Ni muungano gani hasa twautaka Watanzania; hii imekaa je wadau.

Makaimati

JF-Expert Member
Apr 4, 2011
462
87
Ni muungano gani hasa twautaka Watanzania?

Yahya Charahani

KELELE dhidi ya Muungano zinazidi kiasi kwamba, sasa wapo baadhi wameanza kuhoji nini hasa sababu ya muungano huu? Wazanzibari wanalalamika wamemezwa, Watanganyika wanalalamika wamepoteza Tanganyika yao na wananyonywa, lakini Serikali inasema itaulinda Muungano kwa nguvu zote! Hii inatia hamasa kwa mjadala zaidi.

Inatia hamasa sababu mara nyingi Wazanzibari wanahoji Muungano wetu ni muungano gani wa kiuchumi kati ya "The Free Trade Area" au "The Customs Union" au "The Common Market" au "The Economic Union? Wanataka nchi yenye uhuru zaidi, wanataka mipaka yao itambulike rasmi, wanataka maendeleo yao bila kupitia upande wa pili.

Lakini kwa sisi Wabara, mara nyingi tumekuwa tukiwaona Wazanzibari ni walalamikaji hali ambayo imetufikisha kujenga tabia ya kujiona kuwa "sisi Wabara ni bora", au "sisi Wazanzibari ni bora". Pamoja na hayo sisi Wabara hatujijui tunataka nini, bora ya wenzetu za visiwani wana mwelekeo fulani hata kama ni hasi kwa Muungano.

Sitapenda kuingia ndani zaidi kwenye mikataba ya Muungano na ubora, au kasoro zake kinachotosha cha msingi kujiuliza ni lipi muhimu, kuondoa kasoro zilizopo ama kuuvunja muungano.
Zanzibar imeundwa kwa visiwa viwili ambavyo ni Unguja na Pemba. Nchi ya Tanzania ni muunganiko wa nchi mbili tofauti ambazo ni Tanganyika na Zanzibar, ambapo Zanzibar ina mikoa mitano na Tanganyika ina mikoa takribani ishirini na minne sasa , kwa pamoja inafanya Tanzania kuwa na jumla ya mikoa ishirini na tisa.

Waliounganisha walitumia falsafa kubwa na busara za msingi. Sasa inakuwaje kunakuwa na fikra za kunyonyana au kuoneana, au kuwapo fikra za upande mmoja kuuona mwingine mzigo na kupuuza jitihada za awali?

Nafikiri huu ni wakati mwafaka kwa Serikali yetu kushughulikia kwa haraka malalamiko na mtazamo huu wa wananchi juu ya Muungano, kwa kuweza kusikiliza maoni ya Watanzania wengi zaidi, ninaiomba Serikali yetu ifanye kazi yake sawasawa na kuhakikisha kwamba Watanzania wametoa maoni yao.

Ikiwa wananchi kutoka eneo fulani la nchi hawatapewa fursa ya kutoa maoni yao, basi kazi hiyo haitakuwa na maana yoyote.
Mambo ya zamani hatuna haja nayo tena, kuhoji eti Muungano wetu ni haramu, au si haramu ni sawa na kuhoji uhalali wa ndoa ya baba na mama yako wakati tayari mtoto keshazaliwa, kama alivyosema mkongwe wa siasa nchini, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye nakubaliana naye katika baadhi ya hoja zake, ingawa zingine sizikubali.

Haya mambo ya Muungano yataendelea kusemwa kila mahali na ninapenda watu wasikilizwe kwasababu kilio chetu kitatolewa hapo, ninawaomba watu wenye hasira juu ya mambo yanayohusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar waache chuki.

Tusiwe kama Indian Bazaar, ambapo kila mmoja anajisemea mambo yake mwenyewe. Hivi sasa hapa Tanzania kila mmoja akitaka kusema, anasema tu hata kama hakuchaguliwa au hana hoja yenye mantiki wala jambo lolote la msingi.

Kibaya zaidi ni kwamba, wanaozungumza wanawasema vibaya wenzao ndani ya Muungano. Wabara wanazungumza vibaya sana dhidi ya Wazanzibari na Wazanzibari nao wanawasema vibaya wenzao wa Bara na mvutano huu umefikia katika ngazi za kitaifa. Hayo hayafai, nadhani jambo la msingi ni kuzungumza mambo yenye manufaa kwa Tanzania na wananchi wake wote ili tuijenge nchi yetu.

Hii yote ni kwasababu tunasema kwamba kuna uhuru wa kuongea. Lakini maneno na tafsiri zinazotolewa dhidi ya Muungano huu na wanayofanyiwa Watanzania Bara na wale wa visiwani si uhuru wa kuzungumza bali ni mambo wanayoyapenda wao wenyewe.
Ninayo furaha kwamba mpaka sasa Muungano wetu umeleta heshima na kwa maana hiyo mambo yanayozungumzwa bado yana chembechembe za heshima.

Heshima ni jambo la msingi sana. Siku hizi kazi kubwa ya mwanasiasa ni kujaribu kumchafua mwenzake, badala ya kuwajengea watu maisha bora, kuwafanyia wananchi kazi na kuwatafutia mikopo…la hasha, hawafanyi hivyo.

Ni vyema Watanzania tuachane na ubaguzi, kutupiana lawama kwani hata katika vitabu vya dini imekataza ubaguzi wa Uzanzibari na Ubara kwa maana ya ukabila. Naamini haki inapotendeka mambo yatakuwa shwari siku zote na hali itakuwa shwari, lakini kama haki haitatendeka, tuendo tuishi bila amani.


Yahya Charahani ni Mchambuzi wa Masuala ya Jamii, Siasa na Utawala.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom