Njia 6 za kupata matokeo chanya unayoyataka kutoka kwa mtoto wako

Oct 5, 2018
33
58
Wazazi/walezi wengi duniani kote wamekuwa katika mahangaiko ya kutafuta njia sahihi za kuzitumia katika kupata matokeo chanya kwenye nyanja mbalimbali za maisha ya watoto wao: wachache sana wamefanikiwa, lakini wengi wameshindwa kutokana na kutojua njia mbalimbali wanazoweza kuzitumia ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya.

Kati ya njia zote zilizofanyiwa tafiti yakinifu ni njia moja tu, inayotumiwa na wazazi/walezi wengi duniani, njia ya ADHABU. Lakini, njia za kuleta matokeo chanya kwenye mienendo na maisha ya watoto zipo nyingi sana. Katika makala hii nitawaonesha njia zaidi ambazo wazazi/walezi mnaweza kuzitumia katika kuleta matokeo chanya kwenye maisha ya watoto wenu.

Zifuatazo ni baadhi ya njia zinazoweza kumuwezesha mzazi/mlezi kupata matokeo mazuri katika kumkuza na kumuendeleza mtoto wake kijamii, kiafya, kielimu au kitabia: -

1. KUMRUBUNI MTOTO WAKO
Sio kila urubuni ni urubuni mbaya katika kumkuza na kumuendeleza mtoto wako, kuna urubuni unaweza ukawa wenye manufaa. Mtoto anaweza kurubuniwa na akaleta matokeo mazuri. Mtoto anayechukia kula mboga za majani anaweza kuambiwa akila mboga za majani atakuwa na nguvu kama mcheza mpira wa miguu au wa mikono anayempenda sana. Mtoto atafanya unachomtaka afanye bila kupinga.

Japo kuwa utakuwa umemdanganya lakini haijaleta madhara na amekula mboga za majani zenye umuhimu katika maendeleo na ukuaji wa mwili wake. Njia hii inafaa zaidi kwa watoto wadogo ambao ndiyo wameanza kupata ufahamu.

2. KUPONGEZA MTOTO WAKO
Mtoto anaweza kuleta matokeo chanya zaidi pindi apongezwapo kila afanyapo jambo fulani zuri. Mtoto anayepongezwa kwenye mambo madogomadogo kabisa anayoyafanya, huhamasika kuendelea kufanya mambo mazuri zaidi. Njia hii ni nzuri kwa watoto wa kuanzia mwaka mmoja hadi 18. Kila mtoto anapenda kupongezwa. Pongezi huwafanya wajihisi wao ni wa muhimu.

Kumpongeza mtoto kuna mfanya afanye mambo makubwa zaidi kwenye nyanja mbalimbali za maisha yake. Hali itakayopelekea mzazi/mlezi kupata matokeo chanya anayoyatamani kuyaona kutoka kwa mtoto wake.


3. KUADHIBU MTOTO WAKO
Adhabu kwa watoto ni njia ambayo haiepukiki katika kumkuza na kumuendeleza mtoto japo kuwa inapigwa na watu wengi duniani. Adhabu sio njia mbaya endapo mzazi/mlezi atazingatia kanuni nzuri za utoaji adhabu. Cha msingi ni kwamba, mzazi/mlezi ahakikishe adhabu zitakazotolewa kwa mtoto ziwe ni zenye kuweza kumjenga na sio kumbomoa mtoto. Adhabu humfanya mtoto ajihisi mkosaji pindi akikosea, hali inayopelekea akafanya vizuri wakati ujao.


4. KUMTISHIA MTOTO WAKO
Mtoto anaweza kuleta matokeo chanya kwa kutishiwa tu. Vitisho vinaweza kutoa hamasa kwa mtoto kuzingatia au kuepuka kuyatenda mambo fulani. Kwa mfano, mtoto mwenye maendeleo mabaya shuleni anaweza kuambiwa, usipofanya vizuri msimu huu sitokununulia kiatu kipya. Mtoto anaweza kuzingatia kwa kitisho hicho tu, na akafanya vizuri kwenye masomo yake.

Katika hili angalizo ni kwamba, mtoto asipewe vitisho vitakavyo mletea mtoto athari za kisaikolojia.

5. KUMFUNDISHA MTOTO WAKO
Mtoto anaweza kuleta matokeo chanya kwa kumpa mafundisho maalum juu ya masuala mbalimbali. Mtoto anayeendekeza michezo zaidi ya mambo mengine anaweza kupewa mafunzo maalum juu ya matumizi sahihi ya muda wake. Mara nyingine tunaweza kutumia nguvu sana kwa watoto wakati katika uhalisia ni kwamba wanakua hawajui tu, njia nzuri za kufanya mambo ambayo wazazi/walezi wanawataka wayafanye. Maya Angelou anasema; "Ukijua vizuri, unafanya vizuri" Njia hii ni moja kati ya njia ninayoipendelea kuliko zote nilizozijadili haho juu.

6. KUWA MFANO KWA MTOTO WAKO
Mtoto hutaka kuwa kama mzazi/mlezi wake kwa angalau asilimia tisini (90%), hivyo endapo mzazi/mlezi utakuwa vile unavyotaka mtoto wako awe, basi hautotumia nguvu nyingi sana kwani atajikuta anakuwa wewe hata bila ya yeye kujitambua. Mzazi/mlezi asiyependa mtoto wake asinywe pombe, basi ni lazima ahakikishe yeye pia atumii pombe. Ni ngumu sana mtoto kuwa yale ambayo hayaoni nyumbani kwao yaani kwa mama, baba au ndugu zake wengine.

Mwisho nitoe wito kwa wazazi/walezi kutokupenda kutumia njia moja katika kutafuta matokeo chanya kutoka kwa watoto wao. Njia za kuleta matokeo chanya kwa watoto zipo nyingi na kila moja inafanya vizuri katika hali na mazingira tofautitofauti, hakuna hata njia moja kati ya hizo nilizozieleza hapo juu ambayo inaweza kuingia katika kila hali kwenye maisha ya mtoto.


Imeandikwa na:

JUSTINE KAKOKO

Managing Director / Author / Educator/ Parenting Consultant
 
Back
Top Bottom