Elections 2015 Nimeipenda hii ya Mwigamba kwa Mwanakijiji

Kurunzi

JF-Expert Member
Jul 31, 2009
9,236
9,841
Samson Mwigamba
HABARI za siku nyingi wapenzi wasomaji wa
safu hii. Wengi mmekuwa mkinipigia simu na
kunitumia ujumbe mfupi wa simu mkiuliza kwa
nini nimetoweka hewani.
Kama mnavyojua baada tu ya kutoka Uzini
Zanzibar tuliingia katika maandalizi na
hatimaye kampeni za Arumeru Mashariki.
Kwa majukumu niliyonayo hasa ikizingatiwa
kwamba jimbo lenye uchaguzi mdogo liko
katika mkoa ninaouongoza kichama, mara
nyingi nimejikuta nikishindwa kuandika makala.
Naomba mnisamehe na kunivumilia kwa hilo.
Ndugu zangu nimeguswa sana na makala ya
mwanasafu mwenzangu ajulikanaye kama M.M.
Mwanakijiji katika safu yake Jumatano iliyopita
makala aliyoipa kichwa cha “CHADEMA
ikishindwa Arumeru Mashariki uongozi wote
ujiuzulu”.
Naomba nianze kwa kusema kama kuna watu
walinitamanisha kuandika makala, basi
Mwanakijiji ni miongoni.
Kimsingi makala yangu ya kwanza kwenye
gazeti hili ilikuwa ni nyongeza kwa makala ya
Mwanakijiji iliyokuwa imetangulia.
Nakumbuka yeye aliandika makala iliyosema,
“Kuanguka kwa CCM, unabii utatimia”. Makala
yangu ya kwanza kabisa kwenye gazeti
ikaongezea kwa alichokisema na ya kwangu
ikasema: “Unabii wa kuanguka CCM utatimia
hivi."
Nimekuwa nikihusudu sana makala za
Mwanakijiji. Kila Jumatano ninapochukua gazeti
la Tanzania Daima, kabla hata sijasoma tena
makala yangu na kuona mabadiliko
yaliyofanywa na mhariri, huanza kwa kusoma
makala tatu ambazo ni Hoja ya Mwanakijiji,
Tuendako ya Absalom Kibanda na Mwalimu
Mkuu wa Watu ya Paschally Mayega.
Lakini nikiri kwamba kuna wakati mwandishi
huyu mahiri huandika makala na katika kusoma
mimi huona kwamba rafiki yangu huyu anakosa
kitu fulani kwenye siasa za Tanzania ingawa
anafuatilia sana vyombo vya habari vya
Tanzania na mitandao ya kijamii na wakati
mwingine yeye mwenyewe hufanya mahojiano
na watu mbalimbali.
Kitu anachokikosa Mwanakijiji ni kutokuwepo
kwenye eneo husika au la tukio (field) Tanzania.
Nichukue mfano wa uchaguzi mdogo wa Igunga.
Mimi nilikuwa huko mwanzo hadi mwisho wa
kampeni, wakati Mwanakijiji alikuwa si tu nje ya
Igunga bali nje ya Tanzania. Sidhani kama
angeweza kupata taarifa zote za kilichokuwa
kinaendelea Igunga kwa kupitia vyombo vya
habari.
Hata hivi sasa kwenye uchaguzi wa Arumeru
Mashariki, mimi niko eneo la uchaguzi na yeye
hayupo yuko nje ya nchi. Je, kila kitu
kinachoendelea huku ataweza kukijua?
Sina nia ya kupambana na Mwanakijiji wala
kumkosoa kwa makala yake nzuri na nyingine
nzuri ambazo amekuwa akiziandika.
Ninachotaka kufanya katika makala hii ni
kumuongezea rafiki yangu huyu habari ambazo
wakati mwingine anazikosa na akajikuta katika
kuandika anafanya hitimisho ambalo ingekuwa
tofauti kama angejua undani wa mambo huku
nyumbani.
Naamini kwamba kwa kukosa taarifa hizo ndio
maana alijikuta wakati fulani anaunga mkono
ujio wa CCJ na kudhani eti kingekuja kuiondoa
CCM madarakani labda kwa kukumbuka kauli
aliyowahi kuitoa Nyerere kwamba: “Upinzani wa
kweli utatoka CCM”. Lakini mimi niliyekuwepo
hapa nchini nikifuatilia neno kwa neno la
viongozi wa CCJ na kufuatilia hatua kwa hatua
kilichokuwa kinaendelea kati ya “mitume 12”
na mafisadi, niliandika kitu ambacho ndicho
kilichokuja kutokea!
Sasa naomba nizungumzie makala yake na kwa
nini napinga suala kwamba CHADEMA
ikishindwa uchaguzi wa Arumeru Mashariki
viongozi wote wajiuzulu.
Labda nimkumbushe Mwanakijiji historia ndogo
tu ya CHADEMA ya viongozi wakuu walioko
madarakani. Wengi wa viongozi hawa waliingia
madarakani mwaka 2004 isipokuwa Zitto Kabwe
aliyeingia kwenye unaibu katibu mkuu miaka
kadhaa baadaye kufuatia kuondoka kwenye
nafasi hiyo kwa Shaibu Akwilombe aliyeamua
kuhamia CCM.
Wakati uongozi uliopo unaingia madarakani
mwaka 2004 (mwaka mmoja kabla ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2005), chama kilikuwa na
wabunge wanne wa kuchaguliwa Philemon
Ndesamburo – Moshi Mjini, Dk. Willibrod Slaa –
Karatu, Freeman Mbowe – Hai na Kabourou –
Kigoma Mjini) na mbunge mmoja wa Viti
Maalumu (Grace Kiwelu), kilikuwa hakijawahi
kusimamisha mgombea urais na walikuwa
wakiongoza halmashauri mbili za Karatu na Hai.
Mwaka uliofuata walipata wabunge watano wa
kuchaguliwa na wabunge sita wa viti maalumu
na kuongoza halmashauri tatu ikiwemo Karatu,
Tarime na Kigoma kwa ubia na CCM. Kwa mara
ya kwanza wakasimamisha mgombea urais na
Mwenyekiti wa Taifa akajitolea kuacha ubunge
na kwenda kugombea urais bila kuwa na
uhakika kama atashinda.
Katika kipindi chao cha pili cha uongozi
walichokianza mwaka 2009 walimsimamisha
tena mgombea urais (safari hii ikiwa ni zamu ya
Katibu Mkuu kujitolea kugombea urais) na
wamefanikiwa kupata wabunge wa majimbo 23
na wa Viti Maalumu 25 na kufikisha wabunge
48. Wanaongoza sasa halmashauri saba
(Musoma mjini, Ukerewe, Jiji la Mwanza,
Kigoma ujiji, Karatu, Moshi mjini na Hai).
Mgombea urais pamoja na kuchakachuliwa
amebaki na kura za kutosha na kimsingi
msomaji atakubaliana nami kwamba sehemu
nyingi za nchi hii anakopita Slaa anaitwa rais!
Kwa kifupi uongozi wa chama uliopo
umekifikisha chama mahali ambapo
Watanzania wanasubiri tu ifike 2015
wakikabidhi dola na kuiondoa CCM madarakani.
Viongozi wa namna hii wajiuzulu kwa sababu tu
eti wameshindwa katika chaguzi ndogo?
Labda niseme jambo moja muhimu sana
kufahamika kwa watu wengi. CCM imekuwa
ikishindwa kwenye chaguzi ndogo lakini huwa
hawako tayari kumtangaza mgombea wa
upinzani kwamba kashinda uchaguzi mdogo.
Wanamtangaza pale tu inapofika mahali
ambapo hawana jinsi.
Na ili wakutangaze inabidi upate ushindi wa
kishindo ili hata baada ya kufanya hujuma zao
zote wakute bado wanashindwa kupindua
matokeo. Na hilo limeshafanyika katika
majimbo matatu tu tokea kuanza tena kwa
mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka
1992. CCM ilikubali yaishe katika uchaguzi
mdogo wa Temeke mwaka 1996
walipomtangaza Lyatonga Mrema wa NCCR,
baadaye mwaka huo huo ama mwaka uliofuata
wakamtangaza John Momose Cheyo wa UDP
kule Magu hadi mwaka 2008 walipomtangaza
Charles Mwera wa CHADEMA kule Tarime.
Lazima tukumbuke kwamba katika hizi chaguzi
ndogo za baada ya 2005 si CHADEMA peke yake
iliyoshindwa kutangazwa. Kabla ya 2005
waligoma kumtangaza John Cheyo wa UDP
kwenye uchaguzi mdogo wa Busega ingawa
chama chake kilikuwa na nguvu kubwa pale. Pia
waligoma kumtangaza John Cheyo huyo huyo
katika Jimbo la Bariadi Mashariki ingawa Bariadi
unaweza kusema ni Ikulu ya UDP. Wenye
kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba
matokeo ya uchaguzi mdogo wa Bariadi
Mashariki yalitangazwa chini ya ulinzi wa vifaru
vya kivita vya JWTZ.
Wakati huo nakumbuka Danny Makanga wa CCM
alitangazwa kwamba kamshinda Cheyo kwa kura
1,000 na kauli ya Cheyo kwa Makanga ilikuwa
kwamba: “Makanga hujanishinda, nimeshindwa
na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na tutaona
kama 2005 utarudi”.
Ni kweli 2005 Makanga hakurudi! Wenye
kumbukumbu pia watakumbuka kwamba baada
ya Mrema kutangazwa 1996 kushinda uchaguzi
mdogo wa Temeke, alitamka: “Nimeishinda
CCM yote na serikali yote ya Jamhuri ya
Muungano”.
Baada ya 2005, CUF ikiwa na nguvu kubwa sana
katika maeneo ya Mtwara na Lindi, mgombea
wake hakutangazwa kwenye uchaguzi mdogo
wa Tunduru. Tarime walichakachua lakini
wakashindwa watachakua mpaka wapi.
Wakalazimika kuitangaza CHADEMA.
Mwanakijiji nitawaomba wataalamu wangu wa
kompyuta hapa Arusha wakuwekee kwenye
youtube video CD ambayo ni ‘documentary’ ya
kilichotokea kwenye uchaguzi mdogo wa
Tarime ambayo imepewa na CHADEMA jina la
“Ujasiri wa Kidemokrasia Tarime” pengine
utaelewa kwa nini walitangazwa huko lakini
CCM haikuwatangaza Busanda, Biharamulo,
Kiteto na Igunga.
Vijana wa Tarime na Arusha wana ujasiri wa
kipekee lakini huwezi kuwafananisha na wale
wa Kiteto, Busanda, Biharamulo na Igunga.
Sikilizia kitakachotokea Arumeru kama CCM
watataka kuchakachua matokeo.
Wanajua muziki wa Arusha na nikuhakikishie
kwamba tukishinda tutatangazwa washindi!
Mwanakijiji na wasomaji wetu wote, hujuma
zinazofanywa wakati wa uchaguzi mdogo kwa
kuunganisha nguvu za CCM yenyewe, Polisi,
Usalama wa Taifa, TAKUKURU na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi ni kubwa na nzito mno
ukilinganisha na uwezo wa chama cha upinzani
kisicho na pesa, kisicho na jeshi, kisicho na
mtandao wa uongozi hadi chini kwenye matawi,
mashina na nyumba kumi kumi, kisicho na ofisi
hata kwenye kata tu.
Kwa mfano katika majimbo ya Kiteto, Busanda,
Biharamulo na Igunga, CHADEMA haikuwa na
mtandao wowote wa chama.
Wasiojua ni vema nikawaeleza hapa kwamba ile
inayoitwa ofisi ya CHADEMA Wilaya ya Igunga
imefunguliwa wiki mbili kabla ya kuanza kwa
kampeni za uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo
na kodi ililipwa na makao makuu ya chama
ikiwa ni pamoja na kuwekewa viti na meza.
Pia tuelewe kwamba uongozi wa muda wa
chama kwenye ngazi ya kata na matawi
umesimikwa wiki kadhaa baada ya Rostam Aziz
kutangaza kujiuzulu ubunge wa Igunga. Katika
Igunga CHADEMA haikuwahi kusimamisha
mgombea ubunge na ilikuwa na madiwani
wawili tu katika kata zote 26 na haikuwahi kuwa
na hata mwenyekiti mmoja wa serikali ya kijiji.
Kama hilo halitoshi hujuma zilizofanywa ni za
kufa mtu! Na labda niwaeleze hapa nini CCM
wanafanya kwenye uchaguzi mara tu baada ya
kujua jimbo liko wazi. Wanawatumia mabalozi
wao wa nyumba kumi kumi kuorodhesha
wapiga kura wote kwenye maeneo yao. Kila
balozi anatambua kwa mfano kwamba kwenye
eneo lake kuna wapiga kura 30. Kati yao wana
CCM damu ni wanane, wana CHADEMA damu ni
watano na hawa 17 waliobaki hawana chama.
Lakini CCM wanajua kwamba Mtanzania wa leo
asiye na chama, kwenye kampeni si rahisi
akavutiwa na sera za CCM lazima atavutiwa na
upinzani hususan CHADEMA (kama CHADEMA
ndiye ana nguvu kwenye hilo jimbo) na ni rahisi
kushawishika kupigia kura upinzani badala ya
wao.
Kwa hiyo wanawekeza pesa kuanzia elfu tano
hadi laki moja kutegemeana na uelewa wa mtu.
Wanahakikisha wale 17 hawaendi kupiga kura
kwa kununua shahada zao na wakipiga wale 13
ni dhahiri CCM imeshinda.
Hilo moja, lakini mahali pengine wala
hawahitaji kutoa hela, vitisho tu vinatosha
kama wahusika hawakusoma na hawajui haki
zao. Bado propaganda vyama vya upinzani ni
vyama vya vurugu na mengineyo, bado wizi wa
kwenye kituo kwa kuwarubuni mawakala, bado
hujuma kwa kuwatumia wasimamizi kwenye
vituo, bado vituo hewa vyenye masanduku
yenye karatasi za kura zilizopigwa nyumbani
kwa viongozi wa CCM na kutiki zote kwa
mgombea wa CCM, bado mchezo wakati wa
kujumlisha, na yote hayo yakishindikana kuna
kutangaza kwa nguvu CCM imeshinda kama
walivyofanya Shinyanga mjini kwa marehemu
Philip Sherembi, Segerea kwa Fred Mpendazoe,
Kilombero kwa marehemu Regia Mtema, na
kwingineko.
Katika mazingira hayo ya chama kutokuwa na
mizizi yoyote ndani ya jimbo pamoja na
hujuma chache sana nilizozitaja za wenzetu
kwa kutumia serikali yote lakini bado viongozi
wa CHADEMA wakafanikiwa kukiuza chama kwa
mfano kwa watu wa Igunga wakaelewa na
kukabiliana na hujuma za chama tawala mpaka
wakajitangaza kwa ushindi mwembamba kiasi
kile, unawaambia viongozi wajiuzulu?
Arumeru walianza kwa kununua shahada za
kupigia kura. Kampeni zilikaribia kuzinduliwa,
wakaingiza magari 40 ya polisi na askari
wapatao 1,000.
Hivi sasa OCD na RPC hawana kazi. Mamlaka
yao yametwaliwa na maofisa wa ngazi ya juu
wanne waliotoka Dar es Salaam na Mwanza na
ambao wamepewa jukumu moja tu,
kuhakikisha kwamba CCM inashinda.
Wameingiza mabomu ya machozi maelfu na
risasi za moto za kama njugu. TAKUKURU
haifanyi kazi imekufa ganzi tangu kura za maoni
mpaka kampeni.
Nimekutana na maofisa makumi wa Usalama
wa Taifa na wale wa kutoka ofisi ya DCI Dar es
Salaam, wote wako Arumeru Mashariki.
Hivi ninavyoandika tayari kuna vijana wao
wapatao 200 wameshaingizwa jimboni wakiwa
na makombati kama ya CHADEMA.
Hivi sasa wenyeviti wa vijiji na vitongoji
wamepewa ‘assignment’ maalumu ya
kuhakikisha dakika za mwisho wanawaalika
vijana wengi wanaoshabikia upinzani na kuwapa
chakula kilichotiwa madawa ya kulevya ili
walale na kuibiwa kadi za kupigia kura na yule
ambaye hatakuja na kadi achukuliwe na
kufungiwa mahali asiende kupiga kura.
Si hayo tu mmesikia habari ya vituo hewa vya
kupigia kura, mmesikia habari ya watu
waliojiandikisha mara mbilimbili, mmesikia
propaganda dhidi ya chama na viongozi wa
CHADEMA, mmesikia rushwa ya kufa mtu
inavyotawanywa nje nje, mmesikia matusi ya
nguoni dhidi ya viongozi wakuu wa CHADEMA,
mmesikia jinsi kiongozi wetu alivyokamatwa na
kupigwa na kuteswa hadi kwa kubinywa sehemu
zake za siri.
Hujuma ni nyingi siwezi hata kuziorodhesha
zote. Lakini wafanye wafanyalo bado hujuma
zote kwa pamoja hazitoshi kupunguza kura zetu
mpaka wao washinde!
Tunasema tutakabiliana nao mpaka kieleweke
na safari hii hawatoki!
Arumeru Mashariki tutashinda.
Tumewashika na wameshikika. Tumejiandaa
kuhakikisha kwamba tunatangazwa washindi.
Tumejiandaa pia kuhakikisha kwamba hakuna
mkurugenzi wala msimamizi wa uchaguzi
atakayediriki (chini ya ulinzi wowote ule hata
uwe wa ndege za kivita) kumtangaza mgombea
wa CCM wakati ameshindwa.
Mimi ndiye Mwenyekiti wa chama wa mkoa huu
na kwa mamlaka natamka kwamba CCM
wasijidanganye. Na nilishawaambia kwamba
Arumeru Mashariki si Igunga. Wakijaribu!
Wategemee Hosni Mbarak mwingine Tanzania
kutokea Arusha! Wakijitangaza, hakuna kiongozi
wa kitaifa wala wa mkoa wala wa wilaya
atakayejiuzulu badala yake tutaongoza wote
nguvu ya umma mpaka kieleweke! M.M.
Mwanakijiji njoo Arumeru Mashariki ushuhudie,
utaandika vizuri zaidi.
 
Hajui kwamba dunia ni kijiji? Haya tumekuvika mainchaji manyota upo juu kumzidi MM coz wewe upo kwenye field na mwanakijij hayupo kwenye field!
 
Hajui kwamba dunia ni kijiji? Haya tumekuvika mainchaji manyota upo juu kumzidi MM coz wewe upo kwenye field na mwanakijij hayupo kwenye field!



Mwigamba hajafanya hila yeyote hapo dhidi ya MM,ni kujaribu tu kuwekana sawa kwa nia ya Kujenga tofauti na wewe unavyojaribu ku-suggest indirectly kwamba ni Mashindano!!

No Hard Feelings!!
 
Sasa nimetambua ni kwa nini Nape na Nchemba wanaongea kwa kujiamini kwamba wameshashinda maana serikali nzima mpaka Ikulu wako Arumeru Mashariki mmmh mbona vita vinanukia Arumeru?
 
Mmoja hajui alipo, amma CCJ amma CCK amma CHADEMA, kwa uhakika CCM hayupo.

Mwingine sasa anakiri kuwa Igunga si Arumeru, Jee, walipokuwa wakitamba kabla ya uchaguzi wa Igunga walikuwa hawalijui hilo?

Kumbukeni, CCM juu, juu zaidi.
 
Ni maneno ya kujiamini na yenye ujasiri pamoja na dhuluma zinazofanywa naombe MUNGU mambo yaende kwa amani na mshindi atangazwe kihalali.
 
Sasa nimetambua ni kwa nini Nape na Nchemba wanaongea kwa kujiamini kwamba wameshashinda maana serikali nzima mpaka Ikulu wako Arumeru Mashariki mmmh mbona vita vinanukia Arumeru?

Mkuu CCM hujitekenya wenyewe na kucheka wenyewe.
 
:focus::focus:

Same topic zinazungumzia same party na same person kubali kataa mtajimaliza kwa majungu na choyo! Huyo mnaemsifia juzi kazi tu Rev Mzito K alimchana vibaya kwenye thead yake na wengi wenu mlichana pia nashangaa leo hii mnamsifia huu unaitwa ujuha!

Ifike wakati watu watambue michango ya watu ndani na nje ya vyama sio leo asemwe vibaya kesho asemwe vizuri wenye akili timamu watawaona hamnazo! Tuache fitina na majungu yanaoendeshwa na choyo!
 
Nimeipenda sana makala ya Mwigamba. Bahati mbaya ni kuwa yote ambayo ameyasema juu ya kazi ngumu ambavyo wameifanya na wanaendelea kuifanya katika kushinda chaguzi mbalimbali niliyafikiria wakati najenga hoja yangu ya awali. Sina fikra za kujidaganya kuwa ni rahisi kushinda dhidi ya mashine a.k.a CCM. Lakini, kama nilivyosema awali na maneno ya Mwigamba yanashuhudia Arumeru Mashariki wanapaswa kushinda - kwa hili hajatofautina na mimi.

Anachotofautiana na mimi ni matokeo ya kushindwa. Kwamba, wakishindwa hata kihalali bado wataandamana. Binafsi naamini wakishindwa kihalali bado watahitaji KUJIUZULU. Kwa sababu HAWANA SABABU ya kushindwa Arumeru Mashariki. Sasa haitoshi kudai tu kuwa "watangazwe washindi" la hasha ni LAZIMA watangazwe washindi kwa sababu WAMESHINDA. Hatutaki kutengeneza demokrasia ya kusubiri mtu kutangazwa mshindi; tunataka demokrasia ya mshindi wa halali ndiye anatangazwa mshindi.

Maneno kama haya:

Katika mazingira hayo ya chama kutokuwa na mizizi yoyote ndani ya jimbo pamoja na hujuma chache sana nilizozitaja za wenzetu kwa kutumia serikali yote lakini bado viongozi wa CHADEMA wakafanikiwa kukiuza chama kwa
mfano kwa watu wa Igunga wakaelewa na kukabiliana na hujuma za chama tawala mpaka wakajitangaza kwa ushindi mwembamba kiasi kile, unawaambia viongozi wajiuzulu? Arumeru walianza kwa kununua shahada za kupigia kura. Kampeni zilikaribia kuzinduliwa, wakaingiza magari 40 ya polisi na askari wapatao 1,000. Hivi sasa OCD na RPC hawana kazi. Mamlaka yao yametwaliwa na maofisa wa ngazi ya juu wanne waliotoka Dar es Salaam na Mwanza na
ambao wamepewa jukumu moja tu, kuhakikisha kwamba CCM inashinda. Wameingiza mabomu ya machozi maelfu na
risasi za moto za kama njugu. TAKUKURU haifanyi kazi imekufa ganzi tangu kura za maoni mpaka kampeni.
Nimekutana na maofisa makumi wa Usalama wa Taifa na wale wa kutoka ofisi ya DCI Dar es Salaam, wote wako Arumeru Mashariki. Hivi ninavyoandika tayari kuna vijana wao wapatao 200 wameshaingizwa jimboni wakiwa
na makombati kama ya CHADEMA.

Hayana msingi. Kama tukiamini ni ya kweli tunauliza ni lipi kati ya hayo ambalo CCM na serikali hayakufanya Igunga, Kiteto, Biharamulo au Mbeya Vijijini? Ni lipi ambalo halikufanyika Tarime? Sasa, haya yote si mageni na CDM wamekubali kushiriki uchaguzi! Kama yangekuwa mabaya hivyo wangejitoa kupinga lakini wameamua kushiriki kwa hili hatuwezi kuona huruma kwa kweli. Wamekubali kucheza, wamemkubali refa, wamekubali sheria, wamekubali uwanja, wawe tayari kukubali matokeo!

Anasema:

Tumewashika na wameshikika. Tumejiandaa kuhakikisha kwamba tunatangazwa washindi. Tumejiandaa pia kuhakikisha kwamba hakuna mkurugenzi wala msimamizi wa uchaguzi atakayediriki (chini ya ulinzi wowote ule hata uwe wa ndege za kivita) kumtangaza mgombea wa CCM wakati ameshindwa.

Demokrasia gani hii tunataka kuipigania? Mnataka CCM wasitangazwe washindi kama wameshindwa lakini CDM itangazwe mshindi hata kama haijashinda? Haifai na si haki kujiandaa kuhakikisha kwamba "tunatangazwa washindi"! Mlitakiwa kujiandaa toka mwanzo kwamba "mnashinda ili kutangazwa washindi". CDM wasije kudai kutangazwa washindi wakati hawakushinda vinginevyo zoezi zima la kupiga kura litakuwa halina maana!


Lakini nimeyapenda maneno haya pia ambayo yanaonesha kujiamini na kujipanga:

Mimi ndiye Mwenyekiti wa chama wa mkoa huu na kwa mamlaka natamka kwamba CCM wasijidanganye. Na nilishawaambia kwamba Arumeru Mashariki si Igunga. Wakijaribu! Wategemee Hosni Mbarak mwingine Tanzania
kutokea Arusha! Wakijitangaza, hakuna kiongozi wa kitaifa wala wa mkoa wala wa wilaya atakayejiuzulu badala yake tutaongoza wote nguvu ya umma mpaka kieleweke! M.M. Mwanakijiji njoo Arumeru Mashariki ushuhudie, utaandika vizuri zaidi.

CDM haina sababu ya kushindwa Arumeru Mashariki; NONE. Haijalishi CCM na serikali inafanya nini na hiyo ndiyo msingi wa hoja yangu ya awali kabisa. Kwamba, hata tukichukulia mbinu zote chafu na kila aina ya dhulma bado naona CDM inashinda na inapaswa kushinda hasa kama ikitumia mikakati makini. Wenye kupanga na kusimamia mikakati hiyo ni viongozi wa taifa; ndio wao wanapanga bajeti na kutuma watu huko na kusimamia kampeni nzima. Ndio maana naamini kabisa kuwa haijalishi CDM wanaweza kushindwa vipi (kwa dhulma au kwa haki) bado uongozi mzima wa taifa ni lazima ujiuzulu. Na kwa vile kiongozi wa mkoa naye amesema kuwa ni lazima watangazwe washindi (natumaini ana maana baada ya kushinda) basi wakishindwa na uongozi wake wa mkoa nao ujiuzulu.

Wakiamua kuandamana kwenda Ikulu, wafanye hivyo wakiwa tayari WAMEJIUZULU! Nitawaunga mkono.
 
Makala nzuri inayotukumbusha historia na pia Hoja za Mwanakijiji zimejibiwa vizuri.
 
Mmoja hajui alipo, amma CCJ amma CCK amma CHADEMA, kwa uhakika CCM hayupo.

Mwingine sasa anakiri kuwa Igunga si Arumeru, Jee, walipokuwa wakitamba kabla ya uchaguzi wa Igunga walikuwa hawalijui hilo?

Kumbukeni, CCM juu, juu zaidi.
Hata aliye juu siku moja atashuka tu.
 
Hehehe, mbombo ngafu!!! Hapa bwana sitii neno, nasubiri dk 90 tar 1 April.
 
18 Reactions
Reply
Back
Top Bottom