Ni suala au swala?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,003
Swala linatumika sana Tanganyika ingawaje siku za karibuni nimeona matumizi ya suala badala ya swala yakiongezeka sana Bara. Wenzetu wa visiwani wanatumia suala.

Kuna maneno mengi yana tofauti kati ya kiswahili cha Tanganyika na kiswahili cha visiwani. Kwa mfano wenzetu wanatumia marikiti sisi tunaita soko, wao wanatumia skuli sisi tunaita shule, wao wanatumia buku sisi tunaita kitabu.

Je, katika maneno haya mawili suala na swala lipi ni sahihi? Je tunasema nataka kuuliza swali au suali?
 
Proper kiswahili-
Suala na sio swala, sote twajua swala ni mnyama au yaweza maanisha pia ibada hasa kwa waislamu.
Swali(question, pray) na sio suali.
Nafikiri tofauti nyingi zipo kwenye pronounciation tu.
 
Proper kiswahili-
Suala na sio swala, sote twajua swala ni mnyama au yaweza maanisha pia ibada hasa kwa waislamu.
Swali(question, pray) na sio suali.
Nafikiri tofauti nyingi zipo kwenye pronounciation tu.


Kwa mtazamo wangu finyu. Unachozungumza ni ku-bantu maneno yasio na asili ya kibantu. Huko visiwani, matumizi ya kiarabu yalikuwa makubwa kuliko bara. Hivyo maneno ya kiarabu yanachukuliwa kama yalivyo. Lakini bara maneno mengi yanapitia process ya ku-bantu.

Kwa mfano:
Sahil - Swahili
Mohamedi - Mwamedi
Suala - Swala
 
Tujiepushe na makosa haya katika uandishi wetu wa kila siku

MAELEZO yangu hapa chini ni mwendelezo wa makala nilizodhamiria kuwaletea wasomaji wangu kwa lengo la kuwatanabaisha kuhusu makosa mbalimbali yanayojitokeza katika lugha ya Kiswahili. Ni matumaini yangu kuwa mtayasoma na kuzingatia ushauri ninaowapeni. Angalia sentensi zifuatazo zilizopatikana katika magazeti yetu pamoja na marekebisho yaliyopendekezwa.

"Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema kuwa uhusiano uliopo baina ya CCM na CUF unaonyesha ubia wao hasa katika swala la muungano walioufanya huko visiwani Zanzibar."

Waandishi na wasomaji wengi wa Kiswahili wanashindwa kutofautisha kati ya maneno swala, swali na suala. Haya ni maneno yenye maana tofauti kabisa. Swala ni nomino na ina maana zaidi ya moja.

Maana ya kwanza ni ya kidini ambayo ni ibada maalumu katika dini ya Kiislamu inayochanganya kisomo na vitendo fulani kama vile kusujudu ambayo ni lazima kutekelezwa. Maana ya pili ya swala ni mnyama mwenye asili ya kurungu na anayefanana na mbuzi mkubwa.

Kwa upande mwingine, swali likitumiwa kama kitenzi lina maana ya kutekeleza ibada ya swala. Swali maana ya pili ni jambo linalotakiwa kujulikana ili kupata jawabu pia ulizo au hoja.

Kwa upande wa neno suala, likitumika kama nomino lina maana ya jambo linalizungumzwa au linalokatiwa shauri. Wingi wa suala ni masuala.

Kwa hiyo, ilitakiwa kuandikwa, "Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe alisema kuwa uhusiano uliopo baina ya CCM na CUF unaonyesha ubia wao katika suala la muungano walioufanya huko visiwani Zanzibar.

"Binti Sharifa Mpalu aliyekuwa akisomeshwa na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete ameshindwa kuendelea na masomo yake na kupata mimba."

Maneno ‘baada ya' yamekosekana katika sentensi hiyo hapo juu na hivyo kuifanya sentensi kutoeleweka vizuri. Ilitakiwa kusomeka,

"Binti Sharifa Mpalu aliyekuwa akisomeshwa na mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete ameshindwa kwendelea na masomo yake baada ya kupata mimba."

"Siku nne za sherehe ya Jubilee ya kutimiza miaka 60 ya Malkia Elizabeth II nchini Uingereza, mchana wa jana zilihamia katika Mto Thames."

Katika kukamilisha taarifa hii, inatakiwa kuonyesha miaka hiyo 60 ni ya nini. Kwa hakika ilitakiwa kuandika kuwa ni ya utawala wa Malkia Elizabeth II na wala siyo ya kitu kingine. Lengo ni kuweka taarifa wazi ili kuepuka maswali mengi kwa wasomaji ya kujiuliza.

"Alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo uliofanyika Dodoma Hoteli kuwataka wabunge wote wajiunge na chama hicho."
Katika muundo wa sentensi ya Kiingereza, inaruhusu kuandika sentensi yenye muundo wa ‘Dodoma Hoteli', lakini kwa muundo wa sarufi ya Kiswahili, tunaandika ‘Hoteli ya Dodoma.'kama tulivyozoea kusema ,‘Nyumba za Serikali na kwa Kiingereza huwa ni ‘Government Houses.'

"Bolt alipata ajali ya gari mwaka 2009 na kukimbizwa hospitali na katika ajali hiyo alikuwa na mwanariadha mwigine mahiri wa Jamaica, Asafa Powell."

Majina ya nchi huandikwa kulingana na misingi ya Kiswahili. Kwa hivyo, Jamaica huandikwa Jamaika. Pili, neno kukimbizwa limepwaya hapa. Neno hili linatokana na mnyambuliko wa neno kimbia na maana yake ni kufuata kwa mbio nyuma ya mtu au mnyama, fukuza, fanya kitu kiende kasi kama vile kukimbiza gari kwa maana ya kuendesha gari kwa kasi.Ilitakiwa kutumia neno kuwahishwa kwa maana ya kufanya jambo kabla halijaharibika.

Kwa hiyo, isomeke, "Bolt alipata ajali ya gari mwaka 2009 na kuwahishwa hospitali na katika ajali hiyo alikuwa na mwanariadha mwingine mahiri wa Jamaika."

"Abilate alikuwa akitibiwa nchini Ufaransa alipokelewa na Rais wa Togo pamoja na Waziri wa Michezo wa Togo."

Ni sahihi kusema kuwa Abilate alipokewa na Rais kwa maana kuwa akilakiwa na rais. Siyo sahihi kusema kuwa alipokelewana rais kwani hakuna kitu alichopokea rais na waziri kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa hiyo, alipokewa na Rais wa Togo pamoja na Waziri wa Michezo.

"Viongozi wa dini wakisikiliza taarifa wakati uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya uchumi nchini inayosomeka kama, ' The one bilioni question.' jijini Dar es Salaam jana."

Ziko dosari mbili katika sentensi hii. Kwanza, ni kukosekana kwa kiunganishi cha ‘wa' kati ya neno wakati na uzinduzi na hivyo kusomeka kama ‘wakati wa uzinduzi'

Pili, maneno "yanayosomeka kama" kutokidhi haja. Ilitakiwa kuwepo kwa maneno kama ‘inayojulikana kama au inayoitwa. ' Sentensi isomeke, "Viongozi wa dini wakisikiliza taarifa wakati wa uzinduzi wa ripoti kuhusu hali ya uchumi nchini, inayojulikana kama ' The one billion question.'

"Mbunge wa Geita, Hussein Amar ametoa msaada katika zahanati nne za jimbo hilo kwa kuwekeza nishati ya umeme wa jua."

Ni bora angeandika kuwa ametoa msaada huo kwa ajili ya kupata nishati ya umeme unaotokana na nguvu za jua.
Yafaa ijulikane kuwa mtu anapowekeza lengo lake ni kupata faida kwani maana ya wekeza ni kutumia fedha au mali katika biashara kwa lengo la kuzalisha zaidi.

Kwa upande mwingine unapotoa msaada hutarajii kufanya biashara na hivyo kupata faida. Hapa ndipo mwandishi anaweza kuipotosha umma kwa kuandika jambo ambalo halina ukweli.

"Kituo cha televisheni cha ITV kitarusha live tukio hilo."

Huu ndiyo mwelekeo wa vijana wasomo wa Kitanzania tunaosikia katika mazungumzo na sasa umehamia katika maandishi.
Ni hatari kwa matarajio ya baabaye ya lugha ya Kiswahili kwani huko tuendako hakutakuwa na Kiswahili kitakachofuata misingi yake ya asili bali kutakuwa na Kiswahili uchwara ambacho ni mchanganyiko wa Kiingereza na Kiswahili. Kwa mtindo huu tunaiharibu lugha yetu. Jamani wasomi, tujihadhari na mwelekeo huu wa kuchanganya lugha.

"Nilikutana na mama mmoja mtu mzima kikongwe. Kutokana na umri wake anatetemeka, kibiongo kimechomoza mgongoni."
Maelezo yaliyotolewa hayatoshekelezi kupata picha kamili ya mama huyu kikongwe kwa sababu neno kibiongo limetumika vibaya. Maana ya kibiongo ni mtu ambaye amepinda mgongo. Pili, kibiongo ni sehemu ya mgongo wa mtu yenye kinundu. Hivyo, kusema kuwa kibiongo kilichochomoza mgongoni ni makosa kwani kilichochomoza ni kinundu lakini bado mhusika hajaelezwa kama amepinda mgongo.

Maelezo kamili yawe: " Nilikutana na mama mtu mzima na kutokana na umri wake anatetemeka na ni kibiongo."

"Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Zitto Kabwe pia alisimama kwenye kiti na kutaka mwongozo juu ya jambo hilo lakini hata hivyo hakupewa fursa."

Msomaji ataelewa kuwa Zitto Kabwe alisimama na kutaka mwongozo. Kama tutasoma kwa makini sentensi hii, utagundua kuwa si kawaida kusimama kwenye viti kwa wabunge. Inafahamika kuwa mbunge alisimama na kutoa hoja.

Kwa hiyo, kusimama kwenye kiti siyo sahihi. Vilevile, matumzi ya ' lakini na hata hivyo' hayatakiwi kuandikwa kwa mfuatano. Ama tunatumia ‘lakini' au ‘hata hivyo' lakini siyo yote kwa pamoja.

Tujiepushe na makosa haya katika uandishi wetu wa kila siku
 
suala ni jambo fulani
swala ni ibada/ mnyama
na siku zote tunauliza maswali ama swali sio suali

ila napenda kukutaarifu kuwa kuna kiswahili na viswahili
kiswahili ni kile sanifu kilichokubalika kuwa rasmi. viswahili ni kile kiswahili chenye kuathiriwa na vilugha mama vyetu hapa unapata kiswahili cha kisukuma,kimombasa, kichaga ama cha kitanga. hivyo katika kiswahili sanifu unaweza kukuta kitu kinatamkwa hivi ila ukienda sehemu fulani wanakiita vile.
 
Kwa cha Barawa, Mrima, Mvita, Jomvu, Ngazija,Tumbatu, Mgao, Kisangani etc ?

Maana Mrima kwetu ukiulizwa na mkeo "umelalaje?" na kujibu "Nimelala Uzuri" unaweza kuibua kesi na kuulizwa "Uzuri kwa nani?"

Wakati Unguja kusema "nimelala uzuri" au "najisikia uzuri" ni ada.

Kiswahili kipana.
 
Back
Top Bottom