Nilidanganya kuwa mama amefariki ili nipate msaada, roho yangu inahuzunika sana

Restless Hustler

JF-Expert Member
Apr 9, 2017
4,712
17,819
Mimi Ni mzaliwa wa Arusha. Baba yangu alifariki nikiwa na miezi 4 Tangu nizaliwe (hiyo ni mwanzoni mwa 1996, kwa umri huo simkumbuki mzee kwa sura). Ni mtoto wa mwisho kwenye familia ya watoto kumi, wawili walishatangulia mbele ya haki na wawili hawajulikani walipo, walipotea tu kwenye mazingira tata na wadada waliobaki walishaolewa (kawaida ya Maasai kuozesha watoto wadogo), hivyo nilipokuwa mdogo niliwafahamu kaka zangu wawili tu ambao tumefuatana kwa umri.

Baada ya kifo cha baba, kama ilivyo desturi ya Maasai, baba mdogo na mkubwa walitaka kumrithi mama na kugawana watoto wa marehemu kaka yao, mama hakuwa tayari hivyo aliamua kututorosha usiku kutoka Arusha kwenda wilaya moyawapo ndani ya Manyara (kipindi kile Manyara ilikuwa ndani ya mkoa wa Arusha na ilitambulika Kama mbuga au tambarare za Maasai).

Maisha ya huko yalikuwa magumu. Kulala bila kula ilikuwa ni kawaida kwetu. nakumbuka muda mwingi tulishindia mboga za majani, mama alikuwa anaenda kuzichuma porini, anachemsha na kutia chumvi kidogo tunakula. Wakati mwingine anatupikia uji wa dona tunaweka chumvi kidogo tunakunywa. Mama alikuwa anaenda kufanya vibarua vya kupalilia mashamba ya watu ili apewe mahindi kidogo ya kusaga ili atupikie uji.

kidogo kidogo tukakuwa,tukaanza kumsaidia mama, akishika kibarua tunaenda wote Mimi na kaka zangu tunamsaidia inaisha mapema tunapata mahindi tunasaga. tukipalilia kibarua heka moja tunalipwa kilo kumi za mahindi na tulikuwa na uwezo wa kupalilia heka moja kwa siku mbili tu.

Baade mama alipata shamba baada ya kwenda kuuza plot kilichokuwa Arusha na kununua shamba Manyara, kipindi kile mashamba yanagawanywa kwa bei sawa na bure, mtu akishasajiliwa kuwa mkazi wa kudumu, anatoa pesa kiasi kidogo tu anakatiwa msitu Hata ekari 10 ausafishe kuwaajili shamba, hivyo na Sisi tukwa na shamba letu. tulilima kwa jembe la mkono Jambo lililopelekea mavuno hafifu.

Mimi na kaka yangu tulijifunza kuchoma mkaa ili tupate hela ya matumizi ya pale nyumbani.tulifundiwa na wagogo maana wao ndiyo walikuwa wataalam wa kuchoma mkaa pale kijijini, hatimaye na Sisi tukaweza. Wakati mwingine tuliweza kuchoma tanuru kubwa ambalo lilitupatia Gunia tano kwa mkupuo na kila gunia tuliuza kwa shilingi elfu nne kwahiyo yote matano tunapata Elfu ishirini. kuanzia pale matumizi ya pale nyumbani hayakutupiga chenga Wala hatukulala njaa tena.

Mimi na kaka yangu ninayemfuata tulianza shule ya msingi (shule ya kutwa iliyopo jirani na nyumbani), yeye akiwa darasa la pili Mimi la Kwanza. Shule yetu ilikuwa ni mpya, ilikuwa na jengo moja lenye chumba kimoja cha darasa na ofisi ya walimu, hivyo tulisomea chini ya mti. yaani tunapanga mawe kwenye kivuli cha mti tunakalia, mwalimu anakuja na fiberboard (wengine huita sillingboard) iliyopakwa rangi nyeusi upande mmoja,anaegesha kwenye mti na kutumia Kama ubao mweusi, yaani blackboard.

Siku mvua ikinyesha tunachanganyika kwenye Ile room moja ya darasa, tunaimba na baada ya mvua kukatika tunaruhusiwa kwenda nyumbani hata kama bando ni asubuhi na haya ndiyo maisha tuliyoishi kwa miaka saba. Shule iliendelea na baadaye nilimaliza na kufaulu na kupangiwa secondary iliyopo ndani ya wilaya (japo ilikuwa zaidi ya kilometer 100 kutoka nyumbani) ambapo Kaka yangu alipangiwa kabla yangu, hivyo nikiwa kidato cha kwanza yeye cha pili.

Shule pia ilikuwa mpya, haikuwa na bweni la wavulana, wavulana tulikuwa tunalala kwenye ofisi ya kata iliyokuwa karibu na shule, tunatandika magodoro chini tunalala, asubu ratiba za shule zinaendela Kama kawaida. Shule ilikuwa ya serikali lakini kutokana na kuwa mpya, ilikuwa na michango mingi mno na hapo ndipo changamoto ilipoanzia. kulikuwa na michango mingi ambayo haipo shule kwingine. mfano shule haikuwa na meme Wala solar.

Tulitakiwa kwenda na mafuta ya taa, kandili (taa za chemli) kwajili ya mwamnga usiku, mahindi, mchele, maharage, mafuta ya kupikia, kiti na meza, michango ya mlinzi na walimu waliokuwa wanatufundisha kwani idadi kubwa walikuwa ni wa muda tu, hawalipwi na serikali, michango ya Ada, taaluma etc etc. bado mahitaji binafsi na Hali ya nyumbani ndiyo hivyo tena.

Itaendelea...
 
Tusipende kuwahukumu watu kutokana na utashi wa maoni yetu bali kwa kuuvaa uhalisia wa mhusika.

Kil mmoja wetu anapitia au aliwahi kupitia nyakati ngumu kipindi fulani kwenye maisha, na kila mmoja wetu ana uwezo tofauti kiakili na kiuwezo kukabiliana na nyakati hizo. Tusiwe wepesi wa kuwahukumu au kutupa lawama kwa watu bali tunapaswa kuwashauri na kuwatia moyo.
 
22 Reactions
Reply
Back
Top Bottom