Ni mapambano au mapambo ya rushwa na ufisadi?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,890
Ni mapambano au mapambo ya rushwa na ufisadi?

Waziri Kindamba, London Februari 27, 2008
Raia Mwema

MATOKEO ya Kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba wa kufua umeme wa kampuni ya Richmond si tu yameacha maswali mengi bila ya majibu ya kutosha, bali yameleta mwangaza mpya wa matumaini kwamba ‘penye nia pana njia’.

Matokeo hayo yameleta pia maswali kadhaa likiwamo je, chombo cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni chombo cha mapambano dhidi ya rushwa kweli au ni chombo cha kupamba na kupendezesha rushwa na ufisadi.

TAKUKURU iliisafisha Richmond ikisema katika ripoti yake kwamba hakukuwa na dalili yeyote ya rushwa, na kwamba Taifa halikuingia hasara kwa namna yeyote ile, kitu ambacho sasa kila mmoja wetu najua si kweli.

Katika nchi nyingi zilizondelea na zinazohitaji kuleta maendeleo ya kweli, kama chombo kilichopo kwa malengo fulani hakikidhi mahitaji au hakifanyi yale yaliyotarajiwa kufanywa, hakuna njia nyingine isipokuwa kukivunja chombo hicho au kukifanyia mabadiliko makubwa ili kuleta tija na kurudisha imani kwa umma.

Ni kweli sasa itahitaji nguvu ya ziada kuiaminisha taasisi hiyo kwa umma, hasa kutokana na malalamiko ya muda mrefu kwamba chombo hicho kimekuwa kikiwakalia kooni samaki wadogo huku papa wakibaki bila kuguswa.

Viongozi wetu mara kadhaa wamepata kujiuliza na wengine tumesikia wakijiuliza maswali hayo hadharani; kwa nini nchi yetu ni masikini ilhali tunazo sifa zote za kuwa matajiri wenye maendeleo ya kupigiwa mfano?

Tunayo amani na usalama ambayo kwayo ni msingi mkuu wa kuleta hayo maendeleo, na rasilimali tele tulizojaliwa na Muumba. Jibu ni jepesi ingawa halielezeki kirahisi; ni rushwa na ufisadi. Baadhi ya viongozi tuliowaamini si waadilifu na hawana uchungu na nchi. Ni wala rushwa na mafisadi.

Katika hali hiyo nini kifanyike?

Kwa kuwa nchi yetu imezama katika rushwa kubwa kubwa na ufisadi kwa ujumla, ambao TAKUKURU imeshindwa kupambana nao basi haina budi kuvunjwa au kufanyiwa marekebisho makubwa sana na pengine kuunda chombo mfano wa EFCC (Economic and Financial Crimes Commission) cha Nigeria kilichokuwa chini ya mpiganaji wa kweli dhidi ya rushwa na ufisadi, Nuhu Ribadu.

Nuhu Ribadu wakati akiiongoza EFCC si tu kwamba alikuwa ni mwiba kwa mafisadi nchini Nigeria, bali aliweza kurejesha serikalini mali zilizopatikana kwa ufisadi na ameweza kwa kiasi kikubwa kurudisha imani ya jumuia ya kimataifa na wananchi wa Nigeria, nchi ambayo kwa muda mrefu ilisifika kwa rushwa na ufisadi wa kupita kikomo.

Uozo wa namna hii ndio unaotakiwa kuanikwa na kuondolewa popote pale utakapoonekana nchini mwetu. Lakini kama alivyopata kuandika ndani ya Raia Mwema (Bw. Mbwambo- makala ya Ngozi Okonjo wa Nigeria), je tunao akina Nuhu Ribadu wetu hapa Tanzania? Nani atamvika paka kengele?

Inatupasa kuelewa kwamba rushwa, mikataba mibovu na ufisadi kwa ujumla vyote ni ndugu moja, ni watoto waliozaliwa toka tumbo moja, na kama TAKUKURU haiwezi kupambana nao wote ikijitanabahisha kwamba yenyewe ni ya kupambana na rushwa pekee, basi chombo hicho hakikidhi mahitaji.

Muswada wa kuzuia kuchanganya biashara na siasa kama inavyokusudiwa, upelekwe haraka bungeni bila ya kuchelea, ili sheria ije haraka na iwe na meno makali ya kung’ata pale ambapo kutatokea mgongano wa kimaslahi.

Ukweli utabaki pale pale, huwezi kuwatumikia mabwana wawili maana hata vitabu vitakatatifu vimesema hivyo na hata wasio na dini wanalikubali hilo kimsingi. Na kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete ameonyesha utayari katika hilo, ni dalili njema.

Kingine cha kufanya ni kuzuia akaunti za wote waliotajwa kuhusika na ufisadi na akaunti hizo zichunguzwe, pale ambapo tuhuma zitakapothibitishwa kuwa kweli, sheria ichukue mkondo wake na mali zao zitaifishwe. Fedha zitakazopatikana ziingizwe kwenye miradi ya maendeleo.

Kama ambavyo imesisitizwa mara kadhaa, Tanzania yenye neema inawezekana. Lakini itawezekana tu pale ambapo viongozi wetu tuliowapa dhamana, watakapoyavaa matatizo ya wananchi wa kawaida na kuyaona kama matatizo yao binafsi na kupambana na ufisadi kwa kuuchukulia kama vita binafsi.

Waichukie rushwa na kuigopa kama wanavyoogopa ukimwi, wasimamie haki kuhakikisha hakuna mtu anadhulumiwa na kuongeza uwazi katika uendeshaji wa Serikali na vyombo vingine vya umma.

Kama alivyopata kuota Mchungaji Martin Luther King, nami nnayo ndoto ingawa ni tofauti kidogo na Mchungaji King alivyoota lakini misingi ni ileile. Ndoto ya kwamba nchi yetu itafanikaniwa na kuwa na yote mazuri ambayo tunatamani kuwa nayo, nchi isiyo na ufisadi na rushwa, matajiri na masikini kuwa na haki sawa mbele ya sheria, kupungua kwa tofauti kubwa ya kipato kati ya walio nacho na wasio nacho, neema na utajiri wa rasilimali zetu kutumika kwa ajili ya manufaa ya Watanzania kwa ujumla.
 
that goes without question...tukururu haifai!
lakini if you come and think about it, Kikwete atawafukuza wangapi? ccm wote wamehusika kama si na richmond basi wamehusika na EPA, akiwaondoa hao atawachagua nani?

kazi ipo mwka huu
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom