Njiapanda ya Vwasu - Simulizi ya huba

Mogambi

JF-Expert Member
May 25, 2012
209
351
NJIA PANDA YA VWASU (Simulizi ya Huba)

DAVID NGOCHO SAMSON
0629077792

01

Naikumbuka vema ile siku. Alinipigia simu, nami nikaipokea kwa bashasha na furaha tele. Huyu alikuwa mpenzi wangu, mwanamke aliyenipa raha mara nyingi.

'Mambo vipi mpenzi? Uliona email niliyokutumia? Nilikujulisha kuwa narejea nchini, kwa bahati mbaya sijapata tena nafasi ya kucheki kama ulijibu. Kuna mambo fulani fulani yalitokeza na kukatisha mawasiliano. Ajabu napowaza kukupandia hewani, unaniwahi na hii call. I miss you babe!' niliongea kwa sauti ya furaha.

Kawaida, mimi hutabasamu kabla hata ya kusikia sauti ya Hellen, yaani ile nikiona kwenye kioo cha simu yangu jina 'Hellen', basi moyo wangu hufukuta kwa fukuto la furaha, hata kama ningekuwa na huzuni, mie huisahau mara moja hadi pale nitakapomaliza mazungumzo.

Kwa nini sijasevu jina la Hellen kwa mbwembwe za 'my love', au 'Honey' au 'laaziz' unajiuliza eh?! Utafahamu hapo baadaye, lakini yeye Hellen anajua kwa nini jina lake nimelisevu kavu. Sasa basi, naweza kusema, ingawa tupo kwenye mahusiano kwa karibia miezi minne sasa, lakini ukiniona navyotabasamu kumuona Hellen, basi unaweza kukokotoa na kupata jawabu la uongo. Ndiyo, la uongo.

Utajua tu kwamba huyu jamaa, ndiyo kwanza kamuona huyu binti na amemzimikia kinoma. Kawaida pumbazo langu la kwanza nilipokutana na Hellen mara ya kwanza miezi mitatu iliyopita, basi limekuwa likibaki hivyo hivyo hata sasa baada ya miezi hii yote napomuona tena. Aisee! Huyu binti kajua kunishika. Mie zuzu wallah.

Basi, nilipomaliza kumweleza maneno hayo, nilisubiri kwa hamu niisikie sauti ya mpenzi wangu, ambayo kuisikia pekee, hunipatia burudani nafsini mwangu.

'Niliiona Derrick, na nimeshaijibu. Uko wapi?' Hellen Alizungumza kwa sauti tulivu. Sauti ambayo sikuizoea. Haikuwa na ule uchangamfu wa siku zote. Najua haikuwa nao, japo alijaribu kuongea kwa kuniigizia. Namjua mpenzi wangu bwana huwezi kunidanganya kitu. 'Hellen wangu ana shida gani jamani!'. Nilijiuliza. Ah, sikuvumilia kubaki najiuliza tu, nikaamua kuondoa hilo dukuduku moyoni mwangu.

'Vipi dear, mbona umepoa hivyo mpenzi? Kunani tena darling. Eh mamii, are you sick mpenzi?' nililazimika kuhoji, ile furaha yangu ikiyeyuka kama donge la barafu kwenye joto kali. Aisee, sio siri, niambie habari gani sijui, lakini habari za huzuni hunibeba sana mimi. Nadhani, huu ni udhaifu kwangu mimi mtoto wa kiume, kuwa na hisia nzito sana.

Ni mwepesi sana wa furaha na huzuni vile vile. Ndio maana najaribu kusoma soma masuala ya kisaikolojia, kunisaidia kuwatambua matapeli mapema. Si unafahamu matapeli wanacheza sana na hisia! Naam, matapeli buana wakikujua wewe' ni mtu unayepata huzuni ukielezwa tukio la kuhuzunisha, matapeli ni wepesi sana kupita humo, wakakulisha habari ya msiba, ukajikuta unachangia nauli ya kwenda msibani kwa kuwaonea huruma, kutokana na matatizo chungu nzima watakayokuorodheshea.

Huzuni iliyokuwa moyoni mwangu, kusikia tu ukosefu wa uchangamfu kwenye sauti ya Hellen, ungedhani nimepashwa habari za msiba.

'Siku hazilingani mpenzi, hata hivyo kiafya niko poa tu sema nimekumiss. Kama tunaweza kuonana itakuwa poa sana. Nahitaji tuongee!' Hellen alizungumza kwa utulivu ule ule.

'Ok dear, nipo Changanyikeni now. Nije au uje?' nilimtupia swali japo ilikuwa wazi kwamba alinihitaji niende. Kikawaida akihitaji kuja kwangu, yeye huja baada ya kujibiwa message yake ya neno moja ambayo ni mimi tu naielewa 'Hr301'. Hiki ni kifupisho cha moja ya kozi ambazo zilitukutanisha mimi na Hellen miezi mitatu iliyopita. Usijali. Nitakuelezea. Najua unataka ujue ilikuwa vipi.

Kwa kawaida, vyuoni kozi huwa zinakuwa na majina ya vifupisho. Mfano hiyo Hr inasimama badala ya kozi ya 'human rights' (Haki za binadamu …) na hiyo 301, Sina hakika lakini nahisi ilimaanisha mwaka wa masomo. Maana kulikuwa pia hr101 iliyofundishwa mwaka wa kwanza, hr 201 ilifundishwa mwaka wa pili. So nahisi kabisa hiyo ndio ilikuwa maana yake, yaani mwaka wa tatu.

Hellen yeye amesoma kozi ya Archaeology, na mimi nilisomea kozi ya Political Science and Public Administration. Kwa hiyo, tulikuwa kozi mbili tofauti kabisaa na ndiyo maana tulikuja kufahamiana mwaka wa tatu. Ajabu ni kuwa, kwenye semester ya pili ya mwaka wa Mwisho wa masomo yetu, mimi niliamua kuongezea kozi hii ya human rights, kama kozi ya ziada tu. Haikuwa lazima kuisoma, kumbe naye, aliamua kufanya hivyo tusijue kama ndio kitu kingetukutanisha.

Mimi ni mtu mmoja ambaye, napenda kubeba majukumu yangu kwa mikono miwili, tena kwa umakini wa kiwango cha juu kabisa. Na hii naweza kukudhihirishia kwa mambo ninayoamua kufanya, ni lazima nione yamekamilika, ndio naweza kurelax. Sasa basi, kwenye hiyo kozi, nikajikuta nimepangwa semina moja na Hellen. Halafu tena, tukapewa group assignment (kazi ya kikundi) watu kumi, mimi na yeye tukiwa miongoni mwa wanakikundi.

Shida ikawa moja, wadau wote niliopangwa nao, ama walikuwa wapuuziaji wa mambo au walikuwa na mishe nyingine muhimu kuliko shule. Watu hawa, tulipokubaliana muda wa kukutana kwa ajili ya kujadiliana na kutafuta majibu ya kazi tuliyopewa, hawakuonekana. Nikajikuta peke yangu eneo la tukio. Bahati mbaya sana ilikuwa kwenye kikao hicho ndio tukabidhiane mawasiliano kwa ajili ya kupeana taratibu na yanayojiri mengine.

Kitu nilichokuja kubaini baadaye, ni kwamba wale wanakikundi wenzangu, kila mmoja kwa wakati wake, alikuwa anajidanganya kwamba ni yeye pekee hajahudhuria kwenye majadiliano, na hivyo kujitia moyo kwamba hakuna kitakachoharibika. Lo! Walijidanganya sana. Baada ya hali kuwa hivyo, basi nikalivalia njuga suala hilo mimi mwenyewe, nikaanza kuandika kazi ile mimi mwenyewe kwa juhudi kubwa. Uzuri ni kwamba, kwa mfumo wa zile semina za chuoni, kwenye uwasilishaji hoja, angeweza kuteuliwa mmoja akatoa wasilisho lote kwa niaba ya kundi lote, huku wale wengine wakisaidiana naye kujibu hoja ambazo zingeibuliwa kwenye mjadala wa pamoja. Hivyo, nikaamua kuwa jeshi la mtu mmoja.

Hali hii haikuwa ya kwanza kuwahi kutokea, nilikwishakutana na visa vya namna hii mara kadhaa, sema hii ilitia fora. Awali nilikuwa nakutana na watu wachache au wengi, wakakosekana baadhi. Lakini hii ilikuwa mara ya kwanza wote kukosekana. Sikujali. Kwanza kabisa, mimi najijua, napenda sana kufanya uwasilishaji, hivyo hata kama ingekuwaje, tuseme kwa mfano angelichaguliwa muwasilishaji mwingine, bado ningelijiandaa kama vile mimi ndio muwasilishaji mkuu. Ndiyo. Kila mtu na ulevi wake bwana, na mimi wangu ulikuwa huu wa kupigiwa makofi na kupewa sifa kwa uwasilishaji bora na wahadhiri au ma-tutor. So kusema kweli, nilijiandaa vema kwa nondo za uhakika.

Siku ya uwasilishaji, mimi nilienda kwenye semina kama kawaida kwa muda uliopangwa. Kumbe bwana, wale jamaa zangu, kwa kutaka angalau wapate point mbili za kujitetea nazo ikitokea wametakiwa kutoa hoja, waliwahi nusu saa kabla ili wakutane na wahusika wengine, wadandie points. Hali ikawa ngumu pale wote tisa walipojikuta hakuna hata mmoja aliyehudhuria kwenye majadiliano. Kimbembe kikawakumba. Wakaanza kuhaminika. Wajadiliane, waandike, wawasilishe, na bado kazi hiyo ilihitaji kukusanywa ikiwa imechapwa!. Niliwakuta jamaa wameloa jasho wakihangaika.

Ilikuwa dakika tano hivi kabla ya muda wa wasilisho kufanyika. Dah walikuwa wamejikatia tamaa vibaya sana. Mwanaume nikaingia kwa mbwembwe na kabrasha zangu kwenye begi utadhani waziri wa fedha anaenda kusoma bajeti bungeni.

'Oya waungwana, muda wa kuingia kwenye semina huu. Vipi bado mnagaagaa na upwa?' Nikawauliza.

'Hivi si tupo wote wewe?' Aliniuliza jamaa mmoja anaitwa Stanley.

'Yeah man, twendeni tukawasilishe wazee!' niliwaambia.

'Vipi mwanangu uliandaa wasilisho?' akaniuliza tena.

'Haya ndio mambo niliyofuata hapa mlimani. Hebu njoeni hapa wadau, tuwekane sawa kabisa.' nilitamka kwa sauti kubwa yenye mamlaka. Najua kwa wakati huo walikuwa tayari kunisikiliza kwa hamu zote, si nimekuja kuokoa chombo kisiende mrama? Basi wakanisogelea wakiwa watulivu kama vifaranga walionyeshewa. Nikawaangalia nyuso zao zilivyotia huruma, basi nikacheka sana kimoyomoyo.

'Waungwana, tumefeli sana kwenye kipengele cha uungwana, fikiria wote mlikimbia majadiliano na kuniachia mzigo wote nibebe mimi?' nilivyotamka hivyo nikaona nyuso zao zikipata nuru ya tumaini jipya. Kwa sababu walau walipata uhakika kwamba kutakuwa na kazi ya kakabidhiwa kwa profesa.

'Sasa. Hapa nimeshaandaa nondo, nina uhakika wa asilimia mia wa kuwapatieni A ya bure. Lakini mnatakiwa mfahamu kuwa, nimetumia muda na gharama. Hapa tunafanya changisho, ndio unapata fursa ya kusaini jina lako kwenye wasilisho. Kila mmoja anachanga buku mbili. Tufanye fasta, naona bado dakika tatu tuingie kwenye semina.' niliongea kwa kujiamini sana nikiwa nimevalia sura ya kazi. Hakuna aliyebisha. Nikazikusanya buku mbili mbili, tukazama darasani.

Kama kawaida yangu, kumbuka nimekueleza huu ndio ulevi wangu. Muda wa wasilisho ulipofika, nilikabidhi nakala ya wasilisho kwa msimamizi wa semina yetu. Profesa Nkungu, halafu nikaanza mbwembwe zangu za uwasilishaji hoja. Huu ndio uwanja naofanyaga mambo yangu, basi nikawa nipo namwaga sera zangu huku nikishuhudia zinavyowaingia wadau. Nikamuona profesa anatikisa kichwa juu chini kukubaliana na hoja zangu. Nilipoweka kituo baada ya wasilisho, chumba kizima walikuwa wanapiga makofi. Kwangu ilikuwa burudani kabisa. Wale jamaa zangu hawakuamini. Niliwapatia alama A Kama nilivyowaahidi. Profesa akasifia sana kundi letu.

Basi, tulivyotoka kwenye semina, nikiwa naondoka mdogo mdogo kuelekea kwenye vimbweta nikaperuzi peruzi notes zangu. Nikasikia sauti nyuma yangu. 'Derrick'. Ilikuwa sauti laini, sauti ya kike. Ikanilazimu kusimama na halafu nikageuka nyuma, maana chuoni kuna watu wengi na wakina Derrick sikuwa mimi pekee.

'Naomba nisubiri tafadhali' yule msichana alitamka. Nikakumbuka Ni miongoni mwa wale wanakikundi niliowatoza shilingi elfu mbili mbili.

'Mimi?' niliuliza kwa kutojiamini.

'Ndio, wewe si Derrick?' akatamka kwa ulizo.

'Ndio, lakini kwenye chuo kinachosajili maelfu ya wanafunzi huwezi kudhani utakuwa mtu pekee mwenye jina kama lako, sivyo? Nilimweleza.

'Sawa, upo sahihi nadhani.' alitamka yule mrembo.

'Haina kudhani hiyo, ndio uhalisia wa mambo' nikamuhakikishia.

'Kuna hoja unashindwa kujibu kweli?' mrembo huyu aliniuliza.

'Ah hayo masihara sasa. Of course kila hoja inaweza kujibiwa. Kwa kukubaliwa au kupingwa' nilimwambia halafu nikaongezea.

'Pale palikuwa na Helen, Mwajuma, Aisha na Doris, wewe utakuwa nani kati yao?' niliuliza nikiwa nimetaja majina ya wasichana ambao walikuwa sehemu ya kundi langu la wasilisho.

'Tabiri!' alinambia akiwa anatabasamu.

'Haha, mie si Sheikh Yahya bwana. Lakini kwa vile umenipa cheo hicho, wacha nijaribu, kwani nikikosea kuna hukumu?' akatikisa kichwa kulia na kushoto kumaanisha hakuna hukumu. Nami nikaamua kwenda na jina la kwanza.

'Hellen' nikatamka bila kupepesa jicho.

'Nilijua unafahamu, sema Unataka kuniigizia tu!'

'Haha' nikajichekea zangu. Sikufahamu jina lake, lakini sikuona kwa nini nisitumie lift hii niliyokua napewa bure, ya kufahamu nisichofahamu.

'Enhe nambie Hellen, wewe na wenzio mna tabia mbaya sana. Mbona mkaniachia kazi peke yangu' sikuwa na hoja na kulikuwa kumepita ukimya wa sekunde kadhaa kati yetu, hivyo nikaona niongee kauli hiyo kufufua mjadala. Huwa sipendi nikiwa na mtu kuwe na ukimya kati yetu, hasa kama ni jinsia ya kike. Kuepuka kutongoza, basi mimi huanza kuleta simulizi za kutunga za uongo na kweli ili kuepuka ukimya. Mara nyingi, nautafsiri ukimya kama mlango wa kuruhusu mwenzako aingie moyoni mwako na kuibua hisia za mapenzi.

Sio kwamba sipendi kutongoza. La hasha! Ni kwamba, ili kudumisha nidhamu binafsi, sipendi niwe kwenye mahusiano na msichana tunayeonana kila mara. Yaani darasani, kwenye semina, canteen na maeneo ya chuoni. Ndiyo maana niliamua kuwa na mahusiano na msichana ambaye anasoma chuo kishiriki cha chuo kikuu Cha Dar es salaam, kampasi ya Duce - Chang'ombe. Anaitwa Welu.

Hii Ina maana kwamba, tulikuwa tunaonana wikend tu na mara moja moja kati kati ya wiki. Kwangu mimi, hiyo ni heshima. Kuna kumisiana na kutarajiana kunakoamsha penzi na kulifanya liwe kileleni muda wote. Pia inaepusha migongano na migogoro midogo midogo inayoyumbisha penzi kama vile wivu pale unapomuona mwenzio anazungumza na mtu wa jinsia yako, halafu ukajikuta unaanzisha zogo. Inakuwa utoto, maana mara kadhaa nimeshuhudia washkaji wanatandikwa mbele ya mademu zao kwa sababu hizo za wivu. Kukaa unaumia moyoni kwa sababu unajikuta umejipachika ukachero wa kumfuatilia mwenzio nyendo zake, kama vile yeye ni mtoto asiyejua anachofanya.

Mara unaanzisha zogo na shemeji pasipokujua, au mrembo wako anazungumza masuala tofauti, unahisi Ni mapenzi unajitosa umuoneshe umwamba huyo jamaa, halafu unatoka hapo umevimbwa midomo au umepasuliwa komwe. Hayo ndio mambo naepuka kwa kuwakwepa warembo wa kuonana kila mara. Shida kubwa ni kwamba, hujijui kama una wivu,na hata unapofuatilia mambo yake, unakuwa pia hujui kwamba ndio umeanza upelelezi. Unajikuta mtumwa wa mpenzio bila kujua. Ah, hayo mie siyataki kabisa.

'Dah, ungejua ungenipa pole mwenzio!' Hellen aliongea kwa unyonge. Ah, kama nilivyokueleza awali, nina wepesi sana wa kubebwa kihisia. Ndio maana, kusema kweli, sipendi kusikiliza simulizi za huzuni, najikuta tu navutwa makini, na hali hiyo huniondolea mudi ya furaha. Mimi napenda habari za furaha, hizo tu, basi. Sasa, ajabu ni kuwa mtu akinijia na simulizi ya huzuni najikuta namsikiliza huku nikibebwa kihisia utadhani suala husika linanihusu.

'Oh Pole sana Hellen.' nilitamka huku nikiingiza mkono kwenye mfuko wa suruali yangu na kuchomoa wallet.

'Naamini sijakutendea haki kuchukua buku mbili zako, bila kujali ulikuwa na madhila gani. Tafadhali nisamehe.' niliongea huku nachomoa elfu mbili kwenye wallet na kumkabidhi Hellen.

'What?? Noo Derrick, Noo! Actually nimekufuata kutaka kukushukuru kwa jinsi ulivyookoa jahazi. Mimi napenda sana kushiriki kwenye discussion. Siku ile nilipata dharura, kulikuwa na kikao cha harusi na mimi nilikuwa nahusika kwa sehemu kubwa, so nikakosa namna ya kuomba udhuru, hivyo nikalazimika kukosa.'

'Ah, that's better now. Unajua hakuna kitu kinachoumiza kama kuwa-taken advantage of (kuchukuliwa poa) kwa sababu ya matatizo yako. Kwa hiyo, ulivyoanza kwa kusema nikupe pole, nikajua itakuwa tu ulikumbwa na matatizo. Haha, kwa hiyo anaolewa dada au unapata wifi?' nikauliza kwa utani. Nikaona kama Hellen alishituliwa na swali langu, au kuna namna swali hilo lilimuondolea Hali ya kujisikia amani (comfortability).

'Haha, forget about that. Derrick, I love your way of doing things. ( Sahau kuhusu hilo, napenda sana unavyokunyanyasa mambo yako) Jinsi ulivyoshushasha nondo mle ndani najisikia kukutoa out, lakini shida ni moja tu. Natakiwa tena kwenye kikao cha wajasiriamali mjini. So, please accept this as my gesture of appreciation (tafadhali pokea hii kama shukrani na hongera yangu) .' Hellen aliongea huku akinikabidhi noti ya shilling elfu kumi. Wow! Nikabaki nashangaa. Nikawa sina neno la kusema. Hata kusema asante nikasahau.

'Do you mind if I had your phone number?' (naweza kupata namba yako?) Hellen aliniuliza akiniangalia kwa jicho fulani hivi! Sauti hiyo ikanitoa kwenye pumbazo la muda nilikokuwa nimetopea.

'Hellen' nikatamka nikiwa nimekumbatia viganja vyake kwenye viganja vyangu.

'Asante sana, lakini neno tu la shukrani linatosha. Huna haja ya kulipia. You are a nice person. Please keep the money, ok. I appreciate your appreciation.' (Wewe ni mtu poa sana. Hata hivyo, siwezi kupokea fedha yako. Jua tu, nimekubali kunibali kwako) niliongea kwa sauti tulivu. Sauti ya kunong'ona. Huenda kuna namna sauti hii iliamsha kitu ndani yake.

'My numbers are ….. ' nikaanza kumtajia namba zangu, lakini nikasikia sauti yake ikisema
'Wait a minute' (subiri kwanza) nikalazimika kutulia wakati akichomoa simu yake kwenye mkoba. Ilikuwa tablet moja amazing. Well, mimi nilikuwa na kismart changu cha tekno, fresh tu!

'Ok, nitajie' alitamka tena Hellen.

'07174117..' nikamtajia na yeye akaziandika kwenye simu yake. Sekunde kadhaa mbele nikasikia kimeo changu kinaita.

'That's my number' akatamka. Halafu akaniambia
'Sasa, mie niwahi bwana!' Ni kama sikusikia, lakini nilimsikia, sema tu kuna namna huyu dada Hellen alikuwa ananipumbaza kwa sauti yake tamu. Nikiwa nimeganda sijui cha kusema, nikashitukia Hellen amenibusu shavuni halafu yule ananipungia mkono akiwa anaondoka. Nikabaki nimeduwaa. Napopata akili ya nini hasa kimetokea, Hellen alikuwa keshapotea kwenye upeo wa macho yangu. Kama vile bwege, nikabaki napunga hewani mikono yangu.

David Ngocho Samson
2020

FB_IMG_1475683164139.jpg
 
2
NJIA PANDA YA VWASU
David Samson
0629077792 WhatsApp

Tulipoishia!
Ni kama sikusikia, lakini nilimsikia, sema tu kuna namna huyu dada Hellen alikuwa ananipumbaza kwa sauti yake tamu. Nikiwa nimeganda sijui cha kusema, nikashitukia Hellen amenibusu shavuni halafu yule ananipungia mkono akiwa anaondoka. Nikabaki nimeduwaa. Nilipopata akili ya nini hasa kimetokea, Hellen alikuwa keshapotea kwenye upeo wa macho yangu. Kama vile bwege, nikabaki nimeinyanyua mikono yangu juu, nikimpungia hewani, tabasamu tele midomoni mwangu, nikifurahia ufahamu huo mpya. Naam, ufahamu kwamba Hellen huenda ananipenda.

Tuendelee Sasa!

2.

Turejee kwenye mawasiliano yangu na Hellen aliponipigia simu.

Nilipomuuliza Kama anakuja au niende Mimi, Nilijua kabisa kwamba alinihitaji niende. Vinginevyo angekuwa ametuma ujumbe wa 'hr301'. Ujumbe ambao ulikuwa na maana kuwa 'nakuja mpenzi'. Tuliamua kutumia hr301 kwa kuwa Ni kozi iliyotukutanisha na ndio ilikuwa mwanzo wa penzi letu. Lile wasilisho la hr301, ambalo nililibeba peke yangu kwa niaba ya watu kumi na kulitendea haki nikawazawadia A wanakikundi wenzangu, ndio lililozaa penzi kati yangu na Hellen. So kutokuiona meseji hiyo, kulinifanya nijiandae ili nikaonane na Hellen chuoni.

Nikajimwagia maji fasta na kutinga suruali ya jinsi la bluu na fulana yenye maandishi madogo kifuani 'University of Dar es salaam, Gender Club', fulana nyeupe. Miguuni nilivaa openshoes, sandals fulani za kimasai zenye mikanda ya ngozi na rangi ya damu ya mzee. Nikachukua kismart changu cha tekno na headphone, nikazining'iza shingoni, nikafunga mlango wa chumba changu, nikatoka na kumkuta Siwema anafua hapo uani.

'White Derrick huyo!' Siwema alinitamkia kwa utani.

'Oh mtoto mzuri Siwema, naona kama kawaida yako unaandaa mitoko' nilimtania.

'Mitoko gani na wewe hutaki kunitoa?' Siwema alinitamkia kwa aibu.

Siwema ni binti mrembo sana. Mtoto wa kisukuma. Ni kwa vile tu ni jirani yangu. Na kwa falsafa yangu, sianzishagi mahusiano na mtu nayeonana naye mara kwa mara, vinginevyo ningekuwa tayari nimeshaanua vyombo, najilamba kwa utamu. Ukweli ni kwamba binti huyu alikuwa ananizimia ile mbaya na nilijua kabisa. Kuna wakati nilitaka kuharibu kabisa kwa kuvunja miiko yangu lakini kaka yake akatokea mapema. Siwema anaishi hapa na kaka yake ambaye anachukua masomo ya uhandisi, computer engineering pale COET. Na huyu bwana ndio anamsomesha Siwema. Siwema yupo kidato cha tano sasa.

'Unataka nitandikwe fimbo za kisukuma nini? Si nasikia wasukuma ni noma kwa kupigana kwa fimbo!' niliendelea kumtania.

'Unajua sio poa Derrick, naona tu unaleta kutoka mbali wakati nami naishi hapa hapa na nakuhitaji' Siwema alilalama, haikuwa utani. Kuna vile nilimuonea huruma kabisa.

'Ah, unajua shida ni braza yako, keshanipiga biti juu yako.' nilimweleza huku nikianza hatua moja baada ya nyingine na kuondoka. Siwema alikuwa ananizimia sio kidogo. Ile siku ambayo Ilikuwa kidogo niharibu, nilikuwa nimeenda zangu bafuni kuoga. Niliporudi tu ndani, nikamkuta Siwema yupo chumbani kwangu ameketi kitandani. Ah, aisee acha kabisa, ilikuwa bonge la jaribu. Maana mtoto alikuwa ameketi kitandani na nilipoingia tu, akanipokea kwa busu moto moto. Mara, tukasikia mluzi huko nje, ilikuwa kaka yake, mshikaji alikuwa na itikadi za kihenga sana. Yaani alikuwa akirudi, basi lazima ajipigize miluzi halafu anaelekea chooni kwanza, halafu sasa ndio anaingia chumbani kwao. Nadhani alikuwa sahihi lakini, maana kuishi chumba kimoja na dada yako na wote mkiwa watu wazima ni changamoto. Lazima kuweka tahadhari, vinginevyo unaweza kumkuta ndugu anavaa nguo, au ametoka kuoga.

Loh, kwa haraka Sana, Siwema akatoka na kuingia chumbani kwao. Maana chumba cha kaka yake kilikuwa unatoka kwangu unaingia kwao. Daa! Hivyo ndivyo nilivyookoka na lile jaribio la Siwema..

Basi nikaendelea zangu nikipiga hatua moja baada ya nyingine, nikimwacha Siwema anasikitika, nikawa nazitoa headphones shingoni na kuzipachika masikioni. Hatua kwa hatua nikawa nasikiliza makala hamasishi kutoka kwa mhamasishaji maarufu huko Marekani mwenye asili ya kiafrica, Les Brown. Hizo ndio mambo zangu. Napataga maujanja mengi sana kwa kuwasikiliza hawa motiveshono spikaaz na ndio maana mimi mwenyewe nipo vizuri kwenye uwasilishaji hoja.

Haukupita muda mrefu, nikawa naingia pale chuoni, nikajichukulia maji kubwa kwenye duka, nikabugia nusu yake kwa mkupuo, maana joto la jiji hili si la kitoto. Baada ya kuridhisha kiu yangu, nikafuta jasho usoni kwa kitaulo kidogo cha mkononi, nikaanza kushuka taratibu kuelekea kule Hall 3. Pale kuna viunga vya nyasi maridadi sana ambako mara kadhaa mimi na Hellen hukutana na kupata faragha ya kuzungumza mambo yetu kama wapenzi.
Najua unajiuliza tulifikiaje kuwa wapenzi baada ya lile busu la kushitukizwa sivyo? Haha. Mapenzi yaache yaitwe mapenzi bwana.
Ilikuwa hivi.

***
Baada ya kuachwa pale nikiwa nimeduwaa napunga mikono hewani kama zuzu, hatimaye nikashangaa kuna mtu anaishusha mikono yangu chini.

'Oya, acha ubwege wewe. Unampungia nani mikono sasa? Haha!' Ilikuwa sauti ya rafiki yangu Issa Kalinga.

'Haha, kwani hujamuona yule mtoto mzuri aliyekuwa ananipungia mkono?' nikaongea huku nikimwonyesha kule alikokuwa ameelekea Hellen. Mara kule napomuoneshea, akawa anatokeza madam Bernadette, huyu ni professor wa lugha za kigeni hapa chuoni.
'We usinambie unatoka na profesa, kijana ume-advance sana kama unaweza kuwa unatoka na hadi maprofesa.' Isa akaendeleza utani.

'Sio huyo bwana, enewei, forget about it. Enhe nambie, yule mtoto alijipa? Nikamtupia swali.
Issa ni mtu mmoja anapenda sana gymnastics. Yeye anajua kucheza karate, Judo na kungfuu. Yeye anaishi mabibo hostel block D. Ukiingia room kwake, huko amejaza DVD za mapigano ya kina Jet Li, Bruce Lee, na wakali wengine wa kungfu. Ukitoka hapo, utamkuta kwenye muvi za kihindi. Hizo ndio aina ya muvi anaangalia. Sasa, kutokana na hulka hiyo, yeye huvutiwa zaidi na mabinti wanaopenda mazoezi. Mwaka jana kabla sijaondoka Mabibo hostel na kupanga huko Changanyikeni, tulikuwa sisi ni watu wa shato pori (kutembea kwa miguu). Kwa maana ni mara chache sana tulipanda shuttle za kubeba wanafunzi kutoka Mabibo hostel kwenda mlimani. Hatukuona haja ya kufuja fedha kila siku kwa umbali ambao tungemudu kutembea kwa miguu. Kwa hiyo, tulikuwa tunapiga misele, tunakatiza mitaa kwa mitaa kutoka Mabibo hostel hadi chuoni, mlimani. Hasa sana muda wa kutoka chuoni jioni. Asubuhi kuna wakati una kipindi cha saa moja, inakulazimu kuwahi kwa kupanda shuttle. Lakini kama kipindi kinaanza saa mbiIi, tatu au nne huko, tulikuwa tunaenda kwa shuttle pori, yaani miguu yetu.

Sasa, jioni moja tukiwa mdogo mdogo kurejea Mabibo hostel, mitaa ya swimming pool, tukamuona dada mmoja hivi white anapiga mazoezi peke yake. Dah Issa akachanganyikiwa kabisa. Akanambia
'Oy, yule mtoto namuona leo mara ya pili. Kama vipi we tangulia ngoja leo nimpe hai mtoto mkali. Hawa ndio mademu smarter.'

Basi nikaendelea zangu nikimwacha Issa akimfuata white. Hilo ndio jina tulilokuwa tunamwita mrembo yule kwa vile hatukujua jina lake. Baadaye, tulikuja kujua kuwa anaitwa Irene.
Huyo ndio nilikuwa nimemuulizia habari zake katika kuua soo la kunibamba kwenye pumbazo langu kwa mtoto Hellen.

Jioni ya siku hiyo ya kubusiwa na mtoto Hellen, nikiwa zangu Changanyikeni, simu yangu ikapata ugeni wa meseji. Nilipoikamata, nikaangalia ujumbe ule, ulikuwa umetoka kwa Hellen. Nikajikuta natabasamu.

'Mambo Derick, Kesho jumamosi una ratiba gani? Nataka nikualike kwenye semina ya ujasiriamali'

'Nitakuwa free tu, muda gani?' nikajikuta nimeshajibu tayari bila hata kuwaza. Ukweli ni kwamba, siku hiyo ni siku ambayo mimi hukutana na my babe, Welu. Lakini kwa siku hiyo nilikuwa nimemjulisha kuwa ilikuwa nihudhurie kwenye harusi ya braza yangu mmoja anaitwa Toma, ambaye alinipa kadi ya mwaliko licha ya kuwa sikutoa mchango wa harusi. Kwa kweli kipindi cha uchangiaji, nilikuwa na hali ngumu sana mfukoni, bumu lilikuwa limekata na nilikuwa naishi kwa kumpiga mizinga mama. So sikuchangia lakini braza akaamua kunipa mwaliko hivyo hivyo, nahisi alijua ni ukata maana yeye alikuwa kamaliza chuo miaka miwili iliyopita. Hivyo, mimi na Welu ambaye nilikueleza anasoma Duce, hatungeonana wikend hii. Maana yeye pia alinambia alikuwa aende nyumbani kwa shangazi yake jumapili, pale Kurasini, Shimo la udongo.

Kwa hiyo, ujumbe wa Hellen ulinifanya nipotezee Kabisa ratiba hiyo ya harusi ili niende naye huko kwenye semina. Haikuwa poa maana baadaye nilipokutana na braza Toma wiki mbili baadaye alinimaindi kichizi.

'We dogo unadhani maisha umeyapatia huwezi kushiriki kwenye shughuli za wenzio siyo, we ngoja nawe utafikia hatua hizi. Upo jijini, tena wikend unashindwa kuhudhuria harusi yangu?' dah, braza alinimaindi sana. Enewei tuachane na habari za braza Toma. Ujumbe wa Hellen uliingia kwenye simu yangu kunipa maelekezo zaidi baada ya kumuuliza muda gani.

'Kuanzia saa nne hadi saa nane hivi. Lunch itakuwepo free na eneo la semina ni New Africa Hotel' ulisomeka ujumbe wake. Nikasema poa. Nitaenda na Hellen.

'Poa, tutaonana wapi' nikatumia ujumbe huo.

'Tukutane kwenye ATM machine za NBC.'

'Fine' nikamjibu. Basi ikawa hivyo.

Usiku kwenye saa nne hivi, nikapata ujumbe tena kutoka kwa Hellen.

'Mambo Derick?'
'Poa, nambie Hellen!'
'Poa. Ushalala?'
'Hapana bado sijalala.'
"Unafanya nini?'
'Nipo nacheki muvi, wewe je?'
'Ah mi nipo nachati na wewe'
'Kabla ya kutuma message ulikuwa unafanya nini?'
'Nilikuwa nafuatilia mahubiri ya TB Joshua.'
'Anhaa, sawa sawa. Kumbe wewe mlokole eeh?'
'Ndio, nimeokoka na nampenda Yesu.'
'Bwana Yesu asifiwe mpendwa.'
'Amen, vipi wewe unasali wapi Derick?'
'Mh, dah nina kamuda sijaenda kanisani. Naomba nisikudanganye bure mtoto wa Mungu.'
'Sisi sote ni watoto wa Mungu, Derick.'
'Yeah, I guess you're right'
'Yeah, we all belong to him'
'I agree'
'Enhe so, nikupitie jumapili twende church?'
'Ah let me be honest. Umenishtukiza mnoo'
'Haha ok.'
'Yeah'
'So, I can't wait to see you tomorrow tukienda kwa semina.'
'Yeah, I hope soon nitajoin club yenu wajasiriamali.'
'You're warmly welcome. Asante kwa kunipa muda wako Derick.'
'Don't mention it, kwa mtoto mzuri kama wewe hata bahari naweza kukumilikisha'
'You are very funny Derick'
'You sure?'
'Haha, Derick bwana. Sleep tight, ok?'
'And you, sleep loose, haha'
'Hahaha'
'Asante'
'Mh Asante ya nini, Derick?'
'Hujui tu usiku wangu utakavyokuwa murua'
'Kiaje'
'Sio kila mwanaume anapata fursa ya kupewa usiku mwema na mtoto mzuri kama wewe.'
'Niache nilale bwana'
'Didn't think I held you'
'Derick'
'Naam'
'Usiku mwema ee'
'Asante Hellen na kwako pia. Naomba nikuote ee'
'Ruksa!'
'Thank you.'

Basi Ilikuwa burudani kuchati na Hellen. Actually huo utani niliokuwa nachomekea kwenye chat na Hellen niliufanya tu kama utani. Sikuwa namaanisha chochote kitu. Nadhani nilikuwa nataka tu kuona mwitikio wake unakuwaje hasa baada ya kunibusu vile mchana. Nafahamu watu tuna makuzi ya tofauti tofauti, kwangu mimi ah, haya mambo ya kubusiwa nilifanyiwa nikiwa mdogo. Walikuwa wakubwa wakinibeba, utasikia 'hujambo totoo', basi wananizawadia busu shavuni. Na dada yangu Sarah, yeye alikuwa ananikomesha kwa mabusu motomoto yale ya 'abrurrr' tumboni. Basi burudani sana maana hapo ningecheeka hadi nitokwe machozi.

Kwa jinsi nilivyomuona Hellen, alikuwa ni mtoto wa kishua. Nikajua kabisa kwamba, hata lile busu aliloniachia mchana, ilikuwa ni mambo ya kawaida huko ushuani. Mtu akifurahi anatoa busu na inakuwa imeisha hivyo. Sasa sisi waswahili, kila busu unadhani kuna kitu kinatokota nyuma ya mapazia.. Utani wangu hata hivyo ilikuwa kumpima tu nione kama ni easy target. Kama ambavyo umeona chat yetu hapo, huwezi kujua kama mtoto amejipa au la! Maana chat na maneno yake yapo kimtego sana. Hata hivyo, wala sikuwa na nia kabisa ya kumwingiza kingi. Lakini kuna namna nilikuwa nafurahia sana ukaribu wetu huu uliokuwa umeanza kuchipuza.

Jumamosi asubuhi nilimpigia simu Hellen.
'Good morning mrembo' nilimsalimia Hellen halafu kabla hajaitikia nikakumbuka huyu ni mtoto wa TB Joshua, haraka sana nikaongezea

'Bwana Yesu apewe sifa'
'Amen Derick, umeamkaje?'
'Salama tu mpendwa.' nikajibu na kumwachia nafasi.
'Mimi pia nimeamka salama.' Hellen akajibu. Nikagundua nilikuwa nimeishia njiani. Nilipaswa kumuuliza ameamkaje.
'Hellen, about the seminar later in the day…'(kuhusu semina ya ujasiriamali hapo baadaye….) nilikuwa naendelea kuongea alipodakia na kutamka
'Please, don't tell me you won't make it!' (tafadhalali usinambie huji) aliongea kwa masikitiko tayari.
'Noo, on the contrary, nimepania kweli kweli kuwepo. Nimepiga ili unifahamishe dress code ya event.' nilimweleza nikimalizia kwa kicheko laini. Nina kicheko laini, ambacho hukitumia kwa nadra sana hasa baada ya kugundua ndicho kilichomvutia mpenzi wangu Welu hapo awali wakati namlia mingo. So huwa nakitumia sparingly maana kinaweza kuwa na madhara kwa watoto wa kike. Na hapa nilikitumia kwa kusudi, nione matokeo yake kwa Hellen. Nachompendea Hellen, ni wa kishua sana. Unajua utofauti wa mtoto wa kishua na mtoto wa kiswazi ni ile openness(uwazi). Mtoto wa kishua yupo huru sana kujielezea hisia zake. Na huwa wanafanya hivyo without second-guessing (bila kujiuliza-uliza). Kwa hivyo nilipomaliza tu kukitoa kicheko laini, nilijua kama amevutiwa nacho lazima atasema. Kweli bwana, nikasikia.

'Oh oh Derick, napenda vile unacheka. You sure are blessed with many things. By the way hakuna dress code wala cha nini. Just wear casually, ukiwa comfortable ni muhimu zaidi, so vaa vile utajisikia peace.' alinambia.
'Right, basi sawa.' nikatamka halafu nikasikia tena.
'So, umeamua utavaaje D?'
'Ah, niko na suruali ya jinzi la bluu, na juu nitaning'iniza shati la mkono mifupi la kijivu. Kama kawaida yangu, sichomekeagi.'
'Anhaa, great. Don't forget ni saa nne hadi nane so ukianza safari saa tatu itakuwa vizuri tusijekwama kwenye foleni.'
'Yeah right, baadaye!'
'See you!'

Saa tatu na ishirini hivi, nilikuwa kwenye ATM machine za NBC nimetulia nasikilizia motivation speech kutoka kwa mwanagenzi Joel Nanauka. Huyu ni mbongo mwenzetu ambaye niliamua kumsikiliza baada ya kusoma wasifu wake mahali, kuwa alikuwa Tanzania one kidato cha nne halafu chuo kikuu akabamiza gpa ya 5. Imagine. Hizi ni mambo zangu. Kubamiza ma-gpa mazito mazito. Kwa mfano, last year niligonga gpa ya 4.8 kuingia mwaka wa tatu, na huyu mwana ikaonekana sijamfikia bado. So nilitaka nimsikilize nigundue genius yake. Yap, mwana yuko vizuri sana.

Wakati naendelea kusikiliza madini anayomwaga mkali, nikahisi mtu ananigusa begani, maana nilikuwa nimekaa kwenye ukingo wa barabara inayoshuka kuelekea cafeteria. Nikanyanyua macho juu na kumuona Hellen. Wow, mtoto alikuwa mpya. Alikuwa kamechisha nguo zake na zangu. Skirt ya Jeans bluu na fulana ya kijivu. Alipendezaje?
'Oh Hellen you look mwaa!' nilimweleza.
'Hiyo mwaa ndio gani Derick?' akaniuliza kwa sauti fulani hivi. Mtoto ana sauti huyu! We acha tu.
'Namaanisha you look delicious, edible na makila kitu.' nilimtania nikiwa na maana kuwa alipendeza na kuwa mtamu.

'Haha, acha mambo zako Derick. Twende zetu.' alitamka huku ananishika mkono na kunivuta taratibu. Wallah kidogo niruke, maana nilihisi kitu kama shoti hivi. Wee, Ni noma wazee. Basi mdogo mdogo nikawa nashuka na mtoto wa kishua hand in hand. Sometimes ile kutembea na mtoto mkali barabarani na wana wakaona na kuwatumbulia mijicho, hua ni ufahari sana. Sure, maana kuna wana wanaishiaga kuwaona watoto wa kishua kwa mbali. Nikiwa nipo mdogo mdogo tukielekea kwenye barabara ili kupata usafiri mara nikasikia sauti nayoijua vema. Ah kudadeki! Nikajikuta nafyumu kishenzi. Hakawii kuniharibia mtoko huyu mwana.

'Oya Derrick, vipi mwanangu nimetuma maesemues (sms) kibao hureply, kulikoni?' ilikuwa sauti ya Issa.
'Oy niaje, dah itakuwa nilikuwa mbali na simu.' nikaongea naye huku nikimpa ishara kwamba aniache kidogo maana nina mtoko na mtoto mkali wa kishua. Jamaa aliona, lakini huyu mwamba anakuwaga na mambo ya ajabu sana sometimes. Yaani ile kuzingua kwa makusudi. Na hapa alitaka tu nimu-introduce kwa mrembo. Kwa hiyo alikusudia kujongea tulipo.
'Mambo vipi?' alimpa hai Hellen.
'Poa. Habari yako?' Hellen akajibu.
'Njema.' Jamaa akajibu. Nikaona hapa ndio pa kuweka mstari. Issa namfahamu. Ana ujinga mwingi sana.
'Mpendwa Hellen, huyu ni my best friend anaitwa Issa. Issa, this is Hellen. Mtu wangu wa nguvu'
Niliongea kuwatambulisha.
'Oh nice to meet you!' Hellen Alizungumza.
'Oh mtoto anazungumza kinge. Wow, nice to meet you too.' lijamaa likanyoosha na mkono. Dah nilitaka niupangue lakini nikaona itakuwa Soo, so nikavunga.
'Kwa hiyo ni mtu wa nguvu siyo, hebu nyoosheni maelezo bwana.' Issa akaongea huku anatutazama kwa zamu. Nikaona huyu mpuuzi anakusudia kukitia mchanga kitumbua changu. Nikaona nimuondolee uvivu.
'Ah we jamaa, baadaye kwanza. Tunahitaji kuwa mahali now.' niliongea kwa msisitizo.
'Wapi tena?' Jamaa akauliza kwa lafudhi ya kipwani.
'Tunaenda semina Issa. Are you interested?' Hellen akaongea. Ah, nikaona jamaa ametibua mchongo. Nikamkazia macho kuonesha kwamba nataka atoe udhuru. Lakini jamaa kama kawaida yake kuharibu mipango, si akakubali bwana!! La la la! Nilifyumu kishenzi yaani. Yaani nilijikuta naishiwa pozi kabisa. Basi tukachukuwa bajaji hadi mlimani city, jamaa Akiwa ametawala mazungumzo. Mimi kimya, na nikagundua Hellen pia alikuwa anafanya kuitikia tu almradi. Issa ni aina ya watu ambao, anaongea non stop, yaani mfululizo na bila kuchoka. Wale ambao anataka anapoongea uwe msikilizaji tu, yaani akiona kama unawaza kingine basi aidha ataendelea kuongea huku anakugusa gusa au hata kukufinya. Unaweza ulale usingizi wa nusu saa yeye akiwa anasimulia ukaamka jamaa bado anaendelea kuongea hadi midomo imkauke na povu pambizoni mwa midomo lionekane na wala asichoke. Cha muhimu wewe uoneshe kuitikia. Na mara moja moja uchomekee maneno mawili ya kumchaji, basi mtakesha usiku kucha na mshinde mchana kutwa jamaa akiwa bado anasimulia. Basi namna hiyo mshikaji akawa amezingua na kuharibu kabisa siku yangu.

NB: Simulizi hii bado haijahaririwa!

Itaendelea
David.

Usichelewe Sana, kitabu pendwa Cha 'Mateka wa Huba' nakala zimebakia chache Sana. Weka oda yako mapema.
tapatalk_1598866586158.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom