"Nitakuwa Wa Mwisho Kuishabikia Katiba Mpya" Manyerere | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

"Nitakuwa Wa Mwisho Kuishabikia Katiba Mpya" Manyerere

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by KIM KARDASH, Apr 17, 2012.

 1. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #1
  Apr 17, 2012
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  [h=3][/h]
  [​IMG]


  Nimejitahidi kutafakari ni kwa namna gani Katiba mpya itatuletea mabadiliko ya kweli tunayoyataka, nimekosa majibu - na sidhani kama nitayapata.
  Fikra zangu zinanirejesha enzi za kudai Uhuru. Wapo walioamini kuwa kwa kupata Uhuru, taifa letu lingepiga hatua kubwa kimaendeleo. Wapo waliojiaminisha kuwa kwa kupata Uhuru, maana yake umasikini ungetoweka.Wengine wakauona Uhuru kama mwanga wa kutufikisha kwenye nchi ya kimaendeleo mithili ya Marekani na Ulaya. Bila shaka walikuwapo walioamini kuwa kwa kupata Uhuru, basi kila kitu kinachomfaa binadamu kingepatikana katika taifa letu.


  Hizo zilikuwa njozi. Miaka 50 baada ya Uhuru, tuna makabwela wengi kupindukia. Idadi yao inaongezeka. Ile ahueni ya kuwapa Watanzania elimu ya bure, maji bure, huduma za afya bure, imetoweka. Mambo yanazidi kuwa magumu.

  Ugumu huu umewafanya wengi waamini kuwa kwa kupata Katiba mpya, basi kila kitu kitakuwa kwenye mstari. Tunarejea tena kwenye njozi za Uhuru. Wanaamini kwa kupata Katiba mpya, watapata milo mitatu kwa siku, watasomesha watoto, watajenga nyumba, watanunua magari, watafanya kila linalomfaa mwanadamu ili aweze kuishi kwa sifa zitakazomtofautisha na wanyama wengine; na kwa kifupi ni kwamba Katiba mpya, mafisadi wote watayeyuka kama theluji.


  Kwa nadharia hizi, naapa kwa dhati kabisa kwamba hata kama tutapata Katiba mpya, itakuwa kazi bure. Wakati fulani aliyekuwa Rais wa Ghana, Jerry Rawlings, alipata kuuliuzwa ni kwa namna gani ameweza kuifikisha nchi yake kwenye maendeleo ya kupigiwa mfano.


  Rais Rawlings, akajibu kwa kujiamini kabisa kwamba ametumia sera za Tanzania na maandiko ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, kuifikisha Ghana hapo ilipofika. Akasifu maandiko na sera za Tanzania akisema zilikuwa zimebeba mafunzo maridhawa kwa taifa lolote la Afrika kuweza kuzitumia kwa mazingira yake na kujipatia maendeleo.


  Huyo alikuwa Rawlings. Yupo mwingine. Huyu ni Rais Paul Kagame wa Rwanda. Kwa Kagame, Tanzania ni darasa tosha. Amekuwa muwazi kueleza mbinu alizozitumia kuifikisha Rwanda hapo ilipo; nyingi akiwa amezinakili kutoka kwetu. Nidhamu, utendaji kazi na kuyashusha maendeleo kwa wananchi, ni mambo aliyoyazingatia. Haishangazi kuiona Rwanda ikiitumia Oktoba 14 kama siku rasmi ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere.


  Si hao tu, bali yupo Rais Hugo Chavez wa Venezuela, ambaye kama ukiisema vibaya Tanzania kwa sera zake, anaweza kukuadhibu! Nimepata kuhudhuria Mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) katika jiji la Havana, Cuba. Rais Chavez alitumia muda mrefu kumsifu Mwalimu Nyerere na sera za Tanzania kwamba kama vikifuatwa, mataifa ya Kusini yatapiga hatua kubwa kimaendeleo. Chavez ni mmoja wa wafuasi mahiri wa siasa ya Ujamaa. Amehakikisha mali za umma zinabaki kuwa za umma. Zinawanufaisha wananchi wote. Anatumia fedha za umma kusambaza huduma za kijamii kwa wananchi wote bila ubaguzi. Ni mfuasi mkuu wa Mwalimu.


  Waliofaidika kwa sera za Tanzania ni wengi mno. Siwezi kuwataja wote. Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba hata kabla ya Katiba mpya, Tanzania tumekuwa na sheria na sera nzuri sana. Tumepata bahati ya kuwa na maandiko mazuri na viongozi walioona mbali, lakini vyote tumevipuuza. Tumeviweka kando. Sasa tunalilia Katiba mpya kana kwamba itakuja na kitu cha ajabu sana.  Kama hatutabadilika na kuwa watu wa vitendo, hiyo Katiba mpya hata ikipambwa kwa maandishi ya dhahabu na almasi, na ikafukizwa maradhi ya karafuu; itakuwa kazi bure.
  Katiba ya sasa ukiisoma hutaona kama ina dosari nyingi za kuwafanya wengine waisigine. Haina udhaifu huo. Katiba yetu imeeleza vema kabisa namna ya kulinda rasilimali za nchi yetu. Imeeleza dhima ya kila Mtanzania katika kulinda na kuhifadhi rasilimali asilia. Imeainisha haki ya kila Mtanzania kutendewa haki mbele ya vyombo vya utoaji haki. Imesema wananchi wote wako sawa mbele ya sheria.
  Kutoka na Katiba, tuna sheria nyingi. Tuna sheria hadi za kuzuia uvutaji sigara katika hadhira-sheria ambayo haipo katika mataifa mengi duniani. Tuna sheria za kulinda na kuhifadhi mazingira. Sheria hizo zikatungiwa sheria ndogo ndogo zinazozuia kukata miti hovyo, kujisaidia maeneo yasiyoruhusiwa, kutotupa taka ovyo, na kadhalika.
  Pamoja na utitiri wa sheria zote hizo, tujiulize, kitu gani kimetukwamisha hata tusiweze kusitekeleza? Juzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametoa ripoti inayoonyesha namna Tanzania inavyotafunwa. Sheria za kuwabana wezi zipo, tena zipo sheria kali kama ile ya Uhujumu Uchumi. Kila mwaka CAG anatoa ripoti akiainisha majizi wanaolimaliza taifa. Anafichua njama zinazofanywa na viongozi na wafanyabiashara kuhakikisha Tanzania inasalia mifupa. Hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika. Hawachukuliwi hatua si kwa sababu Katiba ni mbaya, au sheria hazipo, bali kwa sababu ya wanaopaswa kuifanya kazi hiyo kuwa nao ni sehemu ya tatizo.
  Ndiyo maana najiuliza, hiyo Katiba mpya itakuja na upako gani utakaowafanya Watanzania hawa hawa, wa tabia hizi hizi, na wa uporaji rasilimali huu huu, wabadilike na kuwa watu tofauti? Silioni hilo.


  Katiba yetu hakuna mahali inasema wageni ndiyo wawe wa kwanza kufaidi rasilimali za nchi. Haisemi wao ndiyo wafaidi samaki wetu maziwani na baharini, lakini leo yote haya yanafanyika huku umasikini ukiongezeka kwa wananchi. Kwenye sheria za nchi yetu ipo inayompa mamlaka rais kuidhinisha mtu anyongwe. Hii ndiyo adhabu kali kabisa katika nchi yetu. Wapo wanaoipiga vita kwa maelezo kwamba haisaidii kumaliza matatizo. Wanasema inakinzana na haki ya msingi ya binadamu ya kuishi.
  Sasa kama hivyo ndivyo- kwamba sheria ya kuua ipo, lakini inatakiwa ifutwe- sheria dhidi ya wahujumu uchumi ipo, sheria ya kufilisi mali za mafisadi zipo, hiyo Katiba itakuja na jipya gani?
  Ndiyo maana nasema Katiba ya kweli ya Watanzania inapaswa kuandikwa katika mioyo na utashi wao, na wala si ya kuandikwa kama hii tunayoililia sasa.
  Tunapaswa kubadilika kifikra. Tunapaswa kuwajibika-kila mmoja kwa nafasi yake-tunapaswa kuwa watu wa vitendo zaidi badala ya blabla na porojo zisizokoma, tunapaswa kusimamia sheria na kanuni tunazojiwekea.


  Tunaweza kuwa na Katiba nzuri sana, lakini bila kuwa na wasimamizi wa kweli wa Katiba hiyo, tutabaki kuwa kichekesho.
  Katiba mpya na nzuri haitoshi kutufanya tushibe, haiwezi kuwasomesha bure watoto wetu, haiwezi kupunguza ajali za barabarani kama madereva wataendelea kubebwa, haiwezi kumaliza umasikini kama kila siku kazi yetu ni kuamkia vilabuni na kushinda kwenye michezo ya “pool”. Katiba mpya haiwezi kutufaa jambo kama wengi wetu tutakuwa tukisubiri kulishwa chakula na mtu mmoja katika familia ya watu 15.
  Wala Katiba mpya haiwezi kutufaa lolote kama maono ya viongozi wetu ni kuwahamasisha vijana kukopeshwa bodaboda badala ya kuwapa matrekta na zana nyingine za kuwawezesha kuzalisha mali kwa njia za kisasa.


  Katiba mpya haiwezi kutufaa kitu kama tutaendelea kuabudu ushirikiana na kuamini kuwa maendeleo ya mtu yanaletwa kwa imani za kijinga za kuwaua ndugu zetu albino na kuchukua viungo vyao. Hatuwezi kubadilika kimaendeleo kama tutabaki kuwa taifa la watu wanaoamini tunguli na matangazo ya waganga matapeli eti wanaosafisha nyota na kutufanya tupande vyeo kazini. Kama ingelikuwa kweli mtu akipata dawa hizo anapanda cheo, basi kampuni ingekuwa na mawaziri 50 au 100 kwa wakati mmoja!


  Tuna rasilimali ya mabonde, wanyamapori, madini, maziwa, bahari, mito, ardhi isiyo na mfano; na ukwasi wa kila aina. Tunachohitaji si Katiba pekee, bali viongozi makini wa kuwafanya wananchi wafaidike na ukwasi huu. Kwangu mimi, suala la kuwabadili kwanza Watanzania kifikra ili waipende nchi yao, wapende kuwajibika ndiyo yangekuwa mambo la maana zaidi kwangu.


  Tukiwa na Katiba mpya, lakini tukawa na kiongozi anayemzuia Waziri kupanua barabara eti kwa sababu kwa kufanya hivyo anawaudhi wapigakura, haki ya Mungu tutaendelea kuonekana kama taifa ya washirikina tu.


  Mwisho, niseme kwamba Katiba “nzuri na tamu” haina maana kama uwajibikaji wa viongozi wetu na wananchi vitakosekana. Je, uwajibikaji utaletwa na maandiko tu; au kwa dhamira na utashi wa wenye nchi? Je, utaondoa dhambi katika jamii kwa kujenga makanisa au misikiti mingi? Au utapunguza dhambi kwa kuwabadili waumini kiroho? Unaweza kuwa na makanisa na misikiti mizuri sana, lakini bila kuvitumia kwa maudhui yake, itakuwa kazi bure. Yapo mataifa yasiyokuwa na Katiba iliyoandikwa, lakini yapo mbele kimaendeleo. Nitakuwa wa mwisho kuamini kuwa Katiba mpya ndiyo suluhu ya madhila yote yanayotufika sasa.


  manyerere@hotmail.com
  0759488 955
  CHANZO: GAZETI LA JAMHURI
   
 2. Narubongo

  Narubongo JF-Expert Member

  #2
  Apr 17, 2012
  Joined: Nov 3, 2010
  Messages: 1,922
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 135
  huyu ni manyerere mayor wa mwanza sio? ukweli mtupu
   
 3. Mwanajamii

  Mwanajamii JF-Expert Member

  #3
  Apr 17, 2012
  Joined: Mar 5, 2008
  Messages: 7,080
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 0
  Hata wewe mheshimiwa ambaye unategemewa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kjitokeza kutoa maoni ya aina Katiba inayotakiwa kwa msatakabali wa Tanzania ya sasa na baadae unakuwa wa mwisho kuiamini? kaz kweli kweli, hayo ulioyaorodhesha suluhu yake si ni aina ya katiba itakayoundwa? utapataje viongozi waadilifu kama unakuwa wa mwisho kuimanini Katiba mpya na kwa maana hiyo wa mwisho hata kutoa maoni? Jmani tuache umbumbumbu wa mawazo. Tukiwa na Katiba safi yote hayo hayatakuwa na mwanya tena. Hivi kama katiba itasema kiongozi asiyemwadilifu na anyongwe kutakuwa na wasi wasi tena wakati watanzania tumeamua kwa pamoja? Shule jamani uanajua siyo lazima ukae darasani. Mheshimiwa unategemewa kuhamasisha wananchi wako wakatoe maoni yao acha kulalama, japo kweli inawezekana kabisa upeo wako wa kutafakari ndo umeishia hapo lakini unapaswa kuwa na ubongo wa ziada .
   
 4. N

  Naytsory JF-Expert Member

  #4
  Apr 17, 2012
  Joined: Nov 3, 2011
  Messages: 1,589
  Likes Received: 244
  Trophy Points: 160
  Jaribu kusoma tena unaweza kuelewa anachomaanisha. Hivi mkuu hata katiba iliyopo ingefuatwa kama viongozi wetu walivyoapa kwa kutumia vitabu vitakatifu tena kwa kumnyooshea Mungu unadhani hali ya nchi ingekuwa hivi? Tatizo ni wasimamizi wa katiba wameasi.
   
 5. Shine

  Shine JF-Expert Member

  #5
  Apr 17, 2012
  Joined: Feb 5, 2011
  Messages: 11,514
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0
  Yetu macho kama hatutawekewa katiba ambayo imechakachuliwa kama kawaida ya ccm kila penye mkono wake pamechakachuliwa
   
 6. C

  Chief Lugina JF-Expert Member

  #6
  Apr 17, 2012
  Joined: Jul 1, 2011
  Messages: 290
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Huyu siyo Mnyerere yule mayor wa Jiji la MWANZA,but huyu ni MANYERER JOCKTANI,Aliye kuwa mwandishi wa RAI aliyeamua kujivua gamba na ndugu yake Bailie nakuanzisha gazeti lao la JAMHURI...
   
 7. m

  mharakati JF-Expert Member

  #7
  Apr 17, 2012
  Joined: Sep 29, 2011
  Messages: 1,275
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  Manyerere yule wa Lowassa au? Jackton? sasa hapa anaonyesha uzalendo kidogo huku anatumikia wale walionufaika na mfumo wa ufisadi...yeye ni mmoja wapo wa hypocrites katika nchi hii wanaorudisha nyuma maendeleo yetu..lazima watz tuwe na msimamo haswokua na haswa watu wenye taaluma na wenye uwezo na mwamko kama yeye ili wengine wafuate, sasa sisi wachache tukinunuliwa na kukosa msimamo tunashindwa kuwabadilisha wale wanaotutegemea huku mashambani na vijijini.
   
 8. doctorz

  doctorz JF-Expert Member

  #8
  Apr 17, 2012
  Joined: Aug 10, 2010
  Messages: 907
  Likes Received: 4
  Trophy Points: 35
  Sasa kama kila mtanzania akiwa kama wewe, si taifa litauzwa?

  Jitahidi kujihusisha na yale yatakayo leta maendeleo na mabadiliko kama mtanzania mwema.
   
 9. b

  bantulile JF-Expert Member

  #9
  Apr 17, 2012
  Joined: Feb 27, 2012
  Messages: 1,439
  Likes Received: 84
  Trophy Points: 145
  Ukimsoma vizuri Manyerere, hakatai Katiba mpya, bali anachosema ni kuwa haamini kama katiba mpya italeta maendeleo. Anasema katiba iliyoopo ikitumiwa vizuri inaweza kuleta maendeleo. Baadhi ya nchi za Afrika zimeitumia katiba hii hii tuliyonayo Watanzania kujiletea maendeleo nchini mwao. Hii pia haina maana kuwa kitu kizuri kisiboreshwe, la hasha! Katiba yetu inaweza kuboreshwa na ikisimamiwa vizuri italeta maendeleo. Nampenda Manyerere. Wazo kuu la Manyerere, ni kutumia vizuri kile tulichonacho kwanza kabla hatujafikiria kingine. Anaweka msisitizo katika matumizi bora na sahihi ya rasilimali tulizonazo. Tutatengeneza katiba nyingi nzuri pasipo matumizi itakuwa kazi bure. hatutapata maendeleo tunayoyataka. Ukionyeshwa njia ya kwenda Kyela pasipo kwenda Kyela kamwe hautafika hata kama mwongozaji wako atakuonyesha kwa vielezo lukuki ikiwa ni pamoja na vibao, ramani nk.
   
Loading...