Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,393
Inapotokea kutofautiana, ni vyema mkayamaliza kwa amani na maisha yaendelee kama kawaida......
Tunatakiwa kujua kwamba lengo la ndoa siyo kuepuka kukorofishana , hapana . Ukweli ni kwamba kukorofishana kunapotumiwa vema huweza kujenga uhusiano mzuri na imara sana. Kwa sababu kukorofishana hakuwezi kuepukika kwenye ndoa kunatakiwa kutumika kama shule na dawa ya kuimarisha ndoa.
Kwa hali hiyo hakuna ndoa ambayo haina makosa, kwa sababu ndoa ni binadamu hao ambao siyo kamili. Kwa hiyo, mtu anapotarajia kuwa au kuishi kwenye ndoa isiyo na kukwaruzana, ni sawa na mtu huyo kutarajia kukutana na binadamu ambaye ni kamili, yaani asiyekosea.Mtu ambaye hakubali au angalau hataki kuelewa kwamba, ndoa ni lazima iwe na mikwaruzo anaweza kukabiliwa na tatizo lingine baya zaidi kwenye ndoa yake. Kwa kutokujua au kuepuka kukwaruzana, hawezi kuwa tayari kukubali kujadili migogoro ya kindoa ili kupata ufumbuzi.
Hawezi kulikubali hilo kwa sababu haamini kwamba ndoa yenye kukwaruzana ni ndoa.Wakati mwingine rafiki, ndugu au jamaa zetu hutusimulia jinsi ndoa zao zisivyo na kukwaruzana kama kwamba ni za malaika watupu. Bila kujua, huwa tunajikuta tumewaamini. Tunapowaamini huwa tunachukulia kukwaruzana kuliko kwenye ndoa zetu kama jambo au kitu ambacho hakikutakiwa kuwepo. Hapo hujikuta tukitamani kuondoka kwenye ndoa hizo kwa matarajio kwamba tunaweza kukutana na "malaika" ambao tutajenga nao ndoa zisizo na doa.
Hata pale ambapo tunasema wanandoa wanapendana sana, bado ndoa yao ni lazima itakuwa na kukwaruzana. Lakini wanachofanya hawa na ambacho huenda wengine hawafanyi ni kujadili tofauti hizo sawia na kuamua kuzisahau na hapo wote kukubali kujifunza kutokana na tofauti hizo. Wale walio tayari kujadili tofauti zao sawia ndiyo ambao ndoa zao huwa na afya sana hadi wengine kushangaa kama siyo pamoja na kuona wivu. Wale wanaodhani ndoa ni mahali pa kila jambo kwenda kama mtu atakavyo, ndoa zao hupogoka vibaya na kufa kwa kishindo........