Nilichokula ni nini (Fumbo)

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,675
40,555
Chakula nilichokula, nakisifia kitamu!
Nimekula bila hila, kimeniondoa hamu,
Cha jirani sitokula, changu chanitosha hamu,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Sikukipika kwa moto, kwani kimekwisha wiva,
Ndani kina jotojoto, chakula hicho si mbeva,
Si chakula cha watoto, si chakula cha mandava,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nilijihisi nayeya, pale nikikirarua,
Pale nilipochoveya, kwenye mchuzi murua,
Nilihisi napepeya, utamu kunizingua,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nilichokula si kuku, si ng'ombe wala si bata,
Msijeanza kushuku, majina mkaniita,
Wakijiji kala chuku, ametiliwa limbwata,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nilichokula si embe, fenesi au nanasi,
Sio ugali wa sembe, au samaki mkisi,
Si tambi wala si pombe, msidhani nawatusi,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nimekula kwa kuguna, nikala kikimya kimya,
N'kang'ata n'katafuna, na pia nikamung'unya,
Mwenzenu nikajichana, miye ninawatambiya,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Chini nikabingirika, utamu kuninogeya,
Na jasho likanitoka, huku nikichekeleya,
Pumzi ikinitoka, kama ninaogeleya,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Sikitaki cha jirani, cha kwangu chatosheleza,
Kinanitosha shambani, na hata Uingereza,
Hata huko Marekani, changu tumbo chanijaza,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nawauliza wenzangu, na wapishi majikoni,
Mmekula kama changu, chakula hiki ni nini,
Nawauliza Marangu, Kitete na Turiani,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Beti miye nazifunga, miye naondoka humu,
Meza yangu naipanga, nile chakula kitamu,
Komeo nimelifunga, sitaki katishwa hamu,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?
 
Kijana mtanashati, najua hizo sichapati,
mlo umeuyeya, shaka kututahamaki,
kutukumbuka umepwea, mate kutufahamaki,
ulio ula mlo weye, bakuri kunusa hatutaki.

SteveD. (Mwangwi wa Handaki)
 
changu changu, chako ni changu,
jicho lanitoka, machungu mengi yangu,
kubweteka kwaniponza, adimu ilikuwa kwangu,
leo waumega, kukebehi mlo wangu

Mwanakijiji weye shinikizi, wengi wakuita haambiliki,
kwenye hili sikusikilizi, mlo wangu umediliki,
ruhusa jambo mufilisi, anga zangu waletashadidi,
mlo wangu kujinafisi, lako shati haliachiliki

SteveD. (Mwangwi wa Handaki)
 
SteveD.. na wewe kumbe umo.. ama kweli wavumao baharini ni papa, kumbe na wengine wamo!! swadaktaaa!
 
Fumbo fumba lifumbuke, wanajambo wafumbulika,
fumbo lisifumbukike, wanamambo wafedhulika,
yupo mwafrikawakike, komando ahitajika,
nyuso zilipuke, fumbo kufumbulika

Nyuso zilipukike, chokonoa nidawa ugumu,
jiko lisalitike, mwanakijiji kulituhumu
stevo asalimike, kuinama sharti uvungu
mlo ulofumbika, ukoko ulo jungu kuu

Mlo ulofumbika, kijiko kilichopindika,
kero kutambalika, utamu hamu kuchuujika,
jicho lilopevukika, chozi fupi kudinda,
mlo ulofumbika, kikohozi kisichokinga

SteveD. (Mwangwi wa Handaki)
 
Chakula nilichokula, nakisifia kitamu!
Nimekula bila hila, kimeniondoa hamu,
Cha jirani sitokula, changu chanitosha hamu,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Sikukipika kwa moto, kwani kimekwisha wiva,
Ndani kina jotojoto, chakula hicho si mbeva,
Si chakula cha watoto, si chakula cha mandava,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nilijihisi nayeya, pale nikikirarua,
Pale nilipochoveya, kwenye mchuzi murua,
Nilihisi napepeya, utamu kunizingua,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nilichokula si kuku, si ng'ombe wala si bata,
Msijeanza kushuku, majina mkaniita,
Wakijiji kala chuku, ametiliwa limbwata,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nilichokula si embe, fenesi au nanasi,
Sio ugali wa sembe, au samaki mkisi,
Si tambi wala si pombe, msidhani nawatusi,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nimekula kwa kuguna, nikala kikimya kimya,
N'kang'ata n'katafuna, na pia nikamung'unya,
Mwenzenu nikajichana, miye ninawatambiya,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Chini nikabingirika, utamu kuninogeya,
Na jasho likanitoka, huku nikichekeleya,
Pumzi ikinitoka, kama ninaogeleya,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Sikitaki cha jirani, cha kwangu chatosheleza,
Kinanitosha shambani, na hata Uingereza,
Hata huko Marekani, changu tumbo chanijaza,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Nawauliza wenzangu, na wapishi majikoni,
Mmekula kama changu, chakula hiki ni nini,
Nawauliza Marangu, Kitete na Turiani,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?

Beti miye nazifunga, miye naondoka humu,
Meza yangu naipanga, nile chakula kitamu,
Komeo nimelifunga, sitaki katishwa hamu,
Nilichokula kitamu, nilichokula nini?



Kwa salaam naanza,
Na kalamu namata,
Kikiwa kitamu kwa kula,
Hakika Duniani kitasifika.
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Nimeshakamata kalamu,
Kukitaja hicho kitamu,
Nikitaja vitu vitamu
Asali imezidi utamu,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga


Ukitaka kufaidi,
Kula siku za baridi,
Na tena ujitahidi,
Pekecha hiyo asali,
Japo hata kwa ulimi,
Hakika utamu usio kifani,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Nimesema siku za baridi,
Utamu wake huzidi,
Kula ukijitahidi,
Utamu kukolea huzidi,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Asali hata iwe ndogo,
Kama kijani cha mhogo,
Mlaji kama gogo,
Yote itaingia kwa mikogo
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Asali ile kama mboga,
Wala usiifanye woga,
Kwa nyuma utaikoga,
Vyo vyote vyote inalika.
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Asali utamue utambue ,
Utataka kila muda ule,
Na asali nyingine ni nene,
Kama zile za nyuki wajane,
Kila saa nonenone
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Tena zingine zanata,
Ni tamu kama kashata,
Utamani kuing'ata,
Yashinda wali hata nyama ya ngamia,
Harahara kujing'ata,
Basi hivyo kwayo tulia,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Kama ukiwa mwepesi,
Tena na wasiwasi,
Itakupanda bilisi,
Utamani kuning'inia.
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Nami asali yangu ,
Toka tangu na tangu,
kwangu haijawa chungu,
Sikia haijawa chungu,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Asali hakuna nadhifu,
Na wala hakuna chafu,
Wajibu wangu kusifu,
Asali kuitunuku,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Kwa sura haina umbo,
Wala haina makambo,
Nisemayo si uongo,
Utamu wa asali mate yako,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Asali ina siku zake,
Ikae ipumzike,
Iondokewe na makeke,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Mimi nimesifu Asali,
Na wala sio sukari,
Na pia sikulaghai,
hilo nakiri,
Kwa hayo niliyo kuhadithi,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Asali ina siku zake,
Ikae ipumzike,
Iondokewe na makeke,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Laukama laukama,
Ufikiriapo Asali kula,
Itowowe yenye kufaa,
Na mate yako yasiwe yenye homa,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga

Mimi naitwa Mutu,
sili nyama ya nundu,
Inaleta gundu,
Nala asali kwa utundu,
Asali ndo-ulokula mzinga umeuchonga
 
Mfumo wa RTD, vina na mizani, silabi za kiswahili 16 kila mstari, mstari unatenganishwa mara mbili katika silabi nane nane.

Angalia similes na metaphors zinazoweza kutaka kuangaliwa zaidi ya mara moja.

Mahenga wa kaskazi, wa lugha yenye mavazi
Chambi mafumbo ya hadhi, yalo kung'amua kazi
Stara tele kama kadhi,katu si za kibazazi
Kipenda roho cha radhi, si cha tui lake nazi

Hukipati kwake Pazi, hata ukwame jahazi
Hicho umekihifadhi, na kujipatia sazi
Njia kutoa angazi, kamwe hutasema basi
Si cha tui lake nazi, chai wala maandazi

Sema nasema kwa sana, kwa marefu na mapana
Nasema bila kukana, usiku hata mchana
Ulichokula kwa sana, ni utamu wa ubwana
uungwana wa maana, raha yake maulana

Uzuri wa ulichokula, hakihitaji iliki
Bila mikiki mikiki, wanawiri na miliki
Katu haipiti wiki,sivyo utatafaruki
Kipi hiki kiso dhiki, kamwe hakiharibiki?

Mla kala leo leo, mla jana kala nini?
Mnywa vinono vileo, si shubiri ya kwinini
Tamu kuliko machweo, yalabi si magirini
Hata wakikupa cheo, utakitupa porini

Beti ninafika sita, kuandika ninasita
Hapa kalamu nakita, pepe naenda kupeta
Kaditama ninafika, majibu yasadikika
Ulichokula hakika, pendezo la roho fika
 
Mwanzoni nilifikiri,humu tumu wale wa ridhaa tu kumbe hata magwiji mmo.Alianza MKJJ na wewe umeingia,
Mna leta changamoto sana kwa sisi tunaopenda mashairi ingawa si wajuzi.
Tafadhali msisite kutukosoa ikiwa tumepotoka katika kutaradhaki hii fasihi hata kutu PM kama kuna la ziada.
 
weweukulachakula,baliumekulatunda
ilotundatokakale,alilitamanieva
yaonekanamgeni,mpakaumelitangaza
wewe haukula chakula baliumekulatunda
 
Mwanzoni nilifikiri,humu tumu wale wa ridhaa tu kumbe hata magwiji mmo.Alianza MKJJ na wewe umeingia,
Mna leta changamoto sana kwa sisi tunaopenda mashairi ingawa si wajuzi.
Tafadhali msisite kutukosoa ikiwa tumepotoka katika kutaradhaki hii fasihi hata kutu PM kama kuna la ziada.

Ndiyo Ndugu Matuta na wana JF, mnajua hiki kiswahili chetu wa kikuza ni sisi wenyewe na wa ku kiua ni sisi wenyewe, pia wa kukitangaza kimataifa ni sisi wenyewe. Hicho kidogo ukijuwacho jaribu kukiongezea kidogo kidogo, kumbuka wahenga welishasema, "haba na haba hujaza kibaba". Wengi hujifunza kutokana na makosa ya awali, kikubwa ni kutokata tamaa tu.

Nimetingwa kikazi, na sehemu niliyopo kwa sasa sina internet, nashindwa kuchangia kama ambavyo ningependa. Ila nitaendelea kuchangia kila nitakapo kuwa napata muda.
 
Hakika hicho chakula, hakuna mpishi wake,
Mungu mwenyewe kapika, kuonyesha wezo wake,
Kapika kikapikika, katafuta mla wake,
Chakula ulichokula, ni penzi ulilopata
 
Hodi babu wa kijiji, mlango nifungulie,
Niandalie na uji, vinono usibanie,
Na ya kuoga maji, bibi aniandalie,
Nimekuja na jawabu, keti nikufunulie.

Kitamu ulichokila, kimepikwa na wawili,
Jinsia ya Jamila, na jinsia ya Ali,
Walaji huvisaula, viwalo katika mwili.
Aliyekileta Mola, Mjuzi wa kila hali,

Kweli ulijifungia, na chakulacho hicho,
Ukawa wakichekea, bila hata ya kificho,
Utamu ulipokolea, mara ukalegeza macho,
Ukawa wajisemea, "hiki kweli hasa ndicho!"

Haa! Maziwa ukamwaga, kukimwagia chakula,
Katikati ya mafiga, yakapenya kwa ghafula,
Na meno ukayasaga, babu hukuwa na hila,
Bahari ya jasho kuoga, ukajiona msela.

Na mara kikalegea, kijiko cha kulilia,
Hapo ukakichomoa, kilele umefikia,
Mwili wote umeloa, nguvu zimekwishia,
Nadhani nimepatia, chakula kukutajia.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom