Ningalikuwa mufti mkuu ningalijizulu kwa kudhalilishwa na ccm

thatha

JF-Expert Member
Apr 29, 2011
15,340
1,563
Na Dk. Hassan Nassir - Imechapwa 14 September 2011 BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limevuna lilichopanda. Ni baada ya serikali kugoma kutekeleza baadhi ya maombi ya baraza hilo. Maombi hayo ni pamoja na kuanzisha mahakama ya kadhi nchini; kuvunjwa kwa kile kinachoitwa mkataba kati ya serikali na madhehebu ya kikristo nchini na kurejeshwa mikononi mwa Bakwata shule za kiislamu zilizochukuliwa na serikali. Akizungumza katika sherehe za Baraza la Iddi, mjini Dodoma, wiki mbili zilizopita, Rais Jakaya Kikwete alisema, “Serikali haiwezi kuunda mahakama ya kadhi nchini na wala haiwezi kutumia fedha ya wananchi ambao ni walipa kodi wote kugharamia mahakama hiyo.” Badala yake, Kikwete aliwataka waislamu wenyewe kuanzisha mahakama hiyo, kuihudumia na kuiendesha, bila kutegemea fedha kutoka serikalini. Kuhusu hoja ya kurejeshwa mikononi mwa Bakwata, shule ambazo zilichukuliwa na serikali, Kikwete alisema, ni vema Bakwata ikajielekeza katika ujenzi wa shule mpya badala ya kug’ang’ania kurejeshwa kwa zilizochukuliwa. Aliishia kusema, “Maombi hayo yamechelewa.” Akahoji, “Siku zote mlikuwa wapi?” Kikwete alikuwa akijibu risala ya baraza hilo iliyosomwa katika hadhara hiyo na katibu mkuu wake, Sheikh Suleiman Saidi Lolila. Katika risala hiyo, Bakwata walitaka serikali iweke utaratibu mwafaka wa kuundwa kwa mahakama hiyo na kisha kuiendesha. Hata hivyo, Kikwete hakusema maombi ya waislamu yamechelewa kwa muda gani. Wala hakusema ni lini serikali ilitoa muda kwa baraza hilo kuwasilisha ombi lake la kurejeshwa kwa shule hizo. Hakusema pia muda huo uliisha lini? Kwa muda sasa, Bakwata imekuwa ikijitambulisha machoni mwa wengi kama mtetezi mkuu wa serikali na Kikwete binafsi. Si mara moja wala mbili, baadhi ya viongozi wake, akiwamo Sheikh Mkuu Simba Shaaban Bin Simba wamekuwa wakisikika kutetea serikali. Hata hivyo, kwa nasaba hii, hakuna aliyetarajia serikali kukatalia ombi lake. Hakuna aliyetarajia Kikwete kueleza aliyoeleza, tena kwa macho makavu. Kwanza, kilichohimizwa na Bakwata kutekelezwa na serikali, ni sehemu ya ahadi za CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Pili, viongozi wa CCM wamelitumia baraza hilo kwa muda mrefu kama sehemu ya tawi lake la chama. Ushahidi ni katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo baadhi ya viongozi wa baraza hilo walijitokeza hadharani, na wakati mwingine wakitumia kofia ya baraza hilo, kupigania Kikwete na chama chake. Tatu, kwa muda mrefu, serikali imekuwa inaiona Bakwata kama mwakilishi pekee wa waislam nchini; jambo ambalo limezua malalamiko mengi dhidi ya serikali. Uamuzi wa sasa wa serikali, umetoa picha nyingi. Kwamba kuzimwa kwa hoja ya kuanzishwa mahakama ya kadhi nchini, kumethibitisha utovu wa uadilifu wa viongozi wake mbele ya wananchi. Sasa madai yameanza kutapakaa kuwa CCM haijawahi kuwa rafiki wa waislamu; kama badhi yao wanavyojitapa. Vilevile, hatua hiyo inathibitisha madai ya mwanawazuoni mashuhuri nchini, Profesa Hamza Njozi, katika kitabu chake cha “Mauaji ya Mwembechai na Hatma ya Kisiasa ya Tanzania” ambacho kinaeleza kile kinachoitwa, “kilio cha waislamu.” Andishi la Profesa Njozi limeungwa mkono kwa kiasi kikubwa na andishi la Sheikh Mohammed Said anayeeleza historia ya waislamu katika harakati za kudai uhuru.” Lakini kuna jingine pia. Mradi wa Bakwata wa kutaka kujionyesha mbele ya waumini wake, kwamba lolote watakalosema serikali ya CCM italikubali – kama ambavyo wao wanakubali kumtetea Kikwete – umekufa kifo cha nyani. Je, Bakwata itaweza kuwa na ubavu wa kujitapa kuwa wao na serikali ni chanda na pete? Wataanzia wapi? Kumekuwa na madai kuwa kwa muda mrefu sasa, Bakwata imekuwa ikitumika “kudhoofisha nguvu ya waislamu.” Imedaiwa kuwa imekuwa ikitenda mambo yake bila kushirikiana na tasisi nyingine. Kwa mfano, tarehe 7 Julai 1999, viongozi wa Bakwata waligoma kuhudhuria mkutano wa kujadili malalamiko ya waislamu uliofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam chini ya rais wa wakati huo, Benjamin Mkapa. Kisingizio kilichotumika ni kwamba wao hawana malalamiko dhidi ya serikali. Kitu pekee ambacho Bakwata wameshirikiana na taasisi nyingine za kiislamu kukitekeleza, ni maandamano ya kupinga nchi za Magharibi kuivamia Libya. Kwa hiyo, kauli ya Kikwete kwamba Bakwata imechelewa, haiwezi kukubalika. Bakwata haikuchelewa kwa makusudi. Imecheleweshwa. Miongoni mwa walioichelewesha ni Kikwete na serikali yake. Kwa miaka mingi, viongozi wa CCM wamekuwa wakiitumia Bakwata kama tawi lake la chama. Viongozi wa baraza hilo wamekuwa wakijitokeza hadharani kukipigia kampeni chama hicho. Kwa muda mrefu, serikali imekuwa inaiona Bakwata ndiyo mwakilishi pekee wa waislam nchini. Imekataa kuyatambua makundi mengine halali yanayopigania haki za waislamu. Serikali imekataa kushirikiana na taasisi kama Baraza Kuu la Shura ya Maimamu, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitaka serikali kurejesha shule za madhehebu ya kidini, hospitari na kutoa usawa kwenye mgawanyo wa mapato. Lakini wa kulaumiwa katika yote haya, ni serikali kutokana na hatua yake ya kuipa Bakwata – iliyoshindwa kazi – mamlaka ya mwisho ya kusimamia mambo ya waislamu. Pamoja na serikali kufahamu kuwa Bakwata haina tofauti na taasisi nyingine za kiislamu, iliipa mamlaka ya mwisho ya kuwakilisha mambo ya waislamu. Serikali inajua pia kwamba ni kinyume cha sheria ya dini ya kiislamu, kwa chombo hiki ambacho “kimeanzishwa na serikali,” kukabidhiwa jukumu hilo peke yake. Hii inathibitishwa na mwendendo wa viongozi wa taasisi hizi. Kwa mfano, wakati madhehebu mengine ya dini yakijipanga kujenga vyuo vikuu, hospitali na shule za msingi, Bakwata wamekuwa wakijipanga katika uuzaji wa viwanja vilivyotengwa kwa ujenzi wa vyuo vikuu. Wakati madhehebu mengine ya kidini wakikaa chini na kuunda mkakati wa pamoja wa kuwa na vyombo vya habari, Bakwata wametumia serikali kukandamiza vyombo vya habari vinavyoonekana kwenda kinyume na matakwa yao. Bakwata isitegemee Kikwete kuwaletea maendeleo. Ishirikiane na taasisi nyingine kujenga umoja wa waislamu. Sijui kama sasa imepata fundisho!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom