NIMR Tanga: Utafiti wa chanjo ya malaria wapiga hatua | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

NIMR Tanga: Utafiti wa chanjo ya malaria wapiga hatua

Discussion in 'JF Doctor' started by Mahesabu, Jun 8, 2011.

 1. Mahesabu

  Mahesabu JF-Expert Member

  #1
  Jun 8, 2011
  Joined: Jan 27, 2008
  Messages: 5,043
  Likes Received: 666
  Trophy Points: 280
  7th June 2011

  [​IMG]
  Daktari anayehusika na utafiti (kulia) akiwa kazini  Utafiti wa chanjo ya Malaria (RTS,S) sasa upo katika hatua ya tatu ya utafiti unaolenga kubaini uwezo wake katika tiba, usalama wa matumizi ya chanjo hiyo kwa afya ya binadamu na ubora wake katika kuamsha viini kinga mwilini yaani Immunogenicity kwa lugha ya kitaalamu.
  Makala haya yaeleza.Dk.Martha Lemnge ni Mkurugenzi wa kituo cha Tanga, anasema kuwa sheria iliyounda NIMR inatoa fursa kwa taasisi kuwa na vituo vikuu viwili vya utafiti mkoani Tanga ambavyo ni Amani na Tanga.
  Anasema kuwa historia ya utafiti wa taasisi hiyo imeanzia Amani Hill katika milima ya Usambara mashariki ambayo yalikuwa makao makuu ya kituo kabla kituo kuhamishia makao makuu katika Ofisi zake Tanga.
  Awali kituo hicho anasema kimekuwa kikifanya utafiti wa magonjwa ya binadamu kama vile malaria, matende, mabusha na usubi ambapo kwa sasa kimepanua wigo wa utafiti na kuhusisha utafiti kuhusu virusi vya Ukimwi na mahusiano yake katika mfumo mzima wa tiba ya magonjwa nyemelezi yatokanayo na Ukimwi.
  Dhamira kuu ya Nimr Tanga anasema ni kufanya utafiti unaolenga kuimarisha afya kwa kuzingata viwango vya kimataifa vya afya ya binadamu hatimaye kukiwezesha kituo kukamilisha dira yake ya kuwa kituo bora cha utafiti wa magonjwa ya binadamu, huduma za hospitali na tiba.
  Kituo hicho cha Tanga kwa mujibu wa mkuu huyo, kina maabara ya Ambrela inayofanya shughuli za utafiti wa chanjo ya Malaria (RTS,S) ambao upo katika hatua ya tatu ya utafiti unaolenga kubaini uwezo wake katika tiba, usalama wa matumizi ya chanjo hiyo kwa afya ya binadamu na ubora wake katika kuamsha viini kinga mwilini yaani Immunogenicity kwa lugha ya kitaalamu.
  Sambamba na hilo kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo ni kwamba Nimr Tanga pia inamiliki maabara nyingine iliyopo katika Hospitali ya Magunga wilayani Korogwe inayojihusisha na utafiti wa ugonjwa wa malaria, tiba mwafaka ya ugonjwa huo pamoja na chanjo.
  Akizungumzia kuhusiana na shughuli za utafiti zinazofanywa na kituo hicho, Dk.Lemnge anasema kuwa, kituo kimekuwa kikiendesha shughuli za utafiti kwa ushirikiano na hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo.
  Anasema kuwa utafiti uliofanywa kwa ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili kati ya mwaka 2004 na 2005 umebaini kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliolazwa katika hospitali ya Bombo kwa wakati huo, hawakuwa na vimelea vya malaria ikiwa pamoja na wale waliofariki dunia hawakuwa na vimelea vya malaria.
  Dk.Lemnge anasema, matokeo hayo ya utafiti yalipelekea hatua zaidi ya uchunguzi wa kimaabara kufanyika na kugundua kuwa asilimia 75 ya watoto waliolazwa wodini kipindi cha mwaka 2004 - 2005 walikuwa na tatizo la upungufu wa damu.
  “ Katika harakati za kutafuta vyanzo vingine vya homa kwa watoto waliobainika kuwa na vimelea vya malaria kupitia kipimo cha kioo damu, Nimr Tanga imeanzisha kitengo cha Microbiolojia ili kuimarisha uchuguzi wa vimelea vya magonjwa vikiwemo vimelea vinavyosababisha homa kwa watoto mbali na vile vimelea vya malaria”,anafafanua Dk.Lemnge.
  Hatua ya uanzishaji wa kitengo cha microbiolojia anasema kuwa, imewezesha kituo kuendesha utafiti wa uchunguzi wa vimelea vya magonjwa mengine yanayoweza kusababisha homa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano waliolazwa hospitalini hapo mwaka 2009.
  Utafiti huo ulibaini kuwa, homa miongoni mwa watoto waliolazwa katika hospitali ya Bombo ilisababishwa na vimelea vya bakteria.
  Aidha anasema kitengo cha Microbiolojia pia kimesaidia Nimr Tanga kufanikiwa kuendesha tafiti za uchunguzi wa magonjwa yatokanayo na ngono isiyo salama, miongoni mwa akina mama wajawazito wanaopatiwa kinga ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
  “ Kutokana na ufadhili wa Path-Mvi na Mcta kituo kwa kushirikiana na mpango wa kudhibiti malaria ( JMP ) kilifanikiwa kufanya majaribio ya chanjo ya malaria ya RTS,S hatua ya pili huko Korogwe ambapo watoto 447 walipatiwa chanjo ambayo ilionekana kuwa salama na kuwa na uwezo wa kuchochea viini kinga,”anasema.
  Majaribio mengine ya chanjo ya malaria MSP3 katika hatua ya kwanza yalifanyika Korogwe ambapo watoto 45 walichunguzwa kati ya mwaka 2007 mpaka 2008 kwa lengo la kubaini usalama na uwezo wa chanjo hiyo kuchochea viini kinga.
  Anaendelea kueleza kuwa, kwa sasa kituo kinashiriki kufanya majaribio ya hatua ya tatu ya chanjo ya malaria RTS,S ambapo watoto zaidi ya 1,600 kutoka katika vijiji 37 watashiriki kupatiwa chanjo hiyo na kwamba uchunguzi wa aina hiyo unafanyika katika sehemu 11 tofauti barani Afrika.
  Mbali na tafiti hizo, tafiti nyingine zinafanyika katika wilaya za Muheza na Korogwe zikijumuisha utoaji wa huduma vijijini kwa kutumia wahudumu wa afya, mpango huo unakusudia kubaini maambukizi ya malaria mapema na kutoa tiba sahihi.
  “Sasa baada ya tafiti hizi kuna ule mpango wa matumizi ya vyandarua vilivyotiwa viuatilifu umeonyesha kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi ya malaria…mfano vijiji vya Magoda wilayani Muheza maambukizi ya malaria yalishuka kutoka asilimia 75 mpaka 20 katika kipindi cha mwaka 2004,” anasema Dk.Lemnge.
  Shughuli nyingine za kituo cha Nimr Tanga kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo ni kufuatilia vifo, vizazi na takwimu muhimu za watu katika vijiji 14 wilayani Korogwe.
  Takwimu kutokana na mpango huo, zinasaidia kufuatilia afya za watu na kupata takwimu muhimu katika kupanga mipango ya maendeleo.
  Anaeleza kuwa, kupungua kwa maambukizi kulionekana katika vijiji vya ukanda wa chini wilayani Korogwe katika kipindi hicho kwani yalitoka asilimia 78 mwaka 2003 mpaka asilimia 13 mwaka 2008, ambapo katika kipindi hicho maambukizi katika ukanda wa juu yalipungua kutoka asilimia 25 mpaka kufikia asilimia tatu ( 3 ).
  Hali ilivyo ni kwamba, matumizi ya kipimo cha papo kwa papo cha malaria yamepunguza matumizi holela ya dawa za malaria katika wilaya ya Korogwe, ambapo takwimu zilizopatikana kutoka kwa ufuatiliaji wa homa vijijini kwa kutumia wahudumu wa afya na mpango wa ufuatiliaji wa vifo na vizazi na takwimu nyingine pia zimetoa msaada mkubwa katika kupima mafanikio ya malengo ya milenia.
  Hata hivyo, Nimr Tanga haikuishia hapo tu bali pia inafanya utafiti wa muingiliano wa dawa za malaria na za VVU kwa watu wenye maambukizi ya malaria na VVU sawia, utafiti huu unatarajia kutoa mwanga wa matibabu sahihi kwa wagonjwa wenye maambukizi ya VVU na athari zitokanazo na matumizi ya dawa za malaria na VVU kwa wakati mmoja.
  “Utafiti mwingine mkubwa unaofanywa na kituo chetu ni ule unaolenga kuainisha matumizi ya dawa za mseto za kuzuia makali ya Ukimwi ili kupunguza kuota kwa usugu na VVU katika mpango wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua na mpango huu wa utafiti unaendeshwa katika Jiji la Tanga,” anafafanua Mkurugenzi huyo.
  Hata hivyo katika kusisitiza kwamba Malaria haikubaliki, Serikali inatarajia kujenga kiwanda kwa ajili ya kuzalisha dawa maalum za kuulia viluilui na mazalia ya mbu, ikiwa ni juhudi za kuimarisha kinga ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria hapa nchini.
  Mpango wa ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania na ile ya Cuba , na kwamba kiwanda hicho kitajengwa katika mkoa wa Dar es Salaam .
  Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Nimr Taifa, Dk. Mwele Malecela wakati alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka 30 tangu taasisi hiyo ilipoanza kazi zake.
  Dk. Malecela anasema hizo ni juhudi za serikali za katika kutokomeza ugonjwa wa malaria na kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kutenga asilimia moja ya pato la taifa kutumika katika shughuli za utafiti, ikiwemo wa masuala ya Afya na kilimo. Anasema kuwa, licha ya kuwa kiwanda hicho kujengwa jijini Dar es Salaam, madawa yatakayozalishwa yatakuwa yakisambazwa nchi nzima ili kufikia azma ya kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini.
  Hata hivyo, Dk. Malecela anasema kuwa, taasisi hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa fedha kwa ajili ya kufanya tafiti zake kwa madai kuwa, sehemu kubwa ya fedha zilizotolewa na serikali zimeelekezwa kwenye utafiti wa kilimo zaidi, huku akiwashukuru wadau wengine haswa mashirika ya kimataifa yanayowafadhili katika tafiti mbalimbali.
  Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Paul Chikira aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa huo Said Kalembo katika maadhimisho hayo, anaipongeza taasisi hiyo kwa juhudi inazofanya katika kukabiliana na magonjwa hayo, huku akitoa wito kwa viongozi na wananchi kufanya juhudi binafsi katika mapambano hayo. “Watafiti hawawezi kufanya kila kitu, hata kuua mazalia ya mbu tutawaachia watafiti na wataalam?... Nashangaa katika tukio kama hili simuoni Mkurugenzi pamoja na watendaji wake wa mitaa ambao walipaswa kuhudhuria kwa kuwa wao ndio wako karibu zaidi na wananchi na wangeweza kuwaelimisha kwa urahisi” alihoji.
  Hata hivyo, aliwataka watafiti nchini kuwasilisha matokeo ya tafiti zao kwa kutumia lugha Kiswahili ili ziwe na manufaa kwa wananchi wa kawaida na kusaidia kubadilisha hali zao za maisha.
  Sambamba na hilo, pia anawashauri kutumia lugha nyepesi na rahisi katika kuandika matokeo ya tafiti hizo badala ya kutumia misamiati migumu, hali inayosababisha tafiti hizo kukosa tija kwa wengi ambao wanashindwa kuzielewa na kuzifanyia kazi kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
  Chikira anasema kuwa, ni wakati mwafaka kwa taasisi kama Nimr inayotafiti magonjwa kama Malaria na Ukimwi ikatumia lugha ya Kiswahili ili wananchi wafaidike na tafiti zao kuliko tafiti hizo kuwasaidia wasomi tu na wataalam wengine.
  Anasema magonjwa hayo hayachagui mtu wa kuugua na kwamba wananchi wa kawaida wakiwemo wa kijijini ndio wanaohitaji sana kupata mafunzo yanayotokana na tafiti kama hizo, hivyo ni wakati sasa wa kuwafikishia elimu hiyo kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
  Anafafanua kuwa, nchi nyingi duniani zilizoendelea zinatumia lugha zao za asili katika nyanja mbalimbali za kitaaluma, ikiwemo kwenye tafiti za kimaendeleo, na kwamba hilo linahitajika kufanywa pia na watafiti wa nchini.
  Kutokana na msingi huo, katibu tawala huyo aliitaka taasisi hiyo kuchapisha jarida lake linaloelezea mambo mbalimbali ya kitafiti juu ya magonjwa ya binadamu kwa kutumia lugha ya Kiswahili, au angalau mchanganyiko wa lugha hiyo na lugha ya Kiingereza.
  Alitoa wito kwa viongozi na wananchi kufanya juhudi binafsi katika mapambano na magonjwa ya Ukimwi na Malaria na kwamba wasiwategemee watafiti kufanya kila kitu.  SOURCE: NIPASHE
   
 2. Riwa

  Riwa JF-Expert Member

  #2
  Jun 8, 2011
  Joined: Oct 11, 2007
  Messages: 2,601
  Likes Received: 234
  Trophy Points: 160
  Utafiti kama huo tayari unaendelea Ifakara Health Institute kituo cha Bagamoyo, na tayari umeshaanza kuonyesha matokeo mazuri. Hii itakuwa ni 'break through' ya kutokomeza malaria na kumaliza vifo vinavyosababishwa nayo especially kwa watoto chini ya miaka mi5, ukijumlisha na interventions nyingine (ACTs, LLINs, IRS in selected regions, na IPTp)!
   
Loading...