Nimesoma vitabu 655 na haya ni mapinduzi makubwa saba yaliyotokea maishani mwangu

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,074
Mwaka 2014 nilipata maono ya kusoma vitabu 500 ndani ya miaka mitano. Hii ni baada ya kuanza kusoma vitabu mwaka 2012 na kuona manufaa yake kwenye maisha yangu, na hapo kuamua kuweka nguvu zaidi kwenye kujifunza kupitia usomaji wa vitabu.

9D1A5855

Maono hayo niliyashirikisha kwenye makala niliyoandika kwenye mtandao wa AMKA MTANZANIA na kuwaalika watu wengine ambao wangependa twende pamoja safari hii. Nilipata maono kutoka kwa wengi, na wengi walisema ni kitu kisichowezekana.

Ili kufikia lengo hilo, niligawa vitabu 500 kwa miaka mitano na kupata vitabu 100 kwa kila mwaka. Kisha nikagawa vitabu 100 kwa wiki 52 za mwaka na kupata vitabu viwili kila wiki. Hivyo lengo likawa kusoma vitabu viwili kila wiki.

Nashukuru nilipata watu wa kuanza nao mpango huu na usomaji ukaendelea. Mwaka huu 2019 miaka mitano inatimia tangu kupata maono ya vitabu 500 kwa miaka mitano. Hivyo nimechukua muda na kuorodhesha vitabu vyote ambavyo nimeshasoma mpaka sasa.


Vitabu

Na idadi ambayo nimeipata ni vitabu 655, na hii ni kuanzia mwaka 2012. Vitabu kama 100 nimevisoma tangu 2012 mpaka 2014 na vitabu zaidi ya 500 nimevisoma tangu mwaka 2014 mpaka mwaka 2019.

Lengo kuu la kusoma vitabu siyo kuvimaliza ili kusema umemaliza vitabu vingi, bali lengo ni kujifunza na kisha kutumia kile ulichojifunza ili kuboresha maisha yako.

Hivyo nimechukua muda wa kuyatathmini maisha yangu, nilivyokuwa kabla sijaanza kusoma vitabu na baada ya kuanza kusoma vitabu.

Nimeona kuna mapinduzi makubwa saba ambayo yametokea kwenye maisha yangu, ambayo nakiri kabisa kwamba kama nisingekuwa msomaji wa vitabu, nisingeweza kufanya mambo hayo.

Na hapa nakwenda kukushirikisha mapinduzi hayo saba na mwisho nitakupa kiungo cha orodha kamili ya vitabu nilivyosoma.

MOJA; MTAZAMO.

Kabla ya kuanza kusoma vitabu, nilikuwa mtu mwenye mtazamo hasi na mwenye kulalamika na kuwalaumu watu wengine. Kila kilichokuwa kinatokea kwenye maisha yangu nilikuwa natafuta nani amekisababisha. Na hakuwa anakosekana. Kuanzia kuilaumu serikali, kuwalaumu watu wengine, kulaumu mazingira na vingine vingi.

Lakini baada ya kuanza kusoma vitabu mtazamo wangu ulianza kubadilika, kwanza kabisa niliacha kuona ubaya kwenye kila kitu na badala yake kutafuta uzuri. Hata kama ni jambo baya kiasi gani limenitokea, nimekuwa naangalia kuna uzuri gani ndani ya jambo hilo.

Silalamiki na wala simlaumu mtu yeyote kwa chochote kinachotokea kwenye maisha yangu. Nimeyafanya maisha yangu kuwa jukumu langu na chochote kinachotokea ni mimi mwenyewe nimekisababisha. Hata kama natembea barabarani, sehemu ya watembea kwa miguu na akatokea mtu kunigonga na gari, siwezi kumlaumu mtu huyo, hilo ni kosa langu kwa sababu nitakuwa nimekosa umakini wa kutosha.

Mtazamo chanya kuhusu maisha na kuyakubali maisha yangu kama jukumu langu kumenifanya nijisukume zaidi na niyaone maisha kama mchezo ambao unaufurahia pale unapoucheza na siyo kuwa tu mshabiki.

MBILI; MAGUMU.

Kilichonisukuma kuanza kusoma vitabu ni baada ya kukutana na ugumu kwenye maisha yangu. Mwaka 2011 nikiwa mwaka wa tatu chuo kikuu, nilisimamishwa masomo kwa muda usiojulikana. Ni kitu ambacho sikutegemea kitokee, hivyo kilikuja kwangu kwa mshangao mkubwa. Kwa kipindi chote cha nyuma nilikuwa naishi ile hadithi maarufu, nenda shule, soma kwa bidii, faulu na utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Na nilitekeleza hayo yote, nilikuwa nasoma kwa bidii sana na ufaulu wangu ulikuwa wa hali ya juu.

Niliposimamishwa masomo kwa muda usiojulikana nilikuwa kama mtu aliyepigwa kofi kutoka usingizini. Niliona jinsi ambavyo hadithi niliyoiishi kwa kipindi chote nilichokuwa shuleni inazimika ghafla. Baada ya kuona hakuna dalili zozote za kurudi chuoni, ndipo nilipofanya maamuzi na kujiambia kwenye haya maisha nitafanikiwa, iwe nina elimu kubwa au sina. Na hapo ndipo nilipoanza kujifunza vitu mbalimbali kuputia usomaji wa vitabu.

Nakiri kwamba usomaji wa vitabu uliniwezesha kuvuka kipindi hicho kigumu kwenye maisha yangu. Nilirudi chuoni miaka miwili na nusu baadaye na niliendelea na usomaji wa vitabu ambao uliniwezesha kuwa imara zaidi na hata ufaulu wangu kuwa mkubwa kuliko awali kabla ya kufukuzwa.

TATU; UANDISHI.

Usomaji wa vitabu umenisaidia sana kwenye uandishi, kwa sababu msingi wa kwanza wa uandishi ni uwe na maudhui ya kuwashirikisha watu wengine. Na hakuna mtu anayezaliwa akiwa na maudhui, ni vitu ambavyo tunajifunza. Kwa kusoma vitabu vingi, nimekuwa najikuta nina maudhui mengi ambayo naweza kuandika vitu vingi.

Kwanza kabisa nimejijengea tabia ya kuandika kila siku ya maisha yangu, na tangu tarehe 01/01/2015 nimeweza kuandika kila siku bila ya kuacha hata simu moja. Kuandika ndiyo kitu cha kwanza ninachofanya pale ninapoamka asubuhi, kila siku. Nimeweza kuandika maelfu ya makala kwenye mitandao mbalimbali.

Pili nimeweza kuandika vitabu 11 mpaka saa, vitabu nane vikiwa kwenye mfumo wa nakala tete na vitabu vitatu vikiwa kwenye mfumo wa nakala ngumu, yaani vilivyochapwa. Yote haya ni matunda ya usomaji wa vitabu. Unaposoma vitabu vingi, unapata maarifa mengi na pia unajifunza mtindo bora wa uandishi ambao unakuwa maada kwako na wasomaji wako.


vitabu vya elfu 10
vitabu vya elfu 5

NNE; FALSAFA.

Wakati napitia magumu kwenye maisha yangu, nilikuwa natafuta ni namna gani naweza kusimama imara, ni namna gani naweza kutumia magumu ninayopitia na yakawa manufaa kwangu. Na hapo ndipo nilipokutana na Falsafa moja ambayo imekuwa na manufaa makubwa sana kwenye maisha yangu.

Falsafa hiyo ni Ustoa (Stoicism), hii ni falsafa ambayo imekuwepo kwa miaka mingi sana, ilianzishwa na mwanafalsafa Zeno miaka 300 kabla ya Kristo. Ni falsafa ambayo misingi yake ni kuishi kwa misingi ya asili (nature), kudhibiti hisia (emotions) na kuwa na tabia njema (virtues).

Falsafa hii imeniwezesha kupokea kila kinachotokea kwenye maisha na kujua ni sehemu ya mchezo. Imenifundisha kuhusu vitu vilivyopo ndani ya udhibiti wangu na vilivyo nje ya udhibiti wangu na hivyo kutoruhusu vinisumbue. Imenifundisha kudhibiti hisia zangu na kufanya maamuzi kwa kufikiri. Na imenifundisha tabia njema nne ambazo kila mtu anapaswa kujijengea, tabia hizo ni HEKIMA, UJASIRI, HAKI na KIASI.

Kama kuna kitu kimoja ambacho naweza kukishukuru sana kwenye maisha yangu na hasa kupitia usomaji wa vitabu, basi ni kuijua na kuweza kuiishi falsafa ya ustoa. Imenifanya kuwa imara na kuweza kukabiliana na kila changamoto ninayokutana nayo kwenye maisha. Imenifanya kutokukimbia changamoto au kutafuta watu wa kuwalaumu. Na pia imenifanya nisiweze kusumbuliwa na wale wanaokatisha tamaa au kukosoa kwa kila kitu.

Falsafa hii imeniwezesha kuondokana na hasira za mara kwa mara, sina mtu yeyote ambaye ninamchukia kwenye maisha yangu, sina kinyongo na mtu yeyote yule na yeyote anayenichukia au kuniwekea kinyongo namuonea huruma, kwa sababu anajinyima nafasi ya kuyaishi maisha yake kwa utulivu.

TANO; UWEKEZAJI.

Kupitia usomaji wa vitabu nimejifunza kwa kina sana kuhusu uwekezaji. Kwa kipindi chote ambacho nimekaa shuleni, sijawahi kufundishwa popote pale, hisa ni nini, hatifungani ni nini, vipande ni nini na unachaguaje uwekezaji wa kufanya. Kupitia usomaji wa vitabu nimeweza kujifunza misingi yote ya uwekezaji na nimeweza kujua aina mbalimbali za uwekezaji.

Kupitia maarifa haya niliyoyapata nimekuwa mwekezaji kupitia vipande vya mfuko wa umoja kupitia UTT na mwekezaji kwenye soko la hisa ambapo ninamiliki hisa za makampuni kama VODA, CRDB na SWISS.

Pia nimeweza kutoa elimu ya uwekezaji na kuwasaidia wengi kuanza kuwekeza hasa kwenye vipande, mfumo ambao ni rahisi kwa yeyote kuweza kuwa mwekezaji kwa kuanza na mtaji kidogo kabisa.

Kuijua misingi sahihi ya uwekezaji kumenisaidia pia kuweza kutambua uwekezaji usio sahihi, hasa utapeli ambao watu wamekuwa wanaanzia kila mara, ambapo watu wanaahidiwa kupata faida mara dufu kwa muda mfupi.

Bila ya kusoma vitabu, nakiri kabisa nisingejua chochote kuhusu uwekezaji.

SITA; UBISHI.

Hapa nikuambie kitu kimoja, siyo kwa ajili ya kujisifia, bali kwa ajili ya kukuonesha ni wapi natokea. Historia yangu ya ufaulu shuleni ni nzuri sana, nimekuwa napata ufaulu wa juu sana kwenye kila ngazi ya elimu. Shule ya msingi nilifaulu vizuri na kwenda sekondari, kidato cha nne nilipata ufaulu wa daraja la kwanza kwa alama 11 (division one, point 11), kidato cha sita nilipata ufaulu wa daraja la kwanza kwa alama tatu (division one, point 3).

Sasa kwa historia kama hiyo, ni rahisi mtu kuamini kamba unajua kila kitu, una akili sana na hakuna anayeweza kukubishia chochote. Ni mpaka nilipoanza kusoma vitabu ndiyo niligundua ni kwa kiasi gani mimi ni mjinga. Kwa sababu kwa kila kitabu kimoja nilichosoma, nilijifunza vitu vipya ambavyo sivijui, lakini pia ndani yake nilijifunza vitabu vingine zaidi ninavyopaswa kusoma.

Huwa naweka orodha ya vitabu ambavyo nimekutana navyo wakati nasoma kitabu kingine, na mpaka sasa orodha hiyo ina vitabu zaidi ya elfu moja, hivyo ni vitabu ambavyo bado sijavisoma.

Kusoma vitabu kumenisaidia sana kuondokana na ubishi na ujuaji, kumenifanya niwe tayari kujifunza kwa kila mtu, iwe naamini anajua au hajui.

Mwanafalsafa Socrates anachukuliwa kama mtu mwenye hekima sana kuwahi kuishi hapa duniani. Alipoulizwa kwa nini ana hekima kiasi hicho, jibu lake lilikuwa anachojua yeye ni kwamba hakuna anachojua, hivyo kila wakati anakuwa tayari kujifunza. Usomaji wa vitabu umenifundisha unyenyekevu huo, hivyo nimekuwa mtu wa kujifunza na siyo kujifanya mjuaji.

SABA; MAONO.

Mtu ambaye hasomi vitabu, hana tofauti na mtu ambaye ni kipofu, kwa sababu anaweza kuwa na macho, lakini asione ni vitu gani vinavyowezekana mbele yake. Usomaji wa vitabu ndiyo dawa ya upofu wa maono, kwa kujifunza kupitia wengine unaona ni jinsi gani inawezekana na kwako pia.

Usomaji wa vitabu umeniwezesha kutengeneza maono mawili makubwa sana kwenye maisha yangu, haya ni maono ambayo nayafanyia kazi kila siku.

Maono ya kwanza ni kuwa bilionea na hii siyo kwa lengo la fedha, bali kama kipimo cha utoaji wa bidhaa na huduma bora kwa wengine na pia kufanya wengine waone inawezekana.

Maono ya pili ni kuwa raisi wa nchi yangu ya Tanzania, nikiamini kwamba nina mchango mkubwa sana ambao taifa hili linanidai na kupitia nafasi ya uraisi nitaweza kutoa mchango huu vizuri.

Tangu nimeanza kushirikisha maono haya makubwa wazi kabisa kwa kila mtu nimekuwa nakutana na watu wengi wanaokatisha tamaa, wanaokupa kila aina ya sababu kwa nini siwezi kuyafikia au hakuna haja ya kujisumbua nayo. Lakini sijawahi kutetereka katika maono hayo makubwa mawili, nayafanyia kazi kila siku na nina uhakika nitayafikia. Kwa sababu sitakata tamaa, nitapambana kila siku nitakayokuwa hai kuyafikia maono hayo.

Rafiki yangu mpendwa, hayo ndiyo mapinduzi saba yaliyotokea kwenye maisha yangu baada ya kusoma vitabu 655. Nakiri kabisa kwamba mambo hayo saba yasingewezekana au nisingeyafikia kwa kiwango ambacho ningefikia kama nisingejijengea tabia ya usomaji wa vitabu.

Na sasa nataka kukusaidia na wewe uweze kusoma vitabu zaidi, uweze kuleta mapinduzi makubwa kwenye maisha yako. Nikukaribishe kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA ili twende pamoja kwenye safari hii ya usomaji.

Orodha kamili ya vitabu vyote 655 nilivyosoma inapatikana kwenye kiambatanisho vha PDF kwenye uzi huu

Kuna kitu kimoja pekee ambacho naamini kinaweza kubadili maisha ya mtu yeyote yule, kutoka chini na kwenda juu zaidi. Kitu hicho ni usomaji wa vitabu. Nakusihi sana rafiki yangu usome vitabu. Na kama umekuwa unakwama katika usomaji, basi karibu twende pamoja kwenye safari hii.

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,

Kocha Dr Makirita Amani.


elimu fedha 2
WhatsApp Image 2019-07-13 at 18.40.49
 

Attachments

  • ORODHA KAMILI YA VITABU NILIVYOSOMA TANGU FEBRUARY 2012 MPAKA DEC 2019.pdf
    415.8 KB · Views: 40
Tunaopenda kusoma vitabu vya riwaya za kipelelezi kama mikataba ya kishetani, dimbwi la damu n.k unatushauri Nini..?
Kusoma kitabu cha aina yoyote ile ni bora kuliko kutokusoma kabisa.
Unaposoma hata kama ni riwaya, unaipa akili yako kazi ya kutengeneza picha fulani na hilo linakuwa na manufaa kwako.
Lakini asiyesoma kabisa, akili yake imelala, halafu inakuwa dhaifu na mwisho inashindwa kumsaidia.
 
Vitabu viwili kwa week unasoma vitabu vyenye page ngapi mkuu?na kazi nyingine huna ni kusoma tu au inakuwaje hii.
Page 200 mpaka 300 kwa wastani.
Nafanya kazi nyingine pia, siku yangu huwa ni ndefu kidogo,
Kila siku huwa najitahidi nipate masaa 8 mpaka 10 ya kufanya kazi, masaa 4 ya kusoma na masaa 2 ya kuandika.
Kusoma na kuandika ni constant, kila siku, hata iwe siku ya sikukuu.
 
Hapo kwenye magazeti nakupinga, magazeti ni muhimu Sana, yanatupa taarifa, pia kuna makala,
Unaweza kusoma magazeti utakavyo mkuu,
Lakini kwanza soma vitabu.
Habari za magazeti nyingi ni za kupita, lakini maarifa unayoyapata kwenye vitabu ni ya kudumu.
Hebu jaribu kufikiria, habari iliyotikisa magazeti siku kama ya leo mwaka jana, hata kama ulisoma magazeti ya siku hiyo unaikumbuka? Na je ina umuhimu wowote sasa?
Lakini fikiria kama mwaka jana siku kama ya leo ulijifunza kuhusu uwekezaji kwenye hisa, na kisha ukanunua hisa chache, leo hii unakuwa mwekezaji.
Hivyo muhimu ni vipaumbele unavyokuwa umejiwekea, lakini kama upo makini na unataka kupiga hatua, vitabu vinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza kabla ya magazeti.
 
Epistemology.
Umejikita kwenye chanzo kimoja cha maarifa, ambacho ni Kusoma vitabu. Hongera sana.
Kweli. Desturi ya kusoma vitabu ni nzuri, lakini ikumbukwe kuwa knowledge is NOT power. Effectively applied knowledge with definitive plans and persistent actions IS POWER. Unaweza kusoma vitabu 1000 vya "self improvement" au "investment" ila kama huchukui hatua madhubuti, utabakia hapo ulipo.
 
Umeelewa umuhimu wa kusoma vitabu, lakini hukueleza ni vitabu gani vya kusoma, hukueleza ni mbinu gani ya kumfanya mtu asome vitabu kwa wingi na kwaharaka kama unavyo fanya wewe
 
Kweli. Desturi ya kusoma vitabu ni nzuri, lakini ikumbukwe kuwa knowledge is NOT power. Effectively applied knowledge with definitive plans and persistent actions IS POWER. Unaweza kusoma vitabu 1000 vya "self improvement" au "investment" ila kama huchukui hatua madhubuti, utabakia hapo ulipo.

Kusoma vitabu kumenibadilisha sana sana...kidg mazingira ya kupata kula yangu yamnifanya niwe nakosa muda!😑 napenda kusoma vitabu sana..km kina group la wasoma vitabu add me pls!
 
Back
Top Bottom