Nidhamu ya Chama: Kiini cha Kudorora Viongozi wa CCM!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,474
39,987
Nimeona tulizungumzie hili leo na kama kawaida nimelizungumza kwa kina.

Hivi umewahi kujiuliza inakuwaje watu wasomi waliobobea, na watu ambao walikuwa viongozi wazuri sana wakiwa ngazi za chini lakini mara baada ya kuingia katika Chama au kupata nafasi za juu wamegeuka kuwa butu? Hivi umewahi kujiuliza inakuwaje mtu mwenye mawazo tofauti katika CCM anaonekana "si mmoja wao"? Watu kama kina Jumbe, Seif, Njelu, Horace, Salim, Mrema, nk imekuwaje wajikute wako nje ya "mfumo"?

Jibu ni rahisi. Ni lile dudu lililoshika hatamu ya chama, liitwalo "Nidhamu ya Chama". Ni tatizo kubwa kwani viongozi wetu wana utii mkubwa kwa CCM kuliko Nchi yao na wako tayari kutetea na kulinda Katiba na Ilani ya CCM kuliko kutetea na kulinda Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano! Ni utii wenye kuogofya kwani wabunge, madiwani, na viongozi wengine ambao hawafurahishwi na mambo fulani ndani ya CCM hawawezi kusema chochote kwa kuogopa hilo jinamizi la Nidhamu ya Chama! Kila kitu ndani ya CCM lazima kiende kwenye vikao, na nje ya vikao uko kwenye matata! Pia hili dudu "nidhamu ya chama" halisamehi! Kama Ngawaiya, Masumbuko n.k walidhani wakirudi CCM watafurahiwa sana, wamejidanganya!!!!

Wabunge wa CCM hawawezi kupiga kelele kuikoromea serikali. Na zaidi hawa wabunge wa kuteuliwa ambao hata chamba hawawezi kuikosoa serikali bila kujikuta wakiung'ata mkono unaowalisha! Bila ya shaka wanaweza kuguna na kukohoa kidogo Bungeni (kuonyesha kuwa wapo) lakini hawawezi kamwe kupinga kwa dhati sera zisizo na manufaa, au kuhoji kwa kina mipango mibovu ya serikali wasije wakaonekana wapindani "ndani ya CCM". Imefikia wakati sasa wabunge wa CCM wenye hoja nzuri wanazungumza na wabunge wa upinzani pembeni ili wabunge wa upinzani ndo wazungumzie hoja hizo!! Hebu fuatilia hili suala la Mikataba ya Madini na hiyo mingine utaelewa ninachosema ni nini. Wako wapi kina C. Mzindakaya? Leo wananyamazishwa kiufundi na kina Juma Akukweti!

Huu utii kwa chama, ni utii hatari, unaovuruga utendaji kazi, na unaowatia watu hofu (Mhe. Spika samahani kwa kutumia neno "kutia"). Ni utii ambao unakigeuza chama kuwa kama kikundi cha Kimafia (La Cosa Nostra) ambapo wale wote walioko ndani hawana budi kujipanga mstari, kufuata kifimbo cha kwaya master! Ni utii unaotaka wacheza ngoma kucheza pale tu CCM ikipiga ngoma kwani wachezaji hawatakiwi hata kupiga filimbi zao isipokuwa zile wanazopewa na Chama! Ni ngoma ya kitumwa! na ya kusukumwa!

Huu ni udhaifu mkubwa wa CCM na hiki ndicho kitakachowaangusha CCM. Wanaweza kutawala kwa miaka 70 au hata mia moja lakini kama wakiendelea hivi, wataanguka "anguko kuu" kama vyama vingine ambavyo vilijidhania kuwa "vimetumwa toka mbinguni". CCM lazima ibadilike, lazime iwape uhuru wanachama wake kupingana kwa hoja na wakubwa bila kutengwa au kunyanyaswa! Ni lazima wanachama ambao hawakubaliani na sera fulani wawe huru kuzipinga bila kufukuzwa au kuitishwa kwenye vikao vya "nidhamu ya chama!" Wakati umefika wabunge waweze kuleta miswada yao ambayo ni tofauti na ile ya serikali ili ijadiliwe Bungeni, miswada mizuri ishinde na CCM iendelee kuwa imara!!

Hata hivyo, ni lazima nikiri kuwa hii nidhamu ya chama ndiyo imekifanya CCM kuwa chama kikongwe, kilichobobea, na chenye umoja (au angalau kuwa na hisia za umoja) kuliko chama kingine chochote nchini. Lakini, niseme pia kuwa umoja huu ni wa kusadikika na si wa kuaminika. Sote tunajua kuna makundi ndani ya CCM, kuna wana Mtandao, kuna watu wa BWM, kuna watu wa JSM n.k. Licha ya jitihada za viongozi mbalimbali kuitisha kuvunjwa kwa makundi hayo, makundi hayo bado yanaendelea! Hata hivyo sitashangaa baadhi ya viongozi mashuhuru wakijikuta wanafukuzwa au kuondolewa katika uongozi pale rungu la Nidhamu ya Chama litakapowapitia.

Kwa yeyote mpenda demokrasia, na anayekipenda chama cha mapinduzi na mtu yule ambaye anaipenda Tanzania, basi CCM ni lazima ibadilike na iende na wakati ili watu wasiogope kuwa viongozi ndani yake kwani kila siku watakuwa wanajiangalia mgongoni kuona kama kuna mtu anawafuata au la! CCM lazima ijifunze kulifunga kamba hili jinamizi na ikibidi iliue kwani maisha ya chama chenyewe yako hatarini. Kwani hili jinamizi likimaliza kule walioko nje, litageukia ndani, na njaa yake haitulizwi! Vinginevyo, tumeanza kuona kuinuka na kuanguka kwa Chama cha Mapinduzi!!

Kigumu chama cha Mapinduzi ! Kigumu ! lakini Kidumu? Kidumu - kikiwa na mabadiliko
 
Wanaotaka Kikwete agombee 2010, wanaogopa nini? (MwanaHalisi Aprili 15, 2009)

kikwetekampeni.jpg

Kuna kundi la watu waoga wanajitokeza ndani ya CCM. Kundi la watu wasiojiamini na wasioamini kuwa Rais Kikwete anaweza kuchagulika tena 2010. Kundi hili lina hofu kuwa Rais Kikwete anaweza kuamua kutokugombea tena 2010 na hivyo kubadilisha kabisa mwelekeo wa kisiasa katika chama hicho na bila ya shaka nchi nzima. Kundi hili limeanza kuonesha dalili ya kutetemeka na kama wapambe wanaoogopa kupoteza ujiko wao limeanza kujitokeza na kuimba wimbo wa "Kikwete mgombea tena 2010 ndani ya CCM".

Ninajiuliza hawa ndugu zetu wanaogopa nini? Ni kitu gani kinawatia hofu hivi kiasi kwamba mapema mwaka huu (miezi mingi tu kabla ya uchaguzi) wameanza kutishwa na sasa wameamua kujionesha wazi kuwa chaguo lao ni Kikwete? Je kwa kujitokeza kwao kusema ‘chaguo lao ni Kikwete' kunamsaidia Kikwete au kunaonesha udhaifu wake uliopo kuelekea 2010?

Kinachonishangaza ni kuwa hawa ndugu zetu wanaonekana wanatambua kitu ambacho wengine hatukitambui; yaani, ndani ya CCM kuna mtu zaidi ya Kikwete ambaye anatamani kugombea Urais mwakani. Mtu huyo nina uhakika si Shibuda kwani Shibuda alifanya hivyo hata mwaka 2005 na sidhani kama anawatisha hivyo. Kitendo cha mtu aliyekuwa Waziri Mkuu, kitendo cha mtu aliyewahi kuwa Spika na jumuiya mbalimbali za CCM mikoani kuanza kujitokeza na kusema Kikwete ndiye atakuwa mgombea wao kunatudokeza jambo moja kuwa kuna mtu mwingine ndani ya CCM anataka kuwania nafasi hiyo ya Urais.

Mtu huyo ni nani? Sitaki hata kumdhania ni nani lakini kama yupo mtu huyo ana nguvu na ujiko wa kiasi gani hadi kuwafanya watu wazima na akili zao kutetemeka katika majumba yao, kusababisha wakongwe ambao majina yao tulishayasahau kutoka katika maficho yao? Mtu huyo ana ubavu gani wa kushindana na mtu aliyeshinda nafasi ya Urais kwa asilimia 80 ya wapiga kura?

Kama kuna mtu huyo ndani ya CCM basi ina maana ya kuwa mwaka 2005 Watanzania walifanya makosa kumchagua Kikwete. Kwa sababu kama kuna mtu ambaye anaweza kumshinda Kikwete leo hii ina maana mtu huyo tulikuwa naye 2005 na hatukumpa nafasi!

Tulifanya makosa?
Jinsi ambavyo watetezi wa uteuzi wa Kikwete wanavyozungumza ni kana kwamba wako tayari kuendelea na makosa yale yale 2010 bila kuyasahihisha hata kama wakipewa nafasi hiyo. Waoga hawa wanaamini kuwa ni bora kuendelea na kosa lao kuliko kulisahihisha na hivyo wao hawajali jingine lolote isipokuwa hawako tayari kumuona mtu mwingine yoyote akigombea nafasi ya urais zaidi ya Kikwete.

Hapa hatuna budi kujiuliza kama kweli tulifanya makosa 2010 kwa kumchagua Kikwete kama Rais wetu? Hivi tulimchagua kwa sababu tuliona nini? Alikuwa na rekodi gani ya uongozi kumlinganisha na mgombea mwingine yoyote? Alikuwa na uwezo gani wa kiuongozi tukimpima na mtu mwingine? Yawezekana wengi waliopiga walipiga kura kwa sababu ya kuangalia ile sura ya ujana na tabasamu lake? Yawezekana wengine walipiga kura kwa sababu waliamini kuwa yeye kweli ni "chaguo la Mungu"?

Sasa kama wananchi leo wamegundua kuwa walifanya makosa na wanataka kuyasahihisha hawa waoga wa CCM wanataka kuwanyima wananchi nafasi ya kubadilisha uamuzi wao kwa njia ya kura? Kwa ubavu gani walionao?

Kikwete sasa anarekodi!
Mwaka 2005 Kikwete hakuwa na rekodi ya kuonesha uongozi wake na kama ingekuwa katika nchi nyingine kuna mambo ambayo angetakiwa kutolea maelezo ndio maana walimkwepesha kufanya midahalo na wagombea wengine ili watu wampime. Kulikuwa na masuala ya IPTL na tuhuma za kupokea fedha toka Iran na Oman. Bahati mbaya waandishi na wana CCM wengi walikuwa wamepigwa ganzi ya mapenzi kiasi kwamba hakuna aliyethubutu kumhoji maswali magumu na hivyo tukampitisha kwa kufaraha kwa kuangalia vile ambavyo si vya msingi.

Sasa hata hivyo ana rekodi ambayo yeye mwenyewe anaweza kuisimamia. Watetezi hawa wa Kikwete wanatuambia kuwa anaongoza mapambano ya ufisadi wakitolea mfano wa kesi uchwara zilizofikishwa mahakamani (ndiyo nimesema uchwara). Hawa wanataka tumaini kuwa watu kufikishwa mahakamani (tusiangalie mashtaka yenyewe ni yapi) basi mapambano dhidi ya ufisadi yanaendelea chini ya Kikwete.

Lakini rekodi yake sasa ni kubwa zaidi na ambayo mwana CCM yeyote anayo haki ya kuipa changamoto, kuihoji na kumpa nafasi Rais Kikwete kuitetea. Je Rais Kikwete anahusika vipi katika kuwaleta Dowans? Je alihusika vipi katika suala la Richmond pale ambapo baadhi ya watumishi walipotaka mkataba huo usitishwe? Je Rais Kikwete alihusika vipi na kuwaacha watoto wa Kitanzania wasote ugenini na kupigwa baridi kwa kitu kimoja cha kuomba elimu na kuwalazimisha kuwarudisha kwa aibu na kwa nguvu Tanzania toka Ukraine? Kwanini hadi leo serikali yake haijaomba radhi kwa hilo?

Rekodi yake ipo na ninaamini hawa waoga walioibuka siku hizi wanajua hawezi kuitetea! Lakini uzuri ni kuwa kwa kumpambanisha na MwanaCCM mwingine basi tunampa nafasi Rais wetu kuona makosa yake, kukiri makosa ya wazi lakini pia tunampa nafasi ya kujipanga upya. Kumnyima nafasi hiyo ni kuendeleza utamaduni wa woga na sera za unafiki.

CCM siyo Rais!
Mojawapo ya utamaduni mbovu ambao ndugu zetu watetezi wa Kikwete wanataka uendelezwe ni ule wa "kumwachia Rais aliyeko madarakani mihula yake miwili". Dhana hii ni potofu, ya kibabe na aina mfanano wowote na utawala wa demokrasia. Kama hili lingekuwa zuri wao CCM si ndiyo wana Bunge na wana Rais kwanini wasiamua kubadilisha Katiba na kuweka awamu ya Rais kuwa ni muhula mmoja wa miaka kumi! Maana kama tayari wanataka Kikwete awe mgombea wao 2010 na mtu mwingine yoyote CCM asigombee basi waamue tu kufanya uchaguzi wa wabunge na ule wa Urais uahirishwe hadi Kikwete atakapomaliza awamu yake 2015!

Vinginevyo, CCM hawaodhi nafasi ya Urais wa Tanzania na aliyeko madarakani hana ubia na nafasi hiyo. Nafasi hiyo Kikatiba inashindaniwa kila baada ya miaka 5 na hakuna garantii kuwa ukiwa Rais basi mhula wako wa pili utapewa kwa dezo. Kikwete ni lazima apambanishwe ndani ya CCM kama tulivyofanya 2005 na kabla yake, ni lazima arudishe fomu za kugombea pamoja na watu wengine wanaotaka kufanya hivyo, na ni lazima atetee nia yake hiyo kama alivyofanya 2005. Nje ya hapo, CCM itangaze kuwa Tanzania ni nchi ya Udikteta wa chama cha Mapinduzi!

Wanaotaka kugombea wasitishwe
Utawala wa Demokrasia unatutaka tutoe nafasi sawa kwa mtu yeyote anayetaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi. NI kwa sababu hiyo naamini mojawapo ya mambo ambayo yafanyike mwaka huu ni pamoja na Bunge hatimaye kubadilisha sheria ili kuruhusu mgombea binafsi wa nafasi yoyote ya uongozi. Haya mambo ya kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama usichokubaliana na nacho hayana msingi! Katika taifa la watu milioni 40 ninaamini kuna watu wa kutosha wenye akili timamu wanaoweza kufikiria jinsi gani ugombea binafsi unawezakufanyika bila kuweka mzigo mkubwa kwa mgombea yeyote kulinganisha na yule wa chama.

Hata hivyo ndani ya CCM kama kuna watu wanaamini wanaweza kuliongoza Taifa letu vizuri zaidi, kwa kuthubutu zaidi na kuliamsha kuelekea mafanikio na maendeleo ya kweli (ya watu siyo vitu) basi watu hawa wako huru kujitokeza bila kuona haya kama alivyofanya Shibuda. Watetezi wake hawana uhodhi wa CCM na wasitumie jina la CCM kuwatisha watu wengine ambao wako ndani ya Chama hicho.

Kama wao wanaogopa kuwa Kikwete asipochaguliwa tena 2010 basi utakuwa ni mwisho wao na madudu yao yatajulikana basi hayo ni matatizo yao. Ni wao waliokaa kimya bila kujitokeza wakati nchi yetu inapitia wizo mkubwa kabisa wa mabilioni ya fedha, lakini linapokuja suala la hamu zao wanajitokeza huku wakitingisha vidole vyao!

Mtanzania yoyote ndani ya CCM anayetaka kugombea nafasi ya Urais ni lazima apewe nafasi sawa.

Vinginevyo, kama waoga hawa wanajua kuwa Kikwete hawezi kushinda akipambanishwa na mtu mwingine CCM basi ushauri wangu ni kuwa wawatimue wale wote ambao wanaonesha nia ya kutaka kupambana na Kikwete! Wawatimue na kuwafukuza katika Taifa la Tanzania! Na wawanyang'anye na uraia kabisa ili wasirudi.

Wakishafanya hivyo, waamue kufuta sheria inayoruhusu vyama vingine ili tuwe na chama kimoja chenye mgombea mmoja tu wa CCM ili Taifa zime limpigie kura za Ndiyo au Hapana. Na kama akipata kura nyingi za Hapana, basi wamuapishe kuwa ni Rais kwani atakuwa bado amepata kura nyingi!

Vinginevyo, wamuache Rais Kikwete afanye kazi yake na akitaka kugombea mwakani agombee akiamua kupumzika apumzike na kuwapisha wengine. Alipotaka kugombea ilikuwa ni kwa miaka 5 na kama kwa sababu zake zozote akiamua kutokugombea basi asijisikie shinikizo la kugombea ili kuwaridhidha watu fulani ambao muda wao wa kisiasa umeshapita!

Lakini akitaka kugombea basi asitumie vyombo vya dola au hawa wapambe kutuma ujumbe wa vitisho kwa watu wanaompinga au ambao wanaamini wanaweza kufanya bora zaidi ndani ya CCM bali awe tayari kusimama na rekodi yake na hoja zake kugombea tena nafasi ya Urais.

Kwa kufanya hivyo Rais Kikwete atathibitisha kuwa yeye ni mwanademokrasia na ambaye hana hofu ya kushindana na mtu yeyote kwenye sanduku la kura. Iwe ni mwana CCM mwenzake au nje ya CCM. Lakini endapo Kamati Kuu au chombo kingine rasmi cha Chama kikitoka na kusema kuwa Mgombea wa CCM atakuwa ni Kikwete tu basi lile shimo la kifo cha demokrasia tuliongezee kina chake ili ndani yake wa kwanza kutumbukizwa atakuwa ni Chama cha Mapinduzi!

Vinginevyo, mwana CCM anayetaka kugombea na kushindana na Kikwete asiwaogope waoga hawa mambo leo na asione haya kuonesha nia yake hiyo na wala asionekane adui bali asimame kama mwanademokrasia na mwanamapinduzi wa kweli kugombea nafasi hiyo na kutoa changamoto hiyo kwa Kikwete. Yeyote ambaye hapendi akimbilie baharini ajitose!

Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com
 
Babu leo umesema sana ,Hakika mngekuwepo kama wewe kumi tungekuwa mbali.
 
Babu leo umesema sana ,Hakika mngekuwepo kama wewe kumi tungekuwa mbali.

Unajua wakati mwingine nikirudi kusoma nilichoandika nashangazwa na ukweli wake. Katika makala hiyo binafsi nimeguswa na kauli yangu hii:
CCM hawaodhi nafasi ya Urais wa Tanzania na aliyeko madarakani hana ubia na nafasi hiyo. Nafasi hiyo Kikatiba inashindaniwa kila baada ya miaka 5 na hakuna garantii kuwa ukiwa Rais basi mhula wako wa pili utapewa kwa dezo. Kikwete ni lazima apambanishwe ndani ya CCM kama tulivyofanya 2005 na kabla yake, ni lazima arudishe fomu za kugombea pamoja na watu wengine wanaotaka kufanya hivyo, na ni lazima atetee nia yake hiyo kama alivyofanya 2005. Nje ya hapo, CCM itangaze kuwa Tanzania ni nchi ya Udikteta wa chama cha Mapinduzi!

nadhani hapa tutakuwa tunatafutana ugomvi kwa kweli.
 
Wanachoogopa ni kuwa wameshahisi kuwa atakaye mpinga muungwana atakuwa yuko kinyume na wao...wanajua wataumbuliwa na kuachwa uchi na hawako tayari kwa hilo!
 
Katiba wameiandika wenyewe leo wanaanza kuipinga tena kwa vitisho.
Nashangaa wasiwasi wao unatoka wapi wakati walituambia kwamba kikwete ni mtu wa watu,ana mvuto,anakubalika na anaiongoza vizuri Tanzania.Hili si ndiyo lingewatoa wasiwasi hawa wazee kuwa hata akija mwana ccm mwingine hata wa type ya SAS hana ubavu wa kumshinda Kikwete?
 
"Kama kuna mtu huyo ndani ya CCM basi ina maana ya kuwa mwaka 2005 Watanzania walifanya makosa kumchagua Kikwete. Kwa sababu kama kuna mtu ambaye anaweza kumshinda Kikwete leo hii ina maana mtu huyo tulikuwa naye 2005 na hatukumpa nafasi!"
Mkuu, mie umenigusa sana tu pia. Lakini hayo maneno hapo juu yamenisisimua zaidi! Mbarikiwe vichwa kama ninyi, taifa linawahitaji mno....Kazi ndio inaanza>
 
Mwanakijiji,

..kwasababu tulimchagua Kikwete wakati akiwa hana rekodi, basi bila shaka tulifanya makosa.

..sasa Kikwete ana rekodi mbaya ya kiutendaji, wananchi tusirudie makosa kumchagua.
 
"Kama kuna mtu huyo ndani ya CCM basi ina maana ya kuwa mwaka 2005 Watanzania walifanya makosa kumchagua Kikwete. Kwa sababu kama kuna mtu ambaye anaweza kumshinda Kikwete leo hii ina maana mtu huyo tulikuwa naye 2005 na hatukumpa nafasi!"
Mkuu, mie umenigusa sana tu pia. Lakini hayo maneno hapo juu yamenisisimua zaidi! Mbarikiwe vichwa kama ninyi, taifa linawahitaji mno....Kazi ndio inaanza>

Kela.. na hiyo nimeirudia mara kadhaa na ukweli wake ninaanza kuona kama katika ukungu. Je yawezekana kuna mtu alikuwepo 2005 ambaye Watanzania hawakumpa nafasi na ambaye leo hii akiamua kugombea 2010 anaweza kumuangusha Kikwete?
 
Unajua wakati mwingine nikirudi kusoma nilichoandika nashangazwa na ukweli wake. Katika makala hiyo binafsi nimeguswa na kauli yangu hii:


nadhani hapa tutakuwa tunatafutana ugomvi kwa kweli.

Mzee, uzuri hata kama wanajifanya kutosikia, kauri zako zinawafikia.
 
Inawezekana tulifanya makosa! Lakini, kumbuka uchaguzi wa kikwete ulivunja ule utamaduni wa CCM wa wazee kuwa viongozi na kweli ameleta vijana katika baraza lake! Pia wanawake wameongezeka bungeni na kwenye ngazi za uwaziri! THumb up for that!

Binafsi, sikumpa kura kikwete, maana nilikuwa na hofu ya itakapoipeleka nchi hii. Sikujua rekodi zake wakati ule ila kila nilipokuwa namsikiliza akiongea yalikuwa hayaniingii kichwani zaidi aliposhidwa kushiriki kwenye mijadala ya wazi ndio nikajiambia sitampaka kura mwake ule.

Ila nilipenda kumuona kwenye televisheni na tabasamu yake murua kabisa! Ndio, utashi ni sehemu moja wapo ya siasa, ni jambo ambalo tunahitaji kulibeba hata vyama vinavyoteua wagombea wake. Ndio, kunamambo mengi tunayohitaji kuangalia, historia yake, uwezo wake wa fikira, na misimamo yake, however, it is equal important to invest on candidate presentation, as at the end of the day politics is perception my friend.

Katika hiyo perception, nadhani Mwandosya anautashi wa Uraisi kwa mtizamo wa haraka haraka! Labda tujue zaidi historia yake na itikadi yake ya maendeleo! Na katika ufisadi kasimama wapi?

Rekodi ya kikwete kwa muono wangu binafsi ni kushidwa kuingoza nchi nyakati ambazo zinahitaji kiongozi. Katika historia ya hivi karibuni nchi hii imekuwa katika fukuto la kashifa mbalimbali na kufanya wanachi kupoteza imani na serikali yao, lakini Raisi wetu kauchuna. Ni dhahiri makali ya maisha yanasababishwa na vitu vingi - ikiwemo kuporomoka kwa uchumi na soko huria, lakini kwa kiasi kikubwa yanaendelezwa na raisi wetu kushidwa kuamua wapi alitaka ama anataka iipeleke nchi hii.

Wapo watakaosema aliamua kuwekeza katika wawekezaji na kufutia nchi kwenye utalii, lakini jitihada hizo hizikuwa na uhalisia wa mahitaji muhimu ya uchumi wa wazalishaji wadowadogo wa nchi hii. Ni kweli, mwishoni mwishoni hapa ameanza kuzungumzia ushirika na wakulima, sijui ni pesa kiasi gani zimewekezwa huko!

Lakini baya kuliko yote, ambalo Kikwete amelitenda, ni wananchi kutokuwa na imani na serikali yao. Hili ni jambo zito sana kwa raisi aliyechanguliwa kwa asilimi 80, ambaye kwa opinion poll za redet umaarufu wake umeshuka. Hii kwangu siliangalie kwa kikwete kama mtu binafsi ila naona hasara kubwa ipo kwa watanzania katika kuamini kwa pamoja wapo katika nchi inayowajali na ungozi wa kikwete ungeleta mabadiliko. Vijana waliahidiwa ajira, wakulima uzalishaji bora, na miundo mbinu kibao. Tukowapi leo? angalia imani zetu zilivyoshuka chini!

Nchi inapokuwa na wananchi ambao hawaamini ungozi, hawawezi kuchangia vyema katika maendeleo ila nawao wanatafuta ni jinsi gani watajisitiri. Wengine wanabaki wamekamatwa na hofu ya wapi tunaelekea – uchungu utatushika kwa njia moja ama nyingine. Hii ni hali ya hatari kwani kwenye akili zetu pia hatufikilia jinsi gani tutajenga, zaidi ya kufikiria jinsi gani tubomoe huo ufundo uliopo. Motokeo yake hata sisi hatujengi na taifa linazidi kuyumba, sio kwa mwelekeo mbaya ila mwelekeo mpya.

Wanaotaka kuogombea wasitishiwe! Wataendelea kutishiwa kwani wenye madaraka sikuzote wanatamaa ya kuwa nayo! Nachoweza wanaotaka kugombea watutumie misuli wagombee. Hakuna mabadiliko yanayokuja kirahisi. Na hili la wagombea wa vyama hatuna madaraka nalo, maana ni wanachama tu wanawea chagua mgombea wa uraisi. Kwahiyo, nyio mliopo humo vyamani, hakikisheni mnapambana na vyombo vyenu ili sisi huku nje tuwasikie. Tuone majina yenu! Mjitokeze! Halafu wawakatalia sisi tutaitikia. Mkikaa kimya basi wote ndio tumeliwa.

Kikwete agombe ama asigombee! Vyote vya wezekana, anachohitaji ni kuinamisha kichwa kusikiliza moyo wake, pili afanye tadhimini binafsi kama anastahili kupata kipindi kingine cha uongozi! Iwapo inadhani inahitaji temu nyingine, chama kiweka grounds sawa za ushindani, akishinda chamani aje jukwaani kwa wanaanchi. Mwakani nitapiga kura, inawezekana nikampigia kikwete, iwapo ataeleza kwa kina wapi alikosea, anadhani atafanyanini tofauti na alichofanya miaka 5 iliyopita, atashughulikia vipi ufisadi. Na kwa mahitaji yangu binafsi, nitataka nijue baraza lake la mawaziri kabla sijampa kura yangu! Najua sheria haisemi hivyo, ila nadhani ni wakati muafaka tuanza kujua package anayokuja nayo raisi!

Kwa maneno mengine, uvundo unaondelea sasa hivi, si raisi peke yake, ni serikali yake kwa ujumla wake. Kama kweli kunakiongozi anayejali maslahi ya umma, tungeona moshi wa msuguano.
 
Kela.. na hiyo nimeirudia mara kadhaa na ukweli wake ninaanza kuona kama katika ukungu. Je yawezekana kuna mtu alikuwepo 2005 ambaye Watanzania hawakumpa nafasi na ambaye leo hii akiamua kugombea 2010 anaweza kumuangusha Kikwete?

Naam hilo la kuangushwa Kikwete linawezekana kabisa, ndiyo maana wale Wazee waliojipachika jina la 'Wazee wa Chama' wakaona umuhimu wa kutumia vitisho na ubabe kwa kutoa kauli ya "Atakayempinga Kikwete atakiona" maana wanajua Kikwete kazi imemshinda na hata ndani ya CCM hana mvuto mkubwa wa kuchaguliwa tena kama mgombea wa CCM 2010.
 
Kela.. na hiyo nimeirudia mara kadhaa na ukweli wake ninaanza kuona kama katika ukungu. Je yawezekana kuna mtu alikuwepo 2005 ambaye Watanzania hawakumpa nafasi na ambaye leo hii akiamua kugombea 2010 anaweza kumuangusha Kikwete?

Kuna dalili kuwa yupo mtu ameonesha dhamira ya kutaka kugombea,na inavyoonekana wanamjua kuwa ni tishio, hapoooo sasa ndipo panakuwa hapatoshi.. wanaanza kupayuka hovyo!!
 
Unajua NIni? Kikwete akisema hatogombea 2010 ndipo tutaona jinsi CCM ilivyogawanyika. Natumaini atatangaza mapema kuwa hana mpango wa kugombea tena..
 
yaani ninaposema kuwa tunatawaliwa na Sultani CCM mlifikiri nafanya utani ,hilo wafuasi wake watalisema (Hawa wanajulikana kama republican guards) ,huzima uasi wowote ndani ya himaya. Na kuutangazia umma kuwa wasibabaike bado Kiongozi wao ataendelea kuwepo madarakani ,dawa ya yote haya ni kutangazwa mgogoro wa Katiba tu ,hakuna kingine kitachoweka sawa jinamizi hili lililoinamia Tanzania ,huu mgogoro ni lazima wapinzani wauvalie njuga kikwelikweli na maandamano ya kila kona ya Tanzania hii yafanyike kushinikiza mabadiliko na ikibidi Katiba Mpya ya Tanzania ,hii katiba ya Chama kimoja iondolewe kabisa haifai haifai hi fi ,makelele tutapiga mengi lakini wao hata hayawashughulishi maana wanafaidika nayo,sasa kumuondoa kwenye tonge hakutapatikana na kubakia na Katiba hii ambayo inawalinda Sultani CCM na wafuasi wake.
 
Unajua NIni? Kikwete akisema hatogombea 2010 ndipo tutaona jinsi CCM ilivyogawanyika. Natumaini atatangaza mapema kuwa hana mpango wa kugombea tena..

Sijui habari za undani! lakini kutogombea litakuwa ni jambo la busara kwakwe! Kama hajui sababu za kutokugombea nimkumbushe tu ataweka historia ambayo uvundo wote wa miaka mitano utasahaulika. CCM kusambaratika itakuwa ni njia mojawapo ya kukuwa kwa demokrasia, kunyongonyeza mizizi ya ufisadi, kuavunja historia ya tamaduni zisizo na tija, lakini cha ziada ccm yenyewe itakuwa.

Kama kunamiracles, but let it be this one for the better of our nation.
 
Lakini wandungu,Tanzania si kuna mfumo wa vyama vingi vya siasa??Sasa kama JK 'kashindwa' kuwa na vision ktk uongozi wake na still akapendekezwa na chama chake kugombea tena 2010 si ndio itakuwa fursa nzuri kwa wapinzani kushinda?Sasa haya ya kusema asigombee ni kama mnakuwa mnamuogopa tu.Yan timu pinzani waingize kikosi kibovu uwanjani then kuna cha kulalamika hapo.Mi naona ndo pa kutake advantage na kuwabwaga chini.
 
Lakini wandungu,Tanzania si kuna mfumo wa vyama vingi vya siasa??Sasa kama JK 'kashindwa' kuwa na vision ktk uongozi wake na still akapendekezwa na chama chake kugombea tena 2010 si ndio itakuwa fursa nzuri kwa wapinzani kushinda?Sasa haya ya kusema asigombee ni kama mnakuwa mnamuogopa tu.Yan timu pinzani waingize kikosi kibovu uwanjani then kuna cha kulalamika hapo.Mi naona ndo pa kutake advantage na kuwabwaga chini.

swala je wapinzani wanamgombea? watajipanga vipi? lengo lao ni kushinda CCM ama kila chama kushinda kivyake!
 
Inawezekana tulifanya makosa! Lakini, kumbuka uchaguzi wa kikwete ulivunja ule utamaduni wa CCM wa wazee kuwa viongozi na kweli ameleta vijana katika baraza lake! Pia wanawake wameongezeka bungeni na kwenye ngazi za uwaziri! THumb up for that!

Mkuu kuongezeka kwa vijana na wanawake bila ya kuongezeka kwa ufanisi ni nini manufaa yake?
 
Mkuu kuongezeka kwa vijana na wanawake bila ya kuongezeka kwa ufanisi ni nini manufaa yake?

Maana yake ni tata, tena tete! ndio maana nasema atahitaji kutoa maelezo inakuwaje nguvu mpya lakini kasi impya haipo. Kwahilo siwezi kumsemea ila nachoweza kusema, hata waje vijana wote kama uongozi hauna dira ya maslahi ya wengi mchezo utakuwa ulele. Hata kama Nchi itaongozwa na kinamama asilimi 80 uvundo wa ubinafsi utashika hatamu kama dira ya uongozi haiweki taifa mbele.

Kwahiyo, swali lako ni la msingi, iwaje vijana wameongezeka na kinamama lakini ufanisi duni? By the way, huo ufanisi duni umeupimaje pimaje? Nachojua ufisadi umeanza kuanikwa hadharini!
 
Back
Top Bottom