Niccolo Machiavelli na kitabu chake The Prince (Of principality). Kwa kiswahili; kuhusu Uongozi. Tusome na kujadili

SURA YA 16

KUHUSU WEMA(UTOAJI) NA UKAUZU(UBAHILI)

Nianze kwa kuzungumzia hiyo sifa ya kwanza. Nasema kuwa, ni vizuri kujulikana kwa sifa ya utoaji, lakini utoaji bila kujulikana ni jambo lenye hasara. Japo kutoa ni kitu kizuri na kinachopaswa kufanywa, lakini kama haijulikani kuwa umetoa hautaweza kuepuka kuitwa bahili(kauzu).
Kwa hiyo, ukifanya jambo la utoaji, na ili dunia ikufahamu kwa sifa hiyo, inatakiwa kufanya hivyo kwa kujionyesha. Tofauti na hilo ni kuwa, kiongozi mwenye muelekeo wa utoaji, na ili kudumisha sifa hiyo, atatumia mali zake zote kufanya hivyo. Na atalazimika kuwatwisha watu wake mzigo mkubwa wa kodi, na baadaye atahamia kwenye kutaifisha mali za watu na kutafuta pesa kokote ziliko. Kufanya hivyo kutamfanya achukiwe na wananchi wake, na kwa kuwa amekuwa maskini sababu ya kutoa, wananchi wake watamdharau.
Kwa hiyo, kwa kuwa utoaji wake umewakasirisha wengi kwa kodi, na kuwanufaisha wachache, atajikuta kwenye hali mbaya kuliko alivyokuwa mwanzo. Zaidi ya hilo, atajikuta hatari alizojitahidi kuziepuka zipo mbele yake. Kwa kugundua hili, na baada ya kutafuta alipokosea, mara moja atageuka na kuwa bahili(kauzu).

Hivyo basi, kwa kuwa kiongozi hawezi kufanya wema ili ajulikane kwa sifa hiyo bila kujiletea matatizo, na kama ana busara, hatojali iwapo watu watamwita kauzu(bahili). Mtu wa aina hii, baada ya muda watu wataanza kumuona ni mwema zaidi. Pale ambapo kupitia ubahili wake anakuwa na pesa za kutosha kujilinda dhidi ya adui bila kuwapa mzigo wa kodi wananchi wake. Na zaidi ni kwamba, anafanya wema kwa raia wengi bila kuwaumiza kwa kodi huku akiwa na sifa ya ukauzu(ubahili) kwa wale ambao hawapatii kitu, na hawa ni wachache tu.

Katika nyakati zetu hatujaona viongozi wanaofanya mambo makubwa, isipokuwa wale wanaosifika kwa ukauzu. Wengine wote waliingia matatizoni. Papa Julius II baada ya kujinadi kuwa na sifa ya wema ili kupata upapa, hakufanya jitihada zozote za kuendelea na sifa hiyo alipokuwa vitani dhidi ya mfalme wa Ufaransa. Lakini aliendesha vita zake bila kutoza watu wake kodi yoyote, aligharamia vita kutoka katika akiba yake aliyokuwa ametumia muda mrefu kuitunza.
Kama mfalme wa sasa wa Hispania angekuwa na sifa ya wema, asingeweza kufanya na kufanikiwa katika mambo mengi aliyoyafanya.

Kwa hiyo, kama kiongozi anaweza kuepuka kupora mali za wananchi wake, kutofilisika, ameweza kujilinda na kuepuka kutodharaulika, hatakiwi kujali kupewa sifa ya ukauzu. Hiyo ni moja ya sifa inayomuwezesha kubaki madarakani.
Na mtu akipinga na kusema kuwa wema ulimfanya Kaisari kushika madaraka, na kuwa kuna wengine wengi waliopanda vyeo vikubwa kwa kuwa wema, nitajibu hivi; 'unaweza kuwa tayari ni kiongozi au unataka kuwa kiongozi, kama ni kiongozi, wema utakutia matatizoni, na kama unataka kuwa kiongozi ni muhimu watu wakuone ni mwema. Kaisari alikuwa anataka kuwa mtawala wa Roma, lakini baada ya kupata cheo hicho angeendelea na matendo yake ya wema, na utoaji bila kubana matumizi, himaya ya Roma ingeanguka.'

Mtu akiendelea kubisha kuwa, viongozi wengi waliosifika kuwa ni wema sana waliweza kufanya mambo makubwa kwa kutumia majeshi yao. Nitajibu hivi; kiongozi anaweza kutumia mali yake na ya wananchi wake, au ya watu wengine kabisa. Kama anatumia mali yake au ya wananchi wake, lazima awe makini katika matumizi. Lakini kama mali hizo ni za watu wengine hatakiwi kujibana katika kuzitumia kutenda wema. Sababu kiongozi anayeongoza jeshi lake yeye mwenyewe, na anayelihudumia kwa kupora wengine na michango ya lazima, huku akitumia mali zao apendavyo, hatakiwi kujibana katika kuhudumia jeshi lake.
Vinginevyo wanajeshi wake wataacha kumfuata.
Kitu ambacho si chako, wala si cha wananchi wako, unatakiwa kukigawa bila kujibana, kama tu walivyokuwa Cyrus, Kaisari na Alexander. Kugawa mali ya wengine hakukuharibii sifa bali kunaiimarisha zaidi. Kitu kitakachokuletea matatizo ni kutumia mali yako mwenyewe, na hakuna sifa inayomuangamiza mtu haraka kama ya kuwa mwema(mtoaji); kadri unavyoitenda, ndivyo unavyopoteza uwezo wa kuitenda. Hilo linakufanya uwe fukara na mtu wa kudharaulika, au labda kwa kuepuka ufukara uamue kuwa mporaji(ukichukua mali za raia wako kwa nguvu), jambo litakalokufanya uchukiwe. Utu wema husababisha moja kati ya hayo mambo mawili(kudharauliwa au kuchukiwa) na kiongozi anatakiwa kujilinda sana dhidi ya hizi sifa mbili.

Kinyume chake; ni jambo la busara kuvumilia kuitwa kauzu(bahili). Sifa hiyo huleta aibu lakini haikufanyi uchukiwe. Lakini tamaa ya kusifiwa kuwa ni mwema(mtoaji), hupelekea kuwa mporaji, na hilo husababisha uchukiwe na kudharaulika pia.
 
Machiavelli anasema kiongozi anayetaka kuonekana mwema mbele za watu mwisho wake huwa mbaya. Anasema jambo la muhimu ni kuonekana una sifa nzuri na si kutenda sifa nzuri.

Mwanzo pale anasema kama unataka kutenda wema/hisani, fanya hivyo kwa kijionyesh(sherehe, picha, vyombo vya habari nk). Vinginevyo watu hawatajua ka wewe ni mwema.
 
SURA YA 17

KUHUSU UKATILI, REHEMA NA IWAPO KUPENDWA NI BORA KULIKO KUOGOPWA.


Kwa kuangalia sifa nilizozitaja hapo juu, nasisitiza kuwa; kila kiongozi anatakiwa ajitahidi asifike kwa rehema na si ukatili. Lakini anatakiwa kuwa makini ili watu wasije kutumia sifa yake hiyo vibaya. Cesare Borgia alikuwa na sifa ya ukatili, lakini ukatili wake uliweza kuisimamisha na kuiunganisha Romagna, pia aliifanya kuwa na amani na utulivu
Kwahiyo basi, iwapo tutaangalia vitu kwa uhalisia wake, tutaona kuwa alikuwa na rehema kuliko watu wa Florence, watu ambao ili kuepuka kuonekana ni wakatili, walivumilia kuangushwa, na kusambaratishwa kwa Pistoja na makundi hasimu.

Kiongozi anatakiwa kutojali ikiwa ataonwa katili, iwapo hilo linamuwezesha kuunganisha watu wake na kuwafanya kuwa watiifu na watulivu. Mwisho wa siku, yule anayezimisha machafuko ndiye ataonekana ni mwenye rehema, kuliko yule ambaye anaruhusu mambo yaendelee hadi kusababisha uharibifu wa mali na umwagaji wa damu. Jambo hili huathiri taifa zima wakati ukatili huathiri watu wachache tu.

Na zaidi ya yote ni kuwa, ni vigumu kwa kiongozi mpya kuepuka sifa ya kuonekana katili, sababu ni kuwa; taifa(au uongozi) jipya huwa na hatari nyingi sana. Kama ambavyo mshairi Virgil alivyoandika maneno ya muanzilishi wa jiji la Carthage, malkia Dido:-

'Ugumu wa mambo, upya na upana wa utawala wangu,

Unanilazimisha kuulinda.'

Hata hivyo, kiongozi mpya hatakiwi kuwa mtu wa kwanza kuzua taharuki, wala mtu wa kuamini watu kupita kiasi. Bali anatakiwa kuwa muangalifu ili kuamini watu kupita kiasi kusijemuweka hatarini, na kushuku kusiko na msingi kusije fanya watu wakaacha kumuunga mkono.

Na hapa linakuja swali, je, kupendwa ni bora kuliko kuogopwa, au kuogopwa ni bora kuliko kupendwa? Linaweza jibiwa kwamba; binadamu tungependelea kuogopwa na kupendwa kwa wakati mmoja, lakini kwa sababu ni vigumu kwa uoga na upendo kukaa pamoja, hivyo tukiamua kuchagua, ni bora sana kuogopwa kuliko kupendwa. Inajulikana wazi kwamba binadamu ni viumbe wasio na shukrani, wenye kubadilika, wenye hila, wenye walafi, wanakuunga mkono wakiwa wanapata faida tu, na kama nilivyosema huko nyuma; wakati wa amani watakuwa tayari kujitolea maisha yao, ya watoto wao na mali zao kwaajili yako, lakini wakati wa taaabu watakugeuka. Kiongozi ambaye hajiimarishi na anawategemea ataangushwa. Urafiki wako nao si kwa sababu ya upendo wao kwako au uaminifu wao, bali ni kwa sababu ya maslahi. Hawawezi kuwa washikamanifu siku zote, badala yake wao hutufelisha pale tunapowahitaji sana.

Pia, watu hawajali na ni rahisi kumkosea mtu anayetafuta kupendwa, kuliko yule anayetafuta kuogopwa. Upendo hushikiliwa na uaminifu na kutendeana wema, lakini kwa sababu binadamu ni viumbe wasio wakamilifu, huvunja mambo hayo pale mtu anapoona anaweza pata maslahi binafsi, lakini uoga huundwa na wasiwasi juu ya adhabu, na hii haifeli katika kunyoosha mtu.

Hata hivyo, kiongozi anatakiwa kufanya aogopwe kwa namna ambayo hata kama haitafanya watu wake wampende, imfanye wasimchukie. Inawezekana kabisa kwa mtu kuogopwa bila kuchukiwa, na hili linawezekana iwapo atajiepusha na mali za raia wake na wake zao. Na ikitokea akalazimika kumuua mtu, anatakiwa kufanya hivyo pale tu anapokuwa na sababu nzuri. Lakini kikubwa zaidi ni kujiepusha na mali za wananchi wake. Ni rahisi kwa mtu kusahau kifo cha baba yake kuliko kusahau kupotea kwa urithi alioachiwa naye. Haitakiwi kutafutiza visababu vya kutaifisha mali za watu wako, na yule anayeanza kuishi kwa kutaifisha mali, kila siku atakuwa anatafuta sababu za kufanya hivyo. Lakini sababu za kuua watu ni chache na baada ya muda zinakuwa hazipo kabisa.

Jambo jingine, kiongozi anapokuwa na jeshi lake, akiongoza jeshi kubwa, anatakiwa kutojali kuonekana katili. Bila ya kiongozi kuwa na sifa hiyo, hakuna jeshi analoweza kulinyoosha na kulisimamia vizuri. Pamoja na kuwa na sifa zingine, Hannibal alisifika kwa sifa hii. Hasa kwa kuwa alikuwa na jeshi kubwa sana, jeshi lililoundwa na watu wa mataifa mbalimbali. Hakuna uasi uliotokea, na hawakufanya uhaini kwa kiongozi wao iwe wakati wa amani au wa taabu. Hili tunaweza kulihusisha na ukatili wake uliopita kiasi. Huo, pamoja na uhodari wake, vilimuwezesha kuheshimika na kuogopwa machoni pa wanajeshi wake. Bila ukatili, sifa zingine zisingemletea mafanikio aliyoyapata.

Waandishi wasioona mbali wanasifia mafanikio yake, lakini wanashutumu sifa kuu iliyowezesha yapatikane. Sifa zake nyingine zisingemfanya awe hodari kama alivyokuwa. Tunaweza kuona hilo kwa kumuangalia Scipio, mmoja kati ya makamanda hodari, si tu kwa wakati wake bali katika historia nzima. Jeshi lake lilipomuasi huko Hispania, sababu haikuwa nyingine bali huruma zake za kupita kiasi. Aliwapa uhuru uliopitiliza wanajeshi wake, kitu ambacho hakiendani na nidhamu ya jeshi. Hilo pia ndilo lililomdhoifisha Fabius Maximus hadi kufikia kuitwa mharibifu wa himaya ya Roma na bunge. Aliambiwa kuwa.' Kuna wengi ambao wanajua sana kujizuia kufanya makosa, kuliko jinsi ya kuwarekebisha wengine wanapokosea.' Tabia hii baada ya muda huharibu sifa hata za mtu kama Scipio iwapo angeiendeleza, na angeendelea kuwa kamanda. Lakini kwa sababu alikuwa chini ya bunge, sifa hii yenye madhara haikuonekana, na baadaye ikawa inaonekana kama ni ya maana.

Tukirudi kwenye swali kuhusu kupendwa na kuogopwa, nihitimishe kwa kusema; sababu kupendwa kwa kiongozi kunategemea wananchi wake, na kuogopwa kunategemea mwenendo wake, kiongozi mwenye busara anatakiwa kuwa makini na kuimarisha mwenendo wake na si kutegemea maoni ya wengine. Lakini kama nilivyosema, anatakiwa kufanya yote anayoweza kuepuka kuchukiwa.
 
SURA YA 18

JINSI UAMINIFU WA KIONGOZI UNAVYOPASWA KUWA.

Kila mtu anaelewa jinsi ilivyo na manufaa kwa kiongozi kuwa muaminifu, na kuishi kwa haki, bila ya kuwa mtu mwenye hila. Lakini tumeona yaliyotokea katika wakati wetu. Viongozi wenye hila, ambao hawatendi wanayoyasema ndiyo walioweza kufanikisha mambo makubwa. Na mwisho wa siku ndiyo waliowashinda wale waliofanya mambo kwa uaminifu. Ieleweke kuwa, kuna njia mbili za kushindana. Njia ya kwanza ni kwa mujibu wa sheria, na nyingine kwa kutumia nguvu. Ya kwanza inawafaa watu na ya pili inawafaa hayawani. Lakini kwa sababu njia ya kwanza mara nyingi haifanikiwi, kunakuwa na ulazima wa kutumia njia ya pili.

Kiongozi anatakiwa kujua jinsi ya kushughulika na wote, watu na hayawani. Jambo hili limekuwa likifundishwa na wanazuoni wa kale kwa siri. Walitoa mfano wa Achilles na viongozi wengine wa zamani. Viongozi hawa walipelekwa kujifunza kwa Chiron ambaye alikuwa ni centaur(mtu mwenye mwili wa farasi). Lengo la kuwa na mkufunzi ambaye nusu ni binadamu na nusu nusu hayawani, lilikuwa ni kuonyesha umuhimu wa kiongozi kuwa na sifa zote. Na yeyote ambaye hana sifa hizo alikuwa hawezi kuwa imara.

Lakini kwa sababu kiongozi anatakiwa kutumia sifa ya uhayawani kwa busara, inampasa kuwa kama simba na mbweha. Simba hawezi kujilinda dhidi ya mitego, wala mbweha hawezi kujilinda dhidi ya mbwa mwitu. Kwa hiyo, kiongozi anatakiwa kuwa kama mbweha kutambua mitego na kama simba kuwafukuza mbwa mwitu.

Kuwa kama simba muda wote si busara. Hivyo, kiongozi mwenye hekima, halazimiki kutenda anayoyasema iwapo kufanya hivyo kutamuingiza matatizoni, au ikiwa sababu zilizomfanya ayaseme hazipo tena. Iwapo watu wote wangekuwa ni wema nisingeshauri hivyo, lakini kwa kuwa watu si waaminifu, wewe pia unatakiwa kutokuwa muaminifu kwao. Na hakuna kiongozi aliyewahi kosa sababu ya kueleweka ya kutetea ukosefu wake wa uaminifu.
Kuhusu hili tunayo mifano mingi sana ya hivi karibuni. Mifano hiyo inaonyesha jinsi ambavyo mikataba, na makubaliano mengi ya muhimu ilivyoshindwa kutekelezwa na kuachwa. Sababu ni viongozi kukosa uaminifu. Na inaonyesha kuwa, wale waliokuwa na tabia ya mbweha ndiyo waliofanikiwa zaidi.

Ni muhimu kuificha tabia kwa namna hii, na kuwa hodari katika udanganyifu na kujifanya. Hata hivyo, watu ni wajinga sana, na wanaongozwa na mahitaji yao ya sasa tu, mtu anayetaka kudanganya hawezi kosa wajinga wa kuwadanganya au kuwapotosha.
Kuna mfano mmoja wa karibuni ambao sina budi kuuelezea. Papa Alexander wa VI hakujali kitu bali namna ya kudanganya, na mara zote alipata namna ya kufanya hivyo. Hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kuwaaminisha watu, au kutoa ahadi kwa matamko yenye kuaminisha, na hakuna ambaye alikuwa hatekelezi ahadi zake kama yeye. Kwa sababu alijua asili ya mwanadamu, udanganyifu wake ulifanikiwa.

Kwa hiyo, si lazima kwa kiongozi kuwa na sifa zote nzuri nilizozielezea kwenye maandiko yangu, lakini ni muhimu sana kuonyesha kuwa unazo. Na pengine nisisitize kuwa, kama kiongozi ameanza kuzifanyia kazi sifa hizo kwa vitendo na anazitenda kwa ukawaida, lazima zitamdhuru. Lakini kujionyesha kuwa unazo bila kuzitenda zitakuwa msaada kwako. Kwa hiyo, ni jambo jema kuonekana kuwa na rehema, muaminifu, mwenye ubinadamu, mtu wa dini, mwenye msimamo na kutenda namna hiyo. Lakini inatakiwa kuwa makini kiasi kwamba ikihitajika, usizitende sifa hizo. Unatakiwa kujua wakati wa kuzitenda na kutozitenda.

Pia unatakiwa kuelewa kuwa, kiongozi na hasahasa kiongozi mpya, hawezi kutimiza sifa zote hizo zinazomfanya mtu kuonekana mwema. Ili kulinda utawala wake, atahitajika kutenda kinyume na uaminifu, utoaji, utu na mshika dini. Hivyo basi, anatakiwa kuwa macho na tayari kubadilika kadri upepo wa mambo unavyobadilika. Na kama nilivyosema, hatakiwi kuacha kutenda mema kama akiona inafaa, lakini pia anatakiwa kujua namna ya kuwa kauzu pale inapolazimu.

Kiongozi anatakiwa kuwa makini sana kuhakikisha kuwa kile anachosema, kinamuonyesha kuwa na sifa hizo tano nikizokwisha kuzitaja. Mtu anayemsikiliza na kumuona anatakiwa kumuweka kwenye kundi la watu wenye sifa ya rehema, uaminifu, kujiheshimu, utu na ucha Mungu.
Na hakuna sifa ya muhimu kwa kiongozi kuonekana kuwa nayo kama hii ya mwisho. Watu huwa wanaangalua tabia ya mtu kijuujuu tu bila kujua hasa matendo yake. Sababu ni kuwa, wengi wanaweza kukuona jinsi ulivyo, lakini ni wachache wanaoweza tambua matendo yako. Kila mtu anajua jinsi ulivyo lakini ni wachache wanaokujua wewe ni mtu wa aina gani hasa. Na hawa wachache, hawawezi kupingana na mtazamo wa wengi ambao wako upande wa kiongozi

Zaidi ya yote, matendo ya watu wote na hasahasa viongozi, na iwapo hakuna uwezekano wa kushtakiwa, tunatakiwa kujali zaidi matokeo na si jinsi matokeo hayo yanavyofikiwa. Kiongozi akiweza kujiimarisha na kuwa na mamlaka kamili, siku zote matendo yake yataonekana mbele za watu kuwa ni ya haki na yanayostahili. Ubaya huonekana kwa jinsi ulivyotendwa, au matokeo ya kutendwa kwake. Lakini ni ubaya mchache tu ndiyo huendelea kutiliwa maanani.

Kuna kiongozi mmoja wa nyakati zetu, ambaye sitamtaja kwa jina; huyo amekuwa ni mtu hodari wa kuhubiri amani na uaminifu siku zote japo ni adui mkubwa wa mambo hayo. Na kama angefanya kama anavyohubiri, basi angepoteza mamlaka yake na utawala wake ungeanguka mara moja
 
Anasema unatakiwa uwe mdanganyifu na mtu wa kujifanya. Pia anakazia kuwa kiongozi hajawahi kosa sababu yenye mashiko ya kutetea kuvunja kwake uaminifu.
 
SURA YA 19

KIONGOZI ANATAKIWA KUEPUKA KUCHUKIWA NA KUDHARAULIKA

Baada ya kuongelea kuhusu sifa kuu hapo juu, zingine zilizobaki nitaziongelea kwa pamoja kama ifuatavyo: kiongozi, kama nilivyokwisha gusia, anatakiwa kufikiria sana jinsi ya kuepuka mambo yatakayomfanya achukiwe au kudharaulika; na kama akifanikiwa kuepuka mambo hayo, atakuwa ametimiza wajibu mkubwa na kujitoa katika hatari hata kama ana sifa zingine mbaya.

Kama nilivyokwisha sema huko nyuma, hakuna jambo litamfanya rais achukiwe haraka kama kuwa mporaji, kuingilia mali za raia wake na wake zao. Hivyo, kiongozi anatakiwa kuepuka sana mambo hayo. Watu huishi kwa amani na kuridhika iwapo heshima na mali zao visipoguswa. Kiongozi anachotakiwa kufanya ni kushughulika na wachache tu ili wasipate nguvu kupita kiasi, na kitu hicho si kazi ngumu.

Kiongozi atadharaulika iwapo ana sifa zifuatazo; kutokuwa na msimamo, muoga, mwenye mizaha, kukosa maamuzi, au kukosa ushupavu. Kiongozi anatakiwa kujilinda sana asionekane ana sifa hizo, na badala yake ajitahidi matendo yake yamuonyeshe kuwa ni mtu mwenye busara, mkuu, na mwenye nguvu. Na anapokuwa anashughulika na raia wake katika faragha, anatakiwa kufanya maamuzi yake kuwa ndiyo ya mwisho, na kuonyesha sifa ambazo hakuna mtu atathubutu kumzoea kupita kiasi, au kumshawishi kufanya jambo asilolitaka.

Kiongozi anayejionyesha kuwa ana sifa hizo, huheshimiwa sana, na yule anayeheshimika ni ngumu kufanyiwa njama, haitakuwa rahisi kumvamia iwapo anajulikana kuwa ni kiongozi mzuri, na anaheshimiwa na wananchi wake. Kiongozi hukabili hatari mbili; moja ni kutoka kwa raia wake, na nyingine kutoka kwa adui wa kigeni. Dhidi ya huyu adui wa pili, anaweza kujilinda kwa kuwa na jeshi imara na washirika wazuri, na kama ana jeshi imara, mara zote atakuwa na washirika wazuri, na utaweza kuwadhibiti adui wa kigeni. Na ukiweza kuwadhibiti adui wa kigeni, itakuwa rahisi kuwadhibiti adui wa ndani, labda kuwe na njama. Na hata kama kuna njama, lakini hakuna adui wa kigeni, kiongozi anayeishi kwa njia nilizoanisha hapo juu, na akiwa hajakata tamaa, ataweza kuhimili shambulio lolote lile, kama nilivyosema; hilo lilitokea kwa Nabis msparta.

Kuhusu raia wake, iwapo hakuna adui wa kigeni wa kushugulika naye, anaweza kuwa na wasiwasi kwamba wanaweza kula njama dhidi yake. Kiongozi anaweza kuwa salama dhidi ya hilo kwa kuepuka kuchukiwa, kudharaulika, na kuwa na uhusiano mzuri na raia wake. Na jambo hili nimeshalizumgumza kwa kirefu sana, ni muhimu kwa kiongozi kutochukiwa wala kudharauliwa na raia wako, ndiyo njia bora kiongozi anayoweza kutumia kujilinda dhidi ya njama. Sababu yule anayefanya njama, mara zote hutafuta kuwafurahisha wananchi kwa kumuua kiongozi. Lakini akiona kuwa, badala ya kuwafurahisha atawaudhi, hawezi kuwa na ujasiri wa kutimiza njama yake. Vikwazo wanavyopitia wala njama ni vingi, na japo tumeona njama nyingi zikitokea, ni chache zimefanikiwa.

Na zaidi ni kuwa, mla njama huwa hawi peke yake, wala hawezi kuchukua mtu yoyote na kula naye njama, isipokuwa wale anaoamini wana vinyongo. Lakini napo, mara tu unapompa mipango yako mtu ambaye anakinyongo, unakuwa umempa njia ya kuondoa kinyongo chake, na kwa kukusaliti anakuwa anajipatia manufaa yote yeye peke yake(Kwa njia zote za kukusaliti atafaidika, kwa kuiba mpango wako, au kwa kutoa siri zako). Na kwa kuona kuwa kwa upande mmoja kuna faida ya hakika, na upande mwingine, jambo la hatari na lisilo na uhakika. Kama akificha siri yako, atakuwa rafiki yako mkubwa huku akiwa adui mkubwa wa kiongozi wake.

Kwa ufupi niseme hivi; upande wa wala njama kuna mashaka, husda na adhabu kali, vitu hivyo ni vikwazo kwake kukuunga mkono. Lakini kwenye upande wa kiongozi kuna utaratibu wa sheria, utukufu wa kifalme, ulinzi kutoka kwa rafiki na serikali; na ukiongezea suala la maslahi ya umma, haiingii akilini kwa mtu kula njama harakaharaka. Japo kwa kawaida mla njama huwa na matatizo kabla ya kutenda uovu wao, lakini mazingira haya(kama kiongozi anapendwa) atakuwa na wasiwasi pia baada ya kukamilisha njama yake. Raia ndiyo watakuwa adui zake, naye hatakuwa na tumaini lolote la kuwa salama

Kuna mifano mingi sana kuhusiana na jambo hilo, lakini nitaelezea tu yale yaliyotokea enzi za mababu zetu. Kiongozi wa Bologna, Bwana mkubwa Annibale Bentivoglio, ambaye ni babu wa huyu Bwana mkubwa Annibale wa sasa, alifanyiwa njama na kuuwawa na Wa-Canneschi, hakuacha mrithi yeyote isipokuwa Bwana mkubwa Giovanni ambaye alikuwa mtoto mchanga wa kubebwa. Mara tu baada ya mauaji hayo, raia wakaasi na kuwaua Wa-canneschi wote. Hili lilisababishwa na jinsi Wa-Bentivogli walivyopendwa katika Bologna; familia hiyo ilipendwa sana kiasi kwamba baada ya kifo cha Bwana mkubwa Annibale hakuna aliyeweza kupewa kuongoza, kulikuwa na imani kuwa mtu wa ukoo wa Bentivogli (ambaye wakati huo ilisadikika ni mtoto wa mhunzi chuma), alikuwa akiishi huko Florence. Wananchi wa Bologna walimfuata na kumuamini kuongoza mji wao, na aliongoza hadi Bwana mkubwa Giovanni alipokuwa na umri wa kutosha kuongoza.

Kwa ufupi ni kuwa, kiongozi hana sababu ya kuogopa njama iwapo wananchi wake wanamheshimu na kumpenda; lakini kama wana chuki dhidi yake na hawaridhiki na utawala wake, anapaswa kuogopa kila mtu na kutomuamini yeyote yule. Nchi zinazoongozwa na viongozi wenye hekima zimehakikisha kuwa watu wa nasaba bora wanatimiziwa mahitaji yao vizuri, huku raia wa kawaida wakiishi kwa kuridhika. Hili ni jambo la muhimu sana kwa kiongozi kulizingatia.

Moja ya serikali inayoongozwa vizuri katika nyakati zetu ni ile ya Ufaransa. Ndani yake kuna taasisi nzuri zisizo na idadi, hizo ndiyo zinalinda uhuru na usalama wa mfalme, na iliyo muhimu kuliko zote ni bunge na mamlaka yake. Aliyeunda na kuipa katiba mamlaka hayo, alijua tabia ya watu wa nasaba bora ya kutaka makuu na kujikweza, hivyo aliona kuna umuhimu wa kuwadhibiti. Na ili kumlinda mfalme dhidi ya vinyongo na chuki, basi ilionelewa kuwa lisiwe jukumu lake kushughulika na watu. Na hilo lilimlinda dhidi ya husda za watu wa uzao bora kwa kuwapendelea raia wa kawaida, au chuki ya raia wa kawaida kwa kuwapendelea watu wa uzao bora. Hivyo alichaguliwaa mtu wa
kati kuwa msuluhishi, ambaye bila kusema kuwa mfalme anahusika aliweza kuwadhibiti watu wa nasaba bora, huku akiwainua wananchi wa kawaida. Hakuwezi kuwa na njia nzuri, ya busara na uhakika ya kumlinda mfalme na ufalme kama hiyo. Hapo tunapata somo lingine, ni kuwa; kiongozi anatakiwa kuwaachia wengine washughulike na maswala yanayohitaji uwajibikaji, huku yeye akibaki na masuala yanayohitaji rehema na zawadi. Na tena, kama nilivyosema; kiongozi anatakiwa kujijengea heshima kubwa na kuepuka kuwa chukizo kwa wananchi wake.

Wengine wanaweza kudhani kuwa; iwapo maisha na vifo vya watawala wengi wa Himaya ya Roma vikichunguzwa, itaonekana kuwa vinatoa mfano ambao ni kinyume na mtazamo wangu. Sababu ni kuwa; baadhi yao walioishi maisha mema na wakajionyesha kuwa ni watu watu wenye sifa nzuri, walipinduliwa na hata kuuwawa na raia wao ambao walikula njama dhidi yao.

Kujibu hoja hiyo, nitaelezea sifa za baadhi ya watawala hao, na hivyo kuonyesha kuwa sababu za kuanguka kwao hazina tofauti na zile nilizozianisha. Na ili kufanya hilo lieleweke vizuri, nitatoa mifano ambayo inaweza kueleweka vizuri na watu waishio sasa. Hivyo, nitazungumzia watawala kutoka utawala wa Marcus mwanafalsafa hadi wakati wa Maximinus. Watawala hao ni, Marcus, Commodus na mwanawe Pertinax, Julianus, Severus na Caracalla mwanawe, Macrinus, Heliogabalus, Alexander na Maximinus.

Kwanza lazima tutambue kuwa, katika falme nyingi, kiongozi anakuwa na kazi ya kuwadhibiti watu wa nasaba bora, na uasi wa raia tu. Lakini watawala wa Roma walikuwa na changamoto nyingine, nayo ni ukatili na uporaji wa wanajeshi wao, ilikuwa ni changamoto kubwa hadi kupelekea kuanguka kwa wengi wa watawala hawa. Sababu kubwa ni kwamba, ilikuwa ni ngumu kwao kuwaridhisha raia wao na wanajeshi kwa pamoja; raia ni wapenda amani hivyo walipendelea kiongozi mwenye busara na mtulivu, lakini wanajeshi walipendelea kiongozi mpenda vita, mkatili, mporaji, na aliyekuwa tayari kutumia sifa hizi kwa raia wake, hii ni ili waweze kujipatia pesa zaidi, na kufanya ukatili wao, uporaji na matendo yao ya pupa.

Kwahiyo, wale watawala ambao hawakupatikana kwa kurithi au kwa uwezo wao wenyewe, hawakuweza kuwa na mamlaka ya kuwadhibiti raia na wanajeshi wao, hilo lilipelekea maangamizi yao. Wengi wao, hasa waliokuwa wageni katika utawala, walipokutana na changamoto hiyo wakaamua kuwaridhisha wanajeshi, na kutojali kuwaudhi wananchi. Na kwa kweli hili lilikuwa ni muhimu kwa wao kufanya, sababu ni kuwa, kwanza kabisa, kiongozi anatakiwa kuepuka kuchukiwa na watu wa matabaka yote, lakini kama hawezi kuepuka kuchukiwa, anatakiwa ajitahidi asichukiwe na tabaka la watu wenye nguvu. Kwa sababu hiyo, watawala waliokuwa wapya walikuwa na uhitaji mkubwa wa kuungwa mkono, hivyo wakaamua kufungamana na jeshi na si watu. Njia hii ilikuwa na manufaa au hasara kadri kiongozi alivyojua jinsi ya kuwadhibiti.

Kwa sababu hizo, ikatokea kuwa, Marcus, Pertinax na Alexander, kwa kuwa walikuwa viongozi wapole, wapenda haki, wanaochukia ukatili na wenye rehema, hawakuwa na mwisho mzuri, isipokuwa Marcus. Marcus pekee ndiye aliyeweza na kuishi na kufa kwa heshima. Hii ni sababu yeye alikuwa ni mtawala kwa kurithi, na si kupitia upendeleo wa wanajeshi au raia. Na pia alikuwa na sifa zilizomfanya aheshimika, hilo lilimuwezesha kudhibiti makundi yote, hakuchukiwa wala kudharaulika.

Lakini Pertinax alichaguliwa kuwa mtawala kinyume na matakwa ya jeshi. Na kwa kuwa walizoea maisha ya kishenzi wakati wa utawala wa Commodus, hawakuweza kustahimili nidhamu ambayo Pertinax alitaka kuirudisha. Kwa hiyo, kwa kufanya achukiwe, na kwa kuwa alikuwa anadharaulika sababu ya uzee wake, alikuwa ameshindwa mara tu alipoanza kuongoza.

Na hapa inatakiwa kukumbukwa kuwa, mtu anaweza kuchukiwa kwa kufanya jambo baya, zuri au sababu zingine. Na kama nilivyokwisha sema, kiongozi anayetaka kulinda mamlaka yake, mara zote atalazimika kutokuwa mwema. Sababu, iwapo tabaka moja, liwe la raia, jeshi au watu wa nasaba
bora, ambalo unaona ni muhimu kupata uungwaji mkono wao ni ovu, utalazimika kuendana nalo na kuruhusu uovu wao, matendo ya wema yatakufanya utengwe nao.

Acha sasa tumuangalie Alexander. Inasemwa yeye hakuwa mtawala wa kawaida, na amepewa sifa nyingi sana. Imeandikwa kuwa, katika miaka kumi na nne ya utawala wake hakuwahi kutoa adhabu ya kifo kwa yoyote bila kumfikisha mahakamani. Pamoja na hayo, alionekana ni dhaifu, na kusemwa kuwa anaongozwa na mama yake. Hilo lilimfanya adharaulike, na jeshi likala njama dhidi yake na kumuua.

Tukigeuka na kuangalia sifa za Commodus, Septimius Severus na Caracalla, tutaona kuwa wote walikuwa ni viongozi katili na waporaji kabisa. Watu ambao ili kuliridhisha jeshi hawakusita kuwatendea ubaya wa aina yoyote raia wao. Na wote, isipokuwa Severus, walipatwa na mwisho mbaya. Severus alikuwa na haiba yenye nguvu iliyomfanya awe rafiki wa wanajeshi japo aliwakandamiza watu wake. Hilo lilimuwezesha kutawala kwa mafanikio mpaka
mwisho wa maisha yake. Sababu ni kuwa, uhodari wake ulimfanya akubalike machoni pa wanajeshi na machoni pa raia. Raia walishangazwa naye na kumstaajabia na wanajeshi walimheshimu na kuridhika naye.

Na kwa sababu matendo yake hayakuwa ya kawaida kwa kiongozi mpya, nitasema kifupi jinsi alivyoelewa namna ya kujivika aina zote za utu, kuwa simba na kuwa mbweha, kama nilivyokwisha sema huko nyuma, ni muhimu kwa kiongozi kuwa na sifa hii.

Kwa kujua uzembe wa mtawala wa Roma, Julianus, Severus alilishawishi jeshi ambalo alikuwa analiongoza huko Illyria. Aliliambia kwamba ulikuwa ni wajibu wao kwenda Roma na kulipa kisasi kwa kifo cha Pertinax ambaye aliuwawa na walinzi wakipretoria. Kwa mbinu hii, na bila kuwaambia lengo lake la kutawala, akawa amefanya jeshi lake kusonga na kufika Italia bila kujulikana. Alipofika Italia, bunge kwa uoga likamchagua kuwa mtawala wa himaya ya Roma na kumuua Julianus. Baada ya kuchukua hatua hii ya kwanza, bado kukawa na vizingiti viwili kwa yeye kuwa mtawala pekee wa himaya yote ya Roma; huko Asia, Pescennius Niger ambaye alikuwa anaongoza majeshi ya mashariki alikuwa kafanya atangazwe kuwa mtawala; mwingine huko magharibi, Albinus, ambaye alikuwa kamanda huko, naye akafanya atangazwe kuwa mtawala. Severus alitambua kuwa ni hatari kutangaza vita dhidi ya wote. Hivyo aliamua kumkabili Niger kwa jeshi na kumkabili Albinus kwa ujanja. Alimuandikia Albinus kuwa, kwa sababu amechaguliwa na bunge kuwa mtawala, angependa kushirikiana naye cheo hicho, hivyo akampatia cheo cha Ukaizari, na kulingana na azimio la bunge, atamchukulia kama mtawala mwenza. Albinus alikubaliana na maneno hayo. Lakini mara tu Severus alipompiga na kumuua Niger, na kuweka utulivu huko mashariki. Alirudi Roma na kulalamika katika bunge kuwa Albinus hana shukrani kwa wema aliomtendea, na amepanga hila kumdhuru; hivyo alikuwa anawajibika kwenda na kumuadhibu kwa kukosa kwake shukrani. Hapo akasonga kwenda mkoa wa Gaul ambako alimvua Albinus cheo chake na kumuua.

Yeyote atakayechunguza matendo ya mtawala huyu kwa makini, atagundua kuwa, ndani yake alikuwa na ukali wa simba na ujanja wa mbweha, na ataona sababu iliyofanya aogopwe na kuheshimiwa na watu, bila kuchukiwa na jeshi. Hivyo hatashangazwa kuwa, japo alikuwa ni mtawala mpya aliweza kudumu akitawala himaya kubwa sana. Sifa zake za kustaajabisha zilimlinda dhidi ya chuki ambayo pengine watu wangekuwa nayo kutokana na ukatili na uporaji wake. Mtoto wake, Caracalla, alikuwa naye kama baba yake, mtu hodari, akiwa na sifa zilizomfanya astaajabiwe machoni pa watu, na kupendwa na jeshi, maana alikuwa ni mtu wa vita. Japo alikuwa ni mwenye uzembe wa kupenda starehe za vyakula na mvivu, lakini ukali na ukatili wake ulikuwa mkubwa sana, ukatili ambao haujawahi kusikika popote(katika nyakati tofauti tofauti alikuwa ameua Raia wengi sana wa Roma, na aliua wakazi wote wa Alexandria kwa wakati mmoja), mambo hayo yalimfanya achukiwe na dunia nzima, na kuogopwa hata na watu wake wa karibu, mwishowe akaishia kuuwawa na afisa wa jeshi lake mwenyewe.

Hapa inatakiwa kujulikana kuwa, vifo vya namna hii vitokanavyo na watu waliojitoa mhanga na waliodhamiria haviwezi kuepukwa na viongozi. Mtu yeyote aliyejitoa mhanga anaweza kutekeleza jambo hilo. Lakini kiongozi hana sababu ya kuogopa jambo hilo sababu hutokea kwa nadra sana. Tahadhari pekee anayotakiwa kuchukua ni kutowatendea vibaya wale wanaomhudumia, au wale walio karibu naye kama maafisa wa baraza, Caracalla alipuuza tahadhari hiyo kwa kumuua kaka wa afisa yule kwa kifo cha aibu, na kwa kuendelea kumtisha afisa yule kila siku ambaye bado aliendelea kutumikia kama mlinzi wake. Jambo hili, kama matendo yaliyofuatia yalivyoonyesha, lilikuwa ni kosa kubwa lililotendwa bila kufikiri.

Sasa tumtazame Commodus, sababu yeye alipata utawala kwa kurithi, inatazamiwa atawale bila vikwazo. Kwa kuwa mwana wa Marcus, alichotakiwa kufanya ni kuiga mwenendo wa baba yake na hivyo kuwaridhisha raia na jeshi. Lakini sababu alikuwa ni mkatili na mwenye roho mbaya, na ili kutimiza tamaa yake ya ulafi wa mali hakujali raia, badala yake alitafuta kuungwa mkono na jeshi na kujiingiza kwenye kila aina ya anasa. Na mbaya zaidi, hakujali kabisa heshima yake, mara nyingi aliingia hadi ulingoni kupigana wakati wa maonyesho ya mapigano ya waroma, na kufanya matendo mengine mengi yasiyomstahili mtawala. Hayo yalimfanya adharauliwe na jeshi. Tendo la kuchukiwa na wananchi huku jeshi likimdharau lilifanya aliwe njama na kuuwawa.

Imebaki sasa kuangalia sifa za Maximinus. Huyu alikuwa ni mtu wa kupenda sana mambo ya vita, na baada ya kifo cha Severus Alexander ambaye tumekwisha muongelea huko nyuma, Maximinus alichaguliwa na kuwa mtawala na jeshi, jeshi ambalo lilikuwa limechukizwa na udhaifu wa mtawala aliyepita. Lakini hakufurahia cheo hicho kwa muda mrefu. Mambo mawili yalitokea yaliyosababisha achukiwe na kudharaulika; sababu moja ilihusiana na asili yake. Ilijulikana na wengi kuwa amewahi kuwa mchunga kondoo huko Thrace, hilo lilifanya wengi wamdharau. Sababu nyingine ni kuwa, baada ya kutangazwa kuwa mtawala, alichelewa kwenda Roma kuchukua cheo. Pia alipata sifa ya ukatili uliopita kiasi kwa sababu ya ukatili uliofanywa na wasimamizi wake huko Roma, na sehemu nyingine za himaya hiyo. Matokea yake ni kuwa dunia yote ilisimama pamoja kwa dharau juu ya asili yake, na chuki juu ukatili wake, Africa ikiongoza, huku bunge na wakazi wa Roma na Italia yote wakifuata katika vuguvugu hilo. Jeshi lake nalo likajiunga katika njama dhidi yake. Wanajeshi wake walipokuwa wameizingira Aquileja, baada ya kuona wanashindwa kuiteka, wakiwa wamechukizwa na ukatili wake, na baada ya kuona kuwa wengi wanampinga wakaacha kumuogapa, wakamuua.

Sitahitaji kuwazungumzia Heliogabalus, Macrinus na Julianus, hawa wote walikuwa ni watu wa hovyo kabisa, na kuanguka kwao kulikuwa kwa haraka sana. Lakini nimalizie kwa kusema kuwa, viongozi wa nyakati zetu hawakabili magumu ya kujitahidi kuwapendeza wanajeshi wao siku zote. Japo wanahitaji kuwadekeza kwa kiasi fulani, uhitaji wa kufanya hivyo huisha mara moja sababu hakuna hata mmoja wa viongozi hao anayemiliki jeshi lake mwenyewe, jeshi ambalo kama lile la Roma, linaloimarika kadri serikali inavyoimarika. Na kama nyakati za Roma ilikuwa ni muhimu kuwaridhisha wanajeshi kuliko wananchi, sababu wanajeshi walikuwa na nguvu kuliko raia, nyakati hizi ni muhimu zaidi kwa viongozi wote isipokuwa wa-Turk na wa-Soldan, kuwaridhisha raia kuliko wanajeshi. Sababu ni kuwa raia wana nguvu kuliko jeshi.

Nimemtoa Turk kwa sababu mara zote anakuwa kazungukwa na wanajeshi kumi na mbili elfu waendao kwa miguu, na kumi na tano elfu waendao kwa farasi, hao ndiyo msingi wa ulinzi na usalama wa ufalme wake, hivyo anahitajika kuwa na uhusiano mzuri nao kuliko raia. Serikali ya Soldan ina hali kama hiyo, yeye pia kwa kuwa tegemezi wa jeshi, anatakiwa kuwajali zaidi ya raia.
Na hapa unatakiwa kutambua kuwa, taifa la wa-Soldan, tofauti na mataifa mengine yote, linafanana sana na utawala wa kanisa la kikistro, ni kwamba haiwezi kusemwa kuwa ni utawala mpya au umepatikana kwa kurithi. Sababu ni kuwa, baada ya kifo cha Soldan anayeongoza, watoto wake hawarithi uongozi, bali anakuwa kiongozi yule anayechaguliwa na wale wenye mamlaka ya kuchagua. Sababu huu ni utaratibu wa miaka mingi, utawala unaochaguliwa hauwezi semwa kuwa ni mpya, na kwa kuwa utawala unaochaguliwa haupati magumu yanayozipata tawala mpya. Japo utawala ni mpya lakini taasisi za taifa bado ni zilezile za zamani, na zimeundwa kwa namna ambayo inamfanya kiongozi aliyechaguliwa aonekane kama ametokana na kurithi.

Tukirudi kwenye mada yetu, ninasema kuwa: mtu akichunguza sababu zilizotolewa hapo juu, ataona kuwa kilichowaangusha watawala niliowataja kilikuwa ni kuchukiwa au kudharaulika. Na pia atatambua kuwa wengine walichagua njia moja na wengine nyingine ambayo ni kinyume chake. Na atatambua kuwa, kwa kila njia ni mtu mmoja tu aliyefanikiwa, wengine wote walikuwa na mwisho mbaya. Sababu Pertinax na Alexander walikuwa ni watawala wapya, ilikuwa ni hasara kwao kuiga matendo ya Marcus, mtawala aliyetokana na kurithi; hivyohivyo kwa Caracalla, Commodus na Maximinus, ilikuwa ni kosa baya kwao kumuiga Severus, sababu hawakuwa na sifa za kuwawezesha kufuata hatua zake.

Kwa kifupi, kiongozi mpya katika kutawala hawezi kuiga matendo ya Marcus, wala si muhimu kwake kuiga matendo ya Severus; lakini anapaswa kuiga kwa Severus yale matendo yanayohitajika katika kutengeneza msingi wa serikali yake, na kutoka kwa Marcus yale yanayotakiwa kuendelea kutawala na kuifanya ifanikiwe baada ya kusimama.
 
Sura ya kumi na tisa ni moja ya sura ndefu na nzuri sana. Somo kubwa ni kumtaka kiongozi aepuke kuchukiwa na kudharaulika. Ina mifano mingi mizuri.
 
SURA YA 20

IWAPO NGOME NA MAMBO MENGINE AMBAYO VIONGOZI HUPENDELEA SANA YANA FAIDA AU NI HASARA

Ili wawe salama, baadhi ya vingozi wamewanyang’anya raia wao silaha. Wengine wamegawa miji yao katika kambi hasimu, wengine wamechochea uhasama dhidi yao wenyewe, wengine wamejaribu kuwavuta upande wao wale ambao hapo mwanzo walikuwa na mashaka nao, wengine wamejenga ngome na wengine wamezibomoa. Japo haiwezi kuelezewa kihakika ni njia gani inafaa kati ya hizo, lakini tukifanya hali zote katika nchi ni shwari, naweza kulielezea suala hili kwa njia inayoeleweka.

Haijawahi tokea kwa kiongozi mpya kuwanyang’anya raia wake silaha. Badala yake, kama amewakuta hawana silaha mara zote aliwapatia silaha, sababu silaha unazowapatia zinakuwa zako, wale uliokuwa na mashaka nao wanakuwa waaminifu, na wale waliokuwa waaminifu wanaendelea kuwa hivyo, na kutoka kuwa raia wako wanakuwa wafuasi wako. Japo huwezi kuwapatia raia wako wote silaha, lakini kama unawajali vema wale weye silaha, utaweza kuwa salama na kuwadhibiti wengine wote. Mapendeleo wanayopata wale uliowapa silaha yatawafanya washikamane nawe, na waliobaki hawatajali na kuwa na kinyongo sababu watatambua kuwa wale wanapendelewa kwa sababu ya majukumu yao. Lakini kwa kuwanyanga’anya silaha unakuwa umewaudhi mara moja. Kwa sababu unawaonyesha raia wako kuwa huwaamini, labda kwa kuwa na wasiwasi juu ya ujasiri wao au uaminifu wao, madai ambayo hukufanya uchukiwe. Na zaidi ya yote, kwa sababu huwezi kubaki madarakani bila jeshi, itakubidi utafute jeshi la mamluki. Nimekwisha onyesha jinsi jeshi la namna hii lilivyo, lakini hata kama ni jeshi zuri, halitaweza kukulinda dhidi ya adui mgeni mwenye nguvu na dhidi ya raia wako ambao huwaamini, kwa wakati mmoja. Hivyo basi, na kama nilivyokwisha sema, kiongozi mpya ambaye anatawala nchi mpya, mara zote amefanikiwa kwa kuwa na jeshi. Na mifano ya jambo hilo ni mingi sana.

Lakini iwapo kiongozi amepata nchi mpya ambayo anauinganisha na ya zamni, ni lazima awapokonye silaha wakazi wake, isipokuwa wale waliomuunga mkono wakati anaiteka. Na hata hawa anatakiwa kuwadhoofisha kadri muda unavyokwenda, na anatakiwa kuhakikisha majeshi yote ya nchi mpya yako chini ya wanajeshi wake, wale waliomtumikia toka katika nchi ya zamani.

Mababu zetu, hata wale walioheshimika kwa kuwa na hekima walikuwa na kawaida ya kusema ‘Pistoja inatakiwa kutawaliwa kwa kuchochea uhasama ndani yake, na Pisa kwa kujenga ngome,’ kwa kufuata kanuni hii walichochea uasi katika miji mingi, wakiwa na lengo la kuitawala kirahisi.
Wakati fulani, ambapo Italia ilikuwa imara, ingekuwa ni hekima kutumia njia hii; lakini kwa sasa inaonekana haiwezekani, mazingira hayaruhusu kutumia sera kama hizo. Siamini kama utengano uliosababishwa makausudi unaweza kuleta manufaa; kinyume chake ni kuwa, miji iliyogawanyika huanguka haraka inapokabiliwa na adui, sababu wale walio dhaifu mara zote watajiunga na mvamizi na wanaobaki hawataweza kusimama peke yao.

Wavenice, naamini kwa kuchochewa na sababu nilizoanisha hapo juu, walichochea uhasama wa kambi ya Guelf na ya Ghibelline katika miji waliyoitawala; japo hawakuruhusu umwagikaji wa damu, lakini walichochea uhasama wao ili kuwafanya raia washughulike na ugomvi huo na kusahau kuhusu kuwaasi wao. Lakini jambo hili, kama tunavyojua, halikuwaletea manufaa kama walivyotarajia, baada ya kushindwa vita huko Vaila, moja ya kambi hizo ilipata ujasiri na kuwafurusha kwenye maeneo yao.

Zaidi ni kuwa, njia kama hizi
zinaonyesha kuwa kiongozi ni dhaifu, chini yenye serikali imara, uhasama kama huo usingevumiliwa. Sababu ni kuwa, uhasama kama huo unafaida nyakati za amani kama njia nzuri ya kuwatawala watu, lakini ikitokea vita imezuka, ubaya wake huonekana.

Na bila ubishi, kiongozi anakuwa mkuu kwa kuushinda upinzani na hali ngumu. Kwa njia hiyo, na kama bahati ikitaka kumkweza kiongozi mpya, ambaye anahitaji sana kukwezwa kuliko yule wa kurithi, huwa inasababisha maadui waibuke na kumshambulia, hili ni ili kumpatia fursa ya kuwashinda na kukwea kwenye ukuu kwa ngazi iliyowekwa na adui zake. Kwa sababu hiyo, wengi wana maoni kuwa; kiongozi mwenye busara, mara apatapo nafasi, anatakiwa kuchochea upinzani dhidi yake kwa uangalifu, hili ni ili ukuu wake udhihirike na kukwezwa kwa kukomesha upinzani huo.

Viongozi, na hasa viongozi wapya wameona kuwa, watu wanaokuwa na msaada na waaminifu sana kwao ni wale ambao hapo mwanzo wa utawala wao walikuwa na mashaka nao, kuliko wale ambao wamekuwa
waaminifu kwao toka mwanzo. Mfano mzuri ni Pandolfo Petrucci, Bwana mkubwa wa Siena, yeye alitawala eneo lake kwa kutumia wale ambao hapo mwanzo hakuwaamini. Lakini ni ngumu kusema moja kwa moja njia ya kufuata kuhusiana na jambo hili, sababu ni kuwa njia inayopaswa kufuata hutegemea hali ya mambo. Lakini naweza sema kitu kimoja, watu ambao mwanzoni walikuwa ni wapinzani kwa kiongozi, mara zote wanaweza kufanywa wamuunge mkono kiongozi huyo kwa urahisi tu. Na ndiyo huwa na muelekeo wa kushikamana naye kwa uaminifu zaidi, sababu ni kuwa wanatambua wanatakiwa kufuta picha mbaya aliyokuwa nayo juu yao kwa matendo. Na kwa njia hii, kiongozi atapata msaada mkubwa zaidi kutoka kwao, kuliko kwa wale ambao kwa kujua anawaamini, wanaacha kujali utumishi wao.

Na sababu mada hii imenileta huku, sitaacha kumkumbusha kiongozi ambaye amepata nchi mpya kwa kukubalika na wakaazi wake kuwa; hapaswi kusahau sababu zilizofanya raia hao wamkaribishe na kumuunga mkono. Na kama ikionekana wamemuunga mkono si kwa sababu wanamkubali, bali ni kwa sababu hawakuridhika na serikali iliyopita, atapata wakati mgumu sana kuwafanya wawe rafiki zake. Sababu ni kuwa hataweza kamwe kuwaridhisha. Kwa kuchunguza jambo hili kwa makini, na kuangalia mifano ya zamani na ya sasa, ataona kuwa ni rahisi zaidi kuwafaya rafiki zake wale ambao walionyesha kuridhika na hali ya mambo ilivyokuwa, wale waliokuwa adui zake wakati anajipatia nchi, na si wale waliomuunga mkono wakati ananyakua madaraka sababu tu hawakuridhika na utawala uliopita.

Imekuwa ni utamaduni wa viongozi kwamba, ili kutawala vizuri maeneo yao huamua kujenga ngome. Hizo hutumika kama ulinzi dhidi ya adui, na kama sehemu salama ya kukimbilia mambo yanapoharibika. Nakubaliana na utamaduni huu kwa sababu umekuwepo tokea zamani sana. Lakini hata hivyo, katika nyakati zetu, Mheshimiwa Niccolo Viteli alionelea kuwa ni jambo la hekima kuvunja ngome mbili huko Citta di Castello ili kuulinda mji huo: naye Guido Ubaldo, Duke wa Urbino, alipokuwa anarudi kwenye eneo lake baada ya kuwa amefurushwa na Cesare Borgia, alivunja ngome zote katika eneo lake. Alisema kuwa, kama ngome hizo zikiondolewa haitakuwa rahisi kupoteza eneo lake tena. Jambo kama hilo lilifanywa pia na wa-Bentivogli waliporudi Bologna.

Kwa hiyo basi, ngome zinaweza kuwa na faida na hasara kulingana na mazingira, zinaweza kukufaidisha kwa namna fulani, lakini zikakuumiza kwa namna nyingine. Inaweza kusemwa hivi: kiongozi ambaye anahofia raia wake kuliko adui wa kigeni anatakiwa kujenga ngome. Lakini yule anayeogopa adui wa kigeni na si raia wake, hapaswi kujenga ngome. Ngome iliyojengwa na Francesco Sforza imeonekana, na itaendelea kuonyesha kuwa ni hatari kwa Wa-Sforza kuliko vurugu zozote zinazoweza kutokea katika nchi hiyo. Hivyo basi, ngome imara zaidi unayoweza kujenga ni kuepuka kuchukiwa na raia wako. Kama wanakuchukia, hakuna ngome inayoweza kukusaidia; sababu watu wakishabeba silaha, maadui wa kigeni mara zote huwa langoni kuwasaidia.

Katika nyakati zetu imeonekana kuwa hakuna kiongozi aliyeweza kusaidiwa na ngome, isipokuwa Forli, yeye baada ya mume wake Girolamo kuuwawa, aliweza kutumia ngome kutoroka shambulio la kwanza la waasi, huko alikaa kusubiri msaada kutoka Milan ili aweze kuipata tena nchi yake. Bahati yake hali za wakati huo hazikuruhusu adui wa kigeni kuwasaidia waasi wale. Lakini muda kidogo mbele, aliposhambuliwa na Cesare Borgia, watu walibeba silaha kumsaidia mvamizi kwasababu ya chuki yao dhidi yake, ngome zake hazikuweza kumsaidia. Kwa hiyo basi, katika hali hii na ile iliyompata hapo mwanzo, lingekuwa ni jambo la manufaa kwake iwapo hangekuwa na ngome, kuliko kwa wananchi wake kumuunga mkono adui.

Nikichunguza mambo kwa mapana, naweza sema, nitamsifu yule anayejenga ngome na Yule asiyezijenga; lakini nitamlaumu yule anayezitegemea, na kudhani ni jambo dogo kuchukiwa na raia wake.
 
SURA YA 21

JINSI KIONGOZI ANAVYOPASWA KUJIENDESHA ILI KUHESHIMIKA

Hakuna kitu kinamfanya kiongozi aheshimika kama kuanzisha jambo kubwa na kudhihirisha uwezo wake kwa kulitimiza.

Kati ya viongozi wa nyakati zetu, mfalme wa sasa wa Hispania, Ferdinand wa Aragon anaweza kuonwa kama ni kiongozi mpya. Sababu alitoka chini kabisa na kuwa mmoja ya viongozi mashuhuri na mfalme mkuu katika tawala za kikristo. Kama ukichunguza mafanikio yake utaona yote ni makubwa, na mengine ya kustaajabisha.

Mwanzoni mwa utawala wake alitangaza vita dhidi ya Granada, jambo hilo ndilo lilikuwa msingi wa nguvu zake. Mwanzoni aliendesha vita hiyo bila wasiwasi wowote wa kuingiliwa, huku akifanya fikra za wakuu wa Castile kujishughulisha kwenye vita hiyo hadi kusahau mabadiliko yaliyokuwa yanatokea nyumbani kwao. Wakati huohuo, bila kugundulika akawa anajitwalia heshima na mamlaka juu yao. Kwa kutumia pesa kutoka kwenye kanisa
na wananchi wake, aliweza kuhudumia majeshi yake, na katika makabiliano hayo ya muda mrefu, alifanikiwa kujenga jeshi lenye nidhamu, jambo lililomletea sana heshima. Zaidi ya yote; ili kuweza kufanya mambo makubwa zaidi, mara zote alijivika koti la dini, alikuwa na kitu tunachoweza kusema ni mshika dini katili. Alitumia kigezo cha dini kuwafurusha wa-moors kutoka kwenye nchi yake, kwa kigezo hichohicho alifanya vita na Africa, aliivamia Italia, na mwishowe aliishambulia Ufaransa. Na kwa kujishughulisha muda wote akipanga, na kutekeleza mipango mbalimbali, alifanya raia wake wamstaajabie na kumheshimu, wakishangazwa na matokeo ya matendo yake ambayo yalikuwa yanafanyika mfululizo kiasi kwamba hakukuwa na muda wa kuyapinga.

Pia ni faida kwa kiongozi anaposhughulika na mambo ya ndani ya nchi yake, kufuata njia kama zile zilizofuatwa na Bwana mkubwa wa Milan, Bernabo. Anatakiwa kutumia fursa zote, za kutenda wema au ubaya kila zinapojitokeza, na anatakiwa kutoa zawadi au adhabu kwa njia itayofanya jambo hilo lizungumzwe na kuenea kotekote. Lakini zaidi ya yote, anatakiwa kuonyesha kwa matendo yake kuwa ni mwema na mkuu sana.

Pia, kiongozi ataheshimika iwapo ni rafiki mshikamanifu na adui imara. Hilo linamaanisha yule anayesema waziwazi huyu ni rafiki yangu, na huyu ni adui yangu. Hili ni jambo lenye faida kuliko kuwa vuguvugu. Chukulia mfano jirani zako wawili wenye nguvu wameanza kupigana. Unaweza ukawa na sababu ya kuogopa yule atakayeibuka mshindi, au ukawa huna hofu iwapo yoyote ataibuka mshindi. Vyovyote vile, itakuwa ni faida kwako ukichagua upande wa kuunga mkono. Usipofanya hivyo, lazima utakandamizwa na yule aliyeshinda, huku aliyeshindwa akifurahia hilo. Na hakuna unaloweza kufanya la kukusaidia kutoka katika hali hiyo; sababu ni kuwa, mshindi hataki marafiki wenye kigeugeu ambao hawawezi kumsaidia; na yule aliyeshindwa hatakuwa na habari na wewe kwasababu hukubeba silaha kumsaidia.

Antiochus alipoombwa na waaetolia kuingia Ugiriki kuwafurusha waroma, alituma ujumbe kwa waachaia ambao walikuwa ni rafiki wa waroma. Aliwaomba wasifungamane na upande wowote. Waroma wao wakawaomba wabebe silaha kuwasaidia. Jambo hilo lilipojadiliwa katika baraza la Achaia, mjumbe wa Antiochus akawaomba tena kutofungamana na upande wowote, lakini mjumbe wa Roma aliwaambia, ‘hakuna kitu kibaya kama ninyi kutofungamana na yoyote katika vita hii, kwa sababu kwa kufanya hivyo, hamtapata mapendeleo yoyote wala sifa yoyote, mtabaki chini ya mshindi, naye atawatendea atakavyo.’
Na mara zote itatokea kwamba, yule ambaye si rafiki yako, atakuomba usifungamane na upande wowote, na yule ambaye ni rafiki yako, atakuomba ubebe silaha kumsaidia. Viongozi wasio na msimamo, na ili kuepuka hatari iliyopo, mara nyingi watatangaza kutofungamana na upande wowote na hilo linakuwa maangamizi kwao. Lakini kama ukitangaza kwa ujasiri waziwazi, ikitokea yule uliyemuunga mkono ameshinda, japo ni mwenye nguvu, nawe unategemea rehema zake, bado atakuwa na deni kwako na tayari kawa rafiki yako; ni kukosa aibu na shukrani kwa kiwango cha juu kwa mtu kumdhuru aliyemsaidia. Na zaidi ni kuwa, ushindi huwa si kamilifu na hilo litamfanya mshindi kufikiria kwa makini matendo anayofanya, hasa yahusuyo haki. Kwa upande mwingine, ikitokea yule uliyemuunga mkono akawa ameshindwa, siku zote atakutambua kama rafiki muaminifu; mara zote akiwa na uwezo atakusaidia, na utakuwa mshirika wake.

Kwa namna ya pili, ambapo wote wanaopigana hawana nguvu za kukufanya uogope ikiwa mmoja wao ameshinda, bado itakuwa ni jambo la hekima kwa wewe kuwa na upande, hapo utakuwa unamuangamiza mmoja wao kwa msaada wa mwingine, ambaye kama naye angekuwa na hekima angejitahidi kumuokoa mwenzake, asingeruhusu mwenzake aangamizwe. Kama yule uliyemsaidia akaibuka mshindi, bado ataendelea kuwa chini yako, itaonekana hawezi shinda vita bila msaada wako.

Na hapa kuna jambo la kuweka akilini. Kiongozi anapaswa kuwa makini, na kamwe asifungamane na yule aliye na nguvu kuliko yeye katika kushambulia wengine, isipokuwa hali ikimlazimu kufanya hivyo. Sababu ni kuwa, kama yule uliyemuunga mkono atashinda basi utakuwa chini ya rehema zake, na viongozi wanatakiwa kuepuka kujiweka chini ya rehema za wengine. Japo wavenice walikataa ushirika na wafaransa, lakini waliungana nao katika vita dhidi ya Duke wa Milan, na jambo hilo likawa maangamizi kwao. Lakini kama kuingia kwenye ushirika hakuepukiki, kama ilivyowatokea waflorence wakati Papa na Hispania walipoongoza majeshi yao kuvamia Lombardy, kwa sababu zilizokwisha tolewa kiongozi analazimika kuchagua upande wa kufungamana nao. Simaanishi kuwa kila taifa linaweza chagua upande kirahisi na kuwa salama, hapana. Bali linatakiwa kuwa makini na kutoamini kupita kiasi maamuzi liliyoyafanya kuwa ni sahihi na salama. Ni jambo la kawaida kwa binadamu kuepuka tatizo moja na kujikuta anatumbukia kwenye lingine. Kwa hiyo, hekima ni kujua jinsi ya kulinganisha hasara na kuchagua uamuzi ambao una afadhali.

Kama nilivyokwisha sema, kiongozi anatakiwa kujionyesha kama mtu mwenye uwezo kupita wengine, na anatakiwa kuwaheshimu na kuwajali wale wanaoonyesha uhodari katika nyanja mbalimbali. Anatakiwa kuwahimiza wananchi wake kufanya bidii katika stadi zao kama ni biashara, kilimo au zozote zile, na katika hali ya usalama ili mtu asijevunjwa moyo kufanya kazi kwa bidii akiamini ataporwa, au wakaepuka kuanzisha biashara kwa kuogopa kodi. Pia anatakiwa kuwapatia ruzuku wale wanaotaka kujiajiri, na wale wote wanaojitahidi kwa njia yoyote kuchangia ustawi wa jiji au taifa lake.

Zaidi ya hilo, katika majira yanayofaa ya mwaka, anatakiwa kuwaburudisha raia wake kwa matamasha na maonyesho. Na kwa sababu miji karibu yote inakuwa na mashirika na vyama vya wataalamu, anatakiwa kuvijali sana, na muda mwingine kushiriki mikutano yao, akionyesha mfano wa mtu mwema, na kuwa ni mtu wa watu. Lakini mara zote akilinda heshima yake ambayo kwa namna yoyote ile haitakiwi kushuka.
 
SURA YA 22

WASAIDIZI WA KIONGOZI

Uchaguzi wa mawaziri wa kiongozi si jambo dogo. Iwapo wasaidizi hao watakuwa wazuri au la, inategemea na hekima ya kiongozi mwenyewe. Kitu cha haraka kinachoweza tambulisha tabia na hekima ya kiongozi, ni watu waliomzunguka. Kama ni waaminifu na wenye kufanya kazi zao vyema, tutasema kuwa kiongozi ana hekima, sababu ameweza kutambua sifa zao na kuwafanya waendelee kuwa waaminifu. Lakini wakiwa na sifa kinyume na hizo, hatutamuona kiongozi huyo kuwa ni mtu wa mwenye hekima.

Hakuna mtu aliyemfahamu mheshimiwa Antonio wa Venafro kama waziri wa Pandolfo, kiongozi wa Siena. Lakini walifikiri kuwa Pandolfo ni kiongozi mwenye busara kwa kumuweka kuwa msaidizi wake. Na kwa vile kuna aina tatu za uelewa, aina ya kwanza ni ile mtu anaelewa kwa uwezo wake. Aina ya pili ni ile mtu anaelewa kwa kuonyeshwa na wengine, na aina ya tatu ni ile mtu haelewi kwa uwezo wake, wala kwa kuonyeshwa na wengine. Aina ya kwanza ndiyo bora kabisa, ya pili ni nzuri na ya tatu ni isiyofaa kitu. Tutakubaliana kuwa, kama Pandolfo alikuwa hana aina ya kwanza ya uelewa, basi alikuwa na aina ya pili. Kama mtu anauwezo wa kung'amua uzuri na ubaya wa yanayosemwa na mwingine, hata kama yeye mwenyewe hana wazo mbadala, anaweza kugundua uwezo wa msaidizi wake. Na ataunga mkono ushauri mzuri na kuusahihisha ule mbaya. Msaidizi hawezi kumlaghai bwana kama huyo, na ataendelea kuwa muaminifu siku zote.

Ni jinsi gani kiongozi anaweza kujua iwapo waziri wake anafaa? Kanuni ifuatayo inamsaada mkubwa sana juu ya hilo. Ikiwa waziri anajifikiria zaidi mwenyewe kuliko wewe, na matendo yake yote ni kwa maslahi yake mwenyewe, jua kuwa huyo hawezi kuwa waziri mzuri unayeweza kumuamini. Sababu ni kuwa, yule ambaye anatanguliza maslahi ya taifa, hawezi kuweka maslahi yake mbele, bali yale ya kiongozi wake. Wala hatamletea kiongozi mambo ambayo hayana maslahi kwake.
Kwa upande mwingine, ili kiongozi awafanye mawaziri wake waendelee kuwa wazuri lazima awajali, awaheshimishe na kuwatajirisha, awafanye kuwa washikamanifu kwa kushirikiana nao utukufu na mizigo ya taifa. Hii ni ili heshima nyingi na utukufu unaowapatia uwazuie kutaka kujipatia wenyewe vitu hivyo. Na majukumu makubwa unayowapatia yawafanye waogope mabadiliko, wakijua kuwa hawawezi kusimama wenyewe bila msaada wa bwana wao.
Kama kiongozi anaishi namna hii na mawaziri wake, uhusiano wao utakuwa mzuri. Kinyume chake, mmoja wao atapatwa na mabaya.
 
SURA YA 23

WANAFIKI HAWAPASWI KUVUMILIWA

Jambo moja baya ambalo viongozi hulipata, isipokuwa wana bahati katika uchaguzi wa marafiki, au ni waangalifu sana. Jambo muhimu sana ambalo sipaswi kuacha kulizungumzia, ni wanafiki. Hawa hujaa kwenye mabaraza, na kwa sababu binadamu hufurahia wakisifiwa, basi hujidanganya kuwa hawawezi kuepuka msongo wa wanafiki, na kwamba wakifanya jitihada kuwaepuka, watajikuta wameangukia kwenye kudharaulika.

Kwa kweli hakuna njia ya kujilinda dhidi ya wanafiki zaidi ya kuwafanya watu watambue kuwa huchukii kuambiwa ukweli. Lakini kama kila mtu yuko huru kukuambia ukweli, heshima yako itashuka. Kwa hiyo, kiongozi mwenye busara lazima awe na usawaziko. Anatakiwa kuchagua watu wachache wasiri, hao awaruhusu wamwambie maoni yao waziwazi juu ya jambo lolote lile, hao tu. Anatakiwa kuwauliza maoni yao kwenye kila jambo, na baada ya kusikia maoni yao anatakiwa kutafakari na kufanya maamuzi yeye mwenyewe. Akiwa nao pamoja au akiwa na mmoja mmoja, anatakiwa kuwaaminisha kwamba, kadri wanavyoongea mawazo yao bila unafiki, ndiyo atakavyowapenda zaidi. Mbali na hawa, kiongozi hatakiwi kumsikiliza mwingine yoyote yule, na anatakiwa kusimamia maamuzi yake bila kuyumba. Atakayefanya kinyume na hivyo atazongwa na wanafiki, au kwa kubadilikabadilika kulingana na maoni ya watu, atadharaulika.

Nitazungumzia tukio la hivi karibuni kuelezea zaidi suala hili. Luka, kasisi ambaye anashiriki kwenye baraza la mtawala Maximillan wa Roma, aliniambia hivi kuhusu mtawala huyo. Alisema Maxmillan haombi ushauri kwa yoyote, lakini pia hajawahi tenda kulingana na matakwa yake. Na hili ni kwasababu alitenda mambo tofauti na njia zilizoshauriwa hapo juu. Kwa kuwa na tabia ya usiri, hakuwahi kumjulisha mtu malengo yake wala kuomba maoni yao. Na ni pale tu mipango yake inapotakiwa kutekelezwa ndipo huomba maoni ya wengine, na wakati huo inaanza kupingwa na wale wanaomzunguka, na kwasababu si mtu imara, hukubaliana nao. Hivyo inaonekana kuwa anachokifanya leo, kesho anakibadilisha, mipango yake na matamanio yake hayatekelezwi kamwe. Haiwezekaniki kutimiza matakwa yake.

Hivyo basi, kiongozi anatakiwa kuchukua ushauri siku zote, lakini ni kwa nyakati na mambo anayopenda yeye, na si kwa mapendezi ya wengine. Pia anatakiwa kuwafanya washauri wake waelewe kuwa, hawatakiwi kuwa vimbelembele kutoa ushauri kwa mambo yasiyoulizwa. Zaidi ya hilo, anatakiwa kuwa huru kuomba ushauri na msikivu mzuri wa ukweli. Hata ikitokea kaudhika na ushauri fulani, anatakiwa kuficha hisia zake.

Wale wanaofikiri kiongozi mwenye sifa ya hekima ameipata kutoka kwa washauri wazuri wanaomzunguka, na si kutokana na uwezo wake, wanakuwa wamekosea sana. Ni sheria iliyo kweli na wazi siku zote kuwa, kiongozi asiye na hekima hawezi kupokea ushauri wenye hekima kutoka kwa wengine. Labda kama atamuachia mtu mwenye hekima amuamulie mambo, hapo atashaurika vizuri, lakini ni kwa kitambo tu. Muda si mrefu mshauri huyo atampoka madaraka. Na kama atasikiliza washauri wengi kupita kiasi, kiongozi asiye na hekima hatakuwa anapata ushauri mzuri kwa ukawaida, na hatajua jinsi ya kuuchambua. Kila mmoja atatoa ushauri kwa namna ya kujifaidisha, na kiongozi atashindwa kuwagundua na kuwasahihisha. Ipo hivyo siku zote. Siku zote watu watafanya wanavyotaka, na kwa faida yao mpaka waone kuwa kuna ulazima wa kuwa waaminifu na watii.

Kwahiyo basi. Ushauri mzuri, haijalishi unakotoka, chanzo chake ni hekima ya kiongozi. Na si hekima ya kiongozi kutoka kwa washauri wazuri.
 
SURA YA 24

KWANINI VIONGOZI WA ITALIA WALIPOTEZA TAWALA ZAO.

Masomo yote yaliyofundishwa mpaka sasa, kama yatafuatwa kwa hekima, yatamfanya kiongozi mpya aonekane kama ni mzoefu. Na yatamfanya abaki madarakani imara na salama. Matendo ya kiongozi mpya huchunguzwa sana kuliko ya yule aliyepata uongozi kwa kurithi. Na kama yakionekana ni ya kustahili, yatavutia zaidi watu, na kufanya wamuunge mkono kuliko hata yule wa kurithi. Watu hushawishiwa zaidi na mambo mapya kuliko ya zamani. Na kama wakiona maisha yao yameboreka kuliko hapo kabla, huwa watulivu bila kuleta matata yoyote. Hata zaidi, wanakuwa tayari kupambana wawezavyo kumlinda kiongozi mpya. Hivyo kiongozi huyu anakuwa amejipatia utukufu mara mbili; kwanza kwa kuunda utawala mpya, ma pili kwa kuweza kuuimarisha kwa sheria nzuri, jeshi imara, raia waaminifu na matendo makuu. Kwa upande mwingine, kuna dharau mbili kwa yule anayepata uongozi kwa kurithi, na ukaupoteza kwa kukosa hekima.

Na kama tukiwachunguza viongozi katika Italia, ambao katika wakati wetu walipoteza tawala zao, viongozi kama mfalme wa Napoli, Duke wa Milan na wengineo, tutaona kwanza kabisa; upande wa jeshi hawakuwa vizuri kama tulivyokwisha ainisha huko nyuma. Jambo lingine, wengi wao hawakuwa wanaungwa mkono na raia, na wale walioungwa mkono na raia hawakujua jinsi ya kujilinda dhidi ya watu wa tabaka la nasaba bora. Lakini pamoja na makosa hayo, tawala zenye majeshi imara huwa haziangushwi.

Tukimchunguza mfalme Philip wa Macedonia, siyo baba wa Alexander mkuu, bali yule aliyeshindwa vibaya na Titus Quintius. Tutaona kuwa hakuwa na tawala yenye nguvu kulinganisha na waroma na wagiriki waliomvamia. Lakini kwa sababu alikuwa ni kiongozi anayejua vita, na aliyejua kushawishi watu kumuunga mkono, na kuwafanya watu wa tabaka la juu kuwa waaminifu, aliweza kubaki madarakani kwa miaka mingi akipambana dhidi ya adui zake. Mwishowe, japo alipoteza baadhi ya majiji, lakini aliweza kulinda ufalme wake.

Hivyo basi, viongozi wetu waliopoteza tawala zao baada ya kuziongoza kwa miaka mingi, hawapaswi kulaumu bahati mbaya bali uzembe wao wenyewe. Wakati wa amani hawakufikiria kuwa mabadiliko yanaweza kutokea(ni asili ya binadamu kutowaza kuhusu dhoruba wakati bahari ni tulivu). Walipopatwa na magumu, hawakufikiria jinsi ya kuyakabili bali jinsi ya kuyakimbia. Walitegemea kuwa labda watu wao wakichoshwa na kujikweza na unyanyasaji wa mvamizi, watawaita na kuwarudisha tena.
Njia hii ni nzuri kuifuata pale ambapo hapana njia mbadala, lakini ni uzuzu mkubwa kutegemea njia hii na kuacha nyingine zote. Hakuna anayetamani kuinuka kwa kutegemea wengine. Watu wako wanaweza wasikuite kamwe, na hata wakikuita hautakuwa salama. Hautaheshimika sababu kurudi kwako hakujategemea uwezo wako, na namna bora ya kujilinda na inayodumu, ni ile inayotegemea uwezo wako wewe mwenyewe.
 
SURA YA 25

JINSI BAHATI INAVYOWEZA KUATHIRI MAISHA YA BINADAMU NA JINSI YA KUSHUGHULIKA NAYO

Naelewa vyema kwamba wengi wamekuwa wanaamini, na hata sasa wengine bado wanaamini kuwa masuala ya binadamu yanaongozwa na bahati, na Mungu. Kwamba binadamu hawawezi kuyabadili masuala yao kwa akili zao, na kuwa hakuna wanaloweza kufanya kuhusiana nayo. Kwa maoni hayo, wamefikia kufikiri kuwa jitihada zozote ni ubatili mtupu, hivyo wanatakiwa kuacha mambo yote yaamuliwe na bahati.

Lakini mara nyingi nikichunguza jambo hili kwa makini, kwa kiasi fulani nakubaliana na maoni hayo, na maoni hayo yanakubalika sana katika wakati wetu, hasa kutokana na matukio na mabadiliko makubwa ya mambo tuliyoshuhudia, na ambayo tunaendelea kushuhudia. Matukio hayo ni kinyume kabisa na matarajio yetu. Lakini hata hivyo si kwamba hatuna kabisa uwezo wa kufanya mambo yawe vile tunavyotaka. Nafikiri matendo yetu yanachangia asilimia hamsini na, bahati inachangia asilimia hamsini.

Naweza kuifananisha bahati na maji ya mafuriko. Yakiwa na hasira hufurika kwenye mabonde, yanasomba miti, nyumba na udongo kutoka kingo hii na kuutupa kingo ile. Kila kiumbe hukimbia mbele yake, wala hakuna anayejaribu kupambana nayo. Japo hii ndiyo asili ya maji ya mafuriko, lakini hayawi namna hiyo katika majira yote. Katika majira ya kiangazi watu wanaweza kujenga mabwawa, na njia mbadala za maji ya mafuriko. Hivyo, mafuriko yakija, wanaweza kuyadhibiti, au kupunguza uharibifu wake.
Na bahati ipo namna hiyo, inakuwa na nguvu pale panapokuwa hakuna mipango na nguvu nyingine ya kuidhibiti. Nguvu yake hujionyesha sehemu pasipo na vizuizi, wala kingo za kuidhibiti.

Kama ukiiangalia Italia, ambayo zamani ndiyo ilikuwa mdhibiti wa mambo, utaona imekuwa uwanda usio na vizuizi wala kingo. Kama ingekuwa imejilinda kwa weledi kama zilivyojilinda Ujerumani, Ufaransa na Hispania, haya mafuriko yaliyotukumba yasingekuwa na athari kubwa kama tulizoshuhudia.

Nafikiri hilo linazungumza kila kitu kuhusu namna ya kudhibiti bahati. Lakini nikichunguza zaidi naona kuwa; huwa tunashuhudia leo kiongozi anastawi na imara, na kesho yake tunashuhudia amepinduliwa bila ya yeye mwenyewe kubadilika kwa namna ya kumfanya apinduliwe.
Naamini hili linasababishwa na sababu ambazo nimekwishazielezea. Kwamba; kiongozi anayestarehe wakati wa bahati njema na neema, atapatwa na majanga bahati hiyo ikigeuka. Zaidi ya hilo, naamini atadumu yule anayebadilika kulingana na nyakati. Na yule ambaye namna yake ya kuendesha mambo haiendani na wakati, hawezi kustawi. Na tumeona kuwa, ili kufikia malengo yao, yaani utajiri na utukufu, watu hutumia njia mbalimbali. Mmoja kwa tahadhari, na mwingine kwa kiherehere. Mwingine akitumia mabavu, na mwingine kwa utulivu. Mwingine kwa subira na mwingine kwa pupa. Na tunaona kuwa mtu anaweza kufanikiwa kwa kutumia njia yoyote kati ya hizo.

Kati ya wawili wanaoongoza kwa tahadhari, mmoja anafanikiwa na mwingine anafeli. Na wawili wengine wakifanikiwa wote japo mmoja anaongoza kwa tahadhari, na mwingine kwa kiherehere. Yote haya hutokea kwa sababu ya hali za wakati husika. Hivyo, kama nilivyosema, inatokea wawili wanaotumia njia moja kupata matokea tofauti, na wawili wengine wanaotumia njia tofauti, kupata matokeo yanayofanana. Na hili husababishwa na kubadilikabadilika kwa bahati.
Hivyo basi, ikitokea mmoja anaongoza kwa tahadhari na subira. Na mazingira na nyakati ni za amani na utulivu, hivyo zinaendana na matendo yake, atafanikiwa. Lakini hali zikibadilika, na yeye hajabadili namna ya kuendesha mambo, ataangamizwa.

Hakuna mtu mwenye hekima kama yule anayeweza kubadilika kulingana na hali. Sababu ni kuwa si rahisi kwa mtu kubadilika kutoka kwenye asili yake, na kwa kuwa alifanikiwa kwa kutumia njia fulani, hawezi kushawishika kuea atanufaika akiiacha. Kwa hiyo, kama hali zitamtaka mtu anayetenda kwa tahadhari kutenda kwa haraka, hataweza kufanya hivyo. Na hilo ndilo litakuwa maangamizi kwake. Lakini kama angeweza kubadilika kulingana na nyakati na hali, angeendelea kusitawi.

Papa Julius wa II alitenda kwa kiherehere na pupa katika mambo yake yote. Lakini alifanikiwa kwa sababu alikuta mazingira na nyakati vinaendana na namna yake ya kutenda. Tazama matendo yake dhidi ya Bologna, wakati ambao bwana mkubwa Giovanni Bentivoglio alikuwa bado yupo hai. Wavenice na mfalme wa Hispania hawakuunga mkono jambo hilo, na majadiliano na mfalme wa Ufaransa kuhusiana na suala hilo yalikuwa bado yanaendelea. Bila kujali hayo, Papa kwa tabia yake ya ubabe na pupa akasonga mwenyewe kuivamia Bologna. Na kwa tendo hili akawafanya wavenice na mfalme wa Hispania wanywee na kuambatana naye. Wavenice kwa sababu ya kumuogopa, na mfalme wa Hispania kwa matarajio ya kuurudisha ufalme wote wa Napoli chini yake. Na wakati huohuo akamfanya mfalme wa Ufaransa amuunge mkono. Mfalme wa Ufaransa alihitaji uungwaji mkono wa Papa katika mpango wake wa kuwadhibiti wavenice, na kwa kuona tayari ameanza vita, akaona hawezi kumnyima wanajeshi wake bila ya kumuudhi.
Kwa matendo yake ya pupa, Papa Julius wa II alitimiza yale ambayo hakuna Papa yeyote, hata yule mwenye hekima za hali ya juu alitimiza. Kama angefanya kama ambavyo Papa mwingine yeyote angefanya, kusubiri kuivamia Bologna mpaka makubaliano yote yafikiwe, asingefanikiwa kamwe. Kwanza, mfalme wa Ufaransa angetoa visingizio lukuki vya kutompa jeshi lake, na wavenice na Mfalme wa Hispania wangempa sababu nyingi za kuwa na tahadhari. Sitazungumzia matendo yake mengine ambayo aliyatenda kwa namna ileile, na akafanikiwa. Lakini kwa sababu maisha yake yalikuwa mafupi, hakuweza kupatwa hali tofauti. Kama angeishi muda mrefu, na ingetokea hali zinazohitaji kufanya mambo kwa tahadhari, angeangamizwa. Sababu ni kuwa hangeweza kutenda mambo tofauti na asili yake.

Kwa ufupi naweza kusema kuwa, sababu hali zinabadilika na watu hubaki wakitenda vilevile kama zamani, wataendelea kusitawi kadri tu matendo yao hayapishani sana na wakati, kinyume chake, hawataweza kustawi. Kutokana na hili, nachelea kuamini kwamba, ni bora kuwa mtu wa maamuzi magumu kuliko kuwa mtu wa tahadhari. Bahati au fursa ni kama mwanamke, na ili kumdhibiti, anatakiwa kupigwa na kutendewa kibabe; na tumeona kuwa anawakubali zaidi watu wa wanaomtendea kwa ujasiri na ushupavu, kuliko wale walio waoga katika matendo yao. Na siku zote, kama tu mwanamke, anapendelea vijana. Sababu si watu wa tahadhari sana na ni wajasiri, hivyo wanamuongoza kwa ujasiri mkubwa.
 
SURA YA 26

WITO WA KUIKOMBOA ITALIA KUTOKA KWA WASHENZI

Nikitafakari kichwani mwangu juu ya mambo yote niliyoyaainisha, na nikijadiliana mimi mwenyewe iwapo katika Italia ya sasa, nyakati na hali zinaruhusu kutokea na kuimarika kwa kiongozi mpya, au kama kuna fursa kwa kiongozi mwenye hekima na ujasiri kubadili mambo, na kujiletea utukufu yeye mwenyewe na waitaliano wote? Ninaona kuwa mambo mengi sana yanachangia kuwezekana kwa hilo, lakini pia naona hakuna wakati unaofaa kuliko huu. Kama nilivyokwisha sema huko nyuma, ili Musa aonyeshe ujasiri na ushupavu wake, ilikuwa ni muhimu kwa wana wa Isarael kuwa watumwa huko Misri. Na ili ukuu na ushujaa wa Cyrus uonekane, ilikuwa muhimu kwa Waajemi kuteseka chini wa Wamedi. Na ilikuwa muhimu kwa waathene kugawanyika, na kutawanyika huku na kule ili uhodari wa Theseus uonekane. Na ili kudhibitisha uwezo wa shujaa yoyote wa kiitaliano, imekuwa muhimu kwa Italia kuwa katika hali mbaya iliyomo sasa. Kuwa watumwa zaidi ya waebrania, kukandamizwa zaidi ya waajemi, kugawanyika zaidi ya waaethene. Bila ya kuwa na kiongozi, wakiishi katika machafuko, waliopondeka na kuchakaa kabisa.

Mkombozi yeyote aliyetokea, labda kwa uhodari unaoonekana ndani yake, au ametiwa mafuta na Mungu ili kuikomboa, lakini mwisho wa siku imeonekana bahati haikuwa upande wake. Kwa hiyo, nchi yetu ipo karibu kuachwa ukiwa huku ikimsubiria mtu wa kuponya majeraha yake, kukomesha uporaji huko Lombardy, ushuru kandamizi uliowekwa juu ya Napoli na Tuscany, na kufunga vidonda vyake ambavyo vimeanza kutoa usaha.

Tumeona jinsi Italia inavyomuomba Mungu, inamuomba atume mtu wa kuikomboa kutoka kwenye huu ukatili na ukandamizaji wa kishenzi. Na tumeona jinsi ilivyotayari kufuata maelekezo kutoka kwa yeyote. Lakini mpaka sasa hatujaona mtu yeyote anayefaa kufanya kazi ya ukombozi, isipokuwa utawala wako wa kuigwa(ukiwa umejaa ushujaa, utajiri, Na ukiwa na kibali cha Mungu na kanisa ambalo uongozi wake uko chini yake)ndiyo unastahili kuchukua jukumu la mkombozi.

Lakini jambo hili si gumu kulitimiza, kama ukiweka akilini maisha na matendo ya wote niliowazungumza huko juu, utaona kuwa walifanya mambo makuu sana, lakini walikuwa ni binadamu kama binadamu wengine tu. Wala hawakuwa na fursa nyingi kama ulizonazo leo sasa. Harakati zao hazikuwa za haki zaidi ya hizi leo, na wala Mungu hakuwa pamoja nao kuliko alivyo pamoja nawe.
Uhalali wa jambo hili uko wazi, hivyo, vita yenye ulazima ni vita ya haki. Na ni tukufu jeshi ambalo matumaini yetu yapo juu yake. Kila mahali watu wana ari kubwa ya kufanya hili jambo, na kama ari ni kubwa, hakuna magumu yasiyowezwa kushindwa. Jambo la muhimu ni kuiga mifano ya wale niliokwisha waelezea.

Lakini zaidi, tumeona baraka za Mungu zisizo na kifani, bahari imegawanyika; wingu limetoka kuwaongoza njia; mwamba umetoa maji; Mana imenyesha kama mvua toka mbinguni; kila kitu kiko tayari kuwaunga mkono. Kilichobaki kufanywa, kinatakiwa kufanywa na wewe mwenyewe. Mungu hataki kutufanyia kila kitu, hataki kutuondolea uwezo wa kujiamulia mambo.

Wala lisiwe jambo la kustaajabisha iwapo hakuna hata mmoja, kati ya wale waitaliano niliowataja, ambaye aliweza kutimiza mambo ambayo tunatarajia kuona utawala wako ukitimiza. Au kati ya harakati nyingi za ukombozi, na vita nyingi ionekane kuwa ushujaa wa kijeshi wa Italia umeisha. Jambo hili limetokana na mfumo mbaya wa jeshi, na hakuna hata mmoja kati yetu aliyeweza kuunda upya
Hakuna kitu kinamheshimisha yule anayeanzisha taifa jipya kama kuunda sheria na taasisi mpya; kama vitu hivi vikisimama imara na vikakua, vitamfanya astaajabiwe na kuheshimika. Na katika Italia hali zinaruhusu kufanyika kwa marekebisho ya kila namna. Kama kichwa ni dhaifu basi miguu ni imara. Na tumejionea kwenye mapambano ya mmojammoja jinsi waitaliano walivyo na nguvu, akili na wepesi. Lakini ukija kwenye suala la jeshi wanaachwa mbali kabisa, na hili halitokani na kitu kingine bali uongozi mbovu wa viongozi wao. Wale wenye ujuzi wa kijeshi hawataweza kutii, na kila mtu anajiona kuwa ana ujuzi wa kijeshi. Na mpaka sasa hatujapata mtu mwenye bahati au uwezo wa kumfanya wengine wamfuate. Hivyo basi, kwa muda wa miaka ishirini ambao vita nyingi sana zimetokea, kila kunapokuwa na jeshi la waitaliano watupu, lilishindwa. Ushahidi huu unaonekana kwanza huko Taro, kisha Alessandria, Capua, Genoa, Vaila, Bologna, Mestri.

Kama utawala wako utafuata mfano wa watu hodari waliokomboa nchi zao katika nyakati za zamani, jambo la msingi kuliko yote ni kuwa na jeshi la kitaifa, hauwezi kuwa na jeshi lenye ujasiri, shupavu, na lenye uaminifu kama jeshi la kitaifa; japo kila mwanajeshi ni bora, wakiwa pamoja ni bora hata zaidi, hasa pale wanapoona wanaongozwa na kiongozi wao mwenyewe; wakipongezwa na kuthaminiwa naye. Kama utataka kujilinda dhidi ya wageni kwa ushujaa wa kiitaliano, hatua ya kwanza ni kuunda jeshi la namna hii.

Japo majeshi ya waenda kwa miguu ya Hispania na Uswiswi husifika kwa ushupavu, yote yana kasoro. Jeshi lililofundishwa kwa namna tofauti, si tu litaweza kusimama dhidi yao bali litakuwa na uhakika wa kuwashinda. Wahispania hawawezi kupambana na jeshi la wapanda farasi, na waswiswi husalimu amri mara wakutanapo na jeshi la waenda kwa miguu shupavu, na lisilotetereka kama wao. Imeonekana na bila shaka itaonekana tena wahispania wakishindwa kuhimili shambulio la wanajeshi wa Ufaransa, na waswiswi wakisambaratishwa na jeshi la waenda kwa miguu la wahispania. Japo hili la waswiswi kushindwa na wahispania hatuna picha kamili, lakini tuliweza kuona ishara katika pambano la Ravenna, huko jeshi la waenda kwa miguu la wahispania lilipambana na vikosi vya wajerumani ambao mbinu zao hufanana na waswiswi; kwenye pambano hilo, wahispania kwa wepesi wao, wakisaidiwa na ngao zao, walifanikiwa kupenya ukuta wa mikuki na kupambana na wajerumani ambao hawakuwa na namna nyingine ya kujilinda. Na kama isingekuwa jeshi la wapanda farasi wa ujerumani kuingilia, wangeangamizwa wote. Kwa kujua udhaifu wa majeshi haya unaweza kulifundisha jeshi lako katika mbinu za kuhimili jeshi la wapanda farasi na kutoogopa waenda
kwa miguu. Hili halihitaji kuunda jeshi jipya bali kubadili mafunzo ya lile la zamani. Na haya ndiyo mambo humpatia kiongozi utukufu na heshima.

Hivyo basi, hii ni fursa ambayo Italia inayotafuta mkombozi haitakiwi kuiacha ipite. Jinsi atakavyopokelewa kwa upendo mkombozi huyo katika mikoa ambayo imeteseka chini ya wavamizi wa kigeni, jinsi watakavyompokea kwa kiu ya kisasi, kwa machozi, na uaminifu, na ushikamanifu ambao maneno yangu hayawezi kuuelezea. Malango gani yatafungwa dhidi yake? Watu gani watakataa kumtii? Husda gani itasimama dhidi yake? Waitaliano watakuwa na nini dhidi yake zaidi ya heshima? Ukandamizaji huu wa washenzi unanuka kwenye kila pua.

Basi acha utawala wako mtukufu ujitwike mzigo wa kufanya jambo hili, na ulifanye kwa matumaini na ujasiri wote ambao jambo la haki hufanyika; hivyo basi, chini ya uongozi wako, nchi yetu ipate kuheshimika tena, na chini ya uangalizi wako maneno ya Francesco Petrarch yatimie:-

Magumu yatakuwa mafupi

Ushujaa ukijivika silaha dhidi ya uonevu wa washenzi;

Sababu roho ya mashujaa wa kale

Bado inapita kwenye mioyo ya waitaliano na kuwajaza uhai.


Ushairi wa Petrarch. XVI, V. 93-96

Mwisho
 
Back
Top Bottom