Kilongwe
JF-Expert Member
- Feb 7, 2008
- 423
- 116

Siku chache zilizopita niliwahi kupata nafasi ya kuzungumza na professor mmoja anayejihusisha sana na mambo ya tafiti za mitandao hapa China, tulizungumza mengi, ila moja ya topiki ya mazungumzo ilikuwa ni kuhusu sababu za China kuzuia na kuendelea kuzuia mitandao mikubwa kama Google, Facebook, Twitter nk. Yeye alisema, sio tu kuwapa nafasi wataalamu wa nyumbani toka ushindani wa mataifa makubwa kama marekani bali pia hakuna kuaminiana kati ya nchi hizi mbili. Ukweli ni kuwa, kuna mambo mengi sana yanayoendelea nyuma ya panzia. Aliongelea mambo mengi, pia akanigusia suala la vikwazo kwa Huawei, malalamiko ya marekani kufanyiwa uspy na China nk. Hivyo, kitu kimoja nilichojifunza hapa ni kuwa, jamaa wanajuana na ndio maana hawaaminiani. Nilipomuuliza je kuna sababu nyingine yoyote, alijibu, "Ken ding ya" akimaanisha haswaa. Sababu nyingine aliyoelezea ni kuwa ni jambo la hatari endapo nchi haitokuwa na umiliki wa taarifa muhimu za watu wake, hivyo kitendo cha kuruhusu makampuni ya kichina kuwa na vitu vya inawasaidia kuwa na jeuri na uwezo wa kulinda vitu vyao. Hii ilinifanya nikumbuke lile vuguvugu la mapinduzi ya nchi za warabu (haswaa Tunisia) lilihamasishwa sana ndani ya Facebook.
Wakati ninatafakari na kutafuta baadhi ya reference kwa ajili ya makala hii, nikasema niende Facebook (ingawa ninajua kuwa ninafuatiliwa, hehe) ili nipate baadhi ya taarifa, nikakutana na picha kwenye ukurasa wa Masanja Mkandamizaji juu ya majina ya waliochaguliwa kujiunga na JKT, kwakuwa mimi ni mmoja wa wapenzi namba moja wa JKT, nikasema ni ngoja nikasome majina ya hawa vijana, nilipofika kule, nikakutana na ujumbe mzito " Bandwidth Limit Exceeded". Hii ikanipa mwanga zaidi wa kufikiria katika mtazamo mwingine.

Wavuti ya JKT kama ilivyokuwa inaonekana leo asubuhi.
Baada ya kuona tukio la JKT, nilituma makala kwenye Facebook yangu, kuna marafiki zangu wengi walichangia, na kunitumia tovuti ya idara ya serikali ambayo ni muhusika mkuu wa shughuli za IT za serikali, Mwanzo : Wakala ya Serikali Mtandao nilitumia muda kupitia wavuti yao kuona nini lengo la hawa mawakala. Kitu ambacho nimejifunza ni kuwa bado kuna changamoto nyingi, kwa mfano, idara inayotegemewa kuja kuwa mkombozi mfumo mzima wa EGA ni utekelezaji na si upangaji. Kwa haraka haraka tunaweza kusema, bado hatujafikia sehemu ya kupanga mfumo ambao utalinda na kuchunga uendeshaji wa serikali kwenye medani ya Tehama.

Mfano mzuri , siku zilizopita tumeona matukio mengi ya kuhakiwa kwa wavuti za wizara (Ikiwemo wizara nyeti ya mambo ya ndani), kuzidiwa kwa bandwidth kwa Necta na hii ya JKT nk. Jaribu kutembelea Tanzania Embassy In USA, utapelekwa Embassy of Tanzania | This is the Official website for the Embassy of Tanzania in the United States of America. ukienda ile ya Italia Ambasciata della Repubblica Unita di Tanzania - Tanzania kuna hadi adsense, je nani anachukua hizo $$ rudi kwenye tovuti mama ya taifa The Tanzania National Website uangalie tovuti walizoweka zipo hai na lini ni mara ya mwisho kusasishwa(updated)? . Je nani wa kulaumiwa, wachunga tovuti (Webmasters) au mfumo mzima? Wengi wanaweza kusema ni kutokana na kutokuwa na mawebmaster wasio na ujuzi. Ila hapa tatizo ni mfumo. Kama tuna mfumo mzuri ambao utayakinisha kazi za webmaster, utarativu wa utendaji wa hazina za IT nk basi kama kazi ulipewa na baba yako mdogo bila kuwa na ujuzi, utakimbia mwenyewe wala hautongojea kufukuzwa.
Dunia ya leo si salama, tumezungukwa na maadui kila pande, hivyo tunahitaji njia thabiti za kujilinda, na njia hizi hazitotoka kokote bali kutokana na mipango thabiti yetu sisi wenyewe (mlizi hawezi toka nje). Tunahitaji utaratibu (Framework) utakaoongoza na kufuatwa kila idara za serikali na za watu binafsi ndani ya mipaka ya Tanzania. Leo hii ni jambo la kawaida kwa kila idara kuwa na na mifumo ya kwao isiyofuata kanuni yoyote na huku wengine wasipokuwa nayo kabisaaa. Athari hizi sio tu kwa idara za serikali, bali pia hata kwa mashirika / watu binafsi.
Nini kifanyike?
Baada ya kuandika mengi, labda nitoe maoni yangu na nini kifanyike kuokoa hili jahazi, kwa njia moja au nyingine linaweza kusaidia wahusika katika kujitegemea kwenye nyanja ya IT.
1. Kuanzisha vituo vya tafiti na gunduzi (Innovation) vya Tehama kwenye vyuo vyote vikubwa vya serikali ambavyo vitahusika kuvumbua, kuratibu, kushauri na kuja na mambo mapya yenye manufaa kwa Tanzania kama nchi.
2. Kuanzishwa (kama ipo kupewa nguvu) tume itakayohusika na upangaji wa mfumo (framework) wa taifa kwa upande wa Tehama na , kusimamia utekelezaji na kuishauri serikali.
3. Tume ya utumishi kuangalia upya utaratibu wa kuajiri watu wa tehama ili kupata wenye vigezo na sio kupeana.
4. Serikali kutoa fursa zaidi kwa Watanzania walio nje ya nchi na wenye ujuzi wa kina kushiriki kwenye ujenzi wa Tehama ya Tanzania. Ingawa hii inaweza kuchukuliwa kivingine, ila ushahidi unaonesha kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaofanya vyema kwenye makampuni / mashirika makubwa duniani kote. (China ina utaratibu wa kuandaa semina ya Wachina walio / waliokuwa nje (haswaa zile nchi bora) inawakutanisha na wenzao walio nyumbani kubadilisha ujuzi kwa mustakabali wa taifa, pia hutoa punguzo la kodi kwao pindi wanapotaka kuja kuwekeza / kurudi nyumbani).
Faida Zake:
1. Kutoka katika mikono ya mabepari ambao wanatufuatilia kila kitu tunachofanya.
2. Kuongeza ufanisi kwenye idara za serikali / binafsi.
3. Kuongeza ajira kwa vijana kwani fursa nyingi zaidi zitagunduliwa.
4. Kuwa na udhibiti mkubwa juu ya taarifa zetu / zinazotuhusu.
Yapo mengi sana ya kuandika, ila yalishanenwa kuwa, uzuri wa mambo ni yale machache na yenye kueleweka. Pia ni vyema kuwapa watu wengine zaidi kuchangia kwenye hili.
Imeandikwa Na: Mkata Nyoni
Chief Business Development Officer - Dudumizi Solutions
Email: mnyoni@dudumizi.com Web: www.mkatanyoni.com