Nionavyo mimi mr ii anastahili heshima na malipo ya tamasha la zinduka | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nionavyo mimi mr ii anastahili heshima na malipo ya tamasha la zinduka

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Iteitei Lya Kitee, Mar 9, 2010.

 1. Iteitei Lya Kitee

  Iteitei Lya Kitee JF-Expert Member

  #1
  Mar 9, 2010
  Joined: Jan 2, 2008
  Messages: 589
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Umetunga kitabu chako kwa miaka miwili, ulipomaliza ukaniletea mimi ili nikusaidie kukisoma kabla hujakichapisha. Nikakipokea na wewe ukaondoka zako kwenda nyumbani kusubiri siku nitakapomaliza kukisoma uje ukichukue kwenda kiwandani kwa ajili ya uchapishaji.

  Mwezi mmoja baadaye rafiki yako akakupigia simu na kukuambia “John, kitabu umekitoa kwa jina jingine?” Unakataa, ukiwa huamini unakwenda mtaani na kukuta kitabu ambacho maandishi yote ndani ni yale uliyoandika wewe lakini juu ya kitabu hicho pameandikwa mtunzi ni Eric Shigongo! Utajisikiaje?

  Mfano wa pili ni msanii mchanga ametunga wimbo wake, kisha akampelekea msanii mkubwa ili ayatazame mashairi yake kabla hajaenda studio kurekodi. Msanii mkubwa badala ya kumsaidia msanii mdogo, akayachukua mashairi yake na yeye akakimbia studio kwenda kurekodi, wiki mbili baadaye msanii mchanga akausikia wimbo redioni na siku ya uzinduzi hatakiwi kuonekana eneo la tukio! Atajisikiaje?

  Takriban wiki mbili zilizopita nilipata simu kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye kwa kweli namheshimu kwa jinsi alivyo mpiganaji, huyu si mwingine bali ni Joseph Mbilinyi ‘Mr II’ akiomba tuonane ofisini kwangu kwa maongezi kidogo juu ya jambo lililokuwa linamtatiza. Pamoja na kazi nyingi nilizokuwa nazo ilibidi nimwingize kijana huyo kwenye ratiba yangu ya siku hiyo sababu alidai suala lake lilikuwa na haraka.

  Siwezi kuficha wala kuongeza chumvi katika hili, Sugu alipokuja na kuingia ofisini kwangu alikuwa akilia machozi ya mwanaume akiwa amevaa miwani yake ya jua. Kwa haraka sana nilidhani ana msiba, nilipojaribu kumdadisi kilichomtokea hakunificha, ilibidi aweke kila kitu kilichofanya anitafute wazi, alianza kwa kusema “Kaka, nimedhulumiwa haki yangu”

  Katika maelezo yake Sugu alinieleza jinsi alivyokutana na wawakilishi wa shirika la Malaria No More linalopambana na Malaria duniani katika jiji la New York, Marekani ambao walimweleza juu ya kazi yao ya kutokomeza ugonjwa huu hatari duniani unaoteketeza maisha ya watu kila siku, akaongea nao kuhusu Tanzania na kwa kuwa Malaria No More hutumia wasanii katika kampeni zao, waliona ni vyema kufanya naye kazi na wakamwuliza namna ambavyo angeweza kushirikiana nao, wakiwa hawajui lolote kuhusu Tanzania.

  Mr. II alitayarisha andiko la jinsi mradi huo ungefanyika, hiyo ilikuwa mwaka 2008 na kuwapelekea, akionyesha ambavyo wangetumia wasanii maarufu na kumkaribisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenye tamasha kubwa ambao lingefanyika kwenye viwanja vya Leaders, jijini Dar es Salaam na baadaye kuendelea nchi nzima. Narudia tena kusema hiyo ilikuwa mwaka 2008 na hicho ndicho kimefanyika majuzi kwenye viwanja vya Leaders kwenye Tamasha la Zinduka. Aliongea yote haya akijifuta machozi na kunionesha vielelezo vyote kuthibitisha alichokuwa akisema. Nitakuwa mnafiki nikisema sikuumia!

  Nilishasikia habari ya tamasha hilo na sikujua kabisa kama lilikuwa likimhusu Mr. II, kwani niliyekuwa nikimwona kwenye vyombo vya habari ni mtu aitwaye Ruge Mutahaba, huyu ndiye aliyekuwa akitajwa kama mratibu akishirikiana na kampuni yake ya THT au Tanzania House of Talents. Nilipatwa na mshituko kidogo na kumweleza Mr II, ilikuwaje shughuli hiyo ikatua mikononi mwa Ruge?

  Jibu lake lilikuwa kwamba: Watu wa Malaria No More walikuja nchini kufuatilia na wakapata nafasi ya kutembelea Ikulu ya Dar es Salaam ambako walikutana na mtu aitwaye January Makamba, akadai huyo ndiye aliyehamisha kazi hiyo kutoka kwake kwenda kwa Ruge Mtahaba.

  Haya yalikuwa ni madai makubwa mno, sikutaka maumivu na hisia zangu zinisukume kutenda jambo lisilostahili, ilibidi nijizuie na kumuuliza Mr II ni kitu gani alichokuwa akitaka kupata, akanijibu “ Haki yangu” ambayo ilikuwa ni fedha kwa muda alioupoteza na kutambuliwa kwamba yeye ndiye hasa mwanzilishi wa wazo hilo. Kwa maelezo hayo nilimwambia kama anachotafuta ni haki si vyema kuanza kuandika habari hizo kwenye vyombo vya habari, kilichopo ni kuketi mezani pamoja na watu wote aliokuwa akiwatuhumu ili kutafuta suluhu.

  Akaniambia hilo lilishafanyika lakini hawakuelewana na alichokuwa amepanga ni kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuzuia tamasha hilo mahakamani, nilimzuia asifanye hivyo na nikamuomba anipe muda nimtafute mtu aliyekuwa akimtuhumu (January Makamba) kwa kumnyang’a anya wazo lake na kumpa mtu mwingine ili niongee naye mimi mwenyewe nikijaribu kutafuta jibu, pia nikamwambia asizuie tamasha kwa sababu lilikuwa linamhusisha Rais wa nchi yetu ambaye alishapiga picha nyingi na wasanii na kutolewa gazetini, kuzuia tamasha ingekuwa kama kumdhalilisha Rais wetu.

  Mr II aliyakubali yote hayo, nami siku hiyohiyo nikampigia simu January Makamba akiwa Dodoma kwenye mkutano wa NEC, akaniambia akirejea Dar es Salaam siku ya tamasha tungepata nafasi ya kuzungumza ingawa hakufahamu tungezungumza juu ya jambo gani. Baadaye usiku Mr II alinipigia simu na kuniambia ameshitakiwa katika Mahakama ya Kinondoni kwa kosa la kutishia kuvuruga tamasha la Malaria na hakutakiwa kuonekana viwanja vya Leaders siku ya onesho hilo! Sikuiona nakala ya wito mahakamani lakini hivyo ndivyo alivyonieleza.

  January Makamba aliporejea Dar es Salaam kabla ya tamasha hatukupata nafasi ya kukaa chini, nafasi ilikuwa finyu kwani alirejea Dodoma siku iliyofuata na baada ya hapo alisafiri kwenda nje ya nchi lakini aliporejea nchini, alinitafuta ofisini tukakaa na kuzungumza.

  Tulizungumza mambo mengi sana kuhusu nchi yetu, ilikuwa ni mara ya kwanza kwangu kuketi na kijana huyu, mwenye umri mdogo lakini anayetekeleza majukumu makubwa kwa nchi yetu. Nilichojifunza kwake ni kijana makini, mwenye uchungu na nchi yake na anayeweza kuwa tegemeo kwa nchi yetu siku za usoni. Haikuwa rahisi kwangu baada ya kukutana na kuongea na January, kuamini alikuwa na uwezo wa kuhamisha wazo la mtu kwenda kwa mtu mwingine ambaye hakustahili.

  Nilipomwuliza juu ya suala hilo alinijibu kwamba, yeye alipigiwa simu na Balozi wa Marekani wa wakati ule hapa nchini, Mark Green ambaye hivi sasa yupo New York kwenye makao makuu ya shirika la Malaria No More na kuambiwa juu ya watu wa Malaria No More kwamba walikuwa na mpango mzuri sana kwa nchi yetu na kumwomba akutane nao, hakuwa na kipingamizi kama suala lenyewe lilikuwa linahusu nchi na Watanzania. Akakutana nao na wakamweleza juu ya mpango waliokuwa nao wa kufanya kampeni dhidi ya ugonjwa wa Malaria na wakamweleza juu ya mtu aitwaye Sugu, ambaye walikutana naye kwenye ndege na wakazungumza juu ya suala hilo.

  Watu hao wa Malaria No More walimuuliza January, kama wangetaka kufanya kampeni hizo ziwe na mafanikio ni nani ambaye angeweza kufanya kazi nzuri ya kuandaa tamasha hilo, kwa uzoefu wake aliwatajia kampuni kama tano hivi wakiwemo Benchmark Production, Entertainment Masters, THT na Primetime Promotion na kuwaachia wao uhuru wa kuchagua. Kamwe hakuwachagulia kampuni, kazi yake ilikuwa ni mambo ya Ikulu, kuhakikisha kuwa Rais anahudhuria tamasha hilo. Hivyo madai kwamba yeye ndiye aliyehamisha kazi hiyo kwenda kwa Ruge hayakuwa na ukweli wowote.

  Baada ya hapo hakujua kilichoendelea, alikuja kuona kwenye vyombo vya habari Ruge na THT ndiyo wakiratibu tamasha hilo, hakuelewa makubaliano yao yalikuwa ya aina gani, hiyo haikuwa kazi yake. Haya ndiyo yalikuwa maelezo ya January Makamba ofisini kwangu akiwa safarini kuelekea Tanga. Hata hivyo, aliahidi kama kuna mtafaruku wa aina yoyote ile, angeweza kuushughulikia akirejea kutoka Tanga hata kwa kumpigia simu Balozi Mark Green ambaye hivi sasa ni miongoni mwa mabosi wa Malaria No More huko New York na kumuomba aingilie kati suala hili ili Mr II aweze kupata haki yake kama ilikuwepo.

  Kwa bahati mbaye sana wakati tunafanya mazungumzo hayo ofisini, kumbe tayari Mr II baada ya kusubiri sana, hatimaye alikuwa ameamua kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuueleza umma kilichotokea kwenye tamasha la Zinduka, lengo likiwa ni kutaka kuuonyesha umma namna alivyodhulumiwa haki yake, ikiwezekana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye tamasha hilo amsaidie kupata haki yake.

  Ndugu zangu, haya ndiyo yaliyotokea ambayo yamenifanya mimi nichukue kalamu na karatasi yangu kuwaandikia na nikaanza na mfano nilioutoa hapo juu. Tamasha la Zinduka hapa Dar es Salaam limemalizika, kama yatafuata mengine mikoani mimi sijui! Majeraha yamebaki, wakati Lady JayDee, Mwasiti, Profesa J, kampuni ya Round Trip iliyokodisha jukwaa wanafurahia malipo yaliyolipwa kwa ajili ya kazi hiyo, muasisi halali, mtu aliyekutana na Malaria No More kabla sisi sote hatujaifahamu na kuwashawishi waje nyumbani, ambaye ni Mr II, ana maumivu makali moyoni mwake na kilichotokea hatakisahau. Je, sote tukae kimya na kuacha hali hii iendelee, hapana ni lazima tujitokeza wachache na kuomba haki na suluhu ipatikane.

  Sidhani kama kuna mtu anaweza kukanusha kwamba Mr II hakukutana na watu wa Malaria No More kabla hawajakutana na Ruge, sidhani kama kuna mtu anaweza kukanusha kwamba Mr II alitumia muda wake tangu mwaka 2008 mpaka 2010 akifuatilia suala hili na mwisho wa siku walionufaika ni wengine? Sidhani kama kuna mtu anaweza kukanusha kwamba Mr II ameumia na hatujui anachofikiria kwa sasa?

  Mambo haya ndiyo yanayonisukuma mimi kuomba wote wanaohusika waweke hasira na chuki zao pembeni na kuangalia ukweli uko wapi kisha kutafuta majibu. Haitusaidii chochote kuendelea kuangalia makosa yaliyotokea. Ni kweli kuna makosa yametendeka, tusiangalie hayo, kamwe tusiyaache mambo yalipo bali tuyaweke mambo yanapotakiwa kuwa. Hasira zote na chuki tulizo nazo zitayeyuka na undugu wetu kama Watanzania utaendelea kudumu, hili ndilo jambo tunalotakiwa kufanya.

  Nionavyo mimi, hata kama Mr II kwa hasira zake, uchungu wake, kutokuvumilia kwake aliamua kuweka mambo haya bayana kwenye vyombo vya habari, ni vyema tukaangalia ukweli ulipo, tukaachana na hasira za kwanini aliweka mambo haya kwenye vyombo vya habari na kukubali kwamba MR II ANASTAHILI

  KULIPWA NA KUPEWA HESHIMA KWA KAZI ALIYOIFANYA KWA AJILI YA NCHI YETU. Huu ni ukweli.
  Sijaandika maandishi haya kukosana na mtu, lengo langu ni kuhakikisha vijana hawa wanaelewana na tatizo linamalizika. Siku zote hatumalizi matatizo kwa ugomvi bali tunamaliza kwa kukaa chini, kama tunauelewa uchungu anaoupata mtu anayeandika kitabu chake mwisho wa siku anaibiwa na kuchapishwa na mtu mwingine, basi ni vizuri tufahamu kwamba Mr II ameumia sana na kama hivyo ndivyo basi namwomba ndugu yangu January Makamba asikate tamaa, aendelee tu na mpango wake wa kuongea na Balozi Green huko New York ili kijana huyu apate haki yake.

  Najua tatizo si kati ya January na Mr II, hapa kuna matatizo kidogo tu ya kiufundi yalitokea, lakini ukweli ni kwamba tatizo lipo kati ya Malaria No More na Mr II. Maana ni Malaria No More ndio walioshindwa kuheshimu mchango ambao Mr II aliutoa mpaka kufanikishwa kwa tamasha hili na kuwapa watu wengine kuratibu, walikuwa na uwezo wa kumchukua mtu mwingine kwa sababu ya ukubwa wa kampuni yake lakini pia wakamuunganisha Mr II ndani kama heshima kwa kazi yake, angalau akalipwa kama alivyolipwa Ruge na watu wengine.

  Bado naamini January Makamba kwa nafasi aliyo nayo katika jamii yetu anao uwezo mkubwa wa kuwabana Malaria No More waje mezani na Mr II ili waweze kumlipa haki anayostahili au hata kumwingiza kwenye matamasha mengine yaliyobaki, ili kuondoa taswira ya kwamba RAIS WETU ALISHIRIKI KWENYE TAMASHA LENYE HARUFU YA DHULUMA. Kitu ambacho nina hakika Rais wetu mpendwa hawezi kukifurahia.

  Kama hili linawezekana, basi lifanyike leo kwa faida ya kesho. Ni vyema kukumbuka sisi ni Watanzania na hii ni nchi yetu, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kufarakana bali tushikamane na kuwa kitu kimoja kama Watanzania, kwa imani kuwa UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU.

  Mungu ibariki Afrika,
  Mungu ibariki Tanzania,
  Asanteni kwa kunisoma.
   
 2. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #2
  Mar 9, 2010
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Duhndefu sana ngoja nisome pole pole ..nichangie hoja
   
 3. Iteitei Lya Kitee

  Iteitei Lya Kitee JF-Expert Member

  #3
  Mar 9, 2010
  Joined: Jan 2, 2008
  Messages: 589
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 35
  Ni ndefu lakini iko too detailed.
  It worth reading ili kumjua mchawi hapo ni nani
   
Loading...