Nimeipenda sana Hadith hii, Tushirikiane kuitafakari hapa

Mcben100

JF-Expert Member
Apr 8, 2013
378
556
KISA CHA MFALME NA JOHO LA AJABU



29/11/2015



1

Hadithi hadithi! Hapo zamani za kale alikuepo Mfalme ambaye alikuwa anajali sana jinsi anavyoonekana na watu, mwenye kupenda makuu na ambaye alikuwa tayari kupata kila anachokitaka.

Mfalme huyo, katika kujiremba zaidi, akaamua kuajiri mafundi cherehani wawili ambao walimuahidi kumshonea vazi la kisasa, la ajabu na ambalo kitambaa chake ni cha ajabu, na hakiwezi kuonekana kwa mtu yeyote yule asiyestahili nafasi ile au mtu ambaye ni juha mkubwa.

Mafundi cherehani hao walitumia muda mrefu kuchukua vipimo mbalimbali vya mwili na mara moja wakaanza kuonekana wakifanya kazi ya kutengeneza nguo ile au vazi lile la ajabu. Watu waliwaona wakikata nguo kwa mikasi wakigeuza geuza kitambaa kisichoonekana na wakati ulipofika wakaanza kukishona asubuhi hadi jioni kwenye cherehani zao.

Walipomaliza kazi yao hiyo ngumu, wakaenda kwa heshima zote kumvisha mfalme vazi lake lile la ajabu. Baada ya kuhakikisha Mfalme amevua nguo zake zote wakamvisha vazi lake lisiloonekana kwa watu wajinga, majuha na wale wasiostahili nafasi kuu.

Kwa vile mfalme hakutaka aonekane juha, akaanza kusifia anavyoonekana na mafundi wakimsifia vile vile alivyopendeza. Wasaidizi wake nao walimsifia kuwa nguo hiyo ‘ya ajabu isiyoonekana’ ilikuwa imemkaa vizuri, na yeye kwa mbwembwe alijizungusha zungusha kwa mikogo.

Kwa vile nguo aliyovaa ilikuwa ni ya “ajabu na isiyoonekana” ikabidi ioneshwe hadharani katika gwaride ambapo Mfalme alivaa vazi hilo na kupitishwa kwenye gari la wazi likokotwalo na farasi.

Kwa vile alikuwa ni mfalme katili vile vile, kila aliyemuona alilisifia “vazi hilo” ili asije akaonekana ndiye juha au mtu asiyestahili, hivyo wasomi, wanasayansi na wanasiasa wote walijikuta wanamsifia Mfalme katika “vazi lake la ajabu lisiloonekana”.

Ilikuwa katika mtaa mmoja ambapo Mfalme alikuwa anapita na vazi lake hilo; huku watu wamejipanga mistari wakimsifia ndipo mtoto mmoja mdogo alishtuka na kupiga kelele: “Mfalme hajavaa nguo, yu uchi!!” na kurudia kelele hizo; huku akiangusha kicheko na ndipo Mfalme akashtuka na watu wakaanza kucheka na ikabidi akimbizwe kuondolewa soni yake.

Imehaririwa kutoka Raia Mwema.
Credit to Lula wa Ndali Mwananzela
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom