Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,474
- 39,987
Maswali haya yote mawili yana umuhimu wa kipekee kwenye mwaka huu wa 2020. Ni nafasi kwa Watanzania kuamua kuthibitisha maamuzi yao ya 2015 au kuyatengua; kuwathibitisha tena kwenye nafasi zao viongozi wetu ama kuwatumbua. Kwa vile madaraka ya kutawala yanatoka kwa wananchi basi ni wananchi ndio wenye uamuzi wa mwisho; siyo polisi, siyo usalama wa taifa, siyo wahisani, siyo vyama vya siasa; ni wapiga kura. Hivyo, wapiga kura katika mwaka huu wanaitwa kufanya uamuzi mkubwa na kila kura itakuwa na thamani yake.
Ili wapiga kura wetu wafikie uamuzi sahihi ni lazima wawe huru kufikia uamuzi huo. Hii ina maana ya kuwa mbinu au kitu chochote kikifanywa ama na chama, vyama au dola kujaribu kuzuia wananchi kufikia uamuzi huo basi kutatia doa maana nzima ya uchaguzi. Ni kwa sababu hiyo, viongozi wote – kuanzia Rais hadi wabunge yawapasa kutambua kuwa hawana sababu ya kuwaogopa wapiga kura. Kama mwaka 2015 watu walienda na kujinadi mbele ya wapiga kura na wananchi wakawakubali basi ni wazi hakuna sababu ya kuwaogopa wananchi hao tena mwaka 2020. Ni muhimu sana kila anayechaguliwa ajijue na aonekane amechaguliwa na wananchi kweli kweli.
Kwa sababu hiyo basi mwaka huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vingine vyote vinavyohusika na mchakato wa kuhakikisha uwazi, usawa na haki katika uchaguzi mkuu vinatekeleza majukumu yao kwa weledi uliopitiliza. Hii ina maana ya kutovumulia vitendo vya uvunjifu wa taratibu, upendeleo, ukandamizaji au uminyaji wa wapiga kura. Kama hili halitatokea, ni kweli tunaweza kuwapata washindi, tunaweza kupata watu watakaoitwa wamechaguliwa lakini watu watakuwa na minong’ono ya kuwa “hawakushinda bali walishindishwa”. Ni muhimu anayeshinda ajulikane ameshinda kweli kweli.
Hata hivyo, ni muhimu pia kujua kuwa demokrasia siyo kushinda tu; na si kweli kuwa demokrasia inakuwepo wakati wa kushinda tu bali pia ni kujua demokrasia ni pamoja na kushindwa. Ni lazima mifumo yetu ihakikishe kuwa mtu anaposhindwa ameshindwa kihalali na kutoa nafasi kwa watu hao au mtu huyo kukiri kushindwa (concede defeat). Swali kubwa la mwaka huu basi haliko katika kushinda tu bali pia katika kushindwa; tumekuwa na shida sana kwa watu kukubali kushindwa na wakati mwingine watu kulazimisha kushinda kana kwamba, wameumbwa kushinda! Tanzania ni ya Watanzania wote, na hata wale walioshindwa nao ni Watanzania na hata wale ambao walikuwa wameshinda 2015 lakini wakajikuta wanashindwa 2020 kujua kuwa nao ni Watanzania. Kushindwa hakumuondolei mtu Utanzania wake, na kushinda hakumfanyi mwingine kuwa Mtanzania zaidi kuliko wengine.
Hivyo, basi tunapoingia taratibu na kwa matumaini mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu 2020 napenda kuwatakia wote kheri na fanaka na baraka kwa wale wote ambao wataitwa kulitumikia taifa letu kwa miaka mitano mingine ijayo. Wale ambao tutasimama kama wagombea, na wale ambao tutawapigia kura wagombea hao sote tutimize wajibu wetu ili kuhakikisha kuwa mwisho wa siku bado Tanzania Moja yenye hatima moja inaendelea kusonga mbele.
Kheri ya Mwaka Mpya – Tukutane Kampeni 2020.
MMM
Januari 1, 2020.