Nilisahau kuweka chanzo na tarehe/ Raia Mwema, Desemba 25, 2019

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,238
BARAZANI

Waziri Mkuu Narendra Modi anavyoikaba demokrasia

Na Ahmed Rajab

INDIA inawaka moto kwa sababu za kidini. Serikali imetunga sheria mpya ya uraia ambayo watu wengi wanasema inawabagua Waislamu. Wenye kusema hivyo si Waislamu peke yao. Hata Wahindu nao wana maoni hayohayo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo mtu yeyote anayethibitisha kwamba ametoka Afghanistani, Bangladeshi au Pakistani ana haki ya kupewa uraia wa India iwapo ameishi nchini humo kwa miaka sita na ni muumini wa mojawapo ya dini zifuatazo: Kihindu, Kikalasinga, Kibuddha, Kijain, Kiparisi au Kikristo.

Mwislamu hatokubaliwa.

Wakosoaji wa sheria hiyo wanasema kwamba inakwenda kinyume na msingi mkuu wa Katiba ya India wa kutoiendesha nchi kwa miongozo ya kidini. Wanahoji kwamba imani ya mtu ya kidini haipaswi kuwa sharti la mtu kupewa uraia.

Mivutano na mauaji baina ya Waislamu na Wahindu si mageni nchini India. Hayakuanza leo wala jana. Yamekuwa yakitokea mara kwa mara tangu karne ya nane Waislamu walipopigana na Wahindu katika jimbo la Sindhi.

Karne iliyopita uhasama baina ya waumini wa dini hizo huko India uliota mbawa, ukapaa ukiivuka Bahari ya Hindi na kutua Zanzibar.

Ninakumbuka katika zile ziitwazo “zama za siasa” kuanzia miaka ya mwanzo mwanzo ya mwongo wa 1950 jinsi Wahindi wa Zanzibar walivyogawika. Kabla ya hapo waligawika kidini na kitamaduni; kuanzia hapo waligawika kisiasa.

Matokeo yake ni kwamba jumuiya za Wahindu na Waislamu zilitumbukia ndani ya jungu la siasa zilizokuwa zikitokota visiwani humo.

Mitaa yetu ya Vuga na Mkunazini, katika Mji Mkongwe, ilikuwa medani za mapambano. Wengi wa Wahindi walio Waislamu walikiunga mkono chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au Hizbu. Kwa upande mwingine, wengi wa Wahindu walielemea upande wa Afro-Shirazi Party (ASP).

Aghalabu jumuiya hizo zikijitambulisha kwa picha zilizokuwa zikitundikwa kwenye maduka yao. Waliopigania Bara Hindi (Hindustani) isisambaratike wakitundika picha za Mohandas Karamchand Gandhi, maarufu kwa jina la Mahatma Gandhi pamoja na za mfuasi wake mkuu Pandit Jawaharlal Nehru, aliyekuwa waziri mkuu wa mwanzo wa India.

Walioshangilia kuundwa kwa Pakistani wakitundika picha za Mohamed Ali Jinnah, muasisi wa taifa jipya la Pakistani.

Zama hizo wimbo maarufu wa mwimbaji Siti binti Saad uitwao “Baba Pakistani, Mama Hindustani” uliingia mjini. Mashairi yake yalitungwa na Mzanzibari wa asili ya Kihindi aliyekuwa akiitwa Ustaadh Mitu (jina lake kamili lilikuwa Ayoub Ahmad Rangoon). Ingawa kiitikio cha wimbo huo ni “Are baba Pakistan, Hindustan, Aah!”, maudhui yake hayagusii kuundwa kwa taifa la Pakistani.

Ilipokuwa India karibu kuwa huru hapakuwa na taifa lililokuwa likiitwa Pakistani. Hilo eneo ambalo baadaye liliitwa Pakistani lilikuwa sehemu ya Bara Hindi au Hindustani, taifa lililokuwa na wakazi wenye kufuata dini mbali mbali.

Bara Hindi ilijumlisha India, Pakistani ya Magharibi (ambayo sasa ndiyo Pakistani) na Pakistani ya Mashariki, ambayo siku hizi ni nchi huru ya Bangladeshi. Wakazi wengi wa Bara Hindi walikuwa Wahindu, wafuasi wa dini ya Kihindu.

Baadhi ya hao Wahindu wakiamini kwamba Bara Hindi ni taifa lao wao peke yao. Si hayo tu bali wengine wakitaka pia pawepo Bara Hindi Kuu itayoziingiza nchi za Nepali na Bhutani. Dhana zote hizo ziliwatia hofu Waislamu.

Waislamu walijawa na hofu kubwa licha ya kwamba viongozi wakuu wa uhuru wa Bara Hindi Mahatma Gandhi na Jawaharlal Nehru, aliyekuwa waziri mkuu wa mwanzo wa India, walikuwa wakisisitiza kwamba India ni taifa lisilo na upendeleo wa kidini. Lisilo na udini. Msimamo huo ni moja ya misingi ya demokrasia ya India.

Waislamu hawakuamini kwamba watakuwa salama katika India huru. Ndio maana waliwashikilia watawala wa Kiingereza walioitawala Bara Hindi tangu 1857 wawatengee taifa lao wenyewe la Waislamu. Ndipo ilipoundwa Pakistani Agosti 14, 1947, siku moja kabla ya India kuwa huru.

Kumeguliwa Bara Hindi na kuundwa Pakistani kulisababisha uhamiaji wa umati wa watu usiowahi kushuhudiwa duniani. Mamilioni ya Wahindu waliokuwa wakiishi katika taifa jipya la Pakistani walivuka mipaka na kumiminika India.

Na upande wa pili, mamilioni ya Waislamu waliokuwa wakiishi India, waliivuka mipaka wakamiminika Pakistani.

Katika msongamano huo na jazba za kidini pakawashwa moto wa chuki za kidini. Ardhi za kijadi zilipotea. Za Wahindu waliohama Pakistani zilinyakuliwa na Waislamu na za Waislamu walioihama India ziliporwa na Wahindu. Watu wakaanza kupigana na kuchinjana.

Inakisiwa kwamba katika zahma hizo watu wasiopungua milioni mbili waliuliwa. Wahindu waliwaua Waislamu na Waislamu waliwaua Wahindu.

Pakistani na India nazo zikawa nchi zilizohasimiana kwa sababu za kidini. Uhasama huo umeselelea hadi leo.

Sio Waislamu wote waliokimbilia Pakistani. Na wala si Wahindu wote walioihama Pakistani na kukimbilia India. Walikuwepo Wahindu waliosalia Pakistani, ingawa hawakuwa wengi sana.

Kwa upande mwingine, walikuwepo Waislamu, tena wengi, waliobaki India. Kwa kujikinga, Waislamu waliobaki India ama walishirikiana au walikiunga mkono chama cha Congress cha kina Gandhi na Nehru. Chama hicho kilihodhi madaraka nchini humo kwa muda wa nusu karne.

Msimamo wa Gandhi na Nehru wa kuifanya India isiwe na upendeleo wa kidini haukuwafurahisha Wahindu wote. Kuna walioshikilia kwamba India ni taifa la Wahindu na kwamba Wahindu wawe na haki ya kuwa juu ya wafuasi wa dini nyingine.

Mmojao alikuwa daktari aliyeitwa Keshav Baliram Hedgewar. Miaka 22 kabla ya India kuwa huru bwana huyo aliunda jumuiya ya kujitolea aliyoiita Rashtriya Swayamsevak Sangh (RSS). Kwanza, kabla ya kuunda RSS, Hedgewar aliunda chama alichokiita “Kranti Dal” (Chama cha Mapinduzi) kwa lengo la kuwatoa wakoloni wa Kiingereza kutoka Bara Hindi.

Baada ya muda aliona kwamba harakati zake za kimapinduzi hazitoshi kuwapindua Waingereza. Ndipo alipounda RSS.

Malengo ya RSS yalikuwa kuwaunganisha Wahindu na kuiimarisha jamii yao. Hedgewar, ambaye wafuasi wake wakimwita “Doctorji”, alikuwa akihoji kwamba sababu ya Waingereza wachache kuweza kuitawala nchi kubwa kama Bara Hindi ni Wahindu kutokuwa na umoja, kutokuwa na ushujaa (“pararkram”) na kutokuwa na uzalendo.

Wafuasi wake wa RSS wakiamini kwamba Waislamu wengi wa Bara Hindi asilia walikuwa Wahindu waliosilimishwa kwa nguvu. Wakiamini vivyo hivyo kuhusu Wakristo. Lakini walizikubali dini za Kibuddha na Kikalasinga kuwa ni dini asilia za Bara Hindi.

Kwa maoni ya Hedgewar, Gandhi na Nehru walikuwa wakiwadekeza Waislamu kwa kuwahami. Kwa hivyo viongozi hao walikuwa ni hatari na si wa kuaminiwa.

Wakati huohuo, mara kwa mara, Hedgewar alikuwa akisema kwamba Wahindu walidhoofishwa na wakoloni waliokuwa wakiwakalia kichwani. Kwa hivyo aliandaa mpango wa kuwaingiza wanaume wa Kihindu, hususan vijana, kwenye jeshi la mgambo na kuwapatia mafunzo ya kijeshi.

Vile vile, kila wiki akiwapatia vijana waliokuwa wakereketwa wa Kihindu masomo ya kiitikadi (aliyoyaita “baudhik”). Itikadi yenyewe ilikuwa ni itikadi ya “Hindutvi”, yaani ya Uhindu.

Vijana wa Kihindu waliokuwa wakisomeshwa itikadi hiyo wakisomeshwa historia ya taifa la Kihindu na mashujaa wake.

Jambo la kushangaza ni kwamba Hedgewar hakuutumia mtandao wake wa RSS na jeshi lake la mgambo kupigana na wakoloni wa Kiingereza. Kuna wasemao kwamba dhamira hasa ya RSS ilikuwa kupigana na Waislamu wa India.

Januari 30, 1948, milango ya saa kumi na moja na dakika 17 za alasiri, takriban miezi sita baada ya India kupata uhuru, Mahatma Gandhi, baba wa taifa hilo jipya, alipigwa risasi na kuuliwa, mjini New Delhi. Alikuwana umri wa miaka 78. Aliyemuua akiitwa Nathuram Vinayak Godse, mkereketwa wa Kihindu aliyekuwa zamani mwanachama wa RSS.

Godse akimchukia Gandhi. Kwa ufupi, fikra zake zilikuwa zile zile kama za Hedgewar na RSS kwamba Gandhi akiwapendelea Waislamu.

Watu wengi wanaiona jumuiya hiyo ya RSS kuwa ndio “mzazi” wa chama kinachotawala sasa India cha Bharatiya Janata Party (BJP) cha waziri mkuu Narendra Modi.

Baada ya kuuawa Gandhi, jumuiya ya RSS ilipigwa marufuku kwa muda. Hata hivyo, baadaye iliibuka tena polepole na ikawa inajizatiti.

Modi alijiunga na jumuiya hiyo ya RSS yenye chuki dhidi ya Waislamu tangu alipokuwa mtoto wa miaka minane. Siku hizo akimsaidia baba yake kuuza chai kwenye kijikioski chake mjini kwao Vadnagar, katika jimbo la Gujarat.

Alipotimu umri wa miaka 13 Modi alipewa mke. Lakini hakuishi naye kwa muda mrefu kwa sababu wakati mwingi alikuwa akijishughulisha na harakati za RSS. Aliapa kwamba hatooa tena na hadi leo hajaoa tena. Ameisabilia nafsi yake kuitumikia RSS.

Mnamo 1987 Modi alijiunga na chama cha BJP ambacho ni tawi la kisiasa la RSS. Toka 2001 hadi 2014 alikuwa waziri kiongozi wa jimbo la Gujarat na tangu 2014 hadi sasa ni waziri mkuu wa India.

Mara kadhaa tangu 1987 Modi amekuwa akihusishwa na mauaji ya Waislamu katika sehemu mbalimbali za India. Kuna kipindi cha takriban miaka 10 ambapo Marekani na Uingereza zilimpiga marufuku asizikanyage ardhi zao. Wakati mmoja hata wakubwa wa chama chake wakimpa kisogo.

Modi ana usuhuba mkubwa na Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel, na uhusiano baina ya nchi zao umezidi kutanuka tangu India iwe chini Modi.

Kuna shutuma kwamba Israel imekuwa ikiisaidia serikali yake katika mikakati yake ya kuwakandamiza Waislamu nchini mwake na katika mgogoro baina ya India na Pakistani.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab


























Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom