Ni kifungu gani kinamlazimisha mwanaume wa kikristo kuwa na mke mmoja?

Khantwe

JF-Expert Member
Dec 20, 2012
59,409
119,014
Hi Ladies, gentlemen and baharias
Naomba nieleweke kuwa lengo langu si kupingana na hili bali nataka tu kueleweshwa. Katika kusoma kwangu biblia sijaona sehemu inayozuia mtu kuwa na wake zaidi ya mmoja, hata katika kusikiliza na kusoma mafundisho mbalimbali sijawahi kuona hoja yenye uzito ila naamini hapa nitapata majibu....nitaweka hapa baadhi ya hoja ambazo huwa zinatolewa

1. Uumbaji. Ukisoma Mwanzo sura ya pili Mungu alipomuumba mwanadamu aliumba mwanaume kisha kutoka kwenye ubavu wa mwanaume akamuumba mwanamke kwa hiyo Mungu alimpa Adamu mke mmoja. Lakini je kulikuwa na haja ya kuumba wanawake wengine wakati wanaenda kuzaana? Ina maana alimaliza kila kitu kwenye hizo sample mbili, ndio maana hatuoni aliumba mzungu, mwarabu, mwafrika n.k Na kama jambo hilo ni haramu kiasi hicho mbele za Mungu kwa nini aliruhusu watakatifu wale wa zamani mf. Yakobo, Daudi na wengineo kuwa na wake zaidi ya mmoja?
2. Mafundisho ya Bwana Yesu. Baadhi ya mafundisho yanayorejewa ni

Mathayo 19:4, 5
4 Akawajibu: “Je, hamkusoma kwamba yule aliyewaumba tangu mwanzo aliwaumba mwanamume na mwanamkea 5 na kusema: ‘Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’

Hapa Bwana Yesu alikuwa anajibu kuhusu talaka, lakini mimi nadhani mtu mmoja anaweza kuwa mwili mmoja na huyu na akawa mwili mmoja na mtu wa pili pia bila kuathiri muunganiko wa kwanza


3. Mafundisho ya Mtume Paulo
1 Wakorintho 7:2
2 lakini kwa sababu ya kuenea kwa uasherati,* kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewea na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe.

Hapa kilichokatazwa ni uasherati, sioni uhusiano wa idadi ya wanawake na hili andiko maana hata ukiwa nao wawili bado ni wake zako mwenyewe.

1Timotheo 3
1 Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. 2 Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkarimu, ajuaye kufundisha; 3asiwe mtu wa kulewa, asiye dhalimu; bali awe mpole; asiwe mbishi wala asiwe mwenye kupenda fedha;.......
Hapa amezungumziwa askofu au mwangalizi wa kanisa, je kama sio askofu? KItu kingine kinachonitatiza hapa ni kuwa Paulo alikuwa anazungumzia watu wanaoamini (kanisa), anaposema askofu awe mwanaume wamke mmoja in maana katika kanisa kuna watu wenye wake zaidi ya mmoja? kwa sababu ni wazi askofu hawezi kutoka nje ya kanisa bali miongoni mwa haohao waumini.
Kama hawapo watu wasio na mke mmoja kwa nini aliweka hicho kigezo?

Samahani siko vizuri kwenye kuandika na kupangilia hoja lakini nadhani mmenielewa.

NB; Nimejikita upande mmoja wa wanaume ili tusitoke kwenye mlengo wa mada
 
34 Reactions
Reply
Back
Top Bottom