhimu huo wa vyama vya ushirika kuliibuka msimu ulioshinikiza kuanzishwa kwa vyama hivyo na kweli vikaanzishwa nchi nzima.
Baadhi ya vyama hivyo ni Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Ruvuma (SAMCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (NCU) na Chama cha Ushirika Mkoa wa Mara (MCU).
Lakini sasa vyama vyote hivyo nilivyovitaja hapo juu na vingine, vimekubwa na ‘Msimu kifo’, vimekufa kifo ambacho mpaka sasa kimebaki kitendawili kutokana na waliohusika kuviua kushindwa kushughulikiwa licha ya kufahamika.
Nasema vyama hivi vimekufa kwa vile hata vbile vilivyopo hali viliyonayo ni sawa na mgonjwa aliyeko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), au sawa na nyumba iliyoliwa na mchwa mpaka kwenye mabati kama alivyoeleza Rais Jakaya Kikwete katika kauli yake wakati wa kuzindua rasmi Chuo Kikuu kishiriki cha Ushirika na Stadi za Biashara mjini Moshi.
“Vyama vya Ushirika vingi vilivyopo viko katika hali mbaya. Kama ni mgonjwa basi yuko ICU, na kama haviko ICU basi vimeliwa na mchwa, maana mchwa ana tabia ya kula miti, lakini kwa upande wa vyama vya ushirika amekula miti na makabati yake”.
Hakuna shaka msimu wake umekwisha, kwa maana msimu wa kifo husahulika mapema sana , hata ushirika nchini umeendelea kubaki kuwa kumbukumbu katika vitabu vya historia tu.
Ukifuatilia kwa kina utagundua jambo moja, nalo ni hili; Waliuofilisi Ushirika huo wao wanaishi kwa neema kwa kula kuku na mrija, soda kwa uma au kwa lugha ya vijana wanaishi kwa ‘Kutanua’.
Wapenda ushirika walipopiga kelele tuliambiwa hadithi ndefu ambazo nazilinganisha na hizi za sasa za ‘Ufisadi mkubwa’ mara majina ya waliofilisi yamekabidhiwa kwa Rais (Wakati huo Benjamin Makapa) lakini tangu majina ya waliofilisi ushirika yakabidhiwe kwa rais wa awamu ya hiyo ya tatu, mpaka leo awamu ya nne, hakuna vigogo wala kigogo aliyefilisiwa ama kuchukuliwa hatua kwa kosa la kufilisi Ushirika.
Si kwamba vigogog hao hawapo au pengine bahati mbaya Mungu aliwaita kuzimu, wapo kama nilivyoeleza wakitanua na kujirusha tena na leo wanashuhudia msimu mpya ambao umeanzishwa tena kuja kuchukua nafasi ya Ushirika walioua ambao umepewa jina la SACCOS.
Kuna madai kuwa baadhi ya vigogo wanaohusika katika kufilisi vyama vya ushirika vya mikoa, hivi sasa wanashikilia nyadhifa za juu za kisiasa, ikiwa ni pamoja na ubunge, ukuu wa wilaya na nyadhifa mbalimbali katika vyama vya siasa hususani chama tawala, labda ndiyo sababu hawachukuliwi hatua.
Mfano tukiangalia chama kimoja cha NCU, ripoti ya mkaguzi wa vyama vya ushirika kuhusu chama hicho inaonyesha kuwa, mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Jacob Shibiliti0, Diwani (Bernard Pollycarp) wote kutoka CCM, pamoja na waliokuwa wajumbe na wenyeviti wa kanda mbalimbali za ushirika huo walihusika lakini bado wanapeta na kuishi kwa heshima zote kana kwamba hawakuiba mali za wakulima.
Licha ya kuijtambua kiini cha ulaji fedha na waliohusika kutochukuliwa hatua bado serikali imeendelea kutoa fedha mfano katika bajeti zake hizi za mwaka 1999/2000 na mwaka 2001/2002 serikali ilivilipia madeni vyama kadhaa vya ushirika, kiasi cha sh 9,940 bilioni zilizodaiwa na wakulima na benki mbalimbali kwa nia ya kuvinusuru kufilisiwa.
Lakini leo kaulize katika fedha hizo ni kipi kimenyanyuka tena na sasa kinasimama, kama hutakuta fedha hizo ziliemndelea kusaidia matumbo ya watu na kuviacha vyama hivyo katika hatari ya kutokomea katika ramani ya uhai wa ushirika zaidi.
Kama nilivyoeleza pengine hakuna haja ya kufuatilia zaidi kujua wakina nani walihusika na kuzitafuna kwa vile msimu wake umepita na sasa tuko katika msimu mpya kabisa wa ushirika ambao umepachikwa jina la SACCOS.
Walaji wa awali wamo, wafujaji wa vyama vyetu ndiyo wanaoziongoza sasa na kama si wao ni vizazi vyao ama jamaa zao ambao wamekuwa na kushuhudia watangulizi wao wakila na kuneemeka bila hatua kuchukiliwa.
Pengine ninaposema msimu wengine hawanielewi, sasa niseme kuwa baada ya kufa Ushirika Tanzania imekumbwa na ‘fashion’ nyingine ya kitu kinachoitwa SACCOS.
Vijana wanalazimishwa kuunagana na kuwa SACCOS, wakinamama wanalazimishwa kujiunga, kila mtu anahimizwa kujiunga sawa na wakati vyama vya Ushurika vinaanza miaka hiyo, ilimradi neno muhimu kwa sasa kwa viongozi wetu ni hilo ‘SACCOS’.
Tumekuwa tukiambiwa kuwa katika SACCOS kutakuwa na Benki Kata, hii ni sawa na wakati wa Ushirika tulipokuwa tukiwambiwa kuwa kutakuwa na Maduka ya Ushirika ambayo yaligeuka kuwa kiini cha kufuja fedha na hatmaye kufa kwa ushirika.
Katika kila kampeni za viongozi neno muhimu limekuwa ni hilo hakuna hotuba kumalizika bila ya kutueleza hatua zilipofikia kuhusu waliokula mali zetu za ushirika bali uzao mpya wa ushirika.
Yeyote, awe Rais, waziri mkuu, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, maofisa wa benki na hata wabunge wetu ambao kwa bahati mbaya hata hawajatuuliza iwapo tunataka tena SACCOS baada ya ushirika kufa wao wamekuwa wakikazania hilo tu.
Sasa Tanzania tumeanzisha SACCOS, kwa kweli ni jambo la kufurahisha na ni jambo linalotia moyo kutokana na mwitikio huo, lakini masuali ya msingi yanabaki msimu huu nani ataulinda usimogolewe na hao mafisadi na kuwaacha wananchi njia panda kama ilivyokuwa kwa ushirika?
Nasema hili kwa vile kila mtanzania anao wajibu wa kujua, kwani fedha hizi ambazo zimekuwa zikimwagwa kwa ajili ya SACCOS na hata zilizomwagwa katika Ushirika na kuteketea ni mali ya Watanzania wenyewe ambao ni walipa kodi. Zinatokana na fungu kutoka katika kodi ya wananchi wote na kila Mtanzania atastahili kupata mrejesho wake mbele ya safari.
Sipigani na kuanzisha SACCOS lakini kinachonipa shaka ni jinsi tulivyoshindwa kushughulikia walaji wa fedha za ushirika na kuzirejesha na leo tumeibuka na msimu ama Fashion mpya ya SACCOS wakati bado tukigali na kundi la walaji.
Sarikali ilipaswa kuhakikisha inasimamia zoezi la watu wote waliokula fedha za ushirika, kwa hali zote, nguvu zote ikiwa ni pamoja na kuwatosa katika mikono ya sheria wale wote waliohusika na kuufilisi ushirika bila ya kujali nyazifa zao kwa vile kitendo cha kula mali hiki kikiachwa kitajenga ujasiri wa kifisadi wa kufilisi ushirika ambao umeota mizizi na kijichimbia katika ardhi ya kisiasa.
Lakini iwapo SACCOS zitakomaa na kupanuka na jambo hilo likabaki kumbukumbu bila ya kuchukuliwa hatua za dhati, basi tujue tunatengeneza mianya mingine ya kukuza mafisadi au Nondo wala ushirika ambao nina hakika hawataziacha salama SACCOS.
Iwapo jambo hilo halijafanyika basi tutarajie kufa kwa msimu wa SACCOS na kuzaliwa msimu mpya ambao sijui utakuwa na jina gani?
Mingu Ibariki Tanzania … tokomeza ufisadi.
 
Back
Top Bottom