Ni kosa gani alilolifanya Aboud Jumbe kustahili 'kifungo cha maisha'?

Kuna mengi yaliendelea achilia nafasi ya umakamu Rais, kuna pesa za karafuu zilizomezwa na muungano na huyu mzee hilo lilimuuma na kuhoji kwanini imekuwa hivyo. Pia kuna swala za Zanzibar kuwa nchi alilisimamia kwani alitaka kuwapo na serikali tatu na hilo likawa mwiba mkali kwa Nyerere akaona jamaa ni msaliti akishirikiana na kina Seif Sharif Hamad. Pia alihoji uhusiano wa Vatican na Tanzania na hilo halikumpendeza Nyerere akaona atamuharibia uongozi pengine (Soma katika kitabu chake).

hapo kwenye blue hapo hebu tufafanulie kuna nin cha zaid, zaid ya uhusiano wa kibalozi kama ilivo tanzania na saudi Arabia au Iran au Palestina.
 
Mdondoaji,

..hata Mzee Mwinyi naye kajibanza huku Tanganyika "analima" maembe.

..Sheikh Idiris Abdul Wakil Nombe naye alikuwa kajinafasi Ilala-Bungoni.

..Maalim Seif naye inasemekana alikuwa akiishi hotelini hapa DSM. sijui kama ni kweli.

..Hamad Rashid Mohamed naye anaishi Tanganyika akifanya biashara ya vyuma chakavu.

..Zanzibar itajengwa na nani kama watu kama hawa hawataki kwenda kuishi huko?
Kweli viongozi wakubwa wanapostaafu na kurudi kwao wanasaidia sana kuchochea maendeleo ya maeneo wanayotoka. Mfano baba wa taifa Mwl Nyerere baada ya kustaafu alirudi kijijini Butiama kuendelea na kilimo kama alivyoamini kuwa siasa ni kilimo.Maendeleo ya kijiji cha Butiama yasingekuwa hivi kama Nyerere asingerudi na hatimaye baada ya kufa alizikwa pale. Cleopa Msuya mmoja wa mawaziri wakuu wastaafu alirudi Usangi na kuchochea maendeleo huko. Siamsahau pia Peter Kisumo. Malecela naye yuko kwao. Nakubaliana kabisa na wewe kuwa ni vizuri viongozi wakubwa wanapostaafu warudi kwao ili kuchochea maendeleo. Wakati mwingine nadhani viongozi wasiorudi kwao huwa wanakuwa ni wale ambao hawakuwa wakithamini kwao kwa kwenda mara kwa mara na kusaidia maendeleo ya maeneo yao hivyo baada ya kustaafu wanashindwa kurudi kwakuwa hawakuweka mazingira mazuri kwao. Wengine huishia kuzikwa nje ya kwao. Vile vile kutokana na kukosa ushirikiano na watu wa maeneo ya kwao wanashindwa kurudi. Hapa ndipo najiuliza imewaje Mkapa ahamie Lushoto badala ya Masasi baada ya kustaafu. Sumaye naye yuko kwao? Mimi nawashauri viongozi wachukue changamoto ya Mwl Nyerere ya kurudi vijijini kwao baada ya kustaafu na sio kung'ang'ani Dar mpaka warudishwe wakiwa wafu. Wakihitajika kwa ushauri watafuatwa huko huko.
 
Inavyosemekana kosa, alilofanya Jumbe ni kuwa na dhamira ya kuanzisha mjadala wa kitaifa kwa lengo la kuanzishwa hapa nchini mfumo wa shirisho badala ya serikali mbili.

Si kweli, Jumbe alitaka kutangaza kuvunjika kwa muungano akiwa ughaibuni nchi moja ya kiarabu. Siku ambayo ilikuwa aondoke Nyerere akaenda Zanzibar na kumfuata pale Ikulu. Saa ilipofika ya kuondoka akamwambia eenhe, itakuwaje sasa juu ya safari yako, maana nasikia una safari leo kwa sababu maalum.

Na huo ukawa mwisho wa Jumbe kisiasa.

Waliochangia katika kuuweka wazi mpango wa Jumbe ni pamoja na Seif. Kusema kweli, walimstahi sana, lazivyo ilikuwa atiwe ndani kwa uhaini.

Baadaye JUmbe alianza kuandika makala za kuikashifu serikali, na wakamwambia vema sana, serikali inayokupa marupurupu yote hayo ndio hiyo unayoitukana. Kwanza mhaini mkubwa wewe. Wakamwondolea benefits nyingi tu!
 
Jamani basi hata kabla ya kutoa tuhuma muwe na uhakika wa historia basi... ati Jumbe yuko kifungo cha maisha!

Miaka ya tisini nimewahi kufika kwa Jumbe na siku ona dalili za kifungo alikuwa anasafiri na kuishi huru labda sijui maana ya kizuizini. alikuwa jirani mzuri kule mji mwema na sikuona akizuiwa kwenda atakako.
 
siasa za uzushi sijui zitatupeleka wapi!!!! Mzee wa watu yupo zake raha mustarehe....! sasa sijui hicho kifungo ni cha namna gani!
 
Mdondoaji,

..inawezekana Mzee Aboud Jumbe hataki kushiriki shughuli zozote zile za kisiasa/kiserikali.

..niliwahi kusoma kwenye magazeti kwamba Mzee Jumbe ameacha wosia kwamba akifariki asizikwe kwa heshima za kiserikali na kijeshi kama inavyofanyika kwa viongozi wengine wakuu.[/QUOTE
Wasia wa Alhaj Aboud Jumbe
unapatikana katika makala ya AN-NUUR
gazeti la Kiislamu la kila wiki toleo na 247:DhulHijja1420/machi31 - april5,2000
 
Last edited by a moderator:

NASAHA ZA MIHANGWA

Joseph Mihangwa Toleo la 292 1 May 2013

MIAKA 29 iliyopita, Januari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), iliyoketi mjini Dodoma kwa dharura, ilimvua (ilimpindua?) nafasi zote za uongozi, Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Alhaj Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi kwa kutenda ‘dhambi kuu' ya kuhoji muundo wa sasa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Nyadhifa alizovuliwa kiongozi huyo na kubakia kuwa raia wa kawaida na kuwekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwake kwa kipindi kadhaa, ni pamoja na urais wa Zanzibar, uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, umakamu wa Rais wa Tanzania na umakamu Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Mkutano huo ulitawaliwa na kampeni chafu dhidi ya Jumbe, huku kambi mbili za Zanzibar zikiumana, kwa kambi moja kuunda tuhuma dhidi yake na nyingine kujibu mapigo, na hivyo kuchonga ufa na uhasama mkubwa miongoni mwa viongozi wa Zanzibar kati ya kambi mbili hizo kinzani; kambi iliyojiita ya ‘Wakombozi' (Liberators), iliyoundwa na waliojiona kama watetezi halisi wa Mapinduzi ya 1964 na ile ya kambi ya ‘Wanamstari wa mbele' (Front liners), iliyotaka mabadiliko ya sera visiwani.

Katika msuguano huo, Kamati ya Wakombozi ilishindwa na Rais Jumbe akatunguliwa kwa mzinga mzito, akaisha. Jumbe alikuwa mrithi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyeuawa katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililoshindwa, Aprili 7, 1972. Kabla ya hapo, Jumbe alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulikia mambo ya Muungano.

Kuuawa kwa Karume kulifikisha tamati ya utawala wa awamu ya kwanza kufuatia Mapinduzi ya 1964, utawala uliotawaliwa na vitisho, hofu, umwagaji damu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya yeyote aliyetoa sauti kuhoji utawala huo, na au kwa aliyedhaniwa tu kuwa mpinzani wa Mapinduzi.

Uporaji huo wa demokrasia, ulitekelezwa na utawala wa Karume kupitia genge katili lilojulikana kwa jina la ‘The Gang of Fourteen (Genge la Watu 14), likiongozwa na Kanali Seif Bakari. Kugongewa mlango tu usiku na genge hilo enzi hizo, kulitosha mtu kupatwa hofu kabla ya kuhojiwa.

Genge hili na sehemu kubwa ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, walitaka kuendelezwa kwa sera za Karume, na mtu pekee waliyeona angeweza kufanikisha hilo kama mrithi halali wa Karume, ni huyo Kanali Seif Bakari.

Hata hivyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliposikia hilo, akaona giza mbele. "Sera za Karume tena? Ukatili na mauaji ya kutisha kwa watu wasio na hatia? Hapana!" alisikika Mwalimu aking'aka mbele ya watu wake wa karibu, na kuamua kutokubaliana na pendekezo la Wazanzibari lililomtaka Kanali Bakari kumrithi Karume. Akajenga hoja nzito kupangua kisayansi hoja hiyo kwa kuhusisha na tukio la kuuawa kwa Karume!

Jaribio la mapinduzi lililoshindwa liliandaliwa na wanasiasa makini wa Kizanzibari kwa kuhusisha baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Zanzibar, ambalo hadi akiuawa, Karume alikuwa bado Amiri Jeshi Mkuu wake; kwa kushirikisha pia wanajeshi kadhaa wa Kizanzibari waliokuwa kwenye Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) kwa upande wa Bara.

Muuaji wa Karume, Luteni Hamoud Mohammed Hamoud, alikuwa wa Jeshi la Zanzibar. Alichukua hatua hiyo yeye mwenyewe baada ya kuhisi kwamba mpango wa mapinduzi umegunduliwa siku hiyo, na kwamba yeye na wenzake walikuwa wanatafutwa; na kwa sababu kikosi cha pili cha mapinduzi kutoka Dar es Salaam kilishindwa kufika Zanzibar muda uliopangwa, baada ya kuonywa kikiwa baharini juu ya kugunduliwa kwa mpango huo na kurejea hima Dar es Salaam.

Luteni Hamoud aliona kwa mikasa hiyo miwili, kwa vyovyote vile, angekamatwa na kuuawa kikatili. Akaamua na lolote liwe, na bila kupoteza muda akaamua kutekeleza mauaji hayo yeye mwenyewe na wenzake wengine watatu tu.

Imeelezwa kwamba ushiriki wa Luteni Hamoud katika jaribio hilo, mbali na kubeba hisia (sentiments) za kisiasa, pia alidhamiria siku nyingi tangu nyuma, kulipiza kisasi kwa Karume kwa kifo cha baba yake, Mzee Mohammed Hamoud, aliyeuawa kikatili na kiongozi huyo akiwa kizuizini kwa sababu za kisiasa.

Mwalimu Nyerere hakutaka mauaji ya Rais Karume yatafsiriwe au yahusishwe na jaribio la mapinduzi, bali alitaka yatafsiriwe kama mauaji ya kisiasa tu. Akasema, hatua yoyote ya kumteua Kanali Seif Bakari ambaye ni mwanajeshi, kuchukua nafasi ya Karume aliyeuawa na mwanajeshi pia, kungetafsiriwa kama Mapinduzi ya Kijeshi. Hapo, Wazanzibari wakanywea, wakatazamana kwa ishara bila kupata jibu kwa hoja ya Mwalimu Nyerere. Hawakuwa na namna isipokuwa kufuta pendekezo la uteuzi wa Kanali Seif Bakari kumrithi Karume.

Ndipo ikawadia zamu ya Mwalimu Nyerere kushawishi na kushauri nani ateuliwe. Akasema, pamoja na kuuawa kwa Karume, ambaye alikuwa mwasisi mwenza wa Muungano wa Tanzania, Muungano huo lazima uendelezwe bila kuyumba; na mtu pekee aliyefaa, kwa maoni ya Nyerere, alikuwa ni Aboud Jumbe Mwinyi, kwa sababu kuu tatu:-

Mosi, ni msomi na mwanasiasa mkongwe mwenye kuzielewa vyema siasa na migongano ya jamii ya Kizanzibari. Pili, ni mtu ambaye hakuwa na majungu wala makundi yenye kuhasimiana. Tatu, wadhifa wake wa Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Mambo ya Muungano) kwa muda mrefu, ilikuwa ni sifa ya ziada iliyompa uzoefu, na uwezo wa kuendeleza na kudumisha Muungano. Hoja ya Mwalimu ikapita; Jumbe akapaa, akawa Rais wa Zanzibar wa awamu ya pili.

Jumbe na Mwalimu Nyerere walifanana kwa mengi. Wote walikuwa wasomi waliosoma pamoja Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, na kisha wote wakawa walimu wa sekondari. Kwa uhusiano mzuri huo, Jumbe alianza kulegeza mengi yenye ukakasi visiwani ambayo yasingewezekana enzi za Karume ambaye aligeuka mwiba kwa Mwalimu, akidai mara nyingi wavunje Muungano kwa kuwa uligeuka koti lililowabana Wazanzibari. Chini ya Jumbe, misuguano kati ya Bara na Visiwani ambayo kabla yake ilizua kero za Muungano, ilianza kutoweka.

Jumbe alianza kukubalika haraka kwa wengi Visiwani na Bara; akawa kipenzi cha Rais wa Muungano, naye akaanza kupaona Bara kama nyumbani kwake. Akajenga makazi yake eneo la Mjimwema, Dar es Salaam. Akilala Mjimwema na kila asubuhi aliruka kwa ndege kwenda Ikulu ya Unguja na kurejea tena jioni baada ya kazi.

Ufanisi wake wa kuihudumia Zanzibar ulipungua kwa sababu ya kuweka nguvu kubwa zaidi kwenye Muungano. Na kadri alivyozidisha ziara za kirais Bara na nje ya nchi kumwakilisha Mwalimu, (majukumu ambayo Mwalimu hakuthubutu katu kumpa Karume), ndivyo alivyozidi kujiweka mbali na siasa za Zanzibar na Wazanzibari.

Kwa kutumia hali hiyo ya maridhiano, Mwalimu alizidi kuchanja mbuga kwenda mbele zaidi bila Jumbe kushuku kitu. Katika kikao cha pamoja cha NEC ya TANU cha Bara na NEC ya ASP cha Zanzibar, kilichofanyika Dar es Salaam, Septemba 5, 1975, Mwalimu Nyerere alipendekeza vyama hivyo viungane ili kuimarisha zaidi Muungano.

Jumbe alikubali kimsingi wazo hilo, lakini akataka ASP kipewe muda kufikiria zaidi. Mwaka mmoja baadaye, Oktoba 1976, maridhiano yakafikiwa ya kuunda Chama kipya ‘Chama cha Mapinduzi' (CCM), kilichozinduliwa Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP miaka 20 nyuma, mwaka 1957.

Licha ya Wazanzibari kushinikiza tarehe na mwezi wa kuzaliwa chama chao, yaani Februari 5, walishinikiza pia na kufanikiwa kubakiza neno ‘Mapinduzi' yaliyoleta uhuru wao Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya. Kwa maana ya Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.

Na hizo ndizo zilikuwa karata mbili pekee kwa Wazanzibari kukubali kuunda Chama kipya, chama ambacho kilipewa ukuu wa kikatiba wa kushika hatamu zote za uongozi wa nchi na kuweza kumng'oa madarakani Jumbe miaka saba baadaye, mwaka 1984, kama kitanzi alichojitengenezea mwenyewe. Hata hivyo, kwa mujibu wa Hati (Mkataba) ya Muungano ya Aprili 22, 1964, vyama vya siasa si jambo la Muungano kuweza kusimamia mamlaka za Muungano. Hivyo utaratibu uliotumika kumng'oa Jumbe unahojika kisheria!

Kadri Jumbe alivyozidi kujiona kukubalika kwa Mwalimu Nyerere, ndivyo alivyojiona pia kama mrithi halali mtarajiwa wa Rais wa Muungano kuliko mtu mwingine yeyote, Bara na Visiwani. Lakini kutokuwepo kwake Zanzibar mara kwa mara kulizua ombwe la uongozi kwa kuwa kila kitu kilimsubiri yeye, hata kama ni idhini ya kukata mti. Na kwa jambo la dharura, Waziri mwenye dhamana ya dharura hiyo ilibidi amfuate Dar es salaam.

Kana kwamba ombwe hilo halikutosha, hofu ilitanda miongoni mwa Wazanzibari pale Mwalimu alipopendekeza mabadiliko zaidi ya Katiba kutaka kuunda Serikali moja badala ya Serikali mbili, wakihofia nchi yao kumezwa na Tanganyika. Hali hii ilimweka pabaya Jumbe Visiwani juu ya uswahiba wake na Nyerere, wakimwita ‘msaliti' wa Mapinduzi ya Zanzibar na Wazanzibari.

Uona hivyo, Jumbe alianza kugeuka nyuma kwa kuchanganyikiwa; akawa njia panda. Wakati hilo halijapoa, jingine kubwa zaidi lilikuwa njiani likija. Mwaka 1983, Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Sokoine alikuwa na mvuto wa watu, shupavu na mwadilifu kiasi kwamba katika kipindi kifupi tu alijidhihirisha kuwa chaguo la watu na mrithi halali wa Mwalimu, ambaye naye alimkubali kwa ishara na kwa vitendo.

Kwa kuridhika na Sokoine, taratibu Mwalimu alianza kumbeza Jumbe kwa sababu nyingi, lakini itoshe hapa kutaja mbili tu. Kwanza, alimwona kama kiongozi mpweke asiye na sapoti na aliyepoteza mvuto Visiwani, pia kama dikteta mkimya asiyeshaurika na watu wa chini yake.

Pili; Mwalimu aliudhika kwa Jumbe kugeuka mhafidhina wa kidini na mpambanaji wa Kiislamu katika Taifa lisilo na dini. Kwa hili, Jumbe alizuru nchi nzima akitoa hotuba kwenye misikiti, na Serikali ikalazimika kutoa Waraka mkali wa Rais, kuwakumbusha na kuwataka viongozi wa kitaifa kutojipambanua au kuendekeza mambo ya kidini. Jumbe alipuuza Waraka huo; kwake ndio kukawa kumekucha.

Habari za Mwalimu kupoteza imani na upendeleo kwa Jumbe hatimaye zilimfikia kiongozi huyo, zikamuuma sana na kumvunja moyo. Hapo uhasama ukazuka kati yake na Mwalimu kwa njia ya kukomoana. Kwa hasira na kukata tamaa, Jumbe akaanza maandalizi ya kuumbua Muungano, kwa minyukano na Mwalimu.

Kuanzisha minyukano hiyo, ilikuwa ni lazima kwanza Jumbe arejeshe imani yake iliyopotea kwa Wazanzibari, kutokana na hatua yake ya kuhamia Mji mwema, Kigamboni na kwa kuwatelekeza Wazanzibari. Baada ya kuridhika kwamba mambo ameyaweka sawa, aliomba mawazo ya Makatibu Wakuu wa Wizara zote na Watendaji Wakuu wengine wa Serikali, ni aina gani ya Muungano unaotakiwa.

Wote, isipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Damian Lubuva, walikataa muundo wa sasa wa Serikali mbili au wa Serikali moja uliokuwa umeanza kupigiwa upatu na Mwalimu na baadhi ya wanasiasa. Jumbe na watendaji wake hao ndani ya Serikali ya Zanzibar wakapendekeza muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu. Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo kumi na moja tu yaliyoainishwa katika Mkataba wa awali wa Muungano.

Mtizamo huo ndio aliouweka wazi Jumbe baadaye katika kitabu chake kiitwacho ‘The Partnership,' yaani ‘Ubia kati ya Tanganyika na Zanzibar,' kilichosambazwa mwaka 1984. Kuthibitisha hilo, ananukuu ibara ya tano ya Mkataba wa Muungano inayosema kwamba kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Muungano, "Sheria za Tanganyika zilizopo na zile za Zanzibar, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo." (The Partnership, uk. 22).

Vivyo hivyo, anathibitisha kwa kunukuu Ibara ya Sita (a) ya Mkataba, inayotanabahisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano, atasaidiwa na Makamu wawili wa Rais (mmoja kwa ajili ya Tanganyika na mwingine kwa ajili ya Zanzibar), Mawaziri na Maofisa wengine anaoweza kuwateua kutoka Tanganyika na Zanzibar ambapo kufuatia uteuzi huo, utumishi wao utahamishiwa kwenye utumishi wa Serikali ya Muungano.

Anahoji: "Kwa kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano Namba 22 ya 1964, vinatambua uwapo na kubakia kwa Serikali za Tanganyika na Zanzibar baada ya Muungano, kwanini Muundo uliokusudiwa usitafsiriwe kuwa Shirikisho? Kama Tanganyika na Zanzibar zinatajwa kuwa nchi ndani ya Muungano, lakini kwa vitendo na hulka kuna nchi ya Zanzibar pekee, Tanganyika ilikwenda wapi?

Hatua iliyofuata na aliyochukua Jumbe, ilikuwa ni kumrejesha kwao Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Damian Lubuva, akimwelezea kama mtumishi asiyeweza kusimamia maslahi ya Wazanzibari; na badala yake akamteua rafiki yake wa zamani, raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy kuwa Mwanasheria Mkuu.

Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, huku wengine wakitaka warejeshewe Visiwa vyao (Zanzibar), kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto ambapo wanajeshi wa Kizanzibari nao walikuwa na malalamiko yao.

Mashambulizi yenye kashfa nzito nzito na matusi ya kisiasa yaliongozwa na redio ya ufichoni iliyopachikwa jina la 'Kiroboto Tapes,' hadi ilipogunduliwa na kuharibiwa na wanajeshi kutoka Bara. Mitafaruku yote hii ilikuwa na ridhaa ya Alhaj, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.

tunamengi ya kujifunza na yale ya zamani ukijumlisha na ya sasa unaweza pat picha ni wapi itakuwa bandari yetu.hope itakuwa bandari salama.
 
Urais kumbe kazi.Sio "urahisi" wa huyu jamaa yetu mbayuwayu ambao ni mwepesi kiasi eti hata cha zito kutaka au kuwa na nia ya kugombea urais.
 
Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, huku wengine wakitaka warejeshewe Visiwa vyao (Zanzibar), kupitia mihadhara, magazeti na redio, yalipamba moto ambapo wanajeshi wa Kizanzibari nao walikuwa na malalamiko yao.

Mashambulizi yenye kashfa nzito nzito na matusi ya kisiasa yaliongozwa na redio ya ufichoni iliyopachikwa jina la ‘Kiroboto Tapes,’ hadiilipogunduliwa na kuharibiwa na wanajeshi kutoka Bara. Mitafaruku yote hii ilikuwa na ridhaa ya Alhaj, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi.

Ukizisoma hizi BOLD mbili unapata picha hii ilikuwa ni vita ya kijeshi, ambapo Jeshi la Visiwani lilishindwa vita na kusalimu amri kwa Jeshi la Bara.
 
Ukizisoma hizi BOLD mbili unapata picha hii ilikuwa ni vita ya kijeshi, ambapo Jeshi la Visiwani lilishindwa vita na kusalimu amri kwa Jeshi la Bara.

Lakini Nyerere aliamua kutomteua Kanali Seif Bakari kumrithi Karume kuwa Rais; Akapendekeza awe JUMBE ili kuondoa UJESHI ndani ya SIASA za ZNZ
 
Mkuu usichanganye mada wakati umeileta wewe mwenyewe. Wewe unaongelea 1972 wakati wa kumteua Jumbe wakati mimi naongelea Ujeshi wa Bara kuishinda Visiwani 1984 kama nilvyoweka kwenye RED and BLUE.
 
Hapa MWL. Aliteleza kuitumia CCM kmuondoa mtu aliyepewa ridhaa kuongoza ni ukandamizaji wa haki na misingi ya utawala bora.
wakati serikali ya mwalimu ilipovunja vifungu vya "articles of the union" haikona tabu, ilipokuwa inafanya ujasusi kwenye ikulu ya ZANZIBAR hawakuona kuwa ni act of war. Sasa tujiulize bara ingetendewa hayo ni wazi ZANZIBAR ingechakazwa tena haraka. Uhuni wa vyama kuamua maslahi ya wengi inabidi upigwe
 
kwa sasa bado alhaj jumbe yuko mji mwema?
au ameshatangulia mbele ya haki? Na bado yuko kwenye kizuizi cha nyumbani?
Ni muda umepita
 
NASAHA ZA MIHANGWA

Joseph Mihangwa Toleo la 294 15 May 2013

KATIKA sehemu ya pili ya makala haya, tuliona namna Rais wa awamu ya pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, alivyoandaa mashtaka dhidi ya Jamhuri ya Muungano, akihoji uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba.

Tuliona pia namna hati hiyo ya mashitaka ilivyopotea mezani kwake Ikulu katika mazingira ya kutatanisha, na hatimaye alivyopata kibano cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM na kuvuliwa nyadhifa zake zote za uongozi kichama na kiserikali.

Tuliona pia namna ilivyokuwa kazi ngumu kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuteua mrithi wake muda wake wa kung'atuka ulipowadia, kutokana na kambi mbili zenye nguvu sawa ndani ya Kamati Kuu (CC) na NEC ya CCM kuumana, hata akateuliwa Ali Hassan Mwinyi, kinyume na matarajio ya Mwalimu Nyerere ambaye chaguo lake lilikwa ni Balozi Salim Ahmed Salim.

Kambi hizo mbili, zote za Kizanzibari, kwa majina zilijulikana kama ‘Kambi ya Wakombozi' (Liberators) iliyotaka kudumishwa kwa sera na fikra za Mzee Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa visiwa hivyo, kama njia ya kulinda Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Kambi hii, ilitaka misingi ya Muungano irejewe upya na kuundwa kwa Shirikisho lenye Serikali tatu; Serikali ya Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Shirikisho.

Kambi ya pili ilijiita ‘Wanamstari wa Mbele' (Frontliners), iliyotaka mabadiliko katika sera na fikra za Mzee Karume visiwani ili kuleta demokrasia na utawala bora. Aidha, kambi hii ilitaka kuimarishwa kwa Muungano kwa muundo ulivyo sasa. Kambi ya ‘Wakombozi,' kwa kuunganisha nguvu na wajumbe wa CC na NEC wa Bara, wakiongozwa na kuunganishwa na kiongozi wao mkubwa, Mzee Paul Bomani na Mama Getrude Mongella, ilishinda.

Nilikusudia kumaliza makala yangu na sehemu hiyo ya pili, lakini kutokana na maombi na kilio cha wasomaji wangu cha kwamba niendeleze makala haya, nimekubali kufanya hivyo. Sasa tuendelee na sehemu hii ya tatu na ya mwisho.

‘Wakombozi' wapeta tena uteuzi Rais wa Zanzibar

Uteuzi wa Mwinyi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, uliofanywa na NEC chini ya mfumo wa chama kimoja, ulikuwa tiketi turufu kwa mteule huyo kushika nafasi hiyo. Kwa jinsi hii, nafasi ya Rais wa Zanzibar aliyokuwa ameshikilia ikawa imebaki wazi.

Wakati wa kupendekeza jina ndani ya Kamati Kuu (CC) ulipowadia, ‘Wakombozi' walikuwa wepesi kupendekeza kwa sauti moja na kwa pamoja. "Abdul Wakil Nombe." Wakil alikuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakati huo. Nayo kambi ya ‘Wanamstari wa Mbele' ikapendekeza jina la Seif Sharrif Hamad, ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wakati huo.

Majina yaliyopendekezwa na CC kwa nafasi za Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, yaliwasilishwa NEC kwa ajili ya kupigiwa kura kupata wagombea, Agosti 15, 1985. Kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, liliwasilishwa jina la Ali Hassan Mwinyi; na kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar, yaliwasilishwa majina ya Abdul Wakil Nombe na Seif Sharrif Hamad.

Nyerere akwaa kisiki tena kuhusu mrithi

Kwa kumtumia Sheikh Thabit Kombo Jecha, aliyekuwa mjumbe wa CC na NEC ya CCM mwenye nguvu ndani ya CCM, Mwalimu alitupa kete yake ya mwisho kuhakikisha kwamba jina la Mwinyi halivuki kihunzi cha NEC, ili jina la Dk Salim Ahmed Salim ambalo halikuwasilishwa na CC ndani ya NEC, liibuke na kupitishwa. Lakini mambo hayakuwa rahisi, na ikiwa kinyume na alivyotarajia.

Kwa kuanza, Sheikh Thabit Kombo alionyesha wasi wasi wake na kwa Chama, kama Rais Mwinyi wa Zanzibar, ambaye alionyesha mafanikio makubwa kiutawala Visiwani kiuchumi na kisiasa na kwa kuleta utulivu katika kipindi kifupi cha miezi kumi na minane tu ya utawala wake, hivi kwamba kuondoka kwake kungeirudisha Zanzibar kwenye enzi mbovu za awamu mbili zilizotangulia, yaani awamu ya Abeid Karume na awamu ya Jumbe.

Sheikh Kombo alizomewa na kauli yake ikazamishwa na kelele za wajumbe wa NEC kutoka Bara wakimkatalia. Ni Khatib Hassan pekee wa kambi ya ‘Wanamstari wa Mbele,' aliyekuwa jasiri vya kutosha kumuunga mkono Kombo. Majadiliano makali yakafuata lakini bila suluhu.

Mwalimu Nyerere akaahirisha kikao, kisha akawaita pembeni kwa siri, Mzee Mwinyi, Mzee Kawawa na Sheikh Kombo na maswahiba wake wachache. Sheikh Kombo, baada ya kikao hicho cha siri, kwa mshangao wa wengi, alikuwa amegeuka tayari kumuunga mkono Mzee Mwinyi kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri; na kwa mara ya kwanza, akamuunga mkono Wakil kwa urais wa Zanzibar.

Kura za ‘Ndiyo' au ‘Hapana' zikapigwa kwa mgombea pekee wa urais wa Jamhuri ya Muungano, Ali Hassan Mwinyi. Kati ya kura 1,732 zilizopigwa, ni kura 14 tu ndizo zilizomkataa Mwinyi.

Ikafuata zamu ya Wakili na Hamad. Katika vuta nikuvute hiyo, Wakil akaambulia ushindi mdogo wa kura 85 dhidi ya kura 78 za Hamad. Ushindi wa nafasi zote mbili hizo, kwa kiasi kikubwa uliwapagawisha ‘Wanamapinduzi' na kuwahuzunisha ‘Wanamstari wa Mbele,' huku wakiulizana bila kupata jibu, kama kweli Mwalimu alikuwa upande wao tangu mwanzo.

Sheikh Hassan Nassoro Moyo na marafiki zake, walisherehekea ushindi huo wazi wazi, huku Getrude Mongella akisikika akijigamba kuwa ni wao (yeye na wenzake) waliompendekeza Mwinyi na Wakil kwenye CC na kuokoa jahazi.

Wapinzani wa Dk Salim Ahmed Salim kutoka Tanzania Bara, walifarijika na kupumua kuona Mwinyi ameteuliwa kugombea urais, kwa kuwa walimwona anaingilika kwa urahisi kuliko Dk Salim mwenye kujiamini na makini katika kusimamia mambo na kwa maamuzi.

Hata hivyo, taarifa za kiinteligensia zilionyesha kwamba Wakil asingeweza kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi mkuu kwa jinsi ambavyo hakukubalika visiwani, ikilinganishwa na Hamad, kama angeteuliwa. Na kama ingetokea Wakil kutoshinda, chama kingelazimika kuteua mgombea mwingine, na pengine Seif Sharrif Hamad huyo huyo.

Ili kuokoa jahazi, Mwalimu na Mwinyi walimwita Hamad pembeni karibu mara tatu kumwomba ampigie kampeni Wakil, na hasa kisiwani Pemba. Kwa upande wake, Hamad alipoitwa na kina Mwinyi akahoji akisema: "Iweje niombwe kufanya hivyo wakati baadhi ya wajumbe wa NEC wanapita mitaani wakijiita ‘Washindi' na mimi ‘Mchakazwa,' na kwamba eti wamemweka Wakil kupindua Serikali ya awamu ya tatu (ya Mwinyi) visiwani; na zaidi eti kwamba Wakil ataitawala Zanzibar vyema kwa staili ya ASP?"

Malalamiko ya Hamad yalimwingia Mwalimu Nyerere, kisha akamwita Dk Salmin Amour na kumwambia: "Ninazo taarifa zote, kwamba wewe unajiandaa kwa kujidanganya kuchukua nafasi ya Waziri Kiongozi; unajitangaza eti wewe ni Mkombozi. Umemkomboa nani kama si kuwagawa Wazanzibari?"

Sheikh Natepe, bila kujali msimamo wa Mwalimu dhidi ya Dk Salmin, aliingilia kati kwa kupinga yaliyokuwa yakitokea visiwani. Kwa sauti ya ukali alisema: "Siwezi kufanya kazi na mwanachama yeyote wa zamani wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP), Zanzibar and Pemba People's Party (ZPPP) au Umma Party na ndugu zao. Watu hawa kamwe hawawezi kuchukua nafasi za madaraka nikiwa bado hai katika nchi hii kwa sababu (hao) ni maadui wa watu wa Zanzibar wanaotaka kulipiza kisasi kwa ASP."

Mwalimu Nyerere alijitahidi kumnyamazisha Sheikh Natepe kwa maneno makali: "Najua, wewe ni kiongozi wa njama hizi, unalo kundi; najua."

Dk Salim Ahmed Salim, ambaye muda wote huo alikuwa kimya akisikiliza, alisimama na kuelezea masikitiko yake juu ya msimamo wa Sheikh Natepe, akaelezea nyadhifa nyingi alizoshika katika kuitumikia Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, na utii wake wa miaka 21 kwa Mwalimu, Chama na Serikali.

Alisema Dk Salim: "Muda wote nimekuwa rafiki kwa kila mtu na sijamdharau mtu yeyote. Kwa hiyo, nashangaa kujiona nakuwa shabaha ya mchezo huu mchafu wa kisiasa na uvumi wa kuchafuliana hadhi. Kama huu ndio mwenendo katika uongozi wa Chama (CCM), basi niko tayari kuachia ngazi zote ndani ya Chama na Serikali, na sitagombea ubunge."

Mwalimu Nyerere akasituka. Ni Mwinyi aliyeokoa jahazi Dk Salim asiachie ngazi, kwa kuishambulia kambi ya Sheikh Natepe kwa kuhubiri na kutenda ubaguzi wa rangi.

Na wakati wa kuhitimisha kikao hicho kifupi, Mwalimu Nyerere alibadili makasia akisema: "Nataka muelewe kwamba nawaelewa vyema vijana hawa (Wanamstari wa Mbele). Ni vijana wakweli na si wasaliti, wala si wahaini. Sitavumilia kusikia wakiitwa au kutendewa kama maadui."

Kwa karipio hilo la Mwalimu Nyerere, kambi ya Sheikh Natepe ikanywea na mmoja wao, Ali Mzee, akaomba radhi. Kwa hiyo, ikaazimiwa kwamba Mwalimu, Mwinyi, Kawawa, Dk Salim na Hamad, waanzishe kampeni kumsaidia Wakil ashinde.

Akiwa Wete (Pemba), Mwinyi alinukuliwa akiwaponda ‘Wakombozi' akisema: "Hawa wajinga wanaojiita Wakombozi, wanaotaka kuirejesha Zanzibar na Wazanzibari kwenye maovu ya utawala wa enzi za Sheikh Karume; wakataeni, msiwasikilize!"

Katika uchaguzi huo, licha ya kampeni kubwa, Wakil aliweza kupata asilimia 58.6 tu ya kura zilizopigwa. Mkasa ukawapata pia wagombea wengi wa Baraza la Wawakilishi waliojipambanua na kambi ya ‘Wakombozi' kwa kushindwa vibaya katika uchaguzi huo.

Lakini kwa yote hayo, ‘Wakombozi' ndio waliokuwa washindi kwa kufanikiwa kuweka madarakani marais wa sehemu zote mbili za Muungano. Mpambano wa kambi hizi mbili, ulibadilika pale baadhi ya ‘Wanamstari wa Mbele' wakiwano Sheikh Sepetu, Ali Ameir Mohamed na Adam Mwakanjuki, walipojiengua na kujiunga na kambi ya ‘Wakombozi' na hivyo kudhoofisha kabisa kambi ya ‘Wanamstari wa Mbele.'

Kwa kutumia mwanya huo, Wakil alivunja Baraza la Mawaziri na kuteua Makatibu Wakuu kuongoza Serikali. Na alipoteua Baraza la Mawaziri jipya, Hamad na ‘Wanamstari wa Mbele' wenzake hawakuwamo. Mwaka mmoja baadaye, Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Kizota, Dodoma, uliwafukuza na kuwavua uanachama, Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid na wengineo.

Kwa kufanya hivyo, CCM kilidhani kilikuwa kinatua mzigo wa ‘wakorofi' hao wachache, lakini badala yake waliungana na kujipanga upya na kuanzisha upinzani imara wa kisiasa nje ya Chama na Serikali na kuitikisa CCM na Serikali yake.

Kwa sababu hiyo, Hamad na wenzake hao walikamatwa na kutiwa kizuizini, na baadaye kushtakiwa kwa kutaka kupindua ‘dola' ya Zanzibar. Na kufuatia kushinda kesi hiyo, Hamad na wenzake walianzisha kikundi cha chini kwa chini cha mapambano ya kisiasa kilichofahamika kwa jina la Kamati ya Mwelekeo wa Vyama Huru (Kamahuru), kama msingi tangulizi wa kuzaliwa kwa Chama cha Wananchi (CUF).

Kufikia hapo, ni dhahiri kwamba mtizamo wa wana-CCM Zanzibar, ni ndoto ile ile ya ‘Wakombozi' ya kutaka kutawala kwa staili ya ASP ya enzi za Mzee Karume, wakati mtazamo wa CUF ni kuona sera za ASP na Karume zinatoweka ili kupata Zanzibar mpya. Je; Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), ina ubavu wa kuzivunja na kuzizika fikra za kambi hizi mbili kinzani na kufikisha tamati historia ya mifarakano ya kisiasa Zanzibar?

Kweli NYERERE AUTOBIOGRAPHY ingekuwa BEST SELLER; Sasa hapo tunaona kuwa kweli NDANI YA NEC/CC enzi za NYERERE kulikuwa na DEMOCRASIA??? Ina Maana Nyerere hakuwa Dikteta na kuweka anaowataka wawe Marais???

This is very Impressive... Lakini kuna Baadhi yetu TUNAMCHUKIA tu kwasababu tunaambiwa HABARI za CHUKI DHIDI yake na hatufany UCHUNGUZI na kujua ukweli bila wa kuambiwa...

Ina Maana kama Nyrere angekuwa Dikteta Salim Ahmed Salim angekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na pia Seif Sharif Hamad angekuwa Rais wa Zanzibar way back...
 
Kupaa na kutunguliwa kwa Aboud Jumbe Mwinyi III

Back
Top Bottom