Nimemkumbuka mkarimu wa Kipemba,aliokota vyeti vyangu na kunirudishia bila hata kupokea shilingi

Ngaliba Dume

JF-Expert Member
Oct 6, 2010
1,702
2,000
Ilinitokea miaka karibu 17 iliyopita.Nikiwa nimechoka sana,natoka katikati ya jiji nikiwa na vyeti vyangu Original vya shule,kidato cha nne na cha sita,cheti cha chuo pamoja na transcript yake,cheti cha kuzaliwa,cheti cha kifo cha mzazi pamoja na passport ya kusafiria.

Sikujua nilikuwa na mawazo gani,lakini nafikiri kwa sbb nilikuwa nimechoka na mizunguko ya kutafuta kazi mjini,sina pesa na mfukoni nimebaki na nauli tu ya kunifikisha geto huku usiku nikiwa sina hakika kama nitakula chochote.

Nilimua kwenda kulala kwa jamaa yangu Tabata,ambaye alikuwa ana chumba na sebule na anafanya kazi Zain wakati huo kama Mpokea Simu.

Nilipofika Tabata sheli,nikashuka kwenye daladala niliyopandia Round about ya Mtaa wa Uhuru K'koo baada ya kuwa nimetembea kwa mguu toka Posta mpaka K'koo.

Nikaacha bahasha ya vyeti vyangu vyotee!!Nilikuwa nimevurugwa sana kwa maisha magumu hapa mjini...Ramani hazisomeki,njaa kaliiiii!!!Nilikaa kiti cha mbele kabisa opposite na dereva.

Kumbe niliposhuka,dereva aliiona bahasha lakini hakujua atanipataje.Akafika kwake akapekua akakuta vyeti vyangu,akawa hana jinsi...Mimi huku nyuma nimetafuta sana daladala za Mnazi Mmoja-Segerea lakini hakuna kitu,kila siku naenda Mnazi naulizia madereva na makondakta kama wameona mtu ameokota vyeti vya mtu asiyemjua.

Kumbe siku ile yule jamaa dereva alikuwa "day waka",na hata hivyo kesho yake gari lilikwenda gereji pale Tabata Dampo,kwa hiyo yeye akavuka maji kurudi kwao Zenji,maana jamaa alikuwa mtu wa Pemba.

Nilitafuta sana sana!!Nikakata tamaa na kutoa taarifa polisi na mahali kwingine ili niweze kusaidiwa kujua napataje vyeti na nyaraka nyingine!Maana siku hiyo nilitoka kwenye usaili nikawa nimeenda na nyaraka orijino.

Bahati nzuri yule Mzanzibari akiwa na mkewe,waliona pembeni mwa bahasha niliyoweka nyaraka zangu kuna namba ya simu,ilikuwa ni namba niliyoandika harakaharaka baada ya kukutana na msela wangu wa O'level.Yeye alikuwa anafanya kazi shirika moja linaitwa Compassion(?),walau akawa na simu ya Nokia ya jeneza.

Walimpigia jamaa,wakamuelekeza,sababu siku ile mimi ndio nilichukua namba ya jamaa yangu kwa wazo kuwa nikipata simu nitamcheki,ikawa ngumu kwa mimi kupatikana sababu sikuwa nimenunua simu.Ikawa tabu sana kupatikana...

Basi jamaa walinitafuta kama miezi miwili hivi,maana Fb,sijui whatsApp wala simu za mchina hazikuwepo.Kumiliki simu ilikuwa kama "anasa".

Siku hiyo nipo zangu town,nikapiga mtaa tuliokutana na jamaa wa Compassion,nikamkumbuka,nilikuwa na jamaa ana simu,nikamwambia anipe nimbeep jamaa yangu fulani anipe michongo,jamaa akasema ana "Extreme" nipige tu.

Ile kumpigia jamaa,aliposikia ni mimi tu,kabla sijamla majanga yangu akanambia,njoo hapa IFM Cafeteria uje ule chakula,upumzike halafu twende Buguruni kwa dereva daladala ukabebe vyeti vyako...Looh nilitaka kuzimia!!Sikuamini..

Haraka mpaka pale,jamaa ndio ananipa mkasa wa Mpemba na vyeti vyangu.Tukaamsha safari mpaka Buguruni,tukamkuta mke wa Mpemba,akatoa bahasha hata sikuamini...Nikasema siondoki mpaka nimuone mumeo,akasema yeye kaamsha gari jioni hii,kurudi hapa ni mpaka saa sita usiku au saba.

Palepale tukampigia mpemba,alipopokea akasema "Amiii we endelea na mihangaiko,maadamu ushapajua hapo napoweka ubavu,waweza kuja siku yoyote,kama utakuja sawaa,usipokuja sawa kwani binadamu tuna mengi,maana mi nshafanya ibada ya kukurudishia mali yako"...Daah hapo ndio Mpemba akanitia wazimu.

Nikamwambia basi naacha hela ya shukrani kwa Mama,Mpemba akasema,Amii ukinipa hela wema wangu unakuwa umeununua,na hutanikumbuka tena...Maana itakuwa umebadili wema kwa pesa,kama ni pesa,hata mie nimemuacha mke wangu usiku huu nipo barabarani naamsha popo.Wewe jisikie amani sheikh,mie nimekupa tu hiyo ni mali yako sio yangu,kwanini unipe pesa??

Mpemba alinifikirisha sana,tukaamua kusepa na jamaa yangu.Lakini nilichukua namba ya Mpemba nikakaa nayo.

Muda ukaenda,kama miaka miwili hivi baadae,mambo yalienda poa.Nikapata kazi...Kusema ukweli kazi nzuri kwa kiwango cha kiafrika.Nilirudi kwa Mpemba pale Buguruni,sikumkuta tena,simu yake haipo hewani.

Nilipomuuliza Mwenye nyumba akanionyesha ndugu zake Mpemba,akasema muda huo wapo pale stand ya Buguruni-Mhimbili wanauza samaki.Akanipa jina la kwenda kumuulizia huyo ndugu yake.Nilipofika pale nikamkuta yule ndugu,nilipomuuliza alipo yule jamaa dereva,akanambia yupo Marapa,japo anaumwa mguu alipata ajali ya gari mataa ya Tabata.

Nikaenda kumuona Mpemba pale Marapa,alishukuru sana sana!!Alishukuru mnooo....Maana kwa kazi yake ya udereva wa daladala alikuwa amekaa ndani miezi mitatu bila kazi,na POP alifungwa la miezi 6.5.

Nikakumbuka wema wa Mpemba na mkewe,nikajitwisha jukumu la "kumshika mkono" katika kipindi chote cha ugonjwa.Kila jioni,kabla ya kufika nyumbani...njia yangu ilikuwa kwa Mpemba then nyumbani.

Mpemba akapona,tukavuka maji mpaka kwao Chakechake,tukala samaki wa kupakwa na ubwabwa wa nazi.Sasa Mpemba ni zaidi ya ndugu yangu,tunatembeleana na kujuliana hali...Nimejifunza mengi kwa Mpemba,mengine siri ya moyo wangu.
 

Van Pauser

JF-Expert Member
Mar 21, 2017
393
500
Hongera sana mkuu siku zote kukumbuka fadhila ni muhimu sana...!!! Umenikumbusha kipindi nipo mwanza nami nilipitia wakati mgumu ila wat wanasema wahaya wana roho mbaya...!!! Nakumbuka kauli moja inasema roho mbaya haina kabila mtu yeyote anaweza kuwa na roho mbaya..!!! Bac nilikaa kwenye nyumba ile ya wahaya hakika walinichukulia kama mwanafamilia japo mm ni mzaliwa wa kanda ya kati sitawasahau wale ndg maana walishakuwa ni kama ndugu zangu
 

barafu

JF-Expert Member
Apr 28, 2013
6,706
2,000
Wapemba kiukweli ni watu wema sana sana!!
Nimekutana nao maeneo kadhaa,ukimkuta Mpemba ambaye hajavurugwa na itikadi za "Muungano" huwa wanakuwa waaminifu na wacha Mungu sana

Hata kuna wakati ilisemwa,ukiwa Pemba ukidondosha hata pochi ya pesa wanakurudishia.Azam Tv walijaribu kuunda kipindi maalumu kujiridhisha tabia hii ya Wapemba

Waliweka kamera ya siri,wakaweka kambi Zenji,wakamseti mtu mmoja akawa anajifanya anapita kando ya watu anadondosha pochi ya pesa,ajabu ni kuwa bila kujua kuna kamera,watu waliokota pochi na kumkimbilia mwenye mali.

Katika watu kumi,watu 8 walikuwa wanarudisha ile pochi ya pesa,na wawili walikuwa wananyuti nayo na kamera unawaumbua.

Wapemba muungano ndio umewavuruga,lakini ni wakarimu sana...
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom