Niccolo Machiavelli na kitabu chake The Prince (Of principality). Kwa kiswahili; kuhusu Uongozi. Tusome na kujadili

Red Giant

JF-Expert Member
Mar 9, 2012
15,658
20,883
KIONGOZI (nimeonelea ndiyo iwe title)

Sasa kitabu hiki kinapatikana ndani ya maktaba app (by pictuss). Inapatikana playstore.

1626826564380.png

Kimeandikwa na: Niccolo Machiaveli, 1513.
Kimetafsiriwa na: Pictuss, 2021.

Email: Pictuspublishers@gmail.com.

©Pictuss2021

Haki zote zimehifadhiwa. Hakuna sehemu yoyote ya tafsiri hii inayoweza kunakiliwa, kutolewa kivuli(photocopy), kuhamishwa, kurekodiwa au kutolewa kwa namna yoyote ile bila ya taarifa ya awali ya kimaandishi kutoka kwa mmiliki.

Kwa mtukufu Lorenzo Di Piero De' Medici

Ni desturi kwa wale wanaotaka kujipendekeza kwa viongozi kumpatia zawadi ya vitu wanavyovithamini sana. Wanaamini kuwa naye atavithamini. Hivyo tumekuwa tukitumia farasi, mavazi ya vita, nguo za dhahabu, vito na zawadi nyingine za gharama zinazostahili kupewa viongozi.

Kwa kufuata desturi hiyo, nimekuja mbele zako kutoa zawadi. Lakini katika mali zangu sijaona kitu cha thamani kama ujuzi wa matendo ya watu hodari. Maarifa niliyoyapata kwa uzoefu wangu juu ya mambo ya sasa, na kwa kusoma historia ya kale. Maarifa ambayo nimeyachunguza na kuyachuja, na kisha kuzalisha kitabu hiki kidogo. Nakutumia kitabu hicho ewe mtukufu, japo naona kazi hii hailingani na utukufu wako. Lakini natarajia rehema zako zitakufanya ukipokee, hasa ukizingatia kuwa nakupatia njia ya kuelewa kwa muda mfupi yale niliyo jifunza kwa muda wa miaka mingi, chini taabu na hatari.

Kazi hii sijaipamba kwa lugha nzuri na madoido mengine kama ilivyo desturi ya waandishi wengi. Ni bora nisijipatie sifa lakini ukweli wa mambo wa suala hili uwe wazi.

Ni sidhani kama nitakuwa najikweza kwa mtu wa chini kama mimi, kuanza kuzungumza habari za namna ya utawala. Sababu ni kuwa; wale wanaochora ramani ya nchi hukaa mabondeni ili kupata ramani ya milima, na hukaa juu milimani ili kupata muonekano mzuri wa mabonde. Kwa namna hiyohiyo, ili mtu awajue watu vizuri, anapaswa kuwa kiongozi, na ili kuwajua viongozi vizuri, anapaswa kuwa mtu wa kawaida.

Hivyo basi, nakuomba ewe mtukufu upokee zawadi hii ndogo ninayoitoa kwa nia njema. Kama ukikisoma kwa bidii utagundua nia yangu ya kutaka ufikie ukuu unaostahili uwezo na fursa ulizonazo. Na iwapo katika kilele cha ukuu wakoutaangalia pande hizi za chini, utaelewa ni jinsi gani, sikustahili lakini nilivumilia ukatili usiokoma wa bahati mbaya.

SURA YA 1

KUHUSU AINA MBALIMBALI YA UTAWALA NA JINSI ZINAVYOSIMAMA

Kuna aina mbili tu ya Serikali ambazo watu wametawaliwa nazo na wanaendelea kutawaliwa. Serikali za kifalme au jamuhuri. Ufalme unaweza kuwa wa kurithi kutokana na uhusiano wa damu na wafalme waliopita au unaweza kuwa ni ufalme mpya kabisa. Ufalme mpya, unaweza kuwa mpya kabisa kama ule wa Milan chini ya Francesco Sforza, au unaweza kuwa ni muendelezo wa mfalme aliyeteka kama ulivyokuwa ufalme wa Napoli chini ya wafalme wa Hispania.

Nchi iliyotekwa inaweza kuwa ilikuwa chini ya mfalme au ilikuwa huru bila mfalme. Anayeteka nchi anaweza fanya hivyo kwa nguvu zake mwenyewe au kwa kutumia nguvu za wengine. Kwa bahati njema au kwa uwezo wake.

SURA YA 2

UFALME WA KURITHI

Sitaongelea kuhusu jamhuri, kwa sababu jambo hilo nimeshaliongelea kwa kirefu sehemu nyingine. Mimi nitaongelea tawala za kifalme tu. Nitaongelea jinsi ya kuongoza tawala za kifalme.

Ufalme unaotokana na kurithi ni rahisi kuongoza kuliko ufalme mpya, kwa sababu wananchi wanakuwa wameizoea familia ya kifalme. Kinachotakiwa ni kiongozi mpya kutokengeuka kutoka katika njia za watangulizi mababu zake.

Kwa hiyo, hata kama kiongozi ana uwezo wa kawaida hatapata taabu kuongoza labda akutane na magumu ambayo ni ngumu kuyashinda. Na hata ikitokea kang'olewa madarakani kwa uasi, ni rahisi kwake kurudi mara tu mambo yanapowaendea vibaya waasi/wahaini hao.

Katika Italia tuna mfano mzuri wa jambo hili kutoka kwa Duke wa Ferrara. Duke huyu asingeweza kuhimili mashambulizi ya wavenice ya mwaka 1484, wala yale ya Papa Julius wa II ya mwaka 1510 Iwapo mamlaka yake isingekuwa imara. Isipokuwa amefanya matendo mabaya kupita kiasi; kiongozi anayetokana na kurithi ana mambo machahe yanayoweza kumfanya kuwa chukizo, na maudhi kwa watu wake. Na zaidi ni kuwa, muendelezo wa utawala wake ambao upo tokea enzi za mababu zake, utafanya watu kutojali sana mabadiliko yoyote yanayoweza kutokea. Na mara zote badiliko moja huzaa nafasi kwaajili ya jingine.
 
SURA YA TATU

KUHUSU UTAWALA MCHANGANYIKO

Katika utawala mpya ni rahisi matatizo kutokea. Na kama utawala huo siyo mpya kabisa, bali umeungana na ule wa kale, hutengeneza kitu kinachoitwa utawala mchanganyiko. Huu hauwi mpya kabisa, Lakini mabadiliko lazima yatatokea kama yatokeavyo kwa falme zote mpya. Watu wanaotaka kuboresha maisha yao, mara zote wako tayari kubadili mtawala kwa matarajio ya maisha bora, watabeba silaha na kuasi dhidi ya kiongozi yeyote. Lakini hili huwa ni kujidanganya tu, na uzoefu unaonyesha kuwa huwa wanajikuta katika hali mbaya kuliko hapo kabla. Hili linatokana na hali ya asili, nayo ni kuwa; kiongozi mpya hawezi epuka kuwakwaza raia wake.

Na kwa upande wa jeshi, anaweza kuwa hajatimiza mahitaji ya wanajeshi wake, au maudhi mengine anayoweza kuwa aliyatenda wakati anaposimamisha utawala mpya. Hapo atajikuta kajenga maadui kati ya wote wale aliowaumiza wakati wa kuangusha utawala wa zamani, lakini pia hataweza kudumisha urafiki na wale waliomsaidia kuingia madarakani. Sababu ni kuwa, hataweza kuwapa mafanikio walivyotarajia. Na kwa sababu wao ndiyo wamemsaidia kupata madaraka, hataweza kutumia nguvu dhidi yao, anakuwa kama mtu mwenye deni kwao. Zaidi ni kuwa, hata kama una jeshi lenye nguvu kiasi gani, unapoingia kutawala eneo jipya, yakupasa kuhakikisha unauungeaji mkubwa wa wakaazi wake.

Ilitokea kwa mfalme Louis XII wa ufaransa. Aliiteka Milan kwa haraka lakini aliipoteza kwa haraka pia. Mara ya kwanza alipoiteka, Lodovico Sforza aliweza kumyang'anya akiwa na jeshi lake tu. Watu walewale waliomfungulia mlango mfalme wa Ufaransa kuingia Milan, ndiyo waliomuasi baada ya kuona matarajio yao hayatimizwi kama walivyotarajia. Hawakuweza kuvumilia dharau na kujikweza kwa mtawala wao mpya. Na ukweli ni kwamba, nchi ikiasi na uasi huo ukazimwa ni vigumu sana kuasi tena na kufanikiwa. Sababu ni kuwa mtawala atatumia uasi huo kama sababu na kisingizio.

Na kwa kisingizio hicho hata sita kujilinda kwa kuwaadhibu vikali wale wanaompinga. Atawahukumu washukiwa na hivyo kujiimarisha kwenye maeneo ambayo alikuwa dhaifu. Kama kitendo cha Duke Lodovico kuikomboa Milan kutoka kwa wafaransa kwa mara ya kwanza kingekuwa kimefanikiwa kuwaamsha wengine kumpinga, basi kwenye uvamizi wake wa mara ya pili wote wangeungana kupambana na mfalme wa Ufaransa. Na jeshi lake lingefurushwa kutoka Italia. Kama nilivyokwisha onyesha, si rahisi kuteka kwa mara ya pili.

Lakini haikuwa hivyo, Milan ilitekwa tena na Mfalme wa Ufaransa. Kushindwa kwa Milan kwa mara ya kwanza sababu zake zimekwisha onyeshwa. Yatupasa kuonyesha sababu za kushindwa kwa mara ya pili, na jinsi mfalme wa Ufaransa alivyobadili mbinu. Mbinu hizo zinaweza kutumiwa na mtawala mwingine yeyote akijikuta katika hali kama hiyo, mbinu zitakazomfanya kudhibiti maeneo aliyoyateka pengine kuliko hata mfalme wa Ufaransa alivyodhibiti.

Niseme kuwa; maeneo mapya ya utawala, yanaweza kuwa ni maeneo yanayoongea lugha na yana utamaduni sawa na ule wa wanaowatawala, au wanaweza kuwa na lugha na tamaduni tofauti kabisa. Kama wanafanana lugha na utamaduni ni rahisi kuwatawala, hasa kama hapo kabla waliishi chini ya utawala wa mabavu na bila uhuru. Kitendo cha kuwaongoza vizuri kitakuwa kimetosha kukomesha utawala uliopita na masalia yake. Kwa sababu, kama wakiendelea kuishi kwa utaratibu wao waliozoea, na utamaduni wao usipovurugwa, binadamu huishi kwa amani. Kama tu tunavyoona kwa Brittany, Burgundy, Gascony na Normandy ambazo kwa muda mrefu zimeweza kuunganishwa na Ufaransa. Japo kunatofauti kidogo kwenye lugha zao, lakini utamaduni wao ni mmoja na wanaweza kuishi pamoja kwa urahisi.

Hivyo basi, kwa yeyote anayeteka nchi kama hiyo, na anataka kuendelea kuikalia anatakiwa kuzingatia mambo mawili: kwanza anatakiwa kuangamiza utawala uliopita na warithi wake. Pili, hatakiwi kufanya mabadiliko yeyote kwenye sheria zao na kodi. Kwa njia hii, nchi mpya itaingizwa na kuungana na ile nchi mama kwa urahisi.

Lakini iwapo nchi iliyotekwa ina lugha, tabia na sheria tofauti. Magumu mengi yatatokea, na jitihada nyingi zitahitajika ili kuitawala. Njia nzuri ya kuitawala nchi ya namna hiyo ni kwa mtawala kwenda yeye mwenyewe kuishi katika nchi hiyo. Hili litafanya utawala wake kuwa thabiti. Njia hii ilifanywa na Turk huko Ugiriki. Pamoja na mambo mengine, yeye mwenyewe alikwenda kuishi kwenye mkoa huo. Ukiwa karibu ni rahisi kugundua machafuko mapema yanavyoanza na kuyazima haraka, lakini ukiwa mbali utayagundua kwa kuchelewa wakati tayari yana nguvu na hayawezi kuzimwa tena. Zaidi ya hayo, mkoa unaoishi, maafisa wako hawataweza kutapanya mali zake, na watu watafurahi kupata nafasi ya kumfikia mtawala wao kwa urahisi. Jambo hilo litawafanya wampende mtawala wao kama wanaridhishwa na uongozi wake, au wamuogope kama hawaridhishwi nao.

Hata adui kutoka nje atafikiria mara mbili kabla ya kuvamia eneo kama hilo. Kifupi ni kuwa, ni vigumu sana kumng'oa mtawala kutoka kwenye eneo analoishi.

Njia nyingine nzuri ni kupeleka raia wako kuwa wakoloni kwenye eneo hilo. Unaweza fanya hivi au ukaweka jeshi kubwa kwenye eneo hilo. Lakini mtawala hatakiwi kutumia pesa nyingi kuhudumia makoloni. Anaweza weka wakoloni na kuwapa msaada kidogo bila kuathiri hazina yake.

kwa kufanya hivyo, watu pekee atakaokuwa amewaudhi ni wale wakazi wa asili aliowapora ardhi kwaajili ya makazi ya wakoloni. Hata hivyo watu hao watakuwa ni sehemu ndogo tu ya wakazi wote, na kwa sababu ni maskini na wametawanyika huku na kule, hawatakuwa kitisho kwa utawala wake. Kwa hiyo, wengine wote usiowaudhi wataishi kwa utulivu, na wakati huohuo wataogopa kukuasi wasije patwa na kilichowapata wale walioporwa ardhi na mali.

Kwa maneno machache niseme kuwa, kuendesha makoloni kuna gharama ndogo kuliko kuweka wanajeshi wengi. Makoloni ni matiifu na wala hayawezi kukusumbua, sababu kama nilivyokwisha sema, wale walioporwa ardhi(wanaoweza leta vurugu) ni maskini na wametawanyika hivyo hawawezi kukusumbua.

Na acha ifahamike vyema kuwa, watu wanatakiwa kutendewa kwa wema au kukandamizwa kwa mkono wa chuma. S ababu ni kuwa watu wanaweza kulipa kisasi iwapo wakidhuriwa kidogo, lakini hawawezi iwapo madhara waliyopata ni makubwa kupita kiasi. Basi, tukitaka kutendea watu ubaya, ubaya huo unapaswa kuwa mkubwa kiasi kwamba tusiwe na sababu ya kuogopa ulipaji wa kisasi.

Lakini badala ya kupeleka wakoloni wewe ukatuma jeshi kushikilia nchi hizo, gharama zake zitakuwa kubwa sana. Mapato yote ya eneo hilo yatatumika katika kulilinda, utachopata humo utakipoteza humohumo. Zaidi ni kuwa, wanachi wa eneo hilo watachukia sababu ya uwepo wa wanajeshi wako. Nao watakuwa adui zako, na adui akiwa nyumbani kwako ni rahisi kukudhuru. Kwa hiyo, kutuma wanajeshi kushikilia nchi nyingine ni jambo lisilo na faida, lakini kufanya nchi hizo makoloni ni jambo lenye manufaa.

Kiongozi ambaye anaenda kutawala nchi/mkoa ambao sheria na lugha yake ni tofauti na ya kwake, anatakiwa kujiweka kama mlinzi wa jirani zake walio dhaifu, na ahakikishe anazidhooifisha nchi zilizo na nguvu. Pia anatakiwa kuhakikisha kuwa hakuna utawala mwingine wenye nguvu kama yeye unapata nafasi kwenye eneo hilo. Sababu ni kuwa, mara zote ufalme wenye nguvu utaitwa ili kuwaisaidia watu wasioridhika, pengine sababu ya maslahi yao, au kwa sababu wanakuogopa.

Kama tunavyoona yaliyotokea hapo kale. Waroma waliitwa kwenda Ugiriki na waaetolia, na mikoa mingine yote waliyoingia walikuwa wameitwa na wakaazi wake. Na kitu kimoja kilekile kilitokea mara zote; mgeni mwenye nguvu anapotokea wale walio dhaifu huungana naye dhidi ya yule aliyekuwa akiwatawala, wakichochewa na chuki waliyoijenga dhidi yake. Kwa hiyo, hakuna nguvu inayohitajika ili kuteka mikoa dhaifu, hujileta yenyewe kwa hiyari kwa mgeni mwenye nguvu. Mtawala anapaswa tu kuwa macho ili wasije wakapata nguvu kupita kiasi. Na kwa kuwatumia akiwa pamoja na jeshi lake, anaweza kumdibiti yeyote aliye na nguvu kwenye eneo hilo, na hivyo yeye pekee kubaki mwenye nguvu katika eneo hilo. Mtu asipolifanya jambo hili kwa weledi anaweza kujikuta akipoteza maeneo aliyoteka, na hata akiyashikilia atajikuta kwenye matatizo na vurugu zisizokwisha.

Waroma walifuata kikamilifu njia nilizozieleza walipokuwa wanatawala nchi walizoziteka. Walizifanya kuwa makoloni na kupeleka watu kuwa wakoloni.

Waliua upinzani, hawakuimarisha falme dhaifu, Walizidhoofisha falme zenye nguvu, na wala hawakuruhusu taifa lolote lijipatie nguvu na ushawishi. Mfano mmoja unatosha kuonyesha jinsi walivyofanya hivyo. Huko Ugiriki, waroma waliwachukua Waaetolia na waachai chini yao, waliudhoofisha ufalme wa Makedonia; Antiochus alifukuzwa. Na japo waliwachukuwa Waaetolia na Waachai, lakini hawakuwaimarisha. Wala ushawishi wa mfalme Philip haukufanya waroma wawe rafiki zake, wala nguvu za Antiochus hazikuwafanya wamruhusu kuwa na mamlaka fulani kwenye mkoa wa Ugiriki. Kwa kufanya hivyo, waroma walifanya kama watawala wenye busara na hekima wanavyopaswa kufanya. Hawakuangalia tu matatizo ya sasa bali pia ya baadaye na walifanya bidii kuyazuia.

Walijua kuwa wakifikiria matatizo ya wakati ujao, wataweza kuyapatia tiba kidogo na yakaisha, lakini wakiyaacha yawe makubwa, yatakuwa makubwa yasiyosikia tiba.

Walikumbuka kile ambacho madaktari hutuambia kuhusu magonjwa. Wanasema kuwa ugonjwa unapoanza ni rahisi kuutibu lakini si rahisi kuugundua. Lakini kadri unavyokua, inakuwa ni rahisi kuugundua lakini ni vigumu kuutibu.

Hata mambo yahusuyo nchi yapo namna hiyo, Wanaovuruga nchi wakigunduliwa mapema wangali hawajapata nguvu, wanaweza kudhibitiwa kwa urahisi. Hilo linawezekana tu iwapo kiongozi ni mtu mwenye weledi wa kutosha. Lakini iwapo hawajagunduliwa na wameachwa kukua mpaka wanaonekana waziwazi, kutakuwa hakuna tiba dhidi yao.

Kwa hiyo, waroma kwa kuona matatizo ambayo bado hayajatokea waziwazi, waliweza kuyatatua. Hawakuyavumilia kukua kisa tu kuepuka vita.

Walitambua kuwa vita si kitu cha kuepuka. Kuepuka vita ni kuihairisha tu, na kitendo hicho kitampa faida adui yako.

Hivyo basi, waroma walichagua kupigana vita na Philip na Antiochus katika Ugiriki ili wasije kupigana nao ndani ya Italia, japo wangeweza kutulia na kuepuka vyote kwa muda. Hawakutaka kitu kama hicho, na wala hawakutegemea tatizo liishe lenyewe; kitu ambacho watu wenye hekima wa wakati wetu wanakitegemea sana, kwamba muda utafanya mambo yatulie.

Waroma walitegemea ushujaa, na hekima yao ya kufikiria mambo yajayo kuwaletea mafanikio. Hawakutegemea muda, walijua muda huja na mazuri na mabaya vilevile.

Sasa tuichunguze Ufaransa na tuone kama walifuata zile njia nilizozieleza. Nitamzungumzia Louis na si Charles. Kwa sababu Louis alitawala Italia kwa muda mrefu, tunaweza kuona vizuri jinsi alivyotawala. Utaona kuwa alifanya kinyume kabisa na alivyopaswa kufanya ili kuweza kuitawala nchi ya kigeni. Mfalme Louis aliletwa Italia na watu wa Venice ambao walitegemea kuwa watapata nusu ya jimbo la Lombardy. Siwalaumu kwa hili, wala uamuzi wa kukubali uliochukuliwa na mfalme. Louis alikuwa anatamani kuikalia Italia, nchi ambayo hakuwa na mshirika bali, kutokana na matendo ya Charles, kila mtu aliwachukia wafaransa. Hivyo Louis alikuwa tayari kukubali mualiko wowote wa urafiki. Na kama siyo makosa yake mengine, mpango wake ungefanikiwa.

Baada ya kuirudisha Lombardy chini ya Ufaransa, Louis alijipatia heshima ambayo Charles alikuwa ameipoteza. Genoa ikasalimu amri na waflorentina, Marquis wa Mantua, Duke wa Ferrara, wa-Bentivogli, Mkuu wa Forli, Makabaila wa Faenza, Pesaro, Rimini, Camerino na Piombino, na wakazi wa Lucca, Pisa na Siena, wote walikuja na kuomba urafiki naye. Kwa wavenice kumkaribisha mfalme wa Ufaransa ili wajipatie miji michache ya Lombardy, wakawa wamemfanya kuwa mtawala wa theluthi mbili ya Italia. Sasa wakawa na sababu ya kujutia hila yao mbaya.

Hebu jionee jinsi ambavyo ingekuwa rahisi kwa mfalme Louis kuitawala Italia kama angefuata kanuni nilizozianisha hapo juu. Kama angewalinda na kuwahakikishia usalama rafiki zake ambao sababu ya uoga na kuwa dhaifu, na wengine kwa kuliogopa kanisa, na wengine kwa kuwaogopa wavenice, wangelazimika kushikamana naye. Na kwa msaada wao, maana walikuwa ni wengi, angeweza kujiweka salama dhidi ya yeyote mwenye nguvu.

Lakini mara tu alipofika Milan, akafanya mambo tofauti kabisa kwa kumsaidia Papa Alexander kuiteka Romagna; hakuelewa kuwa kwa kuunga mkono suala hili, alikuwa akijidhoofisha kwa kujitenga na rafiki zake ambao walikuwa wamejiweka karibu naye. Na wakati huohuo pia alikuwa akiimarisha nguvu za kanisa kwa kulipa nguvu za kisiasa. Na kosa hili la kwanza lilimlazimisha kuendelea nalo. Na mwishowe, ili kudhibiti mpango wa Papa Alexander kuwa mtawala wa Tuscany, yeye mwenyewe alilazimika kuja Italia.

Kama vile haikutosha kuliongezea kanisa nguvu, na kupoteza rafiki zake, akatamani pia kumiliki ufalme wa Napoli na kuutenga na ufalme wa Hispania. Hili likamfanya kumkaribisha mpinzani mwenye nguvu Italia wakati yeye ndiye alikuwa mtawala pekee mwenye nguvu. Mpinzani ambaye watu wasioridhika na wenye uchu walikuwa na sababu ya kumuomba msaada dhidi yake. Na badala ya kumuacha mfalme wa Napoli ambaye angeridhia kutawala chini yake, yeye akamuondoa na kumuweka mwingine mwenye nguvu za kutosha kufanya afurushwe.

Tamaa ya kumiliki vitu ni ya asili kwa binadamu na ni kitu cha kawaida. Watu wanapojaribu kupata vitu vilivyo ndani ya uwezo wao watasifiwa siku zote na si kulaumiwa. Lakini wakiwa wanang'ang'ania kupata vitu vilivyo nje ya uwezo wao, lawama na matatizo hutokea. Kama Ufaransa ingeweza kuvamia Napoli kwa kutumia jeshi lake pekee ingepaswa kufanya hivyo, na kama haikuweza haikupaswa kuigawa. Na kama ikisemwa kuwa, kuigawa Lombardy kati yake na wavenice ndiko kulimfanya kuingia Italia, basi huku kuigawa Napoli kunapaswa kushutumiwa sababu hakukuwa na ulazima wowote.

Kwa hiyo, Louis alifanya makosa matano yafuatayo. Aliziangamiza tawala dhaifu, alimuimarisha mtawala aliyekuwa na nguvu tayari, alimkaribisha kwenye nchi mtawala mwenye nguvu, hakwenda kuishi kwenye nchi aliyoiteka na hakuanzisha makoloni. Lakini makosa yote hayo yasingemletea matatizo makubwa katika kipindi chake. Lakini yeye akaongeza kosa lingine la sita, aliwanyang'anya wavenice utawala wao. Kama ingekuwa hajawaleta wahispania wala kulipa kanisa nguvu, angekuwa na sababu ya msingi ya kuidhoofisha Venice. Lakini baada ya kufanya yote hayo, hakutakiwa kamwe kuruhusu uvamizi wa Venice.

Kwa sababu wavenice walikuwa na nguvu, siku zote wangemsaidia kwa kuzuia wengine kuvamia Lombardy. Wala wasingeingia kwenye makubaliano ya kumkaribisha mwingine ambaye hatawafanya kuwa watawala wa Lombardy. Na mtu mwingine yeyote asingekubali kuwatoa wafaransa Lombardy na kuikabidhi kwa wavenice.

Na kama ikisemwa kuwa Louis alimpa Papa, Romagna, na akawapa wahispania, Napoli ili kuepuka vita, nitajibu kwa sababu niliyokwisha itoa. Hutakiwi kuvumilia kuingiliwa kwenye mambo yako kwa sababu tu ya kuepuka vita. Vita si jambo la kuepukwa bali inaweza kuahirishwa tu, na hili litakupa hasara. Na iwapo wengine watasema kuwa mfalme alikuwa akifanya yale kwa niaba ya Papa, ili Papa abatilishe ndoa yake na kumfanya D'Amboise apate ukardinali. Nitajibu kwa kurejea nitayosema huko mbele kuhusiana na jinsi imani ya mfalme inavyopaswa kuwa.

Kwa hiyo, mfalme Louis aliipoteza Lombardy. Si kwa sababu nyingine bali kwa kutofuata njia ambayo wale wanaoteka maeneo na kudhamiria kuyatawala hufuata. Hili si jambo la ajabu au geni bali ni la kawaida na linapaswa kuwekwa akilini. Kuhusiana na hili suala, niliongea na D'Amboise huko Nantes, wakati ambao Duke Velantino(kama alivyoitwa kwa dhihaka Cesare Borgia, mwana haramu wa Papa Alexander) alipokuwa akiitawala Romagna.

Kardinali aliponiambia kuwa waitaliano hawafahamu masuala ya vita, mimi nilimjibu kwa kumwambia kuwa wafaransa hawaelewi jinsi ya kutawala, kama wangekuwa wanafahamu wasingeruhusu kanisa kupata nguvu nyingi kiasi kile. Matukio yanaonyesha kuwa, kuongezeka kwa nguvu ya kanisa na kuletwa kwa wahispania katika Italia, kulisababishwa na wafaransa. Na kuanguka kwa Ufaransa kulitokana nao. Kwa hiyo basi, tukija kwenye ukweli ulio wazi siku zote, ukweli ambao haujawahi kukosea; yule anayesababisha mwenzake kuwa na nguvu anajimaliza mwenyewe. Sababu ni kuwa itamfanya afanye naye kazi kwa makubaliano au kwa kutumia nguvu, na mambo hayo huleta kutoaminiana kwa watu wenye nguvu.
 
Sura ya tatu ni nzuri sana na moja ya sura ndefu. Nimependa haya.

1. Anasema vita haiwezi kuepukwa bali unaweza kuihairisha tu, na hilo litampa faida adui.
2. Anasema yeyote anayemuimarisha na kumpa nguvu mwenzake anajimaliza mwenyewe.
3. Nafikiri mataifa ya Ulaya yalifuata vizuri ushauri wake wa kuanzisha makoloni.
4. Kwamba ukimdhuru mtu kidogo anaweza lipa kisasi. Hivyo ukitaka kumdhuru mtu, mdhuru vilivyo ili usiogope ulipaji kisasi.
5. Anasema watu wanaotaka mabadiliko kwa nia ya kuboresha maisha yao huishia kuwa dissapointed. Mara nyingi hujikuta katika hali mbaya kuliko hapo mwanzo.
 
SURA YA 4

KWANINI HIMAYA YA DARIO ILIYOANGUSHWA NA ALEXANDER HAIKUASI DHIDI YA WARITHI WAKE BAADA YA KIFO CHAKE?

Baada ya Alexander mkuu kuiteka Asia ndani ya miaka michache. Alikufa hata kabla utawala wake haujasimama imara. Kulingana na ugumu wa kuongoza nchi mpya, tulitarajia kwamba baada ya kifo chake himaya yote ingeasi, lakini warithi wake waliweza kudumisha utulivu. Hawakupata ugumu wowote zaidi ya uliosababishwa na kuoneana wivu wao kwa wao.

Ikiwa unaona hili suala si la kawaida na unajiuliza kwanini lilikuwa hivyo? Najibu kama ifuatavyo. Tawala zote tuzijuazo zinatawaliwa kwa moja kati ya njia mbili tu. Inaweza kutawaliwa na mfalme mmoja na wengine kuwa wasaidizi wake tu. Hawa hupangiwa kazi na mfalme na husimamia kama mawaziri. Njia nyingine ni utawala wa mfalme na machifu. Machifu hawa huwa na mamlaka yao na hawategemei kuteuliwa na mfalme bali huwa machifu kwa kurithi. Hawa wana eneo lao la utawala na wana watu wanaowatambua kuwa ni watawala.

Nchi inayoongozwa na mfalme peke yake akisaidiwa na mawaziri, inamfanya mfalme kuwa na mamlaka yote. Katika nchi yote, yeye ndiye anatambulika kama kiongozi. Wasaidizi wake wanakuwa na mamlaka fulani juu ya wananchi, lakini kunakosekana ile heshima anayopewa mfalme.

Kwa mifumo hii miwili ya serikali, tuna mifano leo ya serikali ya Uturuki, na mfalme wa Ufaransa. Ufalme wote wa Uturuki unatawaliwa na mfalme mmoja, wengine wote ni vijakazi wake. Amegawa ufalme wake kwenye mikoa. Huko ameweka magavana ambao huwahamisha na kuwabadilisha kadri apendavyo. Kwa upande mwingine, mfalme wa Ufaransa amezungukwa na machifu. Kila chifu ametokana na kurithi na anapendwa na kuheshimiwa na watu wake. Kila mtu ana mamlaka kwenye eneo lake na mfalme hawezi kumtoa, labda kama anataka matatizo.

Kwa kuangalia aina hizi mbili za utawala, mtu ataona kwamba ni vigumu kuangusha utawala wa Uturuki lakini ukiuangusha ni rahisi kuutawala. Kikwazo ni kuwa wavamizi hawawezi kupata msaada wa machifu wala hawawezi kupata msaada wa maana kutoka kwa maofisa wa mfalme. Wote wakiwa ni vijakazi wa mfalme hawawezi kushawishika kirahisi. Na iwapo watashawishika, hawatsweza kutoa msaada wowote wa maana, kama nilivyokwisha eleza, maofisa hawa hawana watu wanaowafuata. Kwa hiyo, yeyote anayefikiria kuivamia Uturuki, ategemee kukuta watu wenye umoja.

Anatakiwa ategemee nguvu zake na si kutegemea adui kugawanyika. Lakini ikitokea amemshinda adui yake, anakuwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi. Kinachoweza kumsumbua ni familia ya mfalme tu. Iwapo ataweza kuiangamiza, atakuwa hana cha kuogopa. Hii ni kwa sababu, wengine wote hawatambuliwi na watu kama wana haki ya kutawala. Kwa hiyo, kama ambavyo hakutegemea msaada wa maana kutoka kwao, pia hategemei tishio lolote la maana kutoka kwao.

Tofauti ipo kwa ufalme unaoongozwa kama ule wa Ufaransa. Humo watu wasioridhika na wanaotamani mabadiliko lazima watapatikana. Unaweza kuanza uvamizi kwa kutumia machifu wachache. Hao, kwa sababu zilizoelezwa, watakuwa tayari kufungua milango kwaajili ya uvamizi. Hilo litafanya uvamizi wako kuwa rahisi. Lakini baada ya kuangusha ufalme huu, utakuwa na kazi kubwa sana kuwatawala wale waliokuunga mkono na wale uliowaangusha, wote watakusumbua. Haitatosha kuangamiza familia ya kifalme sababu chifu yeyote anaweza kuibuka na kuasi. Ukishindwa kuwaridhisha au kuwaangamiza, watakuangusha muda wowote wakipata nafasi.

Kwa hiyo, ukiangalia utawala wa Dario utagundua kuwa unafanana na ule wa Uturuki. Ilikuwa muhimu kwa Alexander kumuangusha kwanza Dario kutoka kwenye utawala. Baada ya Dario kufa na kwa sababu zilizoelezwa, nchi yote ikawa chini ya Alexander kwa urahisi. Hata kama warithi wa Alexander wangeendelea kutawala bila kugawana ufalme, wangetawala bila shida yeyote. Kulikuwa hamna matatizo yoyote zaidi ya waliyotengeneza wenyewe.

Lakini nchi inayotawaliwa kama Ufaransa, si rahisi kuitawala kwa urahisi hivyo. Ndiyo maana kulikuwa na uasi wa Hispania, Gaul na Ugiriki dhidi ya waroma. Uasi uliotoka kwa baadhi ya machifu wadogowadogo waliounda mikoa hiyo. Na kadri kumbukumbu za viongozi wao zilipokuwa ndani ya wananchi, waroma hawakuweza kutawala kwa amani.

Lakini kadri kumbukumbu za utawala uliopita zilipofutika, na baada ya utawala wa muda mrefu wa waroma, na waroma walipowekana wao kwa wao kuongoza, kulingana na ushawawishi wa mtu kwenye eneo husika, ndipo waliweza kutawala kwa amani. Hapo wananchi hawakutambua mtawala yeyote bali waroma. Ukiweka hayo akilini basi hutashangaa kwanini Alexander aliweza kuidhibiti Asia vilivyo. Wala Pyrrhus na wengine wengi hawakupata kazi kutawala falme walizoangusha. Hili halitokani na uwezo au udhaifu wa mvamizi bali hutokana na muundo wa falme wanazozivamia.
 
SURA YA 5

JINSI YA KUTAWALA MIJI NA MIKOA AMBAYO KABLA YA KUTEKWA ILIKUWA NA SHERIA ZAKE.

Kama nchi mpya iliyotekwa ilizoea kuishi chini ya sheria zake, kuna njia tatu za kuitawala. Njia ya kwanza ni kuiangamiza, ya pili ni kwenda na kuishi kati yao na ya tatu ni kuvumilia na kuwaacha waishi chini ya sheria zao, na kuweka wazawa wachache kuwa viongozi ambao watawadhibiti wengine, na wewe kuchukua kodi tu. Serikali ya namna hiyo, kwa sababu imewekwa na mtawala mpya, itamtegemea yeye kusimama. Hivyo itafanya kila jambo kuhakikisha anazidi kusimama. Na mji uliozoea kuishi chini ya sheria zake, ni rahisi kuutawala kupitia wazawa wa hapo kuliko kutumia njia zingine.

Tuna mifano ya njia hizi kwa kupitia historia ya wasparta na waroma. Wasparta walitawala miji ya Athens na Thebes kwa kutengeneza tabaka la matajiri lakini mwisho wake waliipoteza miji hiyo. Waroma, ili kudhibiti miji ya Capua, Carthage na Numantia waliiharibu kabisa na hawakuipoteza. Lakini walipotaka kuudhibiti mkoa wa Ugiriki, walifanya kama wasparta, waliiacha na uhuru wake, wakiiacha ijiongoze kwa kutumia sheria zake, kwa hili walishindwa. Iliwabidi kuiharibu miji mingi ya mkoa wa Ugiriki ndipo waliweza kuidhibiti. Kwa kweli, hakuna njia ya uhakika ya kuthibiti zaidi ya kuangamiza, na yeyote anayeteka mji uliozoea kuishi kwa sheria zake na hauangamizi basi ataangamizwa nao.

Sababu ni kuwa, ikitokea wameasi, basi watajitetea kuwa wanafanya hayo kulingana na taratibu na sheria zao. Hata uwafanyie nini na hata muda mrefu upite, hawawezi kuacha njia zao. Hawawezi kusahau sheria na taratibu zao za kuendesha mambo, wala hawawezi kuacha kutamani maisha yalivyokuwa kabla hawajatekwa. Isipokuwa umeharibu mji na kutawanya wakazi wake huku na huko, siku zote watatamani mambo yalivyokuwa. Wakipata nafasi watatumia tamaa hii kukushambulia. Ni kama jinsi Pisa ilivyoasi dhidi ya waflorence licha ya kuishi chini yao kwa mamia ya miaka.

Lakini, iwapo eneo jipya lililozoea kuishi chini ya taratibu zake likawa limetekwa, na mfalme wake na warithi wake kuangamizwa, itakuwa ni vigumu kwa wananchi waliozoea kumtii kiongozi wao, ambaye sasa hayupo nao, kuchagua kiongozi mwingine miongoni mwao. Na kwa sababu hawajui jinsi ya kuishi kama watu huru, watakuwa wazito kubeba silaha kupigana, mgeni yeyote anaweza kuwatawala kirahisi.

Lakini kwa serikali za kijamuhuri mambo ni tofauti kabisa. Watu watakuwa na chuki na kiu ya kulipa kisasi. Kumbukumbu za uhuru wao zitawasumbua siku zote. Hivyo njia salama ya kuwatawala ni kuwangamiza, au kwenda kuishi kati yao
 
SURA YA SITA

KUHUSU UTAWALA MPYA AMBAO KIONGOZI AMEUPATA KWA NGUVU NA AKILI ZAKE

Mtu asistaajabie mifano nitakayotoa ninapozungumzia kuhusu ufalme mpya kabisa. Ufalme ambao nchi na mfalme wake ni wapya. Kwa sababu mara nyingi watu hufuata hatua na kuiga matendo ya wengine. Na mara nyingi hushindwa kuiga na kufuata kwa usahihi, au kupata mafanikio yanayofanana. Basi, mtu mwenye hekima anapaswa kufuata njia walizopita watu hodari, na kuiga matendo ya wale waliofanikiwa. Hata kama hatakuwa kama wao, angalau anaweza kujipatia mafanikio yanayomfaa. Kwa kufanya hivyo anakuwa kama mlenga mshale hodari. Mpiga mshale hodari akitaka kulenga kitu kilicho mbali hulenga mshale kuelekea juu. Si kwamba anataka kupiga angani, bali kwa kwenda kwake juu mshale uweze kufika kwenye shabaha aliyokusudia.

Hivyo ninasema, kwenye ufalme mpya kabisa, ambapo na mfalme ni mpya, ugumu wa kutawala unatofautiana kutokana na uwezo wa mtawala mwenyewe.

Kwa sababu mtu wa kawaida kuwa mfalme kunatokana na uwezo wake au bahati, inaonekana uwepo wa moja ya haya mambo mawili ndiyo utaamua ugumu wa uongozi wake. Lakini inaonekana kuwa mara nyingi yule aliyefanikiwa kuwa mfalme kwa uwezo wake mwenyewe, ndiye hufanikiwa zaidi ya yule aliyetegemea bahati. Na pia ni jambo la faida kwa mfalme mpya ambaye hana eneo lingine la kiutawala kwenda kuishi kwenye nchi yake mpya.

Nianze kwa kuwaangalia wale waliopata ufalme kwa uwezo wao na si kwa bahati tu. Miongoni mwa mifano mizuri tuliyonayo ni Musa, Cyrus, Romulus, Rheseus na wengine wafananao nao. Pengine sikupaswa kumtaja Musa sababu yeye alikuwa ni mjumbe tu, na alipokea amto kutoka kwa Mungu, lakini tukiangalia vizuri tunaona bado anahitaji kusifiwa kwa kuwa na sifa zilizomfanya astahili kuongea na Mungu. Tukimuangalia Cyrus na wengine ambao walisimamisha falme zao toka chini tunaona ni watu wenye kustahili sifa. Lakini matendo yao na falme walizosimamisha zikichunguzwa kwa makini itaonwa kuwa hawana tofauti na Musa, japo yeye alipata maagizo yake toka kwa mwalimu mkuu kupita wote.

Na pia iwapo tutachunguza kwa ukaribu kuhusu maisha yao na matendo yao, tutaona kuwa walisaidiwa na bahati, maana hakuna kingine kilichowawezesha kufanya mambo kadri walivyotaka isipokuwa fursa. Bila fursa, nguvu na jitihada zao zisingezaa chochote. Lakini pia, fursa zingepotea kama wangekuwa hawana uwezo wa kuzitumia. Kwa hiyo, ilikuwa ni muhimu kwa Musa kuwakuta wana wa Israel wakiwa watumwa waliokandamizwa huko Misri ili waweze kumfuata na kuokoka kwenye utumwa wao. Ilikuwa pia bahati kwa Romulus kutokuwa na makazi huko Alba, na kutabiriwa wakati wa kuzaliwa kwake kuwa atakuja kuwa mfalme na muanzilishi wa jiji la Roma. Ilikuwa pia ni muhimu kwa Cyrus kuwakuta waajemi wakinung'unika chini ya utawala wa wamedi, na ilikuwa muhimu pia kuwakuta wamedi wakiwa wazembe baada ya kuishi kwa amani kwa muda mrefu. Hata Theseus asingeweza kuonyesha uwezo wake mkubwa kama asingewakuta waathene wamegawanyika na kutawanyika.

Kwa hiyo, japo ni fursa, zilizowafanya watu hawa kuwa na bahati, ni uwezo wao ndiyo uliwafanya watambue fursa hizo na kuzifanyia kazi. Kazi zilizoleta utukufu na mafanikio kwa chi zao.

Wanaokuwa wafalme kwa kupitia njia hizi, hupatwa na vizingiti vingi lakini, wakifanikiwa hutawala kirahisi. Ugumu mkubwa unatokana na wao kuhitajika kutengeneza sheria mpya na kuunda taasisi mpya kwaaajili ya kuendesha tawala walizozianzisha. Na ifahamike kuwa, hakuna jambo tata, jambo la hatari na jambo lisilo na uhakika wa kufanikiwa kama kwa kiongozi kuanzisha mabadiliko.

Yule anayejaribu kubadilisha mambo, atapata maadui kutoka kwa wale waliokuwa wakifaidika na mfumo wa zamani. Pia atapata uungwaji mkono wa kishingo upande kutoka kwa wale wanaoweza kufaidika na mfumo mpya. Uungwaji mkono huu wa kivuguvugu ni sababu ya kuogopa wale wanaosimamia sheria na mambo kwa wakati huo. Hulka ya binadamu ni kutoamini mambo mpaka yatokee na waone faida yake. Kitakachotokea ni kuwa; wale wanaopinga mabadiliko watapambana kwa nguvu zote, lakini wale wanaotetea mabadiliko watayatetea kidhaifu na hivyo kuhatarisha mpango mzima wa mabadiliko.

Lakini ili kupata uelewa kamili wa jambo hili, yatupasa kuangalia iwapo kiongozi wa mabadiliko anaweza kusimama peke yake, au anategemea msaada wa watu wengine. Kwa maneno mengine, ili wafanikishe mipango yao, je, watageuka kuwa ombaomba na wabembelezaji? au wanaweza simama na kupambana hadi mwisho? Wale wanaoomba na kubembeleza huwa hawafanyi vizuri na hawapati mafanikio yoyote ya maana. Lakini wale wanaotegemea nguvu zao wenyewe na kupambana hufanikiwa. Historia inaonyesha kuwa; mitume wote waliotumia vita walifanikiwa, lakini wale waliotumia maneno matupu waliangamizwa.

Ukiacha pembeni yaliyosemwa, inatakiwa kuwekwa akilini kuwa, akili ya umati ni yenye kubadilikabadilika. Kwa hiyo, japo ni rahisi kuwaaminisha watu kitu, ni ngumu kuwafanya waendelee kuamini siku zote. Kwa hiyo basi, mipango inatakiwa kufanywa ambapo watu wakiacha kuamini, watalazimishwa kuamini kwa nguvu. Musa, Cyrus, Theseus na Romulus wasingeweza kufanya miongozo yao ifuatwe na kutiiwa kwa muda mrefu kama wasingetumia nguvu. Hata katika siku zetu, mambo aliyoanzisha mfriar, Girolamo Savonarola yalifutika haraka mara tu watu walipoacha kuyaamini. Sababu ni kuwa, hakuwa na njia ya kuwalazimisha wale walioamini waendelee kuamini wala kuwafanya wasioamini waamini.

Watu kama hao hupata wakati mgumu sana kutimiza malengo yao. Lakini tatizo hilo linaweza kushindwa iwapo watakuwa na ujasiri. Hapo watayashinda, wataheshimika na watawaangamiza wote waliokuwa na wivu na husda juu yao.

Pamoja na mifano niliyoonyesha hapo juu nitaongezea mwingine. Huu nao ni sawa tu na ile mingine. Namaanisha mfano wa Hiero msairakusi. Kutoka mtu wa kawaida alipanda hadi kuwa mfalme wa Sairakusi, naye huyu mafanikio yake yalitokana kwa kiasi na bahati iliyoletwa na fursa. Wasairakusi walipokuwa wakikandamizwa, walimchagua kuwa kiongozi wao. Aliifanya kazi hiyo vizuri hadi wakamchagua kuwa mfalme wao. Lakini hata alipokuwa raia wa kawaida alikuwa na uwezo mkubwa hadi ilisemwa kuwa alikuwa na sifa zote za mfalme kasoro ufalme. Alivunja jeshi la zamani na kulipanga upya, alivunja ushirika uliokuwepo na kuingia kwenye ushirika mpya. Kwa kutumia jeshi na ushirika mpya aliweza kubadilisha na kuunda mfumo mpya kadiri alivyoona inafaa. Alipata taabu wakati wa kusimamisha utawala wake, lakini hakupata taabu yeyote kuuendesha na kuudumisha.
 
SURA 7

KUHUSU UTAWALA MPYA ULIOPATIKANA KWA MSAADA WA WENGINE, AU KWA BAHATI TU

Wale ambao kutoka kuwa raia wa kawaida, wanafikia kuwa viongozi kwa sababu ya bahati njema, hufanya hivyo bila vikwazo vingi, lakini hupata wakati mgumu sana kudumu kwenye vyeo hivyo. Hawapati ugumu wowote wakati wakupata madaraka yao sababu hubebwa na bahati, lakini magumu yote huwakumba mara wanapokuwa wameanza kutawala. Katika watu wa aina hii, kama ilivyotokea huko majiji ya kigiriki ya Ionia na Hellespont walifanywa kuwa watawala na Dario, walipewa kutawala kwaajili yake; na kama inavyotokea kwa watawala ambao kutoka kuwa raia wa kawaida, wanafikia vyeo vya utawala kwa msaada wa jeshi. Watawala wa namna hiyo, huwa tegemezi kwa wale waliowafanya wapate vyeo.

Utawala wa watu hawa huwa si imara na salama, sababu wanakosa ujuzi na nguvu ya kuwafanya wabaki madarakani. Nasema wanakosa ujuzi kwa sababu, isipokuwa kama mtu ana sifa za kipekee sana, haitegemewi kwa mtu aliyeishi maisha yake yote kama raia, kwamba atakuwa na ujuzi wa kuongoza. Na hawana nguvu kwa sababu hawana kikosi kinachowatii kinachoweza kuwa msaada kwao. Zaidi ya hilo, utawala uliopatikana haraka, kama vitu vyote vinavyozalishwa na kukua haraka, hauwezi kuwa na mizizi ya kuhimili tufani; isipokuwa, kama nilivyokwisha sema, yule aliyekuwa mtawala bila kutarajiwa, ana uwezo wa kujifunza haraka namna ya kulinda bahati iliyomuangukia

Katika kila njia hizo za kufikia kuwa kiongozi, yaani kutokana na uwezo au bahati, nitazungumzia mfano mmoja ninaoukumbuka. Nitazungumzia mfano wa Francesco Sforza na Cesare Borgia. Kwa uwezo binafsi na kupanga mambo vizuri, Francesco Sforza aliweza kupanda kutoka raia wa kawaida hadi kuwa duke wa Milan. Aliweza kutawala bila tatizo japo alipata magumu yasiyo na idadi kufikia kuwa Duke. Kwa upande mwingine, Cesare Borgia, ambaye kwa dhihaka aliitwa Duke Valentino, aliweza kuwa kiongozi kupitia upendeleo wa baba yake, na kwa sababu hiyo aliupoteza uongozi huo.

Japo kwa uwezo wake alitumia jitihada zote na alitenda yale ambayo mtu yeyote mwenye busara na mwenye uwezo angefanya; matendo ya mtu anayetaka kujisimika kwenye utawala alioupata kwa bahati, au kwa kupewa na jeshi. Kama nilivyokwisha sema, yule ambaye hasimiki misingi yake mapema, hata akifanikiwa kuisimika baadaye, lazima italeta utata kwa mjenzi na kuwa hatari kwa jengo lenyewe. Na kama tukiangalia hatua zilizo chukuliwa na Duke Valentino, tutaona jinsi alivyoweka misingi ya mamlaka yake.

Nafikiri haitakuwa kupita kiasi iwapo tutachunguza hilo, sababu sijui jambo la kuweza kumfundisha kiongozi mpya zaidi ya kutumia matendo ya Cesare Borgia kama mfano. Na kama hatua alizozichukua mwishoni hazikumletea manufaa, haikuwa sababu ya makosa yake, bali bahati haikuwa upande wake.

Katika jitihada za kumkweza mwana wake, papa Alexander VI alikabili magumu mengi, ya papo kwa papo, na mengine baadaye. Kwanza kabisa, hakuona uwezekano wa kumfanya kuwa kiongozi wa taifa lolote ambalo halimilikiwi na kanisa. Pia alitambua kuwa, iwapo atamfanya kuwa kiongozi wa eneo lolote lililo chini ya kanisa, basi Duke wa Milan na wavenice hawataridhia; tayari Faenza Rimini zilikuwa chini ya uangalizi wa Wavenice. Zaidi ya hayo, alitambua kuwa, majeshi ya Italia, hasa yale ambayo angeweza kuyatumia kujinufaisha, yalikuwa chini ya watu waliiogopa asije kujikweza ns kuea na nguvu, yaani wa-Orsini, wa-Colonnesi na wafuasi wao. Hivyo hakuweza kuwaamini hawa.

Hivyo kukawa na ulazima wa mambo kubadilika ndani ya Italia, na vurugu kuzuka ili aweze kujiweka kuwa mtawala wa sehemu ya nchi hiyo; na suala hili alilifanya kirahisi pale alipotambuwa kuwa, wavenice, kwa kuchochewa na sababu zingine, walikuwa na mpango wa kuwaleta wafaransa Italia kwa mara nyingine. Hakupinga mpango huu, bali alichochea ufanikiwe kwa kubatilisha ndoa ya kwanza ya mfalme wa Ufaransa. Kwa hiyo, mfalme Louis aliingia Italia kwa kuitikia wito wa wavenice na ridhaa ya Papa Alexander, na mara tu alipofika Milan, Papa akamuomba wanajeshi wa kwenda kumsaidia kwenye vita yake dhidi ya Romagna, mkoa ambao kwa kuogopa sifa za jeshi la Ufaransa, ulisalimu amri mara moja. Mara baada ya kuipata(kupewa) Romagna, na kuwadhibiti wa-Colonnesi, Duke Valentino akawa anatamani kuendelea kutanua himaya yake. Lakini vitu viwili vilimzuia kufanya hivyo.

Ni uaminifu unaotia mashaka wa jeshi lake, na kutotabirika kwa Ufaransa. Hivyo aliogopa kuwa wa-Orsini, ambao alikuwa anatumia jeshi lao watamfanya ashindwe, na si tu kushindwa kumsaidia kutanua himaya yake, bali pia kumpora himaya aliyokuwa nayo, na labda mfalme wa Ufaransa naye atamgeuka namna hiyo. Jinsi ambavyo hakuwaamini wa-Orsini ilionekana wazi mara baada ya kuiteka Faenza, baada ya kuiteka Faenza, aliongoza jeshi lake kwenda kuivamia Bologna, na aliona jinsi wa-Orsini walivyokuwa wakisita na kutokuwa tayari kwenye jambo hilo. Alielewa maoni ya mfalme wa Ufaransa baada ya kuiteka Urbino, baada ya hapo akawa anajiandaa kuivamia Tuscany, jambo ambalo alizamishwa kuliacha na Mfalme Louis. Hivyo basi, Cesare Borgia akakata shauri kutotegemea jeshi wala rehema za wengine. Hatua yake ya kwanza ilikuwa ni kuzidhoofisha kambi za wa-Orsini na Wacolonnesi huko Roma. Wafuasi wao ambao walikuwa watu wa nasaba bora aliwafanya kuwa watu wake wa karibu. Akiwapa majukumu ya kiraia, na vyeo vingine kulingana na matabaka yao; kwa hiyo, baada ya miezi michache wakawa wamejitenga na kambi zao. Na matumaini yao yakawa kwa Duke Cesare Borgia pekee.

Baada ya hapo, akaanza kuvizia nafasi ya kuwaangamiza wakuu wa wa-Orsini, tayari alikuwa amewasambaratisha wa-Colonnesi. Bahati nzuri fursa nzuri ilitokea naye akaitumia ifaavyo. Mara baada ya Wa-Orsini kuona kuwa kukwezwa kwa Duke Cesare Borgia, na kukwezwa kwa kanisa ni maangamizi kwao, wakaitisha baraza huko Magione ya Perugia. Maazimio yao yakazaa uasi huko Urbino, vurugu huko Romagna na hatari isiyokwisha dhidi ya Duke, mambo yote hayo aliyadhibiti akiwa anasaidiwa na jeshi la Ufaransa.

Hapo heshima yake ikarudi, lakini Duke hakuwaamini wafaransa, wala mgeni mwingine yoyote kumsaidia, na sababu hakuweza kuwakabili waziwazi, akaanza kutumia mbinu, na aliweza kuficha mipango yake vizuri sana kiasi kwamba wa-Orsini, kupitia usuluhishi wa Bwana Paolo (ambaye alimpatia zawadi nyingi ikiwemo pesa, nguo na farasi), Walishawishika na kijipeleka kirahisi mikononi mwake huko Sinigaglia, mara baada ya kuwaangamiza viongozi wao, na kuwafanya wafuasi wao rafiki zake, Duke akawa amejiwekea msingi mzuri wa mamlaka yake hapo baadaye. Maana tayari akawa anaitawala Romagna yote na Urbino. Zaidi, akawa amefanya akubalike na watu wote wa sehemu hizo, ambao waliona sasa wana hali nzuri zaidi.

Na kwa sababu matendo yake haya ni yanayopaswa kuchunguzwa na kuigwa, sitayaacha yapite bila kuyazungumzia. Mara baada ya Duke kuiteka Romagna, baada ya kuona kuwa inaongozwa na watu dhaifu, ambao waliwaza zaidi ufisadi wa mali kuliko kuwadhibiti watu wao; na hivyo kuwapa zaidi sababu ya kugawanyika kuliko kuwa kitu kimoja, na kufanya nchi kujaa wanyang’anyi, vurugu na kila namna ya fujo, aliona kuwa ni muhimu wa kuipatia serikali nzuri, ili kuifanya iwe na amani na yenye kutii mamlaka yake. Akamuweka Bwana mkubwa Remiro d’Orco aiongoze. Huyo alikuwa ni kiongozi imara na mtu asiyevumilia uzembe, hivyo alimuamini na kumpatia mamlaka yote. Ndani ya muda mfupi, na sifa nyingi zikimuendea yeye Duke, d’Orco akawa amerejesha amani na utulivu. Lakini baada ya muda, mamlaka asiyo na kikomo yanaweza sababisha chuki, hivyo Duke akaona kuwa hayahitajiki tena, hivyo akaanzisha mahakama ya kirai ya mkoa. Hiyo ilikuwa chini ya uongozi mzuri huku kila mji ukiwakilishwa na mwanasheria wake.

Na kwa kufahamu kuwa unyama uliotendeka huko nyuma, umesababisha chuki kumuelekea. Hivyo, ili kubadili akili za raia na kufanya wamkubali, aliazimia kuwaonyesha kuwa ukatili wowote uliokuwa umetendeka haukutokana na yeye, bali ukatili wa mawaziri wake. Asubuhi moja aliamuru Remiro auawe na kichwa chake kiwekwe sokoni huko Cesana pembeni ya shoka lenye damu. Mara moja unyama huo uliwaridhisha watu.

Lakini tukirudi kwenye mada yetu, nasema kuwa; baada ya Duke kujiona ana nguvu, yuko salama dhidi ya hatari zilizomkabili, ana jeshi lake mwenyewe, na kwa kiasi, kaliondoa lile ambalo kama angeliacha lingeweza kumletea matatizo, akaanza kuwaza; kama anataka kuendelea kutanua himaya yake, ni jinsi gani ya kushughulika na Ufaransa? Sababu aliona wazi kuwa Mfalme Louis hawezi kumuunga mkono tena, ilionekana Mfalme alitambua kosa lake la kumuunga mkono Duke. Hivyo basi, Duke akaanza kutafuta washirika wapya, na kuachana na wafaransa ambao walikuwa wanajishughulisha zsidi na vita dhidi ya wahispania huko Napoli, na kwa wakati huo walikuwa wameizingira Gaeta; lengo lake lilikuwa ni kuwa salama dhidi ya wafaransa, na katika hili angefanikiwa iwapo Papa
Alexander asingekufa.

Hiyo ndiyo njia aliyopita hadi kuingia kwenye hali tete aliyomo leo. Kwa kufikiria wakati ujao, alimbidi kuelewa kuwa kiongozi mpya wa kanisa anaweza kuwa hana urafiki naye, na pengine hata anaweza kumnyang’anya vyote alivyopewa na Alexander. Alipanga kukabili hili kwa njia nne. Kwanza kwa kuwaangamiza ndugu wa viongozi ambao aliwapora mali zao, hilo ni ili wasije kutumika na Papa mpya. Pili, alidhamiria kufanya watu wa nasaba bora wa Roma kumuunga mkono, hili lingemuwezesha kumdhibiti na kumtumia Papa apendavyo. Tatu, kwa kuweza kuliweka baraza la makardinali katika udhibiti wake kadri anavyoweza. Na nne, kwa kuimarisha mamlaka yake kabla ya kifo cha baba yake, hili ni ili aweze kuhimili magumu yanayoweza kumpata mara baada ya kifo cha baba yake.

Wakati Alexander anafariki tayari alikuwa ametimiza mambo matatu, na alikuwa karibu kutimiza jambo la nne. Katika wale viongozi ambao alikuwa amepora mali zao, alikuwa amewaua wote alioweza kuwapata, na ni wachache tu ndiyo walifanikiwa kumtoroka. Tayari alikuwa anaungwa mkono na watu wa nasaba bora wa Roma, na wengi katika baraza la makadinali walikuwa wanamuunga mkono.

Mpango wake ulikuwa ni kutawala Tuscany yote. Tayari alikuwa anamiliki Perugia na Piombino, na tayari alikuwa amejiweka kama muangalizi wa Pisa, mji ambao alikuwa anajiandaa kuunyakua bila kujali wafaransa, na kwa kweli wasingemletea shida, baada ya Ufaransa kuporwa Napoli na wahispania, hali iliyofuatia ilizilazimu nchi zote mbili kutaka urafiki naye. Kama pisa ingetwaliwa, Lucca na Siena zingefuata, labda kwa sababu ya wivu wao juu ya Florence, au kwa uoga wao. Waflorence nao wangejikuta kwenye hali tete sana.

Kama angefanikiwa kwenye mipango hii, kama ambavyo alikuwa akifanikiwa mwaka ule aliofariki Alexander, angejipatia nguvu na utukufu ambao pengine ungemuwezesha hapo baadaye kusimama mwenyewe, akitegemea nguvu na mali zake mwenyewe, bila kuwajibika kwa wengine kwa sababu ya nguvu na fursa walizompatia. Lakini Alexander alifariki akimuacha mwana wake akiwa anamiliki kikamilifu Romagna tu, huku kwingine kote kukiwa na machafuko, akiwa katikati ya maadui wawili wenye nguvu na mgonjwa wa karibu kufa. Basi hayo ndiyo yalikuwa matendo ya kijasiri ya Duke, alijua jinsi ya kufanya maridhiano na jinsi ya kuwadhibiti watu. Misingi aliyojenga kwa muda mfupi ilikuwa imara sana, kama maadui wasingekuwa dhidi yake, au kama angekuwa na afya nzuri angeweza kukabili magumu yote.

Jambo lifuatalo linaweza kutuonyesha jinsi misingi aliyoiweka ilivyokuwa imara. Wakati anaumwa karibia ya kufa Romagna ilimsubiria kwa mwezi mzima, na alikaa kwa amani huko Roma, wa-Baglioni, wa-Vitelli na wa-Orsini walijaribu kumshambulia bila mafanikio. Zaidi ni kuwa, japo hakuweza kumfanya yule anayemtaka achaguliwe kuwa Papa, lakini angalau alifanikiwa kuzuia yule asiyempenda asichaguliwe. Kama angekuwa na afya njema wakati Alexander anafariki, mambo yote angeyatimiza kwa urahisi. Lakini aliniambia siku ile ambayo Julius II alipokuwa akifanywa kuwa kardinali, alisema kuwa alikuwa amewaza kimbele na alijiandaa kwa chochote kinachoweza kutokea baada ya kifo cha baba yake, lakini hakuwa amefahamu kuwa, wakati baba yake anafariki naye atakuwa anachungulia kaburi.

Kwa kuangalia matendo yote haya ya Duke, sijaweza kuona kosa ndani yake. Naonelea ni jambo la akili nikisema alikuwa nimuendelezo wa kile nilichokisema, nilichosema kuhusu wale wanaopata madaraka kupitia msaada wa wengine na bahati. Hakukuwa na njia bora zaidi ya kufanya mambo zaidi ya alivyofanya, hakuna kilichopelea zaidi ya kifo cha baba yake na ugonjwa wake ndivyo vilivyokwamisha mipango yake. Hivyo, yule anayeanza kutawala ufalme mpya, ni muhimu akatokomeza adui zake, akatafuta marafiki, kutawala kwa nguvu au hila, kufanya raia wake wamuogope lakini wasimchukie, anayeheshimiwa na kutiiwa na wanajeshi wake, kuwaangamiza wale wanaoweza au wanaofikiria kumdhuru, kufanya mabadiliko ya mfumo wa mambo wa zamani, kuwa mkali na mwenye urafiki kwa wakati mmoja, kuachana na jeshi linaloweza fanya uasi na kuunda jipya, kuwa na uhusiano na wafalme na watawala wengine kiasi cha kuwafanya waone kuwa kumsaidia ni jambo lenye faida kwao, ni jambo la hatari kukuudhi. Na hakuna mfano mzuri kama wa Cesare Borgia.

Jambo moja ambolo Cesare Borgia anaweza kulaumiwa ni kitendo cha Julius II kuwa Papa, hilo lilikuwa ni chaguo baya. Sababu, kama ambavyo nimekwisha sema, japo hakuweza fanya achaguliwe yule aliyemtaka, lakini alikuwa anaweza kuzuia yeyote asichaguliwe. Na hakutakiwa kuridhia kuchaguliwa kwa kardinali ambaye alikuwa amemdhuru huko nyuma, au yule ambaye baada ya kuwa Papa angekuwa na sababu za kumuogopa; sababu uoga ni adui hatari kama tu chuki.

Wale ambao alikuwa amewaudhi huko nyuma walikuwa ni pamoja na San Pietro ad Vincula; Colonna, San Giorgio, na Ascanio; wengine wote, isipokuwa d’Amboise na makardinali wa kihispania(makadinali kwa kihispania kwa sababu ya mahusiano yao na wajibu wao kwake, na D'Amboise kwa sababu Duke alikuwa na nguvu kupitia uhusiano wake na baraza/mahakama Ufaransa)kama wangepata Upapa, wangekuwa na sababu ya kumuogopa. Kwa hiyo, jambo la kwanza alilotakiwa kufanya ni kupambana apatikane Papa wa Kihispania, kama angeshindwa hilo, basi angeridhia d’Amboise kuchaguliwa kuwa Papa, lakini kamwe si san Pietro ad Vincula. Anajidanganya mtu anayeamini kuwa wema unaotendwa karibuni, hufunika mabaya yaliyotendwa hapo zamani na kuyafanya yasahaulike. Kwa hiyo, Duke alifanya makosa wakati wauchaguzi huo; na kosa hilo ndilo likawa maangamizi yake.
 
SURA YA 8

KUHUSU WALE AMBAO KUPITIA UHALIFU WAO WAMEWEZA KUWA VIONGOZI.

Kutoka kuwa raia wa kawaida mtu anaweza kuwa kiongozi kwa moja kati ya njia mbili. Lakini katika hizo hakuna tunayoweza sema ni bahati au uwezo peke yake ndiyo umemuwezesha kufanikiwa. Ninaonelea nizidokeze hapa, japo moja wapo nitaiongelea zaidi nitakapokuwa naongelea kuhusu jamuhuri.

Njia ninazozizungumzia ni; moja, pale mtu anapopata madaraka kwa kufanya ubaya na uhalifu, na pili ni pale mtu wa kawaida anapokuwa mtawaala kwa kuchaguliwa na raia wenzake. Kwa njia ya kwanza nitatoa mifano miwili, wa kwanza ni wa zamani na mwingine ni wa wakati wetu. Bila kueleza kiundani nadhani mifano hii inatosha kwa yule anayetaka kufuata njia hiyo.

Agathocles msisili alikuwa si tu raia wa kawaida, bali alikuwa kwenye kundi la watu wa hali ya chini kabisa, lakini aliweza kuwa mfalme wa Sairakusi. Baba yake alikuwa ni mfinyanzi, maisha yake yote yalikuwa ni mapotovu, lakini alikuwa na nguvu za mwili na akili. Alipojiunga jeshini alipanda vyeo harakaharaka hadi kuwa kamanda wa Sairakusi. Alipopata cheo hicho akadhamiria moyoni mwake kuwa mfalme, na kutumia nguvu na kutawala kidikteta peke yake.
Inasemwa kuwa, baada ya kumwambia Hamilcar mpango wake(Hamilcar alikuwa na jeshi la Carthage akipigana na Sisili). Asubuhi moja, alikusanya watu na wabunge wa Sairakusi kama vile anataka kupata maoni yao kuhusiana na masuala ya kitaifa. Baada ya kuwapa ishara ya siri, wanajeshi wake waliwaua wabunge wote na raia matajiri. Baada ya kufanya hivyo akajitwalia madaraka bila upinzani wowote kutoka kwa raia. Japokuwa alishindwa vita mara mbili dhidi ya wacarthage, lakini aliweza kulilinda jiji lake lilipozingirwa. Aliacha kikosi kikilinda jiji na yeye kwenda kuvamia Africa ya kaskazini(nyumbani kwa wacarthage) hivyo jeshi linalozingira likalazimika kuondoka. Aliwanyenyekeza wacarthage hadi wakakubali maridhiano, waliondoka Sisili na kurudi Africa ya kaskazini.

Mtu akichunguza matendo na mafanikio ya mtu huyu, hawezi kuona kitu chochote kinachoonyesha kuwa alikuwa na bahati. Kama tulivyoona, alipanda vyeo si kwa upendeleo bali kwa uwezo wake jeshini. Alipanda kupitia hali ngumu na hatari nyingi za jeshini. Aliweza kuwa mfalme na alidumisha ufalme wake kwa kutumia mbinu za hatari na zinazohitaji ujasiri. Kuchinja raia wenzake, kusaliti rafiki zake, kukosa huruma, kukosa aibu na dini, si matendo yanayoweza mpa mtu sifa ya uhodari. Ni njia tu ya kufikia madaraka, lakini ni mambo yasiyoleta heshima yoyote.
Lakini tukizungumzia sifa ya ushujaa aliyoionyesha kwa kupambana dhidi ya matatizo, hatuna sababu ya kutomfananisha na mashujaa hodari waliowahi kuishi. Lakini ukatili wake na kukosa kwake ubinadamu kunatufanya tusimuweke kati ya watu wakuu waliopata kuishi.

Katika wakati wetu wa papa Alexander wa VI, tuna mfano wa Oliverotto wa Fermo. Huyu alikuwa ni yatima aliyelelewa na mjomba wake, Giovanni Fogliani. Alipokuwa kijana alipelekwa kuwa msaidizi wa Paolo Vitelli, ilitarajiwa kuwa, kwa kujifunza chini ya kamanda huyo atapata ujuzi utakaomuwezesha kupanda vyeo vya kijeshi. Baada ya kifo cha Paolo, akawa msaidizi wa kaka yake, Vitellozo. Kwa akili zake na uwezo alioonyesha akawa mmoja ya maofisa kwenye kikosi cha Vitellozo. Lakini hakupenda kutumikia chini ya mtu hivyo kwa msaada wa wa-Vitelleschi na baadhi ya raia wa Fermo wenye hila, akapanga njama ya kunyakua madaraka ya mji wa Fermo.

Inasemwa kuwa alimuandikia barua Giovanni Fogliani akimuambia kuwa, baada ya miaka mingi ya kutokuwepo nyumbani angependa kumuona na kuona mji aliolelewa. Alisema kuwa aliondoka ili kwenda kujijenga hivyo angependa kurudi ili raia wenzake waone kuwa hakuwa amekwenda kupoteza wakati. Alisema kuwa atarudi na wapanda farasi mia moja ambao ni rafiki zake na wafuasi wake; alimuomba Giovanni amuandalie mapokezi makubwa akiwa na wakazi wa Fermo. Alisema hilo si kwaajili ya heshima yake tu, bali ya Giovanni pia sababu ndiye aliyemlea.

Giovanni alimkaribisha vizuri mpwa wake. Aliandaa raia wa kumpokea na alimkaribisha nyumbani mwake. Siku kadhaa zilipopita na baada ya kupanga hila yake vyema, Oliverotto akandaa karamu ambayo alimualika mjomba wake na watu wengine mashuhuri wa Fermo. Baada ya kula na kuburudika, Oliverotto akaanza kuongea kuhusu ukuu wa papa na mwana wake, Cesare na mambo waliyotimiza. Walipoanza kumjibu alisimama ghafla na kuwaambia kuwa kuna jambo la muhimu ambalo angependa waende sehemu ya faragha kulijadili. Akaenda chumba cha faragha na mjomba wake na wale raia mashuhuri wakamfuata. Walipoketi tu, wanajeshi wakatokea kutoka mafichoni na kumuua Giovanni na wale raia wote.

Baada ya mauaji hayo, Oliverotto akapanda farasi na kwenda kumzingira hakimu mkuu. Watu wote waliingiwa na hofu na kukubaliana na serikali mpya iliyokuwa ikiongozwa naye. Wote waliompinga aliwaua, na akajiimarisha kwa kuweka sheria mpya. Ndani ya mwaka mmoja akawa amepata nguvu hadi kuwa tishio hata kwa jirani zake. Kama asingemruhusu Cesare Borgia kumkaribia kupita kiasi, lingekuwa ni jambo gumu kumpindua kama ilivyokuwa vigumu kumpindua Agothocles. Ilitokea wakati wa-Orsini na wa-Vitelli walipokuwa wamezingirwa huko Sinigaglia; naye akawa amekamatwa. Mwaka mmoja baada ya uovu wake naye akawa ameuawa, pamoja na Vitellozzo, ambaye alikuwa mshirika wake katika uovu.

Imeulizwa kuwa; inawezekanaje kwa watu kama Agothocles, watu ambao wamefanya ukatili mkubwa na mwingi kuendelea kuishi kwa muda mrefu kwenye nchi zao wakiwa salama? Wakijilinda dhidi ya adui wa nje na huku raia wao wakishindwa kuwaasi. Lakini wengine kwa sababu ya ukatili wao walishindwa kubaki madarakani hata kwenye kipindi ambacho nchi zao zina amani, ukiachana na nyakati tete za vita?
Naamini hili linatokana na kutumia ukatili vizuri(kama kuna ukatili mzuri) au vibaya. Ukatili tunaosema umetumika vizuri ni ule unaofanyika mara moja kwa nia ya kujilinda, na unaofanywa uonekane ni kwa faida ya raia. Si ule ukatili wa kuendelea kila siku.
Ukatili mbaya ni ule unaoanza kidogo kidogo, na kuongezeka muda unavyokwenda badala ya kupungua. Wale wanaotumia aina ya kwanza ya ukatili, hawatajiingiza matatizoni kama tu ambavyo Agathocles hakuingia matatizoni. Lakini wale wanaotumia aina ya pili ya ukatili ni ngumu kudumu madarakani.

Hivyo tumejifunza kuwa, mtu anaponyakua madaraka, anatakiwa kutenda ukatili wake haraka na kwa jumla ili asije akahitajika kuutenda kila mara. Baada ya hapo anatakiwa kuwaaminisha watu kuwa hawezi kuutenda tena, hilo litafanya wampende. Lakini yule ambaye kwa uoga na kwa ushauri mbaya anafanya tofauti na hivyo, itambidi kuwa tayari kwa vita muda wote. Wafuasi wake hawatamuamini na wale wanaoteseka na ukatili wake wa mara kwa mara hawataweza kumtii kwa uaminifu, na watakuwa na kinyongo naye.
Kwa hiyo, ubaya wote unatakiwa kufanyika mara moja. Majeraha ya mara moja ni rahisi kusahaulika, lakini zawadi au wema ili uthaminiwe unatakiwa kutendeka kidogokidogo na mara kwa mara.
Jambo la muhimu zaidi kwa mfalme ni Kuishi na raia wake kiasi kwamba, hali mbaya au nzuri zisimfanye abadili tabia yake.
 
SURA YA TISA

KUHUSU SERIKALI ZA KIRAIA

Sasa nitazungumzia aina ya pili, nitazungumza kuhusu raia wa kawaida ambaye si kwa ubaya au vita, bali kwa kukubaliwa na raia wenzake anafanywa kuwa kiongozi. Aina hii tunaweza kuiita serikali ya kiraia. Kiongozi wa aina hii anapatikana si kwa sababu ana bahati, wala si kwa sababu anauwezo, bali ni kutokana na kitu tunachoweza kiita ujanja. Kwa hiyo, upatikanaji wa mfalme wa aina hii hutegemea kukubaliwa kwake na raia wenzake au watu wa nasaba bora.
Kwenye kila jiji huwa kunakuwa na dhana mbili zinazopingana. Nazo huanzia namna hii; Kuna raia wa kawaida ambao wamechoka kutawaliwa na kukandamizwa na watu wa nasaba bora, na watu wa nasaba bora nao wanatamani kuwatawala na kuwakandamiza raia wa kawaida. Kutokana na aina hii ya wakazi wanaopingana, kunaweza kutokea vitu vitatu. Ufalme, Jamuhuri au taifa lisilo na utawala/machafuko
Ufalme unaweza kutengenezwa na raia wa kawaida, au watu wa nasaba bora kulingana na hali.
Kama watu wa nasaba bora wakiona kuna ulazima wa kudhibiti raia wa kawaida, humchagua mmoja wao na kumfanya kuwa kiongozi. Lengo ni kumtumia huyu ili kufanikisha malengo yao.
Raia nao kwa upande wao wakiona wameshindwa kuvumilia utawala wa watu wa nasaba bora, huamua kumchagua mtu kati yao na kumfanya kuwa kiongozi. Wakiwa na matumaini kuwa atalinda maslahi yao.

Yule anayefanywa kuwa kiongozi na watu wa nasaba bora huwa na kazi ngumu ya kuongoza kuliko yule anayefanywa kuwa kiongozi na wananchi wa kawaida.
Anayewekwa na watu wa nasaba bora hawezi kuongoza kama anavyotaka. Sababu ni kuwa watu wengi wa tabaka hilo hujiona tu wapo sawa naye, na hakuna alichowazidi. Lakini anayewekwa na wananchi hujikuta amezungukwa na watu wachache tu wanaoweza kujilinganisha naye.

Na zaidi ni kuwa, matakwa ya watu wa tabaka la juu hayawezi kutimizwa bila kuwaumiza wale wa tabaka la chini. Kwa kawaida, mahitaji ya watu wa tabaka la chini huwa ni muhimu kuliko ya watu wa tabaka la juu. Watu wa tabaka la juu huwa na lengo la kukandamiza na kunyonya. Lakini wale wa tabaka la wanyonge hutaka uonevu, unyonyaji na ukandamizaji kukoma. Na pia, hata kiongozi akijitahidi kutimiza matakwa ya watu wa tabaka la juu, jitihada hizo huwa hazithaminiwi.
Lakini kumbuka kuwa, kiongozi hawezi kuwa salama isipotimiza matakwa ya watu wa hali ya chini ambao ni wengi, lakini anaweza kuwa salama dhidi ya watu wa tabaka la juu ambao huwa ni wachache.
Kitu cha kuogopesha kwa mfalme kutoka kwa raia wasioridhika, ni kuwa wataacha kumuunga mkono. Lakini watu wa uzao bor, wataacha kumuunga mkono na pia wanaweza kuunda hila dhidi yake, sababu hawa ni waelewa na watu wenye hila, nao hubadilikabadilika na kumuunga mkono yeyote anayeelekea kupata ushindi.
Kiongozi anatakiwa kuishi kati ya watu wake walewale siku zote. Lakini si lazima kuwa na watu wa nasaba bora walewale siku zote. Sababu yeye ana mamlaka ya kuwapandisha na kuwashusha madaraja apendavyo.

Lakini ili hili suala kuhusu watu wa nasaba bora lieleweke vizuri, niseme yafuatayao. Kati ya watu hawa, kuna wanaokuunga mkono kwa moyo wote, na wale wanaokuunga kwa shingo upande. Wale wanaokuunga mkono kwa moyo wote wanatakiwa kupendwa na kuheshimiwa. Wale wasiokuunga mkono kikamilifu nitawazungumzia kama ifuatavyo; kwa kuwa hawa wanaogopa kukupinga sababu ya kukosa ujasiri, inakupasa kuwatumia, hasa hasa wale walio na hekima. Hawa watakutukuza kwenye mafanikio yako, na wala hawatakuwa tishio kwako wakati wa taabu. Lakini ikitokea wakaanza kupunguza uungaji mkono wao, tambua kuwa wana ajenda zao binafsi, na kiongozi anatakiwa kuwa chonjo na watu hao. Anatakiwa kuwatendea kama adui wengine. Hawa ndiyo wale watakao kukandamiza wakati wa taabu yako.

Kiongozi anayekuwa kiongozi kutokana na raia wa kawaida, lazima ahakikishe ana mahusiano mazuri nao. Na hili ni jambo rahisi tu, kwa sababu wao wanachotaka ni kutoonewa na kuacha kukandamizwa tu. Lakini yule anayefanywa kuwa mfalme na watu wa tabaka la juu, jambo la muhimu kwake ni kuhakikisha anaboresha uhusiano wake na wananchi kwa kuanza kulinda maslahi yao mara moja. Kawaida watu wanahisi wana deni kubwa kwa mtu ambaye walitarajia awafanyie ubaya lakini akawatendea wema, watu watampenda sana kiongozi huyo kwa kulinda maslahi yao, watampenda kuliko hata yule ambaye wangekuwa wamemuunga mkono na kumuweka madarakani.

Kuna njia nyingi za kiongozi kufanya apendwe na aungwe mkono na wananchi. Kwa sababu njia hizo zinategemeana na hali, hakuna kanuni moja ya kufuata, hivyo sitazungumza sana kuhusu suala hilo. Lakini jambo kuu kwa kiongozi ni kuhakikisha ana uhusiano mzuri na wananchi wake. Tofauti na hapo hatakuwa na wakumsaidia wakati wa taabu yake.
Kiongozi wa Sparta, Nabis, alivamiwa na Ugiriki nzima pamoja na jeshi la Roma, lakini alilinda nchi yake dhidi yao. Wakati huo alikuwa na adui wachache kati ya watu wake, lakini kama wananchi wangekuwa wanamchukia asingeweza kujilinda dhidi ya wagiriki na waroma.

Lakini mtu asijebisha nisemacho kwa kutumia methali ya kale isemayo; 'Anayejenga juu ya watu, anajenga juu ya tope,' hii inaweza kuwa kweli kwa mwananchi wa kawaida ambaye anafikiri uhusiano wake mzuri na watu utafanya wamsaidie akiwa matatani dhidi ya adui zake, au dhidi ya mkono wa sheria. Kwa hali kama hizo mtu hujikuta katika hali asiyotegemea, kama tu ilivyowatokea wakinaGraoli huko Roma, au Bwana mkubws Giorgio Scali huko Florence. Lakini kama anayejenga juu ya watu ni kiongozi mwenye mamlaka na ana moyo wa ujasiri dhidi ya taabu, yule ambaye anawapandisha watu wake mori kwa ujasiri wake. Ambaye hapuuzi kufanya mambo kwa hekima na tahadhari; hawezi kusalitiwa na watu wake, bali ataonekana ni mtu mwenye misingi imara.

Wakati mgumu kabisa kwa kiongozi anayetokana na wananchi, ni pale anapotaka kutoka kwenye serikali ya kiraia kwenda serikali ya kiimla. Viongozi wa namna hii huongoza kwa njia mbili. Moja kwa moja au kwa kusimamiwa na mahakama, wale wanaosimamiwa na mahakama, hujikuta wakiwa dhaifu na kwenye hali tete. Wamepewa madaraka na wananchi, na mahakama imeaminiwa kuwasimamia, mahakama inaweza kuwavua madaraka kirahisi hasa nyakati za hali ngumu. Inaweza fanya hivyo kwa kuwapinga au kutowatii. Na kwenye nyakati za taabu ni vigumu kwa kiongozi kujinyakulia mamlaka yote, sababu ni kuwa wananchi walizoea kupokea maagizo kutoka kwa mahakama. Wakati wa taabu hawawezi kukubali kuchukua maagizo toka kwa kiongozi.
Kwa hiyo, kwenye nyakati hizo kiongozi hujikuta amebaki na watu wachache sana anaoweza kuwaamini. Hivyo basi, kiongozi wa namna hiyo asitegemee hali zilivyo kipindi nchi ikiwa na amani, ndivyo zitakuwa wakati wa taabu. Wakati wa amani, ambapo hakuna hatari ya kifo watu hutoa ahadi nyingi, watasema wako tayari kufia nchi nk. Lakini wakati wa taabu, wakati ambao nchi yao inawahitaji hawataonekana. Na ubaya wa jaribio la kunyakua mamlaka ni kwamba linaweza fanywa mara moja tu.
Kwa hiyo, kiongozi mwenye weledi, ni yule anayetengeneza mazingira yatakayowafanya wananchi wake wawe wanahitaji msaada wake na wa serikali yake siku zote. Iwe wakati wa shida au wa raha. Hapo ndipo wataweza kuwa waaminifu kwake siku zote.
 
SURA YA KUMI

JINSI NGUVU ZA KIONGOZI ZINAVYOTAKIWA KUPIMWA.

Tunapopima nguvu za kiongozi, kuna jambo jingine linalotakiwa kuangaliwa. Nalo ni iwapo kiongozi ana nguvu za kutosha, kama hali ikibidi, anaweza kusimama peke yake, au siku zote yeye anahitaji msaada kutoka kwa wengine. Kufanya jambo hili lieleweke vizuri, nawatangaza wanaweza kusimama peke yao, wale ambao kwa kutumia watu wao na pesa zao wanaweza unda jeshi lenye uwezo wa kupambana na adui yeyote.

Wale wanaotaka msaada siku zote, kama wale wasioweza kuunda jeshi la kuweza kupambana na yeyote, wale wanaokimbilia kujifungia kwenye majiji yao, na kujificha ndani yake. Huyu wa kwanza nimeshamuongelea, na nitamuongelea tena itakapobidi. Ila huyu wa pili sina cha kuongelea zaidi ya kumshauri kiongozi wa aina hiyo kuimarisha ngome za miji yake na kutojihusisha na kulinda eneo nje ya majiji yake.

Sababu yule aliyeimarisha ngome ya jiji lake, na kujifungia humo na wananchi wake, lazima atashambuliwa kwa tahadhari kwa sababu watu hawapendi kufanya mambo magumu. Na miji yenye ngome imara, na ambayo kiongozi wake anapendwa na watu wake, ni vigumu sana kuiangusha.

Miji ya ujerumani ina uhuru mkubwa japo haina maeneo makubwa ya kiutawala. Inamtii mfalme pale inapopenda na haimuogopi mfalme wala majirani zao wengine wenye nguvu. Ni miji yenye ngome imara. Imara kiasi kwamba kila mtu anaona kuwa itakuwa ni kazi ngumu kuivamia na kuishinda.

Miji yao inalindwa na mabwawa yaliyochimbwa kuzunguka mji, imezungushiwa matuta makubwa ya ulinzi, na ina mizinga ya kutosha juu ya kuta. Pia ndani ya maghala yao wana vitu vya kutosha mwaka mzima. Pia, ili kuwasaidia wale wasiojiweza, wamewawekea akiba ya kutosha mwaka mmoja kwa malipo ya kazi ya umma ya mwaka mmoja. Pia wanasisitiza sana mazoezi ya kijeshi, na wana majeshi yenye nidhamu ya hali ya juu.

Kwa hiyo, kiongozi ambaye ana mji wenye ngome imara na ambaye anapendwa na watu wake, hawezi kuvamiwa na kudhindwa. Ikitokea amevamiwa, basi wavamizi wake watajikuta matatani maana si rahisi kwa jeshi kuzingira mji kwa mwaka mzima bila kutokea matatizo kati yake.

Watu wakibisha na kusema kuwa; iwapo raia wenye mali zao nje ya mji wakiziona zikichomwa watakosa uvumilivu na watapoteza uaminifu wao kwa kiongozi wao, nitajibu kuwa, kiongozi hodari na jasiri atashinda jaribu hili. Kwa kuwapa watu wake matumaini kuwa taabu yao itaisha baada ya muda mfupi. Kwa kuwatoa wasiwasi juu ya adui yao, na kwa kuwanyamazisha kwa uangalifu walio vimbelembele, atawatuliza. Zaidi ni kuwa, kuna uwezekano mkubwa adui atachoma na kuharibu mali zilizo nje ya jiji mara tu baada ya kulizingira. Huo ni wakati ambao mori wa wakazi wa jiji upo juu na wapo tayari kufanya lolote kulinda jiji lao. Hivyo kuongozi hata kuwa na sababu ya kuogopa watu wake kumuasi. Ndani ya siku chache machungu ya mali zao yatakuwa yamepoa, na kutakuwa na utulivu jijini, na zaidi ya yote, watu watakuwa tayari kufuata chochote wanachoambiwa, na watashikamana zaidi na kiongozi wao ili kulinda jiji lao, maana tayari nyumba na mali zao zimekwishaharibiwa. Na wakati huo, kiongozi ataonekana anawajibu zaidi kwao kwa sababu wamepoteza mali zao ili kumlinda. Na ni hulka ya binadamu, kujihisi anawajibu kutokana na jambo alilofanya au alilofanyiwa.

Kwa hiyo, ikichunguza jambo hili kwa undani utaona kuwa, kiongozi mwenye hekima hawezi kupata ugumu kudhibiti wananchi wake wakati wa kuzingirwa kwa jiji. Anatakiwa tu kuhakikisha ulinzi ni imara na mahitaji muhimu yanapatikana.
 
SURA YA 11

KUHUSU TAWALA ZA KIDINI

Sasa nimebakiza kuongelea tawala za kidini, na ugumu wa kuzisimamisha. Hizi hupatikana kupitia bahati au uwezo, lakini haziendelezwi kwa njia hizo. Hizi huendelea kusimama kwa sababu ya heshima ya watu juu ya utukufu wa dini. Hiki ndicho kinamfanya kiongozi wa aina hii kubaki salama madarakani, haijalishi matendo yake au aina ya maisha yake.
Viongozi wa namna hii, huwa na maeneo ya utawala ambayo hawayalindi, na wafuasi ambao hawawaongozi. Lakini hawaporwi maeneo yao japo hawayalindi, na wafuasi wao hawajali kutoongozwa, wala hawafikirii kuasi, sababu hawana uwezo huo. Tawala hizi huwa salama na zenye furaha, kwa sababu zinalindwa na nguvu iliyo kubwa kuliko uwezo wa kibinadamu. Nitajiepusha kuzizungumzia kwa sababu hizi zimesimikwa na Mungu mwenyewe, itakuwa ni kimbelembele na kujikweza kwa binadamu kuzizungumzia.

Hata hivyo, mtu akiniuliza; kwanini mamlaka ya kisiasa ya kanisa yalidharauliwa na viongozi wa Italia kabla ya nyakati za Papa Alexander. Na si tu viongozi wakubwa, bali hata wale wadogo waliidharau. Lakini sasa kanisa limekuwa na nguvu kiasi hata cha kumtisha mfalme wa Ufaransa, na limeweza kumg'oa Italia na kuwanyenyekeza wavenice?
Japo sababu zinajulikana, lakini natumaini sitakuwa naongea kupita kiasi iwapo nikizikumbushia.

Kabla mfalme Charles wa Ufaransa hajaja, Italia ilikuwa chini ya utawala wa Papa, wavenice, mfalme wa Napoli, mtawala wa Milan na waflorence. Kuna mambo mawili yalikuwa muhimu kwa watawala hawa wote, kwanza hakuna mgeni aliyeruhusiwa kuivamia Italia kijeshi, na pili, hakuna mmoja kati yao aliyeweza achwa akitaka kujinyakulia, au kujiongezea eneo lake la utawala. Wale ambao ilikuwa ni muhimu zaidi kujilinda dhidi yao, walikuwa ni Papa na wavenice.
Ili kujilinda dhidi ya wavenice, ilikuwa ni lazima kwa tawala zote kuungana, kama walivyofanya wakati wakiilinda Ferrera. Na ili kumdhibiti Papa, walitumia wakuu wa familia zenye ushawishi za Roma, wa-Orsini na wa-Colonnesi. Koo hizi zilikuwa zimegawanyika katika kambi mbili zilizokuwa hasimu.
kujiimarisha kwao kijeshi karibu na Papa, kulimfanya awe muoga na asijihisi salama.

Japo kuna nyakati walitokea mapapa wenye nguvu kama Papa Sixtus, lakini hekima yake na utajiri havikuweza kumkomboa kutoka katika kudharaulika. Sababu ya hili jambo ni maisha ya mapapa kuwa mafupi. Sababu ndani ya miaka kumi, ambayo ndiyo wastani wa umri wa papa, asingeweza kuwadhibiti wa-Colonnesi au wa-Orsini. Ilitokea kuwa, kama Papa mmoja alifanikiwa kuwadhibiti wa-Colonessi. Alifuata mwingine ambaye kwa sababu ni adui wa wa-Orsini, akawa hana nia ya kuendelea kuwadhibiti wa-Colonessi, na badala yake akawaimarisha. Hili lilifanya mamlaka ya kisiasa ya Papa kudharauliwa ndani ya Italia.

Lakini alikuja Papa Alexander wa VI, huyu tofauti na watangulizi wake, alionyesha kuwa Papa anaweza kutumia pesa na jeshi kutimiza malengo yake. Kwa kumtumia Duke Valentino, na kujinufaisha na ujio wa wafaransa ndani ya Italia. Na matendo yote niliyokwishayaeleza, aliyofanya kupitia Duke; japo lengo halikuwa kulikweza kanisa bali Duke, mwisho wa siku matendo yake yalilikweza kanisa. Baada ya yeye kufa na Duke naye kufa, kanisa ndilo lilifaidi matunda ya matendo yao

Baada yake akafuata papa Julius. Huyu alikuta kanisa lina nguvu likiwa linaimiliki Romagna yote, na matajiri wa Roma na kambi zao zikiwa zimesambaratishwa na Papa Alexander. Pia alikuta vyanzo vya mapato vimewekwa, vyanzo ambavyo kabla ya Papa Alexander hakuna mtu aliyejihangaisha kuviweka. Julius alitumia mambo hayo mazuri na kuongezea mengine, aliiteka Bologna, aliwapora wavenice madaraka na kuwafukuza wafaransa kutoka Italia. Lakini alidai kuwa alifanya hayo yote si ili kujikweza bali ili kulikweza kanisa. Alifanikiwa kudhibiti uhasama wa wa-Orsini na wa-Colonnesi, na akaweka misingi ambayo iliwafanya wasiwe na nguvu tena. Kwanza, nguvu ya kanisa lililoimarishwa ilikuwa kubwa sana kwao, na pili, hakuteua makadinali kutoka kwa watu wao. Na makadinali ndiyo walikuwa sababu kubwa ya mgogoro kati ya koo hizi mbili. Makadinali, kwa maslahi yao, walikuwa wakichochea machafuko ndani na nje ya Roma. Wakuu walijikuta wakiingia kwenye machafuko kwa maslahi ya makadinali.

Mtukufu Papa Leo alipokuwa Papa, alikuta cheo cha Papa kikiwa na nguvu kubwa sana. Na tunatumaini kuwa, atakifanya cheo hicho kiheshimiwe zaidi kwa upole na matendo yake mema. Kama tu watangulizi wake walivyokiheshimisha kwa kutumia jeshi.
 
SURA YA 12

KUHUSU AINA ZA WANAJESHI, NA MAMLUKI.

Baada ya kuongelea aina mbalimbali za utawala, kuongelea sababu ya uimara na nguvu zao, na kuongelea mbinu watumiazo watu kuwa watawala. Sasa imebaki kuongelea juu ya njia za kuvamia na kujilinda, njia ambazo kila mmoja wa watawala niliowazungumzia wanapaswa kuzifahamu.

Nimeshazungumza kuwa, ni lazima kiongozi ajiwekee misingi mizuri na kujiimarisha, bila ya hivyo ataangushwa. Na misingi mikuu ya taifa lolote, liwe jipya, kongwe au mchanganyiko ni sheria nzuri na jeshi imara. Lakini kwa sababu huwezi kuwa na sheria nzuri bila ya kuwa na jeshi imara, basi sitazungumza juu ya sheria bali nitajikita kuzungumza juu ya jeshi.

Jeshi ambalo mtawala anatumia kulinda nchi yake linaweza tokana na raia wake, mamluki, jeshi la msaada au jeshi mchanganyiko.
Mamluki na jeshi la msaada ni yasiyofaa kitu na ni hatari. Yule ambaye analinda nchi yake kwa kutumia mamluki, hawezi kuwa salama kwenye madaraka yake. Jeshi kama hili huwa halina umoja, huwa lisilotii, lenye hila, uchu, wasioheshimu rafiki zao na waoga mbele ya adui. Pia hawaogopi Mungu, wala si waaminifu kwa binadamu wenzao.
Kila wanaposhambuliwa, lazima watashindwa. Kwa hiyo ukiwa na jeshi la aina hii; litakufilisi wakati wa amani, na wakati wa vita litaacha uporwe na adui zako. Hii ni kwa sababu hakuna kitu kitachowafanya waendelee kupigana zaidi ya malipo yao, malipo ambayo hayawezi kuwafanya wahatarishe uhai wao. Wako tayari kuwa wanajeshi wako wakati wa amani, lakini vita ikitangazwa wanakimbia na kutokomea.
Sitapata taabu kufanya watu waelewe hili, maana hali mbaya iliyonayo Italia kwa sasa, ni kwa sababu imekuwa ikiwaamini mamluki kwa miaka mingi.
Japo kabla ya sasa mamluki walisaidia baadhi ya watu kupata mafanikio, na walionyesha ushupavu, lakini mara tu adui kutoka nje anapoonekana, wao hujionyesha rangi yao halisi.
Hiyo ndiyo sababu Charles wa Ufaransa alisemwa kuwa aliiteka Italia kwa kutumia chaki(alipoingia Italia, alikuwa akipita na kuweka alama kwa chaki nyumba za kukaa wanajeshi wake). Iwapo mtu atasema tulishindwa sababu ya dhambi zetu, atakuwa amesema kweli, lakini si dhambi kama dhambi, bali zile zinazoonekana waziwazi(dhambi ya viongozi kutumia mamluki). Na sababu dhambi hii ilitendwa na viongozi, wao ndiyo walioadhibiwa.
Lakini napenda kueleza zaidi juu ya sifa mbovu za jeshi la namna hiyo. Makamanda wa mamluki huwa ni watu wenye uwezo, au wasio na uwezo. Kama ni mtu mwenye uwezo huwezi kumuamini, sababu muda wote atataka kujikweza, na anaweza kukupindua wewe muajiri wake au kupindua wengine kinyume na mapenzi yako. Kwa upande mwingine, kama makamanda si watu wenye uwezo basi utawala wako utaanguka. Na ikisemwa kuwa, mwanajeshi ni walewale iwe wawe mamluki au wasiwe mamluki, nitajibu kuwa; jeshi linapotumiwa na ufalme au jamhuri, basi kiongozi lazima awe ndiye mtu anayeliongoza. Kama ni jamhuri, basi inapaswa kutuma mmoja wa raia wake kuongoza, na kama hafai inambadilisha. Inamuondoa na kuweka mwingine, lakini kama ana uwezo basi inatakiwa kumdhibiti kwa sheria.
Na tumeona kutokana na uzoefu kuwa, wafalme na jamhuri wanapotegemea jeshi lao wenyewe hupata mafanikio makubwa. Lakini walipotumia mamluki, matatizo na kushindwa vilitokea.
Roma na Sparta zilidumu kwa miaka mingi wakiwa na jeshi imara na nchi huru. Kuna nyakati waswiswi walikuwa watu huru, na wenye jeshi bora zaidi duniani.

Juu ya jeshi la mamluki tunao mfano wa hapo kale; jeshi la wacarthagia. Walipopigana vita kwa mara ya kwanza na waroma wakitumia mamluki, walishindwa vibaya japo jeshi hilo liliongozwa na makamanda wacarthargia. Pia baada ya kifo cha Epaminondas, watheban wakamfanya Philip wa Macedonia kuwa kamanda wa jeshi lao. Baada ya kuwasaidia kupata ushindi mwanzoni, baadaye akageuka na kuwa dikteta juu yao. Wamilan nao hivyohivyo, Duke Philip alipokufa, walimuajiri Francesco Sforza ili kupigana na wavenice. Lakini yeye badala ya kupigana na wavenice, akaungana nao na kuwageuka wamilan na kuwapindua waajiri wake. Baba yake pia, aliyeitwa Giovanna, alikuwa ameajiriwa na Malkia wa Napoli. Bila kutegemewa akamtoroka na kumuacha bila jeshi, kisha akaanza kumshawishi ajisalimishe kwa mfalme wa Aragon.

Na kama ikisemwa kuwa wavenice, na waflorence waliweza kutanua utawala wao kwa kutumia jeshi la aina hii, na kuwa makamanda wa mamluki waliwatumikia kwa uaminifu bila kutaka kuwapindua. Nitajibu hivi; kuhusiana na waflorence, wao walikuwa na bahati, sababu kati ya wale makamanda ambao wangeweza kuwaletea matatizo, wengine walishindwa vitani, wengine walipatwa na upinzani na wengine walibadili uelekea na kufuatilia malengo mengine.

Mmoja wa wale walioshindwa vitani ni Giovanni Acuto, huyu uaminifu wake haujulikani kwa sababu hakufanikiwa vitani. Lakini kila mtu anaweza ona kuwa, endapo angeshinda, basi angewafanya waflorence kuwa chini yake. Wa-Sforza walikuwa na uadui wa kudumu dhidi ya wa-Bracceschi, na hivyo kila mmoja alidhibiti mwenendo wa mwenzake. Pia, malengo ya Fransesco Sforza yalibadilika na kuelekea dhidi ya Milan, wakati yale ya Braccio yakaelekea dhidi ya kanisa na ufalme wa Napoli.
Lakini acha tuongelee yaliyotokea hivi karibuni. Waflorence walimchagua Paolo Vitelli kuwa kamanda wao. Paolo ni kamanda hodari ambaye alianza akiwa askari wa kawaida tu na kupanda hadi kuwa kamanda anayeheshimika. Kama angefanikiwa kuiteka Pisa, basi wote mtakubaliana nami kuwa waflorence wangetawaliwa naye. Maana ingetokea ameungana na adui zao, wangekuwa kwenye hali mbaya sana. Na ili kumfanya awe upande wao ingewabidi wawe chini yake.

Juu ya wavenice, kama tukiangalia kukua kwa nguvu zao tutaona kuwa, walikuwa na nguvu na usalama walipotumia wanajeshi ambao ni raia wao. Lakini walipoanza kufanya vita kuelekea bara wakaachana na njia walizozijua vyema na wakaridhika na kufuata desturi za waitalia(za kutumia mamluki)

Mwanzoni walipoanza kujitanua kuelekea bara, kipindi ambacho walikuwa na eneo dogo tu la utawala waliheshimika vitani. Hawakuwa na cha kuogopa kutoka kwa makamanda wao. Lakini eneo lao lilipoongezeka chini ya Carmagnola waligundua kosa lao. Carmagnola alikuwa shupavu na hodari, na aliwaongoza kumshinda duke wa Milan. Lakini walipoona hayuko tayari kuendelea na vita, wakagundua kuwa hawawezi kupata ushindi tena chini yake. Na kwa kuogopa kupoteza maeneo waliyoyateka, hawakuweza kumfukuza, na ili kujilinda dhidi yake wakalazimika kumuua. Baada ya hapo wakawaajiri kuwa makamanda wao, Bartolommeo wa Brergamo, Roberto wa San Severino, Mkuu wa Pitgliano, na wengine kama hao. Ambao hatari ya kuwa nao haikuwepo kwenye ushindi, bali kushindwa. Mfano ni yaliyotokea huko Vaila, ndani ya siku moja walipoteza kile kilichopatikana kwa juhudi ya miaka mia nane. Ushindi unaoletwa na jeshi la mamluki huja polepole, na huwa si wa maana. Lakini kushindwa kwao huwa kwa haraka na kukubwa sana.

Kwa sababu mifano hii imenirudisha Italia, nchi ambayo kwa miaka mingi imekuwa inalindwa na mamluki, basi sina budi kuchimba zaidi kuhusu hili suala. Hili ni ili tujue chanzo cha Italia kuanza kutumia wanajeshi mamluki, na kuangalia namna ya kulirekebisha jambo hilo.
Inatakiwa kueleweka kuwa, baada ya watu kuanza kukataa kuwa chini ya Himaya ya Roma, na mamlaka ya kisiasa ya papa ilipoanza kuimarika, Italia ikaanza kugawanyika katika vitaifa vingi vidogovidogo. Miji mingi ikaasi dhidi ya viongozi wao, ambao hapo kabla waliungwa mkono na mtawala wa himaya ya Roma. Kanisa likaunga mkono watawaliwa kwa nia ya kujipatia nguvu za kisiasa. Miji hii ikapata watawala ambao hapo kabla walikuwa ni raia wa kawaida tu. Hivyo basi, Italia ikawa chini ya kanisa na jamhuri ndogodogo. Kanisa liliongozwa na makuhani na jamhuri zikiwa chini ya raia wa kawaida. Hawa wote hawakuwa na uelewa wa mambo ya kijeshi, hivyo wakaamua kuajiri mamluki.

Inasemekana kuwa mamluki wa kwanza kuajiriwa alikuwa ni Alberigo wa Conio huko Romagna. Wengine ni Braccio na Sforza ambao katika nyakati zao ndiyo walikuwa waamuzi(mabwana) wa Italia.
Baada ya hao walikuja wengine ambao mpaka leo wanaendelea kuwa mabwana wa Italia. Tulichopata kutokana na uwezo wao ni nchi yetu kuvamiwa na Charles, kuporwa na Louis, kuharibiwa na Ferdinand, Na kudharauliwa na wasiswi.

Jambo la kwanza la mamluki hawa lilikuwa ni kulidharaulisha jeshi la waenda kwa miguu, ili kulipa sifa jeshi lao. Walifanya hivi kwa sababu hawakuwa na maeneo ya kiutawala, hivyo walitegemea kazi yao ya jeshi. Waliona kuwa wanajeshi wachache waendao kwa miguu hawatakuwa na manufaa yoyote, na iwapo wakiwa wengi wangeshindwa kuwahudumia. Kwa sababu hiyo wakawa wanaegemea kwenye jeshi la wapanda farasi, jeshi dogo ambalo waliona litakuwa bora na rahisi kulitunza. Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba ndani ya jeshi la watu ishirini elfu, ulikuwa huwezi pata wanajeshi elfu moja waendao kwa miguu.
Pia walijitahidi kuepuka hatari na kujichosha wakati wa vita. Hawakuuana bali walichukuana mateka ambao baadaye waliachiwa bila fidia yoyote. Walijiepusha kuvamia miji usiku kiasi kwamba watu waliozingirwa hawakujihangaisha kulinda miji yao usiku. Hawakufanya vita majira ya baridi, na kambi zao hazikutengenezwa mahandaki wala matuta ya kuzilinda.
Mambo yote hayo yaliruhusiwa kulingana na kanuni zao za kijeshi walizojiwekea. Kanuni walizozianzisha ili kuepuka kuchoka na hatari. Matokeo yake ilikuwa ni kuifanya Italia kudharaulika na kutawaliwa na wengine.
 
Sura ya 12 inaelezea ubaya wa kutumia Mamluki, au kutegemea jeshi la msaada. Sura nzuri sana.
 
SURA YA KUMI YA 13

KUHUSU JESHI LA MSAADA, JESHI MCHANGANYIKO NA JESHI LA KITAIFA.

Jeshi lingine lisilo na manufaa ni jeshi la msaada. Kusema jeshi la msaada, namaanisha jeshi ambalo linaletwa na mtawala uliye chini yake, au mwenye nguvu kuliko wewe ili kukusaidia na kukulinda baada ya kumuomba msaada.
Hii ni kama ilivyotokea hivi karibuni. Papa Julius II alipoona tabia mbovu za mamluki aliowaajiri kwenye uvamizi wa Ferrara, akaamua kutumia jeshi la msaada. Alikubaliwa na mfalme Ferdinand wa Hispania na kupewa farasi na wanajeshi waendao kwa miguu.

Jeshi la msaada linaweza kuwa na wanajeshi bora na hodari, lakini haliwezi kuwa na manufaa kwa yule anayeliita limsaidie. Kama likishindwa basi anakuwa ameanguka, na likishinda basi anakuwa mfungwa au mtumwa walo, akilazimika kulinyenyekea.
Historia ya zamani imejaa mifano inayoonyesha hiki lakini sitaacha kuzungumzia mfano wa Papa Julius, mfano ambao ndiyo wa karibuni zaidi na bado upo kwenye akili za watu. Katika pupa yake ya kupata Ferrara, aliamua kujiweka katika mikono ya mgeni. Japo aliokoka kwa bahati, na aliepuka madhara ya matendo yake yasiyo na hekima.
Mara baada ya jeshi lililokuja kumsaidia kushindwa huko Ravenna, waswiswi wakamshukia. Kwa mshangao wao na wa kila mmoja wakawatimua washindi kutoka nchini. Kwa hiyo hakutekwa na adui zake maana walitimuliwa. Aliokoka si kwa jeshi lililokuja kumsaidia bali kupitia kwa waswiswi, kwa bahati tu.
Kwa sababu waflorence walikuwa hawana jeshi, waliamua kuleta wafaransa elfu kumi wakati wa kuizingira Pisa. Kitendo hicho kilifanya wapatwe na hali ngumu kuliko wakati mwingine wowote.
Ili kujilinda dhidi ya jirani zake, mtawala wa Constantinople aliwaita wanajeshi elfu kumi wa kituruki. Baada ya vita kuisha wanajeshi hao waligoma kuondoka. Na huu ndiyo ulikuwa mwanzo wa wagiriki kutawaliwa na makafiri.

Basi acha yule ambaye hataki kufanikiwa atumie jeshi la msaada, jeshi la msaada ni hatari kuliko mamluki. Wanajeshi wa aina hii huwa na umoja na huongozwa na makamanda wao. Japo mamluki wanaweza kukudhuru hata baada ya kupata ushindi, lakini wanahitaji muda mrefu na fursa ya kufanya hivyo. Sababu ni kuwa hawa huwa katika vikosi vilivyogawanyika, na wewe ndiye huwapanga na kuwalipa. Yule uliyemuweka kuwaongoza, hataweza kuwa na mamlaka juu yao kiasi cha kuwa hatari na kukudhuru kwa haraka. Kiufupi, tatizo kubwa la kutumia mamluki ni uoga na kutegea kwao vitani, lakini jeshi la msaada hatari yao ipo kwenye ushujaa wao.
Viongozi wenye hekima mara zote wameepuka majeshi ya msaada, na wameyategemea majeshi yao tu. Wameonelea kuwa ni bora kushindwa wakiwa na jeshi lao, kuliko kushinda wakiwa na jeshi la msaada. Walijua kuwa huwezi kupata ushindi wa kweli kwa kutumia jehi la kigeni.

Siwezi kusita kutoa mfano wa Cesare Borgia na matendo yake. Aliingia Romagna kwa jeshi la msaada ambalo karibu wanajeshi wote walikuwa wafaransa. Kwa msaada wao alifanikiwa kuteka Imola na Forli. Lakini baada ya muda aligundua kuwa jeshi la namna ile haliwezi kuaminiwa, hivyo akaamua kutumia jeshi la mamluki ambalo alifikiri litakuwa afadhali na salama. Hivyo akawaajili wa-Orsini na wa-Vitelli. Lakini hawa pia akagundua ni wadanganyifu na wenye hila, hivyo akaamua kuachana nao na kuamua kutumia jeshi lake mwenyewe. Tunaweza ona kwa urahisi tofauti ya majeshi haya kwa kuangalia uwezo alioonyesha Duke alipowategemea wafaransa, alipowaajiri wa-Orsini na wa-Vitelli, na alipoamua kutumia jeshi lake mwenyewe. Tutaona kuwa uwezo wake ulikuwa mkubwa, na kila mtu alimheshimu pale alipojirudi na kutumia jeshi lake mwenyewe.

Ningependa kuendelea kutoa mifano iliyotokea Italia, lakini ngoja sasa tuone mfano wa Hiero wa Sairakusi ambaye nilikwisha mtaja huko nyuma. Baada ya kufanywa kuwa kiongozi wa jeshi na wasairakusi, alitambua mara moja kuwa majeshi ya mamluki, kama yaliyotumika na waitaliano ni yasilofaa. Na kwa vile hakuweza kuendelea kuwatumia na hakuweza kuwafukuza, akaamua kuwachinja wote na baada ya hapo akatumia jeshi la wazawa tu.

Hapa pia naweza kukazia kwa kutumia mfano kutoka katika agano la kale. Daudi alipojitolea mbele ya Sauli ili kwenda kupigana na Goliati, mfilisti; Sauli alimtia moyo kwa kumpatia mavazi yake ya kijeshi na silaha zake. Mara tu Daudi alipoyavaa akaona kuwa hayatamfaa hivyo akayavua na kusema; kwa sababu hajayazoea hataweza kupigana vema. Badala yake akachagua kupambana na kupigana na adui yake akiwa na kombea na panga lake. Kwa maneno mengine, mavazi ya vita ya wengine ni mapana sana, au ni madogo sana kututosha. Yatatupwaya au yatatubana. Baba yake na mfalme Louis wa XI, Charles wa VII, ambaye kwa bahati na ushujaa wake aliikomboa Ufaransa kutoka utawala wa waingereza, aliona umuhimu wa kujiimarisha na kujilinda kwa kutumia jeshi la taifa. Hivyo akatoa tamko juu ya raia wake kushiriki katika utumishi wa kijeshi. Lakini baadaye, mwanaye, mfalme Louis, akaachana na jeshi la taifa na akaanza kukodi mamluki kutoka Uswiswi. Kosa hilo liliendelea kufanywa na watawala waliofuata, na limekuwa sababu ya matatizo na hatari ambayo Ufaransa imejikuta imetumbukia. Kwa kuwatumia wasiswi, jeshi la taifa la Ufaransa likadharaulika, na wakabaki kuwa tegemezi kwa wanajeshi kutoka nje. Na kwa sababu ya kuwategemea sana waswiswi wamefika hatua wanajiona hawawezi kufanya chochote bila wao.
Hivyo basi, wafaransa wanajiona ni dhaifu mbele ya waswiswi, na bila msaada wai hawawezi kupigana.

Kwa hiyo, jeshi la Ufaransa ni mchanganyiko. Kwa sehemu ni jeshi la taifa na sehemu nyingine ni mamluki. Jeshi la aina hiyo ni bora kuliko lile la mamluki au la msaada, lakini si bora kama lile la taifa. Mfano wa Ufaransa unaonyesha hilo, Ufaransa ingekuwa dola imara na isiyoshindwa iwapo lengo la Charles VII la kuunda jeshi la taifa lingeendelezwa. Lakini watu kwa kukosa uelewa, hufanya mabadiliko ambayo mwanzoni huwa mazuri lakini yanakuwa yameficha sumu yake, ni kama tu nilivyozungumza kuhusu magonjwa. Na haiwezi semwa kuwa kiongozi ana busara, isipokuwa awe na uwezo wa kutambua mabaya kabla hayajajionyesha waziwazi. Na viongozi wa aina hii ni wachache sana.

Kama tukiangalia sababu zilizosababisha kuanguka kwa himaya ya Roma, tutaona kuwa chanzo chake ni waroma kuajiri mamluki wa ki-goth. Walipoanza kufanya hivyo tu, nguvu za Roma zikaanza kupungua na ustawi wao ukahamia kwa wa-goth.
Kiufupi niseme kuwa, hakuna utawala unaoweza kuwa salama bila ya kuwa na jeshi la taifa. Kinyume na hivyo, uwepo wake utategemea bahati tu. Taifa kama hilo halitakuwa na nguvu ya kujilinda dhidi ya adui.

Watu wenye hekima waliona kuwa, hakuna kitu dhaifu na chenye kudumu kwa muda mfupi kama sifa ya nguvu ambayo msingi wake siyo jeshi la taifa. Kwa kusema jeshi la taifa, namaanisha lile linaloundwa na raia na si mamluki wala jeshi la msaada. Njia za kuunda jeshi la taifa zinafahamika na ni rahisi tu. Inatakiwa tu kufuata kanuni nilizozianisha hapo juu, na nisisitize kuwa ni muhimu kuzifuata kanuni hizo. Pia yafaa kuangalia tabia ya Philip, baba wa Alexander mkuu, na falme zingine na jamhuri ambazo ziliweza kutumia majeshi yao wenyewe.
 
SURA YA 14

KUHUSU MAJUKUMU YA KIONGOZI KWENYE MASUALA YA JESHI.

Mawazo ya kiongozi yanatakiwa kuwa juu ya jeshi kuliko kitu kingine chochote. Lazima ajue mafunzo na taratibu zake. Lazima aangalie masuala kijeshi kama kitu cha pekee kabisa, raia na wanajeshi wanategemea kiongozi kuwa na ujuzi wa kijeshi na vita. Vita haiwafanyi tu wale waliopata uongozi kwa kurithi kuendelea kuwa viongozi, bali inawafanya hata raia wa kawaida kupanda na kuwa viongozi.
Tumeona viongozi ambao wanajishughulisha sana na anasa kuliko masuala ya kijeshi wakipoteza madaraka yao. Na kama kudharau masuala ya vita na jeshi ni sababu kuu ya viongozi kuanguka, basi kuwa hodari kwenye masuala hayo ni njia ya uhakika zaidi ya kufikia madaraka. Kwa sababu ya ujuzi mkubwa wa masuala ya kijeshi, Fransesco Sforza aliweza kutoka kuwa raia wa kawaida hadi kuwa Duke wa Milan. Lakini vizazi vyake vilipoamua kuepuka taabu, na hali ngumu za maisha ya kijeshi, waling'olewa kwenye uongozi na kuwa raia wa kawaida. Madhara mengine ya kutokuwa na ujuzi wa mambo ya kijeshi ni kudharaulika, na kiongozi anatakiwa kujilinda sana asidharaulike.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya mtu mwenye jeshi na yule asiye na jeshi. Na haiingii akilini kwa mtu mwenye silaha(jeshi) kujinyenyekeza kwa yule ambaye hana, au kwa mtu asiye na silaha kuwa salama kati ya wenye nazo.
Kwa sababu ya kudharauliana na kutoaminiana, binadamu hawawezi kufanya mambo vizuri kwa ushirikiano. Kwa sababu hiyo na kama nilivyokwisha sema, kiongozi ambaye hana uelewa wa mambo ya kijeshi, pamoja na matatizo mengine, atadharauliwa na wanajeshi wake, na yeye pia hatawaamini. Kiongozi hatakiwi kuruhusu kukengeushwa na mambo mengine hadi akasahau masuala ya vita na jeshi, tena wakati wa amani ndiyo anatakiwa kujishughulisha zaidi na mambo hayo kuliko wakati wa vita. Anaweza fanya mambo hayo kwa njia mbili; kwa kufanya mazoezi ya kijeshi au kwa kujifunza masuala ya kijeshi.

Kuhusiana na mazoezi, mbali ya kuwafanya wanajeshi wake kuwa na nidhamu na waliofunzwa vizuri, pia yeye mwenyewe anatakiwa kujiimarisha kimwili na kuuzoeza kuhimili hali ngumu na kuchoka. Wakati huohuo atapata maarifa juu ya maeneo yanayomzunguka, milima ilivyo, mabonde na tambarare zake, mito, mabwawa na kuwa karibu na wanajeshi wake.
Maarifa kama hayo ni muhimu kwake kwa njia mbili; kwanza anajifunza na kuijua nchi yake, hilo linamfanya ajue njia nzuri ya kuilinda. Pia anajifunza sifa za wilaya zake ambazo hakuwahi kuzitembelea. Kwa mfano; mabonde, milima, tambarare, misitu na mabwawa ya Tuscany kwa kiasi fulani yanafanana na maeneo mengine. Hivyo, mtu anaweza kuelewa mikoa mingine ilivyo kwa kuangalia sura ya nchi ya Tuscany. Kiongozi ambaye hana maarifa haya anakuwa anakosa sifa ya kuwa kamanda mzuri, sababu sifa hiyo inamfanya awe na uwezo wa kumfanyia adui shambulizi la kushtukiza, aweze kuchagua sehemu nzuri ya kuweka kambi, jinsi ya kuongoza jeshi lake linaposonga, jinsi ya kujipanga kwaajili ya pambano na jinsi ya kupanga jeshi kwaajili ya kuzingira.

Moja ya ushauri ambao Philopoemon, kiongozi wa wa-Achaia alipata kwa wanahistoria ni huu; wakati wa amani, yeye alikuwa anafikiria masuala ya vita muda wote. Alipokuwa akitembea maeneo mbalimbali ya nchi akiwa na rafiki zake, alikuwa anasimama na kuzungumza nao kuhusu masuala ya vita. Alikuwa akisema, 'Kama adui akiwa kwenye kile kilima na sisi na jeshi letu tukajikuta hapa, nani atakuwa kwenye eneo linalofaa zaidi? Jinsi gani tunaweza msogelea kwa mpangilio bila kujihatarisha? Kama tukilazimika kukimbia, tutakimbilia upande gani? Na iwapo akitukimbia, ni jinsi gani tunaweza kumkimbiza?' Kwa namna hii aliweza kuwafanya rafiki zake waelewe hali zote zinazoweza kulipata jeshi. Alisikiliza maoni yao na kutoa yake na sababu zake. Kwa mtindo huu akawa na uelewa mkubwa wa masuala ya vita, na hata vita halisi ilipotokea, hakupata utata wowote wa kuongoza sababu alikuwa ameshajiandaa kimbinu.

Kuhusu kujifunza, kiongozi anatakiwa kusoma historia. Humo anaweza kujifunza matendo ya watu hodari, ataona jinsi walivyofanya wakati wa vita, na atachunguza sababu za kushinda na kushindwa kwao. Hilo litamuwezesha kuepuka sababu zilizoleta kushindwa na kuiga zikizoleta ushindi.
Zaidi ya yote, kama tu watu hodari wa zamani walivyofanya, anatakiwa kuiga watu waliojulikana kwa uhodari na kusifiwa, matendo ya watu hao anatakiwa kuyaweka akilini siku zote. Inasemwa kuwa Alexander mkuu aliiga matendo ya Achilles, Kaisari naye alimuiga Alexander mkuu na Scipio alimuiga Cyrus.
Na yeyote aliyesoma maisha ya Cyrus kama yalivyoandikwa na mwanahistoria wa Athene, Xenophon, atagundua jinsi Scipio alivyofanikiwa kupitia kumuiga Cyrus kikamilifu. Aliiga matendo yake ya ukarimu, utoaji na urafiki. Aliiga sifa za Cyrus kama zilivyoelezewa na Xenophon.
Kiongozi mwenye busara anatakiwa kutumia njia hizi; Hatakiwi kukaa kizembe wakati wa amani, bali anatakiwa kufanya kazi kwa bidii, na kutumia vizuri nafasi hiyo kujiimarisha, akijiweka tayari na kuwa imara wakati wa hatari, au mambo yakimuendea ndivyo sivyo.
 
Hapa kuna somo kuwa wakati wa neema ndiyo wakati wa kupambana hasa. Wakati wa taabu ukifika uwe tayari.
 
SURA YA 15

SIFA AMBAZO WATU, NA HASA VIONGOZI, HUPONGEZWA AU HUDHARAULIWA KWA KUWA NAZO.

Sasa inabidi tuangalie ni namna gani mfalme anatakiwa kujiendesha mbele ya wananchi na rafiki zake. Sababu najua kuwa wengi wameandika kuhusu hili suala, naogopa nisije kuwa mwenye kujifanya kujua sana iwapo nitaliongelea. Hivyo, mimi nitaandika yale tu ambayo hayakuandikwa na wengine.

Lakini kwa kuwa lengo langu ni kuandika vitu vyenye msaada kwa atakayenielewa, basi nimeonelea ni vyema kuandika ukweli wa mambo na si maoni na nadharia. Jamhuri na falme nyingi ziliwaziwa lakini hazikuwahi kusimama. Namna tunayoishi, na namna ambayo tungependelea tuishi ni vitu viwili tofauti kabisa.
Hivyo basi, yule anayetaka kuwa mwema kwenye kila jambo ataangamizwa na watu wabaya, ambao ndiyo wengi. Ni muhimu kiongozi anayependa kuwa madarakani ajifunze kutotenda mema. Na pia ajue kutumia au kutotumia wema wake kulingana na hali.

Tukiachana na sifa za kumpamba kiongozi, na tukiangalia zile za kweli tu, naona kuwa watu wote wanapoongelewa, na hasa viongozi, wakiwa ni watu wa cheo cha juu zaidi, sifa zao huwa kwenye kundi la kudharauliwa(kulaumiwa) au kupongezwa. Mmoja anachukuliwa kama mtu wa watu na mwingine kuwa kauzu. Mmoja akiwa ni mvumilivu hata katika mambo ambayo ana haki, na mwingine akiwa na muelekeo wa kuchukua hata visivyo haki yake. Mmoja ni mtoaji na mwingine anataka vitu kwa pupa. Mmoja ni katili na mwingine ana moyo wa upole. Mmoja si mwaminifu na mwingine mwenye uaminifu. Huyu ni muoga na yule ni jasiri. Mmoja ni mstaarabu na mwingine ni mshenzi. Huyu hana mambo mengi, na yule ni mwenye hila. huyu ni mwenye msimamo, na mwingine anapelekeshwa, Mwingine ni muumini mwaminifu na mwingine ni asiyeamini. Ipo hivyo.
Kila mtu ninayemjua atakubaliana nami kuwa, kiongozi anatakiwa kuwa na sifa nzuri tu kati ya hizo zilizoainishwa hapo. Lakini kiongozi naye ni binadamu tu, hivyo ni vigumu kuwa nazo na kuzitenda zote. Anachopaswa kufanya, ni kuwa makini kuepuka kuonekana ana zile sifa mbaya. Sifa ambazo zinaweza kuhatarisha utawala wake. Na kama anaweza, aepuka na zile mbaya ambazo si hatari kwa utawala wake.
Lakini pia, hatakiwi kuogopa kupewa sifa mbaya iwapo kuzitenda kunaulinda utawala wake. Sababu, kama akichunguza kwa makini, ataona kuwa kuna matendo yanayoonekana ni yenye kufaa, lakini yanayoweza kuwa ndiyo maangamizi yake. Na mengine yanayoonekana ni mabaya, lakini ndiyo yanayoleta usalama na ustawi.
 
Kiongozi anatakiwa kujitahidi kuonekana na sifa nzuri. Lakini asisite kutenda sifa mbaya iwapo kufanya hivyo kunalinda utawala wake.
 
11 Reactions
Reply
Back
Top Bottom