Ni Tanzania ya Uwazi, Kilimo Kwanza au Viwanda?

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
16,487
40,989
Maendeleo wala hayaji kwa kubahatisha, kuimba na kuitikia kwa nguvu bali kwa mipango thabiti iliyojengeka katika ukweli.

Mwalimu Nyerere, japo hakufanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini inaonekana alikuwa na ufahamu fika ni nini kinahitajika ili kufikia lengo.

Alipotangaza Azimio la Arusha au Azimio la Iringa la siasa ni kilimo aliandaa sera, kukawa na sheria, kukawa na vitabu na majarida mbalimbali. Waliosoma wakati ule watakumbuka mashairi kama 'Ukitaka Mali utayapata Shambani'; au 'Fikiri mimi maskini uvivu wangu shambani '. Vyote hivyo vilikuwa na nia ya kuishirikisha jamii katika sera ya kilimo.

Lakini vile vile Mwalimu alijenga taasisi mbalimbali za utafiti wa mazao mbalimbali ya kilimo kama vile Uyole, Ukiriguru, TAFIRI, n.k.

Mwalimu alijua huwezi kufanikisha jambo lolote bila ya kuwa na vituo vya utafiti. Kwa Mwalimu niishie hapo.

Tumwache Mzee Mwinyi na Ruksa yake.

Akaja Mkapa na serikali yake ya uwazi na ukweli. Haijulikani ilikuwa ni kibwagizo au wimbo. Hakukuwa na sera, hakukuwa na sheria wala hata ushirikishaji umma katika hilo alilloliamini. Ndiyo maana hata huo uwazi mdogo aliouanzisha, amekuja Magufuli ameifuta bila shida. Yeye anapendelea mambo ya giza, mambo ya kificho, mambo ya kutokushirikisha jamii.

Nimwache Kikwete na ari mpya yake lakini wakati wa utawala wake, kwa msisitizo mkubwa wa waziri mkuu wake Mizengo Kayanda Pinda, akaja na Kilimo Kwanza. Nayo haikujulikana ilikuwa nini. Sijui kilikuwa ni kibwagizo, wimbo au matamanio.

Kilimo kwanza kwa vile haikuwa sera na wala hakukuwa na sheria ya kusimamia, alipokuja Magufuli akafyekelea mbali kwa urahisi kabisa. Akapunguza ruzuku kwenye kilimo, akaacha au kupunguza sana kununua mazao ya kilimo, kilimo kikaachwa taabani. Ili kuua kabisa akazuia mazao ya chakula kuuzwa nje. Leo kilimo ni hoi bin taabani.

Magufuli akanyanyuka na Tanzania ya Viwanda. Hiyo Tanzania ya Viwanda haijulikani kama ni kibwagizo au matamanio. Lakini tunachojua siyo sera na wala hakuna sheria ya kusimamia au hata ushirikishaji umma. Ni kama mambo yanayopelekwa kwa pupa bila ya maandalizi yoyote wala kuwepo kwa taarifa zozote za utafiti juu ya namna sahihi ya kuyafikia hayo matamanio.

Kinachotokea sasa ni mazingaombwe. Tunaambiwa kuna viwanda vipya zaidi ya 4,000 vilivyojengwa. Mara ya kwanza nilidhani vipo Dar, ukienda huko huvioni. Nilidhani vipo Mwanza, sijaviona. Nikasema labda Pwani, nako havionekani. Utakavyoviona Pwani, vinavyoonekana kwa macho ya kawaida, havitazidi 5. Mikoa mingine tulipofuatilia, viwanda tulivyoambiwa vinazinduliwa, kumbe vilikuwepo kwenye uzalishaji tangu 2012, na vingine tangu 2014.

Ninachojiuliza, je, viwanda hivi zaidi ya 4,000 ni vya kishirikina kiasi kwamba sisi tusio washirikina hatuwezi kuviona?

Nilishangaa zaidi niliposikia kuwa kumbe hivyo viwanda zaidi ya 4,000 vimeajiri wafanyakazi 12,000 yaani kwa wastani kila kiwanda kina wafanyakazi 3! Hapo ndipo ile hoja ya kuwa hivi viwanda vya Tanzania, huenda siyo vile ambavyo kila mmoja anavidhania. Ni viwanda vya miujiza.

LAKINI KWA UHAKIKA, VIWANDA TUNAVYOVIELEWA SISI SOTE HAVIWEZI KUJENGWA BILA YA KUWEPO MIPANGO THABITI, MIPANGO AMBAYO HUJENGWA KWA KUTEGEMEA TAARIFA SAHIHI ZINAZOTOKA KWENYE VITUO VYA UTAFITI. LEO TAARIFA ZILIZOTAKIWA ZITOKE KWENYE TAASISI ZA UTAFITI ZINATOKA KWENYE VICHWA VYA WANASIASA.

Hatujaweza kuifanya Tanzania ya Uwazi, Tanzania ya Kilimo Kwanza wala Tanzania ya Viwanda.

Tanzania imekuwa ni gari lililokosa mwelekeo. Timeambiwa gari letu linaelekea Ziwa Victoria lakini tukilitizama, leo tunaliona linaelekea Mbagala, keshokutwa Bagamoyo, mara Lipo Rufiji lakini wenye macho yanayozidi uwezo wa macho yetu, wanasema gari limeshika kasi, na sasa linachanja uwanda wa juu wa Singida kuelekea Nzega.
 
Back
Top Bottom