Ni ndoto maneno kuneemesha Watanzania

Kamanda

Senior Member
Dec 5, 2007
150
176
Miaka 47 ya uhuru wa Tanzania ni dhahiri kuwa rasilimali za nchi hazitumiwi/hazitumiki na kama zinatumiwa na kutumika zinawanufaisha wachache sana.

Rasilimali zilizomo Tanzania zilizoanza kutumika/kutumiwa na ambazo hazijaguswa na kuanza kutumika, zinaweza kuifanya Tanzania kuwa na watu wenye ustawi bora wa maisha, masikini wachache, watu walioerevuka kwa kupatiwa elimu bora, wataalamu waliobobea katika fani tofauti, idadi kubwa ya viwanda, huduma bora za afya , hospitali zenye madaktari mabingwa na vifaa vya kisasa.

Kinachosikitisha ni kwamba watu kutoka mataifa mbalimbali, wasomi wa fani na wanasiasa mahiri wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kama; ni vipi Tanzania imekuwa ombaomba na kubakia mkiani mbele ya mataifa mengine ambayo yanakabiliwa na vita ya miaka kwa miaka, uchache wa rasilimali, na nchi nyingi kutokuwa na ardhi zenye rutuba kuliko ardhi ya Tanzania.

Majibu ya maswali haya aghalabu hubaki katika parandesi na hayajibiki kwa wepesi na kwa ufasaha unaostahili mbele ya nyuso za watu wastaarabu,waliosoma na kufuta ujinga na pia kwa wale wahisani na wafadhili wanoisadia nchi hii ya Tanzania kila kukicha kwa kigegezo cha " utulivu na amani" ya kudumu.

Mwaka 2005 ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi Tanzania ambapo jumla ya vyama vyote 17 vya siasa viliingia katika mbio za kuwania udiwani,ubunge na urais wa kuongoza dola kuelekea 2010. Watanzania walioamka wanaitamani nchi yao, urithi walioupata kutoka kwa akina Kinjikitile na Mangi na wengine waliomwaga damu yao kwa kuililia nchi hii ijitawale na itumie rasilimali zake kwa maendeleo yao na vizazi vyao.

Watemi na machifu wetu waliwakataza kwa kupigana vita wakoloni wasiibe pembe za ndovu, ngozi za chui, mamba, dhahabu, almasi katika ardhi yetu ili zilifae taifa hili na vizazi vijavyo.

Matunda haya kamwe sio miliki na urithi wa chama fulani cha siasa na utawala wa aina moja, ni miliki na hazina ya taifa na watu wake bila ya kujali aina ipi ya chama cha siasa kimo madarakani na kutawala.

Lakini, hili halionekani katika Tanzania ya sasa bali linalodhihiri ni kundi la watawala wachache wakipania kuidhinisha matakwa yao kwa kuzitumia rasilimali zetu kwa kujinufaisha wao na familia zao.

Mara baada ya kuruhusiwa kwa vyaa vingi vya siasa, idadi kubwa ya Watanzania walidhani kuwa wamepata msemaji wao na mtetezi, kumbe haikuwa hivyo, viongozi wengi wa vyama hivyo nao wamegeuka kuwa walaji tu.

Ukivitupia macho vyama hivi unaweza kukata tamaa na pengine unaweza useme hakuna haja abadan ya kufanyika uchaguzi na kama unafanyika ni kutaka kujifurahisha na demokrasia katika kutimiza domokrasia-Makengeza na demo-ghasia mjini na vijijini.

Chama Cha Mapinduzi kikiwa chama tawala ndicho kinacholalamikiwa kwa uharibifu na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, kuidhinisha na kuridhia mikataba ya ghiliba kuliko ile ya Karl Peters wa Ujerumani na machifu wa makabila ya Tanganyika.

Kimsingi, wakoloni waliingia mikataba na baadhi ya machifu wetu kwa kuwadanganya na kuwapa shanga na peremende kwa kubadilishana na ardhi iliyojaa madini na kila aina ya utajiri.

Mikataba ile haina tofauti na hali ya sasa ya wawekezaji, haina faida wala tija kubwa kwa Watanzania kwani wanachokibeba wawekezaji katika ardhi yetu ni kingi kuliko maslahi wanayopata wananchi ambayo hayana kipindi kirefu cha maendeleo katika maisha yao na kizazi kijacho.

Ukigeuza macho na kuutazama upinzani unaweza kutema mate na kuona kichefuchefu na ugegezi ukitanda kinywani kwani huko ndiko makundi ya walafi wa ruzuku walikopiga kambi,kufukuzana kusikokwisha na ukiukaji wa katiba zao na dhihaka kubwa ya demokrasia katika vyama hivyo.

Katika kambi ya upinzani mwenyekiti na katibu ndiyo wenye sauti na mamuzi na hawataki kupingwa lau kwa nguvu ya hoja ili kujenga mustakabali wa chama kisichofanana na CCM na kuwatia moyo na ari Watanzania kuamini vyama hivyo vinahitaji mabadiliko aidha ya kiuchumi, kisiasa na kidemokrasia.

Ni ving'ang'anizi wakuu wa madaraka ndani ya vyama hivyo vya siasa hawataki abadani mabadilko ya uongozi wakiaamini kuwa wao ni waanzilishi na kutoka kwao ni kuruhusu kundi jipya la uongozi kujipatia ruzuku ya ubwete ambayo hawakuisumbukia.

Kudumu kwa CCM katika madaraka kwa miaka mingi pengine ni matokeo ya kujisahau kwao katika kuutumikia umma kwa njia za usahihi na uwajibikaji chanya, lakini unaweza kupata kitete unapoutazama upinzani na mustakabali wake ni wazi unaweza useme kheri ya Mussa kuliko ya Firauni.

Domokrasia au Domokrasia katika Afrika na njaa za viongozi wetu zisizo na simile, uroho wa madaraka na ulafi wa kuiba usio na ashakum kwa mali za serikali ni hofu juu ya hofu na sijui kama inaweza kupatikana Tanzania tunayoitaka na tunayoiona inawezekana na kuwa yenye neema stahili mbele ya Watanzania wa mjini hadi vijijini.

Tanzania inahitaji kuwepo kwa utawala bora wa sheria huku watawala na watawaliwa wakijua maana ya kuheshimu na kutii haki za binadanu, uwajibikaji, ushirikishwaji, uwazi na ukweli na uhuru wa watu kusema na kukosoa kwa sauti ya juu ya kujenga bila ya kuchochea na kuhatarisha mchakato mzima wa ustawi wa amani.

Hatutoweza kamwe kutumia rasilimali zetu kwa mizania iliyo sawa ikiwa mikataba ya wawekezaji ina kuwa na usiri mkubwa huku dhamana na maslahi ya Taifa anayekabidhiwa hatakiwi kuhojiwa na kuulizwa ni vipi ameafiki na kuridhia.

Watanzania wana haki ya kuamka na kutanabahi ni vipi ndani ya chama tawala wanaweza kubaini ujinga na uzembe uliomo na wale wa upinzani wazinduke na kuona ni ipi aina ya chama mbadala ipatikane kabla ya kuweka mbele hamasa na jazba zinazopelekea nchi yetu izidi kuwa ya tano kutoka mwisho kwa masikini uliwenguni.

Mfumo wa siasa uliopo unatoa fursa ya kufanya mabadiloko ya utawala ingawaje mabadilko yanazingwa na utata wa mazingira ya sheria katika katiba iliyopo, hii haiwezi pia kuwa kikwazo iwapo vyama vya upinzani vinaweza kujipanga katika mstari mnyoofu wa kujenga nguvu ya hoja badala ya hoja zenye ubabe,vishindo, matusi na makelele.

* Sehemu kubwa ya hoja hii imepatikana kutoka gazeti la KULIKONI la leo
 
Uroho uleule waliokuwa nao machifu wetu ndiyo huo huo walionao watawala wetu leo. Lakini machifu walikuwa even better than watawala wetu leo. Uroho wa leo umezidi. Hatuoni hata haya kuuza natural resourses zetu.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom