Ni bajeti yenye mitikisiko mingi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,319
33,125
Edzigo(2).jpg

Maoni ya Katuni


Bajeti ya mwaka 2013/14 ni ya kwanza katika historia ya bajeti ya serikali kusomwa baada ya wabunge kujadili bajeti za wizara zote. Na kama ilivyo kawaida kwa bajeti zote zinaposomwa, wananchi nao huguswa katika baadhi ya maeneo yanayowaongezea gharama za maisha kutokana na kupanda kwa bei katika bidhaa muhimu.

Bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa Alhamisi ya wiki hii, hakika imepokelewa kwa hisia tofauti na makundi ya wananchi mbalimbali huku baadhi wakiipongeza na wengine wakiikosoa kutokana na ongezeko la kodi na ushuru kwa bidhaa na huduma, kwamba ongezeko hilo litawadidimiza zaidi walala hoi.


Baadhi ya wabunge pia wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusiana na bajeti ya serikali ya mwaka 2013/14, wengine wameisifu na kusema itawakomboa wananchi endapo tu fedha zilizotengwa zitatolewa kwa muda muafaka. Wengine wameiponda wakidai ni ya kisiasa zaidi kwa vile vyanzo vya mapato ya serikali vimeendelea kuwa pombe, sigara na vinywaji baridi.


Bajeti hii imegusa maeneo mengi yakiwa ni pamoja na ongezeko la gharama ya ushuru wa forodha kwa asilimia 25 kwa magari yaliyotumika, huku wananchi wakidai hatua hiyo ni kumkomoa mwananchi asiye na uwezo wa kununua gari jipya, gharama za ongezeko la kodi kwa simu za viganjani, na maeneo mengine yaliyoongezwa tozo pamoja na kodi.


Kimsingi, bajeti hii imesababisha malalamiko na manung'uniko kutoka kila kona yakitoka kwa wananchi wa makundi mbalimbali, huku baadhi ya wasomi, na wanasiasa wakidai kwamba bajeti hiyo haiwezi kubadili hali ya maisha ya watu wa kipato cha chini. Kodi na ushuru zilizotangazwa ndani ya bajeti wamedai kuwa zitadhoofisha hali ya watu wa chini kutokana na gharama za maisha kuendelea kupanda.


Waziri wa Fedha wakati akisoma bajeti hiyo, inayofikia trilioni 18.249 alisema bajeti imejielekeza katika vipaumbele katika maeneo tofauti, ikiwamo kukua kwa pato la taifa kutoka asilimia saba ya mwaka huu mpaka 7.2 kwa mwaka ujao. Pia kipaumbele kingine ni kudhibiti kupanda kwa bei kutoka asilimia 8.3 hadi kufikia asilimia sita ifikapo mwakani.


Maeneo mengine yaliyolengwa kama vipaumbele ni kuongeza mapato ya ndani yatakayofikia uwiano wa pato la taifa wa asilimia 20.2 kwa mwaka 2013/14 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 17.7 ya mwaka 2013. Vingine ni kupunguza tofauti ya viwango vya riba vya benki na kuimarisha thamani ya Shilingi, pia kuwa na kiwango imara cha ubadilishanaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la fedha.


Aidha alisisitiza kuwa ili kufikia shabaha na malengo ya bajeti hiyo, misingi inayokusudiwa na serikali ni pamoja na kuendelea kuimarisha na kudumisha amani, usalama, utulivu na utengamano kwa kutenga fedha kwa ajili ya kutuliza ghasia.


Tunaamini kuwa masuala mengi yaliyoainishwa katika bajeti ya 2013/14 yanakusudia kuboresha maisha ya Watanzania wa ngazi zote, kila mwananchi kwa nafasi yake anawajibika kushiriki katika kujiongezea pato lake ambalo litakuwa chanzo cha kipimo cha nguvu za kiuchumi za taifa.


Kila mwananchi anawajibika kuitafsiri bajeti hii kama sehemu ya changamoto za kiuchumi, ingawa inaonekana si jambo jepesi kukabiliana na vikwazo vya athari zake kutokana na gharama halisi ya maisha ya kila siku kuwa kubwa.


Tunao uzoefu wa kukumbana na ongezeko la kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, na kwa hakika kila mwananchi anao mfumo wa kukabiliana na gharama za ziada kila zinapojitokeza.

Changamoto za bajeti hii zisitukatishe tamaa, bali ziwe chachu ya kuongeza kasi ya uzalishaji na uimarishaji wa uchumi binafsi katika maeneo yetu. Ni imani yetu kuwa serikali itaendelea kufungua mianya na kubuni vyanzo vingine vya mapato ambavyo havina athari kiuchumi kwa wananchi hasa wa kipato cha chini.

Nguvu zaidi zielekezwe katika kuwawezesha wananchi kunufaika zaidi kiuchumi na hasa kutokana na mikopo kwenye taasisi za fedha. Ni bajeti yenye mitikisiko mingi lakini tunaamini serikali ikijipanga vyema tutajinasua kutoka hali ya maisha iliyopo sana na kwenda kwenye neema zaidi.




CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Back
Top Bottom