Noela: Mwanafunzi aliyeshangaza watu kwa kuandika hotuba ya Waziri Mkuu

real G

JF-Expert Member
Feb 7, 2013
5,227
5,287
PIC+NOELA.jpg


"Hata sijui nilipata wapi ujasiri wa kupenya katikati ya watu hadi kufika kule mbele, ingawa kulikuwa na ulinzi mkali lakini nilifanikiwa na kupata sehemu japo ya kusimama na kumsikiliza Waziri Mkuu.”

Ndivyo anavyoanza kusimulia Noela Tekele (11) mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Masahunga wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Binti huyo aliwashangaza watu baada ya kufuatilia na kuandika hotuba aliyokuwa akiitoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea wilaya ya Bunda Februari 17 mwaka huu katika eneo la Kisorya wilayani humo. Hatua hiyo ilimfanya Waziri Mkuu ampe zawadi ya Sh 50,000.

Binti huyo mwenye ndoto ya kuja kuwa mwandishi wa habari wa kimataifa, anasema kuwa siku ya tukio aliondoka nyumbani kwao kwa ajili ya kwenda twisheni.

Alipofika shuleni alielezwa kuwa siku hiyo mafunzo hayo yasingekuwapo kwa sababu walimu walikwenda kumsikiliza Waziri Mkuu aliyetembelea kijiji chao.

Anasema kuwa baada ya kupata taarifa hizo badala ya kurudi nyumbani, akaamua kujongea kwenye mkutano huo ili aweze kusikiliza ujumbe wa kiongozi huyo.

Noela anasema kuwa hajawahi kuhudhuria mkutano wowote uliowahi kufanyika kijijini hapo, ingawa mara kwa mara viongozi mbalimbali wa ngazi za kijiji hadi taifa wamekuwa wakitembelea kijiji chao na kufanya mikutano ya hadhara.

“ Huu ulikuwa mkutano wangu wa kwanza maana sijawahi kuhudhuria hata mmoja kwa hiyo nilivyofika pale pamoja na kukuta watu wengi sana nilikuwa na hamu ya kumuona uso kwa uso waziri mkuu na kusikiliza ujumbe aliokuja nao,’’ anasema na kuongeza:

‘’Ikabidi nijipenyeze haraka haraka katikati ya watu japo ilikuwa ni kwa shida, lakini hatimaye nilifanikiwa kufika mbele na kumuona akiwa kasimama juu ya gari akihutubia wananchi.’’

Anasema kuwa baada ya kufanikiwa kufika mbele, haraka alichoma moja ya daftari lake alilokuwa amebeba kwa ajili ya masomo yake ya ziada pamoja na kalamu na kuanza kuandika hotuba aliyokuwa akiitoa Waziri Mkuu.

Kinachovutia zaidi katika hotuba hiyo ni uwezo wake sio tu wa kuandika nukta muhimu, lakini pia takwimu zilizotolewa na Waziri Mkuu. Noela anasema alivutiwa na hotuba hiyo, hivyo akaamua kuiandika ili kuja kuwa kumbukumbu ya baadaye.

Kilichomvutia anasema ni kipande cha hotuba ambacho Waziri Mkuu alikuwa akielezea mikakati ya Serikali ya kuhakikisha uwepo wa uvuvi endelevu kwenye ziwa Victoria pamoja na namna ambavyo Serikali imekuwa ikipambana na uvuvi haramu.

Anasema kuwa pamoja na kuwa bado ni mtoto mdogo, lakini tayari ameshuhudia athari za uvuvi haramu baada ya kukosekana kwa samaki katika kijiji chao ambacho kiko mwambao wa ziwa Victoria.

Noela anasema kuwa pamoja mambo mengine, ndoto yake ni kusoma hadi kufikia chuo kikuu, hivyo alimuomba waziri mkuu amsaidie kufikia malengo yake hayo kwa kumsaidia kupata elimu katika mazingira mazuri tofauti na hali halisi ilivyo kwa sasa.

Anasema kuwa amekuwa akijitahidi kufanya vizuri katika masomo yake ambapo anasema kuwa katika mitihani yake, mara nyingi amekuwa akishika nafasi ya sita hadi nane kati ya wanafunzi 102.

Anasema kuwa miongoni mwa changamoto zinazomkabili katika masomo yake, ni pamoja na msongamono wa wanafunzi katika darasa lao ambapo alisema kuwa wanafunzi wote 102 hulazimika kukaa katika darasa moja.

Pia, anasema kijiji chao hakina umeme, hivyo kushindwa kujisomea hasa nyakati za usiku kutokana na kukosekana kwa mwanga wa uhakika, huku akisisitiza kuwa kati ya masomo yote, hupendelea zaidi masomo ya Kiingereza, Hisabati, Jiografia na Sayansi.

“Sihitaji zawadi yoyote zaidi ya elimu hivyo namuomba Waziri Mkuu na wengine wanisaidie nipate elimu katika mazingira mazuri ili niweze kufanya vizuri na kufika chuo kikuu, ili hatimaye niwe mwandishi wa habari wa kimataifa au rubani” anasisistiza Noela.

Anasema kuwa alijisikia fahari baada ya kufanikiwa kumshika mkono waziri mkuu, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kumuona na kuchukua hadi kwenye gari la waziri mkuu na kupewa zawadi hiyo aliyonunulia sare, begi na madaftari. Malima anasema kuwa alishangazwa baada ya mtu mmoja kumshtua juu ya binti huyo mdogo aliyekuwa amesimama mbele ya umati mkubwa wa watu, huku akiwa anafuatilia hotuba na kuiandika katika daftari lake la shule mithili ya mwandishi wa habari.

Anasema kuwa aliamua kusogea karibu na binti huyo kwa tahadhari, ili kuona nini alichokuwa akiandika pia kuhakikisha kuwa hamshtui na hatimaye asije akapoteza umakini. Alipomfikia alizidi kupigwa na butwaa kwa namna ambavyo binti huyo alivyokuwa makini akiandika hotuba iliyokuwa ikitolewa.

Baada ya hotuba kumalizika anasema alimchukua Noela hadi kwa Waziri Mkuu ambaye tayari alikuwa ameshaingia kwenye gari tayari kwa kuondoka.

Malima anasema kuwa tayari amewaagiza wasaidizi wake waweze kumuangalia binti huyo kwa ukaribu zaidi na kumpa msaada unaohitajika ili aweze kufikia malengo yake.

Mama mzazi wa Noela, Theopista Alex Malongo anasema kuwa hakuamini pale aliposikia kuwa binti yake ameweza kuandika hotuba ya Waziri Mkuu.

“Hata Mimi nimeshangaa maana huyu mtoto sijawahi kumuona kwenye mkutano wowote hapa kijijini, ingawa mikutano hiyo imekuwa ikifanyika sana hapa kijijini,’’ anasema.

Anasema ingawa binti yake ana maendeleo mazuri shuleni, lakini hakuwahi kufikiria kuwa ipo siku atafanya kitendo cha kijasiri kiasi hicho ambapo ameiomba Serikali kumsaidia binti yake kuweza kufikia malengo yake.

Anasema kuwa mtoto huyo anakumbana na vikwazo katika kufikia malengo yake, ikiwa ni pamoja na mazingira ya shuleni kutokuwa mazuri pamoja na ukosefu wa umeme nyumbani.

Mama huyo mwenye watoto saba wote wakiwa ni wa kike, anasema kuwa Noela ni mtoto wa nne na kwamba mara nyingi amekuwa akimpa kazi za kufanya baada ya kutoka shuleni bila kujua kuwa kwa kufanya hivyo anamyima nafasi binti yake kujisomea, hivyo ameahidi kuanzia sasa atahakikisha kuwa binti yake anapata muda mwingi wa kujisomea.

Chanzo: Mwananchi
 
Great news! Safi Noela, kila ahadi itekelezwe. Kikubwa ni kuboresha miundombinu ya elimu nchi nzima, nchi hii ina vipaji vya kutosha sana. Tatizo huwa ni mazingira ya kulea na kuviendeleza vipaji hivyo kutokana na mazingira ya kimaisha. Noela ni picha tu ya yaliyopo kwenye jamii yetu.
 
Noela amenifurahisha sana. Ndoto yake itatimia tu tuombeane uzima
Kwa Tanzania ndoto zake kutimia ni kama ku betting,

Ingekuwa ulaya sasa hvi angesha hamishwa sehemu husika, labla Mzee Regnald Mengi amchukue, kama yule Stivine wa Itv..

Tofauti na hapo kipaji chake kitafia huko bunda, akifeli darasa la saba ndiyo basi tena asubirie kukeketwa
 
Great news! Safi Noela, kila ahadi itekelezwe. Kikubwa ni kuboresha miundombinu ya elimu nchi nzima, nchi hii ina vipaji vya kutosha sana. Tatizo huwa ni mazingira ya kulea na kuviendeleza vipaji hivyo kutokana na mazingira ya kimaisha. Noela ni picha tu ya yaliyopo kwenye jamii yetu.
Tunapompongeza Noela tusisahau kumpongeza Mkuu wa Mkoa aliyeguswa na tukio hilo hadi kumfikisha Noela kwa Waziri Mkuu. Tunahitaji viongozi wasikivu na wanaojali maendeleo ya watu kama alivyofanya Mh Malima.
 
Taifa lifanye nini kuwatambua akina Noela walioko nchi nzima wanaoishi katika mazingira yasiyo rafiki na ndoto zao?
 
Tumwombee ndoto zake zitimie asije kupigwa risasi kama akwilina na ndoto zake zikazimwa kama mshumaa
 
Dah huyu mtoto ana akil kama mtu mzm kiukwel kama anapata ckul nzur kwel atakujakuwa mtu mkubwa sana asaidiwe jamn amejitambua mapema sana
 
Back
Top Bottom