Nisikilizeni CHADEMA: Tatizo ni UKAWA, Hili ndilo chaguo langu la rais wa 5

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,988
ukawa+px.jpg


Na. M. M. Mwanakijiji

(Angalizo: Makala hii ni ndefu; nakala ya kudownload imeambatanishwa)

Kuna wakati natamani kukaa kimya lakini kuna wakati kukaa kimya sitamani. Mambo mengine ni rahisi kuyaacha yapite tu lakini mengine yakipita ukayaacha dhamira inabakia kukupigia kelele ‘kwanini kwanini?' Hili la chama kikuu cha upinzani nchini CHADEMA kujifunga katika Ushirikiano wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ni miongoni mwa mambo ambayo nimeyazungumza kidogo huko nyuma kama dokezo la kwanini naamini lilikuwa ni kosa jingine kubwa kwa CDM kujifunga nao. Sikuwa shabiki wa UKAWA toka ilipoundwa na hata sasa bado si shabiki wa UKAWA; nimebakia kuwa shabiki wa CDM kama chama kikuu kinachotaka kuongoza mabadiliko nchini lakini UKAWA ilivyo sasa inanifanya niwe na ladha fulani ya uchachuuchachu hivi kwenye fikra zangu. Naombe nilete kesi yangu kwa kadiri ilivyo mawazoni mwangu kwa muda sasa.

Kuna mambo kadhaa ambayo niyaoneshe tu kwanini Ushirikiano huu haukuwa wa lazima na umechelewesha baadhi ya mambo ambayo CDM ingeweza kuyafanya kwa ufanisi mkubwa katika kujiandaa na Uchaguzi Mkuu ambao binafsi naamini wa CHADEMA kuupoteza. CCM haijaweza kuja na majibu ya matatizo ya Watanzania na hata katika kutafuta mgombea wake imejikuta ikirudia kule kule ilikotoka kwa watu wenye fikra zile zile na mawazo yale yale ambayo tayari yamelifikisha taifa hapa. CCM wangemsimamisha mtu kama Jaji Ramadhani na Asha Migiro kwa mfano au Ramadhani na Makongoro labda kidogo tungesema wanataka kufanya kitu tofauti miaka mitano ijayo; kwa kumsimamisha Magufuli wametuambia kuwa bado hawajajifunza makosa yao ya 2005 na hawako tayari kujifunza hata kwa viboko.

UKAWA Haikuundwa Kwa Ajili ya Kuing'oa CCM Madarakani

Ni vizuri tujikumbushe vizuri kuwa huu ushirikiano haukuja kwa sababu ya kutaka kuungana kuindoa CCM madarakani. UKAWA ulikuja kama mwitikio uliochelewa (a delayed response) ya mambo yaliyokuwa yanatokea kwenye Bunge la Katiba. Tukumbuke kuwa upinzani ulipokubali ule mchakato haramu wa Katiba Mpya ulifanya hivyo kila mtu kichama chama. Hata walipoitwa kwenda Ikulu mara kadhaa walifanya hivyo kama vyama huru. Baada ya Rais kutangaza kuanzisha mchakato wa CCM kuandika Katiba Mpya vyama vya upinzani havikukaa pamoja kuwa na msimamo wa pamoja ambao ungewaunganisha kuelekea mchakato huo; kila chama kilipinga au kushiriki kama chama. Na hata wajumbe wa Bunge la Katiba walivyotakiwa kupendekeza kila chama kilifanya hivyo kama chama. Hakukuwa na ushirikiano wa pamoja wa kukabiliana na nguvu kubwa ya CCM ambayo tuliitabiri mapema kuwa itauteka mchakato huo.

Ni mpaka pale walipoona wamezidiwa nguvu huku rasimu ya Katiba ya Tume ya Warioba ikitupwa pembeni na huku viongozi mbalimbali wa CCM wakishikilia nafasi nzito za kuelekeza mchakato huo. Kuanzia aliyekuwa Spika wa Bunge la Muungano Samuel Sitta aliyepewa Uspika wa Bunge la Katiba hadi Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais aliyepewa Unaibu Spika (na sasa kapewa nafasi ya kugombea kama Makamu wa Rais kwa tiketi ya CCM) na viongozi wengine mchakato mzima ulisimamia na CCM au na watu wenye mapenzi na CCM kama Jaji Ramadhani. Upinzani ulijikuta hauna sauti ya pamoja na hapa ndipo haja ya wao kuwa na umoja wa pamoja kupigania kile walichokiita "Katiba ya Wananchi". Yaani, hawakuona haja yakuwa pamoja toka mwanzo, siyo kwenye kukusanya maoni, siyo kwenye kupendekeza wajumbe bali mpaka walipojikuta wanazidiwa nguvu ndio wakasema "tushikamane jamani vinginevyo tutaunguka".

Matokeo ya kuchelewa huku ni kuwa CCM waliuteka mchakato ule wakaenda nao mpaka dakika ya mwisho, taifa likapoteza mabilioni ya fedha na mwisho wa siku hakukuwa na Katiba Mpya wala mtoto wa Katiba Mpya isipokuwa kauli za "tulijaribu". Ukweli huu ni kuwa UKAWA kama ilivyoundwa haikuwa chombo cha kuweza kuunganisha nguvu kuiondoa CCM; kama walishindwa kupitisha Rasimu ya Katiba wakizidiwa nguvu kwa kila kipimo bila ya shaka watakuwa na kibarua kugumu zaidi cha kuunganisha nguvu Oktoba 25 kama ambavyo tumeanza kuona dalili.

UKAWA haikuandaa Kanuni za Ushirikiano (Protocol on Cooperation) Kabla ya Kuanza Kushirikiana

Mojawapo ya mambo muhimu sana yanayofanyika vyama vinavyotaka kushirikiana kuelekea kutawala (siyo kama UKAWA) ni kuandaa na kukubaliana juu ya kanuni za ushirikiano (principles of cooperation) kwamba ili vyama vishirikiane katika kuaminiana bona fide- (in good faith) basi baadhi ya mambo yanahitaji kukubaliwa kuongoza ushirikiano huo. Mambo haya yalitakiwa kufahamika na kukubaliwa kabla ya kutia sahihi makubaliano ya kuelewana au kama sehemu ya makubaliano ya kuelewana (Memorandum of Understanding).

Ikumbukwe kuwa tangu ndani ya Bunge la Katiba hakukuwa na makubaliano yoyote yenye nguvu isipokuwa kauli za "kushirikiana" za viongozi wa vyama vya siasa na makubaliano hayo yalikuja bila hasa kuwa na baraka za vyama husika isipokuwa maamuzi ya viongozi wa juu wa kitaifa. Hili lilikuwa na athari moja ambayo nayo inatudokeza kukwamakwama huku – makubaliano yamesimama au kuanguka na viongozi wa kitaifa.

Kanuni hizi zingeweka msingi wa ushirikiano wa kisera (policy cooperation), ushirikiano wa masuala (issues cooperation) – yaani masuala kama ya kuweka kwenye ilani na ushirikiano wa kutawala (governing cooperation). Ili upinzani uweze kufanikiwa kweli hili la mwisho ndio msingi hasa. Bahati mbaya sana kwa maoni yangu ushirikiano wa UKAWA sasa hivi unaonekana una lengo hasa la kushinda uchaguzi kuliko kutawala taifa. Hili nitalifafanua hapa chini.

UKAWA si Ushirikiano wa Kutawala Bali Kujaribu Kushinda Uchaguzi

Kati ya vitu ambavyo watu wengi tumekuwa tukijadiliana na wengine wameniona kama napinga ushirikiano wa vyama vya upinzani na kusababisha CCM iendelee kutawala. Nimewahi kusema huko nyuma kuwa haitoshi tu kutaka CCM iondoke madarakani bila kutaka uongozi bora kuliko wa CCM. Baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipinga hili wao wanasema "haijalishi nani anaingia kuongoza alimradi CCM imetoka kwanza". Ukiangalia hili kidogo lina ulaghai fulani wa hatari. Hatutaki kuwaondoa CCM madarakani ili yeyote tu aingie madarakani.

Somo hili nimetolea sana mfano wa nchi za Malawi na Zambia. Wananchi kweli walikuwa wamechoka vyama vilivyowaongoza kwenye uhuru na wakafika mahali wakasema inatosha sasa. Zambia wakamuingiza Chiluba na Malawi wakamuingiza Bakili Muluzi. Viongozi hawa wote wawili walikuwa maarufu sana na walionekana kuja kukata kiu ya mabadiliko. Bahati mbaya wote walifeli. Hata Kenya tunaweza kutolea mfano wa Mwai Kibaki. Kimsingi ni kuwa hatutaki kubadilisha watawala tu kwa sababu ya sura za watawala; tunataka kubadilisha utawala kwa sababu ya sera za watawala. Ndio maana wengine hatushtuki sana na kupitishwa kwa Magufuli; Magufuli analeta sura tu tofauti na ya Kikwete na ya Lowassa, Sitta, au Migiro. Hawawakilishi wala kuleta sera mpya. Si watu wale wale wapiga debe tumewaona wamehama kutoka mgombea mmoja na wameenda kwa mwingine wakiimba sifa zake wakati wanaweza kuwa ni miongoni mwa wale karibu elfu moja ambao hawakumpigia kwenye Mkutano wao mkuu?

Hivyo, kanuni za ushirikiano wa upinzani basi ni lazima zilenge katika kufikia nafasi ya kutawala. Sijui kama yale makubaliano yaliyosainiwa Jangwani yalihusu kutawala baada ya kushinda uchaguzi au yalihusu tu kushirikiana kuelekea Uchaguzi Mkuu katika kujaribu kuingoa (dislodge) CCM madarakani. Kama ni ushirikiano wa kujaribu kuing'oa CCM madarakani nini kitafuatia endapo upinzani utashinda? Hili linatuleta kwenye hoja nyingine.

Ukweli huu unatufanya tuhitimishe kuwa UKAWA si Muungano wa vyama vya upinzani kama wengi wanavyofikiria; bali ni ushirikiano tu. Tofauti kubwa ya Muungano na Ushirikiano ni kuwa Muungano unakuwa na nguvu kubwa sana kwa wale wanaoungana kwani wanapoteza nguvu zao fulani fulani na kuziweka kwenye Muungano; Ushirikiano unaacha nguvu kubwa kwa vyama vyenyewe na nguvu kidogo iko kwenye ule umoja wenyewe. Hili ni tatizo la msingi. UKAWA haina nguvu bali nguvu iko kwenye vyama kama tulivyoona katika maelezo ya CUF jana ya kwanin hawakuweza kuhudhuria kile kikao cha mchakamchaka kilichojaribu kutangaza jina la mgombea wa UKAWA. Kwamba, wao walikuwa na vikao vyao vya ndani kwa mujibu wa Katiba yao.

UKAWA Siyo Chama cha Siasa Na Hili ni Sehemu Kubwa ya Tatizo

Ni vizuri kukumbushana tu ukweli huu ili tusije kujikuta tunatatizika na visivyotatizika. UKAWA kama nilivyoonesha hapo juu ni ushirikiano mwepesi (loose cooperation) kwa maana ya kwamba hauna masharti au utaratibu wa kuvifunga vyama vinavyounda umoja huo. Kukosekana kwa yale makubaliano ya Ushirikiano (ambayo yangekuwa na nguvu fulani ya kikatiba) kunafanya UKAWA kuwa dhaifu kwa sababu yenyewe siyo chombo chochote rasmi chenye madaraka juu ya vyama vinavyounda umoja huo.

Kutokana na ukweli huu utaona kuwa hata hivi juzi tulipoambiwa kuwa jina la mgombea kupitia "UKAWA" kitu ambacho kiukweli hakiwezekani – wote tulijikuta tunasubiri na kuulizia habari za vyama vinavyounda umoja huo. Hatukuweza kumuuliza mkuu fulani wa UKAWA au Kamati fulani ya UKAWA ambayo ilipewa jukumu hilo. Hiini kwa sababu watu wote wanaoshughulika suala la kutafuta mgombea huyo wanafanya hivyo kwa niaba ya vyama vyao na hivyo vyama vinajikuta inabidi virudi mara kwa mara kwa viongozi wa juu ili kupata maoni yao.

Kwa vile UKAWA siyo chama cha siasa basi hata mgombea atakayetajwa au wagombea watakaopatikana kwenye majimbo mbalimbali hawatokuwa wa UKAWA per se bali wa chama kitakachowasimamisha. Kisheria kabisa UKAWA haiwezi au haina uwezo (lack of standing) wa kusimamisha mgombea yeyote yule.

Hapa pia kuna jambo jingine; UKAWA haina chombo au utaratibu wa kuwapima na kuwapitisha wagombea ambao watasimamishwa na vyama vingine kwa jina la UKAWA. Haiwezi kwa mfano kusema "huyu asipitishwe" kam amepitishwa na chama chake. Hii ina maana wagombea watakaosimamishwa watakuwa wa UKAWA kwa sababu tu wamesimamishwa na vyama vyao. Hili linatuleta kwenye tatizo jingine la msingi la UKAWA.

UKAWA haina Fedha Zake

Hili nitakuwa tayari kusahihishwa. Sijui kama UKAWA kama chombo ina akaunti zake mahali na inaweza kupewa michango ya kuisaidia ishinde. Kwa jinsi ambavyo nimeona na kuelewa (niko tayari tena kusahihishwa hapa) vyama vinavyounda UKAWA ndivyo vinatoa fedha kwa matumizi mbalimbali – ama kwa zamu au kwa kiasi. Ni nani anayeamua kiasi fulani kiende kwenye jambo fulani kutoka chama fulani? NI nani anasimamia mgawanyo wa fedha hizi (kama zipo)?

Kubwa zaidi ni kuwa wale wagombea watakaopitishwa na kubebwa na jina la UKAWA watafadhiliwa na fedha gani? Je fedha kutoka CUF zitaweza kwenda kutumika (wakiombwa) ili kumsaidia mgombea wa CHADEMA ambaye anapata shida ngumu kwenye jimbo analogombania au kinyume chake? Au huu UKAWA utakuwa ni jina tu lakini bila kuweka fedha zozote kwamba kila chama kigharimie kampeni zake ila UKAWA ni yao wote?

Je vyama vidogo (hapa nafikiria NLD) inaweza vipi kufanya kampeni kama ikiachiwa jimbo dhidi ya nguvu za CCM bila msaada kutoka kwa washirika wake wa UKAWA? Nani anaamua waende kumsaidia na kwa kiasi gani?

Kuachiana Majimbo Ni Mojawapo ya Mambo Hayakufikiriwa Vizuri

Kwa vile UKAWA siyo umoja wenye nguvu za kisheria bali ni ushirikiano tu basi wazo la kuamua baadhi ya vyama visimamishe au visisimamishe wagombea mahali fulani naamini ni wazo baya na lina hatari kwa demokrasia yetu ilivyo. Wazo hili likitekelezwa kama inavyotarajiwa litawanyima wapiga kura nafasi ya kuchagua ama chama wanachokitaka au mtu wanayemtaka. Katika kuamua jimbo fulani waachiwe chama fulani bila ya shaka kutakuwa na vigezo mbalimbali ambavyo vimeangaliwa; ama kwa mfano matokeo ya uchaguzi uliopita, kukubalika kwa mtu au chama eneo hilo n.k. Haya yote ni mazuri lakini kutaka kiutaratibu kuwa mtu fulani au chama fulani kiachwe kwa sababu ya matokeo ya nyuma ni kutotafsiri vyema mabadiliko ya kisiasa yaliyotokea tangu 2010.

Katika hili naamini chama ambacho kitapoteza zaidi itakuwa ni CHADEMA hasa kama hakitaweza kusimamisha wagombea kwenye kila jimbo la Tanzania Bara. Tayari tunajua CDM kimeweza kufanya vizuri sehemu hata ambazo hazikutarajiwa kwa sababu udongo wa mabadiliko ulikuwa tayari kuchipua miche mipya ya mabadiliko. Tuliliona hili kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010 na hata kwenye ule Serikali za Mitaa mwaka jana. Kuanzia kushinda sehemu kama Ukerewe hadi Mbeya Mjini, Iringa Mjini hadi Mbulu, Ubungo hadi Nyamagana! CDM iliweza kupenya sehemu nyingi na safari hii wanaweza kwenda sehemu nyingine mpya ambazo watu hata hawajafikiria na ninaamini kuna vigogo wengi wa CCM watakaoanguka na watu watapigwa na butwaa. Lakini kusema kuwa ati isisimamishe wagombea kama suala la kanuni siyo sawa.

Hii haina maana vyama haviwezi kuachiana majimbo au kumuunga mkono mgombea wa chama fulani kwenye jimbo fulani. Hili lingeweza kufanyika baada ya kumpata mgombea huyo au kwa kuweka utaratibu wa kumpata mgombea huyo kwenye hilo jimbo. Hili nitalieleza kidogo kwenye mapendekezo yangu chini.

Jambo la kujiuliza hapa ni kuwa itakuwa vipi pale ambapo UKAWA wamekiachia chama fulani jimbo na chama hicho kikamsimamisha mtu ambaye hakubaliki au chama ambacho hakikubaliki je vyama vingine vitaruhusiwa kusimamisha mgombea mwingine? Je watu wampigie kura yule wa UKAWA au yule ambaye wao wanaona anakubalika na labda naye pia anaunga mkono UKAWA lakini hakupitishwa rasmi? Au Chama kikataliwe kufanya hivyo kwa sababu kitadhoofisha UKAWA? Vipi kama mwanachama wa chama kingine cha UKAWA akataka kugombea chama chake kimkatalie hata kama anakubalika na anaweza kushinda kuliko yule mwingine wa chama kingine cha UKAWA ile ile?

UKAWA Haina Alama za Ushirikiano Huu

Siasa ni maono, ni alama na ni viashiria. Hadi hivi sasa mtu akisema UKAWA hakuna kitu chochote kinachokuja kwenye mawazo ya mtu kumfanya aihusishe alama hiyo na UKAWA. Hakuna rangi au vitu vyenye kuwakilisha UKAWA. CHADEMA kwa mfano wana alama ya vidole viwili na CUF wana alama yao ya kushikana mikono. Lakini pia kuna suala la rangi; UKAWA haina rangi zake kwani hadi hivi sasa hata wanapokutana kwenye vikao vyama vinavaa au vinatumia rangi zao. Hili ni jambo linalotokana labda na sababu mojawapo hapo juu – UKAWA siyo chombo hasa chenye kusimama chenyewe. Kwenye Uchaguzi Mkuu mgombea wa UKAWA atatumia alama gani ili tujui ni wa UKAWA au kuwa kwake kwenye upinzani tu inatosha; atafanya vipi kampeni kuonekana ni wa umoja?

CUF Haijaomba Radhi Bado Kwa Kufifisha Harakati Mwaka 2010 Kupitia Prof. Lipumba

Mojawapo ya mambo ambayo sikuyaelewa yalitatuliwaje – labda kuna mtu atatujuza humu – ni jinsi gani CHADEMA na CUF wameweza kukaa pamoja kufuatia hujuma iliyofanywa na Mwenyekiti wa CUF dhidi ya harakati za kuindoa CCM mwaka 2010. Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa mgombea wa CUF kwa kiti cha Urais mwaka ule na hakuwa tayari kumuunga mkono Dr. Slaa kuwa Rais na hivyo akafanya hila za kumpigia kampeni Rais Kikwete kinamna kwa kuangalia dini; alitumia dini kumkataa Dr. Slaa na kumkubali Kikwete.

Hili si tetesi au uzushi; ni kwa maneno yake mwenyewe alikiri kufanya hivyo na hadi leo hajafuta kauli yake ile au hata kuonesha kuwa alifanya makosa. Lipumba alialikwa kutoa nasaha zake kwenye Msikiti wa Idrissa Jijini Dar muda umepita sasa. Alipopewa nafasi ya kuzungumza pale bila kujificha wala kuuma maneno alikiri kuwa aliongozwa na udini kumuunga mkono Kikwete kuliko kuacha Dr. Slaa ashinde – bila ya shaka kwa sababu Dr. Slaa ni Mkristu.

Lipumba alikiri kuwa ilibidi mbinu za ziada zitumike kuokoa jahazi (Urais wa Kikwete) n ahata kumfanya aende kwa haraka kwenye kuapishwa Kikwete kuonesha kuwa Kikwete ameshinda hata kama yeye mwenyewe alikuwa anaona uchaguzi haukuwa wa haki. Alinukuliwa kusema kuwa "Ninyi masheikh mnajua vizuri zaidi hali ya kisiasa ilivyokuwa, kwamba ilibidi zifanyike juhudi za makusudi ili kuokoa jahazi. Lakini pamoja na kuliokoa jahazi, hali halisi inaonyesha mpaka sasa hakuna matunda yoyote yaliyopatikana, na tupo katika mtihani mgumu zaidi" na pia kusema "Mwaka 2010 wakati mshindi wa uchaguzi wa rais alipotangazwa, mimi nilikwenda kwenye hafla ya kutangazwa matokeo, na nilikwenda makusudi tu, siyo kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki, ila nilikwenda makusudi kwa kujua hali ya kisiasa ilivyokuwa wakati huo"

Sasa hapa lazima mtu ujiulize; huyu huyu Lipumba leo amekuwa Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA kweli anauamini au kwa mara nyingine ataweka maslahi ya dini yake mbele? Kwamba, kama mgombea atakuwa ni Muislamu basi atamuunga mkono lakini akiwa Mkristu hatomuunga mkono? Inawezekana kabisa hata hii kwikwi tunayoisikia ya kumpata mgombea wa Urais ni kwa sababu inawezekana Dr. Slaa ataweza kupitishwa na ukizingatia 2010 Lipumba alifanya hujma basi safari hii hawezi kula matapishi yake mwenyewe? Ataweza vipi leo – kupitia UKAWA – kumuunga mkono mtu ambaye miaka mitano tu nyuma aliamini anawakilisha Ukristu?

Inawezekana hata hizi kelele za siku za karibuni za kuwa "Ukimkata Lipumba lazima umuonde na Slaa" nazo zinatokana na msingi huu huu? Kwamba Lipumba hayuko tayari kumnadi Slaa kwani ataonekana – na waumini wenzake – amewageuka? Nashangazwa hata na watu wanaoweza kumtaja Lipumba kama mtu anayefaa kuwa Rais; wa nani? Angalau angeomba radhi kwanza tujue alipitiwa au alighafirika ndio ubinadamu ulivyo. Hatokuwa mwanasiasa wa kwanza kusema kitu cha kufarakanisha duniani. Na hili linasameheka.

CHADEMA Haikupaswa Kujifunga Kwenye UKAWA

Mwanzoni sikujali sana CHADEMA kuwa sehemu ya UKAWA wakati wakiwa kwenye Bunge la Katiba walipojaribu kuizuia CCM isiburue mchakato ule. Katika mazingira yale sidhani kama wapinzani na wadau wengine walikuwa na njia nyingine isipokuwa kuungana. Kutoka kwenye Bunge la Katiba kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu kulihitajika mazungumzo mazito zaidi hasa kwa CHADEMA.

Kati ya vyama vyote vinavyounda UKAWA ni CHADEMA ndicho kimelipa gharama kubwa zaidi ya mabadiliko na kujiandaa kwa kina zaidi nchi nzima kuweza kushinda Bunge na Urais. Siyo hivyo tu katika vyama hivi vyote ni CHADEMA ambacho mwaka 2010 kilikuwa tishio dhahiri na kamili kwa utawala kiasi kwamba miaka hii mitano watawala wetu wamejitahidi sana kuidhoofisha na kuivuruga na kuipunguzia makali na hofu yangu ni kuwa kwa kupitia UKAWA hili linaweza kuwa kweli.

Naomba nieleze kidogo kwanini sijapenda hiki kifungo cha hiari ambacho CHADEMA wamejifungia. Tayari walifanya baadhi ya makosa ambayo hayakupaswa kufanya hasa pale walipokubali mchakato haramu wa Katiba ulioasisiwa na Kikwete. Hili lilikuwa kosa kubwa zaidi la kisiasa la CDM katika kipindi cha miaka hii mitano. Linasameheka hata hivyo. Ila kuendelea na makosa yale yale ya aina ya kisiasa kunatuacha baadhi yetu na maswali.

Kuanzia mauaji ya wale vijana wanne Arusha ile Januari 4, 2011 hadi mauaji ya Mwangosi; kuanzia mauaji ya kijana Ramadhani kule Igunga hadi mauaji yaliyotokea Songea; mauaji ya Morogoro na vipigo vya wabunge kule Mwanza na Arusha na uonevu mwingine kutoka vyombo vya dola. Damu ambayo imemwagika miaka hii mitano Tanzania Bara kwa sababu ya watu wakiamini na kuishabikia CHADEMA itakuwa siyo tu kosa bali dhambi kama CHADEMA hawataweza kuongoza harakati ambazo walisababisha watu waandamane, wafuatilie nchi nzima wakiamini wanafuata chama kinachoongoza mabadiliko ya kweli. Kwa CHADEMA kukubali kuwa nyuma ya harakati hizi na kutokuwa huru kuongoza harakati hizi jinsi ilivyo fanya mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 siyo usaliti wa damu ya ndugu zetu ambao leo wanalala mavumbini; ni kufuru ya damu hiyo. Watu wengi waliweka imani yao kwa CHADEMA na siyo tu imani wengine wamepoteza maisha yao, wamepoteza mali zao, wamebambikiwa kesi zinazobambikizika na wengine hata leo wameamua kula hasara ya maisha.

Haya yote ni baadhi ya mambo ambayo yamenifanya mimi nisiwe muumini au shabiki wa UKAWA. Safari hii nimeamua kuunga mkono CHADEMA ili iweze kuongoza harakati za kuiondoa CCM madarakani. Nimeamini kwa muda kuwa CHADEMA haikutakiwa kujifunga kwenye mfumo huu wa ushirikiano.

MAPENDEKEZO YANGU

Mtu akinisoma haraka haraka anaweza kuamini nimesema kuwa CHADEMA isishirikiane na vyama vingine vya upinzani na iende kivyake vyake. Mtu huyo hatokuwa amenisoma vizuri na kwa umakini. Ninachosema ni kuwa mfumo huu wa UKAWA umeifunga zaidi CHADEMA kuwa huru kuongoza kasi za mabadiliko kuelekea Uchaguzi Mkuu kuliko chama kingine chochote.

Ninaamini kuwa ushirikiano wa upinzani unatakiwa uongozwe na baadhi ya kanuni za msingi ambazo zitazingatia ukweli wa hali ya kisiasa nchini na matamanio ya Watanzania. Kwamba;

1. CHADEMA ndiyo chama kikuu cha upinzani na hivyo kitabeba nafasi kubwa ya kuongoza harakati hizo kwa Tanzania Bara;
2. CUF kama chama kikuu cha upinzani Zanzibar kitaongoza harakati hizo Zanzibar
3. Vyama vingine vyenye nguvu kiasi vitapewa nafasi ya kuunga mkono wagombea watakaosimamishwa na CDM (Bara) au (CUF) Zanzibar. Endapo vyama hivyo vitakuwa na wagombea wenye kukubalika kuliko wale wa CDM au CUF basi vyama hivyo vitapewa nafasi ya kusimamisha wagombea watakaoungwa mkono na vyama hivi vikubwa;
4. Vyama vingine ambavyo vimeonesha nguvu ya mahali fulani tu na vinaonekana kuendele kukubalika vitakubaliana na vyama hivi husika (kwenye mahali hapo) ili visimamishe wagombea na CDM au CUF vitaunga mkono wagombea hao;
5. Kama hakuna chama kinachoonekana kukubalika kwa wingi zaidi katika eneo fulani basi vyama vyote vinavyoweza kuweka wagombea vitaweza kuweka mgombea kushindana na yule wa CCM;
6. Endapo kura za upinzani zitaonekana kugawanyika (kwa mfano kampeni za wagombea zinaonekana kuwa na watu wengi sawa na mvuto sawa) basi vyama husika vitafanya mashauriano na wagombea ili mmoja amuunge mkono mwingine; hili litakuwa ni suala la hiari;
7. CHADEMA ikishinda nafasi ya Urais basi wagombea wale waliokubali kujiondoa au kuunga mkono nafasi ya yule mwingine watakuwa kwenye orodha ya kwanza kabisa ya watu ambao wataitwa kutumia taifa katika nyadhifa mbalimbali kama sehemu ya kuwatumia wazalendo hao badala ya kuwaacha pembeni. Watakaoamua kupambana wenyewe na kukataa mashauri ya vyama basi yule atakayepoteza atakuwa amepoteza au atafikiriwa kwenye orodha ya ngazi za chini;
8. Wagombea wote watakaosimama kwa jina la umoja pamoja na kuwa na ajenda zao za mahali wataweza pia kusimama na kunadi ajenda ile ya upinzani (ambayo kimsingi itakuwa ni agenda ya CHADEMA;
9. CHADEMA itakapounda serikali yake itaangalia mgawanyo wa nafasi mbalimbali kulingana na mchango wa ushirikiano kutoka vyama vingine vya upinzani (viwe ndani ya umoja) au nje; Baadhi ya nafasi zitaenda kwa mfano;
· Mwenyekiti wa CUF ataweza kupewa nafasi ya Uwaziri kamili kwa nafasi atakayochagua ukiondoa Uwaziri Mkuu, Mambo ya Nje na Ulinzi.
· Mwenyekiti wa NCCR ataweza kupewa nafasi ya Uwaziri kamili kwa nafasi atakayochagua ukiondoa wizara hizo tatu hapo juu;
· Mwenyekiti wa NLD vivyo hivyo
· Kwa wale ambao siyo wenyeviti lakini wametoa mchango basi nafasi za utumishi zitaenda na michango yao ya kichama au binafsi lakini pia itategemea idadi ya wabunge watakaopata na madiwani watakaopata.
10. Chama chochote cha upinzani ambacho kitapata angalau wabunge kumi kitakuwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (Government of National Unity) chini ya CHADEMA na watatumika kutekeleza ilani ya CHADEMA;
11. CHADEMA ndiyo inapaswa kutoa mgombea wa Urais kwa uhuru wote na ambaye ataungwa mkono na vyama vingine; vyama ambavyo havitotaka kufanya hivyo viwe huru kujitoa kwenye umoja huu na kufanya kivyake vyake lakini kanuni hiyo ya 10 itaweza kutumiwa kwao pia kama katika kampeni yao watakuwa dhidi ya CCM na kushinda viti vya vilivyokuwa vinashikiliwa na CCM.
12. Chama cha Mapinduzi kikiondolewa madarakani kitakuwa ni chama cha upinzani hata hivyo hakitapewa nafasi yoyote ya kutumikia serikalini hasa kama ushirikiano wa vyama vya upinzani utaweza kuunda serikali (Waziri Mkuu kutoka huko) bila kuhitaji kura za CCM; Endapo Waziri Mkuu atahitaji kupatikana kwa kuhitaji pia kura za CCM basi CHADEMA itasimamisha au kumpendekeza Mbunge yule ambaye anaonekana kuunga mkono na pande zote kama ambavyo imetokea miaka hii ya nyuma.

ALAMA ZA UMOJA WA UPINZANI ZIWE NINI?

Binafsi ningependekeza rangi za Njano, Nyeupe na Nyekundu kuwa alama za umoja huu kuelekea kipindi cha kampeni na Uchaguzi Mkuu. Njano kama alama ya utajiri wetu (dhahabu), Nyeupe kama alama uongozi wenye uadilifu (usafi) na nyekundu kama alama ya kuheshimu wale wote ambao wamekuwa sehemu ya kudai mabadiliko Tanzania na sasa wametangulia mbele ya haki wasiyaone mabadiliko hayo lakini zaidi ni wale ambao wamemwaga au watamwaga damu yao kutaka mabadiliko hayo.

Na kama alama ya mnyama basi ningependekeza kichwa cha tembo; hii ni alama ya nini ambacho kimetokea chini ya utawala wa CCM ambao umepoteza urithi wetu (tembo ni mfano tu) kutokana na usifadi. Mnyama mwenye nguvu na mkubwa anapoangamizwa kama siafu Taifa lazima lishtuke na ninaamini ni alama sahihi kwa wakati huu. Hii ni rahisi hata kwa mtu mwenye kutaka kuonesha ushabiki bila kuvaa rangi za chama anaweza kuvaa nguo zenye tembo!

MGOMBEA WA URAIS AWE NANI CHINI YA CHADEMA AKIBEBA UPINZANI?

Makala yangu hii ndefu haitonoga au kumalizika vizuri kama sitotoa pendekezo langu la nani nafikiri anapaswa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika makala yangu ile ndefu ya Lowassa hafai wengi wameniuliza "nani anafaa"; naomba kulijibu swali hili. Ninaamini wakati huu na saa hii mgombea sahihi kusimama na peperusha bendera ya upinzani anapaswa kuwa Dr. Wilbroad Peter Slaa. Sioni mtu mwingine yeyote katika upinzani ambaye tayari ana jina linalojulikana, umakini na historia ya kuongoza harakati hizi za mabadiliko kama ilivyo kwa Dr. Slaa. Ninaamini ni tishio kubwa sana kwa CCM na watawala wa sasa kiasi kwamba kwa muda sasa kumekuwa na jitihada za kutaka asiwe mgombea. Hili lina sababu:

1. Dr. Slaa alitingiza malango na ngome za watawala mwaka 2010 kuliko walivyotarajia. Japo aliingia kama mgombea wa bahati mbaya (baada ya mipango ya kumpokea mtu kutoka CCM kushindwa) aliweza kuamsha na kuwasha mioyo ya Watanzania kwa kupendekeza mapendekezo ya masuluhisho ya matatizo yao kiasi cha kueleweka na Watanzania wa mijini na vijijini;

2. Kwa muda mfupi ule wa kampeni – kama wangekuwa wanaruhusu kujiandikisha wakati wa kampeni ingekuwa vingine – Slaa aliweza kupata zaidi ya kura milioni 2 dhidi ya kura milioni tano tu na kiduchu ambazo ilidaiwa Kikwete amezipata pamoja na "jitihada" za ziada zilizofanyika. Aliweza kupunguza kura za Kikwete toka 9,123,952 za mwaka 2005 hadi kura 5,276,827 za 2010. Hili ni punguza la asilimia 42.

3. Kama Kikwete akienda na umaarufu wake na kutumia nguvu zake za vyombo mbalimbali bado alipoteza asilimia 42 ya kura alizozipata 2005 ni wazi kuwa Magufuli ana kibarua kigumu zaidi dhidi ya Dr. Slaa kuliko ilivyokuwa kwa Kikwete. Ikumbukwe Kikwete alikuja na mafanikio yote ya serikali yake lakini bado wananchi wengi walimkataa; Magufuli tunaambiwa anakuja na mafanikio yake ya kufuatilia barabara (ambayo ilikuwa ni sehemu ya mafanikio ya Kikwete)! Tunaambiwa Magufuli sasa ni jembe; kuliko Kikwete?

4. Dr. Slaa kwa muda ambao amekuwa nje ya Serikali miaka hii mitano ameweza kuona na kuelea mambo mengi zaidi kuliko Magufuli; ikumbukwe Magufuli hajui mambo nje ya madaraka aliyonayo. Kama Kikwete Magufuli miaka hii ishirini amekuwa akishika nyadhifa moja au nyingine; nje ya nyadhifa hizo hana pa kusimamia.
Watanzania wengi hawamjui Magufuli nje ya kofia ya Uwaziri au Ubunge. Utaweza vipi kumlinganisha na mtu ambaye mke wake amepigwa mabomu, yeye mwenyewe kushitakiwa na wanachama wake kuuawa mikononi mwa serikali ambayo Magufuli anaitumikia? Unaweza vipi hata kumfikiria Magufuli kuwa anayaelewa matatizo ya wananchi kuliko Dr. Slaa?

5. Dr. Slaa ana maono ya kupokezana kizazi; amefanya kazi na vijana wengi na wazee wengi ameelewa changamoto za ujana na matatizo ambayo wanasiasa vijana wanayapata lakini pia ameona jinsi gani wazee wameliangusha taifa na kwa namna gani kunahitajika uongozi wenye kuelewa uwezo wa pande hizi mbili. Ndio maana utaweza kuona kuwa labda kati ya vyama vyote CDM safari hii itapendekeza kundi la wagombea wenye uwezo zaidi na ambao wamejaribiwa shambani; watu ambao wengi wamepitia kwenye mikono ya Dr. Slaa;

6. Dr. Slaa ameonesha uwezo wa kuweza kupitia mambo ya kukigawa chama sana na kusimamia misingi ya kile anachoamini ni sahihi. Hii ni tofauti na uongozi wa Kikwete ambaye miaka hi ameufanya Urais uonekane ni kazi tu ya kupita kiasi kwamba inaonekana hata ana ujutia. Sijamsikia bado Slaa kulalamikia kuwa yeye ni kiongozi na wakati mwingine anafanya maamuzi magumu, sahihi na ya lazima yenye kuumiza hisia za watu. Hatutaki Rais mwenye kujali sana hisia za watu kiasi cha kuwa yabisi (impotent);

7. Tayari ajenda kadhaa ambazo Dr. Slaa alizisimamia wakati wa kampeni ya Uchaguzi Mkuu 2010 zimekumbatiwa na CCM na hata kuzifanya ziwe zao. Mfano mzuri ni ajenda ya Katiba Mpya. Slaa alisema wangeanzisha mchakato wa kulipatia taifa Katiba Mpya ndani ya siku mia moja. Hazikupita hata siku sitini Kikwete mwenyewe alijikuta anatangaza nia yake ya kuanzisha mchakato huo mchakato ambao haukuwepo katika ilani ya CCM (Ulitajwa kwenye Ilani ya CDM);

Kama CCM waliweza kukumbatia wazo hili na mengine kwanini usiende moja kwa moja kwenye kisima cha fikra mpya kuliko kusubiri CCM waje wachote halafu wakuuzie wewe?

8. Tayari Dr. Slaa ana hazina hiyo hapo juu; watu zaidi ya milioni mbili na bila shaka wengine wengi ambao wamejiunga na CDM au wanaunga mkono harakati za mabadiliko sasa.

Ningeweza kutoa sababu nyingine nyingi lakini kwa ufupi CDM ifikirie sana inavyotaka kwenda kwenye huu UKAWA na kama ipo haja ya kuutengeneza zaidi ili kiwe chombo ambacho kitaweza kutuletea serikali. Hili ni muhimu ili tusije kujikuta tunaingia kwenye mgogoro mwingine wa uongozi baada ya upinzani kushinda kama tulivyoona kwenye baadhi ya nchi – tumeona Zambia na Kenya hili. Kama nilivyodokeza haitoshi kujipanga kuiondoa CCM madarakani lakini kutokujipanga kuiongoza Tanzania. Na katika yoyote ambayo vyama vitaamua jambo rahisi zaidi kuliamua na kulikubali ni kumpitisha Dr. Slaa kama mgombea wa Urais huku mambo mengine yanazunguka hapo.
Dr. Magufuli hapo na chama chake watapata mchecheto wa karne. CCM kwa kumpitisha kimizengwe Magufuli wameuliza swali tu ambalo jibu lake wanalihofia; wanalitetemekea na wanaliombee lisiwe; Dr. Willbroad Slaa.

Niandikie:Mwanakijiji@jamiiforums.com
 

Attachments

  • NISIKILIZENI CHADEMA.docx
    28.1 KB · Views: 488
Mkuu rekebisha pale juu,aliyekuwa Naibu spika bunge la katiba Bi.Samia suluhu hassan akuwa waziri wa fedha...bali waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais muungano...

Well,artical yako ilikuwa ndani ya mawazo yangu..japo hata mimi sikupenda huu muungano wa UKAWA.asante kwa narration nzuri
 
Mkuu rekebisha pale juu,aliyekuwa Naibu spika bunge la katiba Bi.Samia suluhu hassan akuwa waziri wa fedha...bali waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais muungano...

Well,artical yako ilikuwa ndani ya mawazo yangu..japo hata mimi sikupenda huu muungano wa UKAWA.asante kwa narration nzuri


Naam; asante.
 
CHADEMA walikuwa wanamsikiliza Mwanakijiji kabla ya 2010
walipokuwa wachanga
sasa wako hotheaded na big headed pia na mafanikio kidoogo after 2010
hawamsikilizi Mwanakijiji au tuseme Mwanakijiji amekuwa 'irrelevant' mbele ya CHADEMA

Naamini baada ya uchaguzi wa mwaka huu
watu wengi ndani ya CHADEMA watakua 'irrelevant'

the sands shifted beneath....so fast.....
 
kwel naanza kupingana na fikra kuwa tanzania aliyesoma na asiyesoma tofaut yao ni vyeti na majina tu mfano Dr,prof,etc lakini ufaham wao ni sawa kat ya aliyesoma na asiyesoma kwel jamii forum its home of great thinker mkuu mzee mwanakijiji ume push ur brain to the limit bt cuf wanataka kuleta uswahili katika mambo serious
 
Mbatia anasema Chadema wata tandikwa kweli kweli! we @mwanakijiji washauri tu u.puuzi hawa jamaa zako!
 
Makala ndefu lakini ipo poa sana. Ushauri mzuri sana huu. Pia naamini mapendekezo hayo yapo vizuri. Ulipogusia kuwa kuna wengi wamepoteza maisha na wengine kuumia umenigusa sana. Tupo tuliojitolea mhanga kwenda vijijini kuhamasisha mabadiliko. Serikali za mitaa tulipata response yake. Tunaamini hata kwenye uchaguzi huu tutapata response kubwa sana. Kuna hoja ya udini umeandika. HIYO NDIYOINAYOWASUMBUA CUF. HAKUNA HOJA KUBWA ZAID YA HIYO. CUF WAMETAZAMA KULE CCM KUNA MKRISTU. HUKU TENA MKRISTU? WAMEJIONA WATAPOTEZA. LAKINI HAWANA CHAGUO. LABDA CHAMA KINGINE KISIMAMISHE. CUF WAKITOKA KWENYE USHIRIKIANO HUU, WATAPOTEA KABISA. CHADEMA IMEJIJENGA SANA BARA. INAFAHAMIKA SANA. HATA BAADHI YA MAENEO AMBAYO CUF WATAACHIWA YANAUMIZA SANA CDM KWANI KUNA WATU WALIJIJENGA SANA KUTEGEMEA KUGOMBEA HUKO. SASA HUU MCHEZO WA KUACHIANA UNALETA KINYONGO KWETU. DR SLAA IS THE BEST FOR THIS POST THIS YEAR.LIPUMBA HAYUPO SERIOUS NA URAIS. ANANOGESHA TU BARAZA.
 
HADI.SASA NAJIULIZA.?
yawezekana hivi viziara vya juzi ndivyo vilimpa jeuri huyu mchumi wetu au kuna mkono wa RUPIA toka kwa mahasimu?

-hakika CUF hawaeleweki
 
Back
Top Bottom